SIMULIZI.... PENZI CHUNGU - SIMULIZI.... PENZI CHUNGU
MWANDISHI.. HALFANI SUDY
SEHEMU YA 18
Jicho la kwanza la mama Siyawezi alikitazama kisu, tazamo la pili alijiangalia upande wake wa kushoto wa kifua chake. Pale unapokaa moyo. Nusu ya kile kisu kirefu alichokitazama mara ya kwanza kilikuwa kimezamishwa katika upande wake wa kushoto wa kifua na mkono imara wa mwanaume. Mama Siyawezi, alianguka chini huku akijiangalia kifuani. Akishuhudia damu nyingi zikibubujika katika kifua chake, ilikuwa ni kama bomba linalopitisha maji yenye kasi kali limekatika ghafla, ilikuwa ni picha mbaya na ya kutisha sana, mama Siyawezi alikata roho pale chini, bila kuijua sababu sahihi ya kuchomwa kisu kile, alikufa na kisu kifuani.
kwa mwendo wa kasi, mgeni yule wa kiume mwenye roho inayopaswa kuitwa mbaya, alitokemea mtaani.
Kwa kutumia gari yake ndogo, aina ya Rav 4 nyeusi, Inspekta Jasmine alifika nyumbani kwa mama Suto. Alikuwa anagonga hodi katika mlango wa nyumba ya kina Suto Sutani mara ya tatu sasa, lakini hakujibiwa.
Alijaribu kuusukuma ule mlango,
ukafunguka!
Aliingia sebuleni kwa tahadhari kubwa sana, macho ya Inspekta Jasmine yalikutana na majimaji ya ajabu katika kapeti zuri la pale sebuleni, maji maji mekundu, damu!
Damu ile ilikuwa inaelekea au kutokea chumbani. Inspekta Jasmine aliifata, huku akiwa kaishikilia bastola yake mkononi, tayari kwa kukipiga kiumbe chochote kibaya kitakachotokea mbele yake.
Michirizi ya damu ilimfikisha Inspekta Jasmine hadi chumba cha mama Suto,
Alipigwa na butwaa !
Alikuwa anatazamana na mwili usio na roho wa mama Suto! huku ukiwa na jeraha baya sana kifuani, juu kidogo ya ziwa lake la kushoto. Damu nyingi zilikuwa zimetapaa sakafuni. Bila shaka mama Suto aliuwawa sebuleni na kuburuzwa mpaka chumbani. Inspekta Jasmine aliichunguza nyumba yote kwa umakini mkubwa, hakukuwa na mtu yeyote ndani ya nyumba ile, watu wote waliikimbia nyumba ile baada ya tukio la siku ile usiku, tukio lililompeleka Suto Sutani Segerea.
Inspekta Jasmine alipiga simu Polisi, walifika pale kwa gari yao baada ya dakika kumi. Baada ya taratibu za kipolisi mwili wa mama Suto ulipakiwa na kupelekwa hospitali ya Amana. Baada ya Inspekta Jasmine kuchunguza mazingira ya ile nyumba, akihusianisha na tukio lile, hakupata jibu sahihi.
Alitoka nje ya nyumba ile. Alipofika nje, alipigwa na butwaa !
Alikutana na waandishi wa habari wameshafika eneo lile, wakiongozwa na mwandishi wa habari mahiri wa gazeti la Dumizi, Veronica Raymond Baro.
Waandishi wale walimvamia Inspekta Jasmine, kila mmoja na swali lake lake.
Inspekta Jasmine hakujibu swali hata moja, haukuwa muda wa kujibu maswali, ulikuwa ni muda wa kutafuta majibu ya maswali lukuki yanayotokana na visa vya ajabu tena mfululizo vya kesi ile, aliwaangalia tu waandishi wale kwa macho yake madogo. Alipenya kwa nguvu katika kundi lile kubwa la waandishi wa habari, aliingia kwenye gari yake, akaling'oa kwa kasi kubwa sana, akiwa hajui anaelekea wapi ?
Baada ya kuzunguka kwa muda mrefu na gari bila uelekeo maalumu. Sasa alipata mawazo mawili yakiyokinzana. Aende hospitali ulipopelekwa mwili wa mama Suto, au arudi Tabata kwa mama Siyawezi.
Inspekta Jasmine hakujua kwanini nafsi ilimwambia arudi Tabata, kwa mama Siyawezi, nafsi ilishinda aliamua kwenda huko.
Alipaki gari yake vizuri barazani kwenye nyumba ya mama Siyawezi. Akawa anaelekea mlangoni kugonga mlango. Inspekta Jasmine aligonga sana mlango ule, lakini haukufunguliwa. Alijaribu kuusukuma, ilikuwa kama mlango wa mama Suto, nao ulifunguka bila kizuizi chochote, Alichokiona pale chini ya sakafu Inspekta Jasmine kilimstua sana. Aliukuta mwili wa mama Siyawezi umelala katika dimbwi dogo la damu.
Alichoka sana !
Alishusha pumzi ndefu, sasa, Inspekta Jasmine aliona maji yamezidi unga.
Sasa alijua kwamba anapambana na watu wanaozijua nyendo zake zote. Bila shaka walimwona wakati kaja kwa mama Siyawezi, na walijua pia ataenda kwa mama Suto.
Inspekta Jasmini aliwapigia tena askari Polisi. Waliwasiri baada ya muda mchache, waliuchukua mwili wa marehemu mama Siyawezi na kuupeleka hospitali nao, Inspekta Jasmine nae alielekea huko kwa gari yake...
KESHO