Riwaya : Noti Bandia....!! Mwanzo-mwisho.

SEHEMU YA KUMI NA TISA



Watu wote walikaa kimya ndani ya chumba cha mkutano. Carlos Dimera alionyesha dhahiri hali ya woga na hasira, akivuta sigara kubwa iliyosokotwa kwa karatasi ngumu, alitembea kutoka kona moja ya chumba hiki kwenda kona nyingine huku akitafakari kwa kina kilichokuwa kimetokea. Alijitahidi kuvuta sigara hiyo mpangilio na kupuliza moshi mwingi hewani. Hali iliyowafanya wafuasi wake wapatwe na hofu.

Mama Feka au Sweety, kama alivyojitambulisha kwa Carlos, alikuwa mmoja wa watu waliokuwa ndani ya chumba hiki cha
mkutano wa siri, akishiriki kama mjumbe wa kawaida. Lengo la Carlos ilikuwa kumshirikisha mama huyu katika biashara ya dawa za kulevya.

Mzungu huyu aliutambua urembo wa Mama Feka, awali alikuwa ameteta na Jakina, kuwa unapokuwa na msichana mrembo kama
huyu kwenye biashara yako asilimia tisini mambo yatakuwa shwari. Hata aliposhiriki kikao hiki wajumbe walilitambua kusudi la Carlos, wakampokea Mama Feka kwa mikono miwili.

Mfano wa mtu aliyeshikwa na kigugumizi, Carlos alivunja ukimya uliokuwepo kwa kusema. ..."Imenishangaza mno, watu makini, watu mnaojitambua, kuyachezea maisha yenu mbele ya Simba mwenye njaa, sielewi nini kimewalevya mpaka mnazidiwa maarifa na wajinga?. Haiwezekani, Hawa na Tony wakamatwe kama kuku, halafu, shehena yote ipotee. Lakini cha ajabu na kusikitisha zaidi, wenzetu hawa wamefika mahakamani. Mmmmm, imenifedhehesha sana Nauliza kila baada ya dakika kuhusu hatima ya jambo hili, wakubwa wanataka kujua nini mkakati wetu au tumejipangaje kumaliza tatizo hili, pesa si tatizo, mtu mmoja, mtu mmoja mpuuzi hawezi kufanya tuonekane wapuuzi", alitembea tena kutoka upande mmoja wa chumba hiki kwenda upande mwingine huku wajumbe wakimwangalia.

"Inachosema ni hakika bosi, lakini usitishwe na ukimya huu, ukadhani labda tumeridhishwa na jambo hili, niseme wazi kuwa adui anaishi kwa mbinu, ambazo hakika siku zake za kuishi sasa zinahesabiwa, hivi tunavyoongea, vijana wetu wako katika msako mkali kujua mjinga huyu yuko wapi. Naamini msako huu utafanikiwa haraka iwezekanavyo, kwani tunatumia vifaa vya kisasa", Nombo alieleza.

Haraka Jakina akasimama, tofautu na mwenzake aliyeongea ameketi. "Kama ulivyosikia bosi, mahakama ilikuwa itoe
hukumu ya kesi hii leo, lakini kutokana na jitihada kubwa zilizofanywa, hukumu imeahilishwa mpaka kesho ili tuweze
kujipange. Nakuhakikishia Hawa na Tony kesho wakati kama huu watakuwa huru, mwanasheria wetu pia ni mtu makini sana, cha msingi tuwe wavumilivu, tumalize tatizo hili ndipo tujiulize wapi tulijikwaa", Jakina alieleza.

"Maneno mazuri sana, lakini hayana ufumbuzi wa jambo hili, kila mmoja anaongea kwa mtazamo, kama tunaweza kuwatoa Hawa na Tony kwenye mikono ya sheria, swali langu ni je, huu mzigo utapatikana au utapotea?. Tunapojadili jambo nyeti kama hili, lazima tuangalie uwezekano huo pia", alihoji.

"Swali zuri bosi. Mara tu baada ya Hawa na Tony kukamatwa, haraka tuliwasiliana na watu wetu katika vitego mbalimbali vya usalama wanaopokea mshahara kutoka kwetu, kuwajulisha kilichotokea, hakika ushirikiano wao ni mkubwa mno. Kama unavyojua msimamo wa serikali sasa, unapofikishwa mbele ya mahakama na ushahidi, moja kwa moja unakumbwa na kifungo, lakini maofisa hao ndiyo waliofanikisha mahakama kusogeza hukumu ya kesi hii mbele ili tuweze kujipanga", alisema Nombo.

"Baby naomba uketi", Mama Feka alimwambia Carlos kwa sauti ya mahaba. Sauti ya Mama Feka, ilimfanya Carlos, atabasamu kidogo.

"Asante Sweety wangu, usijali mpenzi, mambo yanapokwenda ndivyo sivyo, lazima tuketi na kutafakari njia sahihi, usiogope Sweety mpenzi, uwe na amani nitaketi", Carlos alisema, halafu akaendelea. ..."Jamani, tupunguze maneno, tupunguze porojo, jukumu lililo mbele yetu ni zito mno, yatupasa kujipanga vyema, Hawa na Tony ni watu kutoka miongoni mwetu. Nasema kwa gharama yoyote lazima watakuwa huru kutoka katika mikono ya sheria. Nataka kuona jambo hill linafanyika haraka iwezekanavyo, hebu jiulize mfano ungekuwa wewe ingekuwaje?", Carlos alihoji baada ya kutoa agizo.

Lakini Carlos na kikosi chake walikuwa wamekosea jambo moja. Hawakujua kama, Mama Feka alikuwa hapo kwa kazi maalumu, alitumia simu yake ya kiganjani kwa usiri wa hali ya juu kurekodi mazungumzo hayo na kuyatuma wakati huo huo moja kwa moja kwenye simu ya Teacher. Carlos Dimera na wafuasi wake waliendelea kujadiliana hili na lile, waliongea mambo mengi, wakipanga hili na lile, hatimaye wakafikia mwafaka.

"Nitalala usingizi mnono iwapo nitasikkia Teacher amekufa, sasa naagiza, kwa gharama yoyote ya pesa, atafutwe ikiwezekana auwawe haraka kabla ya hukumu kesho, uwepo wake unaweza kuharibu mipango yetu", Carlos alisisitiza, huku kila mmoja akipewa jukumu lake.

Hata hivyo, Carlos Dimera aliamua kutumia uzoefu wake wa siku nyingi katika kazi hizi za hatari, aliwatuma kwa siri, vijana wawili Gabriel na George, bila kuwashirikisha wenzake. Hawa walikuwa wakiishi nchini Tanzania kwa siri, wakisubiri matukio kama haya. Vijana hawa wenye uzoefu mkubwa wa mambo ya ujasusi walipewa jukumu la kumtafuta Teacher.

Carlos, aliwaamini sana vijana hawa, waliokuwa wakifanya mazoezi wakati wote, aliujuwa vizuri muziki wao, Ni vijana
ambao wakitumwa kukileta kichwa cha mtu yeyote, wanaweza, kutokana na imani yake kwao, aliwaagiza kumleta Teacher mbele yake akiwa hao ili athibitishe kuwa ndiye, halafu amuue yeye mwenyewe. Hili alilifanya kwa siri kubwa, bila hata Sweety kujuwa.

Mara nyingi majasusi hutumia mbinu tofauti katika kufanikisha mambo yao, Gabriel na George waliishi nchini kwa siri, hakuna mtu aliyefahamu uwepo wa majasusi hawa. Hata Jakina aliyekuwa karibu zaidi na Carlos hakuwajuwa vijana hawa.

Gabriel na George walikuwa majasusi waliohitimu mafunzo ya juu ya ujasusi katika vyuo mbalimbali duniani, walilingana kwa kimo na umri, walionekana kama mapacha, lakini ukweli ni kwamba kila mmoja alikuwa na sifa zake,

George akiwa amezaliwa katika mji wa Kano, nchini Nigeria, huku Gabriel akiwa raia wa Afrika Kusini. Vijana hawa walikutana katika chuo kimoja nchini Cuba, ambako walishabihiana kwa kila kitu, hata walipohitimu mafunzo yao ya ujausi walipangwa pamoja, baada ya kununuliwa na wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya kwa ajili ya kulinda maslahi yao.

*************************

Wakati huo huo, mkutano mwingine wa siri, ulifanyika katika Hoteli ya King Air katikati ya Jiji la Bogota, nchini Colombia, ambapo Wafanyabiashara wakubwa, matajiri wa dawa za kulevya walikutana kwa siri kama ilivyo kawaida yao.

Watu hawa walikutana kujadili mafanikio ya biashara yao pamoja na shehena yao kubwa ya dawa za kulevya kukamatwa Jijini Dar
es Salaam, Tanzania na watu wao kufikishwa mahakamani.


Emilio, mfanyabiashara kigogo, aliyefika Dar es Salaam, kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kuingiza dawa hizo, ambazo awali zilikwamba Ethiopia, alitakiwa kuwaeleza wakubwa hawa kwa nini shehena hiyo ikamatwe baada tu ya kuingia Tanzania.

"Inawezekana hatukuwa makini wakati wa kusafirisha shehena hii? Tanzania kama Tanzania ndiyo njia yetu ya kusafirisha dawa za kulevya kwenda katika nchi nyingine za ukanda wa mashariki. Leo tujiulize, nini kimetokea mpaka shehena hii hii kubwa ikamatwe?", Mfanyabiashara tajiri, ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa mtandao huu, Enock Jonson, alihoji.

"Ni wakati wa Emilio kutoa maelezo, ndiye mtu wetu pekee aliyesafiri hadi Dar es Salaam, lengo la safari ilikuwa kuweka mambo sawa, sasa kama hali ya usalama nchini humo ilikuwa hairuhusu, ilikuwaje wewe ukaruhusu shehena hiyo kuingizwa bila kuwa na uhakika wa hali ya usalama nchini Tanzania", Stephan Bad ambaye kiutendaji ndiye msimamizi mkuu wa biashara ya dawa za kulevya alihoji.

Emilio alikohoa kuweka koo lake sawa, alipaswa kueleza ukweli. Tabia ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya kumuua mwenzao haikuwa tatizo. "Naomba kueleza kuwa wakati naingia Dar es Salaam juzi, njia zote zilikuwa vizuri na wazi kabisa, tukumbuke kuwa nilikwenda Dar es Salaam, baada ya shehena hiyo kukwama, Adis Ababa, Ethiopia, Carlos alikuwa amenieleza kuwa hali haikuwa nzuri wakati huo, lakini baada ya kuweka mambo sawa, hali ikawa shwari, sasa si wakati wa kulaumiana, vijana wanajaribu kila njia kuweka mambo sawa. Tusubiri".

"Wakati mwingine tuwe makini na jambo hili, tusikurupuke kutoa maamuzi", Stephan Bad alieleza. "Hakika, lakini nimesikia kuwa nchini Tanzania sasa njia nyingi zimefungwa, serikali ya nchi hiyo imekuwa macho zaidi, lakini watu wetu Dar es Salaam wamefikishwa mahakamani leo, Carlos amenihakikishia kuwa watatoka kesho,

Hakimu wa kesi hiyo ni mtu wa upande wetu, inasemekana alishinikizwa atoe huku leo, lakini pesa imefanya kazi yake,
ametumia vifungu vya sheria kuweka mambo sawa, jambo hili litakwisha kesho", Emilio alidokeza.

"Punda afe mzigo ufike, nchini Tanzania hatuna mkataba na mtu zaidi ya Carlos Dimera, hao wengine ni vibaraka tu, lazima mtambue kuwa tuna nguvu kubwa Dar es Salaam, hao waliokamatwa tuwaache wafungwe, ili iwe rahisi kuupata huo
mzigo, nakuhakikishia wakifungwa hawa itakuwa na nafasi nzuri kwetu kuupata mzigo huo", Stephan Bad alieleza msimamo wake.

"Itakuwa ngumu zaidi, Carlos amenihakikishia uwezekano wa kuwatoa upo, hakuna sababu ya kuwatosa", Emilio alishauri.

"Hapana, wakati mwingine tumia akili yako ya ziada, fahamu kuwa watu hawa wakifungwa, serikali itatangaza kuteketeza shehena ya dawa hizo, lakini kabla hazijateketezwa zinarejeshwa kwetu, wahusika wanateketeza maboksi na makuti ya mnazi chini ya ulinzi mkali, hatimaye mzigo unaingia sokoni, ndivyo tunavyofanya", Stephen Bad alieleza.

"Ushauri mzuri, Carlos aelezwe kuhusu jambo hili, japokuwa siamini kama anaweza kukubaliana nasi", Emilio alidokeza.

"Hili ni agizo, asikubali yeye nani? Nakuhakikishia Emilio, kama tuna nia njema ya kuupata mzigo huo, hatuna budi kuwatosa Hawa na Tony, waliokamatwa, lakini ukijaribu mbinu nyingine tumeumia", Stephan Bad alisisitiza.

"Hofu yangu ni kwamba tunaweza kukosa mama na mwana", Emilio alidokeza.

"No. Usihofu kabisa, nakuhakikishia hii ndiyo njia salama ya kupata mzigo huo, unakumbuka kilichotokea Msumbuji na Congo? sasa una shaka gani?", Enock Jonson alihoji.

Baada ya majadiliano ya muda mrefu, hatimaye kikao kiliafiki kuwa, Hawa na Tony watoshwe. Carlos Dimera alipewa taarifa ya siri kuhusu mwafaka huo, akautafakari msimamo huo. Lakini hakuwa tayari kuutekelezq.

ITAENDELEA 0784296253
 
SEHEMU YA ISHIRINI



Hali ya utulivu katika Jiji la Dar es Salaam, kiasi fulani ilikuwa imetoweka, Gabriel na George waliokuwa wamehitimu vizuri mafunzo ya ujasusi, katika nchi mbalimbali duniani, waliingia katika mitaa ya Jiji la Dar es Salaam kwa kazi moja tu, kumsaka Teacher. Majasusi hawa wakiendesha magari mawili tofauti, mmoja akiendesha Toyota Brevis yenye rangi ya Blue, mwingine alikuwa ndani ya Toyota Verosa yenye rangi ya Zambarau. Carlos Dimera aliuamini sana utendaji kazi wa vijana hawa, akasubiri kuona nini matokeo.

Mfano wa panya wa Suwa, wenye uwezo mkubwa wa kunusa na kutegua mabomu ardhini, majasusi hawa Gabriel na George, walianza kunusa harufu. Wakitumia mtambo maalumu wa kunasa mawasiliano, hatmaye walifanikiwa kuingilia mawasiliano ya Teacher, mara tu baada ya kuipata namba yake ya kiganjani. Mtambo huo maalumu uliweza kuonyesha mnara unaotumika kwa mawasiliano ya Teacher, baada ya kufanikiwa kuupata mnara huo, kazi ya majasusi hawa, ilikuwa kufuatilia uelekeo wa mahali mnara huo ulipo.

Carlos Dimera, alikuwa amewaeleza majasusi hawa kila kitu kuhusu Teacher, aliwaeleza jinsi Teacher alivyo mwepesi na mjanja wa kubaini mambo. Dimera alimwelezea Teacher kuwa ni mtu mwenye hisia kali katika tasnia hiyo. Hivyo aliwayaka walijiweka vizuri mara mia zaidi kwa ajili ya mapambano. iwapo hali hiyo itatokea.

Hatmaye mtambo ukawafikisha Kinyerezi, kila wanapotafuta uelekeo, mtambo nao unaonyesha mshale wa mawasiliano ya simu husika. kila waliposogea mlio fulani ulisikika ndani ya mtambo huo, kuashiria uelekeo ulikuwa sahihi. Hatmaye wakaifikia Hotel Bella, iliyoko Kinyerezi, nje kabisa ya Jiji la Dar es Salaam, eneo ambalo dakika chache zilizopita Teacher alikuwa amewasiliana na watu kadhaa. Majasusi hawa waliamini kuwa Teacher atakuwa amekia hotelini hapo kwa vile katika eneo hilo, hakukuwa na Hotel nyingine. wakajiweka sawa, wakapanga kuivamia.

Ukweli ni kwamba, baada ya Teacher kufanikiwa kuwaburuta mahakamani, Hawa na Tony, alikubaliana na wenzake Fred, Claud na Nyawaminza, kila mmoja apumzishe akili sehemu aliyoona inamfaa, wakisubiri mahakama kutoa hukumu dhidi ya watuhumiwa wa dawa za kulevya, Hawa na Tony. Akatafuta sehemu nzuri ya kupumzisha akili, sehemu ambayo si rahisi adui kuifikia, akajihifadhi Hotel Bella, kwa ajili ya usiku mmoja wa leo, akiisubiri kesho.

Kwa vile Hoteli Bella iko karibu na mitambo ya umeme wa ges ya SONGAS, baada ya majasusi hawa kufanya utafiti kuhusu eneo hilo, waliingia Hotelini hapo mmoja baada ya mwingine, wakikodi vyumba vya kulala, huku wakijisajili katika kitabu cha wageni kwa majina tofauti. George akijiita Mhandisi Hezdori Stephan, kutoka Zimbabwe nae Gabriel, alijiita Mhandisi David John kutoka Comoro.

Wakati Gabriel anajisajili, alitumia nafasi hiyo kukagua majina ya wageni mmoja baada ya mwingine, kilichomshangaza hakukuwa na jina linaloelekea kuwa la Teacher. Hata hivyo, aliamini kuwa Teacher ni mjuzi katika tasnia hiyo, akaziamini hisia zake.

Kutokana na uzoefu katika mambo ya uchunguzi, Teacher hakupenda kusajili jina lake kwenye kitabu cha wageni, badala yake akajisajili kwa majina ya Mrs Martina Fundi, mhasibu kutoka mkoani Mtwara. Lakini kabla ya kuandika katika kitabu cha wageni alimjulisha mhusika wa Hoteli hiyo kuwa atakuja mgeni mwenye majina hayo, akalipa pesa za chumba halafu akaendelea na mipango yake mingine.

Kulikuwa na idadi kubwa ya wageni katika Hotel hii, wengi walikuwa wahandisi kutoka sehemu mbalimbali ya Tanzania, ambao walifika Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya uzinduzi wa bomba la ges lililojengwa na Serikali kutoka Mtwara hadi Kinyerezi, Dar es Salaam.

Majasusi hawa, George na Gabriel walikuwa tayari wameipata taarifa hii ya uzinduzi wa bomba la ges kutoka Mtwara, wakajiita wahandisi.

********************************

Ilikaribia kuwa saa mbili kamili za usiku, niliingia bafuni, nikaoga haraka haraka, baada ya kuvaa suluali na fulana iliyokuwa kwenye mkoba wangu, nilitoka na kuelekea sehemu ya bar kwa ajili ya kusikiliza taarifa ya habari ya usiku pamoja na kupata bia mbili za kutafutia usingizi. Si kwamba chumbani kwangu hakukuwa na televishen, la hasha, nilikwenda sehemu ya bar kwa ajili ya kunywa kidogo.

Muziki wa taratibu ulisikika, sauti za magwiji wa muziki nchini, akina Tx Moshi Wiliam, Joseph Maina, Kamanda Mzee Muhidini Gulumo wa OTTU Jazz zilisikia, kiasi fulani nilitokea kuipenda bendi hii, ninapozisikia sauti za watu hawa, huwa nafarijika na kusahau machungu.

Watu wachache walikuwa wameketi kwenye meza wakipata moja moto, moja baridi, baadhi walikuwa wakijadili kuhusu hali ya maisha ya sasa, mimi nilipita karibu yao, nikatafuta meza ya pembeni nikaketi. Mimi hupenda kukaa meza za pembeni, kwa sababu ambazo nitakudokeza ukinitafuta, ukinielewa sawa, usiponielewa shauri yako.

"Karibu kaka, nikusaidie kinywaji gani?" mhudumu wa hoteli hii aliniuliza baada tu ya kuketi.

"Nitashukru, umesema unisaidie kinywaji gani, asante kama hapa mnatoa vinywaji bure, niletee?" nilimtania.

"Hapana, hapana kaka, tunauza, labda nimekosea kiswahili, maana yangu unaagiza kinywaji gani, ulipe pesa nikuletee?" msichana huyu alijitetea.

"Nitapata Wisky aina ya Tekla, zinazotengenezwa kwa mkonge?".

"Bila shaka zipo, ila bei yake imechangamka kidogo", alibainisha.

"Bei siyo tatizo, hebu niletee hilo Tekla chupa ndogo, usisahau maji ya kunywa, weka barafu nyingi kwenye glasi", niliagiza.

"Usijali kaka", akaondoka.

Watu waliokuwa ndani ya bar hii walikaa kimya wakifuatilia taarifa ya habari ya saa mbili. Habari kubwa ni utumbuaji majipu unaofanywa na Serikali. Watu walianza kuchoshwa na habari hii ambayo imekuwa ya kawaida kwenye vyombo vya habari.

Wakati najaribu kutafakari hili na hili na kazi zangu za kesho, mara kijana mmoja alisimama mbele ya meza yangu.

"Habari kaka?" alisema kijana huyu huku akivuta kiti kwa ajili ya kuketi.

"Salama", nilimjibu kwa mkato, vinywaji vyangu vililetwa, nikaanza kunywa huku nikimtafakari mtu huyu kimya kimya, sikuwa na sababu za kumzuia kuketi, baada ya kushikana nae mikono, akaketi.

"Samahani, naitwa Mhandisi David John kutoka Comoro, nimekuja kama kwa ajili ya kushuhudia uzinduzi wa bomba la gesi, ama kweli huu ni uwekezaji mkubwa katika eneo hili", alieleza kijana huyu.

"Inawezekana", nilisema kwa mkato

Nilijaribu kumtafakari tena kijana huyu, lakini sikuwa na jawabu la haraka, kutokana na uzoefu wa kazi hii kwa muda niliamini kijana huyu hakuwa mtu wa kawaida, mkono wake pekee ulinidhihirishia hivyo. Nilikunywa taratibu huku nikiwa katika hali ya hofu.

"Samahani kaka, kuna umbali gani kutoka Dar es Salaam hadi Mtwara?", alihoji kijana huyu.

"Sina hakika", nilimjibu kwa mkato.

"Inaweza kuwa kilomita mia sita hivi, au zaidi?" aliuliza kwa mara nyingine.

"Nimesema sijui", niliongea kwa sauti ya kutisha kidogo ili asiendelee kuuliza.

"Nasikia Tanzania kuna bomba la mafuta lililounganishwa na Zambia, hivi ni kweli?" aliendelea kuuliza.

Niliinua glasi, nikanywa wisky yote iliyokuwa ndani ya glasi, "Mimi si Mhandisi. Lakini Wewe umejinadi kuwa ni Mhandisi, kwanini usijue kuhusu hilo bomba la mafuta kutoka Tanzania kwenda Zambia?" akacheka.

Mara nikasikia miguu yangu inaguswa na kitu, nilishituka, lakini nilikuwa nimechelewa. Nilipigwa shoti na kitu ambacho sikukijuwa, miguu na mikono yangu iliishiwa nguvu taratibu nikapoteza fahamu.

ITAENDELEA 0784296253
 
SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA.



Nilizinduka na kujikuta ndani ya chumba kidogo chenye joto kali na giza nene, mikono na miguu yangu ilikuwa imefungwa madhubuti kwa kamba ngumu. Upande wa mikono yangu ulifungiwa kwenye nondo za dirisha, huku miguu ikifungwa upande mwingine kwa lengo la kunizuia kabisa nisiweze kugeuka. Hakika nilikuwa kwenye kitanzi cha mauti.

Kichwa changu kilikuwa katika maumivu makali, nadhani yalisababishwa na aina ya vifaa walivyotumia adui zangu wakati wakiniteka nyara. Nilijaribu kuinua kichwa juu kuangalia jinsi nilivyofungwa sikuweza, nikapoteza matumaini ya kuishi tena katika dunia hii.

Akili yangu ilifanya kazi haraka, nilijiuliza jinsi nilivyofika ndani ya chumba hiki. Baada ya kutafakari kwa kina, nikakumbuka kuwa wakati napata kinywaji pale Bella Hotel, eneo la Kinyerezi, alikuja mtu mmoja akaketi karibu yangu, nakumbuka wakati tunaongea na mtu huyu niliguswa na kitu katika miguuni yangu, nikapoteza fahamu. "Nani hasa wamenileta katia chumba hiki. Kwanini hawakuniua kama kusudi lao lilikuwa hivyo", nilijiuliza.

Kutokana na giza nene lilolokifunika chumba hiki, sikujua eneo nililokuwa, hata kama kungekuwa na mwanga bado ilikuwa vigumu kujuwa. Milijilaumu kuwaacha wenzangu, Julius Nyawaminza, Claud Mwita na Fred Libaba, nilijiuliza jinsi watakavyopata shida kunitafuta bila mafanikio. Lakini pia niliona vizuri wao kuendelea pale nilipofikia. Nilijiuliza hili na lile, nikakosa majibu ya haraka, nikaishia kukubali matokeo.

Niliwakumbuka watoto wangu wapendwa, Warioba, Changasi na Masey, ambao walikuwa bado wadogo sana wakihitaji msaada wangu, niliwahurumia jinsi watakavyolia baada ya kusikia kifo changu. nijaribu kukumbuka tena niko wapi nikakosa jibu la haraka. Nilimkumbuka mama yangu mzazi, Nyamadoho, nilijiuliza jinsi atakavyolia baada ya kupata taarifa za kuuawa kwangu.

Joto kali ndani ya chumba hiki, lilizifanya nguo zangu za mwilini kulowa maji ya jasho, nilijaribu kwa mara nyingine kupima kiwango cha kamba nilizofungwa upande wa mikono na miguu, zilifungwa kwa uhakika.

Nilisikia watu wakitembea nje ya chumba hiki, halafu mlango ukafunguliwa, mimi nikafumba macho na kurejea katika hali yangu ya awali, ya mtu aliyezimia. Watu wawili waliingia ndani, mmoja aliwasha taa, mwingine akasogeza sikio karibu yangu.

"Bado hajaamka huyu. Nadhani, bado masaa machache atakuwa amezinduka, daktari alisema pigo alilopata litamchukua masaa matatu hadi manne, kwa vile mtu mwenyewe anafanya sana mazoezi", mmoja wa watu hawa alieleza.

"Mimi sikuona sababu ya kumuacha hai mpaka sasa, watu wa aina hii ni hatari sana, kwa vile bosi ametaka kumuua kwa mikono yake, basi tusubiri azinduke", alisema mtu wa pili.

"Namsikilitikia sana, maana atakufa kifo kibaya mno, Carlos alivyo na hasira na mtu huyu, anaweza hata kumla nyama", alisema mmoja wa watu hawa, huku mapigo ya moyo wangu yakinienda kasi.

Halafu wakaingia watu wengine zaidi ya sita, akiwemo mzungu Carlos Dimera. Mmoja wa watu hawa alikuja moja kwa moja karibu yangu na kunimwagia maji mengi kichwani, mengine yaliingia katika masikio, nikajidai kushituka na kujaribu kuvuta kamba ili nisimame.

"Tulia wewe masikini mjinga, umerukaruka hatimaye umeingia kwenye anga zangu. Teacher... ulifanikiwa kututia hasara, umevuruga mipango yetu, lakini waswahili walisema siku za mwizi ni arobaini, leo arobaini yako imetimia. Niliahidi kuwa siku moja nitakuchinja kwa mikono yangu, siku hiyo imefika", Carlos alisema huku akicheka.

"Ni kweli... kama ulivyosema, siku za mwizi ni arobaini, lakini mimi si mwizi, hata wewe arobaini yako itafika, heri yangu mimi ambaye arobaini imenikuta nikitetea watuwanyonge, jiulize arobaini yako itakuwaje?" nilimwambia.

"Kwa taarifa yako nguvu yetu ni kubwa, mtu mwenye pesa hafungwi kaka, ndiyo maana nikasema leo ndiyo mwisho wa maisha yako, wenzako wengi walijaribu wakashindwa, nilijiuliza wewe utaweza? Sasa utauawa baada ya mahakama kutoa hukumu ambayo itawashangaza wengi, Hawa na Tony hawana hatia, pamoja na hilo, madawa uliyokama uwanja wa ndege yatarejeshwa mikononi mwetu..., oh pole sana Teacher kwa kupoteza muda wako", Carlos alieleza kwa kebehi.

"Sidhani kama hakimu atakuwa mpuuzi kiasi hicho, mpaka akubali kuharibu kazi yake, hata kama nitakufa leo, sijui kifo gani? Lakini siogopi, maana kifo ni kifo tu, hata wewe siku yako itafika, sijui utajibu nini mbele za mungu", nilimwambia, akasogea karibu yangu na kunipiga kibao kwa hasira.

"Sina muda wa kubisha na mtu mjinga, wengine tunatafuta maisha mazuri, wewe unatafuta kifo, jiandae kufa, kibaya zaidi ni kwamba hata ndugu zako hawataiona maiti yako", alitamba.

"Hewezi kujisifu kwa kumpiga maiti, ungekuwa mwanaume ungenitafuta wewe ili nikuonyeshe kazi, bila shaka habari yangu umewahi kuisikia ndiyo maana ukakodi majasusi kutoka nje ambao siku chache zijazo watakuwa mikononi mwa serikali, kuniua mimi usidhani utakuwa umemaliza tatizo, serikali ipo tu", nilisisitiza.

"Hilo unasema wewe, wenzako katika serikali wanapenda kuishi katika maisha mazuri ndiyo maana nikasema hukumu itakayotolewa leo kuhusu Hawa na Tony, itakushangaza hata wewe na wengine wasiojitambua".

"Mimi najitambua, ndiyo maana nikasema haiwezekani, labda kwa mtu mjinga kama wewe ndiye utaamini hivyo", nilisema kwa hasira huku nikisikia maumivu makali katika mwili wangu.

"Simba na Nyati, mchapeni huyu mpuuzi", Carlos aliagiza, wakaanza kunitandika ngumi za tumboni, walinipiga jinsi walivyoweza, nilisikia maumivu makali, lakini kwa vile nilijua hii ndiyo siku yangu ya mwisho, sikujali.

"Nyie vibaraka, mnaotumwa kuwahujumu wenzenu, shauri yenu, siku yenu itafika, mtalia na kusaga meno", nilisema huku nikipiga kelele.

Baada ya kunipiga sana, mmoja alizima taa, wakatoka ndani ya chumba hiki wakafunga mlango na kuniacha nikiwa nimefungwa madhubuti ndani ya chumba hiki, niliomba mizimu ya kwetu inisaidie, nilimuomba marehemu bibi yangu Matobela, aliyenilea toka nikiwa mchanga. Nilikumbuka jinsi bibi alivyonitokea siku niliyopata ajali katika maeneo ya Gairo, nikitoka Dodoma kurejea Dar es Salaam usiku, bibi akiwa ndani ya mavazi meupe na alinisimamia nikafika salama. Hivyo nilimtegemea leo pia.

Maumivu makali katika mwili wangu nusura nipoteze tena fahamu. Nilimkumbuka Kanali Benny Emilly, Mkuu wa kitengo cha upelelezi, nilijiuliza jinsi atakavyohaha kunitafuta, jinsi atakavyoumizwa na taarifa za kuuawa kwangu, nilijilaumu kwa makosa ya uzembe niliyofanya hata nikakamatwa kama kuku.

Wakati nikiendelea kutafakari, mara nikahisi nyayo za mtu zikiukaribia mlango, sekunde chache baadae taratibu mlango wa chumba hiki ulifunguliwa, mtu mmoja aliingia kwa mwendo wa kunyata. Kutokana na hali ya giza ndani ya chumba hiki, niliangalia kwa makini, alipowasha taa mimi nikafumba macho.

"Teacher, Teacher, Teacher amka", sauti nyepesi ya Mama Feka ilisikika katika masikio yangu.

"Naam", niliitika.

"Nilidhani umezimia tena?", alihoji huku akitoa kisu kidogo kwenye matiti yake na kuzikata kamba zilizofungwa kwenye mwili wangu. "Naomba unisikilize, kuna ulinzi mkali sana huku nje, ukitoka muda huu hutaweza, cha msingi endelea kuwa humu ndani, Carlos anasuburi mahakama imalize kutoa hukumu halafu aje kukuchinja, usihofu, wewe jiweke sawa ili wakija uwe vizuri", alieleza Mama Feka.

"Lo, Mama Feka, ni wewe kweli Molamu au malaika kashuka kutoka mbinguni, hakika umekuja kuniokoa wakati ambao sikutegemea kabisa, amini siwezi kufa tena, nitajitetea kwa nguvu zangu zote, jinsi ulivyoingia nilidhani Ninja", nilitania.

"Kama ulivyonielekeza".

"Tuko wapi hapa?, nilimuuliza.

"Utapajua baadaye, si wajuwa Dar es Salaam mimi mgeni", akazima taa.

"Umejuwaje niko ndani ya chumba hiki?".

"Tutaongea baadae Teacher, wako kwenye kikao cha mwisho, wanasubiri taarifa ili Carlos aongee na wewe tena, halafu akuchinje, ndiyo nikatoka kama nakwenda kujisaidia, muda huu si wa kuongea, nikichelewa watanitafakari", alieleza Mama Feka na kutoweka.

"Kila la heri", nilimwambia huku nikisimama kuweka viungo vyangu vya mwili vizuri, nilitumia nafasi hiyo kufanya mazoezi ya viungo, niliruka na kupiga push up kadhaa, baada ya kuuandaa mwili wangu kwa kazi, niliuvuta mlango taratibu ili nitoke, kumbe Mama Feka alipotoka aliufunga kwa nje. Ikanibidi kusubiri kitakachotokea.

Vifaa vyangu kadhaa vya kazi, ambavyo mimi huvificha sehemu mbalimbali ya mavazi yangu, vilikuwa vimechukuliwa isipokuwa kamba ndogo sana, ambayo niliifungia kiunoni kwangu, kwa muda mfupi nikabaini kuwa watu walioniteka walikuwa wajuzi wa hali ya juu katika tasnia hii. Lakini niliamini kuwa nilikuwa mjuzi zaidi yao. Nilijiuliza kama walikuwa wajuzi wa mambo kwanini wasije wao binafsi kama wao, waliujuwa muziki wangu ndiyo maana walijiandaa, wangekiona cha moto.

Mara nikazisikia nyayo za watu zikiusogelea mlango, haraka nilitumia nafasi hiyo kutoa balbu juu, nikasimama karibu na sehemu ya kuwashia taa. Mlango ulifunguliwa, mtu wa kwanza aliingia akaelekea sehemu ya kuawashia taa, alipobonyeza kitufe ili taa iwake, giza liliendelea kutawala.

"Balbu imeungua", alisema.

"Haiwezekani, imeungua saa ngapi? Labda kuna sababu", alihoji mwingine wakati nae akiingia ndani.

Kutokana na hasira niliyokuwa nayo, niliruka na kumpiga mmoja karate ya shingo, nikamsindikiza za teke la kifua akaenda chini, wakati mwenzake akijiuliza nini kimetokea, nilimdaka na kumgeuza mbele nyuma, huku nimembana vizuri kwenye koromero, akashindwa kutoa sauti. Niliwaua haraka sana, halafu nikawaburuza kuwatoa pale mlangoni.

Walikuwa wamevaa mavazi yaliyofanana, suluali nyeusi, makoti ya rangi ya blue na kofia nyekundu, nilichukua mavazi ya mmoja wao aliyekuwa na umbo kama langu nikavaa, niliwapekuwa, kila mmoja alikuwa na silaha kubwa aina ya AK 47, niliitwaa silaha moja na nyingine nikachomoa magazini, nikiwa na matumaini tele. Mimi nikiwa na aina hii ya silaha hata uniletee Kombania nzima ya jeshi, hawaniwezi.

Nilitoa magazini, nikahakiki idadi ya risasi zilizokuwa ndani, kila magazini moja, zote zilikuwa na ujazo sawa, yaani risasi. Bahati nzuri ni kwamba bunduki hii ilikuwa zimekatwa kwenye mtutu wa mbele ili risasi zinapotoka zisitoe sauti.

"Jamal, Jamal..., fanyeni haraka", sauti kutoka nje ilisikika.

"Njoo uone", nilisema kwa sauti ya kubana. Akasukuma mlango na kujitosa ndani, alivaa kama wenzake, huyu alikuwa na bunduki aina ya SMG ikiwa begani.

"Unasemaje?" nilimuuliza kwa sauti ya kutisha, aliposikia sauti yangu, akaamini kuwa mimi siyo Jamal, akakurupuka ili atoe bunduki begani, lakini alikuwa amechelewa, nilimpiga risasi ya kifua, akaanguka chini. Nilimvua bunduki yake nikatoa magazini, sasa nilikuwa na risasi za kutosha, kukabiliana na adui wa aina yoyote. Nikajidhatiti na kutoka ndani ya chumba hiki.

Nilijiuliza wapi watu hawa wamepata aina hii ya silaha za kivita, silaha ambazo haziruhusiwi kwa watu binafsi, nilitafuta sehemu nzuri, nikajibanza kisubiri kitakachotokea. Sikuwa na saa lakini ilikaribia kuwa saa nane, tisa au kumi za alfajiri, kutokana na utabiri wangu.

Ukuta mkubwa uliopambwa kwa nyaya za umeme juu uliizunguka ngome hii, nilisikia kelele za mashine zikifanya kazi huku na huko, ilionekana sehemu hii ilikuwa ya viwanda, nilitoa kamba yangu niliyojifungia kiunoni nikaikata kidogo, nilitumia kipande hicho kufunga magazini mbili za risasi pamoja, moja ikiangalia chini na nyingine juu, nilifanya hivyo ili magazini moja itakapoishiwa risasi iwe rahisi kwangu kuchomoa na kupachika nyingine haraka.

Pamoja na kuvaa mavazi kama wao, lakini nilitembea kwa kunyata, maana sikujua wanazotumia mawasiliano gani kwenye ngome hii, taratibu nilitafuta mlango mkubwa wa kutokea, nilipouona, nikafanya kazi nyingine ndogo, kutafuta sehemu waya za umeme zinazolinda ukuta huu zilikotokea, hii pia nilifanikiwa.

Kwenye langu kuu kulikuwa na askari wasiopungua sita, wote wakiwa na silaha aina ile ile AK 47, hawa walikuwa wakitembea huku na huku kuangalia usalama wa eneo hilo.

Mara nikawaona watu wawili wakitoka kuelekea kwenye mahabusu yangu, chumba ambacho nilikuwa nimefungiwa, walivaa sawa na mimi, koti la blue, suluali na kofia nyekundu. Niliwafuata taratibu, nilipowakaribia, niliachia risasi kadhaa zikawapata, mmoja alikufa pale pale, mwingine akapiga kelele za kuomba msaada kutokana na maumivu aliyopata. Kumbe nilikuwa nimechokoza mzinga wa nyuki.

Risasi zilipigwa mfululizo pale nilipokuwa, bahati nzuri nilikuwa nimelala kifudifudi, nilisubiri wasogee, halafu nikaachia tena risasi kadhaa zikawapata. Kumbe walikuwa wengi, wengine wakitoka ndani, hivyo ilinipasa kutumia hesabu zaidi.

Nilipanda juu ya ukuta uliokuwa mbele yangu, niliweza kuwaona vizuri, niliachia tena risasi nikaua kadhaa, nikaruka na kukimbilia upande mwingine, nikiacha eneo hilo likichakazwa kwa risasi. Nilikuwa nimejibanza eneo lingine, walipoona kimya wakasogea, nikatumia nafasi hiyo kuwafyatulia risasi, nikaua askari wao kadhaa na kuhama haraka sehemu niliyokuwa. Wakaichakaza tena sehemu hiyo kwa risasi.

Kelele za askari zilisikika kutoka kila pembe ya ngome hii, wakisema, "piga risasi huyo, ua kabisa", lakini mimi nilikuwa na kusudi moja tu, kumsaka Dimera, aliyenipiga kibao wakati nimefungwa kamba. Mara nikamuona Dimera, Mama Feka na vijana wawili wakiingia ndani ya gari, lango kubwa likafunguliwa na gari hilo kutokomea nje.

Ilikuwa nafasi nzuri kwangu kumshambulia Dimera, hata kumuua kwa risasi, lakini niliogopa kitu kimoja, ningeweza kuhatarisha maisha ya Mama Feka. Wakafanikiwa kutoweka huku nikirusha risasi bila mpangilio, askari waliokuwa mlangoni walikimbia nami nikapata upenyo na kutoka.

Nilipotoka nje, sikuyaamini macho yangu, kumbe mahabusu yangu ilikuwa ndani ya kiwanda cha Blanket, kilichoko Keko. Nilijiuliza imekuwaje watu hawa watumia sehemu hii, kutokana na muda, niliahidi kulifuatilia baadaye. Nikaondoka.

ITAENDELEA 0784296253
 
SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA



Baada ya mimi kuachana na wenzangu usiku ule, kila mmoja alitafuta uelekeo wake, Luteni Claud Mwita alipanga Elegant Lodge iliyoko kando ya barabara kuu inayotoka Majumba Sita kwenda Segerea. Julius Nyawaminza hakuona sababu ya kwenda mbali, akajihifadhi FQ Hoteli iliyoko hatua chache kutoka Elegant, katika barabara hiyo hiyo ya Segerea. Fred Libaba yeye aliingia Kilimani Lodge akaweka makazi yake ya muda,

Baada ya kufanikiwa kuwatoroka watu hawa, nilitembea kwa tahadhali kubwa, giza lilikuwa bado limetanda kwa nje. Kutoka kiwanda cha Blanket Keko, niliambaa na barabara ya Chang'ombe hadi, hapo nilikodi Bodaboda iliyonipeleka Segerea.

Ilikuwa saa kumi na moja kasoro dakika kidogo za alfajiri, nilipobisha hodi kwenye mlango wa chumba cha Luteni Claud Mwita, Elegant Lodge kama tulivyokuwa tumeelekezana awali. Niligonga haraka haraka kwenye mbao za mlango huu mara tatu, halafu nikasubiri kidogo. Giza lilikuwa bado limetanda kwa nje, taa zenye mwanga hafifu zilileta nuru sehemu ya kupita kuingia ndani ya jumba hii la kisasa. Baada ya kugonga nilisubiri kwa muda, Wakati najiandaa kugonga tena, ghafla nilisikia shingo yangu ikiwa baridi, chuma kizito kilinigusa vizuri shingoni, nikatulia na kujiandaa kugeuka kwa mzaha.

Kwanza nilidhani ni utani wa Claud. Wakati najaribu kugeuka nyuma yangu ili nifanye mzaha, sauti nzito ilisikika. Haikuwa sauti ya Claud kama nilivyoizoea. "Tulia kaka, inua mikono yako juu, halafu ugeuke taratibu upande wangu. Onyo, usithubutu wala kujaribu kufanya ujanja wa aina yoyote, maana jaribio lako lolote litakusababishia hasara".

Utabiri wangu haukuwa umebashiri vizuri kama nilivyoanza nikidhani ni Claud, matumaini yangu ya kutoka salama kwenye mahabusu ya awali yalitoweka. Jasho jembamba lilinitililika. Nilitii amri hiyo na kuweka mikono yangu juu kama nilivyoagizwa kufanya, niligeuka nyuma, macho yangu yalikutana na macho makali yanayong'ara mfano wa jini. Mtu mrefu mnene aliyeshiba vizuri, Bastola yake ikiwa mikononi mbele yangu, alikotoke sikujua.

"Pole sana Teacher, labda nisema leo una bahati mbaya mno, siku ya kufa kwako imefika, hata utende miujiza ya aina gani leo ni siku ya hukumu yako, ni kweli umefanikiwa kutoroka mikononi mwa Carlos Dimera, lakini umeishia mikononi mwangu, Naitwa Ninja Mweusi asiyeshindwa", alisema mtu huyu aliyefunika uso wake kwa kofia nyeusi na kuruhusu macho yake tu kuona.

Nilimwangalia mtu huyu kwa tahadhari kubwa. Akili yangu ilianza kufanya kazi haraka, nilijiuliza ilikuwaje mtu huyu afike eneo hili la siri, ambalo hata Kanali Emilly hakuweza kulijua. Baada ya kujiuliza na kutafakari, nikabaini kuwa inawezekana mtindo waliotumia kuniteka usiku kule Hotel Bella Vista waliutumia kuwatafuta wenzangu.

"Nimekukosea nini mpaka unitangazie kifo, kwani wewe ni Mungu?" nilimuuliza.

"Usiniulize maswali magumu ya kipuuzi, kwa taarifa yako sikuja hapa kujibu mwaswali, wewe na mpuuzi mwenzio uliyempangishia chumba hiki mmefanikiwa kwa kiasi fulani kurudisha jitihada zetu nyuma, lakini baada ya vifo vyenu, naamini tutaanza kwenda mbele", alisema mtu huyu kwa sauti ya kutisha na kukatisha tamaa.

"Mwenzangu ni nani?" nilimuuliza tena.

"Bila shaka nimekwambia naitwa Ninja Mweusi. Lakini utanifahamu vizuri baada ya kifo chako, malaika watakuletea sura yangu utanifahamu. Haya, haraka geuka nyuma", alisema tena kwa sauti ya kutisha, haraka nilitii amri hii nikageuka nyuma.

"Sikiliza, hivyo hivyo ulivyoweka mikono yako juu, tembea kuelekea upande wako wa kushoto, baada tu ya kushuka ngazi utaelekea tena kushoto, mbele kidogo kuna ngazi fupi, baada ya hizo ngazi utaelekea tena kushoto, fungua mlango utakaokuwa mbele yako, utakapotoka nje utaona gari ndogo BMW yenye rangi ya blue, utafungua mlango wa nyuma upande wa dereva itangia ndani, bila shaka utafurahi kuonana na mwenzio", alisema mtu huyu mimi nikaanza kutembea kufuata maelekezo yake.

Kama nilivyoelekezwa, nilitembea hadi kwenye gari hili, lililokuwa nje. Pamoja na kuingia kwa tahadhali kubwa katika eneo hili, nilijilaumu sana mimi kukamatwa kama kuku. Nilifungua mlango wa nyuma ya dereva, nikaingia ndani. Taa ndani ya gari hili iliwashwa. Claud alikuwa amefungwa mikono kwa nyuma, jasho jingi lilimtoka mwilini, nadhani kwa sababu ya mateso na kipigp alichopata kutoka kwa watu hawa baada ya kumteka. Nilipoingia ndani ya gari hili, haraka mtu mmoja aliifunga mikono yangu kwa kamba ngumu, nikavishwa soksi kichwani ili nisiweze kuoma, mtu mmoja ambaye sikumuona vizuri aliingia na kukaa juu yangu.

"Mnatupeleka wapi? Kama kutuua hata hapa inawezekana", niliwauliza kwa shauku.

"Sehemu ambayo ni nzuri nyinyi kujibu maswali yetu na baada ya hapo vifo vyenu vinafuata, ni kosa la jinai maiti zenu kuonekana baada ya kuuawa", alisema mmoja wa watu hawa.

"Mnadhani sisi tutawajibu nini zaidi ya kusubiri vifo vyetu?", niliwauliza huku dereva akiondoa gari eneo hili.

"Tunakujua kabisa kuwa wewe una kichwa na roho ngumu kama ya paka, lakini leo umekutana na watu wenye vichwa na roho mbaya sana. Tunaweza kuongea na wewe kirafiki, lakini pia tukiona huelewi maana ya urafiki, tutakufanya uongee kwa lazima. Uwezo huo tunao", alisema mtu huyu.

"Unaweza kumfanya marehemu aseme?".

"Ikibidi atasema".

Nilijaribu kutuliza akili yangu ili niweze kuisikia sauti ya mtu huyu vizuri. Alijitahidi sana kuongea kiswahili, lakini hakikuwa kiswahili cha mtanzania halisi. Matamshi ya mtu huyu anaweza kuwa raia wa Congo ama Uganda.

Baada ya mwendo wa dakika kadhaa, gari lilisimama, dereva alipiga honi, tukasikia lango la chuma linafunguliwa. Sauti kutoka ndani ya gari ikahoji. "Bosi yupo?".

"Bosi ameingia muda si mrefu, anawasubiri", sauti kutoka nje ya gari ilisikika.

"Tumewaleta hawa washenzi wengine wawili. Idadi yao sasa imefika watatu, huyo mmoja naamini tutamtia mikononi leo", alisema mmoja wa watu hawa kwa kujiamini. Mapigo ya moyo wangu yalibadilika, akili yangu ilihama, nikaamini kuwa mwisho wetu umefika, nikajiuliza mwenzetu mwingine kati ya Julius Nyawaminza Fred Libaba, nani atakuwa ametekwa kama sisi.

Lango lilifunguliwa, gari likaingia ndani, baada ya mwendo wa sekunde kadhaa lilisimama tena, milango ikafunguliwa watu hawa wakatoka nje. Sisi tulikuwa tumefungwa vitambaa machoni hivyo hatukuweza kuonana kinachoendelea, wala kujua tulikuwa wapi.

"Imekuwaje?" nilimuuliza Claud baada ya watu hawa wote kutoka ndani ya gari na kutuacha peke yetu.

"Hata mimi sijui, nasikia maumivu makali sana kifuani, watu hawa ni wajuzi katika mambo ya ujasusi, inawezekana leo ikawa mwisho wa maisha yetu", Claud alisema kwa sauti ya kukata tamaa.

"Katika maisha, usiogope lolote Claud, kila lililopangwa na Mungu litatimia, acha watuue, wataua wangapi?. Sisi ni binaadamu wa kupita kama ilivyo wao, tukifa leo tutakuwa tumekufa kwa jambo jema, watatokea wengine wataendeleza hapa tulipofikia, mimi naamini hivyo", nilimwambia.

"Lakini tutakuwa tumeacha pengo kubwa sana, vifo vyetu nadhani vitarudisha nyuma kasi ya mapambano, siogopi kufa ila naumia kuona jitihada zetu zinaishia njiani", Claud alilalama.

"Siku zote Mungu husikia kilio cha wengi, sisi tunapigana kuokoa wengi, hata tukifa leo, siku moja majina yetu yatasikika miongoni mwa mashujaa... Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema askari shujaa ni yule anayefia vitani, akirudi nyumbani, anarudi na ushindi, tusikate tamaa, nafasi ya kuishi bado ipo, japo ni finyu sana", nilimwambia.

"Asante kwa kunitia moyo bosi", Claud alisema kwa sauti ya kujiamini. "Nikiwa na wewe siogopi". Milango ya gari hili ilifunguliwa tukatolewa ndani kama kuku. Baada ya kushushwa tulisukumwa kupelekwa sehemu isiyojulikana. Eneo hili lilikuwa kimya kabisa, kwa vile tulikuwa tumefunikwa nyuso zetu kwa kofia nyeusi hatukuweza kujua mahali tulipokuwa.

Kofia nyeusi tulizovalishwa wakati tunaletwa hapa ziliondolewa vichwani mwetu, tulijikuta mbele ya Carlos Dimera, alikuwa ameketi kwenye kiti kikubwa akivuta sigara kubwa iliyosokotwa kwa karatasi ngumu. Sekunde chache baadaye Julius Nyawaminza aliunganishwa nasi, alikuwa amechoka sana, nilipomwangalia niliamini kuwa alikuwa katika mateso makali.

"Ulijitia mjanja, ukanikimbia. Lakini waswahili wanasema ndege mjanja hunasa kwenye tundu bovu, kuku hata awe mjanja kiasi gani anategwa kwa mahindi na punje za ulezi tu, nikusifu kwa kuweza kutoroka sehemu ambayo si rahisi mtu kutoroka, hongera sana", Carlos Dimera alisema huku akiniangalia kwa hasira.

Mama Feka aliketi upande wa kushoto karibu kabisa na Carlos, aliniangalia kwa macho ya wizi halafu akasimama na kuelekea upande wangu. Alivaa mavazi yaliyompendeza sana, suluali nyeusi, fulana ya kijani, raba miguuni na kofia nyeusi. Hakika alionekana kuvutia zaidi.

"Wewe ni binadamu wa aina gani?. Usiku wa kuamkia leo nusura uniue kwa risasi, isingekuwa mipango ya Mungu labda sasa ningekuwa maiti, sasa kabla ya kifo changu, utaanza kufa wewe", Mama Feka alisema huku akitembea kuelekea kwangu. Alinitandika kibao, nikaona nyita.

"Teacher, kabla hamjaingizwa kwenye chumba cha mateso kama huyu mwenzio alivyofanyiwa, nikuulize swali moja rahisi sana, ukijibu nitawaruhusu muondoke", Carlos alisema.

"Niliulize", nilimjibu kwa sauti ya kutojali.

"Yupo mwenzenu mmoja anaitwa Fred, yuko wapi kijana huyu?" Lilikuwa swali kutoka kwa Carlos.

"Simjui", nilijibu kwa mkato.

"Humjui Fred Libaba?" alihoji.

"Nimesema simjui", nilijibu kwa msisitizo.

"Kama humjui Fred, basi ina maana hata hawa uliosimama nao hapa mbele yangu... Huwajui?".

"Hakika siwajui, nimeshangazwa kuunganishwa na watu ambao sijawahi hata kuwaona katika historia ya maisha yangu", nilisema.

"Usinitie hasira, mpumbavu mkubwa, tafadhali usinifanye nikavua hili gamba la ustaarabu nilililovaa leo, kama utapenda kuliona jua la saa nne leo, jibu maswali yangu", Carlos alieleza.

"Nitajibu maswali ambayo nayafahamu, lakini usinilazimishe kujibu maswali ambayo binafsi siyajui".

"Mpumbavu mkubwa, mlipowakamatwa vijana wangu, Hawa na Ton eneo la Kipawa wakiingiza dawa za kulevya, mkawapeleka haraka mahakamani, mliona fahari sana kufanya vile?".

"Unapomkamata mhalifu wa aina ile lazima ufarijike, mimi kama mimi nilijisikia vizuri, pamoja na kwamba wewe ilikukera, lakini wengi walifurahi sana kukamatwa kwa dawa za kulevya ambazo ni hatari kwa matumizi ya watu".

"Ahaa, una hakika ni hatari kwa matumizi ya watu. Wewe na hao wengi unaosema mmenufaika nini baada ya watu wangu kukamatwa?".

"Tumenufaika sana, kuzuia uchafu kuwafikia vijana wetu ni faida kubwa", nilijibu swali hili kwa kujiamini, maana nilijua nitakufa.

"Mussa hebu mtie adabu huyu paka", Carlos aliagiza. Kijana mmoja aliyeshiba vizuri alisimama na kunijia, aliponifikia alinipiga ngumi kadhaa nzito tumboni. Aliendelea kunipiga kwa hasira. Sikuweza kumfanya kitu kwani mikono yangu ilikuwa nimefungwa kwa kamba. Nilisikia maumivu makali tumboni, nikavumilia.

ITAENDELEA 0784296253
 
SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI



Ilikaribia kuwa saa mbili za asubuhi ya Jumatano, siku ambayo ilikuwa rasmi kwa ajili ya mahakama kutoa hukumu dhidi ya watuhumiwa wa dawa za kulevya. Viongozi kadhaa wa Chama na Serikali walifika mahakamani hapa ili kusikiliza hatma ya kesi hii.

Vijana wa Polisi kutoka kikosi maalumu cha kutuliza ghasia walipita huku na huku kuimalisha ulinzi katika eneo hili. Huku magari kadhaa ya Jeshi la Magereza yakiwa na askari wengi kutoka kikosi maalumu wakisubiri. Wafanyabiashara wa dawa za kulevya nao walituma vijana wao kadhaa, ambao walifika mahakamani hapa kusubiri hatma ya Hawa Msimbazi na Tony Sime.

Carlos Dimera, alikuwa amepinga wazo la vigogo wa ngazi za juu katika kundi hilo, waliokutana katika jiji la Bogota, nchini Colombia na kuafikiana kuwatosa watuhumiwa hawa kwa ajili ya kulinda maslahi yao. Dimera alipinga vikali wazo hilo kwani aliwaamini sana vijana hawa. Inasemekana kabla hawajajiunga naye aliwanywesha maji yaliyochanganywa na damu yake.

Katika kikao cha dharura kilichofanyika usiku, Dimera na vijana wake walipanga mikakati ya kila aina ili kuwaokoa Hawa na Tony, kutoka katika mikono ya sheria. Hii ilikuwa siku ya tatu kwa watuhumiwa hawa kuwa mikononi mwa vyombo vya sheria, wakisubiri na kuamini nguvu ya pesa itawaweka huru.

Kutoroka kwa Teacher usiku ule kuliwaumiza sana. waliamini kuwa mipango yao haitafanikiwa. Faraja iliwajia baada ya Teacher kutekwa tena alfajiri, wakaamini kuwa mipango yao itakuwa swa.

Mahakama ilifulika watu, kila mmoja akiwaza hili na lile. Ilikuwa imeahilishwa jana kutokana na hoja mbalimbali zilizowasilishwa mahakamani hapo, kufuatia malumbano ya kisheria na leo ilikuwa siku rasmi ya kutoa hukumu. baada ya taratibu zote za kimahakama, kama kawaida, askari maalum alipaza sauti kuashiria kuingia kwa mheshimiwa Hakimu, watu wote alisimama.

Kanali Benny Emilly, ambaye ndiye Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi, alikuwa mmoja wa watu waliofika hapa, Mzee huyu alikuja kusikiliza hukumu ya kesi hii akiwa na baadhi ya wasaidizi wake kadhaa. Kabla ya kufika mahakamani hapa alifanya kila njia kuwasiliana na Teacher, hakubahatika kupata mawasiliano yake. Baada ya Hakimu kuingia na kuketi katika kiti chake, alichukua baadhi ya mafaili yaliyokuwa mezani hapo na kuyapitia moja baada ya jingine, baadhi aliyaweka kando, hatmaye akabakiwa na faili moja mkononi.

"Kutokana na umuhimu wa kesi ya uhujumu uchumi iliyo mbele yangu, nimelazimika kuahilisha kesi zingine zote zilizokuwa zitajwe leo, wahusika katika kesi hizo wafike chumba cha kumbukumbu kwa ajili ya maelekezo zaidi ikiwa pamoja na kupangiwa tarehe nyingine ya kesi, nitasikiliza kesi ya kuhujumu uchumi inayowahusu Hawa Msimbazi nana Tony Sime, bila shaka wapo?", Hakimu alihoji baada ya kueleza.

"Naam mheshimiwa, wateja wangu wako mbele yako", alieleza Kyaruzi, ambaye ni mwanasheria upande wa utetezi. akaandika maelezo, baada ya kujiweka sawa, akasema.

"Mwendesha mashitaka".
"Mheshimiwa Hakimu, kesi iliyoko mbele yako ni Kesi namba 208 ya mwaka huu, kama ilivyosomwa hapo awali, washitakiwa Hawa Msimbazi na Tony Sime, wanashitakiwa kwa pamoja kuwa mnamo tarehe 15 ya mwezi huu, huko Uwanja wa Ndega wa Dar es Salaam, walikamatwa na askari wakijaribu kuingiza dawa za kulevya aina ya heroine, ambalo ni kosa la kuhujumu uchumi", akageuka.

"Mheshimiwa, baada ya watuhumiwa hawa kukamatwa kwanza walikaidi amri halali waliyopewa na askari, wakidai kuwa mzigo wao si dawa za kulevya isipokuwa ni malighafi kwa ajili ya kiwanda chao cha kutengeneza tembe za kutibu malaria. Ili kujiridhisha, malighafi hizo zilipelekwa kwa mkemia mkuu wa serikali. Ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali imethibitisha kuwa mzigo uliokamatwa ukiingizwa nchini ni dawa hatari za kulevya aina ya heroin ambazo zimepigwa marufuku na Serikali ya Tanzania kuingizwa hapa hapa nchini".

Haraka mwanasheria wa utetezi akasimama na kugonga meza, "Mheshimiwa Hakimu, suala la dawa za kulevya si jambo la kufanyia mchezo, kama wateja wangu walivyoieleza mahakama yako tukufu jana kuwa hawahusiki kabisa na dawa za kulevya, inashangaza sana mwendesha mashitaka wa Serikali kung'ang'ania kuwa ripoti ya mkemia mkuu wa Serikali imethibitisha wateja wangu walibeba dawa za kulevya jambo ambalo si kweli".

Mwendesha mashitaka wa Serikali akasimama tena. "Kama si dawa za kulevya... naomba uieleze mahakama, wewe unadhani watuhumiwa hawa waliingiza nini hapa nchini?. Mheshimiwa kama ishu ni kuagiza mizgo kwanini wasitumie cargo kusafirisha mizigo yao?".

"Mheshimiwa Hakimu, maelezo ya wateja wangu yako wazi kabisa, wameieleza mahakama yako tukufu kuwa mzigo wao ni maalum kwa ajili ya kutengeneza tembe za kutibu malaria. Tena wakasisitiza kuwa kama mzigo huo ni dawa za kulevya si wao, inawezekana wamefanyiwa njama za kibishara mambo haya yapo. Mheshimiwa, kinachoshangaza ni kwamba mzigo uliokamatwa umepelekwa kwa mkemia mkuu wa Serikali bila wateja wangu kuhusishwa hii haikubaliki. Inawezekana wakafanyiwa hujuma, ndivyo inavyoonekana. Mheshimiwa, mahakama ni chombo cha haki, kisitumike kuwaonea wateja wangu", mwanasheria wa utetezi alieleza.

"Mheshimiwa, kama nilivyoileza mahakama yako tukufu jana. Narudia, haiwezekani watu hawa wasafiri kutoka hapa nchini, waende nje ya nchi, watumie pesa nyingi kwa ajili ya kufuata malighafi za kutengeneza tembe za malaria. Mheshimiwa, mzigo uliokamatwa ni mali ya washitakiwa hawa. naamini hata wewe unasafiri nje ya nchi, lakini huwezi kuchukua mzigo usioujuwa, hawa ni wafanyabiashara wazoefu wa bishara chafu, wakiachiwa wanaweza kuligharimu taifa", aliketi baada ya kusisitiza.

"Mheshimiwa, inawezekana kabisa mwendesha mashitaka wa Serikali ana sababu zake binafsi kwa wateja wangu, jambo hili lisichukuliwe kijuujuu, taratibu ziko wazi mheshimiwa, tusitumike vibaya kwa sababu mkemia mkuu wa Serikali, mwendesha mashitaka wa Serikali ndiyo iwe njia ya kuwaumiza wateja wangu, haitawezekana mheshimiwa, kwanza walipaswa kuitwa ili washuhudie vipimo husika, lakini hili limefanyika bila wateja wangu kuhusishwa", mwanasheria wa utetezi alilalama kwa mara nyingine.

Hakimu aligonga meza, ukimya ukatawala kwa dakika kadhaa. "Hukumu. Nimesikiliza hoja za pande zote mbili kwa makini na kupitia maelezo ya pande zote kwa umakini mkubwa. Hivi niwaulize, inawezekanaje mtu ubebe mzigo usioujuwa kutoka huko nje, ukibadili ndege hii na hii hadi unaingia nchini, mzigo huo huo ukaubeba kwenye magari kuelekea nyumbani bila kujua umebeba nini?", Hakimu alihoji.

"Kama umefanyiwa njama au watu wanataka kuharibu biashara yako ama sifa yako, inawezekana kabisa mheshimiwa, wengi wamekutwa na kashfa za aina hii, naiomba mahakama yako tukufu iwatendee haki wateja wangu", mwanasheria wa utetezi alirudia kusihi.

Dakika kadhaa zilipita kukiwa kimya, hakimu akiichezea kalamu yake kwa meno, ..."Usinifundishe kazi. Naam, Mwendesha mashitaka wa Serikali ameieleza mahakama hii kuwa mnamo tarehe 15 mwezi huu, watuhumiwa wawili, Hawa Msimbazi na Tony Sime, mlikamatwa huko Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere, mkiwa na mzigo ambao ripoti ya mkemia mkuu wa Serikali imethibitisha kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroin. Jambo hili ni zito, bila shaka unajuwa kuwa dunia nzima imepiga marufuku matumizi ya dawa hizi, sijui hata mmewezaje kutoka huko nchi za mbali, mkavuka ukaguzi pale Uwanja wa ndege, hatmaye mkaingia nchini na kutiwa mbaroni na vijana waaminifu katika taifa hili", Hakimu alieleza huku wengine wakitazamana.

"Mmmh wamekwenda na maji hawa", kijana mmoja aliyekuwa mahakamani hapo alimnong'oneza mwenzake.

"Mwanasheria wa utetezi anasema inawezekana wateja wake walibeba mzigo wasioujuwa, lakini wamekiri kuwa walisafiri kwa ajili ya kuingiza malighafi za kutengeneza tembe za malaria, walipoulizwa na mwendesha mashitaka inawezekanaje watu watumie gharama kubwa kusafiri nje ya nchi ili kuingia mzigo wa gharama ndogo ambao haukidhi matumizi, hawakutoa jibu. Walipoulizwa tena kwanini wasitumie njia ya cargo kusafirisha mizigo yao hawakutoa majibu. Hii inaonyesha kabisa watuhumiwa hawa walikusudia kuingiza dawa za kulevya hapa nchini", Hakimu alieleza.

"Baada ya kusikiliza kesi hii na kupitia vingu mbalimbali vya sheria, nimethibitisha bila kutia shaka kuwa watuhumiwa hawa wana kesi ya kujibu. Kabla sijatoa hukumu, mnaweza kujitetea.

"Mheshimiwa Hakimu, tunaomba huruma yako, kwa upande wangu nina jukumu la kuwalea wazazi wangu ambao ni wazee sana, nina watoto wadogo wanahitaji msaada wangu mheshimiwa, wakinikosa wataathirika sana, naomba huruma unifikirie kwa hilo mheshimiwa, pia nasumbuliwa na tatizo la kifua", Hawa Msimbazi alijitetea.

"Tunaomba msaada wako mheshimiwa, kimsingi hili ni kosa la kwanza, tunaomba mahakama yako itupunguzie adhabu", Tony Sime alieleza huku hakimu akiandika maelezo yao kwa makini.

"Kuwa na wazazi wazee, watoto wanakutegemea haikupi tiketi ya kukufanya utende makosa, mbona wewe hukuwaonea huruma watoto wa wenzio, dawa za kulevya ni hatari kubwa. Naam ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye mawazo na tabia kama yenu, nawahukumu kwenda jela kila mmoja miaka kumi na mitano", wote wakaanguka chini wakati hakimu akitoka mahakamani.

ITAENDELEA 0784296253
 
Wakuu mkiamka asubuhi mtakuta mzigo hadi mwisho then tunaanza nyingine ya ukweli kinoma,,,,.... Huu mzigo leo leo mida ya wanga kwixh ney...!! Ntaawapa link humu humu ya mzigo mpya....!! Wale wa daku mida ya daku mtaukuta mzigo fullu....!!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom