Riwaya : Noti Bandia....!! Mwanzo-mwisho.

SHAMAC

JF-Expert Member
Feb 9, 2017
1,345
2,000
Kwa wale wapenzi wa riwaya karibuni sana. Nikiwa mdau wa mambo hizi nimeona nishee moja ya riwaya ambayo nimeikuta mahali lakini sijaitunga mimi jamani niwe mkweli. Nimeona si vibaya tuka share starehe na utamu kama huu na wanajukwaa...!! Ipo mwanzo mwisho, hapana kuishia kanisani, No arosto..!!


NI SINDANO TU HADI MLEGEE MMWAGE UDENDA.... HAKUNAGA AROSTO PANDE HIIMukuje na likes za kutosha etiii...!!!
 

SHAMAC

JF-Expert Member
Feb 9, 2017
1,345
2,000
JIJI la Dar es Salaam linatingishika, wezi sugu wanaingiza noti bandia, watu wanaibiwa. Baadhi wanauza majumba, magari na viwanja. Wafanyabiashara hatari wa dawa za kulevya nao wanacharuka, wanatangaza hali ya hatari kwa atakayeonesha kuwaingilia. Patashika linatokea, Dar es Salaam inakumbwa na misukosuko na mauaji ya kutisha.

"Kama unayathamini maisha yako jiweke pembeni". Amri inatolewa, "Vinginevyo yatakupata makubwa". Onyo linatolewa kila pembe ya jiji. Polisi wanagwaya, mauaji ya kutisha yanatokea, tishio linakuwa kubwa zaidi. Rais anapaza sauti, "Lazima hali hiyo ikomeshwe vinginevyo, hatuwezi kuvumilia...".

Mashujaa kadhaa wanajitokeza kuikabiri hali hiyo. Maiti zao ziokotwa kando ya bahari. Teacher anatua uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na kukabiliwa na mtihani mkubwa, gari lake linashambuliwa, anaponea chupuchupu. Lakini anaapa kuikabibiri hali hiyo ngumu. SASA ENDELEA.


SEHEMU YA KWANZA


Na Nyakasagani Masenza
NDEGE ndogo ya kukodi ya Kampuni ya ndege za Coastal ilishuka taratibu kwenye uwanja wa ndege wa mjini Musoma, baada ya kuwa angani kwa takribani dakika ishirini na tano hivi ikitoka katika Jiji la Mwanza. Mara baada ya ndege hii kutua kwenye uwanja huu, ulioko karibu kabisa na ukingo wa Ziwa Victoria, eneo maarufu la Makoko, nilikuwa miongoni mwa abiria watatu tuliosafiri kwa ndege hii kutoka Mwanza ambako tulibadilishiwa ndege.

Hii ilitokana na uwanja wa ndege wa Musoma kutokuwa na uwezo wa kupokea ndege kubwa kwa sasa. Baada ya ndege hii kutua, nilitwaa mfuko wangu mdogo uliosheheni vifaa vyangu muhimu vya safari, taratibu nikavuta hatua kutoka ndani ya ndege hii nikiwa tayari kuelekea nje.

Sikuwa na sababu ya kwenda haraka kutokana na hali ya ndege hii kuwa ndogo, hivyo nilisubiri wenzangu watoke kwanza ndipo nami niweze kutoka. Baada ya kukanyaga ardhi ya mji wa Musoma nilitembea taratibu, mkoba wangu begani, nilipita mapokezi na sehemu ya mapumziko ya wageni mashuhuri, nikaelekea kwenye maegesho ya magari ya kukodi nje ya uzio wa uwanja.

Hali ya hewa ya mji wa Musoma ilikuwa ya kuvutia sana, wingu zito lilitanda angani, kuashiria dalili ya mvua. Hali kama hii pia tuliikuta tuliposhuka kwenye uwanja wa Mwanza ambako tulikuta mvua ya kutosha. Kiasi fulani nilivutiwa na hali hii ya ubadiridi hususan kutokana na joto kali nililoliacha Jijini Dar es Salaam.

"Haraka, nipeleke Mkendo tafadhali", nilimwambia dereva teksi, baada tu ya kuingia na kuketi ndani ya gari yake iliyokuwa imeegeshwa karibu na sehemu niliyotoke.

"Sawa mzee", alisema dereva huyo huku akiwasha gari na kufunga mkanda, nami nikafanya hivyo. Wakati anaanza kuondoka aliuliza, "Mkendo ipi?", alihoji dereva huyo huku akiondoa gari taratibu kutoka kwenye maegesho ya uwanja wa ndege.

"Mkendo... Nadhani utaniacha baada ya njia panda ya mtaa wa Iringo", nilimwambia.

"Nadhani dakika tano", alisema huku akiingia kwenye barabara kuu ya Majita, akaongeza mwendo tukaelekea katikati ya mji. Baada ya kuzipita ofisi za Shirika la Umeme Tanzania Tanesco, nilivunja ukimya uliodumu kwa dakika kadhaa.

"Vipi hali ya samaki katika mji huu, wanapatikana?", nilimuuliza, taratibu akageuza shingo kunitazama, kiasi fulani alionekana kushangazwa na swali langu.

"Samaki!... alihoji kwa mshangao.

"Ndio... Mbona kama imekushituawa sana, wanapatikana?".

"Samaki bwana ni wengi sana. tatizo ni bei. Samaki kama Sato wanauzwa kwa bei mbaya sana, viwanda vimeleta shida, minofu ya samaki katika mji huu ni lulu, inasafirishwwa nje ya nchi, wakazi wa hapa tunaachiwa mifupa", alisema kwa utani huku akinitazama usoni akicheka.

"Mifupa ya samaki?", nilimuuliza. Niliwahi kusikia kuwa idadi kubwa ya samaki wanaovuliwa Ziwa Victoria wanapelekwa viwandani na kusafirishwa nje ya nchi, wenyeji wanaambulia mfupa mkubwa wa katikati na kichwa. Maelezo yake yalinifanya nihamasike kuuliza maswali mengine zaidi.

"Hiyo mifupa unayodai kuwa ndiyo inauzwa kwa wananchi, inafaa kuwa chakula?".

"Samahani kaka, wewe ni mgeni katika mji huu?", alihoji kijana huyu ambaye umri wake haukutofautiana sana na wangu.

"Mgeni mwenyeji, ni mzaliwa halisi wa mkoa huu, nimeishi sana mjini hapa, enzi zetu tulipokuwa wadogo samaki walikuwa wengi sana, sato, sangara, nembe ilikuwa usiseme, ukishuka Mwigonero samaki wa kumwaga, nasikia siku hizi hawapatikani ndiyo nashangaa", nilimwambia wakati anaingia kwenye mzunguko wa barabara za Nyerere na kuacha ile ya Sokoni.

"Umewahi kuona mabaki ya samaki yaliyoondolewa minofu ikabaki mifupa, hapa mkoani yanaitwa mapanki. Umewahi kuyaona?", aliniuliza.

"Hapana?".

"Basi labda nikudokeze, mapanki ni sehemu ya samaki waliotolewa minofu kwa ustadi mkubwa na kubaki kichwa na mfupa mkubwa wa katikati, mabaki ambayo huuzwa tema kwa watu wa kipato cha chini, hii inatokana na bei ya samaki kuwa juu sana. Ndiyo hali halisi ndugu yangu, samaki tunawasikia kwenye bomba tu huko viwandani", alifafanua kijana huyu.

"Aisee, sasa nimekupata. Kumbe ndivyo ilivyo...", nilinyamaza kidogo nikitafakari kisha nikamuuliza. "Kwanini serikali isiingilie kati, kuwasaidia wananchi wapate maisha bora, nina maana kuwa yatengwe maeneo ya wavuvi wa samaki kwa ajili ya wananchi wenye kipato cha chini, viwanda navyo vinunue kwa bei ya juu kidogo ili kuweka usawa".

"Nchi hii kaka, wananchi hawana maamuzi, tumewapa wenzetu dhamana wanaitumia kujinufaisha wao na matumbo yao, tatizo pia liko kwetu wabongo, tunajua kulalamika tu lakini hatuna maamzi ya kukataa jambo", alisema, baadaa ya kunyamaza kwa sekunde kadhaa, akageuka kunitazama. Labda hii serikali mpya italeta maisha bora".

"Labda, tusubiri tuone, maana watendaji ni walewale walioshindwa", nilimwambia akacheka.

Baada ya kupita kwenye mzunguko wa Barabara ya Nyerere, tukauacha mtaa wa Sokoni, tukaingia kwenye Barabara ya Nyerere, baada ya kituo cha mafuta cha GAPCO karibu na ilipokuwa karakana ya mabasi ya United. Sambamba na uwanja wa shule ya msingi Mkendo, tukaingia kushoto ulipo mtaa mdogo wa Rutiginga, moja mitaa yenye historia kubwa mjini Musoma. Inasemekana mtaa huu ndiyo wa kwanza kuwa na kinadada wanaouza miili yako. Baada ya kuuacha mtaa huu wa Rutiginga, moja kwa moja tukatokea barabara kuu ya Mkendo.

"Nimelazimika kupita njia hii kukwepa msongamano wa magari eneo la standi ya mabasi, muda huu kunakuwa na foleni kidogo", alisema wakati akisubiri kuingia mtaa wa Mkendo.

"Usijali, mitaa hii naifahamu vizuri pengine zaidi kuliko wewe, hata tungepita barabara ya Uhuru bado ilikuwa sawa tu", nilimwambia akatabasamu wakati akisimama mbele ya studio ya Issa Mkate, nilitoa kiasi cha pesa nikampatia akashukru na kuondoka.

Nilikuwa nimewasili mkoani hapa kwa likizo fupi ya upendeleo, niliyopewa na Mkuu wangu wa kazi, Kanali Benny Emilly, ambaye ndiye Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi. Lakini kabla ya kuondoka Dar es Salaam nilipanga ratiba fupi ya kuonana na watu kadhaa. akiwemo rafiki yangu kipenzi Luteni Kanali Charles Matumbi anayeishi mtaa huu wa Mkendo.

Kwa mjibu wa ratiba yangu mjini Musoma sikuwa tayari kuonana na mtu zaidi na Luteni Kanali Matumbi, nikihofia kuharibu ratiba yangu, kwani nilipanga pia kufika kijijini kwetu Nyamuswa, Wilayani Bunda ambako nilipanga kukutana na mama yangu mzazi niliyempenda sana. Baba yangu niliyempenda sana alikwisha tangulia mbele ya haki. Nimekuwa nikijiuliza maswali maswali mengi kwa nini Baba yetu tuliyempenda alikataa kula chakula hata akadhoofu na kupoteza maisha. Hii ni siri ya Mungu aliyetuumba na kutufanya tuishi kwa muda katika ulimwengu.

Likizo hii fupi ilitolewa na Mkuu wangu wa kazi Kanali Emilly kwa upendeleo, baada ya ofisi yake kupokea hati ya utambulisho wa kimataifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutambua mchango wa utendaji kazi wangu nikiwa mlinzi wa amani wa umoja huo. Baada ya kushiriki kazi za ulinzi wa amani katika mipaka mbalimbali ya ndani na nje ya Tanzania. Kazi niliyofanya kwa uaminifu mkubwa, nikiwa mkuu wa operesheni za kijeshi kwenye baadhi ya mipaka.

Kwa takriban miaka miwili nilihudhuria kozi na masomo mbalimbali ndani na nje ya nchi yetu na kutunukiwa vyeti na shahada mbalimbali, katika ngazi za Ukamanda, Utawala na Ukufunzi katika Shule na Vyuo vya Kijeshi vya ndani na nje ya nchi. Uangalizi wa Amani katika kituo cha SADC Regional Peacekeeping Training Centre, kilichopo Harare Zimbabwe, ambako nilirudi kufundisha kozi fupi za ‘UNITED NATIONAL MILITARY OBSERVARS’ na ‘UNITED NATIONAL STAFF OFFICES’ kwa nyakati tofauti.

Nikiwa nimeshiriki kazi za uangalizi wa amani katika mpaka kati ya Ethiopia na Eritrea, kwa miezi saba nilifanya kazi hiyo nikipewa dhamana ya mkuu wa operesheni, nikishirikiana na baadhi ya maofisa kutoka katika nchi za Marekani, Norway, Poland, Romania, Kenya, Zambia, Nigeria, India, China na Ukraine. Waliofanya kazi chini yangu kwa nyakati tofauti.

Kutokana na utendaji wangu kama mlinzi wa amani ‘Observer’ wa UN kwenye mpaka wa Ethiopia na Eritrea, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alinitunuku Medali ya amani, ambayo ilimfanya Kanali Emilly afurahishwe sana. Kutokana na utashi wake ameweza kuiongoza Idara hii nyeti kwa ufanisi mkubwa, kutokana na umri wake kufikia wakati wa kustaafu, serikali iliona kuwa bado anaweza kuhimili mikikimikiki ya kazi aliyoizoea wakamuongezea mkataba wa miaka miwili.

Kutokana na uwezo na msimamo wake huo Kanali Emiily amekuwa akishiriki katika kazi za hatari, ambazo zimemjengea heshima. wakati serikali inaangalia nani atakuwa mrithi wa Kanali Emilly, ilimuongezea mkataba wa miaka hiyo miwili, kitendo ambacho kiliungwa mkono na kila mpenda amani duniani.

Baada ya kumaliza kazi na kupewa medali hiyo kama ilivyo kwa wahitimu wengine kutoka mataifa mbali mbali duniani, nilirejea Dar es Salaam nikiwa na matumaini ya kupata hati ya heshima ambayo ni zawadi kwa jeshi na serikali ya Tanzania.

Kama kawaida hati hiyo ilitumwa kwa Jeshi la Tanzania na kupokelewa na Kanali Emilly, ikinielezea kuwa, nimehitimu vizuri na kupata alama B, alama ambayo ni ya juu kutolewa na Chuo hicho, kilichoko kaskazini mwa Jiji la Moscow, nchini Urusi.

Kanali Emilly alifurahishwa sana mimi kupata alama hiyo ya juu, aliniita ofisini kwake na kunikebehi kwa maneno ya utani kiasi kwamba nami niliamini kuwa ndoto zangu zilikuwa ndoto za Kimweri.

Kanali Emilly alitania, "Yawezekana mambo yalikuwa mazito Teacher, sikutarajia, kijana shupavu kama wewe kuchemka, pole sana mwanangu", alisema Kanali Emilly mimi nikimwangalia usoni kwa makini.

"Yawezekana mambo yalikuwa magumu, sikutarajia kupata matokeo ya kushangaza kama unavyosema, nilijipanga vizuri, kama imetokea hivyo sina jinsi", nakumbuka jinsi nilivyomwambia Kanali Emilly akacheka.

"Umejisikiaje kufanya vibaya, Teacher?", alihoji tena.

"Nimejisikia vibaya sana, sidhani kama yupo anayependa kufanya vibaya", nilimwambia.

"Taarifa yako itatoka ubaoni mchana leo, ni taarifa mbaya sana, sina njia nyingine lazima itoke kama ilivyo kawaida", aliniambia huku akionesha tabasamu, lililonishangaza.

"Naomba isiwekwe kwenye ubao", nilijaribu kumshawishi akakataa.

"Hapana, unataka niharibu kazi ili nikufurahishe wewe, sikukutuma kufanya madudu", Kanali Emilly alisema kwa hasira sura yake ilibadilika, nilitoka ndani ya ofisi yake nikitafakari aibu itakayonipata baada ya taarifa hiyo kutolewa.

Nilijiuliza nini nimefanya wakati wa kozi sikupata jibu, nilitembea huku moyo wangu ukisononeka, nikaelekea Kantini, ambako nilikunywa chai na chapati moja tena kwa shida, kisha nikaelekea ofisini kwangu.

Tofauti na jinsi nilivyotarajia, kidogo nipoteze maisha kwa furaha, ubao wa matangazo ulisomeka kuwa nilifaulu vizuri na kupata alama B, alama ambayo ukiipata katika chuo hicho, unatunukiwa cheti cha heshima na Rais wa nchi yako kwa niaba ya Mkuu wa Chuo.

Nilimtafakari Kanali Emilly sikupata jibu, niliporejea mazungumzo yetu ya awali kuwa nimemfedhehesha, nikabaini kuwa Mzee huyu alikuwa akinitania kama ilivyokuwa kawaida yake.

Sikupoteza muda, nilimpigia simu kumfahamisha nilivyofaulu kwa kupata alama B, ambayo tuliipata maofisa wawili, mimi kutoka Tanzania na Meja Charles Katasi wa Jeshi la Uganda.

Kanali Emilly aliniita ofisini kwake na kunifahamisha kuwa, yaliyotokea ni sababu ya furaha aliyokuwa nayo baada ya kupokea hati hiyo. "Unatakiwa Ikulu saa nne ya asubuhi kesho, faili lako limepelekwa kwa Rais, atakubabidhi hati hiyo yeye mwenyewe, maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi watakuwepo, inafurahisha sana Teacher", Kanali Benny alisema huku nikijisikia mwenye furaha ya ajabu kuonana na Rais kesho.

Nilivaa vizuri, nikajipanga pamoja na familia yangu, baada ya kujiweka sawa tulielekea Ikulu, Kanali Emilly na viongozi wengine wa ngazi za juu wa Jeshi walifika kushuhudia tukio hili la aina yake.

Baada ya Rais kunikabidhi hati yangu ya heshima alisema maneno machache, akitoa maagizo kwa maofisa na makamanda wangu kuhakikisha wanathamini mchango wangu na kuongeza vijana na kuwahamasisha kufuata nyayo zangu.

Kutokana na heshima hiyo, nilipewa nafasi ya kutoa neno la shukrani, baada ya kusema niliitwa kupiga picha za kumbukumbu na Rais, maofisa wa Jeshi, familia yangu, wakiwepo watoto wangu wapendwa, Masey, Changasi na Warioba ambaye alibebwa na Rais.

"Karibu Teacher", mawazo yangu yaliingiliwa na sauti nzito ya Luteni Kanali Matumbi.

"Asante Kamanda", niliitika huku tukashikana mikono, tukakumbatiana kwa furaha.

"Ni Afande Matumbi?", nilimuuliza kwa utani na bashasha.

"Hakika ni mimi, wewe ni Teacher?", yeye pia aliuliza.

"Mwili huu unakula nini Kamanda?", nilimtania.

"Samaki na viazi", alijibu kwa utani.

Luteni Kanali Matumbi alinipokea mkoba wangu, kisha mkono wake wa kushoto akaushika mkono wangu wa kuume, tukatembea kuelekea ndani.

"Umenikumbusha mambo ya zamani Teacher, bahati mbaya sana historia hazijirudii, ingekuwa hivyo tungefanya maandalizi ya kutosha kuzirudia historia", alisema tukacheka.

"Kweli kabisa, unakumbuka opereseni ya kula chakula cha wanafunzi wenzetu kule chuoni Nachingwea", nilimkumbusha.

"Operesheni ipi hiyo Teacher, maana tumefanya mambo mengi?", aliuliza wakati tunaingia kwenye sebule ya nyumba yake.

"Wakati wa mafunzo ya awali kule Fam seven teen Nachingwea, tulianzisha operesheni ya kula chakula cha wenzetu, unamkumbuka yule Bahati kutoka Kigoma?", nilimuuliza.

"Bahati..., Bahatiiii, mbona simkumbuki, alitoka Kigoma?", aliuliza.

"Unamkumbuka bwana, alikuwa kijana mchafu sana, alipenda kuiba mchele stoo wakati wa fatiki na kujipikia vichochoroni", nilimkubusha.

"Bahati... namfahamu sana, alikuwa Kombania C, una kumbukumbu sana Teacher, njaa bwana ni baraa, sikujuwa operesheni ile iliendeshwa na nani?", alisema akitabasamu.

"Niliifanya mimi", nilimwambia tukacheka tena. "Maana Bahati alivunja rekodi kwa kukimbia na kofia ya chuma la moto lililokuwa na ubwabwa.

"Ni kweli alitoka Kigoma".

"Huwezi kuamini, tulijiandaa kama kawaida yetu, baada ya kuwazingira na kuwaachia upenyo ili aweze kukimbia, huku tukiwa tumefunga makaratasi meupe miguuno na upande wa kulia wa mkono mfano wa Military Polisi, tulimkurupusha bwana...", nilisema huku Meja Matumbi akishika tumbo kwa kucheka. "Lakini ilikuwa kama abiria chunga mzigo wako, akakimbia na mzigo, tukaambulia patupu".

"Eheee, alikuwa makini sana katika masuala ya misiso".

"Siwezi kumsahau, tulipomkurupusha tu, kitendo cha haraka, tena bila kuchelewa, alibeba kofia ya chuma, tena likiwa la moto..., aisee alimudu kukimbia nalo", nilimwambia huku tukicheka sana.

Baada ya kucheka sana, huku tukikumbushana mambo yaliyotokea wakati tukiwa chuoni, chakula na vinywaji vililetwa tukaanza kula huku tukiulizana hili na lile.

"Teacher", Luteni Kanali Matumbi aliniita.

"Ndio Kamanda".

"Kulikuwa na uvumi kuwa Rais wa Sudani Omari al Bashir anatafutwa ili akamatwe na kufikishwa kwenye Mahakama ya kimatafa ya uhalifu wa kivita, kujibu tuhuma za mauaji, uvumi huo uliishia wapi, naamini wewe kiasi fulani unafahamu kinachoendelea".

Nilivuta pumuzi nikazishusha, nilitafakari kuhusu swali la Meja Matumbi, nikaamini kuwa hata yeye mizozo na migogoro katika nchi za kiafrika inamsumbua sana akilini.

"Ni kweli, mwaka jana mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC, ilitoa hati ya kukamatwa kwa kiongozi huyo wa Sudani, niliwahi kumwambia hata Kanali Emilly kuwa ni vigumu mno kwa kiongozi wa nchi kama Bashir kukamatwa na kufikishwa kwenye mahakama hiyo wakati bado anaongoza nchi, ni vigumu sana".

"Hakika ni vigumu Teacher, lakiniiii..., wakidhamiria kabisa kabisa wanaweza kufanikiwa".

"Wampate wapi, ni vigumu sana Bashir kukamatwa", nilisisitiza.

"Kuna ugumu gani, kwani huyu Bashir hafanyi ziara nje ya Sudani... Wanamvizia akitoka tu, wanamtiwa mikononi, sidhani kama inashindikana", alishauri Luteni Kanali Matumbi.

"Wewe unaona rahisi, nikwambie sasa, huyu Mzee pamoja na kuwepo hati ya mahakama ya uhalifu wa kivita, amefanya safari zaidi ya kumi nje ya nchi yake, tena bila woga, ni vigumu mno", nilimwambia akabaki amekodoa macho.

Nilichukuwa glasi ya maji nikanywa kidogo, nilimwangalia kama ana la kusema, nilipoona ananiangalia bila kusema kitu nikatambua kuwa jambo hili limemgusa mno, maana ni mmoja wa maofisa wapenda amani wenye msimamo usioyumbishwa.

"Mbona umenyamaza Mkuu, kama vile umegushwa mno na jambo hili".

"Teacher, kama ungeweza kujua moyo wangu ulivyo, hakika ungeelewa nini natafakari, viongozi wa aina ya Bashir ndiyo wanaochangia machafuko barani Afrika, mtu mmoja anasababisha mauaji ya mamilioni ya watu, haipendezi Teacher", alisema kwa uchungu.

"Ni kweli, lakini utafanyaje, migogoro imekuwa migogoro, watu wanauana kama wanyama, hii yote inatokana na udhaifu wetu, angalia mfano mtu kama Jonas Savimbi, aliumiza watu wengi nchini Angola, amewaachia watu vilema vya maisha, ICC haikuwa na ubavu, iliishia kusema na kulaani tu, mpaka alipouawa. Kwanini walishindwa kumtia mikononi?", nilimwambia.

"Wewe unadhani nini kifanyike kukomesha mauaji ya waafrika, maana kwa takwimu za haraka nchi zaidi ya 30 zinakabiliwa na migogoro mikubwa, inayotishia amani ya dunia, na kati ya nchi hizo zaidi ya ishirini ziko barani Afrika", alihoji.

"Cha kufanya ni kumuomba Mungu, kwa sababu kila siku mataifa makubwa yanatengeneza silaha, na silaha hizi hazitengenezwi kwa ajili ya wanyama, zinatengenezwa kwa ajili yetu, ili uweze kuwa na nguvu kijeshi, lazima uwe na silaha za kisasa, kila taifa linatamba dhidi ya taifa lingine, unadhani amani itapatikana?", nilimuuliza akakuna kichwa.

"Azimio la Umoja wa mataifa la kupiga marufuku mapinduzi ya kijeshi duniani linatekelezwa kweli?", alihoji.

"Hata kama linatekelezwa, mbona halina meno, toka azimio hilo lipitishwe na Umoja wa Mataifa ni nchi ngapi zimepinduliwa na kuongozwa kijeshi, tumeshuhudia baadhi ya nchi Umoja wa Mataifa ukiingilia kati, na sehemu zingine wakisita kufanya hivyo eti ni kuingilia mambo yao ya ndani".

"Kweli Teacher, ni nyingi", Luteni Kanali Matumbi alisema kwa sauti ya upole.

"Aisee, tutafute siku nyingine tutaongea zaidi, muda wangu wa kuwepo hapa Musoma umekwisha, labda tuonane Jumamosi wakati narudi Dar es Salaam, nitajitahidi kuwahi ili tuongee zaidi", nilimuomba Luteni Kanali Matumbi baada ya kuona muda unayoyoma.

"Nilitegemea utalala Musoma, nimekufanyia maandalizi ya kila aina, hebu lala Musoma leo nikutembeze kidogo uone mji", alishauri nikatingisha kichwa kutokubaliana naye.

"Usijali, lazima niondoke leo, nina shauku kubwa ya kumuona mama yangu mzazi, wajuwa tena Afande, baba na mama ni mungu wa dunia, pamoja na kwamba baba alikwisha tangulia mbele ya haki, tafadhali tuonane siku nyingine", nilisema nikisimama kutoka sehemu niliyoketi, maana nilikuwa nimekula na kunywa vizuri.

"Ok, sina jinsi Teacher, nilitegemea kuvuna uhondo zaidi kutoka kwako, basi bwana, ngoja nikutowe", akabeba mkoba wangu tukaelekea nje.

"Usisahau kupita hapa hiyo Jumamosi, nitafanya maandalizi ili usafiri Jumapili", aliongeza, huku nikitingisha kichwa kukubaliana na mawazo yake, japokuwa haitawezekana kurudi hapa kutokana na ratiba yangu niliyojiwekea. Baada ya kuagana na Luteni Kanali Matumbi nilitafuta usafiri wangu binafsi nikaelekea Nyamuswa.

ITAENDELEA 0754296253.
 

SHAMAC

JF-Expert Member
Feb 9, 2017
1,345
2,000
SEHEMU YA PILI

Na Nyakasagani Masenza

Jijini Dar es Salaam, kilifanyika kikao cha siri katika nyumba moja ya mfanyabiashara maarufu wa dawa za kulevya. Mfanyabiashara huyu alifahamika kila pembe la Jiji, akiitwa Mzungu Carlos Dimera, Umbo lake lilitosha kabisa kuogopwa na wapinzani wake. Asili ya mzungu huyu ilikuwa ni Corombia. Kutokana na uwezo wake wa kushawishi, Carlos aliweka matawi kadhaa katika nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Ndiye aliyeitisha kikao hiki kwa siri kubwa.

Kutokana na uwezo wake wa fedha na ushawishi aliokuwa nao kwa baadhi ya viongozi wa serikali kadhaa za Afrika, Carlos Dimera aliweza kuanzisha vikosi kadhaa vya uhalifu ndani ya nchi kadhaa, mojawapo ya vikosi hivyo ni usafirishaji wa shehena kubwa ya dawa za kulevya, kikosi cha wizi kutumia noti bandia na kikosi maalumu cha mauaji dhidi ya watu aliowaita vihelehele. Vihelehele ni wale walioonekana kuingia mambo yake.

Kikao hiki ambacho yeye Carlso Dimera aliwa Mwenyekiti wake, kiliwakutanisha watu wachache, akiwemo mwanamke mmoja tu, Mwana mama huyu aliitwa Hawa Msimbazi, ambaye kutokana na uwezo wake wa kupanga mambo yakawa, wenzake walimfananisha na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani, Condoliza Rice. Hawa alifananishwa kwa mambo mengi na Mmarekani huyo mwenye asili ya Afrika. Tofauti yao ni kwamba yule alikuwa mtendaji katika Serikali ya Marekani, huyu alikuwa mfanyabiashara wa dawa haramu za kulevya Tanzania.

"Mambo yote yamekamilika kwa asilimia tisini na tisa, vijana wamejipanga vizuri kufanikisha kazi hii, kama itakwenda salama kama tulivyojipanga, nawahakikishia kila mmoja atachagua nchi gani atapenda kuishi pamoja na familia yake", alisema Hamis Nombo, mmoja wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya ambaye kiutendaji ni mtaalam wa mipango katika kikosi.

"Sijui hata niahidi nini, jambo hili si gumu kama mnavyodhania, mambo yote yamefanyika, kama alivyosema Nombo hii ni nafasi yenu kuamua wapi mtapenda kuishi, baada ya kazi hii kumalizika kila mmoja ataihama nchi hii akatumbue raha huko atakapopenda kwenda", alirudia Dimera.

"Bosi, hakuna sababu ya kuumiza vichwa, vijana wamejipanga vizuri, bahati nzuri ni kwamba muda mfupi uliopita wana spoti wetu wametuletea taarifa kuwa serikali imewatuma vijana wawili kutoka Jeshi la ulinzi kuangalia mambo fulani fulani, watoa taarifa wetu wanasema, vijana hao wametumwa kwa siri, baada ya kuona polisi wanasuasua", alisema Hawa.

"Safi sana, aliyekuita Condoliza Rice hakukosea, kazi unazofanya ni kielelezo kuwa jambo hili litafanikiwa, cha msingi sasa, watume vujana wako waonane na askari hao, ili wapewe ahadi zao kabisa, lakini pia wasiwaendee mikono mitupu, nadhani pia waingizwe kwenye orodha ya malipo yetu na wafahamishwe", alishauri Carlos Dimera.

"Jambo hilo limefanyika hata kabla sijasema katika kikao hiki. Mambo ameleta taarifa. Amesema askari hao ni miongoni mwa Makomandoo mahili sana, wana uwezo mkubwa mno, tayari tumeingia nao mkataba. Wako upande wetu sasa", alisema Hawa Carlos akitabasamu.

"Ni jambo zuri sana Hawa, lazima muelewe kuwa kufanya ishu na watu hatari kama hao lazima tuwe tumejiandaa vizuri pia, tuwe makini nao isije ikawa tunamalizana nao halafu wanaanza kutusumbua", anashauri Nombo.

"Kweli, lakini niwaambie jambo moja, hebu tumalize kazi kwanza, mengineyo yatakuja baadaye", Dimera alishauri.

Baada ya ukimya wa sekunde kadhaa, kila mmoja akitafakari hili na lile, Carlos aligonga meza, akatoa angalizo, "Cha msingi tuwe makini na kila hatua tunayopita na kutoka, ahadi yangu kwenu ni malipo mazuri mara dufu, jiandaeni kuishi vizuri.

"Lakini pia tusimsahau Teacher, maana waswahili wanasema usipoziba ufa utajenga ukuta", alikumbusha Aloyce Jackina, aliyekuwa kimya kwa muda mrefu.

"Hana chochote huyu Teacher, jambo hili likiisha tukafanikiwa kuvuka vikwazo, Teacher atakuwa na nafasi gani?", alihoji Dimera.

"Ni tahadhali tu natoa bosi", aliongeza Jackina.

"Umefanya vizuri, ili tuongeze nguvu na umakini", alisema Hawa.

"Kwa maana hiyo tunaachana baada ya kikao hiki, nawatakia mafanikio mema, tufahamishane kila hatua tutakayokuwa, cha msingi ni kutunza midomo yetu. Tukionana kila mmoja awe na jibu la nchi gani atakwenda kuweka makazi yake ya kudumu" alisema akisimama.

Baada ya kikao hicho, Carlos Dimera alikuwa na kikosi kingine chumba cha pili, watu wawili nadhifu sana walikuwa wakimsubiri. Watu hawa walikuwa wamemaliza kazi waliyotumwa na sasa walikuja kupata maelezo ya kazi nyingine.

"Nimesikia kilio mitaani, watu wanalia, tamaa zao zimewafanya walie, kazi yenu ni nzuri sana, nimefarijika, rafiki yangu mmoja kutoka polisi kituo cha kati amenidokeza kuwa kesi zilizofunguliwa hapo ni waliobiwa kwa mpango wetu, wakati hao bado wanalia na kusaga meno wapo wengine wenye tamaa ya kupata utajiri wa haraka. Wewe Oliver Mapunda hakikisha unaingia Chuo Kikuu Mlimani. Maprofesa pamoja na elimu yao katika dunia, ni wepesi kuingia katika kipindi, wakiingia usifanye makosa", aliagiza Carlos Dimera.

"Naam, nimekusoma bosi", anadakia Oliver Mapunda aliyekuwa kimya akiwa amefunga mikono yake kifuani.

"Kuna wastaafu waliolipwa mapesa yao baada ya kustaafu, wakati bado wanatafakari nini wazifanyie pesa hizo, sisi tunazitaka. Wewe Masta Bolendile, kazi yako ni hiyo, lakini usiishie hapo, tafuta mahusiano ya karibu na watendaji wa mashirika ya umma, hawa wana mapesa mengi, lakini ni wagumu kuzitoa, tukijipanga vizuri tutazichukua".

"Naam bosi", anasema Bolendile.

"Dakika chache zilizopita nimetoka kuzungumza na wenzenu upande wa pili, nimesema baada ya kazi ngumu na nzito iliyo mbele yao, kila mmoja apendekeze nchi gani atapenda kuweka makazi yake ya kudumu, kazi yao ni nzito, kazi ya hatari zaidi ya hii yenu".

"Kazi zote zina hatari bosi", Bolendile aliingilia mazungumzo.

"Sawa, lakini hii kazi yenu tunatumia sayansi na teknolojia zaidi, hata ukikamatwa na polisi haina uzito sana. Lakini 'nga', umekutwa na unga, lazima yatoke mawe ya uhakika. Naamini kila mmoja amepata mgawo wake sawa. Mtaniletea taarifa za kazi hii baadae. Kila mbinu itumike Teacher auawe, iwe kwa risasi, kisu au hata akitumiwa msichana ammalize kwa sumu, Kwaherini". Akafunga kikao na kuondoka.

ITAENDELEA 0754296253
 

SHAMAC

JF-Expert Member
Feb 9, 2017
1,345
2,000
SEHEMU YA TATU


Nyamuswa kama ilivyo kwa miji mingine midogo, iliyoko Bunda, mkoani Mara, ulikuwa umechangamka kwa kiasi, wananchi kutoka sehemu mbalimbali zinazouzunguja mji huu walipishana huku na huku wakifanya mahitaji. Ilikuwa Jumapili ya mwisho wa mwezi. Siku ambayo kila inapowadia wenyewe huiita SIKU YA MTERA NYAMUSWA.

Nilikuwa nimewasili kijijini hapa dakika chache zilizopita, lakini barabara iendayo nyumbani kwa wazazi wangu ilikuwa imefungwa na wafanyabiashara waliokuwa wakiuza bidhaa mbalimbali. Kama ilivyo kawaida yangu, niliutwaa mkoba wangu nikaunjika begani, kisha nikamruhusu dereva aliyenileta aondoke, kwani hakukuwa na njia ya kupita.

Haikupita sekunde mkoba wangu ulipokelewa na Taabu dadangu kipenzi, sikumuona jinsi alivyotokea, alionekana mwenye furaha kupita kiasi, labda alifutahi kuniona tena baada ya kuwa mbali nae kwa muda.

"Pole na safari", alisema Taabu.

"Mungu amesaidia, habari ya nyumbani?" nilimuuliza wakati tunapita kwenye kundi la watu kuelekea nyumbani.

"Mama pia nilimuona". alisema akaangaza macho kumtafuta.

"Mwache, mwache asafishe macho. Atanikuta nyumbani". nilisema huku tukitembea na baadhi ya watu wakitusindikiza kwa macho.

Dakika kadhaa mama naye alifika, hakufanya ajizi moja kwa moja alikuja na kunikumbatia. "Pole na safari mwanangu", Akaanza kulia, "Ulizoea kutukuta na baba yako, sasa hayupo tena", alisema mama huku machozi yakianza kumtoka. "Ametuachia ukiwa", alilala.

Machozi ya mama yalinifanya niwe kimya kwa sekunde kadhaa nikitafakari hili na lile, "Nyamaza mama, kilichotokea ni kazi ya Mungu, baba yatu ametutangulia tu, siku moja tutamuona. Siku zote baba alikuwa akisema hatapenda tumtangulie sisi, alitaka atangulie yeye, kwa kuwa siku yake ilifika, mapenzi ya Mungu yalitimizwa, alihitajika kutoka miongoni mwetu", nilisema huku nikimuacha mama na kuliendea kaburi la baba kwa ajili yakufanya maombi mafupi.

Baada ya kumuombea mama, tulianza kuzungumza habari nyingine, mama alitaka kujua habari ya safari zangu nje ya nchi, nilimweleza kifupi kuhusu mafanikio ya safari hizo kwa nchi yetu na jinsi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alivyonizawadia tuzo maalum nilipokuwa katika kazi ya ulinzi wa amani. Alionyesha kufurahishwa sana na maelezo yangu, japokuwa hakujua nini heshima ya tuzo hiyo.

Kwa vile nilikuwa nimetoa taarifa mapema niko njiani, mama na dada waliniandalia chakula nikipendacho, ugali na samaki aina ya ningu na nembe. Nimetokea kupenda aina hii ya samaki, ambao hupatikana sana Ziwa Victoria.

Ilipofika saa tisa mchana, nilipita mitaa kadhaa nikiangalia mji, nilivutiwa na maendeleo yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya vijana. Watu walikuwa wengi, na sehemu za starehe kama baa na hoteli zilikuwa zimejaa watu huku wengine wakicheza pool, karata na bao la solo. Nililazimika kumtembelea shemeji yangu mpendwa Mama Feka, ambaye kwa muda mrefu alikuwa na shauku ya kuniona.

"Ah, karibu sana molamu", alisema Mama Feka akinikumbatia.

"Nafasi ya upendeleo molamu, nina muda mchache sana wa kuwa hapa Nyamuswa, nimehofia jambo moja, nimeogopa usijesikia nilikuwepo na sikukutafuta, sidhani kama ungenielewa?", nilimuuliza.

"Nisingekuelewa kabisa, habari ya Dar... Nadhani umeingia leo".

"Yes, nimeingia leo na ratiba yangu imebana mno, lakini nitajitahidi kuwepo hapa kwa siku mbili tatu hivi", nilimwambia.

"Naamini utakuwa umekula, twende maduka saba nikupe japo bia mbili molamu", alisema. Kabla sijasema kitu haraka aliingia ndani. Hakuchukua hata dakika moja akatoka ameshika kitenge mkononi. "Haya togende molamu", akatangulia, nikamfuata, tukaelekea hapo maduka saba.

Sehemu hii ilikuwa imechangamka kiasi, vijana ninaowafahamu na nisiowafahamu walikuwa hapa wakiangusha moja moto moja baridi, nilipungiana mikono na vijana hao waliokuwa wakibisha kuhusu mchezo wa mpira, Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kati ya Yanga na Simba. Mmoja wa vijana hawa alionekana mwenye jazba sana. "Mwamuzi alichangia kuharibu radha ya mchezo, huwezi kutoa kadi nyekundu dakika za mwanzo kama vile", alisema kijana huyo kwa ghadhabu.

"Ulitaka aachwe aendelee kufanya makosa uwanjani?", alihoji kijana mwingine ambaye pia alisimama kuonyesha msisitizo.

"Molamu, huwezi kuamini baada ya mchezo wa Yanga na Simba, ngumi zilipigwa hapa, wengine wakilalamikia kadi nyekundu iliyotolewa na mwamuzi, wengine walidai eti mwamuzi alikuwa sahihi kutoa kadi hiyo, yaani ni vurugu tupu", alisema Mama Feka nikimwangalia kwa makini.

"Molamu, wewe ni shabiki wa timu gani?", nilimuuliza.

"Aaah molamu... Mabingwa watetezi Yanga Afrika, nikuletee kadi yangu ya uanachama, usije kusema mimi ni shabiki kishoka".

"Umesema, nimekuelewa molamu", nikasimamam kuelekea mahali vijana hao walikuwa wakibishana bila mpangilio.

"Mimi nilijua kabisa kuwa mwanamke hawezi kuchezesha mchezo kama ule", alirukia kijana mwingine.

"Sikilizeni", niliwahadhalisha.

"Tumsikilize mzee, naamini alikuwa uwanjani, sisi tunabishana kwa kuona mchezo katika luninga", alisema Adul Light, mmoja wa vijana hao.

"Kwani luninga ina tofauti gani na kuwa uwanjani, si kila kitu kinaonyeshwa laivu", alidakia kijana mwingine.

"Ndio maana nikaomba mnisikilize... Lazima mtambue kuwa mchezo wa soka unaendeshwa kwa kanuni na sheria za mchezo, mnaweza kumlaumu mwamuzi wa mchezo huo kuwa alimtoa mchezaji wa Simba kwa kadi nyekundu, lakini ukweli ni kwamba mwamuzi hakutoa kadi nyekundu..."

"Unaona sasa. Inaonekana hukufika hata uwanjani, maana hujui kama mwamuzi alitoa kadi nyekundu, eti jamani mwamuzi hakutoa kadi nyekundu?" alihoji kijana huyo akionyesha kuwa na jazba.

"Ungenisikiliza kwanza", nilimsihi kijana huyo." akakubaliana nami. Haraka nikamuomba mtoa huduma awapatie vinywaji. "Kama nilivyotangulia kusema, mchezo wa soka unaendeshwa kwa kanuni na taratibu. Dakika chache baada ya mchezo huo kuanza, mwamuzi alitoa kadi ya njano, kimsingi mchezaji alipaswa kujihami, asifanye makosa. Lakini kabla hata dakika kumi hazijapita akafanya kosa lililostahili kadi ya njano, akapewa yelow card ya pili. Kanuni za soka zinasema, mchezaji akizawadiwa kadi mbili za njano, atapewa kadi nyekundu ili aende nje. Ndiyo maana nikasema hakupewa kadi nyekundu, ila kadi mbili za njano zilimfanya mwamuzi kutoa kadi nyekundu. Si matakwa yake, ni kanuni za mchezo", nilifafanua.

Vinywaji vikaletwa tukaanza kunywa,

"Hali hii iliwahi kuwakuta hata Yanga, wachezaji wake wawili walitolewa uwanjani kwa nyekundu, na hii si kwa Yanga na Simba tu, tumeshudia hata ligi za Ulaya", anabaisha Abdul.

"Yes, kadi nyekundu ni sehemu ya mchezo, ndiyo maana mwamuzi anakuwa nazo mfukoni. Lakini pia yafaa mfahamu kuwa mwamuzi anapowajibika pale uwanjani, kuna mamlaka zingine juu yake, kama atakuwa amekwenda kinyume na kanuni anaadhibiwa", niliwadokeza, wakaonekana kunielewa.

Mara ujumbe mfupi ukaingia kwenye simu yangu, Ujumbe ulisema. "UMEZUKA MOTO NA KUUNGUZA JENGO LA OFISI ZETU ZILIZOKO MTAA WA AZIKIWE, VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA HUSUSAN KIKOSI CHA ZIMA MOTO NA UOKOAJI KINAENDELEA NA KAZI YA KUZIMA MOTO HUO, UNATAKIWA KUREJEA HARAKA KWA AJILI YA TAtHIMINI", Col. Ben. Kwanza nilicheka, mapigo ya moyo wangu yakaongezeka.

"Molamu, nimepata ujumbe wa kushtua kidogo, natakiwa kurejea haraka Dar, es Salaam, hivi tunavyozungumza, moto umezuka ghafla unateketeza jengo la ofisi zetu mtaa wa Azikiwe, kwa hiyo nalazimika kuondoka sasa hivi", nilisema wote wakaonekana kushangazwa.

Aaah molamu, sina bahati na wewe, jitahidi kuvumilia uondoke kesho mapema".

"Muda huu utapata usafiri gani kaka?" alihoji Abdul Light.

"Kama nitaweza kufika Mwanza mapema, saa tatu usiku kuna ndege, bahati nzuri rubani wa ndege hii ni mtu wangu wa karibu, nitamjurisha aniwekee nafasi, nilipenda kuwa nanyi, lakini hali ndiyo kama mlivyoona", nikasimama na kuwaaga kwa mara nyingine nikaondoka.

ITAENDELEA 0784296253
 

SHAMAC

JF-Expert Member
Feb 9, 2017
1,345
2,000
SEHEMU YA NNE
http://mpiganaji/
Ilikuwa saa mbili na dakika arobaini hivi usiku, nilipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Jijini Mwanza, niliwahi kufika uwanjani hapa kama ambavyo inatakiwa abiria wasichelewe kufika kwa ajili ya ukaguzi. Baadhi ya abiria walikuwa wakilalamikia kuachwa na ndege ya saa tisa kwa sababu tu walichelewa kufika uwanjani hapo kwa wakati.

"Nitawashitaki mahakamani, haiwezekani nilipe nauli mara mbili, huu ni wizi", alisema kijana mmoja aliyekuwa karibu yangu, "Tena niliwa
hi nusu saa kabla, lakini wakanigomea", alisisitiza kijana huyo.

"Hata mimi nimewahi nusu saa kabla lakini nikazuiwa kuingia ndani, sasa natakiwa kulipa tenai inashangaza", alisema mama mmoja kwa jazba. "Haiwezekani, haiwezekani..." aliongeza.


Akili yangu ilikuwa juu ya kuungua kwa jengo la ofisi zetu Dar es Salaam. Lakini nilishangazwa vipi vyombo vya habari kama Televishen na redio havikuwa vimeripoti habari ya tukio hilo kubwa. Labda lilikuwa agizo kutokana na unyeti wa ofisi hizi, Nilijiuliza mambo mengi, baada ya kutafakari kwa kina nikijiuliza hili na lile, wazo likanijia. Nikapiga simu kwa Peter Twite, Dar es Salaam.

"Sikiliza Peter, kwanza habari ya saa hizi... Una taarifa zozote kuhusu ofisi zetu Dar es Salaam?. Niko Mwanza" nilimuuliza baada ya salaam.


"Habari si nzuri Mkuu, moto umezuka ghafla na kuteketeza kabisa ofisi zetu, ninavyoongea niko sehemu ya tukio na kazi ya kuzima moto inaendelea, Kanali Emilly anakusubiri kwa shauku kubwa", alisema Peter Twite nikashangaa.


"Ananisubiri... kwanini anisubiri kwa shauku... Nitasaidia nini mimi wakati tayari maji yamekwisha kumwagika?", nilimuuliza akacheka.


"Ukubwa dawa, labda ana jambo lingine la ziada, linapotokea tatizo kubwa kama hili, kila mtu huwa na mtazamo wake, utamsikia ukifika Dar".


Abiria walikuwa wengi. Ili niweze kusafiri usiku huu, nilikuwa nimewasiliana mapema na rubani wa bdege hii, Mapambano Mussa, kumfahamisha kuhusu umuhimu wa safari yangu, akanihakikishia kuwa nitasafiri na ndege ya saa tatu na nusu.


Mawazo yangu yalikuwa juu ya tukio la kuungua kwa ofisi zetu Dar es Salaam. Sasa akili yangu ilikuwa imeamini baada ya Peter Twite naye kunithibitishia hivyo. Nilipita sehemu ya ukaguzi, baadhi ya abiria walikuwa wakilalamikia gharama kubwa ya kulipia ndoo zenye samaki. Papo hapo pia kulikuwa na malipo ya karatasi laini ya kuzuia harufu. Niliumizwa gharama hizi zilizobuniwa na watu kwa ajili ya kuwaongezea mzigo abiria.


Chumba cha abiria kilikuwa kimejaa, waliobahatika kukaa walikaa na waliokuwa na bahati mbaya kama mimi tulisimama. Ndege ndogo zilikuwa zikiruka na kutua, bila shaka zilikuwa za kukodi. Mara nikamuona abiria mmoja anasimama na kukiacha kiti chake, nilinyata taratibu nikaketi.


"Samahani kaka, usikae pana mwenyewe hapa", alisemama mama mmoja.


"Pana mwenyewe!", nilimuuliza kwa mshangao. "Mama, sehemu kama hizi huwa hazina mwenyewe, hizi ni sehemu za huduma, kila mmoja ana haki ya kuketi, mbaya ni kumuondoa mtu kwenye kiti alichowahi kuketi, lakini kama amesimama mwenyewe na mimi nikakaa kuna tatizo", nilijaribu kufafanua.


"Lakini kama mwenzio amewahi tayari ana haki ya kuwa sehemu yake". alisema.


"Si kusudio langu kulumbana na wewe, hebu angalia tiketi yako", akaifungua ili kuangalia, "Angalia namba yako utakayoketi", akafanya hivyo, baada ya kuangalia kwa sekunde kadhaa akageuka kuniangalia. "Namba iliyoandikwa kwenye tiketi hii ndiyo abiria mwingine hawezi kuingilia, hata mahakamani utakwenda kifua mbele", nilisema huku nikisimama kumpisha asijeniona mkorofi.


"Keti tu kaka, wajamaa hawabanani, sote ni abiria, tusikosane kwa sababu ya kiti", alisema mama huyu, nikatabasamu.


"Usijali mamangu, samahani kwa maneno yangu ya utani, usiyachukulie kama ndivyo nilivyo, ni katika kutania tu, tunaposafiri katika chombo kimoja, tumekuwa ndugu katika safari, nikianguka hapa nyote mtaacha kazi zenu kunisaidia, vivyo hivyo na wewe, ukianguka hapa nitakuwa wa kwanza kukusaidia".


"Shetani apishie mbali, tena ashindwe kabisa kwa jina la yesu", alidakia mama huyu, mimi nikacheka na baadhi ya abiria pia wakacheka.


Foker 27, ndege ya abiria ya shirika la ndege Tanzania iliruka kutoka uwanja wa ndege wa Mwanza saa tatu na dakika arobaini usiku, tayari kwa safari ya kuelekea Dar es Salaam. Abiria wote ndani ya ndege tulikaa kimya tukisubiri hatma yetu. Maana kutoka Mwanza. Ukanda wa Ziwa ViCtoria hadi Dar es Salaam ilipo Bahari ya Hindi ni mwendo wa saa moja na nusu hivi.


"Wewe ni mwenyeji kidogo Dar es Salaam?" Mzee mmoja wa makamo aliniuliza baada ya ndege kuruka na kukaa sawa.


Kwa sababu ambazo sizijui nikamjibu, "Hapana. Leo itakuwa mara yangu ya pili kuingia Dar es Salaam. Una tatizo mzee wangu?", nilimuuliza.


"Nimeitwa kwenye kikao cha wafanyabiashara. Kikao kimepangwa kufanyika kesho saa tatu asubuhi, eneo la Sinza. Hii ni mara yangu ya kwanza kuingia katika jiji hili", alisema mzee huyu.


"Kikao kuhusu nini?" nilihoji.


"Ni mambo ya biashara tu. Kuna watu wanatoka nje kwa ajili ya mazungumzo, tumekuwa tukiwasiliana nao kwa njia simu na email, sasa kesho tunakutana rasmi", alifafanua.


"Vizuri, siku hizi dunia imekuwa kijiji, kila aina ya mawasiliano, usafiri na mambo mengine huwezi kupotea, hata mimi tukishuka nachukua taksi kuelekea Kigamboni waliko ndugu zangu. Wewe unahusika na biashara gani?".


"Biashara ya nyumba za kulaza wageni Mwanza na Shinyanga, pia nasafirisha abiria kati ya Mwanza na Bariadi, mkoani Simiyu. Kwetu kabisa ni Simiyu".


"Oh hongera sana, nilikuwa na ndoto ya kuwa mfanyabiashara mkubwa kama wewe lakini ndoto yangu haikutimia, nikaishia kuwa Mwalimu wa shule ya msingi huko Bunda, mkoani Mara", niliongopa.


"Ualimu si kazi mbaya, sasa hivi waalimu ndiyo wanaangaliwa na serikali kama kioo. Rais wetu hataki mchezo, naamini baada ya mwaka mmoja waliokuwa wanachukia kazi ya ualimu sasa wataitafuta wasiipate", alisema mzee huyu, pamoja na matamshi yake kuwa ya kiswahili chenye rafudhi ya Kisukuma, nikaanza kuelewa kuwa ni mzungumzaji mzuri.


"Nimefurahi sana kusikia maneno hayo, zamani kazi ya walimu ilikuwa nzuri sana, sijui kilipita nini walimu wakaonekana si lolote, binafsi namshukru sana Rais wetu, kama hali itaendelea hivi heshima yetu itarudi. Nitakupa namba yangu ya simu, pia utanipa namba ya simu yako ili tutafutane kesho baada ya wewe kumaliza kikao", nilimwambia akaonekana kufurahishwa na maneno yangu.


"Umefuata nini Dar es Salaam?", alihoji.


"Mdogo wangu ni askari polisi, yuko kituo cha kati". Baada ya kupeana namba za simu mazungumzo yakaendelea. Tuliongea mambo mengi kuhusu biashara hizi na zile. Nilianza kumpenda mzee huyu, alionekana muungwana sana, labda ndiyo siri ya mafanikio yake.


"Nitakutafuta kesho tukimaliza kikao, nitakuelekeza mahali nilipo, utakuja tutaongea mawili matatu", alisema wakati ndege inashuka taratibu kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere, Dar es Salaam.


"Naitwa Julius, Mungu akitujaalia tukionana tena tutafahamiana zaidi, nitakuita Bunda siku moja, japokuwa si rahisi masikini kama mimi mwalimu kumuita tajiri kama wewe na ukaja kunitembelea, kama unavyojua masikini kwenda kwa tajiri mara kwa mara ni sawa, lakini tajiri kwenda kwa masikini, akafuate nini?", nilimwambia.


"Hiyo inategemea na aina ya mtu. Sikiliza Mwalimu Julius, kwanza mimi naitwa Paul Mwifa, nina hoteli Mwanza inaitwa New Rehema, nyingine iko Shinyanga kwa jina hilo na Baria pia. Lakini sina majigambo, uliza wanaonifahamu, nitakukaribisha siku moja utaamini maneno yangu", alisema huku tukianza kutoka ndani ya ndege hii.


Nilichukua mkoba wangu mdogo nikauvaa, kwa kuwa nilikuwa karibu na mlango wa kutokea wa nyuma nilimuaga mzee Mwifa nikatoka taratibu kuelekea nje. Nilipita sehemu ambayo abiria husubiri mizigo, kwa vile sikuwa na mzigo wa kusubiri nikapita moja kwa moja kuelekea nje. Watu wengi walifika uwanjani hapo kusubiri wageni, baadhi walibeba mabango yenye majina ya watu. Nilipita kimya kimya nikisumbuliwa na baadhi ya madereva taksi, hatmaye nikavutiwa na maelezo ya dereva mmoja nikaingia kwenye gari lake tukaondoka kuelekea mjini.


Wakati dereva wa gari hii anaanza kuondoka uwanja wa ndege, kupitia kwenye kioo cha kushoto, niliweza kuwaona vijana wawili wakikimbia na kuingia kwenye gari iliyokuwa imeegeshwa karibu na sehemu ya malipo ya gharama za uwanja.


"Jitahidi nina haraka kidogo", nilimwambia dereva akaongeza mwendo. Tulipofika kwenye kizuizi cha kukagua tiketi za malipo, gari hiyo ilisimama nyuma yetu, dereva wangu aliingiza kadi ya malipo, kizuizi kikafungua kuashiria kuwa tumeruhusiwa kupita. Gari hilo pia likafuata taratibu kama tulivyofanya nalo likapita. Ilikuwa BMW nyeusi, ndani kulikuwa na vijana wawili, ambao hata hivyo sikuweza kuwaona vizuri.


Haraka nilifungua mkoba wangu nikatoa lens yangu ndogo ambayo hunisaidia kuona vitu vya mbali. Kulikuwa na vijana wanne, kila mmoja alionekana kuwa majukumu yake kama wenyewe walivyokuwa wamepangiana. "Ingia kituo cha mafuta", nilimwambia dereva wa gari hii akanishangaa.


"Gari yangu ina mafuta ya kutosha, sisi huwa tunajaza full kwa ajili ya kuepuka usumbufu kwa abiria wetu, ni agizo la uwanja, kwa hilo usihofu", alisema.


"Nataka kuingia Super Market kidogo", nilidanganya.


"Hapa wanafunga saa nne usiku, sasa ni saa tano na nusu, labda tujaribu Super Market ya Uchumi", alishauri kijana huyu aliyekuwa akiendesha Toyota Carina muundo wa TI.


Mbele yetu nikaliona gari lingine aina ile ile ya BMW, rangi ya blue, nilipovuta lens yangu kulikuwa na vijana wawili nao wakiwa tayari kutimiza kazi waliyotumwa. Nilijilaumu kwa kutokuweka tahadhari, lakini kwa vile nilikuwa nimegundua hali hii mapema nikajiweka tayari kwa lolote ambalo lingetokea.


Mara ujumbe mfupi ukaingia kwenye simu yangu, 'KUWA MAKINI BOSI, NYOKA MWENYE SUMU KALI ANATEMBEA KARIBU NA MIGUU YAKO, AKIKUNG'ATA UMEKWISHA'. Wakati tunavuka kwenye taa za kuongoza magari za uwanja wa ndege. Gari lililokuwa mbele yangu lilipungua mwendo ili kuruhusu gari letu lianze kupita kwenye taa hizi.


Ghafla nilisikia kelele za risasi, wakati huo nilikuwa tayari nimejitupa nje na kuliacha gari likiseleleka kuelekea mtaroni. Mara lilitokea Lori lililobeba takataka na kuigonga BMW iliyopunguza mwendo ili kuturuhusu sisi tupite, Vijana wawili waliovalia mavazi yaliyoficha nyuso zao waliruka kutoka kwenye lori na kurusha risasi kuyashambulia magari hayo.


ITAENDELEA 0784296253
 

SHAMAC

JF-Expert Member
Feb 9, 2017
1,345
2,000
SEHEMU YA TANO


Ilikuwa asubuhi ya misukosuko, vurugu na jitimai, wakazi wa Jiji la Dar es Salaam walikimbia bila mpangilio. Kila mmoja akijaribu kuitetea roho yake, wakati askari kutoka Kikosi Maalum cha Polisi wa Kutuliza Ghasia walipokuwa wakitekeleza moja ya majuku yao ya kuzuia fujo katikati ya Jiji.
Wakitumia magari yao ya kazi aina ya Landrover Defender TDI za jeshi la polisi Tanzania, zikiwa na rangi ya blue, bunduki maalum za kurushia mabomu ya moshi zikiwa mikononi mwao. Askari hawa walipita mitaani kifua mbele, wakirusha mabomu ya machozi huku na huku ili kutimiza wajibu wao huo.

Mchoro kuonyesha hali halisi ya mapambano ilivyokuwa

Magari haya yaligawanyika katika pande mbili mengine yalielekea upande wa Mnazi Mmoja. Mengine yakaelekea upande wa Ilala, ili kuwakabili vyema wananchi hawa waliodaiwa kukaidi agizo la serikali lililowakataza kufanyabiashara katikati ya jiji. Askari hawa waliendelea kurusha mabomu kila mahali palipoonekana kuwa na mkusanyiko wa watu kuanzia wawili.
Hali hii ilionekana sawa na mchezo wa kuigiza. Sikufurahishwa na kitendo hiki cha askari kurusha mabomu bila mpangilio, wananchi sasa walikimbia huku na huku mfano wa Pundamilia waishio kwenye mbuga za wanyama za Serengeti, wanapofukuzwa na mnyama mwenye njaa kali Simba.
Hata hivyo kulikuwa na ukaidi wa wazi kutoka kwa raia hawa, ambao walionekana wazi kukaidi amri hii iliyotolewa na polisi kupitia chombo maalum cha kukuza sauti. "Amri ya Jeshi la Polisi, mnatakiwa kutawanyika haraka, vinginevyo tutatumia nguvu kuwatawanya", sauti ilisikika kutoka katika chombo hicho maalum.
Wakati huo mimi nilikuwa nimesimama kwenye ukuta wa Shule ya Msingi Uhuru, karibu na makutano ya Barabara ya Uhuru na Msimbazi, nikifuatilia kwa karibu kasheshe hilo, ambalo kwa kiasi fulani lilibadili sura nzuri ya Jiji la Dar es Salaam, hali ya utulivu ikatoweka na hofu ikachukua sehemu yake. Kumbukumbu za mauaji yaliyosababisha kuwa na wakimbizi wengi katika nchi za Congo, Rwanda na Burundi ikanirudia kichwani.
"Hali hii ikiachwa iendelee hivi kama ilivyo sasa, itatuletea matatizo siku za usoni", nilijisemea moyoni. Nilikumbuka somo la usalama wa ndani, nilifundishwa somo hili na Luteni John John, wakati huo nikiwa mwanafunzi huko Monduli, mkoani Arusha, kuwa askari wanapashwa kufuata taratibu zilizowekwa wakati wa kukabiliana na hali kama hii, kukaidi amri halali.
Kila mahali ambapo askari hao waliona kuna mkusanyiko wa watu, walisogea na kurusha kombora, hali ilikuwa mbaya, karibu kila upande kilio kikubwa kilikuwa ni kuwashwa macho, kutokana na moshi huo kuwaingia machoni. Ili hali hii isikupate lazima ufumbe macho, jambo ambalo ni vigumu kukwepa.
Mimi pia nilikumbwa na kadhia hii, baada ya bomu lililorushwa kuanguka na kulipuka karibu kabisa na mahali nilipokuwa nimesimama. Kutokana na uzoefu wangu katika majanga kama haya, nilifanikiwa kutoka eneo hilo haraka bila kupatwa na madhara makubwa. Kila kikubwa cha watu ilikuwa ni kuwashwa macho, wengine walikimbilia maji ili kusafisha nyuso zao, lakini wakabaki kutetea kile walichoona kinafaa.
Kiasi nilibaini kuwa askari hawa hawakuwa makini katika kutekeleza majukumu yao, nilibaini kuwa iwapo wananchi hawa wakipata silaha zenye ubora kama walizonazo wao huenda wangesalimu amri kutokana na mpangilio wao kuwa mbovu, "Mmmh mfano hali hii ingetokea katika nchi za wenzetu na askari hawa wakafanya mchezo kama hivi, itakuwaje?" nilijiuliza.
"Mabomu haya yanayorushwa hovyo, hivi askari hawa hawaoni kuwa wanaitia hasara serikali", alisema mama mmoja wa makamo alisimama karibu yangu akiyahaha kuyasafisha macho yake.
"Hakuna hasara mama, mabomu haya yamenunuliwa na serikali kwa kazi hii, lakini hayakupaswa kutumika sasa, sioni sababu ya tembo kupigana na sungura, polisi wanatumia nguvu kubwa kupambana na adui ambaye hana silaha yoyote ya hatari, nikisema silaha nina maana hata wembe sidhani kama wamebeba hawa", nilisema.
"Kwanini wasitumie silaha kama hizi kukomesha matukio ya ujambazi yaliyokithiri nchini, au kuwakamata maharamia wanaosumbua wanachi katika maeneo ya mipaka na sehemu ya bahari, ambako kila siku tunasikia meli zinatekwa", alishauri mama huyu.
"Kuhusu suala la ujamnazi ni kweli silaha hizi zingesaidia sana mama, lakini hili na kukabiliana na maharamia wanaoteka meli hapa, polisi hawahusiki, hilo ni jukumu la wanajeshi, majukumu ya polisi ni kukabiliana na raia wakorofi, kama hawa waliogoma kutia amri ya serikali", nilimwambia mama huyu akaonekana kutabasamu.
"Nimejifunza kitu kutoka kwako kijana wangu, kumbe mipakani ni jukumu la wanajeshi? Nimeelewa sasa mwanangu", aliongeza mama huyu aliyekuwa na rafidhi ya mkoa wa Mtwara.
Pamoja na rafidhi yake kuwa ya kimakonde, alionekana mama mwenye busara nyingi, baada ya kumtafakari nikabaini kuwa huenda ni mmoja wa viongozi wa taasisi za wanawake ama mjasiriamali. "Kuwasumbua wananchi kwa kuwapiga mabomu kama hivi wewe kwa mtazamo wako unaona sawa?", aliniuliza.
"Si sawa kabisa, lakini pia lazima uangalia chanzo nini? Serikali imetenga bajeti ya kuagiza silaha kama hizi, kwa ajili ya kazi kama hii, lakini busara ilihitajika kwanza, sijui kama wamefuata njia hizo, pengine inatafutwa sababu ili kupunguza masalia ya silaha hizo", nilimwambia akanikazia macho halafu akacheka.
"Kuwachokoza wananchi ili uwarushie mabomu?, hilo umejaribu kuweka chumvi, sijui, labda kwenye Serikali za Kidikteta", alisema tukacheka huku nikimuaga baada ya hali ya vurugu kutulia kidogo.
Gari langu dogo aina ya VW Golf, lenye muundo wa polisi ambalo wengi hawalijui, nililiegesha ndani ya uzio wa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, nilifanya hivyo kuepuka hali hii, ambayo baadhi ya watu huitumia kuwaibia wengine kwa mgongo wa watu wenye msimamo mkali.
Kilichonifikisha katika eneo hili ni kamba maalum niliyokuwa nikihitaji kuinunua, kamba hii ilikuwa na maana kubwa katika kazi zangu za hatari. Nilikuja kuinunua kamba hii baada ya kutokea shambulizi la kushitukiza wakati niliposhuka Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere. Sikujua walionishambulia walikusudia nini. Lakini pia taarifa ya kuteketea kwa jengo la ofisi zetu iliyotolewa na Kanali Emilly, ambayo si kweli iliniongezea tahadhari.
Nilijikuta nikitafakari hili na lile, nikiwaza na kuwazua, nilibaini kuwa kuna tukio la hatari limetokea hivyo, Kanali Emilly alinihitaji haraka ofisi kwake, akalazimika kugeuza lugha, kuwa ofisi zetu tunateketea kwa moto. Hata nilipofuatilia tukio hilo kwenye vyombo vya habari, taarifa hiyo haikuwepo. Hata nilipoongea na Peter Twite, ilionekana hakuna tukio la kuungua jengo la ofisi zetu barabara ya Azikiwe.
Baada ya kupata kitendea kazi kilichonileta eneo hili. Yaani, kamba nyembamba lakini madhubuti kwa ajili ya mambo yangu, nilijiondoa taratibu, nikatembea kwa tahadhari kubwa kuelekea lilipo gari langu, kila mtu karibu yangu alionekana kuwa adui yangu, waswahili wanasema uking'atwa na nyota, ukiguswa na ujani unashtuka, ndiyo hali niliyokuwa nayo, nililikagua gari hilo vizuri, baada ya kujiridhisha nikaingia na kuliodoka taratibu kuelekea Posta, ofisini kwa Kanali Emilly.
ITAENDELEA 0784296253
 

SHAMAC

JF-Expert Member
Feb 9, 2017
1,345
2,000
SEHEMU YA SITANiliendesha gari taratibu kuelekea kwenye ofisi zetu zilizoko Barabara ya Azikiwe. Kichwa changu kilishika hili na lile, nilijiuliza maswali mengi ambayo hata hivyo nilikosa maelezo yake. Nilijilaumu kwa kutozima simu yangu ya mkononi nilipokuwa kijijini kwetu Nyamuswa, ningefanya hivyo, pengine sasa ningekuwa nafaidi samaki, kuku wa kienyeji na maziwa ya mtindi.

Kutoka Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, nilipokuwa nimeegesha gari, nilipita kwenye Barabara za Shauri Moyo na Uhuru nikaibukia kwenye taa za kuongoza magari za Karume, ambapo nilisimama kusubiri ruhusa ya taa hizi. Nilipoingia kwenye Barabara ya Rashid Kawawa, niliongeza mwendo kidogo ili kuwafanya madereva wa magari ya nyuma yangu yasipate usumbufu. Nilipolipita eneo la Msimbazi Centre, niliiacha barabara hii nikaingia kulia halafu kulia tena nikaupita Uwanja wa mpira wa Kaunda, unaomilikiwa na Klabu ya Yanga ya Dar es Salaam.

Shambulizi la usiku uwanja wa ndege liliniongezea hofu na umakini katika kufanya maamuzi, nilijiweka tayari kwa lolote, kila mtu alionekana kuwa adui yangu, nilijiuliza maswali mengi, ningekuwa wapi muda huu iwapo shambulizi lile lingefanikiwa, sikujua sababu za watu hao kufanya shambulizi hilo lililolenga kuniondolea maisha, moyo wangu haukuwa na amani tena, nililitilia shaka kila gari lililoonekana kuwa nyuma au mbele yangu.

Ilikuwa vigumu sana kwa mtu asiye na uwezo wa ziada kama wangu kulibaini gari ninaloendesha, nililazimika kutumia gari hii Toyota Brevis ya rafiki yangu Tigani, ili kukwepa shambulizi lingine, japokuwa dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia hakuna jambo la siri, lolote laweza kutokea.

Shambulizi hilo lilinithibitishia kuwa watu hawa hawana mchezo na wamejipanga vizuri katika mipango yao ya kazi, nilimtafuta Luteni Fred Libaba kwenye simu yake, baada ya kumpata nilimuuliza mahali alipo akanijulisha kuwa yuko Wizara ya Mambo ya Nje kwa kazi maalum nikamtaka asirudi ofisini mpaka nitakapomjulisha ili baadaye tuonane juu kwa juu nje ya ofisi.
**********************

Wakati huo, kikao cha dharura kilifanyika nyumbani kwa mzungu Carlos Dimera. Kikosi maalumu cha matapeli wa kisasa kabisa kikiongozwa na mzungu huyu kilikutana kwa siri kujadili hatua za kuchukua baada ya shambulizi la kumuua Teacher kutofanikiwa.

"Nani aliongoza mpango wa mashambulizi ya usiku kule uwanja wa ndege?" akiwa amechukizwa sana Carlos Dimera aliuliza baada ya wajumbe wote muhimu kufika kwenye kikao hiki.

Tofauti na kikao cha awali kilichofanyika juzi, ambapo Carlos alifanya mazungumza na washiriki pande mbili, kila upande aliupangia majukumu yake, safari hii aliwakutanisha wote, kilikuwa kikao cha pamoja, kikiwahusisha wataalam wa wizi madini feki, watakatishaji wa noti bandia na wasafirishaji wa dawa za kulevya.

"Bosi Carlos... Vijana walijipanga vizuri mno, tulikuwa na asilimia zaidi ya mia kumaliza kazi hii, kwa hili tusitafute mchawi, lazima ufahamu katika mawindo, kuna kuwindwa pia, ndicho kilichotokea usiku. Lakini tukuhakikishie kuwa kutenda kosa siyo kosa, kosa ni kulirudia hilo kosa, leo itakuwa mwisho wa maisha ya Teacher, popote atakapoonekana amekwisha", alisema Nombo.

"Sitaki kusikiliza hadithi za Abunuasi hapa, natoa nafasi ya mwisho, kama Nombo alivyosema kazi hii iishe leo mapema ili tupate uhuru wa kufanya mambo yetu, tukionana kesho tusizungumzie habari ya Teacher tena, nimetenga kiasi cha pesa kwa ajili ya sherehe kubwa, mkimaliza kazi hii vizuri tukutane tupongezane kwa kazi nzuri", Carlos Dimeta alieleza.

"Pamoja na kikao hiki cha dharura, Nyati, Simba na Chui wako katika mawindo, tunawasiliana kila baada ya dakika tano au kumi, kama unavyowajua vijana hawa bosi, jua la kesho Teacher hawezi kuliona kabisa, hasa nikimfikiria Nyati alivyo Teacher amekwisha", alieleza Jackina.

Baada ya mpango huu kuwekwa sawa, mjadala mwingine ulianza, walibuni mbinu nyingi za kuchukua pesa kwa wafanyabiashara matajiri na baadhi ya wastaafu walioorodheshwa bila kusababisha madhara. Mbinu hii ilipangwa na Carlos mwenyewe, mzungu huyu alikuwa na mbinu nyingi na kuwafanya washiriki wa mtandao huu kutegemea zaidi mawazo yake.

Pamoja na kumiliki pesa nyingi, ambazo walifanikiwa kuziiba kwenye mabenki kadhaa ya Dar es Salaam. Pia waliweza kusafiri ndani na nje ya nchi wakitumia hati bandia na mbinu hizi na zile kujipatia pesa.

Carlos Dimera alikuwa karibu na baadhi ya viongozi wa serikali. Nchini Tanzania, alikuja nchini kwa mgongo wa mwekezaji aliyekuja kujenga kiwanda cha kutengeneza tembe maalumu za kope za urembo wa akina dada. Kutokana na ukarimu wake alifahamiana na kila mtu. Machoni mzungu huyu alionekana kama rafiki wa kila mtu, lakini moyoni alikuwa adui mkubwa wa maendeleo ya taifa.

Kumbukumbu zilionyesha kuwa mzungu Carlos Dimera alikuwa amefukuzwa kutoka katika baadhi nchi za Afrika ambako alibainika kufadhili vikundi vya wahalifu. Nchi ya mwisho kutimuliwa ilikuwa Rwanda, ambako aliishi kwa zaidi ya miaka mitatu, akitokea Kampala, nchini Uganda baada ya kutiliwa shaka. Alipoingia Dar es Salaam Tanzania hakuwa mgeni katika nchi ya Afrika Mashariki, kwani alimudu kuongea kwa ufasaha lugha ya kiswahili hivyo haraka aliweza kuunda mtandao wake na kuanza kazi rasmi.

Maofisa kadhaa wa idara za serikali, waliokuwa na dhamana ya kusimamia pesa za umma waliibiwa kwa mbinu hizi na zile, baadhi waliona aibu kuripoti taarifa hizo polisi wakihofia kufukuzwa kazi wengine wakijipeleka polisi wenyewe wakidanganya wamevamiwa na majambazi.

Baada ya kuingia Jijini Dar es Salaam, haraka Carlos aliweza kujenga hekalu au jumba kubwa la kisasa kando ya bahari na kuiomba serikali imruhusu kuweka walinzi wake binafsi, baada ya kupata kibali, aliweka ulinzi mkali kuzunguka jumba hili, akiwatumia askari wa kukodi kutoka kitengo maalum cha ujasusi cha Havana, nchini Cuba.

Vinywaji na vyakula vya aina mbalimbali vililetwa, wajumbe walikula, wakanywa na kusaza, wakiifurahia faida ya kazi yao, kila mmoja alionekana mwenye furaha kupita kiasi, wakimuomba mungu awasaidie kufanikisha jukumu lililokuwa mbele yao.

Pamoja na wajumbe hawa, Carlos Dimera, alikuwa na vijana wengine watatu ambao huonekana kwa nadra sana. hawa waliokuwa wamehitimu vizuri mafunzo ya ujasusi sehemu mbalimbali duniani, vijana hawa pia aliwatumia kwa nadra sana, hususan pale Simba, Chui na Nyati wanapokuwa wameshindwa kutimiza moja ya majukumu yao. Simba, Chui na Nyati walikuwa mfano wa mbwa mwitu, kazi yao kubwa ilikuwa kuteka au kuua watu pale wanapoagizwa kufanya vile.

Kufukuzwa kwa Carlos katika baadhi ya nchi hizo haikumfanya kuvunja mitandao yake huko, kazi ziliendelea kama kawaida kwani ndiye aliyeanzisha utapeli wa noti za bandia, pia ndiye muasisi wa kutegesha vyura, mijusi na wadudu kwenye baadhi ya ofisi za serikali na hivyo kuwafanya watumishi wa ofisi hizo, Mawaziri, Makatibu Wakuu wa Wizara na Wakurugenzi kuzikimbia ofisi zao wakiamini kurogwa na wakati huo huo vijana wa Carlos Dimera wanageuka kuwa waganga hodari wa tiba na kufanikiwa kujipatia mapesa mengi kutoka kwa vigogo hao.

"Bosi, nakuhakikishia vijana wako tayari kwa kazi, tumefanya mengi kupitia ubunifu wa kichwa chako, ili tusonge mbele lazima mtu afe, mtu huyo anajiita Kapteni Teacher, kama alipona katika shambulizi la jana, leo hawezi kuchomoka, vijana wameapa", alisema Hawa kwa kujiamini.

Mwana mama huyu alikuwa katili na kipenzi cha Carlos Dimera, alikuwa na sifa kadhaa za kumfanya awe kipenzi cha mzungu huyu, moja ya sifa hizo ni ukatili pia alikuwa na uwezo wa kubadili jambo, akalisimamia kwa nguvu zake zote hata likawa sheria au kanuni.

"Sikilizeni, nimepata ujumbe wa maandishi kutoka kwa wanaspoti wetu, kama mtakumbuka wiki iliyopita tuliweza kuchukua kiasi kikubwa cha pesa kwa watu wawili, mmoja ni Waziri mstaafu huko Mikocheni, mwingine ni mfanyabiashara wa Sinza". Carlos Dimera aliwaeleza.

"Naam bosi, kilikuwa kibarua kigumu mno, lakini tuliweza kufanikiwa, kuna nini bosi?" alihoji Jackina aliyekuwa kiongozi wa operesheni hiyo.

"Wahusika wametoa taarifa polisi. Lakini sina tatizo na jeshi la polisi, hawa ni watu wetu wanachukua mshahara hapa, mbaya ni kwamba malalamiko yamepelekwa idara ya usalama inayosimamiwa na wanajeshi, Hawa amesema tuna watu wetu huko lakini haitoshi, wanajeshi ni kigeugeu. Jaribio la jana lilikusudia kumuua Teacher na kutoa onyo, baada ya jaribio hilo kushindwa naamini adui yetu atajipanga vizuri zaidi, akionekana popote ua kwanza", alisema Carlos Dimera.

Baada ya kutafakari kwa sekunde kadhaa, Jakina akasimama, "Taarifa kutoka kwa wana mtandao wetu ni kwamba idara hii inawategemea sana maofisa wake wawili. Huyu Kapteni Teacher na mwingine anaitwa Fred, huyu ni afisa wa cheo cha Luteni.

"Safi sana Jackina, ndiyo sababu nakuamini sana, naamini kazi yako itafanyika vizuri, ukitoka hapa pita kwa mhasibu akuongezee nguvu, ikiwezekana Teacher na huyu Fred wasilione jua la kesho. Lakini jitahidi kuwahadharisha vijana wako wasiende kichwa kichwa kwa watu kama hawa", Carlos Dimera alishauri.

"Kuhusu hilo ondoa shaka bosi, hivi tunavyoongea vijana wako nyuma yake, tumewahadharisha wasiwe na papara, kazi hizi hazitaki papara, subiri wakati ufike, utasikia", alisema Jackina kwa kujiamini.

"Naamini kuwa wote mmeinjoy vizuri, haya ndiyo maisha, nani kati yenu atapenda kurudi kijijini, aanze maisha ya kijijini, unaamka alfajiri na jembe mkononi, mazao baada ya miezi sita, unavuna, bado kuna usumbufu kibao, ikiwemo kukopwa mazao na usilipwe kwa wakati au hata usilipwe kabisa", alihoji Nombo.

Baada ya kupanga mipango ikapangika, kikao kilivunjwa, huku Carlos akisisitiza kupewa taarifa ya kifo cha Teacher mapema iwezekanavyo.

ITAENDELEA 0784296253
 

SHAMAC

JF-Expert Member
Feb 9, 2017
1,345
2,000
SEHEMU YA SABAOfisi zetu ziko ghorofa ya juu katika jengo la Benjamin Wiliam Mkapa. Baada ya kuegesha gari kwenye maegesho ya Hotel JB Belmont, nilikwea ngazi mbili tatu nikaitafuta lifti iliyonipeleka juu kabisa. Shambulizi la usiku lilinifanya niliweka ulinzi wa kutosha kuzunguka eneo la ofisi zetu.

Kazi yangu ya kwanza niliyofanya usiku baada ya kutuliza akili yangu ni kuwasiliana na Sajenti Julius Nyawaminza, huyu ni Komandoo aliyebobea, akilitumikia jeshi katika vikosi vya Zanzibar. Nilimwagiza kufika haraka Dar es Salaam, kwa vile Unguja ni karibu alifika Jijini asubuhi na kujiweka kwenye pointi niliyompangia awe.

Kwa kuwa vijana wetu wa Dar es Salaam wanafahamika kwa kiasi fulani, nilipanga kuwatumia kwa kazi zingine, hivyo niliwasiliana pia na Luteni, Claud Mwita kutoka vikosi vya Komandoo mkoani Morogoro, ambaye pia aliweza kufika kwa wakati, akafanya kile alichoelekezwa kufanya.

Nilichelewa kwa dakika kadhaa kufika ofisini kwa Kanali Emilly kama ambavyo tulikuwa tumeafikiana, kuchelewa kwangu kulitokana na mipango ya hapa na pale, maana mtu akikuanza utani lazima ujiandae kutaniana naye, lakini pia akikuanza uchokozi muonyeshe kuwa amepita njia mbaya.

Mapokezi nilipokelewa na Linnah David, Katibu Muhtasi wa Kanali Emilly, "Ulikuwa wapi Teacher? Mzee anakusubiri kwa shauku kubwa, amesema ukitia pua tu, usisimame, moja kwa moja ingia ofisini kwake", Linnah alitania.

"Vipi hali yako Linnah, sikukuacha ofisini, nilisikia wewe pia umepata likizo kulikoni? Au ndiyo umeitwa haraka kama mimi?", nilimuuliza akatabasamu.

"Nitakwambia ukitoka kwa bosi", alisema Linnah huku akinihimiza kuingia ndani ya ofisi ya Kanali Emilly.

Mapigo ya moyo wangu yalianza kunienda mbio, sikujua kilichotokea hata nikaitwa haraka kiasi hiki, taratibu niligonga mlango wa ofisi ya bosi, baada ya kusubiri kwa sekunde kadhaa nilitasua kitasa cha mlango na kuingia ndani. Kanali Emilly aliponiona haraka alisimama na kunielekeza sehemu ya kuketi. Nilishangazwa na hatua hii, kunielekeza mahali pa kukaa karibu kabisa na yeye tofauti kabisa na kawaida yake.

Kanali Emilly alikuwa mzee wa makamo, lakini mwenye busara na nguvu nyingi, hakuwa mwepesi wa kushindwa jambo. Baada ya kupeana mikono na mimi kuketi mahali aliponielekeza, aliinua simu yake ya mezani akamwagiza Linnah atuletee vinywaji. Kabla ya kukata simu, Kanali Emilly alimtaka Linnah kuongeza vinywaji kwa ajili ya wageni wanaokuja. Mimi nikabaki kimya.

"Karibu sana Teacher, pole kwa kukatisha likizo yako fupi, nimekuita kwa sababu kuna tatizo limetusibu, tutakuwa na wageni hapa ofisini muda si mrefu, wanakuja kuongea na sisi, tutawasikiliza, tutashauriana nini cha kufanya", alisema Kanali Emilly, aliinua tena simu yake ya mezani akaongea na watu ambao mimi sikuwajua, akawajulisha kuwa mimi nimefika hivyo waje ofisini kwake.

"Kuna tatizo gani bosi, maana sielewi kinachoendelea?" nilimuuliza Kanali Emilly.

"Kuna tatizo kidogo limetoke. Nikaitwa haraka nyumba kubwa, kutakiwa kurudi kwako haraka ni agizo la Rais. Wakati tunawasubiri hawa ndugu zetu, nitakudokeza kidogo kilichotokea", alifungua droo ya meza yake, akatoa bahasha kubwa iliyojaa mapesa, pia akatoa kiboksi kilichojaa makaratasi yaliyoandaliwa kama pesa, akanipatia.

"Hizi ni pesa zangu?", nilimuuliza Kanali Emilly akache

"Ziangalie kwanza Teacher, halafu nitakueleza sababu".

Zilikuwa pesa nyingi zinazotumika katika mataifa mbalimbali duniani. Zilikuwepo noti za shilingi elfu kumi za kitanzania, nilizipitia noti hizi moja baada ya nyingine, sikuona tofauti. Niliendelea kuziangalia noti hizi kwa umakini mkubwa, zilikuwepo noti za Saandaang Piso zinazotumika Jamhuri ya watu wa Philipines, Diez ya Uruguay, Paundi ya Misri, Birr ya Ethiopia, Yen ya Japan na Won ya Korea Kusini.

Niliendelea kuzipitia pesa hizi kwa umakini sana, Kanali Emilly alikaa kimya akiniangalia, sikufahamu lengo la mzee huyu kunipatia pesa hizi niziangalie tu. Niliendelea na zoezi la kuzikagua noti hizi, Rupiah ya Indonesia, Rupee ya Pakistan, Rand ya South Afrika, Afghan ya Afghanistan, Rouble ya Belerus na Peso ya Cuba.

Kulikuwa na idadi kubwa ya noti, ni vizuri nikutajie aina zote za noti zilizoko mbele yetu ili uweze kunielewa vizuri, kabla mzee hajasema jambo.

Aina nyingine ya pesa sikuwahi kuziona kabisa, kama Rouble ya Russia, Litu ya Luthuania, shilingi ya Kenya, Franc ya Afrika ya Kati, Real ya Brazil, Drams ya Armenia, Lira ya Uturuki, Krone ya Denmark na Riyal ya Saudi Arabia. Zingine ni Paund ya Sudan, Lei ya Romani, Dong ya Vietnam, Dollah ya New Zealand, Peso ya Argentina, Dinar ya Libya, Hryvmy ya Ukraine, Sum ya Uzbekistan, Kwacha ya Zambia, Franc ya Kongo, Franc ya Chad, Dinar ya Algeria, Rouble ya India, Franc ya Cameroun, Mark ya Ujeruman na Dollar ya Marekani.

Baada ya kuzipitia pesa hizi, nikazirejesha mikononi mwa Kanali Emilly, ambaye alizijaza kwenye bahasha kubwa, akaniangalia kwa sekunde mbili tatu, alipoona nimekaa kimya nikimwangalia akatoa bahasha nyingine iliyojazwa makaratasi yaliyokatwa kwa mpangilio mzuri mfano wa pesa. Karatasi hizi zilifungwa kwa mafungu sawa na noti, zikitofautiana kwa ukubwa wa aina ya pesa husika.

Niliendelea kuumiza kichwa changu, nilijiuliza sababu ya Kanali Emilly kuleta pesa hizi mbele yangu, kilichoanza kunizindua ni haya makaratasi yaliyokatwa mfano wa pesa, mawazo yangu hayakunipeleka mbali, nikahisi kuwa huenda karatasi hizi zimekamatwa kwa matapeli waliotapakaa kila kono ya miji ya Afrika Mashariki na duniani, wakiwaibia watu kila siku.

"Naam kamanda wangu, nifahamishe sasa. Kuna habari gani mkuu?", nilimuuliza baada ya kumaliza kazi ya kuzipitia karatasi alizokuwa amenipatia. "Hizi noti na karatasi nahisi zimekamatwa kwa matapeli", niliongeza.

"Afadhali tungekuwa tumewakamata, Teacher hili ni tukio linalotia huruma sana, huwezi kuamini nikikueleza kile kilichofanyika, watu wameuza majumba, magari na wengine wamefirisika kabisa kutokana na pesa na karatasi hizi ulizoziona", Kanali Emilly alieleza.

"Ehee?", nilihoji huku nikikiweka tayari kumsikiliza. Mara simu ikaita, akainua mkonga wa simu na kuiweka katika sikio lake la kushoto, baada ya muda alisema, "Waruhusu wapite tafadhali", akaweka simu chini.

"Teacher, kabla sijakueleza hali halisi ya tukio hili, bahati nzuri wahusika wamefika, utawasikiliza kwa makini, wataeleza kilichowasibu, sidhani kama tutashindwa kuwasaidia katika hili", alisema Kanali Emilly.

"Itategemea na kazi yenyewe bosi, kama ujuavyo hii ni dunia, hata uwe mjuzi wa kuogelea kiasi gani, iko siku maji yatakuzidi ujanja, unaweza kuingia mpaka kimo fulani ukashindwa kuendelea, lolote laweza kutokea", nilimwambia. Sikuona vizuri kumsimulia kuhusu tukio la usiku, hivyo nilimezea.

Mlango wa ofisi uligongwa, Linnah akaingia akifuatiwa na watu wawili waliotakata vizuri, ukiwaangalia huhitaji kuuliza, moja kwa moja niliamini kuwa watu hawa ni vigogo kutoka serikalini ama matajiri wenye mapesa yao.

ITAENDELEA 0784296253
 

SHAMAC

JF-Expert Member
Feb 9, 2017
1,345
2,000
SEHEMU YA NANESajenti Julius Nyawaminza aliwasili bandarini, Dar es Salaam kwa Meli ya Kilimanjaro II majira ya saa moja na dakika ishirini asubuhi akitokea Visiwani Zanzibar. Baada ya kuwasili Dar es Salaam, kutoka bandarini, Nyawaminza alitembea kwa miguu yake hadi eneo la Posta mpya kama alivyokuwa ameelekezwa.
Kijana huyu alikuwa na shauku ya kufanya kazi aliyokuja kuifanya Dar es Salaam, alifikiria mambo mengi aliyozungumza na Teacher usiku, akajiona mwenye bahati kipindi hiki kuitwa kufanya kazi katika mazingira aliyokuwa akiyasubiri kwa siku nyingi.
Baada ya kuhitimu kozi mbalimbali za kijeshi ndani na nje ya nchi, Sajenti Julius Nyawaminza alipangiwa kazi katika vikosi vya Zanzibar. Akiwa Visiwani Zanzibar, alifanya mazoezi yake ya kawaida kila siku akisubiri hali mbaya itokee. Yeyote angemuona barabarani kwa bahati mbaya asingeamini kuwa kijana huyu ni moto wa kuotea mbali, kama huamini mtafute umchokoze ili uamini haya niyasemayo..
Begani, Nyawaminza alining'iniza mkoba wake mdogo wenye vifaa vyake kadhaa vya kazi. Alipofika eneo la Posta mpya alinunua gazeti la michezo, akaketi kwenye mojawapo wa vibanda vya abiria wanaosubiri usafiri vilivyoko mbele ya jengo la Benjamini Wiliam Mkapa na Benki ya CRDB.
Luteni Claud Mwita, kutoka mkoani Morogoro, naye pia alikuwa amewasili katika eneo hilo, yeye alitumia usafiri wa bodaboda kutoka Ubungo, alifanya hivyo kutokana na hali ya barabara za Dar es Salaam asubuhi kuwa na msongamano wa magari mengi, hususan wakati wa kuelekea katikati ya Jiji.
Kama alivyofanya Sajenti Julius Nyawaminza, Claud Mwita alitafuta gazeti ya michezo, baada ya kupitia vichwa vya habari vya gazeti hili, akatafuta uelekeo akaweka makazi yake ya muda akisubiri taarifa kutoka kwa Teacher.
Pamoja na kusoma magazeti, vijana hawa walifika hapa kwa kazi maalum, kuangalia aina ya watu wanaofika eneo hilo na muda wa kukaa kusubiri usafiri wa daladala ama taksi zilizoegeshwa katika eneo hilo. Kila mmoja kwa wakati wake alituma ujumbe mfupi wa maneno kumfahamisha Teacher kuwa tayari amefika na yuko kwenye pointi ya kazi.
Nao Simba, Nyati na Chui kama wanavyofahamika, walifika eneo hilo mapema zaidi, hawa waligawana njia za kuingia na kutoka katika jengo hilo, Simba akiulinda mlango mkuu wa mbele unaoangalia kituo cha daladala, Nyati akajiweka upande wa kuingia na kutoka magari, Chui akaimalisha ulinzi kwenye mlango mdogo unaotokea sehemu ya maduka kama unatokea barabara ya Jamhuri.

Teacher aliingia ofisini kwa Kanali Emilly na kuonyeshwa karatasi zilizoandaliwa mfano wa noti, lakini zilikuwa bandia.
"Karibuni", Kanali Beny Emilly alisimama kuwakaribisha wageni hawa. Kwa sheria za kijeshi ilinilazimu mimi pia kusimama ili kumuunga mkono bosi wangu. Baada ya wageni hawa kushikana mikono na mzee huyu, wakanishika mkono.
"Karibuni, karibuni sana, mnaweza kuketi", Kanali Emilly alirudia kusema huku akiwaonyesha sehemu za kuketi.
"Shukrani sana", walisema wageni hawa kwa pamoja huku wakiketi taratibu kwenye viti vilivyokuwa mbele yangu. Kutokana na uzoefu wangu wa kazi nikabaini kuwa wageni hawa walikuwa na tatizo zito linalosumbua nafsi zao.
"Karibuni tena ndugu zangu, karibuni sana hapa ofisini kwangu, huyu kijana ndiye Teacher ambaye niliwafahamisha amesafiri, nikaona ni vizuri tumsubiri awepo ili tuzungumze wote kuona namna ya kusaidia jambo hili", Kanali Emilly alisema akiwaangalia wageni hawa.
Halafu akanigeukia, "Teacher, hawa ni wageni wetu, nimefarijika kukuona umerejea wakati muafaka kabisa, dunia ya sasa hakuna siri, jana niliitwa Ikulu kwa mheshimiwa Rais, nimeulizwa maswali mengi ambayo nimekosa majibu, nikaamini kuwa ukirudi tutajadiliana na majibu yatapatikana, ndivyo ninavyoamini", alisema huku nikimwangalia kwa makini.
Aliinua simu yake ya mezani akampigia Katibu Mahsusi wake Linnah, akamwambia atuletee vinywaji juisi, soda, maji na sambusa. Haikupita hata dakika tano, vinywaji vililetwa, tukaanza kunywa huku kila mmoja akiliweka tayari koo lake kwa mazungumzo.
"Mko tayari kwa mazungumzo yaliyowaleta, ni muda muafaka sasa kuzungumza?", Kanali Emilly aliwauliza watu hawa.
"Naam, tunaweza kuanza mazungumzo yetu", alisema mmoja wa watu hawa huku akimwangalia mwenzake usoni, mfano wa mtu anayeomba ridhaa ama kibali kwa ajili ya kuanza kutoa maelezo.
"Itapendeza kama mtaeleza kuanzia mwanzo ili tuwe pamoja na Teacher katika mazungumzo haya", Kanali Emilly aliwaeleza watu hawa, halafu akanigeukia mimi", "Teacher jana nilikutana na watu hawa, walinisimulia kwa undani kuhusu jambo hili lakini itapendeza zaidi wakirudia mbele yako ili upate picha kamili" aliniambia.
"Kijana au Teacher kama mzee wetu anavyokuita. Naamini utaelewa vizuri nikianza kwa kujitambulisha, sisi ni nani tunatoka wapi na tumefika hapa kwa sababu gani?".
"Naam", nilijibu kwa mkato.
"Asante. Mimi binafsi naitwa Enock Nyanda, mkaazi wa Msasani ni mfanyabiashara maarufu hapa Jijini Dar es salaam", alisema huku akiniangalia, nikamuonyesha ishara aendelee.
"Huyu mwenzangu anaitwa mzee Sadik Tagazi, makazi yake pia ni Msasani, ni mfanyabiashara wa siku nyingi... Kijana wangu, naamini nitaeleweka vizuri kwako nikisema wazi kuwa tamaa ya kupata mali nyingi imeniponza mimi, imemponza hata huyu mzee mwenzangu, tumeingizwa mjini, nimeibiwa kiasi kikubwa cha pesa, huyu mzee mwenzangu pia amefanyiwa hivyo hivyo, tumeumizwa", alisema huku machozi yakianza kumtoka, jambo ambalo kwa kiasi fulani liliushitua sana moyo wangu.
"Ehee, ilikuwaje mpaka mkaibiwa kiasi kikubwa cha pesa kama ulivyosema", nilihoji huku akili yangu ikibadilika, maana tukio hili ni moja ya matukio ya kawaida ambayo huwatokea watu kila siku, mawazo yangu yakarejea shambulizi la usiku, nikajiuliza ni wizi huu wa pesa uliosababisha nishambuliwe na kuponea chupuchupu.
"Labda, niseme wazi kuwa watu hawa wametumika teknolojia ya kisasa sana, naamini kwa teknolojia hii hata nani angeibiwa, mimi ni mtu makini sana, lakini huwezi amini nimeibiwa kirahisi mno", anaeleza mzee Sadik ambaye kwa muda mrefu alikuwa kimya.
"Ni teknolojia ipi hiyo, mbona mnazunguka tu hamsemi wazi?", niliwauliza.
"Nimewapa nafasi ya kuzungumza, ndiyo maana nikasema uwanja ni wenu, tusipoteze muda, cha msingi elezeni nini kilitokea mpaka mkaibiwa, jambo hili ni kweli linaweza kumpata kila mtu, lakini mengine ni uzembe wa mtu", alisema Kanali Emilly kwa hasira.
"Si kusudi letu kupoteza muda, tunataka kueleza jambo hili kwa kinagaubaga zaidi ili muone jinsi ya kutusaidia pia kuwanusuru ndugu wengine wanaokusudiwa kuibiwa kama sisi, nashauri mwenzangu aanze maana yeye ana taarifa nzuri na muhimu zaidi", alisema mzee Enock.
"Leo ni tarehe ngapi", alihoji mzee Sadik.
"Leo... Jumatatu ya Machi 21, unataka kusema nini?", Kanali Emilly alieleza na kuhoji.
"Ehee ni jambo zito lakini nitafanyaje, Machi 13, mwaka huu watu wawili nadhifu sana walifika ofisini kwangu... Nitaeleza kwa kifupi, utaniuliza maswali itakapobidi", alisema mzee Sadik. "Baada ya watu hawa kufika ofisini kwangu, tulianzia mbali sana, niliamini ni watu safi, tena waungwana sana, wakajitambulisha kuwa wanafanya kazi katika ubalozi mmoja nchini Tanzania, baada ya kujitambulisha walitoa karatasi fulani kuwa hizo ni dola za Kimarekani ambazo hazijasafishwa", alinyamaza kidogo ili kumeza mate.
Linnah aliingia ofisini kwa Kanali Emilly akiwa amebeba faili kubwa, aliliweka sehemu ya mafaili yanayoingia halafu akaniangalia na kufinya jicho lake, nikatabasamu akatoka.
"Ehee, leta habari, baada ya kuonyeshwa karatasi hizo ambazo walidai ni dola wewe kama wewe uliamini kuwa ni dola?", nilimuuliza. Alionekana kupagawa, kiasi fulani alionekana mwenye aibu kiasi.
"Teacher, ukweli ni kwamba hawa jamaa zetu wameibiwa lakini inashangaza jinsi wanavyoona abu kueleza ukweli kuhusu tukio hili, kwa uzoefu wangu, baada ya kukutana nao na kuzungumza nao jana, nimeamini kuwa hawapendi jambo hili litoke nje, yaani kwenye vyombo vya habari, hilo tumelizingatia, sasa watueleze kwa undani jambo hili lilivyotokea", Kanali Emilly alieleza.
"Kama ulivyosema, itakuwa fedheha iwapo tukio hili litarushwa kwenye vyombo vya habari, vinginevyo hakuna tunachoficha, ndio maana nikasema tumeibiwa, wezi wametumia teknolojia ya kisasa kabisa, hata hivyo mimi na mwenzangu tunakiri kuwa tamaa ya kupata utajiri zaidi imetuponza. Kama ambavyo nilivyotangulia kusema, watu hawa walijitambulisha kuwa wanatoka ubalozi wa Marekani na walifika kwangu wakidai kuwa wanatafuta mtu mwaminifu ili wamkabidhi hizo dola azisimamie wakati wa kusafishwa, na kwamba mtu waliyemuona ni mimi", alisema mzee Sadik.
"Uliwauliza, walikufahamu vipi?", nilimuuliza.
"Naam, niliwauliza wamenifahamu vipi, pia niliwauliza wanajuaje kuwa mimi ni mwaminifu katika masuala ya pesa, mmoja wao alisema amepata kusikia sifa zangu na ndiye aliyependekeza waje kwangu, mara moka nikayaamini maneno yake", alisema mzee Sadik.
Nikajiweka vizuri kwenye kiti ili niweze kusikia habari hii, maana kwa kiasi fulani ilianza kuusisimua mwili wangu, "Baada ya hapo nini kiliendelea?".
"Baada ya kuongea mambo kadhaa na watu hawa, nikiuliza maswali nao wakijibu, hatmaye walinidokeza kuwa baada ya tukio la wizi wa dola milioni mbili za Kimarekeni, lililotokea Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, usafirishaji wa dola, paundi na pesa zingine zinazoingizwa nchini Tanzania ulibadilishwa, sasa zinaingia kama karatasi halafu zinasafishwa kwa dawa maalumu ili zianze kutumika kama dola", alinyamaza kidogo ili kupisha swali, alipoona nimekaa kimya akaendelea.
"Nilihoji pia, ili kujuwa kama ni tukio hilo la wizi tu lililopelekea pesa zote zinazoingizwa nchini Tanzania kuchafuliwa, pia nilitaka kujuwa hali hiyo ni kwa Tanzania peke yake, watu hao ambao walikuwa wakiongea taratibu kwa kujiamini sana, walisema uhalifu umeongezeka sana duniani hivyo mamlaka za fedha zimeona hiyo ndiyo njia salama zaidi ya kusafirisha pesa", alieleza.
Aisee ni stori tamu sana, endelea nakusikiliza", nilisema huku Kanali Emilly akitabasamu.
"Baada ya majadiliano ya muda mrefu, maofisa hawa waliodai kuwa wanatoka Ubalozi, walitoa mfano wa karatasi kadhaa zikiwa na rangi nyeusi, wakadai kuwa hizo ni dola orijino ambazo huletwa nchini na baadaye kusafishwa kwa dawa maalumu ambayo walisema pamoja na kupatikana kwake kuwa vigumu, wao wanajua mahali pa kuipata na kazi hiyo ikafanyika vizuri. Una swali?", aliuliza huku akiniangalia usoni, macho yetu yalipokutana, alionekana wazi kuwa mwenye aibu.
"Teacher, karatasi anazoeleza mzee Sadik nimekuonyesha kabla hatujaanza mazungumzo", alisema Kanali Emilly nikatikisa kichwa kukubaliana naye.
"Sasa ilikuwaje ukaamini kuwa hizi karatasi ni dola?", nilimuuliza baada ya kusimama, nikazichukua zile karatasi alizonionyesha Kanali Emilly, nikamuonyesha, maana maelezo haya yaliniingia vizuri, nikasahau kama nilikuwa likizo.
"Lo, sijui shetani gani aliniingia, mwanzo sikuwaanini kabisa, nilipanga kupiga simu kuwajulisha polisi kuhusu watu hawa ili wakamatwe, lakini baadaye nilishawishika kuwaomba vitambulisho vyao, hakika vilikuwa vitambulisho vya ubalozi wa Marekani, nikaanza kuyaamini maneno yao, nikaingia kwenye mtego baada ya mmoja wa maofisa hawa kutoa dawa na kusafisha karatasi kadhaa ambazo ziligeuka kuwa dola halali kwa matumizi. Hakika nilianza kusadiki, baada ya kudai kuwa dawa waliyonayo ni kidogo haiwezi kusafisha zaidi ya karatasi ishirini", alinyamaza kidogo akachukua glasi yake ya juisi akanywa kiasi huku midomo yake ikimcheza mfano wa mtu aliyekutana na baridi kali.
"Teacher, nakuhakikishia kuwa, kazi ya kusafisha karatasi hizo na kuwa dola ilifanyika mbele ya macho yangu, nilifuatilia tukio hilo kwa umakini wa hali ya juu. Karatasi kumi ziliingizwa kwenye dawa nikiona, baada ya sekunde kadhaa zikatolewa zikiwa tayari zimebadilika na kuwa dola mia mia za Kimarekani, wakati huo boksi kadhaa zilikuwa kando zikiwa zimesheheni karatasi hizo, hakika nikauona utajiri mkubwa mbele yangu, nikajua sasa nimeukata", alisema mzee Sadik, alinyamaza kupisha kama kuna mtu mwenye swali, alipoona kimya akaeleza.
Baada ya karatasi hizo kusafishwa na kila moja ilikuwa dola mia za Kimarekani kuonekana, walinikabidhi, halafu wakaanza kusafisha karatasi ambazo walidai ni paundi za Uingereza ambazo pia zilipotakata zilikuwa paundi mia kila moja. Wakadai dawa hiyo imeisha nguvu, wanatafuta watu wa kusaidia ili karatasi hizo zisafishwe na kuwa dola. Wakanipatia dola zilizosafishwa ili niende sehemu ya kubadilishia pesa kuthibitishe kama ni dola halali, nikafanya hivyo, hakika zilikuwa dola halali kabisa, nikajiona mwenye bahati kuonana na watu hawa".
"Aisee, kweli hapo hakuna ujanja, lazima utaibiwa tu", nilimwambia akacheka kidogo huku akisisitiza kuwa huo ni wizi ambao si rahisi mtu kukwepa, labda uwe fukara. Na jamaa hawa hawamfuati mtu asiye na kitu.
"Tamaa ya kupata pesa nyingi imeniponza", alisema akitoa kitambaa cha jasho mfukoni akafuta machozi yaliyokuwa yakimtoka.
"Karatasi walizokuja nazo ofisini kwako na kudai kuwa ni dola ambazo hazijasafishwa, waliziacha kwako?". niliuliza.

"Yes, waliziacha karatasi hizo kwangu huku wakisisitiza kuwa nisitoe taarifa hii kwa mtu yeyote, wakadai kuwa wangerudi kesho yake mapema kuangalia kama nimebadili dola, ili tuangalie uwezekano wa kupata pesa za kununua dawa kwa ajili ya kusafisha karatasi zilizobaki, ambazo walidai iwapo zitasafishwa zote ni zaidi ya shilingi bilioni tano za Tanzania, nilifurahi sana", alisema mzee huyu.
"Kama ndivyo, mbona wewe umefaidika", nilimwambia.
"Hapana, nimeumia sana Teacher, waliporudi mara ya pili walinieleza kuwa karatasi hizo zina thamani kubwa sana, ni mapesa ya kigeni yanayosubiri kusafishwa, kwa hiyo waliniomba mimi kama mwenyeji wao niwatafutie mtu mwenye pesa ili tununue dawa na kusafisha karatasi hizo, ambazo wao walidai kuwa waliziiba ubalozini", anabainisha.
"Ndipo wewe ulipotoa pesa?", nilimuuliza.
"Hapana, kwa vile walinieleza kuwa dawa ya kusafisha karatasi hizi inauzwa kwa bei mbaya, nilimfuata mzee mwenzangu, Enock Nyanda, baada ya kumshawishi alikubali tushirikiane kutoa pesa ili dawa ipatikane, ndipo kazi ya kutafuta dawa ilipoanza".
"Hapo ndiyo patamu sasa, ehee?", niliteka masikio.
Baada ya utaratibu wa pesa kupatikana, maofiosa hawa kutoka ubalozi walituambia kuwa, sehemu ambayo tunaweza kupata dawa ni kwenye maabara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Walishauri kuwasiliana na Profesa waliyedai kuwa anahusika na maabara ya chuo, baada ya kuwasiliana naye kwa simu yake ya mkononi, alitupangia muda ya kwenda kumuona", alitulia kidogo, akaonesha hasira iliyokuwa katika nafsi yake, halafu akacheka.
""Watu hawa walijipanga vizuri", nilijisemea.
"Hakika, kwa mchezo huu walijipanga vizuri kuhakikisha wanafanikiwa", alirukia Kanali Emilly.
"Inaonyesha hivyo. Maana siku iliyofuata tulifika eneo la chuo kikuu, tukakutana na Profesa mmoja anaitwa Davis Magajimbo, kwa vile alikuwa ametuelekeza sehemu ya kumuona, Baada ya kumfahamisha kuwa tunahitaji dawa ya kusafisha dola, alitueleza kuwa dawa hiyo inauzwa bei mbaya na ili kuipata lazima zipatikane shilingi milioni mia moja za kitanzania", alisema, baada ya kutafakari kidogo akaendelea.
Kutokana na thamani ya dola na wingi wa karatasi zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili ya kusafishwa, tulikubali kutoa kiasi hicho cha pesa kwa Profesa, ambaye alitukabidhi dawa huku akidai kuwa dawa hii ni nyingi sana, akashauri kama ikibaki tutaitumia wakati mwingine. Haraka tuliwasiliana na maofisa wa ubalozi kuwajulisha kuwa dawa imepatikana, nao hawakuchelewa kufika".
"Walipofika ikawaje?", niliuliza.
"Kufika kwa maofisa hawa kulitupa faraja, walishauri dawa hiyo ihifadhiwe vizuri kwenye jokofu, ili kazi ya kusafisha dola kwa vile ni nzito ifanyike kesho yake mapema alfajiri, kwa madai kuwa kuna kazi nyingine wanaifanya wakati huo ili kesho yake wasiwe na ratiba nyingine", alisema mzee Enock ambaye alikuwa kimya kwa muda mrefu.
"Ah, jambo hili lilipangwa kwa ustadi wa hali ya juu, tulihifadhi dawa hii vizuri kama watu hawa walivyoagiza, siku ya pili walifika mapema alfajiri kama walivyoahidi, walinihimiza nitoe dawa ili kazi ya kusafisha dola ianze", alipofika hapo machozi yakaanza kumwagika.
"Usilie tafadhali, hii ni hali halisi ya dunia, unaweza kulala masikini ukaamka tajiri, ama ukalala tajiri ukaamka masikini, yote ni mipango ya Mungu", niliwaambia ili kuwatia moyo.
ITAENDELEA 0784296253
 

Bujibuji

JF-Expert Member
Feb 4, 2009
50,546
2,000
Kwa wale wapenzi wa riwaya karibuni sana. Nikiwa mdau wa mambo hizi nimeona nishee moja ya riwaya ambayo nimeikuta mahali lakini sijaitunga mimi jamani niwe mkweli. Nimeona si vibaya tuka share starehe na utamu kama huu na wanajukwaa...!! Ipo mwanzo mwisho, hapana kuishia kanisani, No arosto..!! Kama ilisharushwa humu mnambie nisije nikawa namtawaza mbwa..!! Ila sijawahi kuiona humu so far.


Mukuje na likes za kutosha etiii...!!!
Chukua 'like makinikia'

 

SHAMAC

JF-Expert Member
Feb 9, 2017
1,345
2,000
SURA YA TISA"Teacher, sasa tunawasaidiaje wazee hawa?", lilikuwa swali kutoka kwa Kanali Emilly. Kutokana na swali hili, nilitembea hatua tatu kutoka nilipokuwa nimesimama, halafu nikarejea tena kwenye kiti nilichokuwa nimeketi awali.

"Inategemea...", nilijibu kwa mkato,

Baada ya kutafakari kwa muda, huku tukiangaliana kama mabubu, nililazimika kumweleza Kanali Emilly kuhusu mkakati wangu wa kazi zilizokuwa mbele yangu.

"Afande..., kabla sikaingia kazini rasmi, naomba utambue kuwa kujiingiza katika jambo hili, ni sawa na kuanzisha vita, nasema hivi kwa sababu watu waliofanya uhalifu huu wana mtandao mkubwa mno. Hawa ndio wahusika wakubwa wa dawa za kulevya, ndio wahusika wa uhalifu wa kila aina. Swali langu ni kwamba, uko tayari kwa mapambano na watu hawa?", nilimuuliza.

"Potelea mbali, lolote liwe, dunia itatukumbuka kwa hili, tukilimaliza salama tutashukru, tukiishia njiani naamini wapo watakaokuja kuliendeleza", Kanali Emilly alisema huku akisimama kuonyesha msisitizo. "Niko tayari kabisa".

Nililazimika kumweleza Kanali Emilly, kuhusu shambulizi la jana usiku uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, akaonekana kushangazwa, nami nikatumia nafasi hiyo kumweleza jinsi nilivyojipanga kukabiliana na watu hawa, maana walikuwa wamenianza.

"Afande, kutokana na umuhimu wa jambo hili, nimelazimika kuwaita vijana wetu wawili, Luteni Claud Mwita kutoka Morogoro na Sajenti Julius Nyawaminza kutoka Zanzibar, hawa ni makomandoo wenye uwezo mzuri, bahati nzuri wako karibu na eneo hili. Hapa ofisini nimeamua kuwatumia Luteni Fred Libaba na Sajenti Peter Twite tu, nina sababu za kufanya hivyo", nilidokeza.

"Sababu gani hiyo Teacher, wakati idara yetu hapa inao vijana wenye uwezo mzuri tu, wangeweza kukusaidia kwa karibu zaidi, jambo hili linahitaji ushirikiano wenu", alishauri.

"Afande, nimelazimika kufanya hivi kwa sababu, sielewi ilibainika vipi kuwa nimesafiri, ilifahamika vipi kuwa niko kwenye ndege nikirejea Dar es salaam, na sijui nini kilisababisha hata watu hawa wakanishambulia baada ya kutoka kwenye ndege, hilo linanitia shaka", nilimwambia. "Hawa vijana tutawashirikisha kwa kazi nyingine, kuhusu hii watuache kwanza. Kama utapenda operesheni hii iwe na mafanikio utaniwia radhi kwa hilo".

"Umesomeka, hakuna ubishi katika hilo. Kuna la ziada?".

"Hapana", nilimwambia, baada ya ukimya wa sekunde kadhaa nilimwambia kuhusu ujio wa shemeji yangu Mama Feka. "Afande, kama ulivyosikia nikiongea na simu, shemeji yangu tunayeshibana sana yuko njiani kuja Dar es Salaam, pamoja na kwamba anakuja kwenye mahafari ya chuo kikuu, kwa vyovyote vile atapenda kufikia kwangu, kama unavyojua familia yangu nimeihamisha kabisa ili sasa vita vianze, itakuwa vita ya kufa au kupona", nilisema kwa hasira.

"Sasa kuhusu huyu shemeji yako utafanyaje, maana nyumbani kwako sasa si sehemu salama kama ulivyosema?", alihoji Kanali Emilly.

"Nafikiria kumshirikisha katika vita hivi, maana ujio wake unaweza kuwa faida au hasara, lolote laweza kutokea", nilimwambia Kanali Emilly akaonekana kunishangaa.

"Kwanini umeamua kufanya hivyo Teacher?. Huyu shemeji yako ataweza kumudu hali ngumu ya vita ambavyo hatujui nani adui na rafiki?".

Nilitumia dakika mbili tatu kumweleza Kanali Emilly, kuhusu uhodari wa Mama Feka. Nilimweleza jinsi mama huyu alivyo na msimamo imara katika kutekeleza majukumu yake, nilieleza historia yake fupi, kuwa kabla ya kujiunga na chuo kikuu huria cha Tanzania, alifanya kazi kama mwalimu wa michezo katika shule kadhaa, lakini kabla ya hapo alikuwa ameshiriki mafunzo mbalimbali ya kijeshi kwa mjibu wa sheria.

"Kuhusu hilo nakuachia utaamua mwenyewe. sasa umepanga kumtumiaje huyo shemeji yako, au ni siri yako?".

"Hapana, ndiyo maana nikakushirikisha kuhusu jambo hili. Afande, Mama Feka ni mwanamke mrembo sana, ni mwanamke ambaye anaweza kumshawishi mwanaume yeyote akaingia katika himaya yake. Labda nikudokeze jambo moja".

"Itakuwa vizuri".

"Hapa Dar es Salaam, kuna mtandao wa uhalifu ukiongozwa na mzungu mmoja aitwae Carlos Dimera, kama unavyojua taratibu na sheria za nchi yetu huwezi kumkamata mtu bila kuwa na ushahidi wa kutosha. Taarifa nilizonazo ni kwamba huyu Carlos anapenda sana wanawake warembo, kwa Mama Feka ataingia, akiingia amekwisha", nilifafanua.

"Ni mpango mzuri Teacher, tufanye kila iwezekanavyo watu hawa wakamatwe na ushahidi, hii itasaidia kuwafikisha mahakamani, nikutakie kazi njema, tuwasiliane kila hatua utakayofikia, ukihitaji msaada wa aina yoyote usisite kunijulisha, kuanzia sasa ofisi hii itaacha mambo mengine yote ili tushughulikie jambo hili", Kanali Emilly alisema.

"Nikutakie kazi njema, tuombe mungu ndiye mwenye dhamana ya uhai wetu, lolote likitokea itakuwa kwa mapenzi yake, lakini pia tuko tayari kufa kutetea wengi", nilisema huku tukisimama. Tukashikana mikono.

Muda ulikuwa umeyoyoma sana, nilitoka ofisini kwa Kanali Emilly, huku mawazo mengi yakiwa yamenizonga juu ya jambo hili, nilijiuliza kuhusu mbinu walizotumia watu hawa, kiasi fulani nilijikuta nikicheka mwenyewe na kuwasifu kwa jinsi walivyoweza kufanikisha mpango wao wa wizi na kuwaacha wazee hao kwenye mataa. Nilifungua mlango nikatokea mapokezi. Linnah aliponiona akasimama.

"Pole sana bosi wangu, naona kikao kilikuwa kirefu kupita maelezo", alisema, mama huyu askari mwenye cheo cha Staff Sajenti, lakini aliheshimiwa sana kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka.

"Ndiyo mambo ya kazi. Sikiliza Linnah, naomba nisaidie kazi moja muhimu sana, niitie Sajenti Peter Twite aje ofisini kwangu haraka, ikiwezekana aingie kwa siri. mtu zaidi yako asijue", niliagiza halafu nikaingia ofisini kwangu.

Nilipanga kumtumia Peter kufanya kazi maalumu, kazi ya kimafia, ambayo ingetusaidia kumaliza jambo hili haraka. Baada ya muda mfupi Peter aliingia ofisini kwangu.

"Jambo Afande?" alinisalimia.

"Jambo. Habari ya toka usiku wa jana, Peter ujumbe wako ulinisaidia sana, maana sikujua lolote litatokea, sijui ingekuwaje?", nilimuuliza.

Peter akatumia muda huo kueleza mambo yalivyokuwa uwanja wa ndege, akaeleza jinsi alifika uwanja wa Julius Nyerere kwa ajili ya kunipokea, uwanja wa ndege alikutana na watu ambao aliwatilia shaka, kutokana na uzoefu wake wa kazi baada ya kuwawafanyia utafiti alibaini kuwa walikuwa katika mpango wa kumsubiri mtu.

"Ilikuwa vigumu saba kuwabaini, baada ya kutulia na kusoma mazingira ya uwanja wa ndege, nilibaini magari mawili aina ya BMW, moja likiwa limeegeshwa karibu kabisa na sehemu ya kutokea abiria na lingine liliegeshwa sehemu ya kutokea magari. Ulipoanza kutoka wewe watu wawili walilikimbilia gari la mbele, ambalo lilianza kuondoka, lingine likasuri gari ulilopanda liondoke ndipo wao walifuate gari hilo kwa nyuma. Haraka nikakutumia ujumbe wa tahadhari".

"Ama kweli ulifanya kazi ya ziada, sikuwa na mashaka kabisa, bila wewe pengine siku ya leo ingekuwa ya maombolezo kwangu, asante Peter", nilimshika mkono.

"Usijali mkuu, haya ni matunda yako, kumbuka wewe ndiye uliyenifundisha haya, ulinifundisha jinsi ya kunusa harufu mfano wa mbwa, Nikushukuru kwa kunifikisha hapa", alisema Pete.

"Tuachene na hilo, sasa nataka ufanye kazi moja ya muhimu sana, nimemwambia Mzee Emilly kuwa mapambano yameanza, ni mapambano makali ambayo yafaa tuyapigane sasa, hakuna jinsi, kazi yako tafuta vijana watano, wawe raia wa kawaida tu, lakini waendesha bodaboda jijini, ingia nao mkataba, lakini wapatie pamit na alama ili wasisumbuliwe na migambo. Pikipiki zao waziegeshe kwenye barabara kubwa tano za jiji. Yaani Morogoro road, Ali Hassan Mwinyi, Nyerere road, Kilwa road na Bibi Titi Mohamed, ukimaliza hilo tuwasiliane nitakuelekeza kazi nyingine", niliagiza.

"Nitalifanya hilo haraka sana bosi", alisema Peter.

"Ok, usikose kunijulisha, kumbuka kuwafahamisha kuhusu matumizi ya pikipiki hizo, maana tumepanga kuwatumia wao katika kazi fulani, isifike wakati wakatushangaa, kazi kwako".

Niliwasiliana na Luteni Claud Mwita kumuuliza kama uwepo wake eneo hilo umebaini nini akanidokeza kuwa watu ni wengi, pamoja na kufanikiwa kufahamiana na Sajenti Julius Nyawaminza, wameimalisha ulinzi katika eneo hilo.

Simba, Nyati na Chui, wao walikuwa eneo hilo wakitembea hatua kadhaa kwenda upande mwingine na kurejea kwenye pointi huku silaha zao ndogo, zikiwa tayari zimeondolewa usalama. Risasi zikiwa chemba tayari kwa lolote.

ITAENDELEA 0784296253
 

SHAMAC

JF-Expert Member
Feb 9, 2017
1,345
2,000
SEHEMU YA KUMIBaada ya kupanga mipango yangu, niliyoofanya kimya kimya, nilifungua mkoba wangu mdogo, nikatoa kamba niliyoinunua Kariakoo. Ilikaribia kuwa saa moja ya usiku, giza lilianza kuifukuza nuru, niliwasiliana na wenzangu. Claud Mwita, Julius Nyawaminza na Fred Libaba nikawaomba tuonane kwenye Mghahawa wa YWCA uliopo hapo Posta Mpya kwa ajili ya chakula cha jioni.

Pamoja na kwamba Mghahawa huu uko karibu kabisa na kituo cha Daladala cha Posta Mpya, wengi hawakupajua, lakini pia niliwahadharisha wenzangu kuwa makini. Nilishauri kila mmoja achukua chakula na atumie meza tofauti, baada ya hapo tutakuwa na mazungumzo yetu binafsi nje ya eneo hilo.

Taratibu nilifungua mlango wa ofisi yangu nikachungulia kwa nje, nilitafuta sehemu ya siri nikazificha funguo za gari, halafu nikawasiliana na David, mmoja wa vijana wanaofanya kazi karibu yangu, nikamfahamisha mahali nilikohifadhi funguo hizo ili azichukue na kuipeleka gari kwa aliyeniazima, rafiki yangu Edgar.

Hapakuwa na dalili yoyote ya kuwa na mtu, hata Linnah alikuwa ametoka na kufunga ofisi yake, nilitoka haraka na kuivamia lifti iliyonishusha ghorofa ya kwanza. Nilitembea haraka hadi kwenye maegesho ya magari, sikutaka kupoteza muda, nilichungulia upande wa pili lilipo jengo la ofisi za benki ya CRDB. Baada ya kujiridhisha kuwa hakukuwa na mlinzi eneo hilo wakati huo, nikairejesha kamba yangu kwenye mkoba, baada ya kujiridhisha kuwa hakuna kikwazo cha kunisumbua.

Niliangalia nyuma na upande wangu wa kulia na kushoto, sikumuona mtu, lakini kwa vile jengo hili linalindwa kwa kamera maalumu za usalama, nililazimika kufanya jambo moja ili kamera hizo zisinione. Nilisogea kwenye kivuli, nyuma ya magari kadhaa yaliyoegeshwa hapa, nikatumia nafasi hiyo kujirusha chini, upande wa jengo la CRDB. Haikuwa shida kwangu kuruka sehemu kama hiyo.

Lango la kutokea bado lilikuwa wazi na kwa vile kuna ofisi zingine juu ya ghorofa hili, nilitoka na kuwapita walinzi na baadhi ya askari polisi waliokuwa kwenye kibanda chao cha ulinzi. Nielekea shell ya Gapco, nikakavuka barabara na kuingia YWCA, Wenzangu wote walikuwa wamefika na tayari walikuwa wamepata chakula.

Tulisalimiana na kupeana ishara, kwa vile Mghahawa huu ni wa kujihudumia mwenyewe, na njaa ilikuwa karibu iniue nilielekea kwenye dirisha la huduma, nikaagiza chakula, ambacho nilikula haraka haraka, ili kwenda sawa na wenzangu, ambao kila mmoja alikuwa na hamsini zake.

Wakati huo Carlos Dimera alikuwa akiwasiliana na wakala wa kusafirisha mizigo kutoka Bogota, nchini Corombia, wakala akimjulisha kuwa baada ya masaa ishirini na nne mzigo huo ambao ni dawa za kulevya, utakuwa umewasili kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

"Tunahitaji maelezo kutoka kwenu, hivi tunavyoongea hapa shehena ya dawa za kulevya imetua salama katika uwanja wa ndege Addis Ababa, nchini Ethiopia. Tumelazimika kupitishia mzigo nchini Ethiopia badala ya Ouagadougou, nchini Burkina Faso kama ilivyokuwa awali kwa sababu za usalama, taratibu zote za mzigo kuondoka Ethiopia kesho zimekamilika, kazi kwenu, vipi hali ya usalama huko?", Carlos Dimera aliulizwa.

"Dar es Salaam, Tanzania hali si mbaya sana, japokuwa kuna mawingu na mvua za hapa na pale, lakini haziwezi kutuzuia kuendelea na majukumu yetu. Kuna wingu moja limetanda angani kuashiria mvua, lakini wataalamu wa hali ya hewa hapa Tanzania wanasema wingu hilo halina madhara, waganga wako kazini kuhakikisha wingu hilo halidondoshi hata tone moja la maji, kuhusu hali ya uwanja wa ndege wa Dar es Salaam ni nzuri sana, tunausubiri", alieleza Carlos Dimera kwa simu ya mkononi.

"Oke, lakini kuweni makini sana katika jambo hili, nasikia serikali ya Tanzania sasa hailali?."

"Kuhusu hilo ondoa shaka kaka, niko na mtandao unaoeleweka, mtandao wa vijana wa mjini ambao nimewafundisha mbinu za kila aina, hata hili wingu lililotanda angani mwisho wake wa kutanda na kuleta hofu ni leo, wingu hili halitakuwepo tena", alisisitiza Carlos.

Baada ya Carlos Dimera kumaliza kuongea na simu hiyo, aliingiwa na hofu kidogo, alisimama akatembea hatua mbili, halafu akajiuliza maswali kadhaa, akainua simu yake ya mkononi na kuongea na Nombo.

"Uko wapi Mr. Nombo?", alihoji Carlos Dimera.

"Niko katikati ya mji bosi, nimelazimika kuja huku kuongeza nguvu kwa vijana, kazi hii lazima iishe leo bosi, kuna habari mpya?", Nombo alihoji.

"Hakuna habari mpya, isipokuwa wakala wa kusafirisha mizigo anauliza, hatua gani tumefikia, mzigo umewasili salama Addis Ababa, Ethiopia, yamebaki masaa ishirini na nne tu mzigo uwasili Dar es Salaam, na wingu bado limetanda angani, unadhani kuna uwezekano wa kuliondoa?", Carlos Dimera aliuliza.

"Tulia bosi, tumuombe Mungu atasaidia, maana uwezekano ni mkubwa mno, kwa vile hujafika kwenye uwanja wa mapambano, ungeshuhudia adui alivyowekwa kati, hakika jengo lote la Benjamin Mkapa liko chini ya usalama wetu, kila anayetoka na kuingia anaonekana, kuhusu hilo usijali, leo ndiyo mwisho wa wingu hili, labda utokee muujiza gani".

"Niwatakie kazi njema, jitahidini bwana jambo hili liishe mapema leo, vinginevyo nitume kikosi kazi?, hawa jamaa zetu wapo tu wanasubiri kazi kama hizi, mkishindwa semeni", aliuliza Carlos.

"Hakuna sababu, mapambano ya mchana yangeleta shida kidogo, maana watu walikuwa wengi eneo hili, lakini sasa hali iko shwari, hili giza litatusaidia pia. Kunywa, kula ukiamini kuwa kazi hii imekwisha", Nombo alieleza, Carlos akapata faraja na matumaini.

ITAENDELEA 0784296253
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom