NJAMA
SURA YA SABA
BINTI TANZANIA
III
Ilikuwa yapata saa kumi na mbili wakati dereva wa
teksi aliponishusha hatua chache kabla ya kufika
kwenye mzunguko wa Mtaa wa Jamhuri na Zanaki.
"Hapo hapo pananitosha", nilimweleza huku
nikimpa shilingi ishirini kisha nikatelemka.
Niliangalia kwenye maegesho ya mtaa huu wa
Jamhuri nikaiona gari ya Zabibu. Ilikuwa gari ya
rangi ya kijani ambayo haikuiva sana, na ilikuwa ni
aina ya Ford Mustang muundo wa kisasa. Kama
umeshaiona Ford Mustang zilizoundwa vizuri basi
hii ilikuwa mojawapo. Hata mimi niliipenda kwa
umbo lake maana ilikuwa na milango miwili. Yaani
'Ford Mustang Sports Car', kama wanavyoiita
wenyewe walioitengeneza.
Kule kuona gari hii kulinihakikishia kuwa Zabibu
alikuwepo nyumbani, niliangalia jengo, nikaangaza
huku na huku kuona kama kuna mtu ananifuata,
nikaona hakuna. Kila mtu alionekana kuwa na
hamsini zake. Basi mimi Willy nilijipenyeza kwenye
lango linaloelekea kwenye ngazi za jengo hili.
Nilipofikia ngazi nilianza kupanda taratibu kama
mtu anayejua anapokwenda. Nilipanda mpaka orofa
ya tatu, na nyumba iliyokuwa inatazamana na
ngazi hizi ilikuwa namba 1a na nikajua 7a itakuwa
mkono wa kulia hivyo nikafuatia taratibu.
Kwa sababu giza lilikuwa linaingia nyumba zingine
zilikuwa zimewasha taa na zingine zikiwa giza
kuonyesha wenye nyumba walikuwa bado
hawajafika. Nyumba namba 5a na 6a zilikuwa giza
ila 7a ilikuwa inawaka taa sebuleni. Nilitembea
taratibu bila kupiga kelele mpaka kwenye mwisho
wa namba 6a, niliposikia sauti ya msichana inapiga
kelele ndani ya namba 7a. Harafu nikasikia sauti
ya mwanaume.
"Mimi nisingependa kukuua Zabibu maana mimi
nafurahia uumbaji wa Mungu mzuri aliokuumba
lakini mimi nimeamriwa nikuue hivyo sina njia.
Nisipokuua wewe, mimi nitauawa. Hivyo huna haja
ya kupiga kelele, kufa hakika utakufa".
"Kwani mimi nimekosa nini masikini?", msichana
aliuliza.
"Hata mimi sijui, haya kwa...".
Mimi nilikuwa nimejivuta na kuwa sawasawa na
mlango wa hii nyumba, hivyo nilisikia mazungumzo
haya. Niliona nikichelewa msichana huyu anaweza
kuuawa. Basi nilitudi nyuma, bastola mkononi,
niliurukia ule mlango na kuupiga teke ukafunguka.
Hapo hapo mimi nikatumbukia ndani nikitanguliza
kichwa chini lakini nikafyatua bastola na kumpata
yule kijana niliyemuona ameshika kisu chenye
mpini mwekundu. Ile risasi ilikuwa haikumpata
vizuri hivi alisimama wakati na mimi
nimeshasimama yakaanza masumbwi. Alitupa
konde moja likanikosa mimi nikampa shoto langu
lililompata shingoni akaenda chini na hakusimama
tena.
Mambo haya yalitokea kwa muda mfupi sana.
Zabibu alikuwa amepigwa na butwaa kiasi cha
kwamba yule mtu alipoanguka chini na yeye
akaanguka juu ya kochi na kuzirai. Nilienda
kumwangalia yule mtu pale chini, sikuwa na haja
hata ya kumgusa ili nijue kama amekufa. Niliona
kulikuwa na barafu pale sebuleni, nikaifungua
nikatoa chupa ya maji baridi nikammiminia Zabibu
naye akashituka.
"Kweli huyu Zazibu alikuwa ndiye Binti Tanzania.
Mimi nimeona warembo katika nchi hii, lakini huyu
alikuwa ni zaidi. Ukiwa unaamini kuwa kuna
binadamu wengine hushushwa moja kwa moja toka
mbinguni, basi Zabibu alikuwa mmoja wao, kwani
mpaka sasa siamini kama msichana huyu alizaliwa
na binadamu. Ingawaje haiwezekani kuamini kuwa
mtu anaweza kutelemshwa toka mbinguni, lakini
ukimwona Zabibu wewe mwenyewe utaona
uwezekano. Maana hata mimi niliona inawezekana
kwa huyu kiumbe wa binadamu alikuwa ameumbwa
bila kasoro. Palipo ukweli lazima tuseme;
mwenzetu alikuwa na uzuri sio kifani. Mcho yake
manene ya mviringo yaliyozungukwa na nyusi
zenye rutuba yalifunguka na kuniangalia mimi.
"Umetoka wapi?", aliuliza kwa sauti nyororo
iliyotoboa rohoni mwangu kama miali ya moto.
"Nimekuja kukuokoa".
"Kama wewe si mmoja wao umejuaje kuwa
amekuja kuniua?".
"Kama mimi ni mmoja wao kwa nini nimwue wakati
anataka kukuua?".
"Ndicho kinachonishangaza".
"Basi mimi si mmoja wao, mimi ni rafiki yako.
Kama una akili timamu tuondoke hapa chumbani
kwako maana kinanuka mauti".
"Sijui kwa nini naona kama ninakuamini".
"Kwa sababu ndio jambo la busara".
"Haya nichukue, nitoe hapa, yule mtu kweli
angeniua. Huenda lazima nikushukuru, asante
sana?".
"Bila asante, msichana kama wewe una haki ya
kuokolewa, huna haja ya kushukuru, hiyo ni haki
yako".
"Na huyu mtu tutamwacha humu?".
"Nitafanya mipango aondolewe, simu iko wapi?".
"Chumbani".
Aliniongoza chumbani, nikapigaa simu ofisini
nikamkuta Eddy nikamweleza kwa kifupi, kisha
nikamwambia afanye mpango mtu huyu aondolewe
hapa. Eddy akasema atatekeleza.
"Wewe ni polisi?", Zabibu aliuliza.
"Hapana".
'Sasa wewe ni nani?".
"Mimi ni mtu ninayesaidia warembo kama wewe".
Nilimjengea tabasamu babu kubwa kisha nilimshika
mkono tukazima taa, nakurudisha mlango, halafu
tukaondoka. Nilipata teksi pale chini, tukapanda na
kumwelekeza dereva nyumbani kwangu.
"Tunakwenda wapi?", Zabibu aliuliza.
"Nyumbani kwangu, unaonaje?".
"Nakuona wewe ni mtu wa ajabu ajabu tu,
usingekuwa umeniokoa nisingekuamini hata
chembe!.
Nilikuwa nimeingia na mashaka makubwa kwenda
moja kwa moja nyumbani kwangu. Nilikuwa sijui
kwa nini, hivyo nikabadili mawazo na kumwelekeza
teksi dereva twende Ocean Road ambako ndiko
Eddy alikuwa akikaa. Nilikuwa nina ufunguo mmoja
wa nyumba yake kwa ajili ya nyakati kama hizi.
Tulikwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa
Eddy baada ya kumwelekeza dereva nyumba.
Nilimlipa dereva teksi pesa zake, halafu
tukatelemka. Nilifungua mlango kisha nikawasha
taa.
"Karibu ndani bibie".
Asante sana".
Nilikwenda kwenye barafu nikaifungua.
"Sijui utakunywa nini?".
"Baada ya vituko vilivyotokea nafikiri whiski na
soda kali vitanifaa".
Nilichukua chupa ya whiski na soda kali halafu
nikaendea glasi na kumimina kwenye glasi mbili ya
Zabibu na ya kwangu halafu tukainua glasi zetu.
"Na tunywe kwa maisha yako marefu mrembo",
nilisema.
"Na tunywe", alijibu kisha akanywa whiski ile
haraka haraka.
Mimi nilikwenda kwenye simu nikapiga tena ofisini
nikampata Eddy. Nilimpasha habari kuwa mimi na
huyu mrembo Zabibu tulikuwa nyumbani kwake. Na
yeye vile vile akanieleza juu ya kazi niliyokuwa
nimemuagiza; vijana walikuwa wamempigia simu
kuwa tayari walikuwa wameshaifanya.
Nilimpongeza kwa jinsi kazi yake alivyokuwa
anaifanya haraka kwa juhudi na maarifa.
"Nafikiri kwanza itabidi tufahamiane", nilimweleza
Zabibu.
"Hasa ndilo litakuwa jambo la maana", alijibu.
"Mimi naitwa Willya Gamba, sijui wewe mwenzangu
unaitwa nani?".
"Mimi naitwa Zabibu Abeid".
"Lo kweli aliyekuwa jina la Zabibu alijua kweli,
kwani mimi naamini umtamu kama Zabibu".
"Ndio unataka kusemaje?".
"Nataka kusema wewe ni msichana mrembo
ambaye sijawahi kumwona, na bila shaka aliyekuwa
jina la Zabibu alijua utakuwa mtamu kama Zabibu".
"Usinivike kilemba cha ukoka. Kijana nadhifu
mwenye sura nzuri na vituko vingi namna hii,
haiwezekani kuwa haujamwona msichana mrembo
kunizidi".
"Amini usiamini".
"Asante, lakini hata mimi leo nimemwona mvulana
wa kipimo changu, sijui ulikuwa umejificha wapi mji
huu hata nisikuone?".
"Mimi nilikuwepo nimejaa tele hapa mjini, lakini
najua ingekuwa vigumu kuniona maana George Kiki
alikuwa amekuganda kama kupe".
Pale pale sura yake iligeuka akainua macho yake
marembo kunitazama machoni. Mimi nikamjengea
tabasamu la sheria yake, Zabibu alionekana
alikuwa amechanganyikiwa mawazo.
"Unajua nini juu ya George?".
"Hakuna haja ya kuzungushana sana, nafikiri
inabidi sasa tuelezane ukweli. Na kabla
hatujaendelea mbali ningependa kukuuliza lini
umeonana na Kiki kwa mara ya mwisho".
Kwa kutokana na uzito wa sura yangu, Zabibu
alilegeza sura yake kisha akajibu kwa sauti
nyororo.
"Siku nne zilizopita, alisema atakwenda safari
Botswana na atarudi baada ya wiki tatu".
"Na hauna habari nyingine yoyote kuhusu yeye?".
"Sina, kwani kumetokea nini?".
"Kwani yule mtu aliyetaka kukuua alikuwa
amekueleza nini?".
"Hata, alinieleza tu kuwa alikuwa ametumwa kuja
kuniua ingawaje yeye hakutaka lakini alikuwa
amelazimishwa. Hakunieleza kabisa sababu.
"Nakuomba uwe na roho ngumu, rafiki yako George
Kiki ameuawa jana. Maiti yake ilikutwa chumbani
mwake ikiwa imechomwa kisu chenye mpini
mwekundu".
Nilitoa kisu nilichokuwa nimekiokota nyumbani kwa
Zabibu kabla hatujaondoka.
"Na watu wale wale waliomwua ndio walikuwa
wanakuja kukumalizia wewe".
Zabibu alibubujikwa machozi na kidogo azirai tena.
"Lazima ujitulize kwa sababu mimi niko hapa
kupeleleza mauaji ya mpenzi wako".
"Mimi nilijua tu wewe ni Polisi. Sura yako na
namna ulivyoingia chumbani kwangu sijapata
kuona kwa macho ila ndani ya sinema tu. Zile
sinema za kijasusi".
"Mimi si polisi bali ni mpelelezi. Huenda polisi nao
wakaja kufanya upelelezi wao, lakini mimi bahati
nimewahi na kukuokoa huenda wao wangefika
wakati wewe umekwisha kuwa maiti".
"Una maana gani kusema wewe ni mpelelezi wala
si polisi?".
"Mimi ni mpelelezi wa siri kama umewahi kusikia
watu kama hao".
Macho ya Zabibu yakapanuka.
"Usije ukawa wewe ndiye mtu ambaye huwa
tunasoma habari zake kwenye magazeti
akipambana na majasusi mbali mbali wanaofanya
maovu dhidi ya Afrika".
"Ndio mimi".
Zabibu aliruka pale alipokaa akaja katibu na mimi.
"Ooh! Mungu ni bahati gani kuonana na mtu kama
wewe maana mimi nilikuwa nafikiri ni maneno ya
uzushi tu ya magazeti maana walikuwa hata
hawatoi jina. Kila mara ukisoma unaona tu vijana
wa Afrika wakiongozwa na mpelelezi mashuhuri
kutoka Tanzania wamefaulu katika kuwateketeza
majasusi ya mabeberu yaliyokuwa yanatenda
mambo maovu dhidi ya Afrika. Nitawaeleza rafiki
zangu kuwa ni kweli huyu mtu yupo na mimi
nimeonana naye".
"Halitakuwa jambo la busara, tafadhali fanya hii
iwe siri kati yangu na wewe, nimekueleza tu kwa
sababu unaweza kunisaidia katika upelelezi wangu
juu ya tukio la kutisha lililotokea hapa mjini siku
chache zilizopita".
"Ahaa nimeelewa tumesikia kwenye maredio ya
nchi za nje, kuwa silaha kali za wapigania uhuru
zimeibiwa kwenye bandari ya Dar es Salaam".
"Basi umebashiri sawa".
"Sasa George ana uhusiano gani na tukio hili?".
"Ndio sababu tumekuja kukuona, huenda ukajibu
maswali yangu nitaweza kuambulia jambo lolote
linalomwunganisha Kiki na tukio hili".
"Niko tayari kukusadia, kwanza kwa sababu
umeniokoa, pili kwa sababu unapeleleza kifo cha
mpenzi wangu na tatu nafikiri wewe ni kijana
mwenye kupendeka".
"Asante, swali langu la kwanza nilitaka kujua kama
ulikuwa unajua Kiki ni mtu wa Afrika Kusini?".
"Nilikuwa najua".
"Alikwambia alikuwa akifanya kazi gani?".
"Alisema yeye ni mwakilishi wa chama cha SANP
katika Kamati ya Ukombozi ya OAU".
Nilishangazwa na jibu hili lakini sikuonyesha.
"Kwa hiyo mara nyingi alipokuwa anakuja kwako
alikuwa akiandamana na wanachama wenzake wa
SANP?".
"Hapana, George alikuwa mtu wa pekee, huenda
ndio sababu nilimpenda. Alikuwa kila siku
ananiambia kama ninataka kuepukana na matatizo
nisizoeane na watu wengi. Na yeye kweli alikuwa
hakuzoeana na watu. ila alikuwa na marafiki wawili
tu. Ndugu Ray Sikazwe, rais wa SANP na Patlako
Shuta ambaye ni ofisa mkubwa katika SANP.
Sikumwona na mtu mwingine. Oh, kidogo nisahau,
vile vile walikuwa na rafikio yao mwingine Mzungu
ambaye George alifahamishwa kwake na Sembuche
na mwenzake Shuta. Na hata gari nililo nalo,
George aliuziwa na Mzungu huyu. Kwa vile yeye
alikuwa hapendelei gari kwani alikuwa anatumia
gari la ofisini alinipa mimi".
Kwa mara ya kwanza niliona mwanga kwa mbali,
na nikajua kwa nini msichana huyu alitakiwa
auawe. Nilijivunia bahati yangu kuwahi kabla
hajauawa.
"Unaweza kujua Mzungu huyu anafanya kazi
gani?".
"Lo! hawa ndio wenye lile kampuni kubwa lililo na
makampuni kadha wa kadha katika nchi nyingi za
kiafrika yaani EUROAFRO Limited. Na huyu Mzungu
ndiye mwakilishi wa kampuni hilo hapa akiangalia
akiangalia makampuni yake madogomadogo
yaliyoko hapa".
Kapuni hili EUROAFRO Limited lilikuwa kampuni
kubwa la kibepari lililokuwa na hisa nyingi katika
makampuni katika nchi nyingi za Afrika. Kirefu
chake kilikuwa EUROPE - AFRIKA COMPANY.
Uhusiano huu kati ya wanachama wa chahama cha
wapigania uhuru na kampuni ya kibepari ulinishinda
kuelewa.
"Kwa hiyo unasema huyu Sikazwe na Shuta
walikuwa marafiki wa karibu sana wa Kiki
"Ndiyo, hao ndio alikuwa anatembea nao mara kwa
mara na vile vile walikuwa wanajuja kumwona au
kumchukua pale kwangu mara kwa mara. Lakini
zaidi ya watu hawa wawili na yule Mzungu, George
hakuwa na rafiki mwingine".
"Huyu Mzungu unaweza kumkumbuka jina?".
"Ndiyo anaitwa Tony Harrison".
"Hawa marafiki wa Kiki uliweza kuzoeana nao?".
"Kusema kweli, Shuta na yule Mzungu walikuwa
wananiheshimu kiasi cha kutosha lakini Sikazwe
alikuwa wa ovyo sana. Amewahi kunitongoza mara
nyingi na kunitaka nimwache George. Kwanza
alikuwa anajivuna kuwa yeye ni Rais wa Chama na
George alikuwa mtu mdogo tu, na kwamba
msichana kama mimi sikufaa kutembea na George
ila mtu kama yeye. Mimi nilimponda na
kumwambia cheo na pesa havileti mapenzi, ila mtu
anampenda mtu kwa vile alivyo, maana mtu na mtu
ndio wanapendana".
Lakini nakwambia uso wa msichana huyu
unapoonyesha sura ya haya ndipo uzuri wake
unapozidi. Ingekuwa wewe usingevumilia lakini mie
nilipiga moyo konde na kuendelea na kazi. Nilifikiria
swali jingine nikaona nimepata maelezo ya kutosha
ila nikaamua nimweke zabibu chini ya ulinzi wangu
mpaka hapo baadaye.
Nilikuwa bado nafikiri hivi wakati tuliposikia gari
linapiga breki mbele ya nyumba. Nilitoa bastola
yangu tayari. Mlango ulipofunguliwa na Eddy
akakingia.
"Bosi, twende haraka Veronika amenipigia simu
anasema yuko katika matatizo. Nimekuja sababu
nilijua huna gari", Eddy alisema huku akitweta.
"Oke Zabibu, subiri hapa tutarudi sasa hivi".
Nilifungua mlango kabla Zabibu hajasema neno
lolote.
ITAENDELEA