RIWAYA: Mtutu wa Bunduki (1 - 3)

*****
MVUA KUBWA YA MASIKA iliyokuwa ikiendelea kunyesha ilikuwa imesababisha uharibifu mkubwa wa barabara ile. Kuna baadhi ya maeneo madaraja madogo yalikuwa yamesombwa na mafuriko na kuacha madimbwi makubwa ya maji na makorongo yenye utelezi mkali. Kuna baadhi ya maeneo kwenye barabara ile tulikabiliana na takataka nyingi za msituni zilizosombwa kutoka milimani, maporomoko ya udongo na magogo yaliyosombwa na mafuriko. Kwa kweli safari ilikuwa imetawaliwa na majuto na vilio vya hapa na pale kufuatia kumbukumbu ya matukio ya mauaji yaliyotekelezwa na wale wanajeshi watekaji kule msituni tulipotoka.
Hata hivyo sikusumbuka sana na kumbukumbu ile mbaya badala yake akili yangu ilikuwa imezama katika tafakuri juu ya hali ya mambo itakavyokuwa kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika pale Liberia. Lipo jambo moja lililonitatiza na kuisumbua sana akili yangu. Ni nani aliyewapasha habari wanajeshi wale watekaji kuwa tungepita barabara ile hadi wakafanikiwa kuandaa mtego ule hatari wa kutunasa?.
“Fuata barabara ya upande wa kushoto”. Mariama ambaye alikuwa ameketi kando yangu akanizindua na kuyarudisha mawazo yangu mle ndani ya gari. Tulikuwa tumefika eneo la njia panda, barabara moja ikielekea upande wa kushoto na nyingine upande wa kulia katikati ya msitu mnene. Kulikuwa na kibao elekezi kikielekeza upande wa kushoto kwa maelezo ya Gissie 10 Miles Ahead. Nikapunguza mwendo na kuingia kushoto.
“Baada ya kupanda mlima na kushuka mteremko mkali upande wa kushoto utaingia barabara ya kwanza. Tumekaribia kufika Tibba”. Mariama akanitahadharisha. Sikutia neno badala yake nikachochea mwendo na mbele kidogo nikauona mlima na kuanza kuupanda na wakati tukishuka mteremko nikagundua kuwa eneo lile la nyuma ya mlima lilikuwa limetawaliwa na giza zito sana pasipo dalili zozote za makazi ya watu na hali ile ikanishangaza sana. Chini ya mlima ule baada ya kushuka mteremko mkali nikaiona barabara inayochepuka kuingia msituni upande wa kushoto na kabla Mariama hajatia neno nikachepuka na kuifuata barabara ile nikikatisha kwenye uvungu wa matawi makubwa ya miti kabla ya kuingia kwenye uwanda wa shamba kubwa la miwa na migomba.
Kiasi cha umbali wa maili mbili hatimaye barabara ile ikatufikisha mbele ya nyumba moja kubwa ya matofali ya kuchoma yenye uzio mfupi wa mabanzi ya miti na geti dhaifu la mbao mbele yake. Sikuona nyumba nyingine za jirani na eneo lile la msituni na hali ile ikanishangaza sana. Nikapunguza mwendo na kuendesha gari taratibu hadi tulipolifikia lile geti la mbao. Hatimaye nikasimamisha gari huku taa za mbele za gari nimeziwasha kwa mwanga mkali uliotuwezesha sote kuona vizuri sehemu ya mbele ya ile nyumba. Ilikuwa nyumba kubwa yenye baraza mbele yake na baada ya madirisha mawili ya vyumbani upande wa kulia nikaona banda la kuegeshea gari lenye mlango wa mbao uliofungwa kwa kufuli.
“Hapa ndiyo anapoishi Shangazi?”. Nikageuka na kumuuliza Mariama wakati nikisubiri mtu yeyote afungue malango wa mbele wa ile nyumba na kuja kutufungulia lile geti fupi la mbao.
“Ndiyo”. Mariama akaitikia huku akitazama mbele.
“Anaishi peke yake?”
“Kwa sasa yupo yeye na kijana wa kazi”
“Hana mtoto wala mume?”
“Mume wake alikuwa dereva wa lori na alifariki miaka miwili iliyopita kwa ajari ya gari. Mtoto wake ni afisa uhamiaji katika ubalozi wa Liberia uliyopo Freetown nchini Sierra Lione”
Maelezo ya Mariama yakawa yamenielea vyema na hapo nikageuka na kutazama mbele ya ile nyuma bado nikiwa katika matumaini ya kuona mlango wa mbele wa ile nyumba ukifunguliwa na mwenyeji wetu kutoka nje na kuja kutukaribisha. Hata hivyo hilo halikutokea kwani ni kama tulikuwa tumekosea njia kwani ile nyumba ilikuwa gizani na hakuna mtu yeyote aliyejitokeza kutulaki. Nilipochunguza kwa makini nikagundua kuwa kulikuwa na kila dalili ya kuwa nyumba ile ilikuwa imeachwa ukiwa. Kitu cha kushangaza ni kuwa siyo Mariama, wala yule kijana ndugu yao wala wazazi wake aliyetamani kushuka kwenye gari kwa hali ile.
Wasiwasi ukaniingia kidogo hivyo nikazima taa za gari kisha nikachukua bastola na kurunzi mkononi na hapo nikafungua mlango wa gari na kushuka chini. Nikiwa pale mlangoni nje ya gari nikasimama huku nikiyasawili kwa utulivu mandhari yale mapya kabisa machoni mwangu sambamba na kujitahidi kulizoea giza zito la eneo lile. Nguo zangu mwilini zilikuwa zimelowana chepechepe hivyo hata mvua iliyokuwa ikiendelea kuninyeshea eneo lile ilikuwa si kitu kwangu.
Bado kulikuwa na utulivu usioeleweka hivyo nikaikamata vyema bastola yangu mkononi na kuanza kutupa hatua zangu hafifu za tahadhari kuelekea kwenye lile geti fupi la mbao mbele ya ile nyumba iliyozungukwa na migomba na miwa kila upande. Baada ya kuwasha kurunzi yangu mkononi na kumulika chini nikaona alama za magurudumu ya gari eneo lile. Hali ile ikazidi kunitia mashaka na kuvuta zaidi hisia zangu. Nilipogeuka kutazama nyuma yangu kumbe Mariama tayari alikuwa ameshuka kwenye gari na kunifikia.
“Shangazi ana gari?”. Nikamuuliza Mariama kwa utulivu.
“Ndiyo”
“Gari gani?”. Nikamuuliza Mariama huku nikitazama chini.
“Peugeot 504 ingawa hutumiwa na mwanae pale anapokuja likizo kumtembelea kwani tangu mumewe amefariki gari hilo limekuwa likikaa bandani tu kama kinda la njiwa”. Jibu la Mariama likanifurahisha kidogo kabla ya tabasamu langu kumezwa na mshangao hafifu.
“Kwani kuna nini Tibba?”. Mariama akaniuliza.
“Tazama chini kwa makini utaona alama za magurudumu ya gari”. Maelezo yangu yakampelekea Mariama atazame chini kwa makini zaidi kwa msaada wa mwanga wa kurunzi yangu mkononi.
“Ni kweli kuna alama za magurudumu ya gari”. Mariama akaongea kwa sauti ya kunong’ona iliyopwaya kisha akageuka na kuniuliza.
“Wewe unafikiri nini?”
“Alama hizi za magurudumu ya gari siyo za gari Peugeot 504 ila zinashabihiana na alama za magurudumu ya gari la wale wanajeshi watekaji wa kule msituni”. Nikamtahadharisha Mariama huku taratibu nikiusogeza mlango mmoja wa lile geti fupi la mbao na kuelekea mbele ya ile nyumba. Safari hii Mariama hakunisemesha badala yake akasogea karibu akiambatana na mimi na kutazama huku na kule. Sikuwa na shaka yoyote kuwa akili ya Mariama ilikuwa imetawaliwa na hofu na wasiwasi mwingi hasa kufuatia ile kumbukumbu mbaya ya mauaji ya msituni.
“Tibba…”. Mariama akaniita huku akinishika mkono wa woga.
“Naam”
“Hapa siyo mahali salama tena kukaa”
“Sasa tuelekee wapi mpenzi?”
“Kokote kwengineko lakini siyo mahali hapa”
“Ni kweli mpenzi lakini hatupaswi kufanya maamuzi ya haraka hadi hapo tutakapojiridhisha juu ya usalama wa eneo hili. Mafuta yaliyosalia kwenye gari ni kidogo lakini vilevile huwenda mtu au watu waliofika hapa siyo watu wabaya kama hisia zangu zinavyonituma”. Nikamwambia Mariama kwa utulivu huku macho yangu yakiwa makini kutazama huku na kule. Hatimaye tukafika mbele ya ile nyumba na hapo nikabisha hodi kwa utulivu. Baada ya kubisha hodi mara kadhaa pasipo muitikio wowote nikageuka na kumtazama Mariama kando yangu.
“Rudi kwenye gari mpenzi mimi nitafanya uchunguzi na chochote hatari utakachokiona usisite kunishtua”. Niliongea huku nikimpigapiga Mariama mgongoni kwa mkono wangu na kumuonesha tabasamu la kirafiki ingawa akili yangu haikuwa pale. Nashukuru Mariama alinielewa haraka hivyo akaondoka haraka na kurudi kwenye gari.
Nikaendelea kubisha hodi zaidi pale mlangoni na nilipoona sijibiwi wala ule mlango haufunguliwi nikaamua kubadili uelekeo nikiiambaa na ukuta kuelekea nyuma ya ile nyumba. Nilipofika nyuma ya ile nyumba nikachunguza na kuona banda la kuku wa kienyeji, jiko la kuni la nje, ghara moja ya kuhifadhia nafaka juu ya kichanja na karo kubwa na kuoshea vyombo. Nyuma ya lile banda la kuku eneo lile lilipakana na shamba kubwa la migomba na miwa na nyuma ya shamba lile nikauona msitu mnene kuelekea kwenye bonde kubwa.
Nikasimama nikiyachunguza mandhari yale kwa utulivu na kurunzi yangu mkononi. Hatimaye nikabadili uelekeo na kuelekea kwenye mlango wa nyuma wa ile nyumba. Hapo nikapigwa na mshutuko kiasi cha kunipelekea niongeze umakini na kuikamata vyema bastola yangu mkononi. Mlango wa nyuma wa ile nyumba ulikuwa nusu wazi na nilipomulika chini nikaona alama za buti za jeshi zenye tope kuingia mle ndani. Hata hivyo alama zile zilionesha kuingia na kutoka na mchanganyiko wake sikuuelewa. Nikausukuma ule mlango na kuingia ndani kwa tahadhari huku bastola yangu makini imetuama vyema mkononi.
Ule mlango ulikuwa wa kuingilia sehemu ya chumba cha jiko la ndani na baada kulipita lile jiko nikakutana na korido fupi upande wa kulia lakini ndefu upande wa kushoto. Nikaamua nianze uchunguzi wangu upande wa kulia mwisho wa ile korido kulipokuwa na mlango wa chumba. Mle ndani sikupata chochote cha maana hivyo nikarudi koridoni kuelekea na upande wa kushoto. Kulikuwa na vyumba viwili vyenye milango inayotazamana na sebule ya ile nyumba. Mle ndani ya vile vyumba hapakuwa na ziada yoyote zaidi ya vitanda na makabati ya nguo. Sebule ilifanywa kwa seti moja ya makochi ya mbao yenye mito ya vitambaa, meza fupi ya mbao, stuli nne, picha za ukutani na redio moja ya mkulima.
Nilipoivuka sebule ile kuelekea chumba cha mwisho macho yangu yakapata ugeni wa taswira mbaya. Niliona mwili wa mtu ukiwa umelala kifudifudi sakafuni katikati ya dimbwi kuwa la damu. Nikasogea karibu na kumchunguza kwa makini mtu yule. Nilipomgeuza kwa mguu wangu wajihi wake ukanitanabaisha kuwa mtu yule alikuwa kijana na umri wake ungekuwa kati ya miaka ishirini na tano na ishirini na saba. Mdomo na macho yake vilikuwa wazi na kifuani alikuwa na matundu mawili ya risasi kwenye sehemu ya moyo wake kushoto. Juu ya jicho lake la kulia kulikuwa na uvimbe mkubwa. Ni kama pigo baya la kitako cha bunduki lilitumika kumshambulia sehemu ile. Nilipomchunguza nikagundua kuwa tayari alikuwa ameaga dunia. Kupitia maelezo ya Mariama nikahisi kuwa huwenda kijana yule ndiye aliyesemekana kuishi na shangazi pale nyumbani. Hasira zikanishika na hapo nikauruka mwili wa yule kijana na kuelekea kwenye kile chumba cha mwisho kilichokuwa upande wa kushoto wa ile korido baada ya kuupita mlango wa chumba cha msalani.
Nilipoufikia mlango wa kile chumba mashaka yakazidi kuniingiia baada ya kuyaona matundu mawili ya risasi, tundu moja katikati ya mlango na tundu lingine kwenye kitasa. Nikahisi kuwa huwenda mtu aliyekuwa mle ndani ya kile chumba alijifungia kujihami na uvamizi na mvamizi mmoja alipoona vile akaushambulia ule mlango kwa risasi kuharibu kitasa.
Kwa tahadhari nikausukuma mlango wa kile chumba na kuingia ndani. Sikukabiliana na upinzani wa namna yoyote lakini nilichokiona mle ndani kikanikosesha raha.
Mwili wa mwanamke mnene mwenye umri wa kukadirika kati ya miaka hamsini hadi hamsini na tano ulikuwa umelala chali kwenye kitanda cha mle ndani bila nguo yoyote ya kujisitiri. Nikasogea karibu na kumchunguza mwanamke yule na hapo nikagundua alikuwa amebakwa kwani sehemu zake za siri zilikuwa zimeganda damu na shingo yake ilikuwa imevunjwa. Wavamizi walikuwa wametekeleza unyama ule bila haya. Kwa sekunde kadhaa nikasimama nikimtazama mwanamke yule kwa namna uso wake ulivyohifadhi uchungu mwingi na fedheha. Kwa kweli roho iliniuma sana.
Sasa nilikuwa nimepata picha kamili kuwa wale wanajeshi watekaji wa kule msituni ndiyo waliohusika na unyama ule. Mara tu baada ya mapinduzi ya kijeshi kufanyika wanajeshi wale walitumwa kumtafuta baba yake Mariama hivyo baada ya kufika kule nyumbani kwake Monrovia na kumkosa sehemu nyingine waliyohisi huwenda angekuwa amekimbilia na familia yake ilikuwa ni pale kwa dada yake. Hivyo walipofika pale na kumkosa baba yake Mariama wakaona wamalizie hasira zao kwa kumuua yule kijana kwenye korido mle ndani na kumyonga shangazi baada ya kumbaka. Sikuweza kurudia zaidi kumtazama yule mwanamke hivyo nikaufunika mwili wake kwa shuka pale kitandani na kisha kuelekea nje.
Niliporudi kwenye gari kule mbele ya ile nyumba nikawa nimerejesha matumaini kwenye mioyo ya wale watu. Mariama akataka kufahamu kilichojiri kwenye uchunguzi wangu na mimi bila hiyana nikaweka mambo bayana nikiwaeleza juu ya mauaji yaliyofanyika mle ndani. Wote wakaangua kilio na kusikitika sana lakini kwa baba yake Mariama ilikuwa ni zaidi ya simanzi kwa kuondokewa na dada yake kipenzi.
Kilio kilipopungua nikawaomba washuke kwenye gari na tuelekee sote kwenye ile nyumba. Mimi, baba yake Mariama na yule kijana ndugu wa familia ikabidi tuishughulikie ile miili. Nyuma ya ule nyumba kwenye shamba la migomba tukachimba makaburi mawili na kuzika ile miili. Ilikuwa kazi ngumu na ya kuchosha iliyoambatana na hofu na mshaka kwa vile bado hatukufahamu usalama wa eneo lile. Hatimaye tukamaliza zoezi lile huku tayari kukiwa kumeanza kupambazuka. Mimi na yule kijana tukashusha mizigo kwenye gari na kuiingiza ndani ya ile nyumba kwa kuhofika kuharibiwa na mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha na wakati huo Mariama na mama yake walikuwa wakisafisha damu kwenye ile korido.
Kwa kweli nilikuwa nimechoka sana hata hivyo sikuwa na namna. Kuna wakati nikawa nikiwaza kuwa endapo ningekuwa nimekataa wito wa Mariama mambo yale yote yasingenikuta na siyo ajabu kwa muda ule ningekuwa tayari nipo jijini Dar es Salaam nimejipumzisha nyumbani kwangu. Lakini mapenzi yalikuwa yameniponza kwani kumpenda Mariama kulikuwa kumeniingiza kwenye mkasa hatari. Hata hivyo sikuwa tayari kumuacha Mariama wala familia yake kwenye hatari ya namna ile. Sikuweza kufahamu nini hatima ya mkasa ule na hali ile ilinitia hofu kwa vile bosi wangu katika idara ya ujasusi ya taifa jijini Dar es Salaama hakuwa na taarifa zangu.
_____
KUFUATIA YALE MAPINDUZI YA KIJESHI pale nchini Liberia na wale wanajeshi watekaji niliyopambana nao kule msituni usiku ule, ambao sasa niliamini kuwa ndiyo waliohusika na mauaji ya shangazi yake Mariama na yule kijana aliyekuwa akiishi naye mle ndani. Sasa nikawa nimepata wazo kuwa kuendelea kukaa ndani ya ile nyumba lisingekuwa jambo jema kwa usalama wetu sote. Sikuwa na shaka yoyote kuwa ile serikali ya mapinduzi ya kijeshi kupitia kitengo chake cha ushushushu ilikuwa tayari ikiyafahamu maficho yale na unasaba uliokuwa baina ya baba yake Mariama, waziri Amara Konneh na yule shangazi aliyeuwawa na ndiyo kisa wakawatuma wale wanajeshi wauaji kufanya uchunguzi kwenye maficho yale. Hivyo kulikuwa na kila dalili kuwa baada ya wale wanajeshi watekaji kutorudi huko walikotumwa na wanajeshi wengine wangetumwa kuja kupeleleza eneo lile kwa lengo la kumtafuta baba yake Mariama.
Sikutakwa tukutwe mle ndani na kuvamiwa kiulaini hivyo nikachukua lile turubai tulilokuwa tumefunikia mzigo juu ya gari na kutengeneza hema juu ya kichuguu katikati ya ule msitu wa jirani na nyumba ile. Ndani ya hema ile wakakaa baba na mama yake Mariama pamoja na vitu vingine muhimu kama vyakula, jiko na nguo za kubadilisha. Mimi, Mariama na yule kijana ndugu yao ambaye kupitia maongezi sasa nilikuwa nimemfahamu kwa jina la Max tukakaa ndani ya gari katikati ya ule msitu.
_____
ASUBUHI ILE BAADA YA KUPATA kiamsha kinywa cha wali mkavu wa mafuta ya mawese na kipande cha kuku wa kuchemsha aliyechinjwa kutoka bandani nyuma ya ile nyumba nikapata wasaha mzuri wa kuzungumza na baba yake Mariama juu ya masuala kadha wa kadha ya nchi ile na historia yake. Baba yake Mariama akanielezea mambo mengi sana huku akiyalaumu sana mapinduzi yale ya kijeshi na kusisitiza kuwa lilikuwa ni tukio baya na la aibu sana kwa nchi kama ile lililohitaji kukemewa sana na jamii za kimataifa. Huku akifahamu kuwa roho yake ilikuwa ikiwindwa baba yake Mariama hakuacha kueleza wasiwasi wake juu ya hatima yeka na familia yake.
Kupitia ile redio ya kijeshi niliyoichukua kutoka kwenye lile gari la jeshi Nissan Patrol la wale wanajeshi watekaji kule msituni tukaweza kupata habari kupitia kituo cha redio ya taifa ya Liberia kijulikanacho kama Liberia Broadcasting System-LBS kilichokuwa kikirusha matangazo yake moja kwa moja kutoka chumba cha habari kwenye mji mkuu wa Liberia, Monrovia.
Hadi kufikia asubuhi ile jeshi la People’s Redemption Council lilikuwa limechukua udhibiti wa maeneo yote muhimu ya nchi kama bandari, viwanja vya ndege, vituo vya redio, mitambo ya kufua umeme, benki kuu ya taifa na barabara zote muhimu za nchi chini ya kiongozi wa mapinduzi yale ya kijeshi Master Surgeant, Samuel Doe. Jeshi hilo lilikuwa limefanikiwa kuwaua watu ishirini na sita wa kikosi cha usalama wa rais William R.Tolbert ambaye tayari alikuwa amepinduliwa na kuuwawa ikulu ya Monrovia katika mapigano makali ya wavamizi usiku wa jana.
Taarifa zile zikaendelea kueleza kuwa hadi kufikia wakati ule tayari mawaziri wapatao tisa wa serikali ya rais William R. Tolbert Jr. walikuwa wamekamatwa na wanajeshi wa Samuel Doe. Ingawa mtangazaji yule hakueleza mawaziri hao walikuwa wamekamatwa kwa sababu gani lakini binafsi nilihisi kuwa wangeangukia kwenye mikono ya kifo chenye mateso makali yasiyovumilika. Mara kwa mara mtangazaji wa redio ile mwanajeshi wa jeshi la PRC aliyejitambulisha wa jina la Koplo Edward Dagosseh aliorodhesha majina ya mawaziri wote waliokamatwa pamoja na majina ya mawaziri waliokuwa wakisakwa ambapo waziri wa ulinzi, ndugu Amara Konneh ambaye ni baba yake Mariama na yeye alikuwa kwenye orodha ile.
Mipaka yote ya nchi ilitangazwa kufungwa na wanajeshi watiifu wa mapinduzi yale kutakiwa kuweka doria. Hivyo hakuna mtu yeyote aliyeruhusiwa kuingia wala kutoka nchini Liberia bila ruhusa ya Master Surgeant Samuel Doe ambaye sasa alikuwa amejipandisha cheo na kujiita jenerali. Taarifa zile zikamfikia baba yake Mariama na kumuacha katikati ya hofu isiyoelezeka. Hata hivyo sikuacha kumitia moyo kuwa asiwe na wasiwasi kwani tayari tulikuwa mahali salama.
Kupitia taarifa zile za redioni nikaanza kubashiri ugumu uliokuwa mbele yetu katika kutoroka nchi ile salama. Ingawa nilikuwa siifahamu vyema jiografia ya nchi ya Liberia lakini maelezo ya baba yake Mariama yakawa yamenigutusha kuwa tulikuwa tupo eneo la kaskazini magharibi mwa nchi ya Liberia. Hivyo kwa maana nyingine ni kuwa endapo tungeendelea mbele na safari yetu kwa muda wa siku moja au mbili hatimaye tungeufikia mpaka wa Liberia na nchi jirani ya Sierra Lione. Hivyo endapo tungefanikiwa kuvuka salama mpaka huo na kuingia nchini Sierra Lione tungeweza kupewa hifadhi ya kisiasa na kuhakikishiwa usalama wetu.
Hata hivyo hilo kwa sasa lisingewezekana, kwanza ni kwa vile tayari jeshi la PRC lilikuwa tayari limechukua udhibiti kwenye mipaka yote ya nchi ya Liberia, pili gari letu Landrover 110 halikuwa na mafuta ya kutosha ya kuweza kutufikisha mpakani, tatu kutembea bila ramani kwangu lilikuwa ni jambo hatari sana kuliko hata kukaa sehemu moja na kusubiri hali ya machafuko itulie. Lakini vilevile hatukuwa na pesa ya kutosha, pesa ambayo siyo tu kwamba ingetusaidia kuhonga wanajeshi wa Samuel Doe barabarani kwenye vizuizi na mipakani kwenye doria, lakini pia pesa hiyo ingetusaidia katika kuanza maisha mapya ya uhamishoni endapo tungefanikiwa kuvuka mpaka salama na kuingia nchini Sierra Lione. Hivyo ni dhahiri kuwa pesa ilihitajika sana kwa wakati ule katika kufanikisha kutoroka kwetu.
Sikuwa na namna ila kumshirikisha baba yake Mariama juu ya uhitaji mkubwa wa pesa tuliokuwa nao na namna pesa hiyo itakavyotumika maeneo tofauti katika kununua mafuta ya gari, kuwahonga wanajeshi na kuanza maisha mapya ya ukimbizi uhamishoni. Hoja zangu zilikuwa na nguvu hivyo wote wakawa wamekubaliana na mimi. Baba yake Mariama akaniambia kuwa alikuwa na pesa nyingi kwenye akaunti yake katika benki ya Central Bank of Liberia iliyokuwa kwenye barabara ya Warrent Drive jijini Monrovia. Swali likabaki, Ni kwa namna gani pesa hiyo itapatikana ilhali sote tukiwa pale msituni?.
Baada ya kushauriana kwa kina baba yake Mariama akawa amependekeza kuwa watu wawili miongoni mwetu ingefaa warudi jijini Monrovia ili kushughulikia upatikani wa pesa kutoka kwenye akaunti yake na mafuta ya gari. Hivyo akapendekeza kuwa ingekuwa vyema mimi na Max tuongozane kurudi Monrovia kuonana na meneja wa benki ya Central Bank of Liberia aitwaye Theodore J. Momo, ambaye baba yake Mariama alijinasibu kuwa meneja huyo wa benki alikuwa ni rafiki yake wa karibu sana na kwa vile meneja huyo wa benki alikuwa akimfahamu Max hivyo ingekuwa rahisi kutuelewa na kutuhudumia.
Binafsi sikuona umuhimu wa kuongozana na Max kwa vile nilikuwa tayari nimemuona kuwa ni mtu mzembe na muoga. Nikapendekeza kuwa ingekuwa vyema endapo ningeenda Monrovia peke yangu kushughulikia upatikanaji wa pesa hiyo ili Max abaki pale kama kijana ambaye angeweza kutoa msaada endapo ingejitokeza dharura ya namna yoyote. Hata hivyo baba na mama yake Mariama wakataa wazo langu bila kunipa sababu za msingi na hapo nikajua kuwa bado hawakuwa na imani sana na mimi. Labda walihisi kuwa mara tu baada ya kufanikiwa kupata pesa hizo ningeamua kutoroka nazo na kuwaacha wao kule msituni wakiwa na matumaini hewa.
Kwangu ilikuwa ni afadhali kuongozana na Mariama kwa vile alikuwa msichana mtundu, muelewa, mwepesi kufikiri na mjanja kama nyoka lakini wazazi wake walikataa katukatu wakati nilipowapa pendekezo langu. Kufuatia yale mapinduzi ya kijeshi huwenda walihofia kuwa Mariama angeweza kuingia matatizoni na kukamatwa na wanajeshi wa Samuel Doe kwa vile alikuwa akifahamika sana na kwa vile Mariama alikuwa binti yao pekee wazazi wake hawakuwa tayari niongozane naye katika mazingira yale ya hatari.
Hatimaye sikuona sababu ya kung’ang’ania msimamo wangu kwa vile hitaji kubwa lililokuwa mbele yetu lilikuwa ni kupata pesa na mafuta ya kusafiria kwenye gari. Nilitaka kurudi haraka jijini Dar es Salaam kwa vile ofisi yangu haikuwa na taarifa zozote kuhusu safari yangu ile ya Liberia. Hivyo nikakubali kuongozana na Max kurudi jijini Monrovia bila ubishi.
_____
Nilimuacha baba yake Mariama kwenye hema akiandika barua kwa rafiki yake, ndugu Theodore J. Momo, meneja wa benki ya Central Bank of Liberia kumpa maelekezo yote muhimu ikiwemo kutoa pesa yote iliyokuwa kwenye akaunti yake na kutupatia sisi katika usiri wa hali ya juu. Wakati barua ile ikiandikwa mimi tayari nilikuwa nimepata wazo baada ya kukumbuka gari dogo la rangi ya samawati, Peugeot 504 iliyokuwa kwenye banda la kuegeshea gari kando ya ile nyumba. Nikaenda kuchunguza lile gari kama lingekuwa zima na lina mafuta ya kutosha ya kuweza kutufikisha jijini Monrovia.
Nilipofika kwenye lile banda nikabomoa kufuli na kufungua mlango mkubwa wa mbao kisha nikaanza kulikagua lile gari. Nikafurahi kukuta mafuta ya kutosha kwenye tenki yake lakini kwa kuwa gari lile lilikuwa limeegeshwa kwa muda mrefu bila kutumika umeme wa betri yake ulikuwa hafifu. Hivyo ikanibidi nielekee tena kule msituni kuchukua betri ya ile Landrover 110 na kuja kubusti ile betri ya Peugeot 504. Lile gari hatimaye likawaka hivyo nikarudisha ile betri kwenye Landrover kule msituni na kurudi pale kwenye banda la gari kuendelea na ukaguzi wa vitu vidogovidogo vya lile gari ambavyo vingeweza kuleta hitilafu na kukwamisha safari yetu pamoja na kulifanyia usafi lile gari kwa vile lilivyokuwa limeshika vumbi kwa kukaa muda mrefu bila kutumika bandani.
Wakati wote nikiendelea na zoezi lile nilikuwa makini kutazama ile barabara ya kuingilia pale nyumbani li kama kungekuwa na gari lolote linalokuja niweze kufunga banda haraka na kujificha. Muda wote Mariama alikuwa kando yangu akinipatiliza na kunisaidia juu ya hili na lile. Kwa kweli Mariama alipenda sana tuongozane kurudi Monrovia lakini kwa vile wazazi wake walikataa hakuwa na budi kuwasikiliza na kuwatii.
“Tibba mpenzi wangu…”. Mariama akaniita kwa upole.
“Naam Mariama wangu”. Nikaitikia na kugeuka nikimtazama Mariama baada ya kuacha kunyonya mafuta kwenye mrija wa kabureta.
“Mtarudi lini?. Sifurahii kukaa hapa msituni peke yetu bila wewe”. Mariama akaongea huku machozi yakimlengalenga na hapo nikasogea na kumbusu shavuni kwa mdomo wangu uliokolea mafuta ya petroli na uso wangu ukimliwaza kidogo kwa tabasamu.
“Kama tutafanikiwa haraka huwenda tukarudi leo hii hii usiku. Liberia sina mwenyeji mwingine isipokuwa wewe mpenzi”. Nikaongea kwa utulivu huku nikimuonea Mariama huruma.
“Nina hakika kuwa mtafanikiwa mapema kwani sisi tutabaki tukiwaombea kwa Mungu”. Maneno ya Mariama yakanipa faraja huku moyoni nikijisifu kwa kuwa na msichana mwenye busara namna ile. Kitambo kifupi cha muda kikapita wakati ukimya ule ukimezwa na sauti za ndege wa porini na mvumo wa upepo kwenye matawi ya miti. Mara nikakumbuka kumuuliza Mariama.
“Huyu Max ni ndugu yenu kivipi?”
“Max ni mtoto wa baba yangu mdogo lakini bahati mbaya wazazi wake walifariki akiwa bado mdogo. Hivyo baba akaamua kumchukua na kumlea”
“Ni kijana mwaminifu?”. Nikamuuliza Mariama huku nikimtazama machoni kwa makini lakini hakunijibu haraka badala yake akageuka na kutazama nyuma yangu. Kuona vile na mimi ikabidi nigeuka na kutazama nyuma yangu na hapo nikamuona Max amesimama katika uso wa tabasamu. Max hakutia neno na hapo nikajisikia vibaya baada ya kuhisi kuwa huwenda Max akawa ameyasikia vizuri maongezi yetu na kuanza kutengeneza hisia mbaya juu yangu.
“Mariama unaitwa na baba”. Max akaongea huku akinitazama kwa makini na namna ya utazamaji ule kwa kweli sikuupenda.
“Tunatakiwa kufika Monrovia kabla ya saa saba mchana”. Max akaendelea kuongea wakati Mariama akiondoka eneo lile kuelekea msituni kwenye hema.
“Itategemea na hali ya hewa”. Nikamjibu pasipo kumtazama huku nikikazana kukaza waya wa betri ya gari. Max sikumpenda na sijui ni kwa sababu gani.
_____

ILIPOTIMIA SAA MBILI ASUBUHI kila kitu kikawa kimekamilika. Mariama, baba na mama yake watakuaga kwa sala na maombi kisha watatupa mkono wa baraka. Kwa kweli sikufurahi kumuacha Mariama na wazazi wake pale msituni bila ulinzi wowote. Hata hivyo sikuwa na la kufanya. Mimi na Max tukaingia kwenye lile gari Peugeot 504 na hapo safari ya kurudi mji mkuu wa Liberia, Monrovia ikaanza.
Macho yangu yakaendelea kuwatazama Mariama na wazazi wake kwenye vioo vya ubavuni mwa gari nyuma yangu wakiwa wamesimama mbele ya ile nyumba na kutupungia mkono wa kwa heri ya kuonana. Hatimaye taswira yao ikaptoweka wakati nilipokunja kona kuifuata barabara ile ya msituni. Max aliyekuwa pembeni yangu cha ajabu alioneka mwingi wa furaha na hali ile ilinitatiza sana moyoni.
Mvua ilikuwa imeacha kunyesha na kwa mbali jua la asubuhi lilianza kuchomoza sambamba na sauti za ndege wa porini...ITAENDELEA WIKI IJAYO
 
RIWAYA: MTUTU WA BUNDUKI
SEHEMU: 6

_____

JUA LILIKUWA KALI MNO, joto la fukuto nalo lilikuwa limepamba moto. Sehemu kubwa ya mawingu ilionekana vizuri angani ngawa kulikuwa na kila dalili kuwa mvua kubwa ingenyesha tena baadaye. Kwa kiasi fulani jiji la Monrovia lilikuwa limerudi katika utulivu wake lakini haukuwa utulivu salama. Wanajeshi wa Samuel Doe walikuwa wametanda kila kona ya jiji la Monrovia. Vizuizi vya barabarani vilikuwa kero, kila gari lilisimamishwa na kufanyiwa upekuzi na yeyote aliyehisiwa vibaya risasi zilimhusu palepale hadharani bila huruma.
Ilikuwa tayari imetimia saa sita na robo mchana wakati tulipokuwa tukiwasili jijini Monrovia. Max aliyekuwa ameketi kando yangu tayari alikuwa amechukuliwa na usingizi mzito nakukoroma hovyo kama yupo kitandani nyumbani. Mwanzoni nilidhani Max angeweza kuwa msaada mkubwa katika kunielekeza barabara na vitongoji vya jiji la Monrovia lakini hakuwa na msaada wowote. Hivyo ni kama dereva niliyekuwa nimembeba abiria aliyehitaji msaada wangu juu ya kituo anachoshukia.
Max hakuwa mwongeaji bali ni mtu anayependa kusikiliza na kutabasamu. Nilipomuuliza maswali machache juu ya masuala fulani yaliyohusiana na safari yetu, aliishia kunijibu kwa kifupi na kisha kusinzia. Hivyo kama siyo mabango elekezi juu ya maeneo ya njiani na uelekeo wa jiji la Monrovia, yumkini ningepotea njia. Mwendo wangu ulikuwa wa kasi mno kwa vile tulitakiwa kuwasili mapema jijini Monrovia kabla ya benki hazijafungwa. Bahati mbaya sana tulikuwa tumepata pancha njiani vinginevyo tungekuwa tumefika mapema zaidi.
Niliwaona wanajeshi wengi wakisimamisha magari yaliyokuwa yakiingia na kutoka jijini Monrovia wakati nilipoufikia mzunguko wa barabara ya United Nations Drive. Mwanajeshi mmoja akaingia barabarani kusimamisha gari letu na wakati nikipunguza mwendo ghafla lori moja lililokuwa nyuma yangu likafanya bidii kuniovateki na hapo wanajeshi wale wakanisahau na kuanza kulifyatulia risasi lile lori. Kuona vile nikajua wamenisahau hivyo nikachochea mwendo na baada kukipita kiwanda cha United Motors Company na kiwanda cha Liberty Motors. Nilipomaliza ule mzunguko nikashika uelekeo wa upande wa magharibi baada kuona bango kubwa la barabarani lililoandikwa “Welcome to Monrovia. 30 Miles Ahead”.
Nilikuwa nimeingia barabara ya United Nations Drive na sasa nilikuwa nimelifikia daraja kubwa la Mto Mesurado na kwa mbali niliweza kuyaona majengo marefu ya ghorofa ya jiji la Monrovia. Nilipovuka daraja lile nikaamua kumuamsha Max aliyekuwa akikoroma hovyo kando yangu kwa vile nilihisi barabara za jiji la Monrovia zingeweza kunichanganya. Nikayumbisha gari kidogo na hapo Max akajigonga mlangoni na kuamka huku akishangaa shangaa.
“Tunafuata uelekeo upi?”. Nikamuuliza baada ya kuona barabara ya Water Street kulia kwangu na hatimaye barabara ya Slipway kushoto kwangu.
“Nyooka na barabara hii hadi utakapoifikia barabara kubwa ya Haile Selassie Avenue hapo utaingia kushoto”. Max akanijibu baada kitambo kifupi cha ukimya akishangaa maeneo.
Kulikuwa na magari machache, pikipiki na idadi ya kuridhisha ya watembea kwa miguu barabarani ambapo wengi wao walikuwa vijana waliokuwa wakiendelea kushabikia mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika usiku wa jana pale Liberia. Baadhi ya maduka, ofisi, hoteli na supermarket zilikuwa zimefungwa na katika baadhi ya sehemu za barabarani kulikuwa na mawe ya vizuizi na masalia ya magurudumu ya magari yaliyoteketezwa kwa moto na mashabiki wa mapinduzi yale. Hivyo palihitajika umakini sana kuyakwepa.
Tulipoifikia barabara kubwa ya Haile Selassie Avenue nikaingia upande wa kushoto kuifuata barabara ya Johnson Street baada ya Max kunitaka nifanye hivyo. Barabara ile ilikuwa ikikatisha katikati ya majengo marefu ya ghorofa yenye maduka mengi chini yake. Hapo nikapunguza mwendo kwa vile kulikuwa na msongamano mkubwa wa watu na magari baada ya kulipita duka kubwa la madawa la Itter Pharmacy kwa upande wa kushoto. Niliwaona baadhi ya wanajeshi wakiwa na bunduki zao mikononi wakirandaranda mitaani kufanya doria na kuchunguza watu na magari yaliyotoka na kuingia jijini Monrovia. Niliviona vikundi vya watu kila eneo, huwenda watu wale walikuwa wakijadiliana kuhusu yale mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea usiku wa jana.
“Ingia upande wa kushoto kufuata barabara ya Carey Street na kabla hujalifikia jengo la Business Link, utaona barabara inayochepukia kuingia upande wa kulia, hiyo ndio barabara ya Warrent Street. Fuata barabara hiyo na mbele kidogo upande wa kulia utaliona jengo la ghorofa tatu la rangi ya bluu bahari. Hiyo ndiyo benki ya Central bank of Liberia”
Safari hii Max aliongea kwa uchangamfu zaidi huku akimwemwesa macho yake kutazama nje kupitia kwenye kioo dirishani. Maelezo yake yakanielea vyema, mbele kidogo upande wa kulia nikaona barabara ya lami hapo nikapunguza mwendo na kukunja kona nikiifuata barabara ile na mara hii sikuhitaji maelezo zaidi kwani kiasi cha umbali usiopungua mita ishirini mbele yangu upande wa kulia nikaona bango kubwa kwenye pembe ya jengo la ghorofa la rangi ya bluu bahari. Maandishi yale yakisomeka “Central Bank of Liberia-Prosperity for all”
Warrent Street ulikuwa ni mtaa wenye msongamano mkubwa na pilika za watu kufuatia biashara za maduka makubwa ya nguo, baa za daraja la kati, mikahawa na maduka ya vipuli vya magari. Kulikuwa na magari mengi yaliyoogeshwa kandokando ya barabara ya mtaa ule. Hatimaye nikapunguza mwendo na kutafuta maegesho mkabala na benki ile.
Tofauti na nilivyokuwa nikihofia kukuta benki ile imefungwa kufuatia lile tukio la mapinduzi ya kijeshi, lakini benki ile ilikuwa wazi. Nje ya ile benki niliwaona wanajeshi sita na bunduki zao mkononi wakifuatilia kwa makini mienendo ya watu wanaopita na kusimama eneo lile, na sisi tulikuwa miongoni mwao.
Max akafungua mlango na kutaka kushuka lakini niliwahi kumzuia kwa kumshika mkono na hapo nikajikuta nikikabiliana na uso wake wenye chuki na kisirani. Mwanajeshi mmoja aliyekuwa amesimama nje ya ile benki kwa makini akifuatilia nyendo zetu akasogea karibu na kugonga kioo dirishani. Nikashusha kioo na kumsabahi kwa sura ya ucheshi ingawa sikufanikiwa kuilainisha sura yake ya kikauzu.
“Mnataka nini?”. Mwanajeshi yule akatuuliza wakati sote tulipogeuka kumkodolea macho.
“Tunaingia benki”. Nikawahi kumjibu.
“Kufanya nini?”. Swali la yule mwanajeshi likanishangaza kidogo huku nikijiuliza. Ina maana alikuwa hafahamu huduma zilizokuwa zikipatikana katika benki yoyote duniani au aliishiwa maswali?.
“Tunataka kudroo pesa kidogo”. Max akawahi kumjibu.
“Fanyeni haraka kwani haturuhusu mtu yeyote kusimama eneo hili bila sababu maalum”. Yule mwanajeshi akatutahadharisha na baada ya kutupiga ukope akatuacha na kurudi sehemu yake na hapo nikamgeukia Max kando yangu.
“Naomba ile barua”. Nikamwambia Max huku nimemkazia macho.
“Mimi ndiye niliyeagizwa kumpa meneja wa benki barua hii. Mimi ndiye ninayefahamiana naye na siyo wewe”. Max akaongea kwa kiburi.
“Hatuwezi kwenda wote mle ndani ya benki kwa vile sote hatufahamu hali ya usalama ipoje kwa hili eneo. Mmoja wetu ni lazima abaki humu kwenye gari ili likitokea lolote tuweze kupeana msaada”
“Ni wazo zuri ila ningeshauri wewe ndiyo ubaki hapa kwenye gari kwa vile meneja wa benki ananifahamu mimi”. Max akaendelea kubisha na hapo nikaanza kupata wasiwasi kuwa huwenda mabishano yale yangeweza kuvuta macho ya wale wanajeshi nje ya ile benki na hivyo kukaribisha hatari. Nilimuona mwanajeshi mmoja akisogea taratibu na bunduki yake mkononi kuja pale tulipoegesha gari. Kuona vile wasiwasi ukaniingia hivyo nikafungua mlango na kutoka nje. Max naye akafungua mlango kutoka kwenye gari kisha tukaongozana na kuelekea mle ndani ya benki baada kuvuka barabara.
Mle ndani ya benki kulikuwa na foleni kubwa ya watu kuelekea kwenye vibanda vya tellers vilivyokuwa upande wa kushoto kufuata huduma za kibenki. Kila mteja aliyefika pale benki alionekana yupo pale kwa minajiri ya kutoa pesa zake kufuatia hali ya usalama wa nchi ile kutetereka. Watu wale kwenye foleni walikuwa na wasiwasi mwingi na hivyo kila mara kugeuka na kutazama mlangoni pale alipoingia mtu mpya.
Wakati nikitathmini hali ya mle ndani mara nikamuona Max akishika uelekeo wa upande wa kulia na kuanza kupanda ngazi kuelekea ghorofani bila kunisemesha. Sikuwa na namna ikabidi nimfuate. Muda mfupi baadaye tukatokezea kwenye korido ya ghorofa ya pili iliyotazamana na milango mingi ya vyumba vya ofizi za utawala za ile benki. Mwisho wa ile korido upande wa kushoto juu mlangoni nikaona kibao kidogo chenye utambulisho wa “Bank Manager”. Bila kubisha hodi Max akasukuma mlango na kuingia mle ndani ya ofisi na mimi kuona vile nikamfuata nyuma yake. Pale mlangoni tukapishana na kijana mmoja mfanyakazi wa ile benki akitoka mkononi ameshika kablasha.
Kilikuwa chumba kikubwa cha ofisi chenye dirisha pana lililofunikwa kwa pazia jepesi, kiyoyozi cha analojia, sefu mbili za chuma, rafu ya mafaili ukutani, makochi mawili ya sofa mbele ya meza moja kubwa ya ofisini. Nyuma ya ile meza aliketi mzee wa miaka hamsini na ushei aliyevaa suti nyeusi na shati jeupe, mwenye uharaza kichwani, mnene na mrefu amevaa miwani. Mzee yule akaondoa miwani yake machoni na kututazama kwa mashaka baada ya kuacha kujaza taarifa fulani kwenye fomu iliyokuwa pale juu ya meza. Nikajua alikuwa ameshtushwa sana na namna ya uingiaji wetu mle ndani bila hodi. Kisha mzee yule akageuka na kumtazama Max kwa mshangao.
“Max…”. Yule mzee akaita huku akimtazama Max kwa mashaka na kupitia kibao kidogo cha utambulisho kilichokuwa pale mezani kando ya mhuri wa ofisi na kidau cha wino haraka nikagutuka kuwa mzee yule aliyeketi nyuma ya ile meza ndiye angekuwa Theodore J. Momo, meneja wa benki ya Central Bank of Liberia.
“Naam!. Shikamoo mzee”. Max akaitikia na kusalimia kwa mikogo akinilingishia kufahamika kwake.
“Marahaba Max. Umefuata nini hapa?”. Yule meneja wa benki akauliza kwa tahadhari na kusimama kwenda kufunga mlango wa ile ofisi kwa ndani kisha akarudi na kuketi kitini.
“Nimetumwa na baba”. Max akaongea huku akitia mkono mfukoni kuchukua ile barua yenye maelekezo kutoka kwa baba yake Mariama. Yule meneja wa benki akaipokea ile barua na kuifungua na kabla hajasoma maelezo yake akageuka na kunitazama.
“Kijana una shida gani?”. Akaniuliza.
“Nipo naye”. Max akamtoa hofu na hapo yule mzee akanitazama kwa makini kabla ya kuhamishia macho yake kwenye ile barua.
“Hili ni jambo la hatari sana Max. Hujasikia kuwa mawaziri wote wa Rais William Tolbert wanasakwa kila kona na wanajeshi wa mapinduzi?”
“Nimesikia”. Max akajibu kwa sauti dhaifu.
“Askari wa Samuel Doe wakifahamu kuwa nimehusika kwenye utoroshaji wa pesa kwenye akaunti ya waziri wanayemtafuta huoni kuwa nitakabiliana na kifo?”. Yule mzee meneja wa benki akaendelea kulalama huku akipitia maelezo ya kwenye ile barua.
“Jambo hili haliwezekani”. Mwishowe akaongea huku akiiweka ile barua pale juu mezani na kututazama.
“Amekuomba msaada wako”. Max akasisitiza.
“Labda angekuja yeye mwenyewe”
“Hawezi kuja hapa kutokana na hali ya usalama wake”
“Yuko wapi?”
“Mafichoni msituni”
“Ingefaa aje yeye mwenyewe kwa vile taratibu za kazi haziniruhusu kutoa fedha kwenye akaunti ya mtu bila mhusika mwenyewe kuwepo. Hili ni kosa linaloweza kunitupa kifungoni”. Yule meneja wa benki akasisitiza huku akitutazama kwa makini.
“Lakini huo ni mwandiko wake kabisa”. Max akasisitiza.
“Naufahamu vyema mwandiko wake kwa vile nimefanya naye kazi kwa muda mrefu lakini barua tupu namna hii haiwezi kufanikisha upatikanaji wa pesa kwenye akaunti yake”
“Ameniambia nikusihi sana umsaidie. Hivi tunavyozungumza yupo mafichoni na ni matumaini yake kuwa pesa hizi zitamsaidia kutoroka hapa nchini bila kukamatwa na wanajeshi wa mapinduzi”. Nikajaribu kumshawishi yule mzee kwa upole lakini alinitazama kama mtu asiyenifahamu wala kujua habari zangu na hilo halikuwa kosa lake.
“Vijana!. Ni muhimu mkafahamu kuwa kila kazi duniani ina taratibu zake. Kwamwambieni mzee Amara Konneh kuwa ujumbe wake umenifikia lakini nasikitika kusema kuwa hakuna utaratibu wa benki yoyote duniani unaoruhusu mtu fulani kutoa pesa kwenye akaunti ya mtu mwingine eti kwa utambulisho wa barua ya kuandika kwa mkono tena iliyotoka kusikojulikana”. Yule mzee meneja wa benki akaongea kwa dhihaka huku akiangua tabasamu la kifidhuri. Mara moja nikageuka na kumtazama Max aliyesimama kando yangu. Tathmini ikaniambia kuwa Max alikuwa mbioni kukata tamaa ya kufanikiwa kwa mpango wetu.
“Tafadhali tokeni ofisini kwangu, wanajeshi wa Samuel Doe wanaweza kufika hapa na kudhani kuwa mimi nafahamu alipo mzee Amara Konneh na hivyo kuhatarisha maisha yangu. Tafuteni njia nyingine ya kujipatia fedha na siyo hii. Pia ningewashauri msionekane tena hapa mjini kwani mnaweza kukakamatwa na wanajeshi wa mapinduzi”. Yule mzee meneja wa benki akasisitiza huku akijiegemeza kwenye kiti. Maneno ya yule meneja wa benki kwa kweli yalinikatisha tamaa sana na hapo nikaanza kuona dalili za kutokuwa na mazingira rahisi ya kupata msaada. Akili yangu ikaanza kufunguka huku nikiwaza kuwa endapo nisingetia bidii basi suala la kutoroka kwenye nchi ile lingekuwa gumu.
“Mzee Amara Konneh ni rafiki yako?”. Nikavunja ukimya na kumuuliza yule meneja wa benki.
“Ndiyo”. Yule mzee meneja wa benki akaitikia huku akinikata jicho.
“Kama ni rafiki yako kwanini unashindwa kumsaidia?”. Nikamuuliza.
“Urafiki wangu mimi na yeye siyo kigezo cha kuvunja taratibu za ufanyaji wangu wa kazi. Yeye alikuwa waziri katika serikali ya nchi hii lakini kwa sasa hana nafasi yoyote kwani uongozi wa jeshi tayari umeshika hatamu. Mimi bado ni mfanyakazi wa serikali hii, hivyo namna yoyote ya uvunjaji wa sheria na taratibu za kazi unaweza kunifukuzisha kazi na kufungwa jela”. Yule meneja wa benki akaweka kituo na kukohoa kidogo kisha akasogeza kiti nyuma na kusimama.
“Tafadhali naomba mtoke nje kwani sina namna ya kuwasaidia”. Yule mzee akasisitiza huku akitutazama kwa makini. Sikuona tena kama tungepata msaada hivyo nikamsogelea Max na kumnong’oneza.
“Toka nje ukanisubiri kwenye gari. Ukiona hatari yoyote nishtue kwa kupiga mbinja”. Max akataka kutia ukaidi lakini niliwahi kumsukuma ikabidi kwa shingo upande afungue mlango wa ile ofisi na kutoka nje. Yule meneja wa benki akabaki akishangazwa na tukio lile. Max alipotoka nje nikafunga ule mlango kwa ndani na hapo nikachomoa bastola yangu kutoka mafichoni na kuishika mkononi.
“Utanisamehe sana mzee kwa kitendo hiki lakini hakuna namna. Wakati mwingine msaada hulazimishwa badala ya kuombwa”. Nikaongea kwa sauti thabiti huku taratibu nikimsogelea yule mzee na hapo hofu ikamuingia haraka hivyo taratibu akaanza kurudi nyuma huku kijasho chepesi kikimtoka usoni.
“Kijana unataka kunifanya nini?. Nitakuitia polisi sasa hivi”. Yule meneja wa benki akaongea huku akinitazama kwa mashaka.
“Hutopata muda wa kufanya hivyo” Nikamuonya.
“Ukiniua mimi itakusaidia nini?”
“Nahitaji pesa yote kutoka kwenye akaunti ya Mzee Amara Konneh sasa hivi”. Nikasisitiza na mara hii nilikwishamfikia yule mzee pale alipokuwa hivyo nikamkwida shingoni na kumkalisha kwenye kiti chake cha ofisini.
“Unataka kuniua?”. Yule mzee akaniuliza huku akitetemeka.
“Nahitaji pesa yote sasa hivi. Fanya haraka”. Nikafoka huku kasiba ya bastola yangu ikikitazama kichwa chake.
“Fanya lolote utakalo lakini siwezi kukupa pesa kwani ni kinyume na utaratibu wa kazi yangu”. Yule meneja wa benki akasisitiza.
Ilikuwa kauli dhahiri ya utukutu kutoka kwa yule meneja wa benki na kwa kuwa muda haukuwa rafiki nikaishika vyema bastola yangu mkononi na kuvuta kilimi chake kwenye paja la yule meneja wa benki na kwa kuwa bastola yangu ilikuwa na kiwambo maalum cha kuzuia sauti hivyo mambo yalikuwa kimya kimya. Yule meneja wa benki akapiga yowe la uchungu lakini niliwahi kumzuia kwa kumziba mdomo kwa mkono wangu. Nilimuona akifurukuta na kugugumia maumivu na nilipouondosha mkono wangu wangu mdomoni kwake akaanza kuhema hovyo.
“Tafadhali! kijana wangu usiniue nitakupa pesa yote”. Yule meneja wa benki akalainika baada ya kuona nikihamishia bastola yangu na kuilekezea kwenye paja la mguu wake mwingine.
“Fanya sasa hivi vinginevyo zoezi hili litaendelea taratibu hadi umauti wako”. Nikamtahadharisha.
“Sawa nitafanya hivyo. Niachie”
Nilipomuachia yule meneja wa benki haraka akanyanyua kiwambo cha simu yake ya mezani na kuzungusha tarakimu kadhaa huku akitetemeka na jasho likimtoka. Ile simu ilipopokelewa upande wa pili yule meneja wa benki akatoa maelezo fulani kwa mmoja wa wafanyakazi wake. Alipokata simu haukupita muda mrefu mara mlango wa ile ofisi ukasikika ukigongwa. Nikamuweka sawa yule meneja wa benki kana kwamba hapakutokea kitu chochote baina yetu kisha nikatumbukiza bastola yangu kwenye mkanda wa suruali nyuma kiunoni na kwenda kufungua ule mlango.
Akaingia kijana mmoja barobaro mle ndani, mfanyakazi wa benki ambaye pamoja na kumfungulia mlango kijana yule hakujisumbua kunisalimia badala yake moja kwa moja akapitiliza hadi kwenye meza ya ofisini mbele ya yule meneja.
“Una kazi yoyote unaiyofanya muda huu Ben?”
“Sina”. Yule kijana akajibu.
“Naomba utoe pesa zote kutoka kwenye akaunti hii na uniletee hapa sasa hivi”. Yule meneja wa benki akajilazimisha kuongea katika hali ya kawaida.
“Bosi hili ni jambo hatari kulifanya. Hujasikia kuwa waziri Amara Konneh anatafutwa na wanajeshi wa mapinduzi?”. Yule kijana akaongea huku akigeuka na kunitazama wakati alipohamisha macho yake kwenye karatasi yenye jina la akaunti ya mzee Amara Konneh pale mezani.
“Fanya kama nilivyokuagiza. Sasa hivi”. Yule meneja wa benki akafoka. Yule kijana hakutia neno tena badala yake akachukua ile karatasi haraka pale mezani na kutoka mle ndani na wakati akinipita pale mlangoni akageuka na kunipiga ukope wa hadhari. Yule kijana alipotoka nje nikasogea na kuufunga ule mlango kwa ndani kisha nikarudi pale alipoketi yule meneja wa benki ambapo nilisogeza pazia na kuchungulia kwenye ile barabara chini ya lile jengo la benki. Nilimuona Max akiwa ameketi upande wa dereva huku mara kwa mara akitazama sehemu ya mlango wa mbele wa ile benki. Hakuniona lakini bado hali ilikuwa shwari.
_____
MAJIRA YA SAA YANGU YA MKONONI yakaonesha kuwa muda wa nusu saa ulikuwa mbioni kutokomea tangu yule kijana mfanyakazi wa benki aliyeagizwa na meneja kushughulikia fedha alipotoka mle ndani. Wasiwasi ukaanza kuniingia baada ya kuhisi muda ulikuwa ukienda pasipo yule kijana kurudi mle ndani. Kufuatia lile jeraha la risasi yule meneja wa benki sasa alikuwa akitetemeka hovyo kwa kuingiwa na ugonjwa wa ghafla na hali ile ilinitia wasiwasi. Wakati nikifikiria namna ya kukabiliana na hali ile mara nikasikia mlango wa ile ofisi ukigongwa. Niliposogea pale mlangoni na kuchungulia kwenye tundu la funguo nikamuona yule kijana mfanyakazi wa benki akiwa ameshika begi mkononi. Haraka nikafungua mlango na kumruhusu yule kijana kuingia. Yule kijana mfanyakazi wa benki akaingia mle ndani huku amebeba begi la pesa mkononi na kwenda kuliweka juu ya ile meza ya ofisini.
“Unaweza kwenda”. Meneja wa benki akamwambia yule kijana.
“Kuna tatizo lolote bosi?”
“Hapana!”. Lile jibu likampelekea yule kijana mfanyakazi wa benki ageuke na kunitazama kisha akatoka mle ndani na kufunga mlango. Haraka nikasogea pale mezani na kufungua lile begi. Loh! niliona vibunda vya pesa nyingi sana kwenye begi lile lakini wakati nikitafakari namna ya kumalizana na yule meneja wa benki mara nikasikia sauti kali ya breki za gari. Haraka nikasogea dirishani na kutazama chini kule nje. Niliona gari aina ya Landrover ya jeshi la wananchi wa Liberia likisimama ghafla nje ya jengo la benki ile kisha wakaruka wanajeshi wanne na bunduki zao mkononi na kuingia ndani ya ile benki. Haraka nikahisi jambo la hatari hivyo nikarudi pale mezani na kulizoa lile begi la pesa.
“Unajidanganya bure kukimbia kijana kwani hutofika mbali”. Yule meneja wa benki akanionya huku akijitahidi kutabasamu katikati ya maumivu makali ya jeraha la risasi pajani.
“Funga mdomo wako”. Nikamfokea yule mzee meneja wa benki na kumchapa kofi la usoni kisha nikaharakisha na lile begi la pesa kueleka mlangoni. Loh! sikufanikiwa kwani nilisikia sauti ya vishindo vya buti za wale wanajeshi kupanda ngazi za korido kuja kwenye ule mlango wa ile ofisi ya meneja. Kijasho chepesi kikanitoka. Sikuwa na namna ya kufanya bali kugeuza haraka na kurudi kule dirishani na hapo haraka nikasogeza pazia kando na kuchungulia nje.
Nikamuona Max akiwa anatazama kwenye mlango wa ile benki. Nikashangazwa kidogo na tabia ile kwani Max hakunipigia mbinja baada ya kuwaona wale wanajeshi wakiingia mle ndani kama tulivyokubaliana hapo awali. Jibu sikupata lakini vilevile sikutaka kusubiri kitakachoendelea. Hivyo kwa kutumia kitako cha bastola yangu mkononi nikapiga pigo moja makini na kukisambaratisha kioo cha dirisha la ile ofisi kisha nikachungulia kule nje. Loh! hapakuwa na sehemu ya kukanyagia endapo ningeamua kutoroka kwa kupitia lile dirisha. Chini usawa wa lile dirisha kulikuwa na magari yaliyoegeshwa na watu wachache eneo lile hivyo sikushawishika kuruka kwa kuhofia kuwa raia wa eneo lile huwenda wangenitegea vibaya na kuzuia harakati zangu za kutoroka.
Hivyo nikamshtua Max kwa kupiga mbinja kali pale dirishani. Max akashtuka haraka na kunitazama pale juu na hiyo ikawa nafasi yangu nzuri ya kumrushia lile begi la pesa. Akalidaka kwa ustadi wa hali ya juu kwenye gari dirishani. Nilipogeuka pale mlangoni zile sauti za vishindo vya hatua za wale wanajeshi tayari zilikuwa nje.
Kufumba na kufumbua ule mlango ulipigwa teke moja la nguvu ukafunguka bila kupenda kisha mwanajeshi mmoja hatari akaingia mle ndani kwa mtindo wa sarakasi huku bastola yake mkononi. Tayari nilikuwa nyuma ya mlango hivyo wakati akisimama nikamsindikiza kwa teke moja hatari la mgongoni lililomtupa kwenye sefu moja ya chuma na kujipigiza vibaya. Mwenzake akaingia kichwa kichwa huku mtutu wa bunduki yake Smg kautanguliza mbele. Nikamchapa teke la kifua lililomrudisha nje na kumtupa chini pale mlangoni. Muda uleule nikasikia sauti mbaya ya risasi iliyofyatuliwa kunilenga na mwanajeshi mmoja kati ya wale wanajeshi wawili waliosalia pale nje mlangoni. Nikawa kujitupa chini hivyo ile risasi ikachana anga na kutokomea dirishani. Wakati yule mwanajeshi akijiandaa kunichapa risasi nyingine nikamuwahi na kumlaza chali kwa risasi yangu moja ya kifuani. Mwenzake kuona vile akapaniki na kuingia mle ndani mzimamzima huku akifyatua risasi hovyo mle ndani. Wenzake pamoja na yule meneja wa benki wakapiga mayowe ya hofu kufuatia ile taharuki. Hakutabaruku zaidi yule bwege nikamtuliza kwa risasi ya shingo iliyomtupa sakafuni.
Yule mwanajeshi aliyeangukia kwenye sefu ya chuma ya mle ndani akajizoazoa na kusimama lakini nilimrudisha chini kwa pigo hatari la teke la shingo akaanguka na kuzirai palepale. Hivyo mle ndani tukabakia mimi, yule mwanajeshi niliyemchapa teke la kifuani na meneja wa ile benki ambaye hadi kufikia pale alikuwa akiniogopa kama bomu la kutegwa kwa mkono. Yule mwanajeshi akajitahidi kusimama pale chini lakini pigo langu lilikuwa limemtia udhaifu mkubwa. Hakufanikiwa kusimama akapiga mwereka chali huku akikohoa hovyo na kujishika kifuani.
“Kwa herini Mungu akipenda huwenda tukaonana tena japo mna roho mbaya sana”. Nikawaambia lakini hakuna aliyeniitikia badala yake wote wakanitazama kwa hofu. Bastola yangu nikaichomeka nyuma kiunoni na kutoka nje ya kile chumba. Loh! lakini wakati nikishuka ngazi kuelekea sehemu ya chini ya ile benki nikaona kikosi cha wanajeshi nane wameingia ghafla mle ndani na kupewa maelekezo kutoka kwa raia mmoja aliyekuwa akiwaelekeza kule juu. Nikasita na kugeuza nikirudi kule juu nilipotoka lakini mwanajeshi mmoja alikuwa tayari ameniona akaanza kunifyatulia risasi ambazo ama kwa hakika nilizikwepa na kutokomea mbele.
Kabla sijafika mwisho wa ile korido nikaona korido nyingine upande wa kulia nikachepuka na kukimbiaa nikiifuata korido ile ambayo ilinifikisha nje ya mlango uliokuwa mwishoni. Nikaurukia kwa miguu yangu miwili na kuusambaratisha ule mlango nikitokezea ndani ya kile chumba. Loh! nilikuwa nimetokezea kwenye ukumbi mkubwa na mle ndani kulikuwa na wafanyakazi wakiendelea na mkutano.
Watu wale wakataharuki sana na kupiga mayowe lakini niliwapuuza huku tayari nimeshika bastola yangu mkononi. Madirisha ya ule ukumbi yalikuwa wazi hivyo nikasimama na kutimua mbio hadi kwenye dirisha moja la ukumbi kisha nikajirusha kwa mtindo hatari wa komando na kuangukia nje. Huko nikasimama na kuanza kutimua mbio nikirudi mbele ya ile benki. Loh! nilipofika nikashikwa na mshtuko lile gari tulilokuja nalo na Max halikuwepo wala sikumuona Max eneo lile na hapo nikaishiwa nguvu na kukata tamaa huku nikiendelea kushangaa shangaa. Niliona gari lingine Nissan Patrol la jeshi likisimama nje ya ile benki kisha wakashuka wanajeshi sita na bunduki zao mkononi. Mmoja ambaye nilimtambua kwa cheo cha Kapteni akakimbilia mle ndani ya benki na bastola yake mkononi na wale wanajeshi wanne waliosalia, wawili kati yao wakashika uelekeo wa upande wa kushoto na wengine wawili wakishika uelekeo wa upande wa kulia kulizunguka lile jengo wakija usawa wangu kule nilipokuwa.
Kuona vile nikageuza na kuanza kutimua mbio kuelekea kwenye ukuta wa nyuma wa kuizunguka ile benki. Nilipoufikia ule ukuta nikaurukia juu na kuangukia upande wa pili huku risasi za wale wanajeshi nyuma yangu zikinikosakosa.
Nje ya ule ukuta nilipoangukia nikajikuta uani sehemu iliyoanikwa nguo kwenye nyumba kuukuu yenye mlango wazi katika korido ndefu inayotokezea upande wa pili wa ile nyumba. Nikasimama na kuanza kutimua mbio huku nikichechemea nikitaisha kwenye korido ile na hapo nikamkumba mama mmoja na kumtupa chini hata hivyo sikusimama. Mbele ya ile nyumba kulikuwa watu wameketi kutia soga nikakatisha kati yao na kusababisha taharuki ya aina yake. Upande wa kushoto nikaona ukuta dhaifu nikauruka ukuta ule kama mchezo na kuangukia kwenye kichochoro kilichofanywa baina ya kuta mbili za nyumba zinazopakana kuelekea kwenye barabara ya mtaa wa pili. Muda mfupi nikawa nimetokezea upande wa pili wa kile kichochoro na kukutana na barabara ya lami yenye pilika za watu na magari hapo nikapunguza mwendo na kujichanganya kati yao huku nikitembea kwa tahadhari huku nikishindwa kuamini kuwa Max alikuwa ameniacha solemba na lile begi la pesa.
Wakati nikifika mwisho wa ile barabara nikakumbuka kugeuka nyuma na mara hii nikashtuka. Kiasi cha umbali wa mita hamsini nyuma yangu niliona kikosi cha wanajeshi zaidi ya kumi wakitimua mbio kunifukuza na hali ile ikazua taharuki kwani kila mtu alianza kutimua mbio akishika uelekeo wake. Kuona vilevile na mimi nikaanza kutimua mbio, mbio kali za jasusi. Kuona vile wale wanajeshi wakaanza kufyatua risasi hovyo kunilenga lakini sikuwa mzembe kiasi kile.
Mwisho wa barabara ya ule mtaa nikaingia upande wa kushoto kuifuata barabara nyingine na baada ya mbio fupi nikawa nimefika kwenye soko lenye msongamano wa watu. Nilipogeuka kutazama nyuma nikaona wale wanajeshi bado walikuwa wakiniandama hivyo nikachomoa bastola yangu na kufyatua risasi mbili hewani. Watu wakataharukia na kuanza kutimua mbio kila mtu na uelekeo wake hivyo nikajichanganya kati yao na kushika uelekeo wangu lengo langu likiwa kuwapoteza kabisa wale wanajeshi waliokuwa wakinifukuza nyuma yangu.
Nilipovuka soko nikaingia upande wa kulia kuifuata barabara ya Lynch Street huku nikipishana na magari machache na watembea kwa miguu. Haukuwa mtaa wenye msongamano sana kwa vile maduka mengi ya mtaa yalikuwa yamefungwa. Wakati wote nikitembea sikuacha kugeuka nyuma katika kujihakikishia usalama wangu. Mwisho wa ule mtaa nikakutana na barabara kubwa ya Broad Street iliyokuwa ikitoka upande wa magharibi kuelekea mashariki ambayo mbele yake ingekutana na barabara kubwa ya Haile Selassie Avenue.
Niliwaona wanajeshi wa Samuel Doe katika barabara ile nyuma ya vizuizi vya barabara na hapo nikaiona miili kadhaa ya watu waliouwawa kwa kupigwa risasi na kutelekezwa barabarani. Kuona vile nikaghairi kushika uelekeo wa magharibi hivyo nikavuka barabara ile na kunyoosha nikikatisha katikati ya majengo marefu ya ghorofa huku nikitembea kwa tahadhari. Nilipopita jengo la bekari kubwa ya mikate la Monrovia Sweet Breads & Snacks nikaingia upande wa kulia kuifuata barabara ya mtaa wa Ashmun. Nilipofika mbele nikavuka barabara ya United Nations Drive nikiambaa na ukuta wa Access Bank kisha nikakata vichochoro hadi nilipotokezea kwenye barabara Slipway Road iliyokuwa kandokando ya Mto Mesurado.
Kufikia pale nikapunguza mwendo baada ya kujiridhisha kuwa hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa akinifuatilia nyuma yangu kwani wale wanajeshi nilishawapoteza nyuma yangu. Hata hivyo sikuona kama lilikuwa jambo salama kutembea kandokando ya barabara ile hivyo nikaachana nayo na kutokomea vichochoroni hadi nilipotokezea kwenye ufukwe wa Mto Mesurado sehemu yenye vibanda vya makuti vya kupumzikia wavuvi na baa za daraja la kati. Niliona boti na mitumbwi mingi iliyotia nanga kwenye ufukwe ule pamoja na soko la samaki. Nikatembea kwa utulivu nikifurahishwa na mandhari yale na baada ya kupita soko la samaki nikaona baa moja iliyojitenga. Nje ya baa ile kulikuwa na meza na viti vya plastiki chini ya miavuli mikubwa ya Cocacola. Ilikuwa sehemu yenye utulivu na upepo mwanana yenye watu wachache hivyo nikatafuta meza moja iliyojitenga na kuketi. Msichana mhudumu wa eneo lile alipokuja kunisikiliza nikaagiza ugali wa mboga za majani na kambare wa kukaanga pamoja na bia moja baridi ya Club Beer kwa ajili ya kujituliza na jua kali la fukuto la mchana ule.
Angalau sasa nilikuwa nimepata mahali tulivu pa kupumzisha akili yangu. Wakati nikisubiri mlo nilioagiza nikajikuta mawazo yangu yakihamia kwa Max na mara hii sikutaka kabisa kuamini kuwa Max alikuwa ameniacha solemba na kutoroka na lile begi la pesa. Kufikia pale sasa niliamini kuwa Max alikuwa amehusika kikamilivu katika kuniuza kwa wale wanajeshi kule benki na ndiyo maana hakujishugulisha kupiga mbinja wakati wanajeshi wale walipokuwa wakivamia benki kunikamata. Loh! nikamshukuru Mungu kwani kama nisingekuwa makini na kuchungulia dirishani chini ya ile benki wakati niliposikia breki kali ya gari la jeshi basi yumkini kabisa muda ule ningekuwa nakipata cha mtemakuni kutoka kwa wanajeshi wa Samuel Doe kama siyo kuuawa kabisa. Mawazo yale yakanipelekea nijihisi mnyonge sana kwa kuzidiwa kete na mtu niliyemdharau. Moyo wangu ukaanza kunisukuma nimtafute Max kwani vinginevyo hakuna kitu chochote ambacho kingeweza kufanyika. Lakini nitawezaje kumtafuta Max wakati nilikuwa mgeni kabisa katika jiji la Monrovia lenye historia mbaya barani Afrika?. Nikajiuliza na jibu sikupata.
Ugali ulipoletwa nikanawa mikono na kuanza kujipatia mlo huku mara kwa mara nikishushia na mafunda ya Club Beer, bia maarufu sana nchini Liberia. Ingawa macho yangu yalivutiwa sana na mandhari ya ufukwe ule wa mto wenye pilika nyingi za wavuvi lakini akili yangu ilikuwa kazini kama moyo usukumavyo damu kwenye mwili wa kiumbe hai yoyote hapa duniani. Kumbukumbu juu ya Mariama na wazazi wake kule mafichoni msituni iligeuka kuwa mwimba mkali kwenye nafsi yangu. Ni dhahiri kuwa matumaini yao yote yalikuwa juu yetu, yaani mimi na Max. Lakini sasa kufuatia pesa zile kuibwa na Max safari yetu ya kutoroka pale Liberia ilikuwa hatarini.
Nilipoendelea kuwaza nikajikuta nikitaka kushawishika kurudi kule mafichoni msituni na kuwaeleza Mariama na wazazi wake namna Max alivyonisaliti na kutoroka na pesa zote. Lakini nilipopisha tafakuri vizuri kichwani mwangu nikaamua kuachana na mpango huo kwani kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kutokuaminika kama siyo kuonekana fala.
Ingawa nilikuwa na kiasi kidogo cha pesa niliyokuwa nimepewa na baba yake Mariama kabla ya kuanza safari kule mafichoni msituni, kama pesa ya dharura lakini sikuona kama lilikuwa jambo la busara kurudi kule msituni mafichoni bila zile pesa zilizoibwa na Max. Baada ya kufikiri sana nikawa nimepata wazo jipya.
_____
AMRI KUTOKA KWA SERIKALI YA MAPINDUZI ya kijeshi pale nchini Liberia ilikuwa imekataza mtu yeyote kutembea mitaani mara baada ya kutimia saa kumi na mbili na nusu jioni. Hivyo kwa kukwepa misukosuko isiyo ya lazima, ilipotimu saa tisa na nusu alasiri nikalipa bili ya chakula na kinywaji na kuachana na ule ufukwe wa Mto Mesurado nikielekea mjini. Jioni hii niliamini kuwa wale wanajeshi waliokuwa wakinisaka baada ya kuwatoroka kule benki wangekuwa tayari wamekata tamaa ya kunipata na hivyo kuendelea na hamsini zao.
Nilipotoka kwenye ule ufukwe wa Mto Mesurado nikatembea kwa miguu hadi barabara ya King Sao Bosso Street. Njiani nikanunua jaketi zito kwa ajili ya kujikinga na baridi. Nilipofika mwisho wa barabara ile nikajihisi kutaka kupotea kwa vile nilivyokuwa mgeni wa jiji lile hivyo nikaamua kukodi teksi nje ya hoteli ya Ocean View. Dereva mmoja kijana wa makamo machachari akaniwahi na kunikaribisha kwenye teksi yake na mimi bila kupoteza muda nikafungua mlango wa nyuma na kuingia na kumtaka yule dereva anifikishe eneo la West Point pembeni ya kiwanda cha kusaga nyama ya ng’ombe. Muda uleule teksi ikaacha maegesho yake na kuingia barabarani.
Tuliwasili eneo la West Point ndani ya nusu saa baada ya dereva yule kufanya umakini katika kukwepa barabara zenye vizuizi vya barabarani. Teksi iliposimama nje ya kiwanda cha kusaga nyama cha Monrovia Fresh Beef Canning, nikamlipa yule dereva pesa yake na kushuka na hapo nikashika uelekeo wa kaskazini wakati teksi ile ilipogeuza na kurudi mjini.
West Point kilikuwa kitongoji kilichopakana na bahari ya Atlantiki kwa upande wa magharibi, chenye mchanganyiko wa makazi ya watu. Baadhi ya maaneo yalipendeza kwa majengo mazuri ya ghorofa na makazi yenye mpangilio wa barabara safi. Kwengineko kulitia kinyaa kwa makazi duni ya watu na madampo ya takataka ngumu zinazotoa harufu kali katikati ya barabara. Yasemekana kuwa maeneo hayo ndiyo kulikokuwa na biashara kubwa ya ngono ya bei rahisi kwa wasichana wadogo lakini hilo siyo lililonifisha pale.
Kupitia maelezo ya Mariama wakati tukiwa kule mafichoni msituni ni kuwa John Varma, yule dereva aliyefika kutupokea kule kiwanja cha ndege na Mariama alikuwa akikaa nyumba namba 102, floo ya nne katika jengo la ghorofa sita la shirika la nyumba la taifa la Liberia. Baada ya tafakuri ndefu nikawa nimepata wazo kuwa John Varma angeweza kuwa mtu muhimu sana katika kunisaidia sehemu nitakayoweza kumpata Max. Kwa vile alivyokuwa mtu wa karibu sana na familia ya ...... wiki ijayo
 
RIWAYA: MTUTU WA BUNDUKI
SEHEMU: 7
_____

ILIKUWA TAYARI IMEKWISHATIMIA saa tano na robo usiku wakati nilipowasili kwa mara ya pili nyumbani kwa John Varma, nyumba namba 102 eneo la West Point kandokando ya jiji la Monrovia. Baada ya kumkosa jioni ile nilikuwa nimeamua kutafuta baa ya karibu na eneo lile ambapo nikiwa humo niliburudika na kauli nzuri za wadada warembo waliovaa sketi fupi wenye maumbo na sura za kuvutia, wahudumu wa baa ile iliyokuwa mtaa wa pili nyuma ya mtaa aliokuwa akiishi John Varma. Lengo langu hasa likiwa ni kupoteza muda wakati nikiendelea kumsubiri John Varma huko alipokuwa ameenda arejee nyumbani. Sasa nilikuwa mbali na kelele za muziki wa baa ile na maongezi ya walevi ambayo mengi yalijikita katika kuzungumzia mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika pale Liberia usiku wa jana.
Mara hii niliutazama mlango ule wa nyumba namba 102 katika ghorofa ya nne huku nikiwa nimezama kwenye tafakuri. Shauri langu sasa lilikuwa ni katika kutaka kufahamu kama John Varma angekuwa tayari amerudi mle ndani au lah!. Usiku huu nyumba zote katika korido ile zilikuwa gizani na zaidi ya pale utulivu wa eneo lile ulinitia wasiwasi. Usiku huu mvua ilikuwa imeanza kunyesha na kama siyo jaketi nililolinunua njiani wakati nikija pale kwenye kitongoji cha West Point huwenda ningekuwa nikitaabika vibaya na baridi ile kali ya usiku.
Kwa tahadhari nikatega sikio langu pale mlangoni kujaribu kusikia sauti ya kitu chochote mle ndani lakini hapakuwa na kiashiria chochote cha uwepo wa mtu le ndani na hali ile ilinishangaza sana. Nikasogea na kujaribu kuchungulia mle ndani kupitia dirishani hata hivyo sikuambulia kuona chochote kwa vile giza zito lilivyokuwa limenawiri mle ndani. Kilipita kitambo kifupi nikiichunguza ile nyumba kwa makini kisha nikaanza kugonga pale mlangoni. Mara hii nilikuwa makini zaidi katika kugonga kwa kukwepa kuwashtua majirani au mtu yeyote ambaye angekuwa eneo lile. Hata hivyo pamoja na ufundi wangu wote wa kugonga lakini sikujibiwa. Nilipogonga kwa zaidi ya mara nne bila ya kujibiwa nikahisi ni kama niliyekuwa nikipoteza muda. Hivyo kwa msaada wa funguo zangu za kazi nikafyatua kitasa cha mlango ule na kuzama ndani taratibu huku bastola yangu tayari ikiwa mkononi.
Mara baada ya kuingia mle ndani na kuufunga ule mlango nyuma yangu nikasimama kwa utulivu kuishughulisha milango yangu ya fahamu. Kwa kufanya vile nikasikia kelele za muungurumo wa jokofu na mshale wa saa ya ukutani iliyokuwa imetundikwa sehemu fulani katika sebule ya ile nyumba. Sikuhisi mjongeo wowote wa kiumbe hai wala sauti ya mkoromo wa mtu aliyeko usingizini hivyo nikachukua kurunzi kutoka kwenye mfuko wa koti langu na kuiwasha nikianza kumulika mle ndani.
Nilikuwa nimetokezea kwenye sebule kubwa ya nyumba ile. Niliona seti moja ya makochi ya mbao yenye mito kuizunguka meza fupi ya mti wa mkaratusi katikati ya sebule ile. Upande wa kulia niliona kabati kubwa la vyombo vya dongo pembeni ya mlango wazi kuelekea kwenye ukumbi mdogo wa kulia chakula wenye meza ya umbo duara iliyozungukwa na viti sita. Nilipofika katikati ya ile sebule upande wa kushoto nikaona korido fupi iliyokuwa ikipakana na milango mitatu ya vyumba. Nilipofika pale nikasimama na kuupima utulivu. Bado sikuweza kusikia sauti ya kitu chochote hivyo nikapiga hatua zangu kwa tahadhari kupeleleza ule ukumbi wa chakula uliopakana na dirisha dogo linalotazama na chumba cha jiko kwa upande wa kulia.
Sikuona kitu chochote hivyo nikarudi pale sebuleni na kuanza kupeleleza kwa makini zaidi. Kwa kufanya vile nikaiona simu ya mezani juu ya stuli iliyofunikwa kwa kitambaa cha kufuma kwa mkono kwenye kona ya sebule ile. Ukutani nikaona picha nzuri za kuchora kwa mkono na nyingine zikimuonesha John Varma akiwa katika maeneo tofauti. Kulikuwa na redio ndogo ya bendi sita ya Hitach katika meza ndogo ya mapambo yenye ua dogo la kitenge. Mandhari yale yalikuwa safi na tulivu sana.
Hatimaye nikaondoka eneo lile kwa tahadhari na kuifuata ile korido ya kuelekea vyumbani huku bastola yangu ikiwa mkononi. Loh! sikuwa nimeona vizuri gizani hivyo nikajikwaa kwenye kona ya korido ile mahali kulipokuwa na ndoo ya bati. Ile ndoo ikajigonga ukutani na kusababisha ukulele mle ndani. Nikashtuka sana na kuzima kurunzi yangu mkononi huku nikisikiliza. Kikapita kitambo kirefu bila mtu yoyote kujitokeza kwenye ile korido na hapo nikapata mashaka kuwa huwenda mle ndani hapakuwa na mtu. John Varma alikuwa bado hajarudi nyumbani kwake?. Nikajiuliza bila kupata majibu.
Hata hivyo nilitaka kupata hakika juu ya hisia zangu hivyo nikaanza tena kunyata kuelekea vyumbani kufanya uchunguzi. Sikufika mbali mara nikahisi nyuma yangu kulikuwa na mtu. Hofu ikanimeza haraka huku kijasho chepesi kikininyemelea maungoni. Mara hii nikapanga kugeuka haraka kwa hila lakini sikufanikiwa kwani nilijikuta nikitulizwa kwa mkuno wa chuma baridi kisogoni.
“Usijaribu kuleta hila yoyote John. Tupa bastola yako chini tafadhali!”. Sauti kavu ya mwanaume kutoka nyuma yangu ikanionya.
“Wewe ni nani?”. Nikamuuliza yule mtu nyuma yangu.
“Paye Dolo. Nimekuwa humu ndani nikikusubiri kwa muda mrefu”
“Ulikuwa unanisubiri mimi?”. Nikamuuliza yule mtu baada ya kugutuka kuwa alikuwa amechanganya mahesabu.
“Ndiyo. Nilikuwa nakusubiri wewe kwa muda mrefu humu ndani hadi nikaanza kukata tamaa kuwa umekwishatokomea. Lakini Mungu siyo Athumani kwani hatimaye umeingia kwenye kumi na nane zangu”. Yule mtu nyuma yangu akajigamba.
“Unasema ulikuwa humu ndani ukinisubiri kwani mimi na wewe tulipeana miadi ya kuonana?”. Nikamuuliza yule mtu huku taratibu nikigeuka kumtazama lakini sikufanikiwa kwani kabla sijafanikiwa vizuri kugeuka nikashtukia nikichapwa kofi baya shingoni na hapo moto wa maumivu ukasambaa haraka shingoni.
“Sasa mbona unanipiga?”. Nikamuuliza yule mtu.
“Sijakwambia ugeuke nyuma kwanini ujitie kiherehere?”
“Okay, samahani sana mkuu lakini bado hujanijibu swali langu”
“Swali gani?”
“Kama tumepeana miadi hadi ulalamike kutumia muda mrefu kunisubiri humu ndani”
“Acha maswali yasiyo na msingi wewe tumbili”. Yule mtu nyuma yangu akanionya huku akianza kunipekua mwilini. Alipomaliza akafanikiwa kuchukua bastola yangu.
“Una shida gani na mimi hadi univamie kibabe namna hii?”. Nikamuuliza yule mtu na mara hii nikagundua kuwa alikuwa hamfahamu vizuri John Varma. Ni kama alikuwa ametumwa kumshughulikia mtu asiyemfahamu vizuri kwani vinginevyo alipaswa kutofautisha sauti yangu na ya John Varma.
“Idara yetu ya ujasusi inakuhitaji”. Yule mtu akavunja ukimya.
“Ndiyo mnivizie ndani kwangu usiku wote huu kwani simu yangu hamuijui?”. Nikamuuliza yule mtu nikijitia mimi ndiye John Varma.
“Tumekuwa tukipiga simu yako mara kwa mara lakini haipokelewi”
“Sikuwepo nyumbani”
“Na ndiyo maana nikaamua kukufuata mwenyewe hapa kwako John”
“Idara ya ujasusi inanihitaji kwa jambo gani?”
“Utusaidie kutueleza mahali alipo mzee Amara Konneh”
“Sifahamu alipo”
“Com on, acha kudanganya John, hakuna yoyote anayeweza kukuamini kwa maneno yako. Kama hutozungumza ukweli idara haitalaumiwa kwa kifo chako”. Yule mtu akanionya huku akivuta kilimi cha bastola yake kuiruhusu risasi kuingia kwenye chemba.
“Mnadhani kuniua mimi ndiyo utakuwa ufumbuzi wa haja yenu?”
“Huwenda lisiwe suluhisho lakini angalau hutoweza kutudanganya tena”
“Kwani nimewadanganya nini?”
“Mara hii umesahau kuwa wewe ndiye uliyetuhakikishia kuwa Amara Konneh na familia yake pamoja na yule kijana mgeni wangekuwa wamekimbilia Gissie na kumbe siyo kweli?”
Maelezo ya yule mtu nyuma yangu yakanizindua, akili yangu ikaingiwa na taharuki baada ya kung’amua kuwa JohnVrama ndiye aliyewaelekeza wale wanajeshi kutuwekea mtego wa barabarani usiku wa jana wakati tukitoroka kuelekea Gissie. Kwa kweli nilijihisi kuishiwa nguvu.
“Lakini mimi sikuwadanganya?”. Nikajitahidi kujitetea.
“Huwenda ukawa na nafasi nyingine ya kujitetea lakini hapa siyo mahala pake. Nimetumwa kukukamata na kukufikisha kwa wakuu”
“Kwa kosa gani nililofanya?”
“Hata mimi sijui”. Yule mtu nyuma yangu akanikata kauli kisha kwa wepesi usioelezeka mikono yangu ikashikwa na kuzungushwa kwa mtindo wa ajabu na wakati nikitaka kufurukuta tayari nikajikuta nimeshapigwa pingu mikononi. Paye Dolo alikuwa mtu hatari wa kuogopwa kwa namna alivyofanikiwa kunidhibiti kwa kasi ya umeme wa radi. Kisha akanisukuma na kunitanguliza mbele huku kasiba ya bastola yake ikikodolea macho kisogo changu kwa nyuma.
Sasa tulikuwa tumebadili uelekeo. Paye Dolo alikuwa nyuma yangu akiniongoza kuelekea nje na hapo nikajua kuwa kulikuwa na mipango kamambe ya kuniteka na kunifikisha huko kwa wakuu wake wa kazi. Kwa kweli sikuwa tayari kufikishwa popote na kwa mtu yoyote usiku ule, iwe kwa watu salama au wasio salama. Hivyo wakati nimetangulizwa mbele nikawa makini sana kufanya tathmini juu ya mazingira mazuri ya kuchoropoka kwenye mtego ule.
Sasa tulikuwa karibu kuufikia ule mlango wa sebule kuelekea nje. Kuona vile nikakusanya nguvu kisha kwa tukio hatari la kushtukiza, kufumba na kufumbua nikajitupa ukutani na kukita miguu yangu kisha nikajitupa kunyumenyume na kumvamia Paye Dolo nyuma yangu. Kwa nguvu ile niliyoitumia sote tukapiga mweleka na kuanguka chini. Lakini kwa mimi ambaye nilikuwa nimefungwa pingu mikononi tukio lile lilikuwa hatari zaidi. Bastola ya Paye Dolo ikamponyoka mkononi na kuangukia kusikojulikanana huku na mimi nikijiviringisha kando. Paye Dolo naye kuona vile akajiviringisha sakafuni kunifuata huku akinitupia mapigo hatari ya kareti na mateke kunishambulia. Hata hivyo aliambulia patupu kwani mchezo wa gizani niliupenda sana kwa vile ulimpunguzia adui umakini. Nikaendelea kujiviringisha hadi kwenye kona ya sebule ile hapo nikaukita mguu wangu kisha nikajibetua kwa mtindo hatari wa sama soti kusimama.
Loh! ilikuwa kabla sijapata mhimili vizuri Paye Dolo akanichapa teke hatari la tumbo lililonivuruga vibaya na kunitupa nyuma. Nikaangukia kwenye kochi moja la pale sebuleni na kulivunja vipandevipande huku maumivu makali yakisambaa mwilini. Hata hivyo nikawahi kujizoazoa pale chini na kusimama. Paye Dolo akanifikia tena, akatupa ngumi tatu makini kichwani lakini nilizikwepa kama mchezo na hivyo zikakata upepo na kumpunguza nguvu. Kuona vile Paye Dolo akabadili mtindo na kunitupia pigo baya la kareti shingoni, pigo lile likanipunyua kidogo lakini nikafanikiwa kulikwepa. Kisha nikakusanya nguvu na kumtandika kichwa cha pua na kuupasua vibaya mwamba wa pua yake huku akipiga mweleka mbaya na kuanguka chini. Nikamuwahi pale chini na kumchapa teke la korodani na hapo akapiga mguno na kubweka kama mbweha lakini aliwahi kusimama na kunijia kwa kasi ya kimbunga.
Nilijaribu kumzuia lakini sikufanikiwa na hapo nikajikuta nikichapwa pigo baya la kareti mbavuni na maumivu yake yakanipelekea niachie mguno mkali wa maumivu. Nikayumba hovyo nikirudi chuma na kabla sijapata mhimili vizuri Paye Dolo akanichapa teke la kifua lililonitupa chini na kunilambisha sakafu. Kwa kweli nilisikia maumivu makali sana kifuani kama niliyepigwa na tofali huku nikikohoa hovyo. Paye Dolo hakuniacha na mara hii akaongeza kasi zaidi akinijia kwa mapigo ya mateke ya haraka ambayo nilijitahidi kwa kila namna kuyapangua kwa mikono yangu iliyofungwa pingu.
Nilipohisi kuwa Paye Dolo alikuwa mbioni kuishiwa nguvu nikajitupa sakafuni kumfuata na kabla hajaishtukia hila ile nikazungusha mguu wangu sakafuni na kumchota mtama uliompaisha vibaya hewani. Alipoanguka chini akatua juu ya ile meza fupi ya pale sebuleni na kuivunja vipandevipande. Kiuno chake kikapata hitilafu huku mkono wake mmoja ukivunjika vibaya na hapo akapiga yowe kali la maumivu. Paye Dolo hakuwa na namna ya kufanya hivyo haraka akachomoa kisu kiunoni kwake na kunitupia lakini hakuwa na shabaha makini hivyo kisu kile kikanikosa na kwenda kukita kwenye mbao ya juu ya dirisha.
Kisu cha alichonirushia almanusura kinipate kifuani lakini nikawahi kukikwepa kisha nikajitupa chini kujiviringisha kumfuata katika mtindo wa zigizaga hali iliyompelekea ashikwe na kiwewe katika namna ya kunidhibiti. Wakati akiendelea kushangaa nilipomfikia nikamchapa teke la tumbo na alipoanguka chini nikamrukia na kumtundika kabari ya miguu ya mtindo wa judo. Paye Dolo akajitahidi sana kufurukuta kwa vile alikuwa ni mtu mwenye nguvu nyingi hivyo tukaanza kuepelekana huku na kule hata hivyo sikumuachia.
Kumdhibiti mtu mwenye nguvu kama Paye Dolo ilihitajika kazi ya ziada hivyo nguvu zikaanza kuniishia. Nilipoona anakaribia kuchomoka kwenye kabari ile matata nikamuongezea kabari nyingine ya shingoni nikitumia pingu zangu mkononi na mara hii sikumpa Paye Dolo nafasi ya kuomba maji kwani niliikaza mikono yangu kisawasawa. Jicho likamtoka pima kama mjusi aliyebanwa na mlango, mishipa ya kichwa ikamtuna huku jasho likimtoka. Nilikuwa nimemdhibiti vizuri hivyo akaanza kutupa mikono na miguu yake huku na kule kujitetea. Hivyo pakatokea patashika ya aina yake pale sebuleni lakini sikumuachia. Hali ilipozidi kuwa mbaya Paye Dolo akajitutumua na kusimama na mimi huku nimemng’ang’ania shngoni kisha akanibwaga chini. Sote tukaanguka chini lakini bado sikumuachia kwani kabari yangu ilikuwa ni zaidi ya tumbili aliyenasa kwenye mtego wa nyati.
Muda mfupi baadaye nikamuona Paye Dolo akianza kuishiwa nguvu na kupunguza kutapatapa pale sakafuni nilipomng’ang’ania na hatimaye akatulia. Bado sikumuachia hadi pale nilipojiridhisha kuwa tayari alikwisha kata roho. Taratibu nikaondoa ile kabari ya pingu shingoni mwake na kujitupa kando huku nikihema hovyo kutafuta pumzi iliyokuwa mbioni kuniishia. Mikononi nilisikia maumivu makali sana kwani vifundo vya viganja vyangu vilikuwa vimechubuka vibaya kufuatia ile kabari niliyomtundika Paye Dolo shingoni.
Niliendelea kujilaza pale sakafuni kwa kitambo hadi pale hali yangu ilipoanza kuwa nzuri hapo nikasimama na kumsogelea Paye Dolo pale chini alipolala. Nilipompekuwa mifukoni nikamkuta na funguo za ile pingu aliyonifunga mikononi hivyo nikachukua ile funguo na kufungua ile pingu nikiitupilia sakafuni pale sebuleni. Kisha nikaendelea na upekuzi wangu mifukoni mwake. Nilipomaliza upekuzi ule nikawa nimefanikiwa kumfahamu vizuri Paye Dolo kuwa ni mtu wa namna gani.
Kupitia kitambulisho chake nilichokikuta kwenye wallet yake ya ngozi ya nyegere kwenye mfuko wa nyuma wa suruali yake ya dengrizi nikagundundua kuwa Paye Dolo alikuwa shushushu au afisa usalama kutoka katika idara kuu ya ujasusi ya taifa ya pale Liberia iliyofahamika kwa jina la NSA-National Security Agency. Serikali ya mapinduzi ya kijeshi iliyojitwalia madaraka kwa mapinduzi ya kijeshi baada ya kuvamia Ikulu na kumuua rais William Tolbert ilikuwa imemtuma kumtafuta John Varma, dereva wa aliyekuwa waziri wa ulinzi, mzee Amara Konneh. Baada ya kukosa kumkamata mzee Amara Konneh, jitihada zilikuwa zimeelekezwa katika kumtafuta John Varma kama mtu wa karibu wa mzee Amara Konneh ambaye angeweza kuwafahamisha mahali alipo. Bahati mbaya sana Paye Dolo baada ya kuandaa mtego wake mle ndani nikawa nimenasa mimi na siyo John Varma, mtu aliyekuwa amemkusudia. Hii ilimaanisha kuwa Paye Dolo aliwahi kufika na kuingia mle ndani kwa siri kisha akajificha na kumsubiri John Varma ajitokeze. Niliwaza.
Baada ya kumaliza kufanya upekuzi wangu mle ndani bahati mbaya sana sikuwa nimeambulia kitu chochote cha maana. Muda uliendelea kusonga bila John Varma kujitokeza kwenye maskani yake na hali ile ikanitia wasiwasi kuwa huwenda nilikuwa nikipoteza muda wangu bure mle ndani baada ya kuhisi kuwa John Varma angekuwa tayari ameshtukia juu ya kuwindwa kwake na wanausalama wa serikali ya mapinduzi ya kijeshi hivyo alikuwa ameamua kutorokea kusikojuliana. Mawazo hayo yakazidi kuzamisha matuamini ya kumpata Max na pesa alizokimbia nazo. Kwa kweli nilijihisi kutaka kupata muda wa kuzidi kutafakari zaidi kwani kufuatia kumkosa John Varma mle ndani mipango yote ilikuwa imevurugika.
Hatimaye nikaamua kutoka kwenye ile nyumba kwa kuhofia kukutwa na wanausalama wengine na hivyo kujiingiza upya kwenye matatizo. Mvua ilikuwa imeanza kunyesha hivyo nilipofika chini ya lile jengo la ghorofa nikaamua kujifunika kwa kofia ya jaketi langu baada ya kuhisi baridi kali ikinishambulia kichwani. Wakati nikitembea kwenye korido ya nje ya lile jengo la ghorofa sikuona mtu yeyote, pikipiki au gari likikatisha mitaani na hapo nikatambua kuwa ile amri ya jeshi ya kutokutembea mitaani kwa raia mara baada ya kutimia saa kumi na mbili na nusu ilikuwa imezingatiwa kikamilifu. Hivyo nikajionya kuchukua tahadhari huku mara kwa mara nikigeuka nyuma kuchunguza kama kungekuwa na mtu yeyote ambaye angekuwa akinifuatilia nyuma yangu. Sikumuona mtu yeyote kwa vile giza lilivyokuwa nene lakini sikuacha kujipa hadhari.
Ukweli ni kwamba sikujua ni wapi nilipaswa kuelekea kwa usiku ule kwa vile sikuwa na mwenyeji mwingine yeyote pale jijini Monrovia. Wazo la kuelekea katikati ya jiji la Monrovia likanijia haraka baada ya kuamini kuwa nikiwa huko ningeweza kupata baa moja iliyochangamka usiku ule na kuzamia humo huku nikipanga vyema mikakati yangu. Lakini hilo halikutimia kwani wakati nikiwa nimezama kwenye tafakuri ile mara ghafla nikashtukia nikipigwa na kitu kizito nyuma yangu kichwani. Loh! lilikuwa pigo sana na hapo nikayumba hovyo karibu ya kuanguka chini huku nikiupeleka mkono wangu kwenye mfuko wa koti langu kuifikia bastola.
Hata hivyo sikufanikiwa kwani wakati nikigeuka nyuma kutazama ni kitu gani kilichokuwa kikinitokea nikajikuta nikikabiliana na pigo lingine baya mbele ya kichwa changu. Muda uleule macho yangu yakaingiwa na giza zito, mdomo wangu haukuweza tena kuzungumza neno hata pale nilipofungua kinywa changu kupiga yowe la kuomba msaada. Bastola yangu mkononi ikaniponyoka na kuanguka chini, miguu yangu ikalemewa ghafla na uzito wa kuogopesha na hivyo kunipelekea nijihisi kama mlevi wa pombe kali. Nikaendelea kujikaza huku nikiinama kuiokota bastola yangu pale chini ilipoangukia lakini sikufanikiwa kwani pigo la tatu kichwani likafanikiwa kunibwaga chini na kulala chali na baada ya pale sikufahamu kilichoendelea.
_____
NILIYAFUMBUA MACHO YANGU kwa taabu baada kumwagiwa ndoo mbili za maji baridi yenye harufu mbaya ya shombo ya samaki. Nikazinduka na kutazamatazama huku na kule sehemu ile. Nikagundua kuwa nilikuwa sehemu ngeni kabisa katika maisha yangu. Tukio lile likaambatana kizunguzungu kibaya na hisia za maumivu makali yaliyoamshwa upya kichwani mwangu. Nilipomwemwesa macho yangu vizuri nikagutuka kuwa mikono na miguu yangu ilikuwa imefungwa kwenye kiti cha chuma kilichokuwa mbele ya meza kubwa. Nyuma ya meza ile kwenye kiti aliketi mwanaume mmoja mwanajeshi mwenye cheo cha Luteni Kanali kama cheo chake begani kilivyojieleza.
Niseme sijapata kuona mwanaume mrefu na mweusi kama yule katika pilikapilika zangu huko nyuma kwani mwanga hafifu wa mle ndani uliniwezesha kidogo kuyaona macho na meno yake wakati alipokodoa kunitazama. Tathmini yangu ya haraka ikanitanabaisha kuwa mtu yule hakuonekana kuogopa kitu chochote hapa duniani zaidi ya kupenda kutoa roho za watu. Ingawa mtu yule alijitahidi kutabasamu lakini hali ile haikufanya sura yake mbaya kurudisha matumaini wala macho yale yenye unyama na chuki kutangaza amani.
“Loh! masaibu gani tena haya?”. Nikajisemea kimoyomoyo huku nikitembeza macho yangu kutazama huku na kule.
Tulikuwa kwenye chumba kikubwa kishichokuwa na dirisha lakini chenye kuta imara. Katikati ya chumba kile ndiyo kulikuwa na vile viti tulivyoketi na meza kubwa ya chuma iliyotutenganisha katikati. Juu ya meza ile ilining’inizwa balbu ya umeme wa mwanga hafifu kutoka katika dari ya chumba kile. Nilipoendelea kuchunguza nyuma ya yule kamanda wa jeshi kiasi cha umbali wa mita zisizopungua tano nikauona mlango mkubwa wa chuma uliofungwa. Sikuweza kugeuka nyuma kwa vile nilivyokuwa nimefungwa mikono na miguu kwenye kile kiti lakini nilihisi kuwa huwenda kulikuwa na mtu au watu ambao ndiyo wangekuwa wamehusika katika kunimwangia yale maji baridi ili kunizundua. Mle ndani kulikuwa na utulivu kana kwamba tulikuwa kwenye chumba cha mtihani wa taifa na hali ile ilinipasha tumbo joto.
Fahamu zilikuwa zimenirudia baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani na mtu nisiyemfahamu mara baada ya kutoka kupambana na Paye Dolo kule nyumbani kwa John Varma, kitongoji cha West Point. Hofu ikazidi kuiteka nafsi yangu wakati macho yangu yalipoweka kituo kutazama pale mezani. Nikaiona bastola yangu iliyotenganishwa na kiwambo maalum cha kuzuia sauti, risasi nne zilizotolewa kwenye magazini, pingu niliyotumia kumnyongea Paye Dolo, pasipoti yangu ya kusafiria ya jamhuri ya muungano wa Tanzania na karatasi ya viza ya kuniruhusu kukaa pale nchini Liberia kwa muda wa mwezi mmoja na nusu.
Pale juu ya meza nilipochunguza vizuri hofu ikaongezeka zaidi baada ya kuiona nembo kubwa ya NSA-National Security Agency, shirika la ujasusi la Liberia. Sasa sikuwa na shaka yoyote kuwa nilikuwa nimefikishwa kwenye makao makuu ya shirika la ujasusi la Liberia kuhojiwa. Kijasho chepesi kikaanza kunitoka maungoni.
Yule mtu mbele yangu alipojiridhisha kuwa nilikuwa nimerudiwa vizuri na fahamu akaondoa kofia yake ya kijeshi kichwani na kuiweka pale juu mezani na hapo nikapata kuuona upara wake uliong’aa na kusukwasukwa na mishipa ya damu kama mizizi ya kitunguu. Yule mtu akakohoa kidogo kusafisha koo lake na hatimaye kuvunja ukimya huku akiegemeza mikono yake mezani na kunitazama.
“Ni vizuri sasa tukafahamiana. Jina langu naitwa Lansanah Dagosseh, mwanajeshi mwenye cheo cha Luteni Kanali katika jeshi la mapinduzi hapa Liberia. Lakini vilevile mimi ni mkurugenzi wa upelelezi wa idara ya usalama wa taifa ya hapa Liberia, NSA-National Security Agency”. Yule kamanda akamaliza kujitambulisha na kupisha tafakuri ya kimya huku akinitazama. Nikajua alitaka kusikia kutoka kwangu lakini sikuwa na cha kuongea. Alipoona muda unayoyoma bila mimi kujitambulisha akaamua kuvunja ukimya huku akinitazama.
“Wewe ni nani?”
“Najiona mateka katika sehemu nisiyoifahamu”. Nikaongea kwa utulivu huku nikimtazama yule kamanda mbele yangu.
“Jina lako tafadhali!”. Yule kamanda akanikatisha huku amanikazia macho. Baada ya kufikiri kidogo nikaona kuwa hapakuwa na haja ya kudanganya kuwa mimi ni nani kwa vile pasipoti na viza yangu vilijieleza.
“Jina langu naitwa Tibba Ganza, raia wa Tanzania”
“Umefuata nini hapa Liberia?”
“Nimekuja kwenye matembezi tu”
“Kumtembelea nani?”
“Kutembelea nchi yenu na vivutio vyake, bahati mbaya sana kabla sijaanza matemebezi yangu ndiyo nikapigwa kichwani na wahuni. Sasa ndiyo nimezinduka nashangaa kujikuta humu ndani nimefungwa mikono na miguu namna hii”
“Umefikia sehemu gani hapo Monrovia?”
“Kumbe hapa ni Monrovia?”. Nikamuuliza yule kamanda huku nikijitia hamnazo, hata hivyo sikuona tashwishi yoyote usoni kwa yule mtu mbele yangu.
“Nijibu swali langu tafadhali!”
“Oh!, samahani sana kwa kukawia kukujibu bwana mkubwa. Nilikuwa nimepanga kufikia Bella Casa Hotel na ndiyo nilikuwa njiani kuelekea huko wakati nilipokutwa na masaibu haya. Loh! wahuni wa mjini kweli siyo watu”
“Uchunguzi unaonesha kuwa uliwasili uwanja wa ndege wa James Spriggs Payne Airfiled saa 10:30 asubuhi siku ya juzi ukitokea Ibadan nchini Nigeria. Unaweza kunieleza muda huo wote tangu ulipowasili hapa Monrovia ulikuwa ukikaa wapi?”. Yule kamanda akaniuliza huku akinitazama kwa udadisi na swali lile likanipelekea nigutuke huku kijasho chepesi kikianza kunitoka. Sasa nilianza kuona hatari kubwa mbele yangu kwa namna shirika la kijasusi la Liberia lilivyokuwa limepiga hatua katika kupata taarifa zangu.
“Muda wote huo nimekuwa nikishinda kwenye baa mbalimbali za hapa jijini Monrovia kabla ya mapinduzi ya kijeshi kufanyika”. Maelezo yangu yakampelekea yule kamanda anitazame kwa kejeli hata hivyo hakutia neno. Baada ya kitambo kifupi cha ukimya mle ndani hatimaye nikamuona yule kamanda taratibu akiegemea kiti chake kustarehe. Kisha akaingiza mkono kwenye mfuko wa gwanda lake na kuchukua pakiti ya sigara. Humo akatoa sigara moja na kuibana kwenye kingo za mdomo wake kisha akajiwashia mche ule wa sigara kwa kiberiti cha kasha. Baada kuvuta pafu mbili akaupuliza moshi mbele yangu na kurejea kwenye maongezi.
“Umesema umekuja hapa Monrovia kutembea?”
“Ndiyo”. Nikaitikia
“Ungewezaje kukaa muda wote huo hapa Monrovia wakati huna pesa?”
“Pesa zangu zote zimeibwa na wahuni walionishambulia kichwani”. Nikadanganya.
“Na hii bastola mali ya jeshi la Liberia uliokutwa nayo unaweza kuniambia uliipata wapi?”
“Sijawahi kumiliki bastola achilia mbali kuitumia”. Nikajitetea.
“Kwa hiyo vijana wangu ni waongo?”
“Kwani vijana wako ndiyo walionivizia na kunipiga kichwani?”. Nikauliza nikijitia sielewi vizuri somo.
“Bado hujapigwa ila walichokifanya ni utaratibu wa kawaida kabisa wa kumkamata mhalifu”. Yule kamanda akasisitiza huku akilazimisha tabasamu kuumbika usoni pake.
“Huu ni utekaji na uvunjaji wa haki za binadamu. Nikiamua ninaweza kuwafungulia mashtaka ya kidiplomasia kwa unyanyasaji kwani nimefuata taratibu zote za kuingia nchini mwenu na sijafanya uharifu wowote”. Nikaendelea kujitetea hata hivyo nilikuwa na matumaini makubwa kwa vile nilikuwa na hakika kuwa hakuna mtu aliyekuwa akinifahamu kama mimi ni jasusi hatari wa kuogopwa.
“Tunayo haki ya kumkamata mtu yeyote, awe mgeni au mzawa ambaye mienendo yake inaonekana kutishia usalama wa nchi yetu. Huwa sipendi kumuona mtu analeta masuala ya siasa kwenye mambo ya msingi”. Yule kamanda akanionya huku akiendelea kuvuta sigara yake taratibu.
“Ni kwa vipi mienendo yangu imetishia usalama wan chi yenu?”. Nikamuuliza yule kamanda na baada ya kutoa sigara yake mdomoni na kukung’uta majivu kando akavunja tena ukimya.
“Mmoja wa vijana wangu amekuona ukitoka kwenye nyumba namba 102 iliyopo kitongoji cha West Point. Mkazi wa nyumba hiyo anaitwa John Varma, huyu ni mtu hatari katika kutishia usalama wa nchi ambaye tumekuwa tukimtafuta kwa muda mrefu. Mtu wetu mmoja amekutwa ameuwawa kwa kunyongwa kwa pingu shingoni kwenye nyumba hiyo wakati mwenyeji wake hafahamiki alipo. Je, tunawezaje kukutenganisha na tuhuma hizi?”. Yule kamanda akaniuliza na mara hii akinikata jicho kali la utafiti.
“Siwafahamu hao watu wote uliowataja na wala sijawahi kuyasikia majina yao hata kwenye matangazo ya vifo redioni. Nawezaje kuingizwa kwenye tuhuma za mauaji ya mtu nisiyemfahamu?. Nadhani ingekuwa busara kumtafuta mkazi wa hiyo nyumba na kumuuliza. Mimi ni mgeni nipo hapa kufurahia matembezi yangu na siyo kuvunja sheria”
“Tazama viganja vyako”. Yule kamanda akaongea kwa utulivu. Haraka akili yangu ikatumbukia tena mtegoni na mara hii nikahisi kuwa nilikuwa nimekutana na mtu makini na mwenye hila nyingi za masuala ya usalama katika kucheza vizuri na saikolojia ya mtu. Loh! ile michubuko ya pingu kwenye vifundo vya viganja vyangu wakati nikimnyonga Paye Dolo kule West Point nyumbani kwa John Varma ilikuwa imeniumbua. Nikameza funda la mate kujipa utulivu huku nikiichunguza ile michubuko viganjani mwangu. Nilipoinua macho yangu kumtazama yule kamanda tayari nilikuwa nimetengeneza hila.
“Sioni kitu labda mnifungue mikono”
“Viganja vyako vimekutwa na michubuko ya pingu. Sina shaka yoyote kuwa pingu hizo ndiyo zilizotumika kumnyongea Paye Dolo kwenye nyumba namba 102 kule West Point”
“Sasa kamanda huoni kuwa taarifa zenu zina mkanganyiko?”. Nikaingiza hoja.
“Kwa vipi?”. Yule kamanda akaniuliza kwa udadisi.
“Kama mimi nashukiwa kumuua Paye Dolo kwa vipi natuhumiwa kumnyonga kwa kutumia pingu wakati inasemekana nilikuwa na bastola. Huoni kuwa risasi ndiyo ingelikuwa njia rahisi zaidi ya kuhitimisha uhai........ wiki ijayo
Shunie naomba uwatagi wengine wooooote wadau wa adithi. Au yeyote atag watu
 
Hii ndio shida ya story za JF, yaani ujanja ni kutafuta ambayo imeshafika mwisho ndio uanze kusoma la sivyo jiandae kupata shida ya kusoma nusu then kusubiria kwa wiki kadhaa.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom