RIWAYA: Mifupa 206

NILIMALIZA KUVUTA SIGARA YANGU ya mwisho kisha nikakitupa
kipisi cha sigara ile kwenye kibakuli kidogo cha majivu ya sigara kilichokuwa
juu ya stuli ndefu chakavu kando yangu huku nikihisi mapafu yangu kuwaka
moto. Kwa muda wa masaa machache yaliyopita tayari nilikuwa nimeteketeza pakiti
mbili za sigara zilizonifanya nianze kujihisi mgonjwa wa maradhi nisiyoyajua huku
nikiwa nimeketi kwenye kochi moja kuukuu lililokuwa mle ndani wakati mawazo
mengi yalipokuwa yakipita kichwani mwangu.
Hiki kilikuwa chumba kidogo kati ya vyumba vingi vya jengo moja la ghorofa
lililotelekezwa pasipo kumaliziwa baada ya mmiliki wake kujikuta katikati ya mgogoro
mkubwa na maafisa wa ardhi kwa kujenga eneo lisilostahili kando ya eneo moja
la ufukwe wa bahari ya Hindi. Jengo hili sasa lilikuwa likitumika kama maskani ya
watoto machokoraa wa jiji la Dar es Salaam pamoja na vibaka na wakabaji. Nilikuwa
nimeyagundua maficho haya huko siku za nyuma hivyo nikawa nimeamua kukarabati
chumba kimoja na kukiwekea ulinzi mkali ambacho ningekitumia kama maficho
wakati wa harakati zangu au sero ndogo ya kuwasweka washukiwa wangu kabla ya
kuwatapisha taarifa muhimu ninazozihitaji.
Baada ya yule mateka wangu niliyempata kutoka katika zile figisufigisu za kutekwa
kwa Mwasu kule kwenye mnara wa Askari monument eneo la posta nilikuwa
nimempeleka kwenye hospitali moja ya kichochoroni iliyopo eneo la Magomeni ili
kupatiwa tiba dhidi ya yale majeraha yake ya risasi kabla ya kumchukua na kumfikisha
kwenye maficho haya yenye chumba kimoja kidogo kisichopigwa plasta,choo kidogo
cha ndani na dirisha dogo linalopitisha mwanga hafifu lisilomruhusu mtu kupenya.
Mle ndani kukiwa na kitanda kidogo cha chuma cha futi sita kwa nne chenye godoro
la sufi huku kando yake kukiwa na kochi moja kuukuu la sofa,stuli ndefu na kibakuli
cha majivu juu yake.
Mara baada ya kutupa kile kipisi cha sigara mkononi mwangu taratibu nikasimama
kutoka kwenye lile kochi na kuvinyoosha viungo vyangu mwilini kabla ya kupiga
mwayo hafifu wa uchovu huku nikianza kuzitupa hatua zangu tulivu na kusogea
kwenye kile kitanda cha mle ndani nilipomlaza yule mateka wangu baada ya kumuona
akijigeuzageuza pale kitandani kama aliyeshtuka kutoka usingizini. Vile vidonda vyake
vya majeraha ya risasi begani na pajani vilikuwa vimesafishwa vizuri,zile risasi kwenye
majeraha zilikuwa zimetolewa na yale majeraha kufungwa vizuri kwa pamba na
bandeji safi. Sindano mbili za kupunguza maumivu alizodungwa bila shaka zilikuwa
zimempelekea nafuu ya maumivu mwilini. Nilipotazama kando ya kile kitanda
kwenye nguzo moja ya chandarua nikagundua kuwa hata ile dripu ndogo ya damu
niliyomtundikia kwa msaada wa maelekezo ya yule daktari nayo ilikuwa mbioni kuisha
na hali ile ikanipa matumaini kuwa afya yake ilikuwa mbioni kuimarika.
Nilipofika pale kando ya kile kitanda nikasimama na kumtazama yule mateka
wangu kwa makini. Alikuwa amefumbua macho yake na kunitazama kwa utulivu kama
mtu anayenishangaa halafu akili yake ilipotulia nikamuona ameshikwa na mshtuko
akajitahidi kunyanyuka pale kitandani hata hivyo hakuwa na nguvu za kufanya vile
hivyo akarudi tena chini na kukiegemeza kichwa chake kwenye mto mmoja wa pale
kitandani kwani afya yake bado ilikuwa dhaifu.
“Unajisikiaje kwa sasa?” nikamuuliza yule mtu na hapo akasimamisha macho yake
na kunitazama kama ambaye alikuwa akiendelea kukusanya kumbukumbu za kutosha
kichwani mwake baadaye nikamuona akivunja.
“Kichwa kinaniuma”
“Chukua hivi vidonge umeze” nikamwambia yule mtu huku nikiingiza mkono
mfukoni na kuchukua vidonge vya kutuliza maumivu nilivyopewa na yule daktari
kule Magomeni kisha nikachukua chupa ndogo moja ya maji kutoka chini ya uvungu
wa kile kitanda na kumpa. Yule mtu akavichukua vile vidonge na kuvitupia kinywani
kisha akafungua ile chupa ya maji na kugida mafunda kadhaa kabla ya kuitua ile chupa
kando yake pale kitandani alipolala ambapo niliichukua na kuiweka chini ya kitanda
kisha nikasogea na kuketi kitandani karibu yake. Yule mtu akawa ni kama anayejisogeza
mbali nami pale kitandani hata hivyo niliwahi kumshika miguu na kumzuia.
“Ondoa shaka sina mpango wa kukudhuru” nikamwambia yule mtu huku
taratibu nikimshika mkono wakati bado akiendelea kunishangaa kwani ni dhahiri
hakuwa akifahamu kitu kilichokuwa kimemtokea hadi yeye kuwepo mle ndani katika
mazingira tofauti kabisa na yale aliyoyazoea.
“Wewe ni nani?” yule mtu akaniuliza kwa woga.
“Chaz Siga,mtu mliyekuwa mkimtafuta wewe na wenzako” yule mtu kusikia
vile akashtuka na kunitazama kwa mshangao sana. Hata hivyo niliupuuza mshtuko
wake na kumuuliza wakati huo vitu vyake vyote muhimu kama simu,kadi ya benki na
kitambulisho chake cha kazi kinachomtanabaisha kama afisa usalama kikiwa juu ya
stuli mle ndani.
“Unaitwa nani rafiki?”
“Dan Maro’’ yule mtu akaniambia kwa utulivu baada ya kitambo kifupi cha kusita
huku akinitazama.
“CID Dan Maro wa idara ya usalama wa taifa…sivyo?’’ nikamuuliza kwa utulivu
huku nikimtazama yule mtu. Jambo moja lililonitia matumaini ni kuwa kachero yule
alikuwa hajanidanganya kwani vitambulisho vyake vyote vilikuwa na lile jina la Dan
Maro alilojitambulisha nalo kwangu.
“Unataka nini kwangu?” yule mtu akaniuliza kwa hofu.
“Labda mimi ndiyo nikuulize swali hilo maana nilisikia kuwa wewe na wenzako
mlifika kule ofisini kwangu kunitafuta. Sasa huoni kuwa huu ndiyo wasaha mzuri
wa kuzungumza baada ya kuwa tumeonana?” nikaongea huku nikitabasamu na
nilipomtazama yule kachero usoni akayakwepesha macho yake na kutazama pembeni
na hapo nikajua ile hoja yangu ilikuwa imeziteka fikra zake.
“Wenzako wamempeleka wapi katibu muhtasi wangu?” nikamuuliza pasipo
mzaha.
“Mimi nipo humu ndani nitafahamu vipi?”
“Mbona tukio lenu la utekaji linaonekana kuwa ni jambo mlilokuwa mmelipangilia
vizuri?”
“Mimi sikuhusika kwenye utekaji” yule kachero akajitetea huku akitazama pembeni.
Nikamtazama kwa makini kabla ya kumchapa ngumi mbili za uso zilizomsababishia
maumivu makali pale kitandani.
“Nahitaji ushirikiano wako vinginevyo sitokuwa na sababu ya kuendelea
kukuuguza humu ndani” nikaongea kwa utulivu huku nikimtazama kwa makini yule
kachero.
“Ushirikiano upi ninaoweza kukupa nikiwa humu ndani tena katika hali hii?” yule
kachero akajitetea huku akiugulia maumivu pale kitandani. Hasira zikiwa zimenishika
kwa majibu yake yasiyo na tija nikamzaba kibao kimoja cha nguvu.
“Nahitaji kufahamu ni wapi mlikompeleka katibu muhtasi wangu vinginevyo
wenzako watakuokota ukiwa maiti” nikamfokea yule mtu kwa hasira huku sura yangu
ikiwa mbali na mzaha hali iliyompelekea yule kachero aanze kutoa maelezo.
“Tuna sehemu nyingi za kuwafanyia mahojiano washukiwa wetu na kwa kuwa
mimi nipo humu ndani siwezi kuwa na hakika ni wapi alipopelekwa katibu muhtasi
wako” yule kachero akaniambia na nilipomtazama usoni nikagundua hoja yake ilikuwa
na ushawishi kidogo ingawa sikumwamini.
“Katibu muhtasi wangu anashukiwa kwa kosa gani?”
“Tulikuwa tumetumwa kukukamata wewe lakini baada ya kuambiwa na katibu
muhtasi wako kuwa wewe haupo tukaona tumkamate yeye huku tukiwa na hakika
kuwa baadaye angetusaidia kukupata wewe”
“Mlitaka kunikamata kwa sababu gani?” nikamuuliza yule kachero na baada
ya kitambo kifupi cha ukimya kupita mle ndani huku akionekana kufikiria jambo
hatimaye akavunja ukimya.
“Tulipewa amri hiyo na mkuu wetu ya kukukamata”
“Bado hujajibu swali langu,nimekuuliza mlitaka kunikamata kwa sababu gani?”
nikamuuliza yule kachero huku nikimtazama usoni.
“Taarifa kutoka ofisi kuu zinakuelezea wewe kama ndiye mshukiwa namba
moja wa mauaji ya makachero wa usalama yanayoendelea kufanyika hapa jijini Dar
es Salaam” maelezo ya yule kachero yakanipelekea kwa sekunde kadhaa nibaki
nikimkodolea macho huku nikishindwa kuyaelewa vizuri maelezo yake kabla ya
kuvunja tena ukimya nikimuuliza.
“Mna ushahidi wowote wa kunitia hatiani kuwa mimi ndiye ninayehusika na hayo
mauaji ya wanausalama wenu?”
“Mimi sifahamu” yule kachero akajitetea.
“Sasa mnawezaje kutaka kunikamata wakati hamna hakika kuwa mimi ndiye
ninayehusika?”
“Sisi ni watu wa kutekeleza amri za wakubwa wetu ofini hivyo siyo jukumu letu
kufahamu sababu ya amri husika inayotolewa”
“Nani aliyewapa amri ya kunikamata?” hatimaye nikamuuliza yule kachero huku
nikianza kupata picha kuwa ni kwa namna gani nilikuwa nikisakwa kwa udi na uvumba
na makachero wale. Kisha wakati nikiendelea kufikiri fikra zangu zikahamia kwa
yule mrembo aliyeniokoa chini ya lile jengo la ghorofa kule maeneo ya posta siku ile
dhidi ya wale makachero waliotaka kunikamata. Kwa kuwa mauaji ya makachero hao
sikuwa nimeyafanya mimi basi niliamini kuwa mshukiwa namba moja wa mauaji hayo
bila shaka angeweza kuwa ni yule dada ingawa hadi wakati huu sikuweza kufahamu
ni kwanini mlimbwende yule hatari alikuwa akiendesha kampeni ya kimyakimya ya
kuwaua makachero wale. Hata hivyo kwa namna moja au nyingine nilikuwa nimeanza
kuamini kuwa yule dada huwenda angekuwa askari jeshi tena mwenye mafunzo ya
kijeshi ya hali ya juu ambayo yalikuwa yakimsaidia vyema kutekeleza mipango yake
bila ya kukamatwa. Kwani vinginevyo kama angekuwa ni mtu wa kawaida mpaka sasa
tayari angekuwa ameshakamatwa na wanausalama wale na kuswekwa ndani akisubiri
hukumu ya kifo.
“Sulle Kiganja” hatimaye yule kachero akatamka kwa kusitasita.
“Sulle Kiganja ndiyo nani?” nikamuuliza yule kachero huku nikimtazama kwa
makini.
“Sulle Kiganja ni mkuu wa intelijensia ya ujasusi ya usalama wa taifa” jibu la yule
kachero likanipelekea nishtuke kidogo na kumtazama huku kijasho chepesi kikianza
kunitoka usoni. Sasa nilifahamu kuwa idara ya taifa ya kijasusi ilikuwa na taarifa zangu
hivyo mpaka kufikia wakati ule niliamini kuwa makachero wa usalama wangekuwa
tayari wametupa nyavu zao kila kona katika kuhakikisha kuwa wananinasa kabla
sijafika mbali zaidi katika harakati zangu.
Nikiwa bado nimeketi kando ya kile kitanda mawazo mengi yakawa yakiendelea
kupita kichwani mwangu huku nikiwaza namna ya kujiepusha na hatari kubwa
iliyokuwa mbele yangu pamoja na kumnasua Mwasu kutoka katika mikono ya
makachero wale hatari. Baada ya kufikiri sana hatimaye nikawa nimepata wazo.Mara
hii nikayapeleka tena macho yangu pale kitandani kumtazama yule kachero CID Dan
Maro kabla ya kuvunja ukimya.
“Nahitaji namba ya simu ya huyo mkuu wako aliyewatuma!”
“Sulle Kiganja…?”
“Labda kama kuna mwingine” nikaongea kwa utulivu huku nikimtazama yule
kachero ambaye sasa alikuwa chini ya himaya yangu ndani ya chumba kile cha siri
chenye dirisha dogo la kupitisha mwanga hafifu. CID Dan Maro akanitazama kwa
mashaka kama niliyekuwa nikiomba namba ya simu ya mkewe na nilipomuona akizidi
kusitasita nikamzaba tena makofi mawili ya nguvu yaliyompelekea apige yowe kali la
maumivu pale kitandani nami nikavunja ukimwa huku nikimtazama.
”Mimi siyo muuaji kama mkuu wenu anavyotaka kuwaaminisha. Nimelitumikia
jeshi la wananchi wa Tanzania kwa muda wa miaka nane kama kamandoo wa daraja la
kwanza mwenye mbinu zote za kijeshi katika mapambano ya kivita huku nikitekeleza
vizuri wajibu wangu katika nchi kadhaa barani afrika zenye migogoro ya amani. Lakini
pamoja na hayo yote siku moja nikajikuta nikipoteza kazi yangu na kutumikia kifungo
cha jeshi chenye kazi ngumu na mateso makali kwa muda wa miaka minne kwa kosa
la kutoa ripoti ya siri inayoeleza ni kwa namna gani baadhi ya viongozi wangu wa jeshi
wanavyonufaika binafsi na migogoro hiyo. Ukweli wangu ukaniponza,nikadhulumiwa
kazi na mafao yangu lakini nashukuru kuwa hawakuweza kunipokonya maarifa na
ujuzi kichwani mwangu. Hivyo nikaamua kufungua ofisi inayoshughulika na upelelezi
wa kujitegemea kama sehemu ya kujipatia kipato cha kuendesha maisha na sasa sipo
tayari kuiona idara yenu ya usalama ikinitumbukiza kwenye janga lingine ambalo kwa
sasa limeanza kuutishia uhai wangu. Ninachohitaji kutoka kwako ni ushirikiano juu ya
nini kinachoendelea vinginevyo wewe utakuwa ni mtu wa kwanza kufa humu ndani
kabla ya wengine kufuatia” nikaweka kituo na kukohoa kidogo kisha nikageuka na
kumtazama yule kachero kwa makini pale kitandani.
“Nahitaji namba ya simu ya Sulle Kiganja” sauti yangu ilikuwa kavu na yenye
hakika huku macho yangu yakiwa yameanza kupoteza utulivu. Yule kachero kuona
vile taratibu akaanza kunitajia ile namba ya simu ya mkuu wa intelijensia ya ujasusi
ya usalama wa taifa,Sulle Kiganja. Alipomaliza na mimi nikawa nimemaliza kuinakili
vizuri namba ile ya simu kwenye simu yangu na muda uleule nikaipiga. Kitambo kifupi
cha ukimya kikafuata kabla ya ile simu kuanza kuita jambo ambalo liliamsha upya hisia
zangu na kunipa matumaini. Baada ya miito kadhaa hatimaye ile simu ikapokelewa
upande wa pili na hapo sauti nzito,tulivu na yenye mamlaka ikasikika.
“Haloo,nani mwenzangu?”
“Chaz Siga bila shaka wewe ni Sulle Kiganja!” nikauliza kwa utulivu hata hivyo
sikujibiwa mapema badala yake kitambo kifupi cha ukimya kikafuata huku nikisikia
kelele hafifu upande wa pili wa ile simu na kutokana na uzoefu wangu nikajua kuwa
Sulle Kiganja pamoja na watu wake walikuwa katika harakati za kuinasa sauti yangu
kwenye vifaa vyao maalumu vya kijasusi jambo ambalo halikunipa wasiwasi wowote.
Baada ya muda mfupi ile sauti ya Sulle Kiganja ikarudi tena hewani huku hisia zangu
zikinieleza kuwa kando yake kulikuwa na watu wengine tayari kusikiliza maelezo
yangu.
“Safi sana Chaz Siga!,nilijua tu kuwa hatimaye utajitokeza mwenyewe na
kunitafuta. Niambie unazungumza kutoka wapi rafiki yangu?” Sulle Kiganja akaongea
kwa dhihaka na kuangua kicheko hafifu cha dharau.
“Mwasu yuko wapi?”
“Yuko sehemu salama kabisa,ondoa shaka”
“Nahitaji kuongeanaye sasa hivi”
“Amelala sehemu tulivu na daktari amesema kuwa hatakiwi kusumbuliwa” Sulle
Kiganja akaongea kwa kujiamini.
“Anaumwa nini hadi daktari ampumzishe?” nikauliza kwa hasira baada ya kuhisi
kuwa Mwasu angekuwa ameteswa sana na kwa muda ule hali yake ilikuwa mbaya
sana.
“Uchovu wa kawaida tu” Sulle Kiganja akaongea kwa utulivu huku akiangua
kicheko cha ushindi.
“Najua kuwa umemtesa sana Mwasu hata hivyo nakushauri kuwa uachane na
mpango huo kama bado unapenda kumuona afisa wako CID Dan Maro akiwa
mzima” maelezo yangu yakapelekea kile kicheko cha Sulle Kiganja kutoweka haraka
na sauti yake kuingiwa na utulivu.
“Usijaribu kunitisha Chaz Siga badala yake nakushauri kuwa ujitokeze mwenyewe
huko ulikojificha vinginevyo watu wangu watakukamata muda siyo mrefu”
“Sikiliza vizuri na kwa makini Sulle Kiganja,pengine unaongea hivyo kwa sababu
hujui unazungumza na mtu wa namna gani. Fahamu kuwa sijakupigia simu hii
kukusalimia kama unavyoendelea kunipotezea muda wangu. Saa mbili usiku wa leo
nitakupigia simu tena kuzungumza na Mwasu na kama sitoweza kuongeenaye afisa
wako CID Dan Maro anafahamu vizuri nini nitakachomfanya na tusilaumiane”
“Okay,okey…nimekuelewa. Sasa na mimi utanihakikishia vipi kuwa afisa wangu
Dan Maro bado mzima?” Sulle Kiganja akaongea kwa utulivu huku ile hoja yangu
ikionekana kumuingia vizuri na muda uleule nikageuka na kumchapa Dan Maro kofi
moja la uso kisha nikamuwekea ile simu sikioni huku bado akilalamika kwa maumivu.
“Dan…!” Sulle Kiganja nikamsikia akiita upande wa pili wa ile simu.
“Ndiyo mimi mkuu…!” CID Dan Maro akaongea kwa taabu huku akilalama
kwa maumivu makali ya kipigo changu hata hivyo niliwahi kuiondoa ile simu sikioni
mwake na kuiweka sikioni.
“Afisa wako Dan Maro anaendelea vizuri kama ulivyomsikia,naomba tuwasiliane
saa mbili usiku bila chenga” nilimwambia Sulle Kiganja na kabla hajatia neno nikawahi
kukata ile simu kisha nikaizima na kuitia mfukoni.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom