RIWAYA: Mifupa 206

Fortunatus Buyobe

JF-Expert Member
Nov 9, 2011
463
1,107
Kama nilivyoahidi hapo jana kuwa mwandishi wetu wa riwaya ya mtutu wa bunduki ameniomba niwajulishe kuwa adithi yetu itaendelea kuanzia ijumaa ijayo. Hii inatokana na kutingwa na majukumu mengine katika ujenzi wa taifa. Lakini pamoja na hayo amenipa jukumu la kuwaletea riwaya yake ya MIFUPA 206. Nawaomba muwasiliane na mtunzi kwa namba
0688058669 kwa ajiri ya kupata nakala za vitabu vifuatavyo
1.Tai kwenye mzoga (hiki nacho nitakileta humu mpaka nitakavyoelekezwa tofauti na mtunzi)
2.Msitu wa madagascar
3.Mifupa 206
Nawaomba tuthamini kazi za watunzi wetu kwa kuwaunga mkono kwa kununua kazi zao ili wafaidi matunda ya vipaji vyao. Twende kazi.......
Mods naomba mnisaidia kuexpand hiyo attachment ambayo ni cover ya kitabu
 

Attachments

  • Newcover MIFUPA 206.pdf
    2.2 MB · Views: 485
Kelvin Mponda ndo mwandishi wa hivi vitabu kwakweli mi nimekisoma hicho cha Tai Kwenye Mzoga kiukweli ni kizuri mnoo nakivutia kasi hiki kingine sababu najua jamaa si mbabaishaji kwenye kazi zake!
 
MIFUPA 206 KEVIN e. MPONDA

MSITU WA GOVENDER KIVU YA KASKAZINI
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

UKIMYA WA KUTISHA ulikuwa umetawala eneo lote la msitu wa Govender
katika jimbo hili la Kivu ya Kaskazini nchini D.R Congo. Mvua kubwa
iliyonyesha kwa muda wa masaa matatu ilikuwa imeninyea chapachapa huku
nikiwa nimelalia tumbo langu juu ya tawi nene la mti mrefu na mkubwa aina ya Liana￾Entada gigas.
Mvua hiyo sasa ilikuwa imeacha athari kubwa za mafuriko ya kutisha na kelele
kali za vyura zilizokuwa zikihanikiza kila mahali pamoja na zile kelele nyingi za ndege
wa mwituni kama Mchochea mvua, Kitwitwi, Yombiyombi, Furukombe, Kanga,
Kware, Nderi, Tetere, Kirukanjia, Kulastara, Hondohondo, Kinega, Kuzumburu,
Gogota, Mnana, Mwewe, Vumatiti, Mwari, Kwarara na wengine wengi mara kwa
mara wakizikung’uta mbawa zao na kuzipa tena uhai sauti zao baada ya kusalimika na
athari za mvua hii kubwa ya aina yake.
Upepo mkali uliyokuwa ukivuma katika msitu huu uliliyumbisha tawi nililolilalia
huku na kule ukilisukasuka ovyo hata hivyo sikuliachia wala kukata tamaa kwani
kanuni za kijeshi zilinifunza uvumilivu hususani nikiwa kama mdunguaji makini
ninayehitaji matokeo mazuri ya kazi yangu.
Muda wa masaa tisa ulikuwa tayari umetokomea tangu nilipoukwea mti huu
mkubwa na mrefu msituni wenye maficho mazuri ya majani mengi makubwa
na matawi imara ya kuubeba uzito wangu bila wasiwasi wowote huku nikiendelea
kusubiri mtu au watu fulani nisiyokuwa na miadi nao wajichanganye kwenye targets
zangu ili niwachakaze vibaya kwa risasi.
Jicho langu la kazi kamwe halikuhama kwenye Eyepiece Lens ama sehemu ya kuona
ya durubini pandikizi yenye nguvu kali iliyokuwa juu ya bunduki yangu maalum ya
kudungulia adui.
Kwa kuwa nilikuwa naipenda sana kazi yangu hii hivyo nilikuwa nimechukua
vifaa vyangu vyote muhimu vya kazi kama bunduki yangu maalum ya kudungulia
adui ama Sniper Rifle aina ya 338 Lapua Magnum yenye uwezo wa kudungua bila bugdha
yoyote windo lililopo ndani ya umbali wa mita 1400 ama sawa na urefu wa viwanja
kumi na nne vya mpira wa miguu na iliyojazwa risasi za kutosha. Redio ya upepo ya
mkononi kwa ajili ya mawasiliano. Kisu chenye dira ama Compass/GPS. Kibuyu cha
maji ya kunywa ama Water Bladder. Filimbi ndogo. Dawa ya kujipaka mwilini kwa
ajili ya kujikinga na wadudu wabaya wenye sumu wa porini ijulikanayo kama Insects
Repellent. Min Thermometer. Mchanganyiko wa chakula chepesi lakini chenye kushibisha
kwa muda mrefu. Vifaa muhimu vya huduma ya kwanza. Vifaa vya kuzuia sauti kali
na wadudu wasiingie masikioni. Kurunzi ndogo mfano wa kalamu yenye mwanga
mkali iitwayo Penlight. Mlipuko mdogo wenye moshi mwingi ambao nikiutupa
hulipuka na kutoa wingu kubwa la moshi ili kumzuia adui asinione wakati nikitoroka
uitwao Chemical Mace. Rangi za kujipaka ili kujikinga nisionekane kwa urahisi na adui
iitwayo Camouflage Paste. Strobe Light ama mlipuko mwingine mdogo ambao nikiulipua
hewani hutoa mwanga mkali wa rangi tofauti pale inapotokea kuwa nimepoteana na
wenzangu ili waweze kufahamu nilipo au pale ninapohisi kuwa mbele yangu kuna
adui ili niweze kuyaona maficho yake na kummaliza. Pia kitabu kidogo na kalamu kwa
ajili ya kuandika mambo muhimu ya kazi yangu pamoja na Laser Ranger Finder ama
kifaa kidogo kinachotumika kutambulisha umbali wa adui.
Kwa muda wa siku tatu sasa nilikuwa sijatongoa lepe la usingizi wa kueleweka.
Mapigano yenye upinzani mkali yaliyodumu kwa muda wa siku tatu kati ya vikosi vya
jeshi la MONUSCO-Organization Stabilization Mission in Democratic Republic of the Congo
chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa UNFIB- The United Nations Force Intervention
Brigade na lile la waasi wa M23 yalikuwa yameniacha hoi taabani kwa uchovu. Hata
hivyo tulikuwa tumefanikiwa kuiteka miji mitatu muhimu kutoka mikononi mwa
waasi wa M23. Miji hiyo ikiwa ni mji wa Kitchanga, mji wa Nyiabiondo na mji wa
Kibati.
Kwa kiasi fulani uchovu niliokuwanao ulikuwa umemezwa na furaha ya mafanikio
binafsi niliyoyapata katika kazi yangu. Kwa muda wa wiki mbili tangu vikosi vyetu
vya MONUSCO vilipoanza operesheni zake za kupambana na waasi nilikuwa
nimefanikiwa kuwadungua wapiganaji 18 wa jeshi la waasi la M23 huku wachache
wakifanikiwa kunipa mgongo na kupotelea msituni. Hivyo bado kazi yangu ilikuwa
inaridhisha.
Nikiwa nimelala juu ya tawi la mti huu mrefu mawazo mengi yalikuwa yakipita
kichwani mwangu. Mawazo ambayo mara kwa mara yalikatishwa na sauti za sokwe
waitwao Bonobo na nyani aina ya Black Colobus, Golden Lion Tamarind, Black Titi, Proboscis,
Black-Crested Mangabey, Black-Crested Macaque-Macaca Nigra na Baboon waliokuwa
wakipiga kelele bila sababu ya kueleweka akilini mwangu.
Kuna wakati akili yangu ilipumbazwa kwa muda na kelele za maporomoko ya
maji yaliyokuwa jirani na eneo lile yakitokea sehemu za juu za misitu hii ya Ikweta.
Maporomoko hayo hatari yakisomba magogo,wanyama wa porini na takataka nyingine
za msituni lakini bado jicho langu halikuhama kwenye lenzi ya bunduki yangu.
Kwa muda wa takribani masaa matatu yaliyopita nilikuwa nimepitiwa na nyoka
hatari wenye sumu kali waliopo katika msitu huu kama Rhombic Night Adder, Rhinocero’s
Horned Viper, Albino Burmese Python, Green Mamba na African Bush Viper ambao walipita
mikononi mwangu, shingoni, kichwani, mgongoni na hatimaye kuendelea na safari
zao huku wakiniacha nimeganda kwenye tawi kama sanamu. Hali iliyopelekea mapigo
ya moyo wangu yasimame kwa sekunde kadhaa katika vipindi tofuati.
Kwa kweli msitu ulikuwa unatisha sana ingawa zile sauti za milipuko na kelele za
risasi zilikuwa zimekoma muda mfupi uliyopita baada ya adui kushindwa nguvu na
kukimbia.
Nilikuwa nimefanikiwa kuwadungua wapiganaji wawili wa M23 waliokuwa nyuma
ya gogo umbali wa mita takribani mia sita na ushei wakinitazama. Kazi ilikuwa rahisi
tu kwani risasi moja niliyoiruhusu ilipita katikati ya kioo cha darubini ya mmoja wa
adui wale kisha jichoni na kuufumua vibaya ubongo wake nikimlaza chali. Mwenzake
alinisumbua kidogo akijibanza nyuma ya mti mkubwa uliyokuwa pembeni ya eneo
lile. Sikutaka kuwa na haraka hivyo nilisubiri kwa muda mrefu nikitaka kumwaminisha
adui yule aliyesalia kuwa mambo yalikuwa sawia.
Baada ya kitambo kirefu cha kusubiri yule adui akafanya makosa ambayo
yalimgharimu. Akiamini kuwa mambo yalikuwa sawa sawia akachungulia katikati
ya tundu la mti lililotengenezwa na ndege wa porini aina ya Woodpecker. Jicho langu
makini likiwa kwenye Eyepiece Lens, mkono wangu wa kushoto ulikikamata kilimi cha
bunduki na ule wa kulia ukashika sehemu ya kurekebishia pembe nzuri ya shabaha
kwenye darubini ya juu ya bunduki ama Elevetion Adjastment Knob. Taswira ya adui yule
ilipoenea vizuri kwenye Objective Lens nikabana pumzi ya kutosha kisha nikavuta kilimi
cha Sniper Rifle na hapo kufumba na kufumbua matunda ya kazi yangu yakaonekana.
Risasi moja tu niliyoiruhusu ilipenya kwenye lile tundu la mti yule bwege alipokuwa
akichungulia kisha ikapita jichoni na kulifumua vibaya fuvu lake na hapo nikapapasa
katika mfuko wa gwanda langu la kijeshi na kuchukua pipi ya kijiti kisha nikaimenya
na kuitia mdomoni. Mambo yote yalikuwa kimyakimya kwani bunduki yangu ilikuwa
na kiwambo maalum cha kuzuia sauti ama Sound Suppressor.
Kwa upande huu wa msitu tulikuwa wadunguaji watatu makini kwenye mpango
wa Quick Reaction Force of Task, Group Alpha ya Brigade. Kati ya wadunguaji hao
watatu,wadunguaji wawili tulikuwa ni askari wa kutoka Tanzania Army Special Force.
Yaani mimi Koplo Tsega codename Lady butterfly na Sajenti Chacha Marwa codename
Chameleon. Mdunguaji mwingine akiwa ni wa kutoka jeshi la D.R Congo mwenye cheo
cha Private akifahamika kwa jina la Gina Yhombi-Opango Makiadi codename Lovebird.
Umbali wa kutoka hapa nilipo hadi alipokuwa mdunguaji mwingine ulikuwa si
chini ya mita mia tano na mara kwa mara tuliweza kuwasiliana kupitia redio zetu
za upepo katika kujulishana hali ya usalama ilivyokuwa ikiendelea. Kwa kweli
nilikuwa nimevutiwa sana na Private Gina Yhombi-Opango Makiadi kwa namna
alivyokuwa mpiganaji hodari ingawa alikuwa na umri mdogo zaidi yangu. Binti huyo
wa kikongomani alikuwa amepata shabaha zote wakati wa kufanya mazoezi hali
iliyonishangaza sana kwa uwezo wake mkubwa wa kulenga shabaha.
Nikiwa bado nimelala juu ya tawi hili mawazo mengi yalikuwa yakipita kichwani
mwangu huku nikikumbuka matukio yote yaliyotokea tangu nilipokuwa jijini Dar es
Salaam kabla ya majina yetu yaani mimi na Sajenti Chacha Marwa kupendekezwa
katika mpango wa amani wa hapa Kivu kaskazini nchini D.R Congo.
Sote tulikuwa kwenye tume maalum inayoshughulika na udhibiti na upambanaji
wa biashara haramu ya dawa za kulevya nchini Tanzania. Kwa muda wa miezi
sita tangu tulipojumuishwa kwenye tume hiyo ya kudumu tulikuwa si tu kwamba
tumeiletea mafanikio makubwa tume hiyo lakini pia tulikuwa tumetoa muelekeo
mzuri wa kuwatambua na kuwafikia wachuuzi wakubwa wa biashara hiyo haramu.
Hata hivyo kwa kuwa sisi hatukutaka mambo ya kisiasa katika kukabiliana na wale
washukiwa wa biashara hiyo hivyo mara kwa mara tulikuwa tukikutana na upinzani katika ufanyaji wa kazi yetu kama si kulaumiwa kuwa tulikuwa hatuzingatii misingi ya sheria za nchi na haki za binadamu katika kushughulika na janga hilo lililokuwa mbioni kuimeza kabisa nguvu kazi ya taifa.
Kwa kuzingatia ukubwa wa janga lenyewe tume yetu ilikuwa imeundwa na watu
wa kutoka idara tofauti kutegemeana na umuhimu wa uwepo wa watu hao. Askari wa
kutoka jeshi la wananchi wa Tanzania tulikuwa watatu;yaani mimi Koplo Tsega kutoka
kikosi 92 cha makomandoo Sangasanga mkoani Morogoro. Meja Khalid Makame
kutoka kambi ya kijeshi 521 ya Chukwani kisiwani Zanzibar na Sajenti Chacha Marwa
kutoka kikosi 36 cha kambi ya jeshi Msangani mkoani Pwani. Wengine walikuwa ni
wajumbe wa kutoka shirika la kimataifa la haki za binadamu-Human Rights Watch.
Mwanasheria wa serikali. Wajumbe kutoka idara ya usalama wa taifa. Wanasiasa
kutoka maeneo tofuati ya kiutendaji pamoja na askari polisi waandamizi akiwemo
kamishna mkuu wa jeshi la polisi na wawakilishi wa vijana.
Kitu kilichokuwa kimenishangaza sana ni kuwa wakati kazi yetu ikiwa mbioni
kutoa suluhisho la kudumu katika kukabiliana na biashara hiyo haramu ya dawa za
kulevya nchini Tanzania ndiyo tukapewa barua za kuingizwa kwenye mpango wa
amani ya kudumu hapa nchini D.R. Congo. Tena wanajeshi wote watatu tuliyokuwa
kwenye tume hiyo tukienguliwa bila sababu za kueleweka.
Kwa kuwa kazi yetu katika tume hiyo ilikuwa bado haijafikia ukomo na tulikuwa
tukielekea katika hatua nzuri zaidi ya kuwaweka bayana wafanyabiashara hao.
Tulijaribu kwa kila hali kupingana na hoja ya kujumuishwa kwetu kwenye mpango
wa amani ya kudumu ya hapa D.R Congo lakini hatimaye tuligonga mwamba
kwani viongozi wetu wa juu walitumia mamlaka yao kupingana na hoja zetu. Hivyo
hatukuweza kukaidi zaidi ya kutii amri zao kitendo ambacho kilinitia hasira sana. Hata
hivyo, sikuwa na namna kwani mojawapo ya misingi inayoliletea sifa kubwa jeshi letu
ni utii na nidhamu. Na sasa nilikuwa hapa eneo la Bunagana msituni juu ya mti mrefu
nikitekeleza wajibu wangu kwa taifa.
Niligeuka kuitazama saa yangu ya mkononi na hapo nikagundua kuwa ilikuwa
tayari imekwishatimia saa nane usiku na dakika chache mbele yake. Manyunyu hafifu
ya mvua yalikuwa yameanza kuanguka tena kutoka angani na kwa kweli sikupenda
mvua iendelee kunyesha katika msitu huu ingawa kunyesha kwa mvua kubwa lilikuwa
ni jambo la kawaida sana katika nchi za Ikweta kama nchi hii ya D.R Congo yenye
kilometa za mraba 2,345,410 hali ya hewa ya joto na baridi yenye wastani wa jotoridi
nyuzi 25 digrii sentigredi na wastani wa mvua kiasi cha sentimeta 130 hadi 200 kwa
mwaka ardhini.
Taa nyekundu ndogo iliyowaka haraka kwenye redio yangu ya upepo ikayahamisha
mawazo yangu na hapo nikageuka na kuitupia macho huku nikiitazama kwa mshtuko
kama niliyeshikishwa bomu. Taa ile ilikuwa na maana kuwa kulikuwa na simu
iliyokuwa ikiingia jambo ambalo lilikuwa la kawaida kabisa kutokea lakini sijui ni
kwanini nilishtuka sana.
Haraka nikaizungusha durubini yangu juu ya bunduki ku-scan taswira yoyote iliyokuwa eneo lile na hapo nikaona kuwa hali ilikuwa shwari hivyo nikabonyeza kitufe kwenye redio yangu ya upepo kuruhusu ile simu kuingia. Kwa kufanya hivyo
ile taa nyekundu ikapotea na kuwaka taa ya kijani halafu kukasikika sauti ya mvumo
wa upepo. Koo langu likakauka ghafla pale nilipokumbuka kuwa simu ya namna ile
ilikuwa ikitoka kwa mmoja wa wadunguaji wenzangu katika msitu huu. Ile sauti ya
mvumo wa upepo ilipokoma nikasikia sauti ya upande wa pili wa simu ambayo haraka
niliweza kuitambua kuwa ilikuwa ni sauti ya Sajenti Chacha Marwa codename Chameleon.
“Lady butterfly are you there? ...unanisikia?” sauti ya upande wa pili iliongea hata
hivyo niliitambua haraka kuwa sauti ile ilikuwa ikipwaya kwa hofu na iliyotawaliwa na
kitetemeshi…’Jambo la hatari?’ Nilijiuliza.
“Lady butterfly unanipata?” Ile sauti ikajirudia safari hii kwa nguvu kidogo.
“Ndiyo nakupata Chameleon, any trouble?” Nilimuuliza kwa wasiwasi.
“Yes! I got shot, very severely.”
“What!...umepigwa risasi?” Nilimuuliza kwa taharuki
“Ndiyo! Risasi mbili Lady Butterfly. Risasi moja imenipata begani na nyingine
imenitoboa sehemu ya kushoto kifuani sentimita chache mbali na moyo,” Chameleon
alizungumza kwa sauti hafifu ya kukoroma.
“Oh! My God uko wapi sasa?” Nilimuuliza.
“Nyuma ya jiwe umbali mfupi kutoka pale nilipokuwa,” Chameleon aliendelea
kuongea kwa shida huku sauti yake ikionekana kuzidi kupoteza mhimili.
“Okay! Hold on Sajenti am coming right now.”
“Don’t ever try to come here Lady Butterfly kwani inavyoonekana ni kuwa anajua tulipo
hivyo itakuwa kazi rahisi kwake.”
“Nani?” Nilimuuliza Chameleon kwa mshangao.
“Adui mdunguaji,” Chameleon aliendelea kuniweka bayana lakini sauti yake ilikuwa
ikizidi kuyoyoma.
“Nakuja!” Nilitaka kuzidi kumdadisi Chameleon lakini nilighairi wazo langu kwa
haraka kwani ningekuwa nikipoteza muda wangu na huwenda asingenijibu kutokana
na udhaifu wake.
Nilihisi kuwa bado kulikuwa na nafasi ya kuyaokoa maisha yake endapo ningeweza
kucheza na muda wangu vizuri ingawa maelezo yake yalikuwa na kiasi kikubwa cha
ukweli wa kunionya.
“Chameleon…! Chameleon unanisikia?” Niliita tena lakini mara hii sikujibiwa na
badala yake kwa mbali nilisikia sauti ya mikoromo yake hafifu.
“Chameleon unanisikia?” niliita tena lakini sauti ile upande wa pili ilipoteza uhai
na hapo huzuni ikaniingia moyoni. Machozi yaliyoanza kutafuta makazi machoni
mwangu nikayazuia kwa kufumba macho na kumeza funda kubwa la mate ili
kuitowesha hasira kifuani mwangu.
Bila kupoteza muda zaidi nikaikata ile simu kisha nikabonyeza tena vitufe kadhaa
vya simu yangu halafu nikaishikilia vizuri simu yangu. Baada ya kitambo kifupi cha
kusubiri ili simu yangu ipate signals nzuri za mawasiliano hatimaye ile simu ikaanza kuita tena upande wa pili huku nikitarajia kuisikia sauti ya mdunguaji mwingine Private Gina Yhombi-Opango Makiadi codename Lovebird. Hata hivyo hilo halikutokea kwani ile simu iliendelea kuita mara kadhaa pasipo kupokelewa. Kwa kweli nilijihisi
kuchanganyikiwa. Nikaikata ile simu na kuipigia tena huku nikiwa na kihoro cha aina
yake lakini bado ile simu haikupokelewa na tukio lile likazidi kuwa ishara mbaya zaidi
kwangu.
“Lovebird are you there?...zungumza Lovebird unanisikia?” niliendelea kuita lakini ni
kama niliyekuwa nikijiuliza mimi mwenyewe. Ile simu haikupokelewa wala sauti ya
Lovebird kusikika. Moyo wangu ukapiga kite kwa nguvu kisha koo likanikauka na hapo
baridi nyepesi ikaanza kusafiri taratibu nyuma ya mgongo wangu. Sikuwa na namna ya
kuendelea kusubiri zaidi hivyo nikaizima simu yangu ya upepo na kuichimbia kwenye
mfuko wa gwanda langu huku nikiwa nimeanza kuingiwa na hofu ingawa sikutaka
kupoteza umakini.
Muda mfupi uliyofuata nikaifyatua bi-pod stand ya bunduki yangu Sniper Rifle 338
Lapua Magnum na kuikunja vyema kisha nikaanza kujivuta taratibu nikiteleza kwenye
tawi lile la mti kwa ulaini kama Boomslang nyoka hatari kwa vipenyo. Kwa namna
nilivyojipamba kwa majani mwili mzima jicho lolote la kiumbe hai eneo lile lisingesita
kunifananisha na kichaka.
Kidole cha mkono wangu wa kushoto kikiwa kimekamata vyema kilimi cha Sniper
Rifle nikaifyatua kamba iliyokuwa kiunoni mwangu na kuifunga kwenye tawi imara
la mti kisha kwa msaada wa kamba hiyo nikaanza kushuka kwenye mti ule taratibu
huku mara kwa mara nikiweka vituo kutazama hali ya usalama wa eneo lile. Wakati
nilipokuwa nikikaribia kufika chini ya ule mti mara hisia mbaya zikanijia kuwa sehemu
fulani mbali kidogo kwenye msitu ule macho ya mtu fulani yalikuwa yakinitazama na
hali ile ikazidi kunipa wasiwasi. Hivyo nilipomaliza kushuka chini ya ule mti haraka
nikaivuta ile kamba na kuanza kuikunja na wakati nikifanya hivyo kiasi cha umbali wa
kama mita miamoja na ushei mbele yangu nikakiona kichaka kidogo kikichezacheza
baada ya mwanga mkali wa radi kumulika eneo lile.
Hofu ikazidi kunishika hivyo nilipomaliza kuikunja vizuri ile kamba nikajibanza
nyuma ya ule mti niliyoushuka muda mrefu uliyopita na bila shaka bahati ilikuwa
kwangu kwani ni muda uleule risasi iliniparaza begani na kuvunja tawi la mti uliyokuwa
jirani na eneo lile. Nikajua kuwa maficho yangu tayari yalikuwa yamefichuliwa. Adui
yule alikuwa mdunguaji mahiri sana aliyeweza kucheza vizuri na akili yangu. Ile risasi
moja aliyoifyatua alikaa kimya tena akitaka kuniaminisha kuwa nilikuwa nikiota juu ya
tukio lile au huwenda yale yalikuwa mawazo yangu.
Nilimuelewa vizuri na kwa kutaka kulithibitisha hilo nikautikisa kidogo mti mfupi
usawa wa kimo changu uliyokuwa jirani yangu kwa buti langu gumu mguuni. Mti ule
mfupi ulipotikisika risasi moja akakata vitawi vidogo vya mti ule na kuvipeperusha
hewani na hapo nikajua kuwa adui yule alikuwa mtu makini sana na kazi yake. Kisha
baada ya pale hali ya ukimya ikafuatia tena.
Wakati nikiwa nimejibanza nyuma ya ule mti sikutaka kujiridhisha kuwa pale nilikuwa sehemu salama. Mvua ilikuwa imeanza kunyesha tena sambamba na upepo mkali uliyoanza kuyumbisha matawi ya miti na vichaka vya eneo lile. Ilikuwa ahueni kwangu kwani adui yule mkorofi kwa vyovyote angepoteza umakini kwa kuyumba
kwa vichaka vile. Hivyo kwa kuichangamkia vizuri fursa ile nikajitupa chini na kuanza tutambaa kwa tumbo nikienda mbele kutoka usawa wa ule mti. Muda mfupi baadaye nikawa nimefanikiwa kujichomeka kwenye kichaka cha jirani na eneo lile. Niligeuka tena kutazama kule kwenye kile kichaka na sikuona chochote ingawa hali ile haikuweza kunithibitishia kuwa adui yule alikuwa amenisamehe.
Kichaka kile hakikuwa maficho mazuri ingawa kilinihifadhi kwa muda kidogo
kabla ya kutambaa tena na kuhamia kwenye kichaka kingine kilichoshiba miti zaidi
kilichokuwa eneo lile pembeni. Nikiwa katika kichaka kile niliitumia tena darubini ya
bunduki yangu kulichunguza eneo lile hata hivyo kwa kuwa ule mti niliyojibanza hapo
awali ulikuwa umenizuia kuona kule nyuma ilinibidi nihamie kwenye kichuguu kidogo
kilichokuwa mbele kidogo ya eneo lile.
Nikiwa nyuma ya kichuguu kile niliifyatua bi-pod stand ya Sniper Rifle na kuitega
vyema kisha kupitia darubini yake yenye nguvu nikaanza kufanya scaning makini eneo
lile. Sikuweza kuona kitu chochote eneo lile na hali ile ilinishangaza sana. Kile kichaka
ambacho hapo awali kilikuwa kikitikisika sasa kilikuwa kimetulia pia sikuweza kuona
kiumbe chochote eneo lile hivyo mwishowe nikakata tamaa kabisa huku nikiunyanyua
mkono kuitazama saa yangu ya mkononi na wakati nikifanya hivyo mwanga wa radi
uliyomulika eneo lile ukanisaidia kuona kule mbele.
Mtu fulani alikuwa amechepuka kutoka nyuma ya mti mmoja uliyokuwa eneo
lile na kwenda kujibanza nyuma ya mti mwingine kiasi cha umbali wa mita mia moja
na ushei mbele yangu na hapo nikatabasamu na kujifuta maji ya mvua yaliyokuwa
yakichuruzika uso wangu. Nikajilaza tena vizuri nyuma ya kichuguu kile kisha
nikalisogeza jicho langu kwenye Eyepiece Lens ya darubini ya Sniper Rifle na safari hii
nilichokiona kikanipelekea nizidi kutabasamu.
Yule mtu sasa alikuwa amejibanza nyuma ya ule mti na kwa kuwa ule mti ulikuwa
mwembamba kidogo ilikuwa ni sawa na mtu aliyejifunika shuka fupi kwani mabega
yake yalikuwa yakionekana. Yule mtu alikuwa amejikinga nyuma ya ule mti huku
akiitumia nafasi ile kujaza risasi kwenye bunduki yake na hilo lilikuwa kosa kubwa
kwani nilimjaza vizuri akaenea kwenye Objective Lens ya darubini yangu na hapo
nikavuta pumzi nyingi na kuibana. Risasi moja niliyoiruhusu ikaniletea majibu ya
hakika kwani risasi hiyo ilipenya kwenye bega lake la kulia kisha ikapekenya mfupa
wake na kuendelea mbele na safari. Yule mtu akapiga yowe kali huku bunduki yake
ikimponyoka mkononi na kuangukia chini na hapo akayumbayumba na kupoteza
mhimili. Hilo likawa kosa jingine kwani kwa kufanya vile kichwa chake kikaenea
vizuri kwenye lenzi ya darubini yangu. Tukio lile likanifanya nipige mruzi mwepesi
wa furaha. Risasi nyingine niliyoiruhusu kufunga safari ikakifumua vibaya kichwa cha
yule adui na kuutawanya vibaya ubongo wange huku yule adui akitupwa hewani. Jicho
langu bado halikuhama kwenye Eyepiece Lens ya darubini yangu hivyo yule mtu wakati akitua chini nikamkandamiza kwa risasi nyingine ya kifua iliyomlaza chali kimya. Kazi ikawa imekwisha hivyo nikaitoa pipi yangu ya kijiti kutoka mfukoni kisha nikaimenya na kuitia mdomoni.
Niliendelea kujibanza nyuma ya kile kichuguu huku jicho langu likiendelea kufanya kazi kwenye ile darubini kulichunguza eneo lile hadi pale niliporidhika kuwa hali ya usalama wa eneo lile ilikuwa shwari ndiyo nikachukua mashine yangu ya kazi na kusimama. Niliitazama tena saa yangu ya mkononi na kushtuka kuwa muda ulikuwa
umeenda tangu nilipoongea na Chameleon.
Niliichukuwa tena simu yangu ya upepo na kumpigia Chameleon lakini simu haikupokelewa. Nikampigia tena simu Lovebird lakini bado hali ilikuwa vilevile kwani ile simu yake haikupokelewa. Sikupenda kuendelea kupoteza muda zaidi hivyo muda mfupi uliyofuata nilikuwa nikiupangua msitu ule kwa mbio zisizo za kawaida.
Kwa kuwa nilikuwa nikiyafahamu vizuri maficho ya wenzangu hivyo sikupata shida katika kuwafikia. Nilimkuta Sajenti Chacha Marwa Code-name Chameleon akiwa ameegemea jiwe kubwa kando ya maficho yake na hapo nikajua kuwa baada ya
Chameleon kushambuliwa na adui alikuwa ametoroka kwa shida na kujificha nyuma
ya jiwe lile. Mdomo na macho yake vyote vilikuwa wazi ingawa nilipomsogelea na kumshika alikuwa wa baridi huku kifo tayari kikiwa kimemchukua. Damu nyingi kutoka kwenye majeraha yake ya risasi kifuani na begani ilikuwa imezitotesha vibaya gwanda zake. Kitu cha ajabu na kilichonishangaza ni kuwa Chameleon hakuwa na ile redio yake ya upepo wala ile silaha yake ya kudungulia adui na hali ile ilinitia mashaka
sana. Nilisimama kidogo nikimtazama Chameleon kwa huzuni kama mtu ambaye
nisingeweza kuonana naye tena hapa duniani. Sikuwa na jinsi hivyo nikamsogelea
pale alipoketi na kumfumba mdomo na macho yake huku nikizikumbuka enzi za
urafiki wetu tangu tulipoanza kufahamiana kwenye tume ya udhibiti na upambanaji
wa biashara haramu ya dawa za kulevya jijini Dar es Salaam. Hivyo nikaichukua kamera yangu ndogo na kumpiga picha chache kama sehemu ya kumbukumbu zangu za mwisho kwake.
Muda mfupi baadaye nilikuwa tena porini nikikimbia kuelekea kwenye maficho
ya mdunguaji mwingine Private Gina Yhombi-Opango Makiadi codename Lovebird.
Kwa kweli nilichokiona baada ya kufika kilizidi kupeleka simanzi moyoni mwangu.
Nilimkuta Lovebird akiwa ananing’inia mtini kama nyama ya ng’ombe kwenye mtungo buchani. Ni kama alikuwa kwenye jitihada za kushuka kutoka juu ya mti ule yalipokuwa maficho yake lakini hakuwa amefanikiwa kutimiza adhama yake. Risasi za adui zilimfumania wakati akiwa anakaribia kufika chini ya ule mti na hivyo kumuacha akining’inia kwenye kamba ile huku umauti ukiwa tayari umemfika. Mbaya zaidi ni
kuwa Lovebird hakuwa na kichwa na badala yake kilibakia kichuguu cha shingo yake
tu ambacho kwa wakati huu kilikuwa kikiendelea kuvuja damu taratibu. Risasi kali za
adui zilikuwa zimekifumua kichwa chake na kuutawanya ovyo ubongo wake.Roho iliniuma sana kwa kumpoteza rafiki yule mwenyeji wetu hata hivyo sikuwa na jinsi. Machozi yalinitoka wakati nikichukua picha zake kwa kamera yangu ndogo yadigital. Nilipoendelea kumchunguza vizuri Lovebird nikagundua kuwa kama ilivyokuwa
kwa Chameleon naye pia silaha yake na vitu vyake muhimu vilikuwa vimechukuliwa
bila shaka na adui. Kilichonisikitisha zaidi ni kuwa hata ile kamera yake kubwa ya
ki-uandishi wa habari vitani aina ya Toymaster ilikuwa imekwenda. Mbali na kuwa
mwanajeshi na mdunguaji mahiri Private Gina Yhombi-Opango Makiadi codename
Lovebird pia alikuwa mwandishi wa habari aliyeajiriwa na shirika la habari la The Reuters
kwa mkataba akichukua picha matukio ya vitani. Hivyo ile kamera ya kuchukulia
picha za matukio alikuwa amepewa na shirika hilo.
ITAENDELEA
 
Kuweni makini pitieni mara kwa mara kwenye post yangu kwani huwa narudi napost humohumo kwenye uzi wangu mpaka ijae ndo naweka kwengine. Mkiona sijaandika itaendelea jueni narudi kujazia
 
RIWAYA:MIFUPA 206
MTUNZI:KELVIN e MPONDA
0688058669

2
Wakati nikiendelea kutafakari tukio lile hisia fulani zikanijia akilini. Hisia
ambazo zilinisukuma na kunifanya nitake kurudi kule kwenye yale maficho yangu
nilipomchakaza vibaya yule adui mkorofi aliyekuwa amejificha nyuma ya ule mti.
Nilikubaliana vizuri na hisia zangu kwa haraka na hapo nikageuka na kuanza kutimua
mbio nikirudi kule kwenye maficho yangu nilipotoka. Ingawa kulikuwa na umbali wa
kueleweka lakini katika hali ile ya kuwapotea wenzangu sikuona adha yoyote.
Baada ya mbio ndefu kidogo nikawa nimefika kwenye yale maficho yangu kule
msituni kisha nikaelekea kwenye ule mti nilipomchakaza vibaya yule adui. Nilipofika
nikaiwasha tochi yangu na kummulika yule adui pale chini. Nilichokiona kikaupelekea
mwili wangu ushikwe na ganzi. Taharuki ikausimanga moyo wangu na hapo
nikaachama mdomo kwa mshangao.
Kwa dakika chache zilizopita taswira iliyoumbika machoni mwangu ilikataliwa
kabisa kufanyiwa tafsiri na ubongo. Koo likanikauka mate na hapo jasho jepesi
likaanza kunitoka sehemu mbalimbali za mwili wangu. Maiti yule mtu aliyelala pale
chini ilikuwa ni ya Meja Khalid Makame mpiganaji na mtanzania mwenzetu na vilevile
msimamizi wa shughuli zote za wadunguaji katika jeshi la MONUSCO. Ingawa kichwa
chake nilikuwa nimekichangua vibaya kwa risasi lakini nilimkumbuka vizuri kupitia
cheo chake kilichokuwa mabegani na jina lake lililokuwa kwenye beji yake kifuani.
Kwa kweli nilijihisi kuchanganyikiwa huku nikijiuliza maswali mengi yasiyokuwa
na majibu. Kitu cha kushangaza zaidi ni kuwa ile kamera ya Lovebird aina Toymaster Meja
Khalid Makame alikuwa ameining’iniza kiunoni mwake halafu mbali na ile bunduki
yake pia alikuwa na bunduki nyingine mbili pamoja na zile redio mbili za upepo yaani
redio ya upepo na Chameleon na ile ya Lovebird. Nilisogea zaidi na kuzichunguza vizuri
zile bunduki na mara hii nikazikumbuka kuwa bunduki moja ilikuwa ni ile ya Lovebird
na ile nyingine ilikuwa ya Chameleon na hapo tusi zito la hasira likaniponyoka mdomoni.
Sasa nilikuwa nimepata picha kamili juu ya hali ya mambo ilivyokuwa ikiendelea
Kwa tafsiri ya haraka ni kuwa Meja Khalid Makame alikuwa ametusaliti wapiganaji
wake. Nikaanza kukumbuka misukosuko ya mambo yote yaliyotokea kwenye tume
ile ya udhibiti na upambanaji wa biashara haramu ya dawa za kulevya kule jijini Dar es
Salaam-Tanzania kabla ya kuenguliwa kwetu kwenye tume hiyo. Sikuwa na shaka tena
kuwa mimi na Sajenti Chacha Marwa tulikuwa tumeuzwa na tangu tulipoanza safari
ya kuja hapa nchini D.R Congo roho zetu tayari zilikuwa zimewekwa kwenye mnada.
Loh! jasho jepesi likaanza kunitoka mwilini huku hasira zikinipanda hasa pale nilipowaza kuwa ukweli wetu ndiyo ulikuwa umepelekea roho zetu ziwekwe rehani.
Kwa kweli niliumia sana moyoni na hapo ndiyo wazo la safari mpya likachipua katika
fikra zangu. Safari ya kufa na kupona. Safari ya kurudi jijini Dar es Salaam nikiwa
katika sura na mwonekano mpya kabisa. Niliichukua ile kamera yangu haraka na
kuipiga picha ile maiti ya Meja Khalid Makame pale chini kisha nikaitia mfukoni halafu
nikaichukua ile kamera ya Lovebird aina ya Toymaster iliyokuwa kiunoni mwa maiti ya
Meja Khalid Makame na muda mfupi uliyofuata nilikuwa nikiupangua tena ule msitu
kwa mbio zisizo za kawaida nikirudi kule kwenye maficho ya mdunguaji Lovebird.
Nilikuwa nimepata wazo fulani kichwani,wazo ambalo sikupenda kupoteza muda
katika kulifanyia kazi. Nilifika kwenye yale maficho ya Lovebird na kuukuta mwili wake
bado ukiwa unaning’inia kwenye ile kamba hivyo nikaikata ile kamba kwa kisu changu
na kuushusha mwili wake chini. Halafu pasipo kupoteza muda nikamvua Lovebird zile
gwanda zake za kijeshi na nilipomaliza nikavua na gwanda zangu kisha zile gwanda
zake nikazivaa mimi na zile gwanda zangu nikamvalisha yeye. Hivyo kwa vyovyote
vile mtu yeyote katika kikosi chetu cha kijeshi ambaye angekuja pale na kuiona ile
maiti ya Lovebird eneo lile bila shaka angedhani kuwa yeye ndiye mimi kwani maumbo
na rangi zetu za ngozi vilikuwa vinafanana sana na zaidi ya yote gwanda zile za kijeshi
nilizomvalisha Lovebird zilikuwa na utambulisho wangu kama cheo changu na nembo
ndogo ya bendera ya taifa langu Tanzania.
Huku nikiona kuwa muda ulikuwa ukiyoyoma haraka niliisogeza ile maiti ya
Lovebird na kuilaza kwenye nyasi nzuri za ukoka zilizokuwa chini ya mti ule aliyoukwea
hapo awali. Kisha nikasimama na kufanya ishara ya msalaba usoni mwangu huku
machozi yakinitiririka mashavuni bila jitihada zozote za kuyazuia kufanikiwa.
“Kwa kheri! comrade Mungu akipenda tutaonana tena jijini Dar es Salaam” nilijikuta
nikiisemesha maiti ya Lovebird huku hasira imenijaa kifuani. Muda mfupi uliyofuata
nilikuwa mbali na eneo lile.
Mvua kubwa ilikuwa ikiendelea kunyesha sambamba na radi kubwa na upepo
mkali katika misitu ile mizito ya Ikweta nchini D.R Congo. Kwa mujibu wa ramani
yangu ndogo ya kijasusi ya kukunja iliyokuwa mfukoni ni kuwa ule uelekeo nilioushika
ulikuwa ni wa kuelekea upande wa mashariki ulipo mpaka wa nchi ya D.R Congo na
nchi ya Rwanda.
Bunduki yangu ya kudungulia adui Sniper Rifle aina ya 338 Lapua Magnum ikiwa
inaning’inia begani wala sikuwa na shaka yoyote na kiumbe chenye uhai ambacho
kingeamua kuniwekea pingamizi la aina yoyote mbele yangu safarini. Mvua kubwa
bado ilikuwa ikiendelea kunyesha katika misitu ile minene na mizito ya Ikweta.

****** ********

PROFESSIONAL PRIVATE DETECTIVE AGENT – Chaz Siga. Kwa mara
nyingine nilipomaliza kuyasoma maelezo yale yaliyoandikwa kwenye kioo cha
mlango wa ofisi yangu akili yangu ikapata afya njema na hisia zangu za kikazi
zikafufuka upya na kunifanya nijihisi kuwa sasa nimerudi tena kazini baada ya likizo
ndefu ya miezi kadhaa kwenye ofisi yangu hii ya upelelezi wa kujitegemea iliyopo
kwenye ghorofa tano ya shirika la nyumba la taifa katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Ofisi hii ni kama ilikuwa mpya kwangu na hivyo kunifanya kila kitu nikionacho
humu ndani kuwa kigeni kabisa machoni mwangu. Likizo ilikuwa imeniweka mbali
kabisa na ofisi hii huku nikijitahidi kwa kila hali kuzifukuza fikra zangu mbali na
mazingira haya.
Kabla ya likizo nilikuwa nikijishughulisha na upelelezi wa kifo cha msichana
mmoja mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam aliyejiua kwa kujirusha chini
kutoka ghorofa ya sita ya hoteli moja maarufu iliyopo katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Kutoka kwenye chumba alichosemekana kukikodi siku mbili kabla ya umauti wake.
Nimewahi kuona aina nyingi za vifo vya ajabu na vya kutisha lakini kifo cha
msichana yule Muyasa Munge mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa shahada ya
usimamizi wa rasilimali watu si tu kilikuwa kimenishtua na kuniogopesha lakini hata
sababu iliyopelekea kifo chake ilikuwa ni habari ya kuvutia.
Nakumbuka siku ile nikiwa katika mizunguko yangu ya kawaida katikati ya jiji
la Dar es Salaam taarifa zile za kujiua kwa kujirusha kutoka ghorofani za msichana
Mayasa Munge zilinikuta katika mgahawa mmoja uliyopo umbali mfupi karibu na
eneo lile la tukio nikijipatia kikombe cha kahawa muda mfupi baada ya kutoka ofisini
kwangu.
Nilikuwa miongoni mwa mashuhuda wachache wa mwanzoni waliowahi kufika
chini ya hoteli ile kushuhudia maiti ya msichana yule muda mfupi kabla ya mwili wake haujaondoshwa na polisi waliofika eneo lile. Nilipoitazama mara moja tu maiti ya
Mayasa Munge nikajua kuwa alikuwa amedhamiria kujiua.
Kichwa chake kilikuwa kimepasuka upande wa pembeni wa sikio lake la kulia
na hivyo kuupelekea ubongo wake kusambaa sehemu ile alipoangukia. Damu
nyigi ilikuwa ikimtoka puani,machoni na masikioni. Pembeni yake niliyaona meno
yake manne yaliyovunjika kutoka kinywani. Sehemu iliyosalia ya mwili wake ilifaa
kutazamwa. Mapaja laini yaliyonona yaliyojificha ndani ya suruali yake nyepesi ya jeans.
Kiuno chake chembamba chenye aina tofauti za shanga na mstari wa nywele fupi na
laini uliotoka sehemu ya katikati ya mapaja yale na kuishia kitovuni.
Blauzi yake ilikuwa imetatuka vibaya pengine kutokana na rabsha za mwanguko
wake na hivyo kuyapelekea matiti yake yasiyositiriwa ndani ya sidiria kubaki wazi.
Hali iliyompelekea kila mtu aliyefika eneo lile kujionea malighafi ile bila kificho huku
nywele zake ndefu,nyeusi na laini zikiwa zimechanguka ovyo.
Sikuweza kuiona vizuri sura yake kutokana na damu nyingi iliyotapakaa usoni
mwake lakini haiba yake ilinieleza kuwa Mayasa Munge alikuwa msichana mzuri sana
machoni mwa watu. Bado naikumbuka vizuri taswira yake.
Nikiwa nataka kufahamu sababu iliyompelekea msichana yule ajiue kikatili
namna ile sikupoteza muda hivyo nilikuwa wa kwanza kufika eneo la mapokezi
la hoteli ile lile tukio la kujiua lilipotokea. Kupitia mhudumu wa hoteli ile nikapata
maelezo niliyoyataka. Msichana yule aliyejiua alikodi chumba hotelini pale siku mbili
zilizopita na alikuwa akimsubiri mwanaume. Mwanaume huyo alipofika mhudumu
yule akaniambia kuwa hakuwaona tena wapenzi hao wakitoka tangu walipoingia
chumbani.
Baada ya maelezo ya yule mhudumu nikaelekea ghorofa ya sita ya jengo lile la
hoteli kilipokuwa chumba namba101 alichokodi yule msichana mapema kabla ya
polisi hawajafika na kuanza upelelezi. Nilichokikuta ndani ya chumba kile kilikuwa
ushahidi tosha juu ya tukio lile la kujiua kwa yule msichana.
Chumba kilikuwa kidogo cha wastani chenye kitanda kikubwa cha futi sita kwa
sita,zulia maridadi jekundu sakafuni na runinga kubwa ukutani na zaidi ya hapo
hapakuwa na kitu kingine cha kunivutia mle ndani.
Upande wa kushoto wa chumba kile dirisha kubwa lilikuwa wazi na hapo
nikatambua kuwa yule msichana aliyekufa alijirusha kupitia dirisha lile muda mfupi
uliyopita.
Nilikuwa na hisia kuwa endapo ningechelewa mle ndani huwenda polisi
wangenikuta mle chumbani hivyo bila ya kupoteza muda nilianza uchunguzi.
Mara tu nilipolisogeza kidogo shuka la kitanda kilichokuwa mle ndani vitu viwili
vikaanguka sakafuni.
Kadi ndogo inayofanana na zile za kutolea pesa kwenye mashine za ATM za
benki na kipande kidogo cha karatasi. Nilipoiokota ile kadi na kuichunguza vizuri
nikatambua kuwa ile haikuwa kadi ya ATM ila kitambulisho cha mwanafunzi wa
chuo kikuu cha Dar es Salaam anayesomea shahada ya usimamizi wa rasilimali watu,mwanafunzi wa mwaka wa mwisho mwenye jina la Mayasa Munge.
Nilikitupa kitambulisho kile juu ya kitanda baada ya kukifuta vizuri ili kuondoa alama za vidole vyangu ambazo huwenda zingekuwa chanzo kizuri cha upelelezi kwa polisi kisha nikaiokota ile karatasi ndogo na kuanza kuyasoma maelezo mafupi yaliyoandikwa juu yake.
‘Binti! nashukuru sana kwa huduma yako ya kimwili. Hakika nimeridhishwa sana na ufundi
wako mzuri wa kitandani,hongera sana!. Leo umeongeza idadi ya wasichana wengi niliyofanikiwa
kuvunja nao amri ya sita tangu nilipojigundua kuwa mimi ni mwathirika wa virusi vya UKIMWI.
Hakuna msichana atakayetumia pesa yangu bila kuifidia,na nakuomba usijihangaishe
kunitafuta kwani mimi huwa sirudii mwanamke. Siku njema!
-Kampeni inaendelea’.
Nilimaliza kuyasoma maelezo kwenye karatasi ile na kuitupia pale kitandani.
Mikasa ya mapenzi haikuwa sehemu ya kazi yangu hivyo niliamua kuwaachia polisi
waendelee na kazi yao.
Nikiwa nimeridhika kuwa nimefuta alama zote za ushahidi wa uwepo wangu
ndani ya chumba kile hatimaye nilifungua mlango na kutoka nje.
Kulikuwa na watu wengi walioongezeka pale chini ya hoteli kushuhudia tukio
lile la kujirusha ghorofani kwa msichana yule Mayasa Munge na wakati nikikatisha
kwenye kundi lile la mashuhuda niliziona sura kadhaa za makachero na waandishi wa
habari waliofika kufuatilia kilichokuwa kikiendelea eneo lile. Nikashika hamsini zangu.
_____
MIEZI MINNE SASA ILIKUWA IMEPITA
Taratibu nilikizungusha kiti changu cha ofisi nilichokikalia kwenda upande wa
kushoto sehemu kulipokuwa na rafu yenye mafaili mengi yaliyoshika vumbi na hapo
nikaweka kituo nikiyatembeza macho yangu kudadisi kama kungekuwa na kesi nzuri
ambayo ningeanza nayo kazi.
Faili la kwanza lilikuwa la upelelezi wa kesi ya mbunge wa chama fulani cha siasa
ambaye picha zake za ngono na binti mwanafunzi wa shule moja ya sekondari jijini
Dar es Salaam zilikuwa zimerushwa mitandaoni na kusambazwa kama njugu. Faili
la pili lilikuwa ni juu ya upelelezi wa kesi ya mjumbe mmoja wa kamati ya kukusanya
maoni ya katiba mpya nchini Tanzania aliyeuwawa katika mazingira ya kutatanisha.
Faili la tatu lilikuwa ni la upelelezi wa kesi ya mtandao wa watu fulani wanaosadikika
kuwashambulia viongozi wa dini na kuchoma moto nyumba za ibada. Faili la nne
lilibeba maelezo ya upelelezi wa kesi mbili zilizokuwa bado zipo kwenye uchunguzi
wa kina. Kesi ya utafunwaji wa mabilioni ya fedha za serikali kwenye akaunti ya nje
EPA na miamala ya kihuni iliyoruhusu ukwapuaji na ugawanaji wa mabilioni ya fedha
hapa nchini-ESCROW.
Wakati nikilifikia faili la tano nikasita kidogo baada ya kuisikia simu yangu ya mezani mle ndani ofisini ikianza kuita. Tukio lile likanipelekea nikizungushe kiti changu kuisogelea karibu ile simu pale mezani kisha nikaunyanyua ule mkonga wa
simu na kuuweka sikioni huku macho yangu yakiutazama mlango wa kuingilia mle
ndani.
Sauti nyepesi ya kike kutoka upande wa pili wa ile simu ilinitanabaisha kuwa
mzungumzaji alikuwa Mwasu ama katibu muhtasi wangu kutoka chumba cha pili cha
ofisi yangu.
“Haloo Mwasu!” niliwahi kuongea kabla Mwasu hajaniambia dhumuni la simu ile
baada ya kuisikia sauti yake.
“Bosi! kuna mtu anahitaji kukuona” sauti nyepesi ya Mwasu ilipenya sikioni
mwangu.
“Ana shida gani?”
“Amesisitiza kuwa anahitaji kukuona wewe”
“Mwanaume au mwanamke?”
“Mwanaume,mzee wa makamo”
“Mruhusu aje!”
“Sawa bosi”
Simu ya Mwasu ilipokatwa niligeuka na kuitazama saa ya ukutani mle ofisini huku
mawazo yangu yakisafiri na kufikiri aina ya mgeni anayetaka kuniona.
Baada ya sekunde chache kupita mara nikauona ule mlango wa ofisi yangu
ukifunguliwa kisha machoni mwangu ikajengeka taswira ya mzee mwenye umri
wa miaka hamsini na ushei. Mrefu na mwembamba akiwa katika mwonekano wa
kupendeza wa suti ya rangi ya kijivu na tai nyeusi shingoni akiingia. Uso wa mzee yule
ulifanana na fuvu na namna ya macho yake makubwa na makali pamoja na mtindo
wa unyoaji wa ndevu na nywele zake ulitosha kunifahamisha kuwa mzee yule alikuwa
kachero. Moyo wangu ukapigwa na baridi ya ghafla.
“Karibu mzee” nilimkaribisha mzee yule huku nikimtathmini.
“Nashukuru kijana nimeshakaribia” mzee yule aliniitikia huku akiyatembeza macho
yake mle ndani kuipeleleza ofisi yangu kisha akapiga hatua zake taratibu kuisogelea ile
meza yangu ya ofisini na alipoifikia akavuta kiti na kuketi. Utulivu ukachukua nafasi
yake mle ndani huku macho yangu yakiweka kituo kumtazama yule mzee.
“Jina langu naitwa James Risasi” mzee yule alivunja ukimya.
“Karibu sana mzee”
“Wewe ndiye Chaz Siga?” mzee yule akaniuliza.
“Unataka kuonana na Chaz Siga au huduma inayotolewa na ofisi hii?” nilimuuliza
kwa udadisi zaidi.
“Vyote!” mzee yule akanijibu kwa utulivu huku akiumba tabasamu hafifu usoni
mwake.
“Chaz Siga ndiyo mimi mbele yako mzee na hii ni ofisi yangu”
“Ofisi yako inashughulika na nini?”
“Upelelezi wa kujitegemea na malipo yake hutegemeana na uzito wa kesi yenyewe”
“Una leseni ya kufanyia hii biashara?” mzee yule aliniuliza huku akijipapasa papasa
kisha akaitoa sigara kutoka mfukoni na kuitia mdomoni. Alipokuwa akijipapasa
kutafuta kiberiti nikawahi kumwashia sigara yake kwa kiberiti changu cha gesi
kilichokuwa pale juu mezani na hapo nikamuona akifurahi. Alipoitoa sigara mdomoni
akageuka na kunitazama.
“Bado hujanijibu swali langu” yule mzee akaongea baada ya kuitoa sigara yake
mdomoni na nilipomtathmini vizuri nikamtambua kuwa alikuwa ni mtu mcheshi na
anayependa masihara.
“Wewe ni afisa wa TRA?”
“Nahitaji kufahamu kama ofisi hii inatambulika kisheria ili niwe na hakika ya kazi
yangu kama mteja”
Maelezo ya yule mzee yakanipelekea niweke macho yangu kituo kumtazama kwa
udadisi kisha nikachukua sigara kutoka kwenye pakiti iliyokuwa kwenye mtoto wa ile
meza yangu ya ofisini na kuibana kwa kingo za mdomo wangu. Halafu kwa msaada
wa kiberiti changu cha gesi nikajiwashia na kuvuta mapafu kadhaa. Nilipoitoa sigara
mdomoni niliupuliza moshi wake pembeni kisha nikavunja ukimya
“Tuzungumze kuhusu kazi yako. Ofisi yangu imesajiliwa na huwa nalipakodi kila
ninapohitajika kufanya hivyo” niliongea kwa utulivu huku nikimtazama yule mzee.
“Mimi ni mfanyakazi wa idara maalum ya usalama wa taifa inayoshughulika na
masuala nyeti ya kiusalama” mzee yule aliweka kituo na kuingiza mkono kwenye
mfuko wa koti lake kisha akaitoa picha fulani ambayo aliisogeza karibu yangu pale
juu ya meza.
“Jina lake anaitwa Gabbi Masebo…” akaniambia
Niliichukua ile picha pale juu ya meza na kuitazama kwa makini. Ilikuwa ni picha
ya mwanaume shababi mwenye umri wa miaka thelathini na ushei na mwenye urefu
wa wastani. Mwanaume yule alikuwa amevaa suruali ya jeans na koti jeusi la kodrai.
Uso wake ulikuwa na furaha na alikuwa akitazama kitu fulani ambacho pale pichani
hakikuonekana. Sura yake haikuwa nzuri lakini vilevile isiyochukiza. Uso wake ulikuwa
mwembamba na wenye macho tulivu yaliyohifadhi kumbukumbu ya taswira za
matukio mengi ya nyuma. Pua yake pana na ndevu nyingi zilizokizonga kidevu chake
ziliusanifu vizuri mwonekano wake. Ilikuwa picha ngeni kabisa machoni mwangu.
“Gabbi Masebo…!” nilirudia kulitamka jina lile huku nikizama kwenye tafakari.
“Nataka unitafutie ukweli juu ya mtu huyo” yule mzee aliniambia baada ya kuitoa
sigara yake mdomoni.
“Ukweli kuhusu nini?” nilimuuliza huku macho yangu yakielea juu ya ile picha.
“Kama amepotea au amekufa na kama amekufa nahitaji mifupa yake”
“Mifupa 206?”
Yule mzee akatabasamu kidogo pindi alipoitoa tena sigara yake mdomoni.
“Idadi ya mifupa ya binadamu aliyekamilika akiwa hai au mfu”
“Hilo litakuwa jina la faili litakalobeba maelezo ya upelelezi wa kesi yake-Mifupa
206,unaonaje?” nilimuuliza.
“Bila shaka!”
Nilimtupia macho tena yule mzee nikimtazama kwa udadisi halafu nikageuka
kushoto kwangu na kuchukua faili moja jipya kutoka kwenye rafu ya mle ofisini.
Nilipoliweka lile faili juu ya meza nikavuta mtoto wa meza na kuchukua kalamu kisha
nikaandika juu ya lile faili jina MIFUPA 206 halafu nikaendelea na maelezo kadha wa
kadha kuhusiana na upelelezi wa kesi ile mpya. Nilipomaliza nikayahamishia macho
yangu kuitazama tena ile picha ya Gabbi Masebo kabla ya kumtupia yule mzee swali
jingine.
“Idara yako ya usalama wa taifa inayoshughulikia masuala nyeti imeshindwa kabisa
kukupa majibu ya haja yako?”
“Ningeweza kuifanya kazi hii mwenyewe kama ningekuwa na umri kama wako
lakini kwa sasa mimi ni mzee kama unavyoniona. Gabbi Masebo alikuwa kijana
wangu,rafiki yangu na vilevile mfanyakazi mwenzangu niliyefanyanaye kazi bega kwa
bega. Huu ni mwaka wa kumi tangu Gabbi Msebo alipotoweka kusikojulikana. Siwezi
kusema amekufa au amepotea kwani sina uthibitisho wa hilo ndiyo maana niko hapa”
mzee yule aliweka kituo huku akionekana kusikitika.
“Itakusaidia nini kama ukijua amekufa au amepotea?”
“Kama amepotea nikutanishe naye na kama amekufa nahitaji ushahidi wa mifupa
yake na baada ya hapo kazi yako itakuwa imekwisha!”
Nilitabasamu kidogo huku nikayakung’uta majivu ya sigara kwenye kibakuli cha
majivu ya sigara kilichokuwa pale juu mezani huku nikilitafakari ombi la yule mzee.
Kwa kweli nilikuwa nimeshangazwa sana kwani tangu nianzishe ofisi ile sikiwahi
kutembelewa na mtu mwenye shida kama yake. Nilipomaliza kuyakung’uta majivu ya
ile sigara tukaanza mapatano ya malipo. Baada ya mvutano wa hapa na pale hatimaye
tukawa tumefikia makubaliano kuwa kiasi fulani cha pesa kingetangulia kwenye
akaunti yangu kama malipo ya advance na kiasi cha fedha kilichobaki kingemaliziwa
baada ya kukamilika kwa kazi yenyewe.
Mzee James Risasi alinipa maelezo ya kutosha kuhusu Gabbi Masebo juu ya
mwonekano wake,maeneo gani aliyokuwa akipenda kuyatembelea,hulka na haiba
yake,aina ya marafiki, kimo cha urefu wake na rangi ya ngozi na mambo mengine
muhimu ambayo yangenisaidia katika upelelezi wangu. Kisha akaniambia kuwa Gabbi
Masebo alikuwa ameachana na mkewe miaka miwili baada ya ndoa yao kufungwa
katika kanisa moja maarufu jijini Dar es Salaam. Na katika kipindi hicho cha miaka
miwili ya ndoa yao hawakuwa wamebahatika kupata mtoto.
Nilipomuuliza kama alikuwa na taarifa zozote kuhusu huyo mkewe aliyeachana
naye mzee James Risasi akakiri kutokufahamu mwanamke huyo alipo. Baadaye
akaendelea kunieleza juu ya nyumba ya Gabbi Masebo sehemu ilipokuwa kwa kunipa
jina la barabara na mtaa nyumba hiyo ilipokuwa ikipatikana kule eneo la Sinza jijini
Dar es Salaam.
Hatimaye maongezi yetu yakafika ukomo baada ya mzee James Risasi kunijibu
maswali yangu kadhaa ambayo majibu yake yangenipa angle nzuri ya kuanzia kazi yangu. Tulipomaliza nikampa jina na namba ya akaunti yangu ili pale atakapokuwa
tayari anitumbukize kiasi cha pesa za utangulizi tulichokubaliana huku akisaini baadhi
ya mikataba ya makubaliano yetu.
Hatimaye nikasimama na kushikana mkono na mzee James Risasi tukiagana na
wakati nikishikananaye mkono nikagundua kuwa umri wa mzee yule haukwendana
kabisa na nguvu ya mwili wake. Mzee James Risasi Bado alikuwa mtu mwenye nguvu
na imara kama Simba.
Wakati mzee James Risasi akitoweka mbele ya macho yangu ilikuwa ikielekea
kutimia saa tatu na robo asubuhi. Nilielekea dirishani na kulisogeza pazia ambapo
niliiegemeza mikono yangu na kutazama chini ya lile jengo na hapo nikagundua kuwa
jiji la Dar es Salaam lilikwishachukuwa sura mpya. Foleni za magari kwenye baadhi ya
mitaa ya jiji zilikuwa zimeshamiri na ongezeko la watembea kwa miguu,kelele za watu
na honi za magari na pikipiki viliongeza ziada nyingine.
Niliiacha sigara yangu ikiteketea taratibu mdomoni huku nikiyapanga vizuri
mawazo yangu kichwani juu ya namna ya kuanza na mkasa huu usiyoeleweka. Sigara
ilipoisha nikafunga dirisha na kusogeza pazia kisha nikaelekea kwenye kabati la chuma
lililokuwa pembeni ya meza yangu ya ofisi. Nilipolifikia kabati lile nikafungua droo
yake ya juu na kuchukuwa bastola yangu makini aina ya OTs-38 Stechkin Silent Revolver
yenye uwezo wa kushambulia windo lililopo umbali wa mita 50 katika ukimya wa kifo
na yenye mdomo wa chini na juu. Na wakati nikiichimbia bastola ile kwenye maficho
yangu kiunoni tabasamu hafifu likaivamia sura yangu huku nikimpongeza raia wa
urusi Igor Yakovlevich Stenchkin kwa kusanifu bidhaa matata namna ile.
Nikiwa nimeridhika kuwa nilikuwa nimechukuwa vifaa vyangu vyote muhimu
vya kazi niliufungua mlango wa ofisi yangu na kutoka. Nje ya chumba kile nikawa
nimetokezea kwenye chumba kingine kilichokuwa kikitumika kama ofisi ya katibu
muhtasi wangu. Msichana mrefu mweusi na mrembo wa haja lakini mwerevu na
makini sana aitwaye Mwasu.
Nilimkuta Mwasu akiwa anachapa taarifa fulani kwenye kompyuta yake. Kuniona
mimi kukamfanya aachane na kile alichokuwa akikifanya na kugeuka akinitazama
huku tabasamu maridhawa lingali limejivinjari usoni mwake.
“Vipi bosi mbona unatoka mapema?” Mwasu aliniuliza kwa mshangao kidogo
“Kazi imeanza mama!” nilimwambia huku nikimsogelea pale alipoketi
“Usiniambie…!”
“Yule mzee aliyetoka amekuja na kismati” nilimwambia kwa furaha
“Kazi gani?” Mwasu akaniuliza kwa shauku.
“Anataka nipeleleze na kumpa ukweli juu ya mwenzake aliyetoweka kusikojulikana”
Nilimuona Mwasu akiyatafakari maelezo yangu na kitu cha kushangaza sikuona
tashwishwi yoyote usoni mwake.
“Unadhani kazi inaweza kuwa nyepesi kiasi hicho?” hatimaye Mwasu aliniuliza
huku akinitazama usoni.
“Huwenda ikawa nyepesi au isiwe nyepesi lakini nafikiri kitu cha muhimu ni kuangalia malipo ya kazi yenyewe” nilimwambia Mwasu huku nikimtathmini usoni.
Bado sikuona tashwishwi yoyote na hali ile ikazidi kunishangaza zaidi.
“Sawa! lakini nafikiri unapaswa kuwa mwangalifu zaidi juu ya ombi lake” Mwasu
aliongea kwa utulivu
“Usiwe na wasiwasi Mwasu ingawa bado sijafahamu uzito wa kazi yenyewe lakini
siko tayari kuachana na malipo yake” nilimwambia Mwasu huku nikimshika begani.
Mtu yeyote ambaye angetuona mle ndani angeweza kuhitimisha kuwa tulikuwa
wapenzi lakini hali haikuwa hivyo. Mimi na Mwasu tulikuwa tukiheshimiana sana na
hata kama kulikuwa na hisia za mapenzi baina yetu lakini hadi sasa hakuna aliyekuwa
na ujasiri wa kumweka mwenzake bayana ingawa umri wetu kwa hakika ulikuwa
ukielekeana.
“Sasa unaelekea wapi?”
“Nataka kuvuna taarifa za awali za hii kazi”
“Umeshapata sehemu ya kuanzia?”
“Nadhani hivyo!”
“Sawa! mimi nipo namalizia viporo vya kazi ya jana”
“Usijali endelea na kazi yako mimi natoka kidogo tutaonana baadaye”
“Take care!”
“You too!”
Nilimwacha Mwasu akiwa anaendelea na kazi yake kisha nikaelekea kwenye
mlango ambapo niliusukuma na kutoka nje.
_____
TASWIRA YA MZEE JAMES RISASI ilikuja na kutoweka katika vipindi tofauti
vya fikra zangu na pale taswira hiyo ilipotoweka jina la Gabbi Masebo likachukua nafasi
na hapo hoja mbalimbali zikaanza kuchipua kwenye mawazo yangu. Gabbi Masebo
mwanausalama aliyepotea kwa muda wa miaka kumi iliyopita na kumbukumbu zake
kufutika katika uso wa dunia sasa hoja yake ilikuwa imeibuliwa upya na mzee James
Risasi,mfanyakazi na rafiki yake wa zamani. Swali likabaki ni kweli kuwa jamii yote ya
usalama wa taifa ilikuwa imeshindwa kabisa kutafuta ukweli juu ya kutoweka kwa Gabbi
Masebo?. Swali hili likiwa linaendelea kuzitongoza fikra zangu nikaitia sigara yangu
mdomoni na kujiwashia kwa kiberiti changu cha gesi.
Jiji la Dar es Salaam sasa lilikuwa limepata uhai mpya wakati huu. Baada ya mvua
kubwa kunyesha usiku mzima sasa jiji lilikuwa safi na linalopendeza. Anga lilikuwa
tulivu na hivyo mawingu yanayosafiri angani kuonekana vizuri zaidi na kwa urahisi.
Nilishusha kioo cha dirisha kuuruhusu moshi wa sigara uliyoanza kusambaa
ndani ya gari langu Peugeot 504 kutoroka na hapo nikapata wasaha mzuri wa kuweza
kutathmini athari za mvua ile kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia leo katika eneo lile
la jangwani.
Foleni kubwa ya magari katika eneo lile la jangwani ikanipa nafasi nzuri ya
kutathmini athari hiyo. Mto Msimbazi ulikuwa umezidiwa na wingi wa maji na hivyo kutapisha maji yake katika makazi ya watu na baadhi ya watu hao walikuwa
wamepanda juu ya mapaa ya nyumba zao zilizokuwa hatarini kumezwa na maji hayo.
Kwangu lilikuwa tukio la kushangaza sana katika jiji maarufu kama lile.
Foleni ilipopungua nikapata nafasi ya kupita eneo la Magomeni mapipa kisha
nikaingia Magomeni usalama,Mwembechai,Njiapanda na nilipofika eneo la Kagera
wazo la kuongeza mafuta kwenye gari likanijia baada ya kuhisi kuwa mafuta
niliyokuwanayo kwenye gari yasingetosha kukamilisha mizunguko yangu. Hivyo
nikaingia kwenye kituo cha kujazia mafuta cha Oilcom.
Muda mfupi baadaye nilikuwa tena safarini nikilipita eneo la Manzese, Darajani,
TipTop kisha nikalipita eneo la kona ya Mabibo halafu eneo la Urafiki kabla ya kufika
Legho. Nilipoifikia kona ya Shekilango nikaingia upande wa kulia nikiifuata barabara
ielekeayo eneo la Sinza hadi Kijitonyama.
Nilisafiri na barabara ile kwa kitambo kirefu kama ninayeelekea eneo la
Kijitonyama na nilipofika mbele nikaingia upande wa kulia. Barabara niliyoingia
ilikuwa ni barabara nyembamba ya vumbi iliyokatisha katikati ya makazi ya watu huku
kando yake ikipakana na shughuli nyingi za kibinadamu kama maduka, baa, gereji
bubu na nyumba za kulala wageni za daraja la kati na chini.
Baada ya mwendo mfupi wa safari yangu nikiingia mtaa huu na kutokea mtaa ule
hatimaye nikawa nimetokezea kwenye mtaa mmoja wenye utulivu na wenye nyumba
za kueleweka. Kwa mujibu wa maelezo ya mzee James Risasi ni kwamba nyumba ya
Gabbi Masebo ilikuwa ya mwisho kabisa katika mtaa ule hivyo nikatafuta sehemu
nzuri ya maegesho ya gari langu na kusimama.
Kabla ya kushuka kwenye gari nilitulia kidogo nikiutathmini vizuri mtaa ule na
aina ya wakazi wake. Shughuli za kibinadamu zilikuwa hafifu sana. Niliyaona maduka
mawili ya bidhaa za rejareja na kibanda kimoja cha kuuzia chipsi na karibia nyumba
zote zilizokuwa eneo lile zilikuwa zimekaa kifamilia.
Hakuna mtu yeyote aliyeonekana kuvutwa na uwepo wa gari langu eneo lile
kwa kuzingatia kuwa kulikuwa na magari mengine manne niliyoyakuta yakiwa tayari
yameegeshwa kando ya barabara ya mtaa ule.
Nikiwa nimeridhishwa na tathmini yangu juu ya mazingira yale nikafungua mlango
na kushuka huku nikianza taratibu kutembea kuelekea mwisho wa mtaa ule sehemu
ilipokuwa nyumba ya Gabbi Masebo. Nilipoikaribia ile nyumba nikagundua kuwa
ilikuwa ni nyumba iliyojitenga na nyumba nyingine za jirani na ilikuwa imezungukwa
na ukuta mrefu kiasi mbele yake kukiwa na geti jeusi.
Nilipokuwa nikilikaribia lile geti la ile nyumba mara nikashtuka kuona mlango
mdogo wa geti lile ukiwa wazi. Hivyo wazo la kuingia mle ndani ya ile nyumba moja
kwa moja likatoweka kichwani mwangu na badala yake nikavuka barabara kuelekea
upande wa pili kulipokuwa na nyumba moja inayotazama na ile nyumba ya Gabbi
Masebo.
Mbele ya nyumba ile kulikuwa na duka hivyo nikajipapasa mfukoni na kutoa sigara
na nilipoitia mdomoni nilikuwa tayari nimeshafika kwenye lile duka. Kijana mdogo anayekimbilia umri wa balehe muuzaji wa duka lile akaniamkia kwa heshima zote
“Shikamoo!”
“Marahaba kijana, hujambo!”
“Sijambo!”
“Nipe kiberiti” nilimwambia yule kijana aniuzie kiberiti ingawa tayari nilikuwa
na kiberiti mfukoni huku lengo langu likiwa ni kutaka kumdodosa mambo mawili
matatu juu ya ile nyumba ya Gabbi Masebo. Nilipopewa kiberiti nikajiwashia sigara na
kisha kumlipa pesa ya kiberiti yule kijana. Halafu nikavuta mapafu kadhaa kwa utulivu
na kuupuliza moshi pembeni ya mdomo wangu katika mtindo unaonipendezesha
mwenyewe kisha nikageuka na kumtazama yule kijana muuza duka.
“Wewe ni mwenyeji wa eneo hili?” nilimuuliza yule kijana.
“Siyo sana!”
“Mwenyeji wa nyumba ile unamfahamu?” nilimuuliza yule kijana huku
nikimtazama kwa udadisi.
“Ile nyumba haina mwenyeji”
“Sasa mbona geti lake lipo wazi ni nani anayeishi mle ndani?”
“Hakuna anayekaa mle ndani”
“Na wale ni akina nani?” nilimuuliza yule kijana baada ya kuwaona wanaume
watatu wakitoka kwenye geti la ile nyumba. Mwanaume mmoja alikuwa mfupi na
mnene mwenye kitambi na kipara. Wanaume wawili waliosalia walikuwa wenye
urefu wa wastani na wembamba huku wote wakiwa na umri unaoelekeana wa miaka
thelathini na ushei.
“Yule mwanaume mfupi mwenye kitambi na kipara ni dalali na nahisi amewaleta
wateja kuitazama ile nyumba kwani nasikia kuwa ile nyumba inauzwa”
Maelezo ya yule kijana yalinishtua kidogo hata hivyo nikaitia sigara yangu mdomoni
kisha nikageuka na kuwatazama vizuri wale watu. Mara hii nikawaona wale watu
kuwa walikuwa wakielekea kwenye gari moja jeupe aina ya Land Cruiser lililokuwa
limeegeshwa kando ya barabara ya mtaa ule. Muda mfupi baadaye niliwaona wale
watu wakiingia kwenye lile gari na kuondoka.
Nilimaliza kuvuta sigara yangu kisha nikakitupa kipisi cha sigara ile na kumuaga
yule kijana nikielekea kwenye ile nyumba.
Ule mlango wa geti dogo ulikuwa wazi kama ulivyokuwa umeachwa na wale watu
waliotoka muda mfupi uliyopita hivyo sikupata upinzani wa aina yoyote katika kuingia
mle ndani.
Mara tu nilipoingia mle ndani ya lile geti nilisimama kidogo nikiitazama ile
nyumba iliyokuwa mbele yangu na hapo nikatambua kuwa Gabbi Masebo hakuwa
ni mtu aliyechezea maisha. Pamoja na kuwa ile ilikuwa ni nyumba iliyotelekezwa kwa
muda mrefu bila ya kufanyiwa ukarabati lakini ubora na thamani yake vilikuwa bado
havijatetereka.
Ilikuwa ni nyumba kubwa ya kisasa ambayo ujenzi wake ulikuwa umegharimu
pesa nyingi sana. Upande wa kulia wa nyumba ile kulikuwa banda maalum la kuegesha gari hata hivyo sikuweza kufahamu kama ndani ya banda lile kulikuwa na gari au lah!
kwani mlango wa banda lile ulikuwa umefungwa.
Eneo lote la kuizunguka nyumba ile lilikuwa limefunikwa kwa sakafu nzuri ya
vitofali vidogovidogo vilivyopangwa katika namna ya kupendeza. Upande wa kushoto
wa nyumba ile kulikuwa na sehemu maalum iliyotengenezwa kwa ajili ya kuanikia
nguo na pembeni yake kulikuwa na karo kubwa.
Nikaanza taratibu kutembea nikiizunguka nyumba ile katika namna ya kuipeleleza
na wakati nikifanya hivyo nikashikwa kidogo na mshangao kwani usafi na ubora wa
mazingira ya nyumba ile haukufanana na ule muda wa miaka kumi ambao nyumba
ile ilisemekana kutelekezwa na hapo nikaanza kushikwa na mashaka kuwa huenda
kulikuwa na mtu aliyekuwa akiishi kinyemela ndani ya nyumba ile kwani mazingira
yake yalikuwa masafi.
Baada ya kuyazunguka na kuyapeleleza vizuri mazingira ya ile nyumba hatimaye
nikawa nimefika nyuma ya ile nyumba na hapo nikaviona vyumba viwili vya uani na
banda dogo la wavu.
Nilisogea karibu kuvichunguza vyumba vile. Chumba cha kwanza nilikitambua
haraka kuwa kilikuwa kikitumika kama stoo ya mkaa ya nyumba ile kutokana na
mabaki ya mkaa yaliyokuwa yamesalia mle ndani. Chumba cha pili kilikuwa ni jiko la
nje la ile nyumba.
Nikasogea tena karibu na lile banda dogo la wavu na nilipolichunguza vizuri
nikagundua kuwa lilikuwa likitumika kufugia kuku. Zaidi ya vile sikuona kitu kingine
cha kunivutia hivyo nikapiga hatua zangu taratibu kuuendea mlango wa nyuma wa ile
nyumba.
Mlango ulikuwa umetulia kama uliokufa na sikuona dalili zozote kuwa mlango ule
ulikuwa ukitumika hata hivyo hali ile haikunishangaza. Nikaanza kugonga hodi kwenye
ule mlango hata hivyo sauti ya mwangwi iliyofanywa kwa mwitikio wa ugongaji wangu
ikanifahamisha kuwa nyumba ile ilikuwa tupu. Hivyo nikachukua funguo zangu
malaya kutoka mfukoni kwangu na kuzipachika kwenye tundu la kitasa cha mlango ule
na baada ya kujaribu funguo kadhaa hatimaye ufunguo mmoja ukafanikiwa kufungua
kitasa cha ule mlango. Hivyo nikausukuma ule mlango na kuingia ndani huku taratibu
nikiurudishia ule mlango nyuma yangu. Milango ya vyumba vya ile nyumba ilikuwa
wazi hivyo kupitia mwanga hafifu wa jua uliyokuwa ukipenya kupitia madirisha ya
vyumbani ukaniwezesha kuona kuwa nilikuwa nimetokezea kwenye korido pana kiasi
iliyokuwa imetenganisha vyumba vya nyumba ile kuelekea sebuleni.
Nikiwa makini kuhakikisha kuwa sauti ya hatua zangu haisikiki na kiumbe
chochote hai ambacho kingekuwa mle ndani nikaanza kuzitupa hatua zangu taratibu
nikivikagua vile vyumba vilivyopakana na ile korido. Kama ilivyokuwa ile sauti ya
mwitikio wa ule mwangwi vyumba vyote vya mle ndani vilikuwa vitupu. Hivyo
nikachukua kurunzi yangu ndogo na nyembamba kutoka mfukoni yenye mwanga
mkali kisha nikaiwasha na kuanza kumulika mle ndani nikianzia sehemu za maliwato
ndani ya vyumba vile.
Niliendelea na uchunguzi wangu hata hivyo sikuweza kupata chochote cha maana
ndani ya vyumba vile. Joto kali la jua lililokuwa likiongezeka mle ndani ya ile nyumba
lilinipelekea kutokwa na jasho jepesi kwenye paji langu. Nilijifuta kwa kitambaa
changu cha leso huku nikiendelea kumulika sehemu mbalimbali za mle ndani.
Niliendelea kufanya upekuzi wangu kwa makini nikiingia na kutoka chumba
kimoja baada ya kingine. Vyumba vyote vilikuwa vitupu bila samani hata moja na hali
ile ilinishangaza sana huku nikijiuliza kuwa samani za nyumba ile zingekuwa wapi.
Nilipomkumbuka yule dalali aliyetoka ndani ya hii nyumba muda mfupi uliyopita
huku akiwa ameongozana na wale wanaume wawili warefu hoja ya kuwa huenda
samani za nyumba hii zingekuwa zimechukuliwa na yule dalali ikaanza kujengeka
kichwani mwangu.
Ile nyumba ilikuwa na vyumba vinne vikubwa vyenye sehemu za maliwato,bafu
na makabati ya nguo ukutani. Vyumba vitatu vilikuwa tupu bila ya samani za aina
yoyote ndani yake. Chumba cha nne na cha mwisho kilifaa kuitwa Master bedroom
kutokana na mwonekano wake. Chumba ambacho bila shaka Gabbi Masebo alikuwa
akiishi na mkewe kabla ya ndoa yao haijavunjika.
Nilipoingia ndani ya chumba kile nilisita kuendelea na upelelezi wangu kwani
tofauti na vile vyumba vya awali katika chumba kile kulikuwa na kitanda kikubwa
cha mbao chenye godoro kilichotandikwa vizuri kwa shuka safi na mito miwili ya
kuegemea. Katikati kwenye dari ya chumba kile juu ya kitanda chandarua kisafi
kilikuwa kimening’inizwa.
Nilisimama pale mlangoni nikayatembeza macho yangu mle chumbani kisha
nikazitupa hatua zangu taratibu kuingia mle ndani. Nyuma ya mlango wa chumba kile
kulikuwa na nguo chache za kiume kama mashati,suruali na tai. Nilikizunguka kitanda
cha mle ndani taratibu huku nikikichunguza kwa ukaribu na nilipofika kwenye pembe
moja ya kile chumba nikaona kibeseni kidogo cha takataka ama dustbin. Nilisogea na
kukitazama kile kibeseni na ndani yake kulikuwa na vipisi vya sigara,makasha ya viberiti
vilivyoisha,masalia ya vocha tofauti za muda wa maongezi wa simu zilizotumika,pakiti
tupu za mipira ya kondomu za kiume na kondomu zilizotumika.
Macho yangu yakiwa yameanza kuvutika na aina ya uchafu uliyokuwa ndani
ya kibeseni kile cha takataka niliinama na kuutazama vizuri mchanganyiko ule wa
takataka ili nione kama kungekuwa na chochote cha kunisaidia katika upelelezi wangu.
Nikachukua glovu moja ya mpira kutoka mfukoni mwangu kisha nikaivaa
mkononi na kuanza kupekuapekua ule uchafu. Hakukuwa na chochote cha maana
hivyo nilihamishia upekuzi wangu pale kitandani. Nikaiondoa ile mito ya pale kitandani
kwa uangalifu na kuanza kuifanyia upekuzi hata hivyo sikupata kitu chochote cha
maana. Nikaendelea kutoa shuka na hatimaye lile godoro nikilifanyia upekuzi lakini
bado sikupata kitu chochote cha maana. Hivyo nika virudishia vile vitu vizuri pale
kitandani na hapo hisia za kuwa nilikuwa nikifanya upelelezi usio na tija zikanijia.
Lakini vilevile hisia za kuwa pengine upekuzi wangu ungeniletea majibu ya haja yangu
zikatengeneza ukinzani.Hivyo nikainama tena na kuchunguza chini ya kile kitanda na kwa kufanya hivyo
nikaziona jozi mbili za viatu vya ngozi na kandambili. Nilipovikagua vile viatu sikuona
kitu chochote cha maana hivyo nikasimama na kuanza kuyatafakari mandhari ya mle
ndani. Nikakumbuka kuwa nilikuwa sijafanya upekuzi kwenye zile nguo zilizotundikwa
nyuma ya ule mlango wa kile chumba.
Ndani ya muda mfupi nikawa tayari nimekamilisha upekuzi wangu huku nikiwa
nimepata pakiti moja ya sigara aina ya Portsman yenye sigara mbili ndani yake,kiberiti
chenye njiti chache,noti ya shilingi elfu mbili na burungutu la makaratasi yaliyokunjwa
vizuri. Nikaiacha ile pakiti ya sigara,kiberiti na ile noti ya shilingi elfu mbili na kuchukua
lile burungutu la makaratasi.
Nilipokuwa nikilipekua lile burungutu la makaratasi nikagundua kuwa yale
makaratasi yalikuwa ni hati za ile nyumba kutokana na maelezo yaliyokuwa kwenye
yale makaratasi. Yakieleza idadi ya vyumba vya ile nyumba,ukubwa wa eneo la ile
nyumba na jina la mtaa nyumba ile ilipo. Kitu kilichonishangaza katika hati zile ni
kuwa mmiliki wa nyumba ile hakuwa Gabbi Masebo kama nilivyotarajia kulingana
na maelezo ya mzee James Risasi bali jina la mmiliki wa nyumba ile aliitwa Abraham
Masha. Nikatabasamu kidogo kabla ya kuliyeyusha tabasamu langu haraka usoni
kama kipande cha siagi kwenye kikaango cha moto kisha nikazirudisha zile hati za ile
nyumba pale nilipozichukua.
Hatimaye nikayatembeza macho yangu kwa mara ya mwisho mle chumbani
pembeni ya kile kitanda sehemu kulipokuwa na kiti cha mbao. Juu ya kiti kile nikaiona
chupi nyekundu ya kike na hapo nikajikuta nikipiga mruzi mwepesi. Hatimaye
nikatoka mle ndani na kumalizia upekuzi wangu sebuleni,jikoni,ukumbi mdogo wa
kulia chakula,stoo na bafu ambamo pia sikupata kitu chochote cha maana. Mwishowe
nikatoka kwenye ile nyumba na kufunga mlango pasipo kuacha ushahidi wowote wa
uwepo wangu.
_____
“NAHITAJI KUMFAHAMU mtu anayeitwa Abraham Masha”
“Abraham Masha…!”
“Ndiyo! mtu anayeitwa Abraham Masha. Mnaye mtu yeyote mwenye jina hilo
ofisini kwenu?” nilimuuliza mzee James Risasi baada ya kuitafuta simu yake na kuipata
hewani. Kitambo kifupi cha ukimya kikapita huku sauti ya mzee James Risasi ikipwaya
hewani kabla ya kurudiwa tena na uhai.
“Simfahamu”
“Abraham Masha!...”
“Nimekwambia simfahamu mtu wa namna hiyo”
“Okay! mmiliki wa nyumba ya Gabbi Masebo kwa sasa ni mtu anayefahamika kwa
jina la Abraham Masha” nilimwambia mzee James Risasi katika hali ya kutaka kupata
hakika ya maneno yake.
“Umeenda nyumbani kwake?”
“Nilihitaji kupata mwanzo mzuri wa kazi yangu mzee”
“Umejuaje sasa kama huyo Abraham Masha ndiye mmiliki wa nyumba ya Gabbi
Masebo kwa sasa?”
“Kupitia hati za nyumba nilizozikuta mle ndani”
“Kwanini usifikirie kuwa hizo hati za nyumba ni za nyumba ya mtu mwingine na
siyo za nyumba ya Gabbi Masebo?” mzee James Risasi aliniuliza kwa utulivu na mara
hii nilimuona kuwa alikuwa na hoja yenye nguvu.
“Ni kutokana na maelezo yaliyokuwa kwenye hati ile ya nyumba yanayoeleza
sehemu nyumba ile inapopatikana,ukubwa wa nyumba na eneo lake na jina la mtaa.
Hivyo kwa vyovyote kilichobadilishwa pale ni jina la mmiliki tu. Nadhani hapo
umenielewa sasa”
“Okay! bila shaka huo ni mwanzo mzuri Chaz. Sasa unataka mimi nifanye nini?”
“Tafadhali naomba uchunguze kama Gabbi Masebo alikuwa akitumia jina la
Abraham Masha”
“Okay! vuta subira nitakupigia baadaye” mzee James Risasi alisisitiza
“Sawa! nasubiri jibu kutoka kwako” nilimwambia mzee James Risasi kisha
nikakata simu na kuitia mfukoni nikiendelea na safari yangu. Sasa nilikuwa mbali na
ile nyumba ya Gabbi Masebo.
Niliitazama saa yangu ya mkononi na kuridhika na mwenendo wake. Ilikuwa
ikielekea majira ya mchana na hali ya hewa ya jiji la Dar es Salaam ilikuwa ni ya joto
kali kana kwamba mvua haikuwa imenyesha usiku wa jana. Jua lilikuwa kali mno na
hivyo joto lilikuwa likiongezeka kila dakika iliyoyoma.
Wazo la kupata chakula cha mchana lilikuwa limenijia kichwani baada ya kusikia
miungurumo ya njaa tumboni na sehemu nzuri ya kupata mlo ambayo nilikuwa
nimeifikiria ilikuwa ni katika mgahawa mmoja maarufu uliyopo eneo la Mlimani City.
Hivyo mara baada ya kutoka nyumbani kwa Gabbi Masebo nilikuwa nimeingia
kwenye barabara ya kutokea Shekilango inayokwenda kukutana na ile barabara ya
Bagamoyo. Mbele kidogo ningeingia upande wa kushoto nikiifuata barabara ya Sinza
makaburini barabara ambayo mbele yake ingenikutanisha na ile barabara ya Sam
Nujoma inayotoka eneo la Ubungo kwenda Mwenge. Hivyo baada ya muda mfupi
ningekuwa eneo la Mlimani City nikijipatia mlo makini.
_____
KULIKUWA NA MAGARI MACHACHE yaliyoegeshwa kwenye eneo la
maegesho ya mgari la Mlimani City hivyo sikupata usumbufu wowote wa kuegesha
gari langu katika viunga vile. Kisha nikashuka na kuelekea mgahawani na wakati
nikiukaribia ule mgahawa tabasamu hafifu likazitongoza fikra zangu.
Ukweli ni kwamba burudani ya kipekee inayopatikana katika eneo la Mlimani City
ni kwamba kila mtu unayemuona au kukutananaye eneo hili hujidai kuwa ni mtu
wa daraja la juu kimaisha wakati watanzania wengi vipato vyetu ni vya kusumbua
kichwa. Kwa wanafunzi wengi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam wanaotoka kwenye mikoa iliyotengwa kimaendeleo hapa ndiyo sehemu yao kubwa ya kusafisha macho
na kujidai. Basi ilimradi ni burudani tu kwa mtu yeyote anayefika eneo hili.
Nilichagua meza moja iliyojitenga na watu na mhudumu alipokuja nikamuagiza
aniletee ugali na samaki aina ya sato,saladi ya matunda na maji baridi ya chupa kubwa.
Mlo ninaoupenda siku zote za maisha yangu.
Wakati nikipata mlo nilipokea simu ya Mwasu iliyokuwa ikinifahamisha juu ya
wateja waliyokuwa wakihitaji kuonana na mimi kule ofisini kwangu. Kwa kuwa
nilikuwa mbali ikanibidi niwape miadi ya kuonana nao jioni na wale waliokuwa na
shida ndogondogo nilimwambia Mwasu amalizane nao.
Nilimaliza kupata mlo wangu wa mchana kwenye mgahawa ule kisha nikamlipa
mhudumu pesa yake na kuondoka nikirudi ofisini kwangu Kisutu.
_____
NILIPORUDI OFISINI nikakumkuta Mwasu akiwa anaendelea na kazi yake
baada na yeye kumaliza kupata mlo wa mchana kwenye mgahawa mmoja uliokuwa
chini kwenye jengo lile la ghorofa.
Wateja wawili waliokuwa wakinisubiri kwenye viti vya wageni vilivyokuwa pale
kwenye ofisi ya Mwasu niliwahudumia haraka mmoja baada ya mwingine. Mteja
mmoja alikuwa mwanamke wa makamo mfupi na mweusi akinitaka nipeleleze juu ya
kupotea kwa mwanawe wa kiume mwenye umri wa miaka kumi na mbili aliyetoweka
na msichana wake wa kazi wakati yeye akiwa kazini. Mteja mwingine alikuwa
mwanaume mwenye umri unaoshabihiana na wangu akinitaka nipeleleze na kumpa
majibu juu ya upotevu wa silaha yake aliyokuwa akiimiliki kihalali.
Wateja wale walipoondoka nilitoka ofisini kwangu na kwenda ofisini kwa Mwasu
chumba cha pili huku nikiwa na lile faili jipya la upelelezi wa kesi ya MIFUPA 206
nikimtaka Mwasu aanze kuandaa maelezo ya awali kufuatana na ule mwenendo wa
upelelezi wa ile kesi ulivyokuwa ukiendelea. Mwasu alilipokea lile faili na kuanza
kunifanyia mahojiano mafupi ambayo yangemsaidia kuandika taarifa zile kiutalaamu
zaidi na kwa kuwa alikuwa mwerevu na mzoefu kazi ile zoezi lile halikuchukuwa
muda mrefu.
Hivyo hatimaye nilirudi ofisini kwangu na wakati nikisubiri majibu kutoka
kwa mzee James Risasi niliendelea na shughuli nyingine za mle ndani zikiwemo
kuandika taarifa za awali juu ya upelelezi wa kesi za huko nyuma ambazo zilikuwa
zimeshawasilishwa ofisini kwangu na wateja ili baadaye Mwasu aziandalie utaratibu wa
kimaandishi utakaomsaidia mhusika afahamu kwa urahisi juu ya mambo yalivyokuwa
kufuatana na tukio lenyewe.
Watu husema ofisi huwa haiishiwi na kazi hivyo nilipomaliza kazi moja nikashika
kazi nyingine ilimradi kazi zote za mle ndani zilikuwa na uhusiano na ofisi yangu.
Mwasu ambaye alikuwa chumba cha pili mara kwa mara nilimsikia akipokea simu
kama siyo sauti ya vitufe vya keyboard ya kompyuta yake alivyokuwa akivibonyeza kwa
haraka kama mitetemo ya sherehani wakati akiandika taarifa za kiofisi. Muda uliyosalia niliutumia katika kupanga vidodoso na vielekezi ambavyo
vingenipa uelekeo makini katika kushughulika na upelelezi wa kesi ya MIFUPA 206
iliyoanza kunivutia kwa namna yake. Hata hivyo mara kwa mara nilijikuta nikisitisha
kwa muda kile nilichokuwa nikikifanya na kupokea simu zilizokuwa zikimiminika
ofisini kwangu bila utaratibu maalum.
Kila nilipopata utulivu mawazo yangu yalijikuta yakizama kwenye tafakari ya kina
juu ya jina la Abraham Masha huku nikishindwa kuelewa nini kilichokuwa kikiendelea
kwenye nyumba ile niliyoitembelea asubuhi.
Hatimaye nilimaliza shughuli zangu zote na kwa kuwa sikuwa na kitu kingine cha
kufanya nikajipumzisha kwenye kiti cha ofisi yangu nikiununua muda kwa kusoma
riwaya ya The Cleaner iliyoandikwa na mwandishi nguli wa riwaya za kipelelezi nchini
Marekani Brett Battles.
Kurasa za riwaya ile zilikuwa zimeniteka fikra zangu na kunitupa kwenye ulimwengu
mwingine na hivyo kunifanya nijihisi kama niliyekuwa mmoja wa wahusika muhimu
katika mkasa ule wa kusisimua.
Ilipofika saa moja kasoro usiku Mwasu alikuja ofisini kwangu na kuniaga kuwa
kulikuwa na sehemu aliyokuwa akihitajika kupitia kabla ya kurudi nyumbani kwake
eneo la Fire nyumba namba 27. Tuliagana na Mwasu akashika hamsini zake huku
akiniacha mle ndani ofini peke yangu nikisafiri kwenye kurasa za mkasa ule wa aina
yake. Masaa nayo yakaendelea kuyoyoma huku nikiwa makini kuisibiri simu ya mzee
James Risasi.
Hatimaye mlio wa simu ukazipokonya fikra zangu zilizokuwa zikisafiri kwa hisia
kali kwenye mkasa ule wa kusisimua wa mpelelezi makini Jonathan Quinn. Nikaichukua
simu yangu kwa hamasa kama iliyopokea ujumbe wa ingizo la pesa na nilipoitazama
simu ile nikaiona namba ya mzee James Risasi ikiita na hapo mzuka wa kazi ukaniingia
upya.
“Uko wapi?” sauti ya mzee James Risasi ikasikika upande wa pili mara tu
nilipobonyeza kitufe cha kupokelea na kuiweka simu sikioni.
“Ofisini kwangu,vipi umepata chochote kuhusu Abraham Masha?”
“Gabbi Masebo hakuwahi kutumia jina la Abraham Masha” mzee James Risasi
akaongea kwa utulivu.”Nimejaribu kutafiti kwenye vyanzo vyote muhimu lakini jina
la Abraham Masha halipo”
“Kwa hiyo jina la Abraham Masha huwenda likawa jipya kabisa kwako!”
nilimwambia mzee James Risasi.
“Kwa sasa ninaweza kusema hivyo”
“Lakini umechelewa sana kunipa majibu”
“Nililazimika kutafiti katika kila idara hapa ofisini”
“Okay! nashukuru sana mzee”
“Hatua gani inayofuata?” mzee James Risasi akaniuliza kwa udadisi
“Nafikiri ni kufuatilia na kufahamu huyu Abraham Masha ni nani halafu baada ya
hapo nitajua nini cha kufanya”
“Sawa basi utaendelea kunifahamisha yatakayojili”
“Ondoa shaka!” niliongea kwa utulivu kisha simu ile ilipokatwa upande wa pili
nikaitia simu yangu mfukoni huku jina la Abraham Masha likianza tena kuzitawala
fikra zangu.
Saa ya ukutani ya mle ndani ofisini ilionesha kuwa dakika chache zilikuwa zimesalia
kabla ya kutimia saa nne usiku. Nikashtuka kuwa masaa yalikuwa yakiyoyoma sana.
Sikuwa na muda wa kupoteza tena hivyo nilikiweka kile kitabu cha riwaya kwenye
mtoto wa meza kisha nikasimama na kuelekea ukutani ambapo nilizima taa ya mle
ndani halafu nikaelekea mlangoni na kutoka.
_____
NILIWASILI ULE MTAA WENYE NYUMBA ya Gabbi Masebo ikiwa tayari
imetimia saa sita na dakika chache usiku. Kabla ya kufika pale nilikuwa nimeamua
kupitia kwenye mgahawa mmoja uliyopo eneo la Kariakoo kujipatia mlo wa usiku.
Niliegesha gari langu umbali mfupi kabla ya kuifikia ile nyumba ya Gabbi Masebo
na wakati huu wa usiku barabara ya mtaa ule ilikuwa imemezwa na ukimya wa namna
yake. Hakukuwa na gari lolote lililoegeshwa wala watu waliokuwa wakirandaranda
eneo lile na hali ile iliashiria kuwa muda ulikuwa umeenda na wakazi wa mtaa ule
wengi walikuwa usingizini.
Niliporidhika kuwa hali ya eneo lile ilikuwa tulivu nikashuka kwenye gari
na kuelekea kwenye ile nyumba ya Gabbi Masebo. Ule mlango wa geti ulikuwa
umerudishiwa tu bila kufungwa kwa ndani na komeo hivyo niliusukuma taratibu na
kuingia ndani.
Taa za ndani na nje ya nyumba ile zilikuwa zimezimwa hata hivyo hilo halikunifanya
nisite kuendelea na harakati zangu.
Hii ilikuwa ni mara yangu ya pili kufika kwenye nyumba ile hivyo niliingia ndani
kama mwenyeji. Hata hivyo kwa tahadhari ya hali ya juu kiasi kwamba mtu yeyote
ambaye angekuwa ndani ya ile nyumba asingeweza kunisikia.
Sikuwa mtu wa kuamini kitu kinachoitwa bahati hivyo taratibu niliichomoa bastola
yangu kutoka mafichoni na kuikamata vyema mkononi kisha nikaanza kutembea
taratibu kuizunguka ile nyumba huku macho yangu yakijitahidi kulikagua eneo la
mbele yangu kabla sijalifikia.
Nilipokaribia usawa wa kile chumba chenye kitanda nikasikia sauti hafifu za
mahaba na miguno ya watu waliopagawa kwa penzi. Nilizisikiliza sauti zile na hapo
nikajua kuwa mle ndani kulikuwa na mwanamke na mwanaume. Nilijaribu kuzizoea
vizuri sauti zile za kimahaba masikoni mwangu na niliporidhika kuwa hakukuwa na
ongezeko la sauti nyingine ndani ya ile nyumba nikapiga hatua zangu kwa utulivu
nikielekea nyuma ya nyumba ile. Nilipofika nikasimama kidogo nikidadisi kama
kungekuwa na ongezeko la sauti nyingine ya mtu au watu mle ndani ya ile nyumba.
Hali bado ilikuwa shwari hivyo niliusogelea ule mlango wa ile nyumba kisha
nikapachika funguo zangu malaya kwenye kile kitasa. Kwa jitihada kidogo tu mlango ule ukafunguka hivyo nikausukuma taratibu na kuingia mle ndani ya ile nyumba huku
nikiurudishia nyuma yangu.
Sasa niliweza kuzisikia vizuri zile sauti za mahaba namna zilivyokuwa zikihanikiza
mle ndani na hapo nikajikuta nikiwalaani binadamu wale kwa namna walivyokuwa
wafujaji wa mapenzi.
Hata hivyo nilizipuuza zile sauti na hapo nikaanza kufanya uchunguzi kwenye
vile vyumba vingine vilivyokuwa tupu hapo awali katika kutaka kujiridhisha na hali
ya usalama wa mle ndani. Hatimaye nikahitimisha safari yangu kwenye kile chumba
cha wale wapenzi. Nilipokuwa nikikaribia kile chumba mchanganyiko wa harufu kali
za jasho,manukato mazuri ya kike,moshi wa sigara na pombe kali ukapenya puani
mwangu.
Wale watu walikuwa wamezama kwenye mapenzi mazito hivyo nilikuwa na
hakika kuwa hakuna aliyeshtukia uwepo wangu mle ndani. Nilifika kwenye mlango
wa chumba kile na kusimama. Kupitia mwanga hafifu uliyopenya kupitia dirishani
ukitoka kwenye taa za nyumba ya jirani kwa shida niliweza kuyaona maumbo ya
wapenzi wale namna walivyokuwa wakigaragazana pale kitandani na hapo nikasogea
karibu na kuiwasha taa ya mle ndani. Wale wapenzi wakashtuka na kuachiana huku
matusi mazito yakiwaponyoka vinywani mwao.
Tabasamu jepesi likapita usoni mwangu kabla ya kutokemea kusikojulikana na
hapo nikasogeza kile kiti kilichokuwa pembeni ya kitanda na kuketi huku nikayapuuza
macho yao yaliyokuwa yakinitazama kwa mshangao na hasira ya kuingiliwa katikati ya
starehe yao.
“Wewe ni nani na unataka nini humu ndani?” yule mwanaume ambaye hapo awali
nilimtambua kama dalali alifoka huku akifanya jitihada za kuvaa nguo zake. Hata hivyo
yule msichana hakufanya jitihada zozote za kujisitiri badala yake alibaki akinitazama
kwa dharau yenye mshangao.
“Toka nje!” yule mwanaume akafoka huku akikazana kuvaa nguo zake. Mimi
niliendelea kumtazama tu.
“Milla huyu bwege ni nani?” yule mwanaume aliuliza kwa dharau huku akifunga
zipu ya suruali yake kwa pupa.
“Mimi namjulia wapi!” yule msichana alimjibu yule mwanaume huku akiendelea
kunitazama na hapo umbo lake likapeleka ujumbe wa hisia kali za mapenzi moyoni
mwangu. Alikuwa msichana mzuri sana kwa kila idara ambaye mwanaume yeyote
angeweza kumkabidhi kadi yake ATM huku akiogopa kuuliza juu ya mwenendo wa
matumizi ya pesa anazozichukua kila uchwao.
“Nina maswali machache tu ya kuwauliza halafu baada ya hapo nitawaacha
muendelee na starehe yenu” nilivunja ukimya huku nikiyatembeza macho yangu
kuwatazama wale wapenzi.
“Wewe ni nani mpaka utuulize sisi maswali?. Toka nje vinginevyo utaijutia nafsi
yako” yule mwanaume alifoka huku akinijia kwa ghadhabu. Lengo langu lilikuwa ni
kuvuna taarifa zote muhimu ambazo zingenisaidia katika harakati zangu za kipelelezi na siyo rabsha zisizokuwa na mpango. Hivyo haraka niliichomoa bastola yangu
kutoka mafichoni na kuikamata vizuri mkononi. Tukio lile kikapeleka ujumbe kwao
kuwa mimi sikuwa mtu wa kawaida na hapo hofu ikatanda kwenye nyuso zao huku
yule mwanaume akisita kunikaribia.
“Nahitaji kuonana na Gabbi Masebo ama mmiliki wa nyumba hii na nyinyi mkiwa
kama wenyeji naamini mnaweza kunisaidia” niliwaambia wale wapenzi na hapo
nikawaona wakigeuka na kutazamana katika namna ya mshangao dhidi ya swali langu.
“Mmiliki wa nyumba hii ni mimi!” hatimaye yule mwanaume akafoka huku
akijitapa hata hivyo sauti yake ilipwaya kwa hofu.
“Mbona imekuchukuwa muda kinijibu?” nilimuuliza yule mwanaume kwa utulivu
“Unashida gani?” yule mwanaume akaniuliza kwa jazba.
“Wewe ndiye Gabbi Masebo?” nilimuuliza yule mwanaume.
“Gabbi Masebo ndiyo nani wewe bila shaka umechanganyikiwa ukakosea
nyumba” yule mwanaume akafoka huku akiangua kicheko hafifu cha dharau.
Dharau kamwe sikuwahi kuivumilia katika maisha yangu hivyo nilivuta kilimi cha
bastola yangu na risasi moja ikachepuka na kuuvunja mfupa wa bega lake huku risasi
ile ikimtupa chini na hapo akapiga yowe kali la maumivu. Nilitabasamu kidogo huku
nikiwaza kuwa majirani wa eneo lile wangeweza kutafsiri yowe lile kama lililopigwa
na mtu aliyezongwa na jinamizi baya usingizini. Sauti ya ile risasi niliyoifyatua ilikuwa
umemezwa na kiwambo maalum cha kuzuia sauti kilichokuwa kwenye bastola yangu.
Yule msichana kuona vile akaanza kunisihi nimsamehe kana kwamba nilikuwa
nikimdai hata hivyo nilimpuuza huku nikimfuata yule mwanaume pale alipoangukia.
Hata hivyo yule mwanaume alikwisha ishtukia dhamira yangu na pasipo kutarajia
akanyanyuka kwa kasi ya ajabu na kunipiga kumbo lililonipeleka chini bila kupenda.
Halafu yeye akajirusha pale kitandani huku mkono wake ukipotelea chini ya mto
mmoja wa kuegemea. Alipoutoa mkono ule ulikuwa umeshika bastola.
Yule mwanaume wakati alipokuwa akitafuta shabaha nzuri ya kunishindilia risasi
sikutaka kusubiri hivyo nikawahi kulishika pindo la shuka la kile kitanda na kulivuta
kwa kasi. Nguvu za mikono yangu zikawapigisha mwereka pale kitandani huku wote
wakianguka chini na hapo nikaiona pochi ndogo ya kiume ya ngozi pale kitandani
ama Wallet nyeusi. Yule mwanaume akapoteza shabaha na hapo nikasikia sauti kali
ya mfyatuko wa risasi sambamba na kupasuka kwa taa ya mle ndani na hapo nikajua
kuwa ile risasi iliyofyatuliwa na yule mwanaume bila malengo ilikuwa imepoteza
shabaha iliyokusudiwa na badala yake ikapasua taa mle ndani.
Yule msichana akapiga yowe la hofu na kabla sijaituliza vizuri akili yangu
nikashtukizwa na pigo matata la ngumi ya shingo na hapo tusi zito likaniponyoka
huku nikipepesuka na kupoteza mhimili. Mapambano ya ana kwa ana tena gizani
yalikuwa sehemu ya taaluma yangu na ninayoyamudu vizuri. Hivyo pigo la pili
lilipokuja niliinama kidogo likapita bila majibu huku upepo wake mkali ukitengeneza
wimbi masikioni mwangu.
Kabla yule mtu hajatulia vizuri nikainuka na kumtandika teke maridhawa mgongoni na kichwani na hapo nikamsikia yule mtu akipiga yowe kali la maumivu
wakati akijipigiza ukutani. Hata hivyo aliwahi kujirudi na kabla sijamfikia akatupa
ngumi ya nguvu usawa wa kichwa changu. Nikakwepesha kichwa changu kidogo
kuipotezea ngumi yake shabaha kisha nikaudaka mkono wake na kuuzungusha kwa
nguvu na hapo nikasikia sauti ya mvunjiko wa mfupa wa bega lake. Yowe alilopiga bila
shaka liliwaamsha majirani wa eneo lile. Kuona vile yule mwanaume akaanza kufyatua
risasi ovyo mle ndani bila shabaha maalum. Sikutaka kusubiri kwani muda siyo mrefu
nilihisi kuwa risasi zile zingeyavumbua maficho yangu hivyo nikawahi kujirusha chini
ya uvungu wa kile kitanda mle ndani.
Jambo pekee lililonishangaza ni kuwa sikuyasikia tena yale makelele ya hofu ya yule
msichana mle ndani hata hivyo sikujishughulishanaye. Zile risasi ziliendelea kurindima
ovyo mle ndani huku yule mtu akitukana matusi yote ya ulimwengu huu. Rasasi zile
zilipokoma nikasikia vishindo vya hatua za mtu akiyoyoma na hapo nikajua kuwa yule
jamaa alikuwa akinikimbia baada ya kuishiwa risasi kwenye bastola yake. Muda mfupi
uliyofuata nikausikia ule mlango wa nyuma wa ile nyumba ukifunguliwa na kufungwa
kwa pupa huku ile sauti ya vishindo vya hatua ikitokomea. Sikutaka yule mtu anipotee
hivyo nilijiviringisha kutoka kule uvunguni mwa kitanda kisha nikasimama na kuanza
kutimua mbio nikimfukuza yule mtu.
Nilipotoka nje ya lile geti la ile nyumba yule mtu alikuwa ndiyo anatokomea
kwenye kona ya barabara ya ule mtaa huku akikimbia kwa kuchechemea. Bila kusubiri
nikaanza kutimua mbio nikimfukuza yule mtu. Yule mtu alikuwa ameniona hivyo
aliongeza mbio japo kwa kuchechemea chechemea vilevile.
Japokuwa nilijitahidi sana kwendana na kasi yake lakini yule mtu alikuwa hodari
wa mbio zisizoendana kabisa na umbo lake fupi lenye kitambi. Tuliingia barabara ya
mtaa wa pili na tulipokuwa mbioni kuimaliza barabara ile yule mtu akakatisha kwenye
uchochoro hafifu wa kutokea barabara ya mtaa wa tatu. Tulipotokezea kwenye
barabara ya mtaa ule yule mtu nilikuwa nimemkaribia katika umbali wa kuridhisha na
alipogeuka na kuniona nikiwa karibu kumfikia niliweza kuiona hofu iliyokuwa usoni
mwake. Hofu ya kupoteza maisha kabla ya kuzikamilisha starehe za dunia.
Halafu yule mtu akafanya makosa,makosa ambayo yaliushtua hata moyo wangu.
Yule mtu akiwa anakimbia huku anaangalia nyuma akafika kwenye makutano ya
barabara nyingine. Ghafla wakati yule mtu akifika kwenye eneo lile la makutano ya
barabara nikaliona gari dogo aina ya Subaru likikatisha kwa kasi mbele yake. Dereva wa
gari lile akajitahidi kumkwepa yule mtu katika kila namna lakini jitihada zake hazikufua
dafu kwani muda uleule nikasikia sauti ya kishindo cha aina yake huku yule mtu
akitupwa hewani. Nilisimama kwa taharuki nikishuhudia tukio lile. Yule mtu alipotua
chini magurudumu ya lile gari yakapanda kifuni mwake na picha ile haikunishawishi
kuitazama. Ile Subaru ikapoteza uelekeo ikiyumbayumba na hatimaye ikaingia kwenye
mtaro uliyojengewa kando ya barabara ile. Dereva wa lile gari kuona vile akafungua
mlango na kutoka akitimua mbio kuelekea kichochoroni.
Hakukuwa na dalili zozote za uhai kwa yule mtu wakati nilipomfikia na kumchunguza. Pasipo kupoteza muda nikainama na kuanza kumpekua kwenye
nguo zake. Nilichokitaka sikukipata kwani mifukoni mwake nilikuta pakiti mbili za
kondomu za kiume,sigara tatu na kiberiti cha gesi. Ama kwa hakika Mungu asingeweza
kumpokea mtu wa namna ile kwenye himaya yake.
Baadhi ya watu walikwishaanza kukusanyika eneo lile hivyo sikutaka kuwa kivutio
badala yake nikawahi kujichanganya miongoni mwao na kutoweka eneo lile.
Nilirudi haraka kwenye ile nyumba huku tumaini langu pekee likibaki kwa yule
msichana niliyemuacha mle ndani. Nilifika na kuingia kwenye kile chumba kulipotokea
zile purukushani na wakati huu hofu ya kushindwa iliniingia kwani yule msichana
hakuwepo wala ile wallet ndogo nyeusi iliyokuwa pale juu ya kitanda. Baridi yabisi
ikautafuna mtima wangu.
_____
TAA ZA MAKUTANO YA BARABARA ya Morogoro eneo la Ubungo
ziliponiruhusu kuendelea na safari nilikishusha kidogo kioo cha dirisha kisha
nikayakung’uta majivu ya sigara kwa nje huku nikiyapuuza matusi ya madereva
waliokuwa nyuma yangu wakinitaka niharakishe kuendesha gari. Hatimaye
nikakanyaga pedeli ya mafuta na kuendelea na safari nikiyavuka makutano yale na
kuelekea eneo la Mbezi kwa Msuguli nilipokuwa nikiishi.
Kila nilipoukumbuka ule mkasa uliotokea muda mfupi uliyopita kwenye ile
nyumba ya Gabbi Masebo. Homa ya kushindwa iliisimanga nafsi yangu lakini
sikushindwa kabisa la hasha! kwani bado nilikuwa na chanzo muhimu cha kuendelea
na upelelezi wangu. Mazingira ya kuendelea na upelelezi huo yalikuwa wazi kabisa na
yanayoniruhusu kupiga hatua ya mbele zaidi. Sikuwa na shaka kabisa kuwa mtu yule
aliyekufa kwa ajali ya gari niliyekuwa nikimfahamu kama dalali wa nyumba ya Gabbi
Masebo hakuwa dalali kwani alikuwa mahiri wa kujihami na anayeijua vizuri bastola
na matumizi yake kama alivyokuwa stadi wa kutumia kondomu kwenye matendo
yake ya kizinzi. Kitu fulani kilikuwa kikiendelea katika mkasa ule,nilijiambia.
Usiku huu hakukuwa na foleni ya magari hivyo sikutumia muda mwingi hadi
kufika nyumbani kwangu. Nilipofika eneo la Mbezi kwa Msuguli nikaiacha barabara
ya Morogoro na kuingia barabara hafifu ya vumbi inayochepuka upande wa kulia
ikikatisha katikati ya mtaa wenye nyumba za watu wenye vipato vya kueleweka.
Zilikuwa nyumba za kisasa zenye sistimu maalum za umeme wa kuzuia wezi na wakati
nikizipita nyumba zile niliweza kuzisikia kelele za mbwa wenye hasira waliokuwa
wakibweka ndani ya kuta zilizozizunguka nyumba zile.
Nilipomaliza kuivuka barabara ile nikapandisha kilima kidogo ambapo juu yake
nilikutana na barabara nyingine iliyokatisha mbele yangu.
Nilipofika kwenye makutano ya barabara ile nikachepuka kuifuata barabara
ielekeayo upande wa kulia halafu mbele kidogo nikaingia upande wa kushoto na
hapo nikasimama mbele ya geti jeusi la ukuta mrefu unaoizunguka nyumba yangu ya
ghorofa mbili yenye bustani kubwa ya maua ya kupendeza na bwawa moja la kuogelea.Nilishuka kwenye gari na kwenda kufungua geti lile kisha nikarudi kwenye gari
na kuingia mle ndani. Nilipolifunga lile geti niliitazama kwa muda nyumba yangu ya
kifahari na wakati huu nikaiona kama pango la upweke. Labda ningekuwa na mke
na mtoto hali ingekuwa tofauti lakini kazi yangu ilihitaji mwanamke mwenye uelewa
mkubwa na harakati zangu. Kuwa mbali na nyumbani wakati mwingne kwa kipindi
kirefu kisichojulikana mwisho wake halafu pale unaporudi nyumbani unakuwa na
makovu ya risasi ni jambo linalohitaji moyo.
Hatimaye nilifungua mlango na kuingia mle ndani huku nikiwa nimechoka mwili
na akili. Sebule yangu ya kifahari yenye ushawishi mkubwa kwa ma-star wa filamu
za kibongo ilinikaribisha vizuri na kwa utulivu. Nikawasha taa za nje na kupanda
ghorofa ya juu kilipokuwa chumba changu cha kulala. Kwa muda ule sikupenda
kujishughulisha na kitu chochote zaidi ya kupumzika.
Kabla ya kwenda kuoga nilijaribu kuchunguza kama kulikuwa na ugeni wowote
usio rasmi uliofika kunitembelea pale nyumbani wakati nilipokuwa kwenye mizunguko
yangu kupitia Closed-Circuit Television (CCTV) katika screen ndogo inayoonesha
picha zote zilizonaswa kupitia kamera za usalama zilizopandwa kwenye kona zote
kuizunguka nyumba yangu.
Hakukuwa na ugeni wowote kwani picha zote nilizoziona zilikuwa za kawaida tu.
Kulikuwa na watoto wadogo waliokuwa wakicheza mbele ya geti muda mfupi baada
ya mimi kuondoka asubuhi ile. Pia niliwaona wapenzi wawili wakiwa wamesimama
sehemu ya nyuma nje ya ukuta wa nyumba. Watu wengine waliosalia walikuwa wapita
njia wakiendelea na hamsini zao. Mwishowe nikajiona mimi mwenyewe muda mfupi
uliopita wakati nilipokuwa nikiingi nyumbani.
Nikiwa nimeridhishwa na mwenendo wa picha zote zilizonaswa na kamera
za kiusalama zilizopandwa kuizunguka nyumba yangu nilivua nguo zangu kisha
nikajifunga taulo na kuelekea bafuni kujimwagia maji. Muda mfupi baadaye nilirudi
mle chumbani nikavaa nguo zangu za kulalia na kujitupa kitandani. Muda mfupi
uliyofuata usingizi ukanichukua na kunitupia sayari nyingine.
_____
FREDY BAGUNDA ALITULIA huku tabasamu hafifu likijipenyeza taratibu
usoni mwake hali iliyompelekea kazipangusa taratibu kingo za mdomo wake kwa
ulimi. Mtandao ulikuwa umenasa vizuri kwenye kompyuta yake baada ya kitambo
kirefu cha kusubiri. Saa ya ukutani ilionesha kuwa ilikwisha timia saa mbili asubuhi
na jiji la Dar es Salaam kama ilivyo kawaida yake lilikwisha kuchukua sura mpya ya
pilikapilika za kila siku za wakazi wake. Pamoja na joto lililoanza kijihimarisha lakini
kiyoyozi ndani ya ofisi ile iliyopo ghorofa ya tano mtaa wa Patrice Lumumba kilijitahidi
kikamilifu kupambana na joto lile.
Baada kitambo kingine kifupi cha kusubiri akaunti yake ya ujumbe kwa njia
ya eletroniki ama electronic-mail ikafunguka na ndani yake kulikuwa mails kadhaa
zilizoingia. Miongoni mwa mails hizo zilikuwepo mails za kutoka pembe tatu tofauti za dunia. Moja ilitoka Karachi nchini Pakistani nyingine ilitoka Hong Kong na ya
mwisho ilitoka Johannersburg nchini Afrika ya kusini. E-mail zile tatu za mwisho
ndiyo alizokuwa akizisuburi kwa hamu hivyo akaanza kuzifungua moja baada ya
nyingine akizisoma huku akianza na ile ya kutoka nchini Afrika ya kusini kwa mtu
aliyejulikana kwa jina la Lola Ndaba.
Mara simu yake iliyokuwa juu ya meza pembeni ya kompyuta ikaanza kuita. Tukio
lile likampelekea aichukue ile simu kwa pupa huku akiitazama namba ya mpigaji.
Kuliona jina la mtu anayempigia kukampelekea abofye kitufe cha kupokelea na
kuiweka simu sikioni. Sauti ya upande wa pili iliposikika Fred Bagunda akataharuki.
“What…?”
“Nani aliyekwambia?...hebu njoo ofisini sasa hivi!”
Simu ilipokatwa upande wa pili Fred Bagunda akabaki ameishikilia kama
anayetafakari jambo huku macho yake yakitazama mlango wa ofisi lakini akili yake
ikiwa mbali. Hatimaye akaupeleka mkono kujikuna kidevu chake katika namna ya
tafakari nzito iliyoufanya ubongo wake usitishe shughuli zake kwa sekunde kadhaa.
Kisha akauachia mwili wake mkubwa ujiegemeze vizuri kwenye kiti chake cha ofisini
alichokikalia chenye foronya laini.
Muda mfupi baadaye yule mtu aliyekuwa akiongeanaye kwenye simu alikuwa
amesimama nje ya mlango wa ofisi ile huku mkono wake mmoja ukigonga mlango wa
ofisi kwa utulivu. Fred Bagunda akiwa ameridhika kupitia picha aliyonaswa na kamera
za usalama kuwa mtu aliyesimama nje ya mlango alikuwa sahihi akabonyeza kitufe
fulani ukutani na hapo ule mlango ukafunguka na kumruhusu yule mtu kuingia ndani.
Kijana wa makamo mwenye umri wa kati ya miaka ishirini na nane na thelathini
na mbili,mrefu na mwenye mwili uliojengeka vizuri katika mwonekano wa suti yake
nadhifu nyeusi,shati la kijivu na tai ya rangi damu ya mzee akaingia. Huku sura yake
nzuri inayoweza kutia nanga kwenye moyo wa msichana yeyote mrembo ikishindwa
kuonesha tashwishwi yoyote.
“Pole na kazi” yule kijana akamsalimia Fred Bagunda huku akiyatembeza macho
yake mle ndani.
“Ahsante!,karibu uketi Njama”
Njama akavuta kiti na kuketi kwa utulivu huku akiipeleleza sura ya Fred Bagunda
na alichokiona ni taharuki. Kwa kipindi kirefu walichofanya kazi pamoja katika ofisi
hii inayoshughulika na usafirishaji wa vifurushi vya kimataifa ama International Parcels
Njama hakuwahi kumuona Fred Bagunda katika hali ile lakini kwa taarifa alizompa
alishahili.
“Niambie kuhusu Alba Gaumo nahisi hatukuelewana vizuri kwenye simu” Fred
Bagunda akavunja ukimya tena huku akimtazama Njama kwa wasiwasi.
“Hakuna mabadiliko yoyote Alba Gaumo amekufa ni kama nilivyokwambia”
“Nini kimetokea?,tulikuwa wote usiku wa jana hadi saa tatu hapa ofisini”
“Kifo chake kimetokea kati ya saa tano hadi saa saba usiku”
Fred Bagunda akayakaza macho yake akisikiliza kwa makini maelezo ya Njama kisha akashusha pumzi nyingi kwa mkupuo huku akisikitika kisha akauliza tena
“Amekufaje?”
“Amegongwa na gari dogo aina ya Subaru na dereva wa gari hilo ametokomea
kusikojulikana”
“Umezipata wapi taarifa hizo?”
“Mtu mmoja aliyejitambulisha kama msamaria mwema alinipigia simu muda
mfupi baada ya ajali hiyo” Njama aliongea kwa utulivu huku akionekana kuzama
kwenye fikra fulani.
“Huyo mtu alizifahamu vipi namba zako za simu?” Fred Bagunda akauliza huku
akizama kwenye tafakari.
“Kwa mujibu wa maelezo yake ni kuwa aliiokota simu ya Alba Gaumo eneo la
ajali na katika kutaka kusaidia kutoa taarifa kwa watu wa karibu wa Alba Gaumo ndiyo
akabahatika kuiona namba yangu”
“Alikuwa akifanya nini eneo hilo?”
“Kwa kweli bado sina hakika labda alikuwa akifanya biashara,hakuna anayejua”
Njama akaongea huku akiviminyaminya vidole vyake mkononi.
“Ajali hiyo imetokea wapi?” Fred Bagunda akauliza huku akisikiliza kwa makini.
“Eneo la Sinza barabara ya mtaa wa tatu kutoka kwenye ile nyumba”
“Kwa hiyo alikuwa kwenye ile nyumba?”
“Nahisi hivyo bila shaka!”
“Okay! na vipi kuhusu huyo msamaria mwema aliyekupigia simu?”
“Hana hatia na haelekei kuwekwa katika mtazamo tofauti. Alikuwa akitoka kwenye
shughuli zake wakati alipojikuta yupo miongoni mwa mashuhuda wa ajali hiyo”
“Umeichukua simu ya Alba Gaumo toka kwa huyo msamari mwema?”
“Ndiyo!”
“Umefanya vizuri Njama sipendi polisi wajiingize kwenye suala hili”
Wakati Fred Bagunda akimaliza kuongea Njama akaitoa simu ya Alba Gaumo
kutoka kwenye koti lake la suti na kuiweka pale mezani.
“Una hisia zozote tofauti juu ya hili?” Fred Bagunda akauliza kwa utulivu kama
aliye elemewa na mzigo wa mawazo kichwani.
“Nahisi jambo” Njama akaongea kwa utulivu huku akimtazama Fred Bagunda.
“Jambo gani?” Fred Bagunda akauliza huku akimkata jicho Njama.
“Nimepata taarifa fulani kutoka kwa huyu msamaria mwema aliyenipiga simu
kunieleza juu ya kifo cha Alba Gaumo na sidhani kama tarifa hizi ni za kuzipuuza”
Njama akaongea huku akionekana kufikiria jambo fulani. Maelezo yake yakapeleka
mshangao mwingine kwa Fred Bagunda.
“Taarifa gani?”
“Inavyosemekana ni kuwa Alba Gaumo alikuwa akikimbia wakati alipogongwa
na gari” maelezo yale yakampelekea Fred Bagunda amtazame Njama kama ambaye
anaiona picha tofauti mbele yake.
“Alikuwa akikimbia nini?”
“Hapa ndiyo swali linapokuja” Njama akaongea kwa utulivu.
“Una hakika kuwa huyo msamaria mwema alimuona Alba Gaumo akikimbia?”
“Binafsi sioni kama yule mtu alikuwa na sababu ya kunidanganya”
“Halafu…!”
“Baada ya Alba Gaumo kugongwa na hilo gari yule msamaria mwema aliendelea
kunieleza kuwa alimuona mtu fulani akimfuata Alba Gaumo pale alipoangukia na
kisha kuanza kumpekua mifukoni. Lakini hili haliwezi kunipa mashaka sana maana ni
kawaida iliyozoeleka kwa wahanga wa ajali kupekuliwa pale ajali inapotokea”
Maelezo ya Njama yakazidi kumchanganya Fred Bagunda kiasi cha kumfanya
atulie huku macho ameyatumbua kwa mshangao kama aliyesikia au kuona tukio la
kustaajabisha sana. Kisha akaegemeza viwiko vyake juu ya meza akimtazama Njama
kwa udadisi halafu akavunja ukimya.
“Nenda kwenye ile nyumba ukajaribu kuchunguza kama kuna kitu chochote
kinachoweza kuwavuta polisi katika kufanya uchunguzi wao. Alba Gaumo ni mtu
rahisi kufahamika” Fred Bagunda akaongea huku amezama kwenye tafakari nzito.
“Wakati nilipokuwa nakupigia simu nilikuwa natoka kwenye ile nyumba. Hata
hivyo sidhani kama polisi wanaweza kujihangaisha katika kutaka kufahamu Alba
Gaumo ni nani. Vingenevyo watataka kufuatilia na kufuhamu mmiliki wa lile gari
lililomgonga Alba Gaumo kwa sababu kuna mwanya mzuri wa kupata pesa kutoka
kwake”
Fred Bagunda akatabasamu kidogo huku akimtazama Njama kwa utulivu baada
ya kufurahishwa na umakini wake katika kufikiri.
“Umefanya vizuri sana Njama sitaki polisi wapate mwanya wa kutufikia” Fred
Bagunda akaongea huku akitabasamu kisha akachukua sigara kutoka kwenye mfuko
wa shati lake na kuitia mdomoni. Alipoiwasha akaivuta mara kadhaa na kuupuliza
moshi wa sigara hiyo mbele yake huku akiutazama kwa makini kama mdunguaji
kwenye darubini ya kunasia taswira ya windo lake.
“Okay! niambie Njama what have you got from the house?”
“Hakuna cha maana lakini…!”
“Lakini?”
“Ni kuhusu hali ilivyokuwa ndani ya ile nyumba!”
Maelezo ya Njama yaliyoishia njiani yakampelekea Fred Bagunda amtazame
Njama kwa udadisi huku akijaribu kuzipima vizuri hisia zake kisha akayakung’uta
majivu ya sigara kwenye kibeseni maalum cha majivu ya sigara kilichokuwa pale
mezani huku akikohoa kidogo kabla ya kuuliza.
“Niambie kuna hali gani?”
“Inavyoonekana kulitokea purukushani fulani kwenye ile nyumba. Purukushani
ambayo huwenda nikaihusisha na huyo mtu aliyeonekana kumpekua Alba Gaumo
baada ya ajali kutokea”
Ukimya ukachukua nafasi yake mle ndani huku Fred Bagunda akiiweka na
kuitelekeza sigara yake iteketee yenyewe taratibu kwenye kile kibeseni cha majivu pale mezani. Halafu akaketi vizuri na kuanza kuviminyaminya vidole vyake huku
akionekana kuvutiwa na sauti uliyotokana na zoezi lile.
“Nini ulichokiona kwenye ile nyumba?” akauliza tena.
“Huwenda kulitokea varangati la aina yake mle ndani kwani vitu vilikuwa
vimetawanyika ovyo sakafuni vilevile kulikuwa na maganda kadhaa ya risasi”
Fred Bagunda aliyasikiliza kwa makini maelezo ya Njama na mara hii kitu fulani
kilianza kujengeka kichwanini mwake.
“Naanza kupata wasiwasi kuwa huwenda kuna uchunguzi wa kimyakimya
unaofanyika juu yetu”
“Ni mapema sana kusema hivyo ingawa hatupaswi kupuuza” Njama akaongea
kwa utulivu.
“Tangu sasa tunatakiwa kuwa makini na kama kutajitokeza jambo jingine jipya
na tofauti nitatoa taarifa kwa wakubwa” Fred Bagunda akaongea huku akiyafikicha
macho yake.
“Hata mimi naafikiana na suala hilo”
“Umejaribu kuchunguza namba mpya za simu zilizoingia na kutoka kwenye simu
ya Alba Gaumo?”
“Imekuwa ni vigumu kuweza kuziona calls na missed calls kwenye simu yake kwani
kutokana na maelezo ya msamaria mwema ni kuwa aliiokota simu ya Alba Gaumo
ikiwa imechanguka”
“Ondoa shaka bado tuna njia nyingine ya kufahamu hilo. Nenda kwenye ofisi
yoyote ya mtandao wa simu aliokuwa akiutumia Alba Gaumo uwaombe wakuangalizie
halafu baada ya hapo tutajua wapi pa kuanzia”
Maelezo ya Fred Bagunda yakampelekea Njama asogeze kiti chake nyuma na
kusimama kisha akaagana Fred Bagunda na kuanza kuufuata uelekeo wa ule mlango
wa ile ofisi. Muda mfupi baadaye alikuwa mbali na ofisi ile.
_____
KAMA NINGEKUWA NIMEAJIRIWA basi sikuwa na shaka kuwa ofisini
ningemkuta bosi wangu akiwa amenuna na amevimba nusu ya kupasuka kwa hasira
kwani wakati huu ningekuwa nimechelewa sana ofisini. Lakini hilo kamwe haliwezi
kutokea kwani ofisi ilikuwa yangu huku mimi nikiwa ndiye bosi mwandamizi na hivyo
hakuna mtu yoyote wa kuniuliza. Kwa mara ya kwanza nikajikuta nikifurahia matunda
ya kujiajiri.
Saa yangu ya mkononi ilionesha kuwa ilikwishatimia saa nne na robo asubuhi
wakati nilipokuwa nikitafuta maegesho ya gari langu chini ya jengo lile la ghorofa
lenye ofisi yangu eneo la Kisutu. Nilikuwa na bahati kwani eneo lile la maegesho
lilikuwa limefurika magari lakini nilipolikaribia mara nikaliona gari moja likitoka
kwenye maegesho yale. Lilikuwa gari la wakili mmoja maarufu wa kujitegemea ofisi
yake ikitazama na yangu kule juu ya lile jengo la ghorofa.
Wakati nikipishana na wakili yule akanisalimia kwa kunipungia mkono nami nikafanya vivyo hivyo huku nikiendesha gari langu hadi kwenye yale maegesho
yaliyoachwa wazi na gari la yule wakili. Kisha nikashuka na kuelekea sehemu ilipokuwa
lifti ya jengo lile nikielekea juu ghorofani ilipokuwa ofisi yangu.
Muda mfupi baadaye nilifika kule juu na lifti iliposimama nikatoka na kuingia
kwenye korido pana yenye vyumba vya ofisi vinavyotazamana. Wakati nikitembea
kuelekea kwenye ofisi yangu nikapishana na kusalimiana na baadhi ya wafanyakazi
waliokuwa na ofisi zao kwenye jengo lile huku wengi wao wakionekana kuwa na
haraka.
Nilimkuta Mwasu tayari keshafika ofisini akimalizia kufanya usafi kwenye ofisi
yangu na hapo tukasalimiana huku Mwasu akionekana mwingi wa furaha
“Habari za asubuhi Mwasu!”
“Oh! salama tu sijui na wewe umeamkaje” Mwasu aliniitikia huku akitabasamu
“Kama unavyoniona bukheri wa afya” nilimuitikia huku nikiachia kicheko hafifu
na hapo akaniuliza.
“Vipi jana ulifanikiwa chochote?”
“Kwa kweli bado ila ni matumaini yangu kuwa huwenda siku ya leo ikawa tofauti
na siku ya jana”
“Okay! karibu sana,vipi nikutengenezee chai?” Mwasu akaniuliza na kweli alikuwa
akinijali mno kiasi cha kunifanya niumie sana pale anapokuwa mbali na mimi.
“Hakuna haja ya kusumbuka kwa sasa wewe malizia kwanza kazi zako halafu
baadaye utaniletea kikombe cha kahawa ofisini” nikamwambia huku nikielekea ofisini
kwangu. Mwasu akabaki amesimama akinisindikiza kwa macho nyuma yangu hadi
pale nilipopotea kwenye usawa wa macho yake ndiyo akageuka na kuendelea na kazi
zake.
Niliingia ofisini kwangu nikiwa na ari mpya ya kazi na baada ya kuweka vitu
vyangu sawa mle ofisini nikaketi na kuanza kuandika ripoti fupi ya kazi niliyoifanya
jana usiku. Ambapo baadaye ningemkabidhi Mwasu ili awaze kuiandaa vizuri katika
mtiririko sahihi ambao ungewekwa katika lile faili la MIFUPA 206.
Nilipokuwa mbioni kumaliza kazi ile nikasikia kelele za kitasa kikizungushwa
kisha Mwasu akaingia huku akiwa amebeba sinia lenye chupa moja ya kahawa na
vikorombwezo vingine vya kifungua kinywa. Alipoingia mle ndani akaliweka lile
sinia mezani na kunikaribisha huku yeye akirudi ofisini kwake. Nilimshukuru huku
nikimalizia kazi yangu kisha nikaanza kufungua kinywa.
Tofauti na siku ya jana hali ya hewa ya jiji la Dar es Salaam ilikuwa imetawaliwa
kwa kiasi kikubwa na mvua kubwa na kuifanya ile hali ya hewa ya joto kali iliyozoeleka
kupungua. Kupitia dirisha la ofisi yangu niliweza kuwaona baadhi ya watembea kwa
miguu wakiwa na miamvuli kujikinga na mvua ile na barabara nyingi za mitaa ya jiji la
Dar es Salaam zilikuwa zimekaukiwa na watu.
Nilimaliza kufungua kinywa kisha kwa simu ya mezani iliyokuwa mle ndani ofisini
nikampigia mzee James Risasi nikitaka kumueleza juu ya maendeleo ya upelelezi
wangu. Baada ya miito kadhaa ya simu hatimaye simu yake ikapokelewa huku akinieleza kuwa alikuwa kwenye foleni barabarani kwenye gari lake akielekea kazini.
Hata hivyo alikuwa tayari kunisikiliza hivyo nikaanza kumueleza mambo yote yaliyojili
katika upelelezi wangu huku nikimuahidi kuwa baada ya kazi kukamilika majibu yangu
yangeambatana na ripoti maalum.
Nilimkabidhi Mwasu ule muendelezo wa ripoti yangu ili aendelee kuiandaa na
kuiweka mle kwenye lile faili la MIFUPA 206 halafu nikarudi ofisini kwangu na
kumsikiliza mteja mmoja aliyefika muda ule. Yule mteja alipoondoka nikaendelea na
shughuli nyingine za kiofisi.
Mchana ulipofika nilitoka ofisini kwangu nikamuaga Mwasu na kuhamishia
harakati zangu mitaani.
_____
OFISI YA ULE MTANDAO WA SIMU uliyokuwa ukitumika na simu ya Alba
Gaumo ilikuwa kwenye kona ya barabara ya mtaa wa Uhuru kutokea eneo la Kariakoo
ikitazamana na duka kubwa la samani na vyombo vya nyumbani. Njama alikuwa
akiifahamu vizuri ofisi ile kwani mara kwa mara alikuwa akifika kupata huduma za
simu za kifedha na zile za kimtandao. Kwa kufanya hivyo akawa amejenga urafiki na
wasichana mrembo mhudumu wa ofisi ile aitwaye Farida.
Wakati Njama akiingia kwenye ofisi ile Farida alikuwa akimaliza kumuhudumia
mteja mwingine hivyo mara alipomuona Njama akiingia mle ndani akampokea kwa
bashasha zote.
“Karibu mpenzi” Farida akamkaribisha Njama huku akiumba tabasamu usoni.
“Ahsante mrembo!” Njama akaitikia huku akiyatembeza macho yake kuzitazama
sura za watu waliokuwa mle ndani. Kisha akapiga hatua zake kwa utulivu kuelekea
lilipo dawati la wateja huku tabasamu lake likiyatongoza macho ya Farida. Alipofika
kwenye lile dawati la wateja akaegemeza mikono yake juu ya meza huku akivigongesha
vidole vyake vya mkononi taratibu juu ya meza ile.
“Kila nikuonapo Farida moyo wangu unaenda mbio utadhani nimekopa benki na
tarehe ya marejesho imefika”
“Mh! maneno yako nishayazoea Njama. Kama kweli ungekuwa na haja na mimi
si ungenitafuta” Farida akaongea kwa utulivu huku usoni akiliachia tabasamu lake bila
kificho.
“Basi niseme kuwa kazi zimenibana mpenzi lakini vinginevyo”
“Mh! we sema tu umenitupa baada ya kupata kimwana mwingine” Farida
akalalama huku akionekana kukata tamaa na maneno ya Njama. Farida bado alikuwa
na kumbukumbu za starehe za kukata na shoka walizozifanya na Njama tangu
walipoanza mahusiano ya kimapenzi yasiyo rasmi mwaka mmoja uliyopita.
“Haya niambie” Farida akavunja ukimya tena huku akimtazama Njama kwa hisia
za kimapenzi.
“Nina shida mpenzi”
“Shida gani?” Farida akauliza huku akimkazia Njama macho ya udadisi na hapo Njama akachukuwa kalamu iliyokuwa juu ya lile dawati la wateja na kuandika namba
ya simu ya Alba Gaumo kwenye karatasi ndogo iliyokuwa pale juu ya lile dawati la
wateja.
“Nahitaji kujua majina na namba za wahusika waliopiga na kupigiwa na namba hii
kwa muda wa wiki mbili zilizopita” Njama akaongea kwa utulivu huku akiwa tayari
kukabiliana na upinzani wowote kutoka kwa Farida. Farida akaitazama ile namba ya
simu kwenye ile karatasi kabla ya kuyahamishia macho yake kwa Njama.
“Kuna shida gani?” hatimaye Farida akauliza kwa mshangao.
“Kuna mtu anataka kumtapeli rafiki yangu hivyo tunajaribu kuchunguza ili tuandae
mtego mzuri wa kumnasa” Njama akadanyanga huku akiliachia tabasamu lake jepesi.
“Sasa kwanini huyo rafiki yako asije mwenyewe?”
“Yupo mbali kidogo kwa wakati huu”
Jibu la Njama likamfanya Farida aweke kituo kidogo akifikiri jambo fulani kisha
akavunja ukimya.
“Hii ni kinyume na taratibu zetu za kazi mpenzi istoshe bosi wetu leo yupo ofisini”
Njama akayatembeza tena macho yake mle ndani hadi ilipokuwa ofisi ya bosi wa
Farida upande wa kushoto wa ofisi ile na hapo akamuona mwanamke mrefu aliyevaa
suti nadhifu nyeusi akiwa amainamia kompyuta yake ndani ya chumba kidogo cha
wastani kilichozungukwa na kuta nne za vioo visafi vinavyoonesha ndani. Alikuwa
bosi wa Farida kwani mara nyingi Njama alipokuwa akifika katika ofisi ile alikuwa
akimuona mwanamke yule asiyependa masihara wakati wa kazi.
“Kwa hiyo huwezi kabisa kunisaidia mpenzi?” Njama akaongea kwa sauti tulivu
ya lawama.
“Anyway ngoja nijaribu lakini nikishindwa usinilaumu” Farida akaongea huku
akiichukua ile karatasi na kupoteanayo sehemu ya nyuma ya ofisi ile kwenye uficho
mdogo na wakati akiondoka Njama akapata wasaha mzuri wa kulichunguza umbo
lake namba nane lenye mzigo mkubwa wa makalio yaliyokuwa yakitikisika kwa zamu.
Mruzi mwepesi ukamponyoka mdomoni pasipo kuwatilia maani wateja wengine
walioingia mle ndani.
Farida alipopotea kwenye macho yake Njama akageuka upande mwingine wa ile
ofisi sehemu walipokuwa wafanyakazi wengine wa ile ofisi wakiwahudumia wateja.
Hata hivyo wale wafanyakazi walikuwa wamezamana katika hamsini zao.
Muda mfupi baadaye Farida alirudi akiwa na karatasi moja mkononi huku usoni
akionesha matumaini.
“Umekawia kidogo nikajua bosi wako kakufuma!” Njama akaongea huku
akichombeza utani.
“Ah! wapi ni mtandao tu ulikuwa unasumbua” Farida akaongea huku akimkabidhi
Njama ile karatasi.
“Vipi umefanikiwa?” Njama akauliza pasipo kuitazama ile karatasi.
“Kila kitu kiko sawa nendeni mkamtafuteni huyo tapeli wenu” Farida akaongea
kwa hakika. Njama akaipokea ile karatasi na kuipitishia macho haraka. Ilikuwa ni karatasi iliyoonesha miamala ya fedha iliyofanyika kwenye simu ya Alba Gaumo
pamoja na muda wa simu alizopigiwa na kupiga. Njama akatoa noti mbili za elfu kumi
kutoka mfukoni na kumpa Farida.
“Enjoy your lunch honey” akaongea hukua akiitia mfukoni ile karatasi
“Ahsante my dear” Farida akazipokea zile noti na kushukuru huku haraka
akiyatembeza macho yake mle ofisini kutazama kama kuna mtu yeyote aliyekuwa
akimtazama.
“Mimi naenda!” Njama akaongea huku akiipuuza hofu ya Farida.
“Lini nitakuona tena mpenzi?”
“Nitakupigia simu wala usijali”
“Haya karibu tena!”
“Ahsante! kazi njema” Njama akaaga kisha akaanza kutembea taratibu akielekea
kwenye mlango wa kutokea wa ofisi ile huku nyuma yake akimuacha Farida
akimhudumia mteja mwingine. Alipoufikia ule mlango akaufungua na kutoka. Muda
mfupi uliyofuata Njama alikuwa akitafuta maegesho ya gari lake kwenye eneo la Mnazi
mmoja Park kisha akaichukua simu yake na kumpigia Fred Bagunda. Baada ya miito
michache ile simu ikapokelewa upande wa pili
“Ndiyo Njama…!” sauti ya Fred Bagunda upande wa pili ikauliza
“Nimefanikiwa” Njama akazungumza kwa utulivu.
“Hebu niambie…!”
“Mawasiliano mengi yaliyofanywa na simu ya Alba Gaumo ndani ya muda wa
wiki mbili za mwisho yalikuwa yakiwahusisha watu wetu. Lakini kama kawaida
kuna namba mpya zilizoingia na kutoka na nimejaribu kuzichunguza namba hizo
nikagundua kuwa zote ni za wanawake”
“Safi sana!”
“Sasa tunafanyaje?”
“Watafute hao wanawake mmoja baada ya mwingine bila shaka huwenda tukapata
hakika ya wasiwasi wetu”
“Sawa!”
“Sasa hivi upo wapi?”
“Mnazi mmoja Park”
“Ukimaliza nataka uende nyumbani kwa Alba Gaumo ukaweke mambo sawa”
“Ondoa shaka”
Sauti ya Fred Bagunda ilipotoweka hewani Njama akakata simu na kuitia mfukoni
kisha akawasha gari na kuingia tena barabarani. Mvua ilikuwa imeanza tena kunyesha.
ITAENDELEA
 
Kama nilivyoahidi hapo jana kuwa mwandishi wetu wa riwaya ya mtutu wa bunduki ameniomba niwajulishe kuwa adithi yetu itaendelea kuanzia ijumaa ijayo. Hii inatokana na kutingwa na majukumu mengine katika ujenzi wa taifa. Lakini pamoja na hayo amenipa jukumu la kuwaletea riwaya yake ya MIFUPA 206. Nawaomba muwasiliane na mtunzi kwa namba
0688058669 kwa ajiri ya kupata nakala za vitabu vifuatavyo
1.Tai kwenye mzoga (hiki nacho nitakileta humu mpaka nitakavyoelekezwa tofauti na mtunzi)
2.Msitu wa madagascar
3.Mifupa 206
Nawaomba tuthamini kazi za watunzi wetu kwa kuwaunga mkono kwa kununua kazi zao ili wafaidi matunda ya vipaji vyao. Twende kazi.......
Mods naomba mnisaidia kuexpand hiyo attachment ambayo ni cover ya kitabu
Hii riwaya ya mifupa unaleta halafu baadae unasitisha ama ? Naona kama umeileta sokoni
 
Naona mkuu upo active leo hongera sana kwa kazi zako nzuri stay blessed (tutegemee leo mkuu)
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom