25phiri12
Senior Member
- Jun 19, 2021
- 120
- 92
RIWAYA: MATEKA
MTUNZI: EMMANUEL PHIRI
NAMBA: 0758 195 890
(KIPANDE CHA KWANZA)
UTANGULIZI
Licha ya baridi kuwa kali kwa sababu ya mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha, lakini bi Nadia Ali Rayan aliendelea kutokwa na jasho huku moyo wake ukimwenda mbio kama mtu aliyekimbia mashindano ya mbio ndefu. Hakuwa tayari kushuhudia mtoto wake akiangukia mikononi mwa vyombo vya usalama au magenge ya kihalifu. Mtoto wake alikuwa akisakwa usiku na mchana na vyombo vya usalama ili ashitakiwe na kuhukumiwa kwa makosa ya jinai aliyokuwa akiyafanya, vile vile alikuwa akisakwa na magenge ya kihalifu ili yamteketeze kwa usaliti na mauaji aliyokuwa akiyafanya dhidi yao. Bi Nadia Ali Rayan alikuwa tayari hata kuua kila atakayemsogelea mwanae kwa lengo la kumkamata au kumdhuru.
Japokuwa mwanae alikuwa mhalifu na alilitambua hilo lakini hakuhalalisha kifo chake. Aliamini mwanae hakuzaliwa kuwa mhalifu bali dunia ndiyo iliyoamua awe hivyo. Aliamini mwanae alikuwa akilipiza kisasi cha maisha ya nyuma aliyoyaona au kusimuliwa kuhusu familia yake. Kumbukumbu za bi Nadia Ali Rayan zilisafiri miaka mingi iliyopita, akakumbuka kifo cha mume wake kilichosababisha atengeneze taswira mpya ya maisha yake, ilikuwa kumbukumbu mbaya sana ambayo kila anapoikumbuka huhisi kumwaga damu za maadui zake. Ni heri mume wake angeugua akamuuguza mpaka akafariki kuliko kilichotokea. Mume wake aliuliwa mchana kweupe. Bi Nadia Ali Rayan aliamini kwa asilimia mia moja kuwa magenge ya wauza madawa ya kulevya yaliyokuwa yakishirikiana na mume wake ndiyo yaliyosababisha kifo hicho. Uchunguzi wa kifo cha mume wake ulifichwa fichwa, ukapakwa mafuta mpaka ushahidi ukakosekana.
Miaka ilisogea, bi Nadiya Ali Rayan akapotezana na familia yake iliyobaki. Hata hivyo mtoto wa bi Nadiya Ali Rayan alikuwa akiishi chini ya kivuli cha mama yake pasipo yeye mwenyewe kujua, alijua alikuwa akipambana na wahalifu waliomuua baba yake kwa nguvu zake mwenyewe, kumbe nguvu za mama yake zilihusika kwa asilimia kubwa kwa kila hatua na tukio alilokuwa akilifanya. Siku hiyo mtoto aliangukia mikononi mwa mama yake baada ya dunia nzima kumuangukia ikihitaji kuondoa maisha yake, na siku hiyo hiyo ndiyo alibaini ukweli kuhusu mama yake mzazi. Ukweli kuwa mama yake alikuwa hai na alikuwa akimiliki genge kubwa la kigaidi lililokuwa likiendelea kufanya kazi za kigaidi nyuma yake pasipo yeye mwenyewe kujua. Bi Nadiya Ali Rayan alimtazama kwa huzuni mwanae aliyekuwa kitandani akiipigania roho yake baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kitako cha bastola alichopigwa usiku uliopita. Walikuwa wameshaongea mara chache lakini mara chache hizo hawakufikiana muafaka mzuri kutokana na hali ya mtoto wake. Chozi lilimtoka kisha sauti nyembamba toka moyoni kupitia mdomoni mwake ikasikika
“Kuanzia siku uliyotoweka mikononi mwangu nilikupatia jina la Aqsa, sitaki kukuita jina lako la zamani kwa sababu sio kitu tena mbele yangu. Kwa sasa, Jina Aqsa linafahamika nchi nzima lakini hata wewe ufahamu kama ni jina lako”
Japokuwa mwanae alikuwa hoi kitandani lakini aliisikia vizuri kauli ya mama yake, alifumbua macho na kumtazama mama yake aliyekuwa ametengeneza mifereji ya machozi usoni mwake. Mtoto akalazimisha kutabasamu lakini mbavu zake zikamsaliti, mbavu zilimuuma sana. Tabasamu likaishia njiani. Akafungua mdomo wake na kuongea huku akimtazama mama yake usoni
“Sasa leo hii nimemfahamu Aqsa ni nani? Nilikuwa sijui chochote kuhusu neno Aqsa…sasa nimetambua nastahili kuitwa Aqsa”
Akakohoa kikohozi kikavu kilichosababisha afumbe macho kwa maumivu aliyoyasikia, kisha akaendelea kuongea na mama yake
“Lazima nimalize kazi niliyoianza mama, lazima niwasambaratishe wote watakaojaribu kunizuia…nashukuru kwa jina jipya mama. Sasa naitwa Aqsa, jina toka kwa mama yangu niliyempoteza miaka mingi. Asante mama”
Huzuni iliyokuwa imetawala sura ya bi Nadiya Ali Rayan ilianza kupotea taratibu baada ya kusikia mtoto wake akimuita ‘mama’, ilikuwa imepita miaka mingi pasipo kusikia akiitwa namna hiyo. Vile vile alifurahishwa zaidi na kauli kutoka kwa mtoto wake, kauli iliyojaa ujasiri wa kupambana. Kauli iliyokosa chembe ya hofu japokuwa alikuwa kitandani akiugulia maumivu makali yaliyosababishwa na harakati za mapambano yake. Ndivyo alivyohitaji bi Nadiya Ali Rayan. Mtoto jasiri kwake ndiyo mtoto. Suala la mtoto wake kuongelea jina lake jipya hakulipa nafasi ya kuanza kulijadili. Hakutaka maongezi marefu kuhusu mada hiyo, alichotaka ni mtoto wake kufahamu kuwa jina la Aqsa ni jina lake na siyo vinginevyo.
Lilikuwa jina zuri sana kwa upande wake kwa sababu jina hilo lenye asili ya Kiarabu lilikuwa na maana ya ‘mwenye akili’ au ‘intelligent’ kwa watu wa mataifa ya magharibi. Japokuwa lilikuwa jina lenye maana nzuri lakini jina hilo lilikuwa na sifa mbaya sana katika taifa hilo, lilikuwa ni miongoni mwa majina yaliyokuwa yakitafutwa usiku na mchana kwa lengo la kudhibitiwa na mamlaka zenye dola lakini ilishindikana. Hakuna aliyekuwa na ushahidi wa kumfahamu Aqsa, japokuwa wapelelezi waliendelea kuwatilia mashaka baadhi ya watu. Akili ya mama na mtoto iliamini kuendelea kufanya mauaji kila inapowezekana, wao waliamini mauaji watakayofanya dhidi ya maadui zao yatakuwa faraja kwa wapendwa wao waliouliwa kinyama miaka mingi iliyopita. Walinuka roho ya visasi na waliamini hakuna mtu au idara itayoweza kuwazuia kutimiza azma yao. Waliimba mauaji.
1
RWAMA MWANZO, 2020
David Samson alimtazama mpenzi wake aliyekuwa akihesabu pesa iliyokuwa juu ya meza yao chakavu, meza iliyopoteza rangi yake ya asili kwa kupauka chaka chaka. Mpenzi aliyeishi nae kama mke na mume pasipo vigezo vyovyote, hawakuwa na baraka yoyote toka upande wowote wa asili yao. Mwanamke yule aliipata idadi kamili ya pesa, akamwambia David Samson.
"Imebaki mia saba na hamsini mpenzi"
Kichwa cha David kilikuwa moto kwa mawazo, hakujua afanye nini kwa wakati huo ili apate pesa kwa haraka, pesa atakayotumia katika huduma za kujifungua kwa mpenzi wake huyo, pamoja na huduma za kujikimu katika maisha yao. Mwanamke wake alikuwa na mimba ya miezi tisa, walitegemea kupata mtoto wao wa kwanza siku yoyote. Aliwaza kuomba msaada kwa ndugu na jamaa lakini aliamini hawezi kusaidiwa kwa sababu ameshawachosha kwa uombaji wake wa pesa. Alikuwa akinuka madeni kwa ndugu na marafiki zake. Upande wa mwanamke wake aliyefahamika kwa jina la Winnie Ngocho hakukuwa na namna yoyote wangeyoweza kuitumia ili kuupata msaada wao, kwa sababu upande ule haukuridhia kabisa David Samson kuishi na mtoto wao. Hivyo basi, walimzira mwana wao na kumfukuza moja kwa moja wakimwambia asije kugeuza kichwa nyuma kuwatazama. Walimaanisha kumuondoa kwenye idadi ya wana familia na ukoo kwa ujumla. David Samson aliinamisha kichwa chini kama kobe anayetunga sheria kisha akakiinua, tayari alikuwa ana majibu ya nini alichopaswa kufanya. Alimwambia Winnie Ngocho
"Acha nitoke niende mtaani kutafuta pesa, lazima pesa ipatikane kwa sababu siku yoyote unaweza kupata uchungu wa kujifungua"
Ilikuwa kauli nzuri katika masikio ya mpenzi wake lakini bado ilimpa mashaka na taharuki za kutosha. Ilibidi kuuliza ili apate ufafanuzi zaidi
"Unaenda wapi kutafuta pesa?"
David Samson alishindwa kumjibu mpenzi wake, aliamini akimwambia akiwazacho akilini mwake lazima apate pingamizi kali toka kwake. Aliapa kutomwambia kabisa. Swali la Winnie Ngocho lilikuwa na maana sana kwa sababu David Samson hakuwa na kazi yoyote baada ya kufukuzwa kazi ya ulinzi aliyokuwa akiifanya katika kampuni ya ujenzi iliyokuwa ikiongozwa na kampuni toka nchini China. David Samson aligeuza kichwa akamkazia macho mpenzi wake kisha akamwambia
"Ukimzaa mwanangu utamwita jina langu, endapo akiwa wa kike utamwita jina lako au jina la marehemu mama yangu"
Kauli ya David Samson ilikuwa ngumu kueleweka katika kichwa cha mpenzi wake, ilikuwa kauli tata kuwahi kusikia kutoka kwake. Winnie Ngocho alijiuliza maswali kadhaa wa kadhaa akilini mwake lakini alikosa majibu kamili. Baadhi ya maswali hayo yalikuwa
“Anataka kunitoroka na kuniacha peke yangu? Anataka kujiua? Anawaza nini kichwani kwake?”
Winnie Ngocho alipoinua kichwa chake kwa lengo la kuuliza maswali yake lakini hakubahatika kumuona mpenzi wake, David Samson alikuwa ameshatoka ndani ya nyumba hiyo. Hofu ikampanda Winnie Ngocho, mawazo yakazidi maradufu kichwani kwake. Uchungu wa uzazi ukachukua nafasi. Akaanza kulia kwa uchungu, kilio kile kilifanikiwa kuyafikia masikio ya David Samson aliyekuwa nje akivaa viatu tayari kwa kuondoka. David Samson alirudi ndani haraka akamkuta mpenzi wake akilalamika kwa uchungu. Macho yalimtoka pima David Samson. Alimbeba mpenzi wake mikononi mpaka barabarani, bahati ilikuwa upande wake kwa sababu alifanikiwa kuiona bajaji na kuisimamisha. Haraka kwa sauti ya kitetemeshi alimwambia dereva wa bajaji
"Tupeleke hospitali ya mkoa haraka"
Dereva alipoona hali ya Winnie Ngocho na uharaka aliokuwa nao David Samson aliamini hapo ndipo pa kupatia pesa, aliamini dau lolote atakalosema lazima wakubali. Aliongea
"Utanilipa elfu kumi ndugu yangu"
David Samson hakuwa na muda wa kujibizana na dereva, alimpandisha mpenzi wake kisha naye akapanda. Hata hakuelewa alichoambiwa, akili yake ilikuwa ikiwaza maumivu aliyokuwa akiyapitia mpenzi wake. Safari ilianza kwa mwendo kasi kwa sababu David Samson alikuwa akimshinikiza dereva wa bajaji awahi ili kunusuru maisha ya mpenzi wake pamoja na mtoto aliyekuwa njiani. Walifika hospitali, Winnie Ngocho akachukuliwa na manesi haraka wakampeleka wodi namba moja, wodi maalumu kwa masuala ya uzazi. David Samson alibaki na dereva wa bajaji. Alijisachi mfukoni kama mtu atafutaye pesa lakini hakuwa na kiasi chochote mfukoni. Akakumbuka hata ile shilingi mia saba na hamsini ya akiba imebaki katika nyumba walichopanga, akili ikawaza moto. Akamtazama dereva wa bajaji kisha akamuuliza
“Hivi ulisema shilingi ngapi?"
Dereva hakupendezwa kabisa na swali lile, aliamini kitakachofuata ni usumbufu kwa sababu alishuhudia jinsi David Samson alivyokuwa akihangaika kujisaji mifukoni pasipo kupata chochote. Akamjibu kwa hasira
"Elfu kumi jamaa"
David Samson alishituka kama mtu aliyeona au kusimuliwa kitu cha ajabu au chenye kutisha. Alikataa katakata akimwambia dereva yule kuwa hawezi kumlipa pesa kubwa kiasi kile sehemu ambayo kwa kawaida hulipa elfu mbili mpaka tatu. Mzozo ukaibuka. Kipindi mzozo ukiendelea, mmoja kati ya manesi waliompokea Winnie Ngocho alifika eneo lile na kuwatuliza kwa maneno ya upole. Walipotulia akamuuliza David Samson kwa sauti ya utulivu
"Bila shaka wewe ndiye uliyekuja na yule dada mwenye uchungu aliyevaa gauni lekundu?"
David Samson alijibu kwa haraka kwa sauti ya kuhema juu juu kutokana na majibizano aliyokuwa nayo na dereva wa bajaji
"Ndiyo dada yangu, wala hujakosea"
Sasa ilikuwa zamu ya nesi kuongea lakini alisita kidogo, akamkazia macho David Samson aliyekuwa na hofu pamoja na taharuki ya kutaka kufahamu nini kinachoendelea. Nesi akaongea
"Mwanamke uliyemleta ana njia ndogo ya kujifungua, siyo nzuri kwa mtu anayehitaji kujifungua kwa njia ya kawaida. Daktari na manesi wanajaribu uwezekano wa kumsaidia kujifungua kwa njia ya kawaida lakini lolote laweza kutokea. Ikishindikana kabisa atajifungua kwa upasuaji. Waweza kujiandaa kwa gharama za upasuaji pia japokuwa hatuombei apasuliwe"
Akili ya David Samson ilipaa kabisa akawa kama akiota huku amesimama wima, alishindwa kuongea wala kujibu chochote. Kwa mbali alisikia kelele za dereva wa bajaji, kelele zilizosisitiza kulipwa elfu kumi yake ya nauli. David Samson aliona jinsi maji yalivyozidi unga. Hakuwa na jibu lolote kwa nesi wala kwa dereva wa bajaji. Akili yake ikaikumbuka kauli ya rafiki yake kipenzi, kauli iliyomsisitiza kuwa jasiri ili afanikiwe kimaisha. Sasa aliona ni wakati wa kukubaliana na kauli ile ili aweze kupata pesa na kutatua matatizo yanayomzunguka. Nesi alivyoona ukimya wa David Samson alimpuuza na kuondoka zake eneo lile. Mzozo wa David Samson na dereva wa bajaji ukaanza upya, safari hii dereva alikuwa moto sana tofauti na awali. David Samson ilibidi awe mpole kama mtoto aombaye pesa ya ada kwa mzazi wa kambo. Akamwambia dereva wa bajaji
"Mimi ni mwanaume mwenzako naomba unielewe, sina pesa ya kukulipa ndugu yangu. Nimevurugwa hapa".
Kauli hiyo ilikuwa kama tusi kwenye masikio ya dereva yule. Kelele zikaongezeka maradufu. Watu wakajaa kushuhudia nini kilichokuwa kikiendelea, vile vile hata walinzi wenye kazi ya kudumisha ulinzi na usalama wa hospitali walifika haraka. Walijaribu kuwasikiliza wote, makosa yakaangukia kwa David Samson kwa kutolipa nauli, japokuwa hata dereva wa bajaji alikosolewa vikali kwa bei aliyoitaja. Baadhi ya raia walimtetea David Samson wakiamini atakuwa amevurugwa na hali ya mwanamke wake. Dereva alizidi kuwa mkali akihitaji pesa yake. Kelele zilivyozidi zilikuwa kero, David Samson akaamua kuondoa kero hilo, alikuwa tayari kujidhalilisha ili maneno yaishe. Alimwambia dereva yule kuwa ampe saa, mkanda na viatu alivyovaa ili awe amelipa deni lake. Dereva alikubali haraka sana, aliamini vitu vile vilikuwa na thamani kubwa kuliko pesa anayodai. Lakini kabda David hajavua chochote, ilisikia sauti nyororo ikisema
"Usimdhalilishe mwanaume mwenzako, muache aondoke zake nitamlipia deni lake"
David Samson aligeuka nyuma kumtazama aliyeongea, hakika alikuwa ni mrembo. Alikutanisha macho na mtoto mwenye asili ya Kiarabu akimtazama kwa huruma. Binti yule alitoa noti mbili za shilingi elfu kumi, moja akamkabidhi dereva wa bajaji na nyingine akamkabidhi David Samson kisha akamwambia
"Utafanya nauli ya kurudi kwako"
David Samson alimshukuru sana dada yule aliyekuwa kama malaika aliyetumwa na Mungu aende kumuokoa na aibu ya dunia. Dereva wa bajaji hakuwa na neno la kuongeza, hakumuaga yeyote wala hakuhitaji kumbeba tena David Samson kwa sababu walikuwa wameshatibuana vibaya. David Samson baada ya kumuaga binti yule wa Kiarabu aliondoka ndani ya jengo la hospitali haraka huku akili yake ikiwaza mpango alioambiwa na rafiki yake. Japokuwa alipewa pesa ya nauli lakini aliamua kutembea kwa miguu, aliamini akitumia pesa hiyo kwa wakati huo hatopata pesa nyingine. Mawazo yakarudi kumfikiria mpenzi wake aliyemuacha wodini, akazifikiria gharama alizoambiwa
"Eti gharama za upasuaji"
Aliamini lazima aingie kwenye kazi aliyoikataa awali. Ilikuwa kazi hatari lakini hakujali tena, alihitaji kupata pesa za haraka. Kipindi akipiga hatua kuelekea kwa rafiki yake, akili nyingine ilimkumbusha umuhimu wa kuandaa chakula cha mpenzi wake aliyemuacha wodini. Alibadilisha mawazo ya kwenda kwa rafiki yake. Aliona bora aende kwenye nyumba aliyopanga amuombe mpangaji mwenzake amsaidie kuandaa chakula cha mpenzi wake ili akipeleke hospitali. Ndivyo alivyofanya. Alimpatia Edna ile elfu kumi aliyopewa na dada yule mwenye asili ya Kiarabu. Edna hakuwa na hiyana yoyote, alikubali kuandaa chakula cha Winnie Ngocho. Alienda dukani kisha sokoni akanunua mahitaji ya Winnie Ngocho kisha akaingia jikoni na kuanza kupika. Kipindi upishi ukiendelea, David Samson alihisi akizidi kuchelewa kwenda kwa rafiki yake mwenye kazi za kijasiri. Aliondoka kimya kimya pasipo kumuaga Edna, akatokomea kusiko julikana.
Edna alipomaliza kuandaa chakula hakumuona David Samson, alipojaribu kumpigia simu iliita pale pale alipokuwepo. David Samson aliiacha simu yake makusudi. Edna alimsubiri David Samson pasipo mafanikio, masaa ya kuona wagonjwa yalipokaribia Edna aliamua kubeba chakula mwenyewe na kuelekea hospitali. Kitendo kile kilimuudhi sana Edna na kilimshangaza sana kwa David Samson kuondoka bila kumuaga na kuelekea mahali pasipo julikana wakati anafahamu hali ya mwanamke wake. Edna alifika hospitali na kapu lake la chakula. Mungu siyo Athumani, alikuta Winnie Ngocho amejifungua mtoto wa kike kwa njia ya kawaida. Lakini kitendo cha Edna kupeleka chakula pasipo uwepo wa David Samson kilimpa mashaka sana Winnie Ngocho aliyekuwa amembeba mtoto wake kipenzi mikononi. Alipomuuliza Edna ndiyo alizidi kuchanganyikiwa zaidi na kupatwa na taharuki.
Kipindi akiendelea kupambana na mshangao wake ghafla aliletewa risiti ya malipo ya huduma zote alizokuwa ameshahudumiwa hospitali hapo. Alipoitazama risiti ile kilikuwa kiasi kikubwa cha pesa kulingana na hali waliyokuwa nayo. Alijiuliza, David amepata wapi pesa hiyo haraka hivyo? Kwanini risiti iletwe na nesi? David yupo wapi?
Winnie akamuuliza nesi aliyemkabidhi risiti ile
"David yupo wapi?"
Jibu la nesi lilimuacha Winnie mdomo wazi, nesi alijibu
"Aliyenipa risiti alijitambulisha kwa jina moja la Zimwi, na siyo David. Kijana mwenye rasta fupi, alisema ni mdogo wako mnayefatana"
Jibu la nesi lilimvuruga zaidi Winnie Ngocho, eti mdogo wake wanayefatana wakati yeye ndiye mtoto wa mwisho katika familia yao! Alihisi kuna kitu hakipo sawa. Alimfikiria David Samson, sasa aliamini atakuwa ameenda kufanya kazi aliyomkataza kujihusisha nayo. Aliiona hatari mbele yake.
Zilipita siku mbili tangu Winnie Ngocho aruhusiwe kutoka hospitali. Mtoto wake wa kike aliyempa jina la Lucia, jina la marehemu mama yake na David Samson. Mtoto alikuwa na afya nzuri kabisa. Siku zote hizo hakufanikiwa kumuona David. Hofu na hali ya sitofahamu vilizidi kuchanganya akili ya Winnie Ngocho, alishangaa sana siku zilivyozidi kusonga pasipo kumuona kipenzi chake aliyekuwa akitamani kuwa naye kila dakika. Alijiuliza maswali akajijibu mwenyewe. Alishangazwa na kitendo cha David kushindwa kwenda kumuona mwana wake wa pekee.
Siku zilisogea kama kawaida, maisha ya shida yalikuwa rafiki yake. Siku moja jioni ya saa kumi na mbili Winnie Ngocho alipokea mgeni asiye mfahamu kabisa. Mgeni yule alikuwa akinukia marashi ya bei ghari sana, mgeni alijitambulisha kuwa ametumwa na mama yake ampelekee zawadi ya kujifungua. Winnie Ngocho alishangaa sana kusikia taarifa kutoka kwa mama yake mzazi aliyemkana na kumkataa baada ya kuamua kuishi na David Samson. Mgeni yule alimkabidhi begi dogo Winnie Ngocho alilomuhakikishia kuwa limetoka kwa mama yake kipenzi. Mgeni aliaga na kuondoka zake pasipo kujitambulisha kuwa yeye ni nani haswa. Winnie Ngocho hakujali hilo, yeye alifurahishwa pasi kifani na zawadi kutoka kwa mama yake mzazi. Baada ya kumaliza shughuli zake za nyumbani, Winnie Ngocho alifungua begi lile kwa lengo la kuangalia zawadi kutoka kwa mama yake. Alipata mshangao mkubwa na mapigo ya moyo yakaongezeka maradufu, haikuwa zawadi toka kwa mama yake kama alivyoambiwa awali na mgeni yule bali ilikuwa zawadi kutoka kwa mpenzi wake, David Samson. Begi lilikuwa na picha ya David Samson, kipande kidogo cha karatasi pamoja na noti nyingi za fedha. Alisoma kipande kile cha karatasi kilichokuwa na ujumbe uliosema
"Napambana kwa ajili yako na mwanangu. Chunga sana maisha yenu, uhai wenu ndiyo uhai wangu"
Winnie Ngocho alielewa fika kuwa aliyempa begi hilo atakuwa sehemu moja na mpenzi wake, na aliamini aliamua kumpa pesa zile kwa njia ile kwa sababu aliogopa kuulizwa maswali mengi kuhusu mpenzi wake. Moyo ulimuuma sana na kujilaumu kwanini hakufungua zawadi ile mbele ya mgeni wake. Alitamani asiitumie pesa aliyotumiwa kwa kuamini itakuwa haramu yenye damu za watu lakini alikosa jeuri hiyo, hali ngumu ya maisha aliyokuwa nayo ilimwambia kuwa pesa zile ni halali kabisa. Siku zilisogea kama kawaida, siku mara wiki mbili zikapita pasipo kumuona David Samson. Lakini suala la kupata pesa katika mazingira ya kutatanisha liliendelea kama kawaida. Kuna siku aliamka na kukuta mfuko wenye pesa mlangoni kwake, siku zingine watoto wadogo wa mtaani kwake walimpelekea bahasha ya kaki yenye hela na alipowauliza wamepewa na nani bahasha ile walimjibu hawamjui kabisa, na hawajawahi kumuona mtaani kwao. Vile vile aliendelea kupokea ujumbe tofauti tofauti wenye kumsisitiza kujitunza yeye pamoja na mwanae. Matumaini ya kumuona David Samson yalianza kupotea taratibu.
***
Ulikuwa usiku wa manane, nyota zilikuwa zimelipamba anga kila kona ya dunia. Mji ulikuwa kimya huku raia wengi wakiendelea kuota njozi njema za mafanikio. David Samson alikuwa kazini. Alikuwa amevaa begi dogo la mkanda mmoja, ndani ya begi hilo kulikuwa na madawa ya kulevya aina ya heroine aliyokuwa akiyapeleka katika pwani ya ziwa Kuu, sehemu maarufu kwa jina la forodhani. Sehemu maalumu ambayo wavuvi huegesha vyombo vyao vya majini. Alihakikishiwa kuwa akifika eneo lile atakutana na kijana mweusi mwenye miraba minne, amkabidhi begi hilo kisha aondoke zake. Ndivyo ilivyokuwa. Alifanikiwa kumuona kijana huyo wa miraba minne akamkabidhi begi lile kisha wakaagana. Kijana mwenye mwili wa miraba minne aliwasha boti lake la mwendo kasi kisha safari ya kuelekea nchini Congo ikaanza. David alibaki akijiuliza
"Atawezaje kuingia na mzigo wa madawa nchini Congo?"
Hakika David Samson alikuwa hajakomaa kwenye biashara hiyo. Taratibu akageuka na kuanza kurudi alipotoka. Lakini Mungu hakuwa upande wake, ghafla alishangaa mwanga mkali wa tochi ukimpiga usoni. Alibabaika kwa hofu. Kabda hajachukua hatua yoyote alisikia sauti kali ya kukwaruza ikimshurutisha kusimama na kuweka mikono juu. Kilikuwa kitendo cha haraka sana kilichomchanganya. Alibaki akitetemeka kama mtoto mdogo na alishindwa kutii amri ile kwa sababu hakuelewa kabisa alichoagizwa kufanya. Taswira ya mpenzi wake akiwa na mimba ikamjia kichwani. Moyo ukamuuma sana kuona anaelekea kwenye shimo la hewa. Shimo litakalo mtenga na familia yake. Mwanaume aliyemshurutisha awali akaipaza sauti yake kwa mara ya pili
"Naitwa kapteni Mussa toka jeshi la polisi, upo chini ya ulinzi kwa kujihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya"
Mwanzo David Samson alimurikwa na tochi moja, lakini muda huo alikuwa akimurikwa na matochi zaidi ya saba kitu kilichomaanisha aliyepaza sauti hakuwa peke yake. Mwanga uliongezeka maradufu machoni, macho ya David Samson yakashindwa kuvumilia kabisa akajikuta akiukinga uso wake kwa mikono ili kupambana na mwanga ule, lakini alihisi kuna miale ya mwanga iliendelea kupenya. Alitamani ageuke nyuma ili atimue mbio lakini alijihakikishia kitendo hicho lazima kimpeleke kuzimu, aliamini lazima apigwe risasi za mgongo kisha kifo kichukue nafasi yake. Akili ilikataa, aliona bora aende gerezani kwa sababu atapata wasaa wa kuonana na mwanae pamoja na mpenzi wake, Winnie Ngocho. Alibaki amesimama wima kama mlingoti wa umeme huku mikono yake ikiendelea kupambana na mwanga uliokuwa ukimshambulia pasipo huruma. Vijana zaidi ya saba waliokuwa na matochi zenye mwanga mkali walimfuata taratibu. Walikuwa wakijihakikishia usalama wao. Walipomfikia hawakuwa na jambo la kuuliza wala kuongea. David Samson alipigwa kitako cha bunduki kichwani, alishindwa kuvumilia maumivu yake, mikono iliyokuwa usoni ikipambana na mwanga ilihamia kichwani mahali aliposhambuliwa. Alipiga kelele zilizomaanisha alikuwa akipitia maumivu makali, kijana mwenye sauti kali ya kukwaruza hakujali kilio cha David Samson, alipaza sauti
"Kaa kimya mpuuzi wewe, unaleta utoto hapa"
Sauti ile ilipenya vizuri katika masikio ya David Samson, alijikuta akikaa kimya pasipo kupenda, kwa mbali alisikika akilia kilio cha kwikwi. David Samson aliinua kichwa chake kisha akawatazama vijana wenye matochi, alijihakikishia walikuwa zaidi ya saba, hakuna hata mmoja aliyekuwa amevaa mavazi ya polisi japokuwa walikuwa na silaha za moto. Vijana wale walikuwa wamevaa mavazi ya kisasa yanayopendwa na vijana wanaoanza kubarehe mpaka vijana wenye miaka thelathini na sita au arobaini. Hakujali muonekano kwa sababu polisi siyo lazima avae jezi zake, kuna baadhi ya kazi humlazimu kuvaa kiraia. David Samson alijaribu kujitetea lakini vijana wale hawakuwa na muda wa kumsikiliza. Walimfunga pingu mikononi kisha akavishwa soksi usoni, soksi iliyomzuia kuona chochote. Alikuwa akiona giza mbele yake. Aliinuliwa kwa nguvu na kuanza kuongozwa njia, hakujuwa walikuwa wakielekea wapi kwa sababu soksi aliyovishwa ilitoa pingamizi la kutosha. Alijutia maamuzi yake ya kujiunga katika kundi haramu linalosambaza na kuuza madawa ya kulevya ndani na nje ya nchi, alikumbuka mara kadhaa alivyokatazwa na mpenzi wake kuhusu kujiingiza kwenye mtandao huo. Aliuona usaliti wake, usaliti uliomponza sasa. Akajisemea moyoni
"Nisamehe Winnie wangu, sikusikiliza kauli yako. Acha dunia inifunze"
Hakika hakusikiliza kauli ya mpenzi wake lakini angefanya nini wakati alikuwa akihitaji pesa za haraka kwa ajili ya kumsaidia mpenzi wake pamoja na mtoto?
Safari ya kibubu bubu ilishia ndani ya gari, David Samson aliingizwa garini kisha akalisikia likiondoka kwa mwendo wa wastani. Hakujuwa ni aina gani ya gari na walikuwa wakielekea kituo gani cha polisi, alichojuwa yeye walikuwa ndani ya gari linaloelekea kituo cha polisi. Alijisemea na kujiapiza ndani ya moyo wake kuwa hatawataja wenzake anaofanya nao kazi, alijihakikishia kuwa hata apigwe namna gani hatofungua mdomo wake kuwataja wenzake. David Samson alihofia usalama wa familia yake, aliamini endapo akiwataja wenzake atakuwa ameihatarisha familia yake. Aliamini lazima waishambulie na kuiteketeza kabisa. Hakutaka kusikia suala la kifo cha mpenzi wake wala mtoto. Aliamini yeye ndiye wa kuwatetea kwa sababu hawakuwa na msaada sehemu nyingine. Hakika alitaka kosa alilolifanya limuhukumu mwenyewe.
ITAENDELEA