IAmShedeOne
JF-Expert Member
- Jul 2, 2015
- 202
- 382
MARY MARIAM (01)
BEKA MFAUME
Alizaliwa nje ya ndoa. Baba yake hakuwahi kumwona ingawa aliamini yuko hai. Alisikia tu akiambiwa baba yake ni Mwarabu. Aliamini hivyo kwa sababu hata damu yake ilimdhihirishia ukweli huo. Alikuwa shombe wa Kiarabu aliyezaliwa na mama wa Kibondei mwenyeji wa Muheza mkoani Tanga kwenye Kijiji cha Lusanga. Hakuwahi kuambiwa na mama yake au babu yake aliyemlea, kuwa baba yake ni Mwarabu. Alisikia baba yake alikuwa akiitwa Mahfudh, jina ambalo halikutakiwa asilani kusikika kwenye familia yake! Alipewa jina la Mary kulirithi jina la bibi yake mzaa mama yake aliyekwishafariki miaka mingi ya nyuma. Akapewa ubini wa Goda ambalo ni jina la babu yake, kwa sababu ndiye aliyemlea.
Akaitwa Mary Goda.
Akakiri, kweli alikuwa mtoto wa haramu!
MAMA yake aliitwa Mboza. Alipata ujauzito wakati akifanya kazi za ndani, nyumbani kwa tajiri wa Kiarabu anayeitwa Mahfudh, mmiliki wa duka la rejareja kwenye mji mdogo wa Muheza kilomita chache kutoka mji wa Tanga.
Mahfudh aliishi na mkewe, naye pia ni Mwarabu waliotoka pamoja Yemen, waliofunga ndoa ya kindugu, mtu na binamu. Mkewe alikuwa mkorofi mwenye tabia ya kupayuka wakati wote, aliyesumbuliwa na wivu dhidi ya mumewe kwa hofu asije akatembea na wanawake wa Kiswahili.
Pamoja na sifa hizo za mkewe, bado Mahfudh aliweza kumrubuni Mboza, akafanikiwa kufanya naye mapenzi humohumo ndani ya nyumba bila ya mkewe kujua. Hatimaye Mboza akapata ujauzito!
Ulikuwa mshtuko uliomtingisha Mboza kujigundua ana ujauzito. Kwanza alifanya siri, akaogopa kumwambia Mahfudh. Aliogopa kwa sababu hata tajiri yake, naye alikuwa mkorofi. Alihofu endapo angemwambia kuwa ujauzito ni wake, asingeikubali. Ukimya wake wa kutomwambia, ukamfanya Mahfudh aendelee kufanya naye ngono huku Mboza akiambulia kuhongwa vibaba vya mchele, unga, mafuta ya kupikia, maharage na vijisenti vya hapa na pale kama kitulizo.
Ujauzito hauna siri, tumbo la Mboza likaanza kuumuka, shangazi yake akawa wa kwanza kugundua. Akamwita, akamhoji. Dakika za mwanzo za mahojiano, Mboza alikataa kujibu. Lakini alipobanwa kwa aina tofauti ya vitisho, akakiri kuwa kweli ni mjamzito. Akamtaja Mahfudh kuwa ndiye mhusika wa ujauzito huo! Taarifa zikamwendea babu yake anayeitwa mzee Goda ambaye ni mlezi wake. Naye akamwita ili kupata uhakika wa taarifa hizo. Mboza akaulizwa, akakiri yeye ni mjamzito. Akarudia kwa mara nyingine kumtaja Mahfudh kuwa mhusika na ujauzito huo!
Mzee Goda, akachukua hatua za kuwaarifu wazee wenzake. Wakakubaliana jambo hilo lisiachwe hivyohivyo. Wakachaguliwa baadhi ya wazee waende wakamwone Mahfudh kwa mazungumzo ya kina ili ijulikane hatima ya binti yao.
Ikapangwa siku, wakaenda.
******
ILIKUWA baada ya sala ya Insha inayosaliwa mapema usiku, Mahfudh alipokuwa akitoka msikitini. Wazee watatu waliokwenda kumwona, wakamwona. Wakamwangalia Mahfudh aliyekuwa akitembea peke yake, wakamfuata.
“Sheikh Mahfudh!” mmoja aliita.
Mahfudh akasikia, akageuka nyuma. Akawaona watu watatu wakimfuata. Akasimama na kuwaangalia kwa umakini. Akagundua hamjui hata mmoja.
Wakasalimiana.
“Tumeshindwa kukufuata nyumbani, suala lenyewe ni zito kidogo,” mmoja wao aliyeonekana kuwa kinara, alimwambia Mahfudh.
“Suala gani?” Mahfudh aliuliza kwa sauti iliyokosa nidhamu baada ya kuhisi wamemfuata kwa shida ya pesa.
“Inamhusu binti yetu Mboza!”
“Ana nini?”
“Ni mjamzito!”
Macho ya Mahfudh yakapepesa kwa haraka kuonyesha mshtuko. “Sasa hilo linanihusu nini?” aliuliza kwa sauti iliyoongeza kiburi. Taswira ikasomeka usoni mwake. Alikuwa ameshahisi kinachotaka kuzungumzwa!
“Mzigo ni wako!”
Mahfudh akaduwaa kwa sekunde. Alipoona wazee wale wakimwangalia machoni, akapepesa macho na kutoa kicheko kidogo cha kuigiza lakini kilichofanikiwa kuonyesha dharau.
“Hivi mna akili kweli?” alisema. “Mnakuja kunidhalilisha kwa kuniambia nimempa ujauzito binti yenu? Ndivyo alivyowaambia?”
“Ametuambia, wewe ndiye mwenye mzigo ule!”
“Kwa akili yenu mnadhani mimi ninaweza kutembea na binti yenu? Kwa kitu gani?” Mahfudh alisema huku akionekana kukosa mhimili wa kujizuia kubaki kwenye busara. “Mimi nitembee na mtu mweusi? Hakika mmejua kunidhalilisha. Si mnajua kama yeye ni kijakazi cha pale nyumbani kwangu?”
“Hilo tunalijua,” mwingine alijibu kati ya wale wazee.
“Kwa hiyo mimi nimetembea na kijakazi changu?” Mahfudh aliuliza. “Hakika mmejua kunitusi!”
“Amekutaja wewe!” mzee mwingine aliamua kujibizana na Mahfudh huku akiijenga sura ya mapambano.
“Nendeni mkamuulize vizuri ni nani aliyempa hiyo mimba! Anafikiri kunitaja mimi kumtamsaidia nini? Huku ni kunidhalilisha! Kwanza yeye Mkristo, nitatembeaje na Mkristo wakati mimi ni Mwislamu? Sitopenda habari hizi zikimfikia mke wangu. Akizisikia, zitamhuzunisha. Ni yeye ndiye mwenye kumkarimu kwa kumpa vyakula kila siku, halafu leo asikie uvundo kama huu? Amewadanganyeni! Nendeni mkambane vizuri, atawaambia ni nani aliyempa mimba hiyo. Na nyie watu wazima badala ya kufikiri, mnabebeshwa uongo na kuja kupotezeana muda. Kwa kweli mmenisikitisha!” Baada ya kusema hivyo, Mahfudh akaondoka na kuwaacha wazee hao wamepigwa na butwaa.
Baada ya kupiga hatua kadhaa, Mahfudh akageuka ghafla na kuwaangalia wale wazee. “Na sitaki kumwona tena akija nyumbani kwangu. Nimeshamfuta kazi!” alibwata na kutokomea!
Mzee Goda akapelekewa taarifa kuwa Mahfudh ameikataa mimba, akapewa na nukuu za kejeli alizozitoa. Jazba ikampanda mzee huyo, akavumilia kwa siku mbili akitafakari hatima ya binti yake huku akichemka kwa hasira kila alivyorejewa na kumbukumbu za kejeli zilizotolewa na mwarabu huyo.
Siku ya tatu mzee Goda akamwendea Mahfudh dukani kwake akiwa na bakora mkononi! Akamkuta.
“Wewe ndiye Bwana Mahfudh?” mzee Goda aliuliza kama kwamba alikuwa hamjui Mahfudh.
Mahfudh akasita kujibu haraka. Kwanza alikuwa hamjui mzee huyo. Pili, sura aliyokuwa akikabiliana nayo ilijenga shari. Wakatazamana kwa sekunde chache huku wateja wawili waliokuwepo dukani wakionekana kuvutika na tukio hilo.
“Wewe ni mgeni hapa Muheza?” Mahfudh aliuliza kwa sauti ya kijeuri kumaanisha yeye ni mtu maarufu sana hapo mjini.
“Usiniletee ufedhuli!” mzee Goda aling’aka kwa jazba. “Umesikia? Nakwambia usiniletee ufedhuli! Niambie, wewe ndiye Mahfudh?”
Macho ya Mahfudh yakaiangalia bakora iliyo mkononi mwa mzee Goda, akakiri moyoni kuwa, asipokuwa makini na mzee huyo, bakora hiyo inaweza ikamwingia mwilini.
“Ndiyo!” Mahfudh alikiri na kumwangalia mzee Goda kwa hadhari.
“Mimi ni baba yake Mboza!” mzee Goda alisema huku kidole chake gumba kikipiga kwenye kifua chake na kumtolea macho Mahfudh kama kwamba utambulisho huo uliwakilisha kila kitu.
Na kweli! Utambulisho wake ukaleta uwakilishi uliotakiwa. Mahfudh akanywea ghafla. Akawaangalia wateja waliokuwepo pale dukani. Akawaona wamevutiwa na tukio hilo.
“Nisubiri kidogo nimaliziane na hawa wateja,” Mahfudh alimwambia mzee Goda kwa sauti iliyosihi.
Mzee Goda akatulia. Mahfudh akawahudumia haraka wateja waliokuwepo na kuwamaliza. Lakini hawakuondoka!
“Sasa mnasubiri nini?” Mahfudh aliwageuzia kibao wateja wake. “Nimekwisha wahudumia, ondokeni!”
Wateja wale wakaondoka.
“Kulthum!” Mahfudh aliita kwa sauti ya juu baada ya wateja kuondoka eneo hilo.
Kulthum akaja. Alikuwa ni mkewe, aliyetembea kwa kujikokota kutokana na uzito wa mwili uliomsababisha kuumwa miguu. Wakazungumza kwa lugha ya Kiarabu. Mke wa Mahfudh akamwangalia mzee Goda, mzee Goda akayatuliza macho bila ya kupepesa kumwangalia mwanamke huyo. Mke wa Mahfudh akakwepesha macho, akendelea kuongea na mumewe, kisha Mahfudh akatoka nje na kumwacha mkewe dukani.
“Twende tukazungumze,” Mahfudh alisema kwa sauti iliyopwaya, iliyoondoka kwenye kiburi na kujenga nidhamu.
Watu hao wawili wakaongozana hadi kwenye kibanda kilichokuwa na bucha siku za nyuma iliyomilikiwa na Mahfudh. Wakasimama nyuma ya kibanda hicho kwa ajili ya kivuli, wakawa peke yao.
Mzee Goda akaenda moja kwa moja kwenye hoja yake. “Binti yangu anadai wewe ndiye uliyempa ujauzito. Unasemaje?”
Mahfudh akaruka kimanga. Akaapa kwa viapo vyote hahusiki na ujauzito huo.
“Sikiliza Mahfudh,” mzee Goda alisema huku akinyoosha bakora aliyokuwa akiitetemesha mkononi mwake ambayo ncha yake iligusa kifua cha Mahfudh huku akisema kwa msisitizo. “Sitaki kukulazimisha kuwa mimba ile ni yako kwa sababu sina ushahidi. Lakini, endapo binti yangu atajifungua mtoto mwenye damu ya Kiarabu, nakwambia Mahfudh, utamuoa Mboza unataka, hutaki! Wewe dini yako si inakuruhusu kuoa mke zaidi ya mmoja? Basi utamuoa Mboza! Labda mtoto atakayezaliwa asiwe na damu ya Kiarabu!” Baada ya kauli hiyo, mzee Goda akaondoka kwa hasira bila ya kumuaga Mahfudh.
Jeuri ya Mahfudh ikapotea, akamwangalia mzee Goda alivyokuwa akiondoka. Hakuthubutu kutamka lolote wakati mzee huyo akitokomea kwenye barabara yenye udongo mwekundu! Tishio la mzee huyo likawa limemweka mahali pagumu. Hofu ikamwingia huenda ujauzito unaozungumzwa ukawa ni wake kweli. Hata hivyo, akaliona tatizo jingine mbele yake. Asingeweza kumuoa Mboza, hata kama ujauzito huo ungekuwa ni wake! Yeye mwenyewe binafsi hakuwa tayari kumwoa mwanamke mweusi. Kwanza angeshutumiwa na familia yake, lakini hata ile iliyoko Uarabuni nayo ingemshutumu kwa kuchafua rangi ya jamii yao kwa kuingiza damu isiyotakiwa!
Pili, Mboza alikuwa dini tofauti, Mkristo! Kwao udini uliwatawala kwa kiasi kikubwa. Hiyo ingekuwa dosari nyingine! Tatu, ingekuwa aibu kwake kuzaa na mtumishi wake wa ndani, pamoja na kwamba alijiwa na fikra, hata Nabii Ibrahim alizaa na mtumishi wake, lakini kwake yeye alijiona amekwenda mbali. Yaani mtoto atakayezaliwa mwenye nasaba na mtu mweusi, ahalalishwe kuwa ni wake na jamii ikalijua hilo? Angeuweka wapi uso wake? Nne, Angejieleza vipi kwa mkewe kuwa, ni kweli mimba hiyo mhusika ni yeye! Alikiri udhaifu aliokuwa nao mbele ya Kulthum, kuwa alikuwa hana kauli kwa mkewe! Moja kwa moja akatambua, asingeweza kuukabili ugomvi utakaoanzishwa na mkewe endapo atazisikia habari hizo!
Miezi miwili iliyofuata, Mahfudh akaliuza duka lake kwa Mwarabu mwenzake raia wa Yemen. Akaichukua familia yake na kuikimbia nchi, akarudi kwao Yemen!
Huku nyuma, Mboza akajifungua mtoto wa kike, akapewa jina la Mary. Babu yake akamchukua na kumlea.
Akaitwa Mary Goda!
*****
MZEE Goda alifariki Mary akiwa na umri wa miaka kumi na moja!
Mboza ambaye alimwacha Mary mikononi mwa baba yake baada ya kumzaa, yeye ndiye aliyetaka mwanaye apewe jina la ‘Mary’ ili iwe kumbukumbu ya marehemu mama yake mwenye jina hilo ambaye naye alifariki wakati yeye Mboza akiwa mdogo. Mara baada ya kumwacha Mary mikononi mwa mzee Goda, Mboza alihamia kijiji cha Lusanga kilicho kilomita chache kutoka Muheza kwa kile alichodai, anakwenda kulima. Akaishi huko hadi kifo cha baba yake, mzee Goda kilipotokea.
Kifo hicho kikamlazimisha arudi Muheza kumchukua mwanaye, Mary baada ya kushindikana kulelewa na aliyekuwa mke wa mzee Goda. Mary akapelekwa kijijini Lusanga kuanza maisha mapya akiwa na mama yake. Huko ndiko tofauti ya maisha ilikoanza kwa mtoto huyo.
Maisha ya Muheza alikolelewa na babu yake yalikuwa ya kijukuu, pamoja na kwamba hayakuwa yenye kipato kizuri, lakini yalikuwa ya kawaida. Alikuwa akila milo yote mitatu na alikuwa na furaha wakati wote. Kuletwa kwake Lusanga, kukabadilisha taswira yote ya maisha hayo aliyokuwa akiishi nayo Mji wa Muheza.
Akiwa Lusanga, Mary alipambana na sulubu za maisha zilizoandamwa na umaskini uliokithiri na mfumo wa maisha alioukuta. Mama yake ambaye alishaathirika na tabia ya ulevi uliopindukia wa kunywa pombe za kienyeji hasa pombe ya mnazi, aliishi na bwana ambaye naye alikuwa mwathirika wa ulevi huo uliopitiliza ambaye ndiye angekuwa ni baba yake!
Baba yake huyo aliitwa Mgaya, mwenye kazi ya ugemaji wa pombe ya mnazi iliyokuwa ikimpatia kipato duni. Yeye akawa kichwa cha kuangalia maisha ya familia hiyo ya watu watatu. Biashara ya ugemaji pombe na kisha baadaye kupelekwa kuuzwa kwa wateja, haikuwa yake. Yeye aliajiriwa na mmiliki wa kitalu cha minazi inayogemwa tembo hilo. Pamoja na kugema, lakini pia akawa na kazi ya usambazaji kwenye vilabu tofauti vya kuuzia pombe hiyo kwa kutumia baiskeli. Kipato kilichopatikana kutokana na ajira hiyo hakikutosheleza mahitaji ya nyumbani. Na ili kujiongezea kipato, ikamlazimu kuhifadhi nyumbani baadhi ya pombe na kuiuza kwa wateja wachache ambao ni majirani.
Akiwa amehamia shule ya msingi iliyopo hapo Lusanga baada ya kutoka Muheza ambako alikuwa na uwezo mzuri wa masomo, Mary aliendelea kuwa mmoja wa wanafunzi wanaofanya vyema shuleni, akishika namba za juu, kuanzia moja hadi tatu katika mitihani ya shule aliyokuwa akiifanya. Lakini kadri siku zilivyokuwa zikienda, hali ngumu ya maisha iliyopo nyumbani kwao, ukawa ni mtihani mwingine kwake.
Ulevi uliokithiri wa wazazi wake ukawafanya kukosa umakini wa kukijali kipaji chake. Badala yake, Mary akawa anatumika kama jembe la kufanya kazi zote za hapo nyumbani. Siku zote alizokuwa akitoka shule hakuwahi kukuta amewekewa chakula. Hali hiyo ilimlazimu awe anajipikia mwenyewe ugali endapo atakuta mboga. Na endapo hakutakuwa na mboga, aliishia kupika uji na wakati mwingine aliunywa bila ya sukari.
Siku zote alienda shule bila ya pesa mkononi, kama hiyo haikutosha, pia alikuwa akiondoka bila ya kifungua kinywa. Aliishi kwa kudoea vitafunwa vilivyonunuliwa au kuletwa na wanafunzi wenzake. Baadhi ya siku, wanafunzi wakawa wanamkwepa na kumsimanga kwa kebehi zilizohusisha tabia za ulevi wa wazazi wake. Mary akakosa uthubutu wa kujibu kwa sababu ni ukweli aliokuwa akiuona!
Siku zote alipambana na sulubu ya kuchota maji kwenye bomba lililokuwa umbali wa mita mia moja au zaidi kutoka nyumbani kwao. Sare zake za shule alizotoka nazo Muheza, zikaendelea kuchakaa, zikakosa mbadala. Shati la sare yake hiyo likapoteza mwonekano, likakaribia kufanana na bendeji huku kola yake ikiwa na mwonekano wa chandarua.
Akawa mpishi wa kila siku wa chakula cha usiku. Siku zote ikawa ni ugali na mboga ya majani aina ya mchunga au dagaa kavu la chukuchuku. Pamoja na kutumika kote huko, bado alitakiwa na wazazi wake kusaidia kuwauzia wateja pombe hapo nyumbani. Kitendo hicho kikamfanya agombane na wateja mara kwa mara waliokuwa wakipenda kumtomasa mwili wake. Ingawa alivilalamikia vitendo hivyo kwa wazazi wake, bado alikosa msaada wa kutetewa kutoka kwao.
Wazazi wake wakawa wanavichukulia vitendo vya kutomaswa mwili binti yao, ni kama sehemu ya kukomaa kwake kuelekea utu uzima. Hakuna aliyejali au kutafakari kama binti yao huyo alihitaji muda wa kufanya kazi za shule zilizotakiwa kufanywa nyumbani. Mzunguko huo wa kukosa utulivu wa akili ukaathiri uwezo wake wa masomo darasani. Maendeleo yake ya shule yakaporomoka na kuwa mabaya. Walimu wakataka kujua chanzo cha maendeleo yake kuwa mabaya. Wakagundua ni mazingira mabovu yaliyopo nyumbani kwao ndiyo chanzo cha matokeo mabaya. Nao wakashindwa kumsaidia kwa sababu wazazi wake hawakuwa waelewa pamoja na kuitwa na uongozi wa shule zaidi ya mara moja, lakini hawakuwa msaada. Mary akaachwa kama mshumaa unaoteketea!
Mtihani wa Taifa wa darasa la saba ulipowadia, yeye akiwa ni mmoja wa watahiniwa, shule yao ikafaulisha wanafunzi tisa, jina la Mary Goda likiwa halimo!
*******
MATOKEO hayo yalimwumiza Mary baada ya kwenda kuyasoma. Akarudi nyumbani na kumfuata mama yake huku akilia kwa lengo la kutaka kumfahamisha.
Mama yake akamwangalia kwa mshangao. “Kinachokuliza?” alimuuliza mwanaye.
“Mama nimefeli!” Mary alisema mara moja na kuangusha kilio cha wazi.
“Huko kufeli ndiyo ulie?” mama yake alihoji kwa kejeli. “Hebu niondokee! Kwanza maji yameisha humu ndani, fanya ukachote badala ya kunililia kama mimi ndiye niliyekufelisha!”
Likawa pigo jingine kwake!
Akiwa anayafikiria maisha anayoendelea kuishi nayo hapo, Mary akawa anajiuliza karibu kila siku kama hayo ndiyo yatakuwa aina ya maisha atakayoishi nayo kwa wakati wote wa uhai wake? Akakifikiria kijumba anachokaa. Kibanda, mbavu za mbwa. Chumba chake hakikuwa na dirisha, nuru iliyokuwemo ilipatikana kupitia mwanga wa jua uliofanya miali iliyopenya kwenye matobo yaliyosheheni kwenye kuta za kibanda hicho. Ndani ya chumba chake hakukuwa na kabati wala sanduku. Kamba ya katani iliyokatiza kutoka ukuta hadi ukuta, ndiyo iliyochukua nafasi ya kuhifadhi viguo vyake vilivyoning’inia na kuonekana kama malapulapu yaliyowekwa kwa mafungu.
Akiwa amejilaza kwenye kitanda chake cha kamba kisicho na godoro huku nguo kuukuu zilizotandazwa katikati ya kitanda na kuwa sehemu ya godoro, Mary alikuwa akilia kwa uchungu kutokana na kukosa kuchaguliwa kujiunga na masomo ya elimu ya sekondari. Akiwa katika hali hiyo, huko nje akawa anamsikia mama yake akimzungumzia kwa wateja waliokuja kunywa pombe kuhusu kutochaguliwa kwake kwenda sekondari. Alikuwa akizungumzia kwa furaha kama vile jambo hilo lilikuwa la kawaida. Na wakati mwingine akawa anabeza hata tukio la kulia kwake!
Kauli za aina hiyo zikaendelea na kumpa hitimisho ni namna gani suala lake la elimu lilivyokuwa halipewi kipaumbele na wazazi wake. Hali hiyo ikamrudishia kumbukumbu ya malezi aliyoyapata kutoka kwa babu yake na maisha anayoishi hapo na wazazi wake hao wawili. Yalikuwa maisha ya aina mbili tofauti. Siku zote babu yake alikuwa akimwonyesha upendo kwa kumhimiza kwenda shule. Walikuwa wakikaa pamoja wakizungumza, kucheka na kutaniana. Mambo ambayo kwake yakabaki kama historia isiyosahaulika.
Alimshuhudia mama yake akikosa upendo na yeye. Alimwona akijali ulevi na kumthamini mumewe. Kati yao hakuna aliyekuwa akimjali. Kuanzia kutoendelea kwake shule wala kujali hatima yake itakavyokuwa. Matokeo ya shule yaliyotoka, yakawa yamezimisha matumaini yake yote. Hakuijua hatima yake na kila kitu kilikuwa kiza mbele yake!
Pamoja na kuamini hivyo, lakini kulikuwa na kitu kilichokuwa kikimwambia, hayo siyo maisha unayotakiwa uishi. Hakujua kwa nini alijiwa na hisia hizo mara kwa mara. Pamoja na kuwa na msukumo huo wa matamaini asiyoyaona, ukweli ukawa uko palepale. Mji wa Muheza na kijiji cha Lusanga anachoishi, ndiyo ulimwengu pekee anaoujua!
Kukoma kwa maisha ya kwenda shule, kukamwingiza kwenye maisha mapya. Maisha ya kuamka kila asubuhi, kufanya usafi wa nyumbani na kuandaa mazingira ya wateja kuja kunywa pombe, huku yeye na mama yake wakishirikiana kuuza! Shughuli hiyo ya kuuza pombe, ikamfanya kila siku inayoingia agombane na wateja waliokuwa hawachoki wala kukoma kumtongoza kwa lugha rahisi na za kipuuzi. Wapo walioahidi kumwoa na wengine walidiriki kumrubuni kwa vijipesa vyao huku wakimshawishi ajifunze kunywa pombe, wakiamini kwa kufanya hivyo, ingekuwa njia rahisi kwao kumpata wakati akishalewa. Vitendo hivyo vikamwingiza baba yake kugombana na wateja hao.
Kumwona baba yake akimtetea kukampa nafuu ya kutopata bughudha za mara kwa mara, lakini pia kukamwezesha kuwajibu jeuri wale wote waliojaribu kumtomasa sehemu tofauti za mwili wake. Hata hivyo, laiti Mary angeijua sababu ya baba yake kumlinda, kamwe asingejiona yupo salama ndani ya nyumba hiyo!
***