Riwaya:Kufa na Kupona

Sura ya Kwanza

Karatasi za Siri

Ilivyo ni kwamba mimi siku za Jumapili hulala mpaka saa tatu au saa nne. Na kama huamini hiyo si shida yangu. Ilikuwa Jumapili nyingine. Usiku wa jana, yaani Jumamosi, nilikwenda kwenye dansi na rafiki yangu mmoja msichana. Tulirejea nyumbani mnamo saa tisa na nusu za asubuhi. Kutokana na uchovu mwingi ulionielemea nikafahamu wazi kwamba Jumapili hii nitaamka kama saa tano hivi. Lakini utastaajabu nikikwambia kuwa Jumapili hiyo ilinibidi niamke saa kumi na moja alfajiri!

Kengele ya simu ililia mnamo saa kumi na moja, na miye nilikuwa nimelala saa moja tu hivi. Nilipuuza kuichukua kwani nakueleza nilivyochukia, Mungu ndiye anayejua. Iliendelea kulia na kulia, mwishowe nikaona nisipoijibu pia nisingeweza kulala kwa sababu ingaliendelea kuniudhi. Huyu binti aliyekuwa amelala karibu na hii simu naye aliamka, akaniomba afadhali niijibu. Basi kwa shingo upande, nilimwambia huyu binti anisogezee. Yeyote yule aliyekuwa amepiga hii simu nilikuwa mpaka sasa nimechukia kiasi cha kwamba angalikuwa karibu ningalimwuma.

"Hallo, huyu ni Chifu." Nilisikia sauti ikisema.

Usingizi ulipotea papo hapo, nikajua kuna jambo, maana, S, anapojifahamisha kwa jina la Chifu jua kuna kazi, na kazi kubwa. "Halo, huyu ni Willy. Chifu mbona unapiga simu wakati kama huu? Nadhani ingefaa uwe kitandani, la sivyo utazidi kuzeeka upesi, kwa mtu wa makamo kama yako, " nilimjibu.

"Sikiliza Gamba, hapa ninapopigia simu ni ofisini, na wala si nyumbani-kitandani kama ambavyo ungalifikiria. Na miye nakuhitaji hapa ofisini mnamo nusu saa bila kuchelewa. Kuna jambo la muhimu na la haraka, hili si ombi ila ni amri, asante sana," alimalizia Chifu.

Nakueleza, hakika kweli, kuna wakati mwingine ninapochukia hii kazi yangu, lakini hata hivyo kwa mtu kama mimi nipendaye visa, nikiwa nasikia kuna jambo kubwa kubwa basi moyo nami huwa unanidundadunda ukiniambia nenda, huenda mara hii kuna visa zaidi.

Della ambaye ndiye msichana niliyekuwa naye hakupenda kuniona naondoka saa kama zile. Akaniambia, "Willy hii ndiyo sababu nakuchukia. Sasa karibu tena uende kwenye masafari yako ya ovyo ovyo, hasa unapoitwa na hilo lijanaume linaloitwa liChifu. Kweli kama mara hii ukikubali kwenda miye naweza kufa."

Nilimjibu Della nikisema, "Wajua kabisa ya kwamba hii ndiyo kazi yangu, ndiyo inayonipa unga, mboga na starehe za kila aina. Nisipofanya hizi safari, itakuwa kama wewe usipoenda ofisini."

Kwa sababu Della ni msichana mwenye hekima alinyamaza na kuelewa nimesema nini. Kumwacha msichana huyu, na asubuhi kama hii amelala kitandani, na miye nikakimbia ofisini, ati kusudi nikapige ripoti kwa Chifu, moyo wangu ulidunda mara nyingi zaidi. Kama ningehesabu wenda mapigo yangefika tisini kwa dakika moja. "Nitarudi mapema baada ya kumaliza shughuli na Chifu," nilimwambia Della.

Nilifungua mlango, nikaangaza nje maana kulikuwa bado giza giza. Macho yalipozoea nikafunga mlango kwa nyuma, nikaenda kwenye gari langu. Nikaingia ndani na kuliwasha gari hilo. Kutoka kwangu ambako ni Upanga, mpaka ofisini kwetu ni mwendo wa dakika kumi. Kwa sababu wakati kama huu hakuna magari mengi nilitegemea kuchukua dakika tano hivi. Ingawaje ni kawaida ya Dar es salaam kuwa na joto jingi, asubuhi hii kulikuwa na baridi sana. Nilitia gari moto, nikashika barabara ya United Nations moja kwa moja mpaka Jangwani kwenye taa za 'traffic.' Nikaona hakuna gari ingawaje zilikuwa haziniruhusu kupita. Lakini nilienda tu. Nikaingia barabara ya Morogoro hadi Independence Avenue.

Nilipoingia Independence Avenue, niliona gari moja inakuja kwa nyuma. Na ilionekana kama kwamba ilikuwa imesimama katika barabara ya Morogoro wakati nikipita, kwa hiyo nikapunguza mwendo, na hiyo pia ikapunguza. Miye nilikuwa sipendi mtu yeyote ajue kuwa nilikuwa nikienda ofisini, saa kama zile. Na kwa nini hilo gari likawa linanifuata? Hiyo ndiyo pia nilikuwa sitaki. Nakwambia, kwa sababu nilishafutwa na magari mengi, mara moja tu naweza kutambua kuwa lile gari linanifuata hata anayenifuata awe mjanja namna gani. Wakati huu nilikuwa nimebakiwa na dakika kumi tu kuripoti kwa Chifu.

Nilikata shauri kurudi mara moja nikaone nani aliyekuwa ananifuata. Basi nilipiga kona na kuanza kurud. Hilo gari lilipoona nimerudi, likatia moto kuja kwa kasi sana. Likanipita na kwenda mwendo wa kama maili mia moja kwa saa. Dereva wa hiyo gari alikuwa amejifunga shuka. Alikuwa amevaa miwani mweusi ya jua. Nikabahatisha kuwa, huyo alikuwa mtu ninayemfahamu, hivyo alivaa ili kusudi nisiweze kumtambua. Gari lake lilikuwa aina ya Datsun 160 SSS lakini alikuwa ametoa sahani ya namba.

Nilikata kona tena nikaendelea na safari yangu mpaka ofisini. Niliendelea mbele kidogo ya ofisi kusudi nione kama hilo gari lilikuwa karibu hapo. Ilionekana huyo jamaa alikata shauri kwenda zake. Nilianza kupanda juu ya jumba ambalo ndimo zilimo ofisi zetu hapo Independence Avenue karibu na jengo la Bima ya Taifa. Ilikuwa tayari saa kumi na moja na nusu. Niligonga kwenye mlango wa ofisi ya karani wa Chifu. Nilisikia sauti ya Maselina ikinikaribisha.

Nilifungua mlango na kuingia ndani. Nilimuhurumia sana Maselina maana naye alionekana mwenye usingizi mwingi. Nilipomuuliza alifika saa ngapi ofisini alinieleza kuwa Chifu alikuwa amempitia nyumbani kwake huko Magomeni Mikumi, yapata saa kumi hivi, wakati yeye alipokuwa amefika kutoka 'Afrikana Hoteli' ambako alikuwa ameenda kustarehe na rafiki zake. Akazidi kunieleza kuwa lazima kulikuwa na jambo kubwa sana kwani Chifu alionekana hana furaha kabisa.

Kweli Maselina alifaa sana kuwa karani wa Chifu, maana alikuwa msichana mwenye bidii sana ya kazi. Hata mimi nilimpenda kwa ajili ya bidii zake na pili alikuwa na umbo la kupendeza. Alizidi kunieleza kuwa Chifu alikuwamo ndani akiningojea. Maselina alimpigia simu Chifu na Chifu akamwambia aniambie niingie. Basi niligonga kwenye mlango ulioandikwa "MKURUGENZI WA UPELELEZI." Nilisikia sauti ya Chifu ikisema, "Ingia ndani Gamba."

Nilipoingia ndani nilimkuta Chifu anavuta mtemba. "kaa chini," aliniambia. Sura yake ilionyesha kama kwamba kulikuwa na jambo ambalo hakulipenda. Alikaa kama dakika kumi hivi akiniangalia tu bila kunieleza neno. Hata miye mwenyewe nilijisikia sina furaha hata chembe. Kisha Chifu alitoa mtemba wake kwenye mdomo, akakung'utia majivu ya tumbaku katika sahani la majivu. Akaanza kutia tumbaku mpya. Halafu akainua macho yake na kuanza kusema,
"sikiliza kwa makini sana tafadhali maana sitaki kuwepo makosa yeyote ambayo yanaweza kuleta hatari. Habari niliyonayo ni muhimu sana, hivyo kwamba, kosa la mtu mmoja tu, linaweza kuleta maangamizi ya Afrika nzima."

"Mnamo usiku wa manane, nimepokea simu nyumbani kwangu ikitoka kwa mkubwa wa Polisi. Mkubwa wa Polisi alinieleza ya kwamba, ofisi moja ya wapigania uhuru imebomolewa. Na kwamba karatasi fulani za siri zimechukuliwa." Alipofika hapo Chifu alionekana hana furaha katika kutaja neno hili 'zimechukuliwa.' Aliendelea kusema, "Na polisi wanafikiri kwamba jambo hili limefanyika kati ya saa nne usiku na saa tano. Askari Polisi aliyekuwa akilinda amekutwa amekufa kwa kupigwa risasi tatu kifuani. Polisi walifika hapo ofisini yapata saa tano kamili, baada ya kupigiwa simu na mtu mmoja aliyeiona hiyo maiti ambayo ilitupwa barabarani. Mtu huyo alikuwa akitoka dansini akielekea nyumbani kupitia mtaa wa Nkurumah.

"Polisi walifika na Dakitari. Daktari alieleza kwamba huyo askari alikuwa amekufa yapata saa moja iliyopita, ambayo ilionekana ilikuwa saa nne. Mkubwa wa wapigania uhuru alifika baada ya kupigiwa simu na akachunguza vitu vilivyopotea. Ilionekana kwamba kila kitu kilikuwemo ila kabati moja la chuma ambamo mlikuwa na karatasi za siri, kufuli la kabati hilo lilifunguliwa kwa kutumia bastola .45. Karatasi hizo zilizochukuliwa ni za maana sana kwamba lazima 'kwa njia nzuri ama mbaya' zipatikane. Maana zisipopatikana, zinaweza kuleta maangamizi kwa wapigania uhuru na kwa nchi huru zote za Afrika."

Alipofika hapa mimi nilisema, "ingefaa unieleze jinsi ninavyohusika katika mambo haya, maana mpaka sasa bado inaonekana hakuna jambo au kiini cha kuweza kuzipata iwapo hawamjui mtu yeyote aliyehusika na mambo haya."

Chifu hakusita kupanua midomo kunieleza, "baada ya kuelezwa yote haya, imeonekana kwamba. Na pia wakuu wa serikali wanafikiri kuwa wizi wa karatasi hizi, Ureno na Afrika ya Kusini ndiyo wako nyuma ya mambo yote haya, pia Indonessia. Lakini watu waliofanya au waliozichukua hizo karatasi ni watu au majambazi wa papa hapa Afrika ya Mashariki. Maana kutokana na wizi wenyewe ulivyotokea, imeonyesha kwamba ni watu wenyeji wa Afrika ya Mashariki tu wanaweza kuendesha wizi huu.

"Mimi sasa ninavyofikiria ni kwamba hizo karatasi zina mambo yote jinsi wapigania uhuru wanavyoweza kufaulu katika mambo yao. Kwa hiyo wakafanya jitihada wazipate, lakini hawakuweza, maana wapelelezi hao wote wamekamatwa kama unavyojua. Hivyo wakaona jambo wanaloweza kufanya ni kuwafuata majambazi katika Afrika Mashariki ambao haja yao kubwa ni pesa. Sasa basi, hao watu wakafuata hao majambazi na kuwambia kuwa watalipwa pesa kiasi kikubwa. Na hapo ninavyofikiriwa. Majambazi wakakubali kufanya hivyo.

"Zaidi ya hayo," aliendelea Chifu, "hao majambazi hawajali kama wapigania uhuru wanashindwa ama wanashinda. Na wala hawaoni hatari za mbele kwa nchi zote za Bara la Afrika. Kweli, hao majambazi ninavyofikiria kuwa ndiyo wamefaulu.

"Sasa hapo ndipo sisi tunaingia katika habari hii. Na sasa sikiliza kwa makini. Wakuu wa Serikali wamekaa na kufikiri usiku huu huu na kuona watupe sisi kazi hii, na ni lazima tufaulu ama sivyo bara zima la Afrika litaumia si Tanzania wala Zambia wala Ethiopia wala Kenya zitakazoumia pekee. Wala si Msumbiji na Rhodessia na Angola peke yake. Kwa hiyo nimekuita wewe na utaondoka leo hii kwenda kwenye tume hii. Ninavyofikiria ni kwamba karatasi hizo hazijatoka katika Afrika Mashariki, maana Polisi katika nchi zote wameishafahamishwa na kuna ulinzi mkuu katika mipaka, viwanja vya ndege na mahali penginepo.

"Hao majambazi wanajua kwamba Serikali itachukua hatua kuzitafuta hizo karatasi kwa njia nzuri ama mbaya watajaribu kuwapa wanaohusika upesi iwezekanavyo. Lakini nadhani hawatazitoa mpaka wamepokea fedha yao. Lakini lazima ujue kuwa makundi ya majambazi yana akili sana wanangojea sisi tuanze kushughulika kusudi wajue kama kweli tunaweza kuwafikiria wao. Watakapoona kuwa tunawashutumu, mara moja na wao, wataanza kupambana nasi, maana hawatakubali kupoteza hiyo fedha. Hapo ndipo maisha yatakuwa magumu maana itakuwa ua au uawa. Na huenda wakasaidiwa na majasusi toka Ureno, Afrika Kusini na Rhodesia.

"Na pia nilifikilia kuwa, hao majambazi watapanga mahali pa kuonana na hao watu ili wabadilishane hivi vitu. Na lazima wapelelezi wa nchi hizi ndiyo watatumwa na Serikali zao kuja kuonana na hao majambazi. Hatari nyingine ni kuwa hao majambazi lazima wawe na majina ya wapelelezi wetu maarufu, na wewe ukiwa nambari moja kwenye orodha hiyo. Sasa ninafikiria kuwa ofisi kuu ya majambazi hao iko Nairobi. Kwa hiyo utaondoka hapa kwenda Nairobi, leo hii saa tatu unusu na ndege ya shirika la ndege la Afrika Mashariki.

"Vyeti vyote vya kusafiria viko tayari. Huenda itakubidi usafili mpaka Afrika Kusini au Ureno au Rhodesia ikiwa lazima. Mambo ya safari katika nchi hizo pia yako tayari. Ukiona ni lazima kusafiri katika nchi hizo usisite. Jina lako tangu sasa ni "Joe Masanja," na kazi yako ni uandishi wa habari juu ya maonyesho ya mavazi. Maana tangu kesho maonyesho ya mavazi yataanza kote ulimwenguni. Upashanaji wote wa habari kati yetu katika kazi hii, utajulikana kama "Kufa na Kupona." Na pia nakupa hiki cheti ambacho kimetolewa na Serikali, kikikuruhusu kuua kama ni lazima. Nakutakia mafanikio mema. Mungu akusaidie ila nakuonya usihusiane sana na mwanamke, na katika hii safari usimwamini mwanamke yeyote."

Chifu alimalizia kunieleza, lakini bado niliona mambo yote hayo ni kama muujiza. Kwani hakukuwa hata na chambo cha kuanzia. Ilikuwa kwamba nitaenda Nairobi bila hata kuwa na fununu ya mtu ambaye anaweza kuhusika habari yote niliona kama ya mwendawazimu. Kweli ilikuwa uendawazimu mtupu. Kisha nikamuomba Chifu kama angaliweza kuniruhusu kuuliza swali, naye akakubali.

Nilimuuliza, "kuna mtu yeyote ambaye anaweza kunisaidia huko Nairobi?"

"Nitapata jina la huyo mtu mnamo saa mbili na nusu asubuhi hii, na kama pia kutakuwa na maelezo yoyote zaidi nitakupa wakati huu."

Nilitoka ofisini kwa mkurugenzi wa upelelezi, na kufungua mlango. Nilimkuta Maselina amelala kwenye meza: Nikamgusa hakaamka. Akaniuliza ilikuwa ni saa ngapi. Nikamweleza ilikuwa saa kumi na mbili unusu. Akaniomba nimweleze kwa kirefu palikuwa na nini. Lakini sikuwa na muda, kwani ilikuwa inanibidi nijitayarishe upesi iwezekanavyo, nipate ondoka saa tatu.

Nilimweleza kwa kifupi tu mambo yalivyokuwa. Maselina akaniambia, "Willy, kweli safari hii mambo ni mengine, na kesi hii inaonekana imejisokota vibaya sana. Lakini naamini unaweza ukaisokotoa na kurudi salama Mungu awe nawe."

Nakwambia kama mtoto huyu angalikuwa anakuaga wewe, walahi usingefanya safari, maana utadhani badala ya kukuombea usalama, anakuombea maafa! Maana hiyo sauti yake ilikuwa mno mbichi mbichi. Nilimwaga Maselina.

Nilitoka nje nikakuta kulikuwa kumeishapambazuka. Nikaingia katika gari langu, huyoo Upanga. Mitaani bado hakukuwa na watu maana kumbuka kuwa hii ni Jumapili. Nilipofika nyumbani kwangu nilimkuta Della bado amelala. Lakini baadae aliponiona tu, jambo la kwanza kuniuliza ni kama nitaondoka. "Naondoka mnamo saa mbili zijazo."

Della alianza kulia, na huyo mtoto anapolia, ndipo anakuwa mzuri kiasi cha ajabu. Utadhani mwelekevu ambaye Shaaban Robert anamzungumza katika kitabu chake cha 'Adili na Nduguze. Kama hujakisoma miye Willy nakuomba ukakisome ndipo utajua Della ni msichana mzuri wa kiasi gani.

Nilimbembeleza Della na kumwambia, "Usijali sana. Safari si mbaya sana, na nitarudi muda si mrefu." Lakini moyoni nilijua hii safari ilikuwa "HATARI TUPU!"

Della aliamka akaanza kutengeneza kahawa, wakati mimi nikifungasha vitu vyangu vya lazima. Muda mchache kijana mmoja alibisha hodi mlangoni. Nilipomuona nikafahamu kuwa alikuwa mfanyakazi ofisini kwetu. Daudi alikuwa ametumwa na Chifu kuniletea kamera moja ya gharama sana, ambayo ningetumia kama mwandishi wa habari na mchukua picha za maonyesho ya mavazi. Pia alibeba bastola mbili zote " automatic .45." Visu sita na vitu vingine ambavyo ningeweza kuvitumia safarini.

Pia alinieleza kuwa Chifu alikuwa amekata shauri niende pamoja na ofisa mwingine wa upelelezi, kwa jina la Sammy Rashidi. Huyu kijana nawambieni nyie kuwa ni mwamba, maana katika kazi yetu hii kila siku ni nambari mbili akinifuata mimi. Na mara nyingi ameponyesha maisha yangu. Alishawahi kushinda mashindano ya kutupa visu katika mashindano ya Jumuia ya Madola. Ukiwa na bastola na Sammy akiwa na visu, jua umekwisha kazi!

Kusikia Sammy anakwenda na mimi, Moyo wangu ulipata furaha kidogo. Daudi alinieleza kuwa Sammy atakwenda akitumia jina la Athumani Hassani. Kazi yake itakuwa msaidizi wangu katika mambo ya kuchukua picha, na yeye ndiye atakayekuwa mchukuaji picha, na kwamba tutaonana naye kiwanja cha ndege cha hapa Dar es Salaam saa tatu.

Sasa ilikuwa saa moja na nusu, Della alikuwa tayari ameweka kahawa, mayai na mkate. Miye nilikuwa nimemaliza kufungasha vitu vyangu. Nilikuwa nangojea tu habari zaidi kutoka kwa Chifu. Tulikaa mezani na Della na kuanza kunywa kahawa. Nilizidi kumbembeleza Della, "Usijali sana juu ya safari yangu. Na kama mola akipenda tutaonana tena."

Ilipofika saa mbili kamili, simu ilisikika. Nikaenda kuijibu, na kama ilivyotegemea, ilikuwa inatoka kwa Chifu. Chifu alisema, "Gamba sikiliza. Nairobi mtaonana na Ofisa mwingine wa Upelelezi aitwaye John Mlunga. Huyu ni kijana tunayemuamini sana. Nadhani mlishawahi kuonana. Yeye aliishafika Nairobi toka Kampala asubuhi hii. Atakungojea saa nne asubuhi katika Hoteli ya Fransae huko Nairobi. Inaonekana yeye anafununu kidogo kuhusu hii habari mpaka wakati huu. Maana anajua mambo mengi sana ya hapo Nairobi baada ya kufanya kazi hapo kwa siku nyingi akipambana na majambazi wa hapo kwa muda mrefu. Sasa tayarisha kila kitu uondoke. Nakuombea safari njema."

Baada ya kupata habari zote hizi kwa Chifu nilionelea sasa niondoke kwenda zangu kwenye kiwanja cha ndege. Ilibidi Della anisindikize mpaka kwenye kiwanja ili apate kurudi na gari. Sikuwa na mzigo mkubwa sana, kwani huwa nina mfuko mmoja wa ngozi ambao nikiufunga unaonekana mdogo sana lakini ndani yake unaweza kubeba hata ngamia! Della alitia gari moto tukaondoka. Niliangalia nyuma kuiangalia nyumba yangu na sehemu ya Upanga kwa makini sana. Sijui ilikuwa mara ya mwisho kuiona ama nitaiona tena, huo ulikuwa ndiyo wasiwasi wangu.

Nilionelea nipite kwanza mtaa wa Nkurumah nikaone hilo jengo lililobomolewa, kwa sababu nilikuwa bado na dakika ishirini za kupoteza kabla sijafika kwenye kiwanja cha ndege. Na mwendo wa kutoka mjini mpaka kiwanja cha ndege. Ikiwa Della anaendesha ni dakik tano, kwani huyu msichana anafahamu kuvuta gari.

Nilipofika kwenye hilo jengo, nilimwacha Della ndani ya gari nikamwambia, "usitoke garini humu ila uwe ukiangalia ikiwa kuna mtu yeyote anayeonekana na wasiwasi wa kuiona hii gari hapa."

Wakati huu watu wengi walikuwa wamekusanyika kwenye hilo jengo, kwa hiyo ilikuwa rahisi sana kuchunguza mambo fulani fulani bila mtu kuwa na wazo lolote juu yako. Polisi walikuwa wanasukumasukuma watu wasikaribie sana, hata mimi nilianza kusukumwa lakini polisi Inspekta mmoja alivyoniona alinichukua na kunionyesha kila kitu. Jambo moja nililofikiria ni kwamba hao watu waliobomoa hili jengo walikuwa wakifahamu kabisa kuwa hizo karatasi za siri zilikuwa kwenye hili kabati la chuma, maana la sivyo, wangalikuwa wamejaribu kupinduapindua na kutafuta tafuta kila mahali. Lakini vitu vyote hata wino katika vidau, haukuwa umemwagika japo tone moja hii inaonyesha kuwa walikuja moja kwa moja bila kugusa kitu kingine chochote, na kupiga kufuli la kabati kwa risasi na kuchukua karatasi na kwenda zao. Pia inaonekana haikuwachukua muda mrefu.

Hili jambo ambalo nimekueleza hapo juu, linanipa wazo. Na kama wewe pia ni mtu mwenye kufikirlia kama miye Willy nadhani tayari umepata wazo ni kwamba hizi karatasi zilikuwa zikifahamika kwa watu wachache sana. Na kama hata zilijulikana kwa wapigania uhuru kuwa zipo, wachache walijua zipo wapi. Kwa hiyo ingawaje hao majambazi walijua zipo, wasingeweza kujua mahali gani zilipo, mpaka wameambiwa na mtu anayejua zaidi juu ya karatasi hizo. La sivyo wangalitafuta kila mahali kabla ya kuzipata. Hivyo tungalikuta vitu vimevurugwa vibaya sana. Kama una kichwa cha kufikiria nadhani umejua nina maana gani.

Baada ya kupata fununu fununu, na kufikiria mambo mawili matatu, niliondoka hapo mahali na kurudi kwenye gari ambamo Della alikuwa akiningojea. Della aliniambia, "Sikumuona mtu yeyote ambaye alionekana kuwa na wasiwasi juu ya gari hii. Ila tu niliona gari moja aina ya Dutsun 1600 SSS, dereva wake alikuwa amevaa shuka na miwani myeusi. Dereva huyo alinitupia macho kidogo tu."

Nadhani hiyo habari ya Della inakupa wazo jingine kwani hilo gari ndilo lililokuwa likinifuata wakati nikienda ofisini kwa Chifu. Della alivuta gari moja kwa moja mpaka kiwanja cha ndege ambako tulimkuta Sammy akiningojea kwa hamu. Nilimwaga Della kwa kumbusu kisha akarudi zake hali machozi yakimtoka.
 
Sura ya Pili
Wasiwasi

Sammy alikuwa ameelezwa kwa kifupi na Chifu juu ya habari yote, hivyo aliomba nimweleze kwa urefu mambo yalivyo. Wakati wote huo hata Sammy, hakuwa akiona dalili yoyote ya kupata mwangaza wa jambo hili. Wote tulionekana vibuda.

Hapo uwanja wa ndege palikuwa na ukaguzi mkali sana. Lakini kwetu siye Chifu alikuwa amefanya mipango yote, kwa hiyo tulipita moja kwa moja mpaka kwenye ndege. Wakati huo nilikuwa bado najaribu kufikiri jambo hili na lile, kama naweza kutoa jambo kamili lakini wapi. Yule mtu mwenye shuka na miwani myeusi alikuwa akija kwenye mawazo yangu kila wakati. Mambo niliyofikiria kwenye lile jengo lililobomolewa pia yalikuwa yakinijia mara kwa mara. Nikamweleza Sammy kila fununu, au jambo lolote nililofikiria linaweza kutusaidia. Sammy naye akanipa mawazo yake.

Ilipofika saa tatu u nusu ndege iliondoka. Tuliiangalia Dar es Salaam kama kwamba hatutaiona tena. Hakuna aliyeamini ataiona tena. Wasafiri wenzetu walionekana kuwa wachovu wote kama sisi tulivyokuwa, kwani kama unavyojua ni Jumapili asubuhi. Mie nadhani ndiye niliyekuwa mchovu kushinda wote. Kwa hiyo nilimwambia Sammy awe macho wakati mimi nikijipumzisha kidogo maana katika kazi yetu hii huwezi kujua ni nani adui na nani rafiki. Wote ni maadui zetu mpaka tutakapohakikisha wenyewe mia kwa mia, ni nani rafiki yako. Na pia nilimweleza kama kukitokea kitu chochote ambacho atakishuku aniambie. Kwani nilijua mchana huo Nairobi kungekuwa na shughuli kubwa sana.

Sammy aliponiamsha niliona kuwa tulikuwa tayari tumefika kwenye kiwanja cha ndenge cha Embakasi. Tulitelemka kwenye ndege. Kisha tulitafuta gari la kukodi twende zetu mjini. Sammy alinunua gazeti la "Sanday Nation" aone kama kuna kitu chochote juu ya tukio hili lakini hakukuwa na lolote, ila mambo mengi juu ya maonyesho ya mavazi na mashindano ya muziki mjini Nairobi. Tulikuwa tumemweleza Chifu asiruhusu hili jambo kuchapishwa mpaka Jumatatu wakati tutakapokuwa tayari tumeanza kazi yetu huko Nairobi.

Tulitazama huko na huko ili tupate gari gani tukodi. Tangu tutoke kwenye ndenge ulikuwa umepita muda wa robo saa na ushee hivi. Nia ya kungojangoja hapo kiwanjani ni kutaka kuona kama kuna watu wowote ambao walikuwa wanategemea kurejea kwetu, kwani siye kushuku kila mtu ndiyo kawaida yetu.

Tulipoona hakuna lolote, tulikodi gari moja la"Archers Tours." Tukamweleza dereva atupeleke mpaka Embassy Hoteli, ambako nduko tulitegemea kulala. Lakini Sammy hakuonelea vizuri wote kukaa katika Hoteli moja kwa hiyo yeye alitaka tumtelemshe Hoteli Pigalle. Tulipanga tuonane mara moja Hoteli Fransae, kusudi tupate kuonana na John Mullunga, kama ilivyopangwa.

Mimi nilishuka Embassy Hoteli, nikaenda katika ofisi yao, ambako nilijiandikisha kama Joe Masanja. Halafu huyo binti ambaye ndiye karani hapo Hotelini akanipa cheti changu, funguo na nambari za chumba. Nikaingia chumbani. Kilikuwa chumba kizuri maana kilikuwa kwenye pembe ya nyumba. Kilikuwa na madirisha mawili. Dirisha moja kwenye upande wa mtaa wa Koinange na moja lilikuwa limezibwazibwa na nyumba zingine. Baada ya kuweka vitu vyangu nilitelemka mara moja kwenda zangu Hotelini Fransae. Nilipopita pale ofisini, nikamweleza mshughulikaji wa simu kuwa kukija simu yangu achukue hiyo habari. Halafu nikampa shilingi ishirini. Akanitazama kwa macho ya kusema asante mara mia. Kwani tarehe ishirini kwenye jiji kama Nairobi, ni mwambo mbaya sana.

Kisha nikaharakisha kwenda zangu Fransae. Nilipofika mlangoni, nilimuona Sammy naye anamaliza kuingia. Nilimuona John amekaa kwenye pembe ya mlango upande wa kushoto kama ukiwa unaingia tu hotelini. Sammy alikuwa hamjui John, kwa hiyo yeye alikuwa bado anaendelea kwenye kaunta ya hoteli. Nilipoingia nilimpigia mluzi akageuka tukamfuata John pale pembeni. Tumewahi kufanya kazi na John huko Kampala, wakati tulipotumwa kuwatafuta waibaji almasi. Na ninakwambia wewe msomaji John kusema kweli si mchezo. Katika kila kesi wanayomweka John hawa watu wa Uganda jua kuna makubwa. John alikuwa amekaa na kijana mwingine mwenye sura ya kupendeza sana. Nafikiri John alimfanya rafiki yake kusudi huyo kijana awe anamtengenezea mpango kwa ndasa, kwani alidhani kuna msichana yeyote ambaye asingesimama kama huyo rafiki wa John akimpigia mluzi.

Tulipofika hapo John alitukaribisha tukae. Kisha akatufahamisha kwa rafiki yake ambaye anaitwa Robin Mwangi, Kikazi akiwa ofisa wa usalama nchini Kenya. Nayo Serikali ya Kenya ilikuwa imemleta Robin kwenye kazi hii. Mimi nilijifahamisha kama Joe Masanja, na Sammy kama Athumani Hassani. Na mikamfahamisha John kwa Sammy kama Fred Kamau. John tayari alikuwa amepata habari zote za kuja kwetu, na jinsi ambavyo Chifu alivyomweleza kama angeweza kumtambua Sammy, kwa kule kuwa na kamera shingoni. Wote tayari tulikuwa tumeshaelezana majina ambayo tutatumia. John alituagizia vinywaji. Aliagizia "Marteli Cognac" toti nane, pamoja na soda kwenye barafu.

Wakati tukinywa, John alitueleza, "Hapa tulipo si mahali pazuri sana kwa kuelezana habari, kwa maana watu wengi huwa wanakuja kuzimua hapa hotelini saa kama hizi, siku za Jumapili. Hata hivyo nitawatolea muhtasari wa habari niliyokwishapata," Alinyamaza, kisha akaanza kusema, "Joe kusema kweli tukio hili linatisha kuzidi matukio yote, kwani inaonekana wote tuko gizani kabisa. Miye nilidhani nitapata jambo lolote la maana lakini wapi. Robin nilimweleza mnamo saa moja aweke vijana wake mahali fulani kusudi huenda wakaweza kutupatia maelezo yoyote ama kama wanaweza kupata fununu yoyote. Lakini ajabu ni kwamba vijana wanne wameisha uawa katika muda huu wa saa mbili. Hii inaonyesha tutakuwa na muda mgumu sana, tena sana.

"Mmoja alikuwa amepigwa risasi huko Embakasi. Mwingine ametiwa kisu huko "Uhuru Park". Wengine wawili walikutwa wameuawa huko Lavington Green kwa risasi. Sasa hata hatuwezi kuunganisha vifo hivi, ila tu kwamba watu hawa wako kila mahali. Na linaonekana kuwa kundi kubwa sana. Lakini jambo kubwa ni kwamba lazima tufanye kichwa cha tukio hilo.

"Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa kwenu amenieleza kwa simu anavofikiria. Nami ninakubaliana naye, kwani huyu mzee akibashiri kitu, naamini ni hivyo. Kwa hiyo sisi itatubidi tuendelee kama alivyofikiri, la sivyo tumekwisha".

Bado mimi nilikuwa sijaweza kuunganisha jambo lolote. Ilikuwa bado ajabu. Ajabu kubwa. Hapo nilimwuliza John, "Unafikiri, sasa tutaanzia wapi?"

"Mimi nafikiri tutaonana usiku huko Starlight Klabu maana, yule kijana aliyekutwa Uhuru Park, alikuwa sehemu hizo. Na miye nilipochunguza sana ilionekana kama kwamba huyu mtu aliuawa katika nyumba fulani halafu akatupwa Uhuru Park. Kama unavyojua leo ni Jumapili watu wengi walikuwa bado wamelala.

Baada ya kukaguakagua afisa mmoja wa polisi alisema aliona tone la damu kwenye mlango wa Klabu hiyo. Nikaonelea vizuri nimwambie Mkurugenzi wa Usalama wa hapa amueleze Mkuu wa Polisi. Niliwataka wasiulize jambo lolote, au wasiulize maswali yoyote juu ya vifo hivyo mpaka baadaye. Kwa hiyo sasa tutatawanyika halafu tutaonana usiku huko Klabu. Wakati huu Robin na mimi tutaendelea kukusanya habari chache chache toka kwa maafisa wake. Nendeni mkapumzike.

Tuliagana na Robin akanieleza, "Kama ukitaka msaada wowote wa watu waweza kupiga ripoti ofisini kwetu, Chifu huko Dar es Salaam tayari amefanya kila mpango na wakubwa wa usalama katika nchi zote tatu za Afrika ya Mashariki."

Tulikubaliana kuwa wote tutaonana Starlight Klabu mnamo saa tatu usiku. Sammy alienda hotelini kwake, nami nikarudi hotelini kwangu kupumzika kidogo.

Nilipoingia hotelini kwangu nikaenda mpaka kwa mshughulikaji na simu kumwuliza kama amepata simu yoyote. Naye akasema kwamba alikuwa bado hajapata. Nilienda moja kwa moja kitandani kwangu nikalale.

Nilipoamka ilikuwa saa kumi na mbili za jioni. Nilioga na kunyoa ndevu. Halafu nikajitayarisha kwa kila njia ili niweze kuonekana kama mwandishi kweli kweli. Halafu nikaagiza chakula. Sikula chakula kizito sababu hali yangu haikuwa nzuri sana. Baada ya kula nilimpigia simu Sammy anipitie mnamo saa mbili na nusu.

Ilipofika saa mbili na nusu Sammy alinikuta baa ya Fransae. Tukafunga safari kwenda Starlight. Mimi nilitaka tuchukue taxi, lakini Sammy alikataa, kwa kusema, "Twende kwa mguu, maana tunaweza tukapata jambo la kufurahisha. Pia ni lazima uchukue bastola yako, maana kunaweza kuwa na mambo ya hatari."

Nilirudi chumbani kwangu, nikaweka bastola yangu ndani ya mkoba wake wa begani. Nikaweka koti langu juu nikafunga tai sababu mwezi wa saba, ni baridi sana Nairobi. Ningekuwa sehemu za Dar es salaam, wakati huo ningekuwa ninavaa furana. Kweli nilipojiona kwenye kioo nilionekana mwungwana. Na ninakwambia ninapokuwa nimevaa koti, huwezi kujua kuwa hata siku moja nimewahi kugusa bunduki. Nilirudi huko, baa kumpitia Sammy ili twende zetu.

Tulienda na mtaa wa Koinange, halafu tulipofika New Avenue Hoteli, tukashika Kenyatta Avenue. Tuliendelea na Kenyatta Avenue mpaka tuliposhika Uhuru Highway, tulikoingia katika kijinjia kinachopitia Uhuru Park. Tuliangaza huku na huko katika Uhuru Park lakini ilionekana hapakuwa na watu. Nadhani watu walikuwa wameishasikia kifo cha huyo kijana. Pia tulitegemea kuwa kama watu hao wamekuwa wakifuata myenendo yetu, huenda wakawa wanatufuata. Hivyo Sammy akawa tayari tayari na visu vyake ikiwa kutatokea matata. Lakini hatukupata jambo lolote.

Tulipoachana na Uhuru Park, tulishika Kirk Road. Tukaenda zetu moja kwa moja mpaka Starlight. Nje ya Klabu hiyo tulikuta watu wengi wakikata tikiti. Wanawake walikuwa wengi sana hapo nje, na walionekana wakitafuta wanaume wa kuwaingiza ndani. Lakini sisi tulikata shauri tusiwajali maana wangeweza kuingilia kazi yetu. Nilienda nikakata tikiti halafu tukaingia ndani.

Hii Starlight Klabu inapendeza mno maana hali ya hewa ya humo ndani ni tulivu kabisa. Kila mtu alionekana ni Mwungwana. Watu wengi walikuwa wameishaingia. Wengi wao walikuwa wawili wawili, yaani" Kitu Mtu." Nadhani unanielewa ninaposema hivyo. Tulienda tukakaa kwenye pembe moja ya kulia karibu na mlango mkubwa wa kuingilia. John alikuwa bado hajafika. Tulishangaa sana, lakini tulijua tu ya kwamba atafika muda si mrefu. Punde si punde Robin alifika. Na mara alipotuona akatufuata.

Robin aliuliza, "Fred yuko wapi?"

"Hata siye bado hatujamuona. Tulidhani mngefika wote hapa, "alijibu.

"Hata, aliniambia kuwa yeye atakuwa hapa mnamo saa mbili u nusu, kama ni hivyo basi huenda yuko kwenye ile baa ya nje, au amepata habari fulani ambayo anaishughulikia."

Kisha Robin aliondoka akaenda kwenye baa ya nje kuchunguza kama Fred yuko huko. Aliporudi alitueleza kwamba Fred hakuweko. Sammy aliagiza vinywaji. Muziki nao ulianza kupigwa na vijana wa Fiesta Matata ambao hupiga muziki taratibu kabisa. Wakati huo wote tulikuwa tukimngojea Fred lakini hakuonekana. Tulianza kupatwa na wasiwasi mwingi sana. "Kwani Fred anaishi wapi?" Sammy alimwuliza Robin.

"Anaishi Princess Hoteli."

"Afadhali nikampigie simu huenda anaumwa," nilisema

"Sammy uwe unaangalia kama yuko mtu mwenye shauku na mimi nipigapo simu."

Nilipopiga simu hotelini kwa Fred ilionekana hayuko kwani kengele iliendelea kulia kwa muda mrefu sana. Nilikata simu na kurudi pale kwa akina Sammy. Niliporudi Sammy alinieleza, "Ulipokuwa ukienda msichana mmoja ambaye alikuwa amevaa mini alikuwa akikuangalia kwa jicho la pembeni pembeni. Msichana huyo alikuwa akicheza dansi na kijana fulani. Halafu alipokuona ukienda kwenye simu alisogea mpaka kwenye kiti cha karibu na simu, kisha akajifanya kuwa anasoma gazeti. Na baadaye msichana huyo akapotea mumu humu mwenye watu."

Hilo jambo niliona huenda ni hatua moja wapo. Lakini hatua hii ilikuwa bado haina uhusiano wowote na tukio letu. huenda ni kwa sababu ameona ajabu kwa nini tulipiga simu, na kwamba tulikuwa tumekaa tu bila wanawake na hali tunaonekana vijana nadhifu mno.

"Habari zenu," sauti nyororo ilitoka kwa nyuma yetu. Kila mtu kati yetu alipatwa na kigugumizi cha kujibu, kwani wote tulipotupa macho nyuma yetu, tulimwona msichana mzuri mmno!

Nakwambia maishani mwangu nimeona wasichana, lakini ilivyo ni kuwa huyu msichana alishinda. Nilisikia nywele zikinisimama nilipomwangalia tena. Nilijikaza kisabuni nikamjibu, "Siye wazima tu, vipi wewe?"

"Miye salama tu. Nilidhani kuwa huenda nyiye ni wageni hapa. Na kwamba huenda mlipofika hapa mlifanya mpango na wasichana fulani fulani mwonane nao, lakini hawajaonekana, si hivyo?"

"Kidogo huenda uko sawa, lakini si sana,"nilimjibu.

"Mbona unaonekana mwenye wasiwasi basi? Nilidhani kwamba ulienda kupiga simu kwa madhumuni ya hao wasichana." Akanyamaza hali akinitazama machoni.

Kweli mimi nakwambia sitaki wasichana wanaonitazama machoni. Kwa hivyo msichana huyu mara moja alinitisha. Macho yake yalionekana kusinziasinzia, lakini yanaweza kukusoma moyoni mwako.

"Nilikuwa napiga simu kwa rafiki yangu mmoja ambaye ni mwandishi juu ya mambo ya muziki. Yeye tulimwacha Acadia Klabu. Nilitaka kumweleza aje huku kwani, muziki wa hapa unaonyesha umeshinda. Lakini inaonekana kuwa muziki wa huko umewaingia sana hata hawasikii mlio wa simu," niliongopa.

Alitabasamu. Tabasamu hilo lilifanya nywele zangu zisimame tena.

"Kweli nimeupenda muziki wa hapa," alisema msichana huyo. "Hata mimi huwa napenda bendi hii hii, na mahali papa hapa."

"Jina lako nani, "aliulizwa na Sammy.

"Mimi naitwa Lulu. Lulu Jack, kazi yangu ni kuonyesha mavazi. Nimetoka Kampala kuja kwenye maonyesho ya mavazi hapa Nairobi ambayo yatachukua kama wiki mbili hivi." Alinyamaza kwa muda wa kupisha mate yapite kooni. Kisha akauliza," Na nyiye ni akina nani?"

"Miye ni Athumani Hassani, na huyu," alisema Sammy akionyesha kidole kwangu," ni Joe Masanja. Na huyo ni Robin Mwangi. Kazi yetu sisi ni uandishi wa habari juu ya maonyesho ya mavazi. Hata sisi tumeletwa na yaya haya maonyesho ya mavazi. Hivyo inaonyesha tutaonana mara nyingi toka sasa. Naamini nitakuwa mtu mwenye furaha sana nitakapokuwa nakuchukua picha. Maana mimi ndiye mchukuaji picha katika kundi letu hili."

"Nitafurahi sana kuzidi kuonana na nyinyi kwani mnaonekana kuwa watu waungwana sana. je, mnatoka wapi?" Aliuliza.

"Siye tunatoka mjini Mwanza, Tanzania," alijibu Sammy. Kisha Lulu alituaga akaondoka kwenda kucheza dansi. Mimi huwa siwaamini wasichana wazuri kama hawa. Nakumbuka siku moja mama yangu, Mama-Willy, alinieleza kuwa kati ya wanawake wote, ukiona mwanamke mzuri sana jua mwanamke kama huyo ni hatari sana. Na nilipoanza kazi kila siku ninapotumwa kwenye shughuli fulani jambo la kwanza la Chifu ni kunisihi nisifuate wanawake wazuri sana. Maana wanawake kama hao ni sumu kali sana. Lakini mimi Willy, ingawaje nakubaliana na Mama Willy pamoja na Chifu, nimekuja kutambua kutokana na kazi zangu kuwa, kutokana na mwanamke mzuri sana unaweza kupata habari za ajabu sana. Nilikata shauri kuwa sitamwachia Lulu vivi hivi lazima nitafute mengi ya maisha yake.

Huyo mtoto Lulu ni Lulu kweli kweli. Kwani toka kwenye dole gumba mpaka utosini hana dosari yoyote. Ukimwona hutaamini kuwa alizaliwa na mwanadamu ila labda mtoto wa jini, kama unaamini kuwa kuna majini, ama amefyatuliwa kutoka katika mashine baada ya kuchongwa na mchongaji nambari moja hapa ulimwenguni. Nakwambia kama Lulu ataacha wazi sehemu ya kifua chake halafu umtazame, utababaika. Hutaweza kumwangalia mwanamke mwingine yeyote. Utawahesabu wanawake wengine kama wanaume tu. Kama Mungu amewahi kupendelea, basi huyu Lulu amempendelea hasa.

"Sammy," niliita, "angalia kila mtu anayehusiana na Lulu katika hii klabu. Nawe Robin pata watu wa kumfuatia Lulu ili tupate kujua anakaa wapi." Nilinyamaza kidogo kisha nikaendelea, "Mimi itanibidi niende kule hotelini kwa Fred nikajue kuna nini, maana mpaka sasa yapata saa nne na nusu na bado hajaonekana. Ninawaacheni wote hapa ili kuangalia mambo ya hapa klabu. Lakini Sammy unipigie simu kama ukiona nimechukua muda mrefu, zaidi ya dakika arobaini na tano. Na upige kule kule chumbani kwa John. Kwaherini." Nikaondoka.

Nilikodisha gari nje na kwenda moja kwa moja mpaka Ambassador Hoteli. Sikutaka anitelemshe hapo Princess Hoteli. Niliposhuka hapo, ilinibidi nichukue Government Road nionekane kama kwamba nataka kuchukua 'bus' kwenye kituo cha 'mabus' cha Ambassador. Nilikwenda nikazungukia mtaa wa Duke, halafu nikaingia katika mtaa wa Tom Mboya.

Nilipoingia Princess nikakuta watu wengi sana katika baa. Nikajifanya kama miye pia mpangaji wa hapo lakini nilitazama huku na huko hapo hotelini ili nione kama kuna mtu ananichunguza. Lakini watu wote walionekana wakishughulika na unywaji wa pombe na kadhalika. Nilipanda ngazi mpaka ghorofa ya kwanza, Robin alikuwa amenipa nambari za chumba ambamo John alikuwa akilala. Nilikwenda mpaka kwenye hicho chumba. Kabla sijagonga nilikagua vyumba viwili vilivyokuwa upande wa kuume na kushoto wa hicho chumba. Lakini sikuona wa kusikia chochote. Ilionekana hivyo vyumba havikuwa na watu, au wote walikuwa wamekwenda kutembea.

Niligonga kwenye mlango wa John lakini sikusikia lolote. Nikafikiria kutoka, lakini nikaona afadhali niingie ndani pengine nitaweza kupata habari zozote. Ama huenda akawa ameacha habari fulani fulani. Nilichukua funguo zangu malaya ili nifungue mlango kwani ulikuwa umefungwa.

Nakwambia sijawahi kushituka kama nilivyoshitushwa na hali niliyoikuta humo chumbani nilipowasha taa. Hofu iliniingia, nikaanza kugwaya. John alikuwa amelala kifudifudi. Amekufa! Fahamu zilinitoka kwa muda wa dakika tano hivi. Baada ya kuzinduka nikaenda karibu na maiti ya John ili niichunguze vizuri. Niliona kuwa alikuwa amepigwa risasi sita, zote kifuani.

Ilionekana kuwa huyo aliyempiga hizo risasi, bastola yake ilikuwa .45. Kwani miye nimewahi kuona matundu ya risasi hizi. Haya mauaji yalikuwa ya kutisha sana. Yalikuwa mauaji ya kikatili sana, maana aliyemwua alimwachia risasi nyingi kana kwamba alimwua ng'ombe. Na ilionekana kwamba waliingia kwa ghafla, kiasi ambacho hata John hakuweza kujitetea.

Kifo hicho cha John kiliniuma sana hata nikaapa kuwa huyo aliyemwua, lazima nimkamate na kumwua mimi mwenyewe, kama nitakuwa mzima wakati wote wa madhila kama hayo. Woga ulianza kuniingia kwa mara ya kwanza.Tangu nianze kazi hii sijapatwa na woga kama huo. Kitu kilichofanya nitishike sana ni jinsi wauaji hao walivyomfahamu John. Na kama ni hivyo, basi hata sisi tutakuwa tumeisha fahamika. Na kama wameweza kumwua John ambaye ni mpelelezi mashuhuri katika Afrika ya Mashariki, lazima watu hawa wawe miamba kweli. Na lazima wawe ni wenye akili nyingi sana juu ya kuwinda watu.

Kweli tulikuwa tunanuka vifo siye sote. Hazijapita hata saa ishirini na nne, watu watano tayari wameishakufa! Hata kama ungekuwa na moyo mgumu kama wa Farao, hata wewe ungeweza kutishika.

Nilikata shauri, kuufunga mlango na kuiacha hiyo maiti halafu niende kuwapigia simu polisi. Lakini kabla sijatoka niliona heri nipekuepekue mifuko ya John ili huenda nikapata kitu chochote kilichofanya hata wamfuate. Na kama unafikiri sana unaweza kuona kuwa lazima John, wakati sisi tunashangaashangaa yeye alikuwa amegundua jambo fulani ambalo ndilo lililosababisha kifo chake. Kisha nilienda mpaka kitandani ambako kulikuwa na mkoba. Nilipoinama tu,nikasiki sauti ikiniambia,"Tafadhali kaa ulivyo wala usisogee hata inchi moja. La sivyo utapata idadi ya risasi zile zile zilizomwingia huyo mshenzi karibu nawe hapo."
Nikaduwaa....!
 
Ikifika mwisho nitag, maana nyinyi waandishi wa riwaya munazingua.kuna yule alietupia riwaya ya mtutu wa bunduki,kala kona hadi leo unaingia mwaka wa pili hajaweka muendekezo.hayo ni matangazo ya vijarida vyenu
 
Sura ya Tatu
Nilijiona siwezi kufanya lolote. Na kama kweli ningefanya upuzi hapo, nilijua hata mimi ningeyala marisasi. Kwa hiyo nilionelea ninyamaze tu mpaka hapo nitakapopatiwa yangu. Jinsi huyu mtu alivyoingia hata sifahamu maana aliingia kama mchawi bila hata kishindo. Zaidi nilikuwa nataka nimwone ni nani, lakini niliona kwamba ningegeuka uso tu, ningekwisha kazi. Nilijua hata mimi huo ndio mwisho wangu. Mara nyingi huwa katika hatari kama hizi, lakini kwa mwujiza wa Mungu hutokea nikaponyoka. Mara hii mambo yalionekana kuwa tofauti kwani watu hao hawakuweza kufanya kosa hata moja.

"Wewe ni nani, na unafanya nini hapa?" Niliulizwa.

"Mimi naitwa Joe Masanja, na nimekuja hapa kumtazama huyu Fred Kamau ambaye ni mwandishi mwenzangu. Sote tunaandika habari juu ya maonyesho ya mavazi ambayo yameanza hapa. Na nimestaajabu sana kumkuta ameuawa." Nilinyamaza kisha nikasema kwa upole mwingi, "Lakini mbona unanijia kijeshi namna hii, kama kwamba miye nimefanya jambo lolote? Ninashangaa kujiona nimeshikiliwa bunduki mgongoni. Ninaweza kuzimia hivi. Na wewe ni nani? Niliuliza.

"Nyamaza," alijibu "sina muda wa kujibu maswali yako, nimo kazini. Ila nataka kujua uliingiaje humu! Mlango ulikuwa umefungwa. Na kwa nini baada ya kuingia humu ukaonekana kuchunguzachunguza vyumba vilivyo karibu na hiki, kama kwamba ulikuwa ukijua kwamba ulikuwa unafuatwa?"

"Nilifungua mlango kwa kutumia ufunguo niliopewa na huyu rafiki yangu Fred, maana alikuwa na funguo mbili. Nilikuwa nimesahau nambari ya chumba ndiyo sababu ilinibidi nithibitishe ni kipi kati ya hivi vitatu,"nilimjibu. Wakati huo zilikuwa zimepita dakika arobaini na saba, na simu ilikuwa bado haijalia. Hivyo nilizidi kukabiliwa na wasiwasi.

"Wewe ni mwongo - mwongo nambari moja. Hii inaonyesha unafahamu mambo mengi kuliko hivyo unavyotaka kusema. Huyu si Fred ila ni afisa wa upelelezi aitwaye John Mullunga," alijibu kwa sauti ya hasira. "Na siye tulikuwa tunajua kwamba atakuja mtu wa aina yake kuangalia. Na wewe lazima ni mmoja wao, ila tu unajidai ni mwandishi. Hivyo lazima na wewe ufe kusudi tuweze kuendelea na mipango yetu."

"Hayo ni maneno yako wala si yangu. Na hata kama ukiniua, siku moja nawe utakamatwa. Miye sikuwa nikijua kuwa huyo ndiye John Mullunga. Na wewe tu ndiye umeniambia maneno haya. Na kama huyu kweli ndiye John Mullunga ambaye nimesikia habari zake, na nyiye mmemwua, basi serikali ikifahamu, itawawinda mpaka watawatia vitanzi." Nilimueleza.

Wakati wote huu nilikuwa nasema kusudi dakika zizidi kwenda ili pengine baadaye nipate mkombozi. Alianza tena kunitisha, "Maiti huwa hazielezi habari. Sitakusikiliza kwa maana wewe ni maiti tayari." Alianza kucheka kisha akaniambia,"Toa sala zako za mwisho. Na kama wewe pia ni afisa wa upelelezi, serikali itatukoma, maana hizi serikali bado hazitutambui. Na 'bosi' wangu nadhani atafurahi sana kusikia John amekufa na kijishenzi kingine."

Wakati huu wote nilikuwa nafikiri namna ya kuweza kujiponyesha. Lakini niliona hakuna. Bastola yangu nilikuwa nayo kwapani lakini nilijua nikijitingisha kidogo tu nitaingia kuzimu! Kwa hasira na uchungu nikasema, "Niue basi sasa unafanya nini? Unapoteza muda wako."

"Fumba macho, usali kwa dini yako, ama vyovyote."

"Naomba nipige magoti basi." nilisema.

Alicheka akasema, "Lo! Nadhani polisi watakaokuja humu watapata tishio, kwani watakukuta wewe umekula risasi sita hali umepiga magoti kitandani unasali. Halafu wataona rafiki yako amelala kifudifudi hapo chini, akiwa kama anaomba msamaha. Naye pia amekula risasi zipatazo sita." Sauti ya huyu mtu ilinionyesha kuwa ni mwuaji, na ni mtu ambaye anafurahia kuua. Pia alionyesha kuwa mtu katili na jambazi.

Nilikuwa wakati wote huu nikifikiria njia ya kujiokoa. Na kule kuomba nipige magoti, ni jaribu la kwanza kama huyo mtu akikubali tu nimtengeneze mara moja. Nikajifanya kuwa nilikuwa natetemeka ovyo. Bastola yake ilikuwa nusu inchi kutoka kwenye mgongo wangu. Nikabaki katika kufikiria jinsi ya kuirusha. Nilijua kuwa mtu huyo alikuwa mwuaji na hatanihurumia.

Mama-Willy alinishauri siku moja kwa kusema. "Mwanangu kama umo hatarini, usife kama kondoo, kufa kama mwanaume ambaye wakati wa kuzaliwa mama yake alishikwa na uchungu wa ajabu."

Tangu siku hiyo sikukubali kufa kikondoo. Basi niliposogea kwenye kitanda, hili jambazi lilipitisha mkono kwenye koti langu. Likatafutatafuta na kukuta bastola yangu ambayo aliichukua. Halafu likacheka. "Yee, eti wewe ni mwandishi. Mwandishi gani anatembea na bastola, automatic '45' katika Afrika ya Mashariki? Mawili, wewe ni jambazi ama afisa wa upelelezi."

Wakati huo akizungumza nilijua nimeishapatikana. Nukta yoyote ningeweza kula risasi. Na kicheko alichocheka kilikuwa cha hasira. Nilisikia akiitupa bastola yangu upande mwingine wa chumba. "Upesi piga magoti. Huwezi kunidanganya mimi ati ni mwandishi. Ingekuwa Marekani ningelikubali, lakini Afrika ya Mashariki usinitanie."

Wakati ninapiga magoti na huku najifanya kama kwamba natetemeka, nilitupa shoto langu kama umeme. Kufumba na kufumbua, bastola ya hilo jambazi iliruka na kwenda kwenye pembe moja ya chumba. Hapo hapo nikamgeukia. Akanitupia ngumi moja, nikaikwepa. Nikatupa shoto langu tena likampata kwenye taya mpaka chini. Ilivyo ni kwamba shoto langu likikupata, ukiwa dhaifu hutaamka tena hadi siku Yesu atakapokuja kwa mara ya pili!

Niliruka mpaka alipo, lakini akanipiga kwa mguu tumboni. Nikaenda kuangukia kitanda! Wakati huo alikuwa ameisha simama. Akanijia wakati nikijaribu kusimama. Akanitia ngumi shingoni na kujikuta niko chini! Halafu akanitia teke la usoni na kuikimbilia hiyo bastola. Kabla hajafika niliruka kama swala na kumchukua 'judo' mpaka kitandani. Katika maisha yangu ya miaka sita katika kazi hii sijaonana na mtu kama huyu. Kweli siku hii, lo, maisha yaliniwia magumu.

Kabla hajasimama nikamtia ngumi nyingine kwa mkono wangu wa kulia. Na hapo nikaona amedhoofika. nikaondoka kukimbilia bastola. Kabla sijafika nilipata teke la mgongoni na kunifanya nipepesuke. Kabla hajashika hiyo bastola nilimpa tena shoto langu mpaka akaanguka chini. Nilimfuata hapo chini na kumtia teke la tumboni, na jingine ubavuni. Maana majitu kama haya, ukijigamba kuyapiga kichwani tu utacheka. Yanavyo vichwa vigumu kama paka.

Alipodhoofika kabisa niliiendea bastola. Kurudi nikakuta amezimia. Ilikuwa yapata saa tano na robo za usiku sasa. Niliendea chupa ya "whisky" iliyokuwa humu chumbani na kuanza kummwagia na kumnywesha kidogo kidogo. Kisha akaanza kuzindukana. Hapo nikashikilia bastola yangu kwenye taya lake.

"Niambie wewe ni nani, la sivyo utameza risasi zote hizi zilizomo katika hii bastola," nilimwambia.

"Yeeeh, sitaweza kusema hata ufanye nini na afadhali uniue tu," alijibu.

"Sasa kama hutaki kusema jina lako huyu uliyemuita 'bosi' wako ni nani?"

Hakujibu alinyamaza tu. Nikaona nisipokuwa katili hapo sitaweza kupata fununu yoyote. Niliwasha kiberiti changu. "Usiponieleza jina lako nitakuchoma masikio yako ingawa unaonekana kuwa hujali."

Basi nilisogeza moto kwenye sikio lake nikaanza kumchoma. Kwanza alijifanya hajali ingawaje alionyesha kuhisi uchungu wa ajabu. Hii ilinionyesha kuwa yeyote yule ambaye anaitwa 'bosi' wa watu hawa lazima anajua kuchagua watu wake. Kwani kweli ni wanaume. Ni watu wachache sana wanaoweza kuvumilia moto. Lakini maumivu yalipozidi alianza kuguna halafu akaanza kulia.

Mwishowe alisema, "Acha, niachie, nihurumie. Ngoja nitakwambia, hebu niache."

Nilitoa moto penye sikio lake kumpa nafasi aseme.

"Mimi naitwa

Kabla hajasema jina lake alipigwa risasi toka dirishani. Akafa! Niligeuka kutazama aliyemwua, lakini sikuona mtu. Na wala sauti ya bastola au bunduki iliyomwua sikuisikia. Hii ilionyesha kuwa bastola zao zote zina viwambo vya kunyamazisha sauti, ambavyo huitwa "sailensa."

Kupigwa risasi kwa mtu huyo kulinipa wasiwasi zaidi. Moyo ulipiga mara nyingi mno. Chuki ilinijia maana hawa watu wanaonekana kuwa wameipanga mipango yao kiasi cha kwamba wanahakikisha hawafanyi makosa, hata chembe ya kosa. Nilikata shauri nitoke hapo mahali. Niliangalia zile maiti kwa mara ya mwisho. Nikaamua kwenda kuuchunguza ule mfuko wa John kabla sijaondoka. Lakini kabla sijafika kwenye huo mfuko, nilisikia sauti ikisema, "Simama hapo hapo ulipo, na usijitingishe."

Moyo uliniuma na hofu ilinizidi kwani niliona mara hii hawatafanya makosa kama mara ile.

"Angusha chini bastola yako," mtu huyo nisiyemtambua alisema kwa sauti ya hasira.

"Geuka unitazame."

Niligeuka upande wake na huku nimeinua mikono juu. Huyo mtu alionekana katili zaidi ya yule mwingine. Alikuwa kijana mwenye sura mbaya mbaya. Mweusi na mwenye umri upatao miaka ishirini na minane. Kwa umri tulikuwa tukilingana.

Mimi pia nilikuwa nina umri wa miaka ishirini na minane. Na kuadhimisha sikukuu yangu ya kuzaliwa ilikuwa wiki moja toka siku hiyo. Nilimwacha Della akialika watu kwenye hiyo sikukuu yangu. Lakini huenda badala ya kuadhimisha sikukuu yangu ya kuzaliwa, watakuwa wakiadhimisha matanga yangu, siku hiyo. Maana sasa kila dakika ilinuka kifo kitupu.

"Mara hii hatutafanya makosa. Huyo mshenzi waahedi hapo chini, alifanya makosa na ndiyo sababu na yeye amepata zawadi yake. Wewe ni nani? Maana unaonekana kuwa tisho kwetu zaidi ya wengine wote. Hakuna aliyewahi kupambana na Kasha akabaki mzima. Hebu nipe maelezo kwa kifupi. Maana utake usitake utakufa tu. Huwa sifanyi makosa mimi."

Nilipomtazama alionekana kuwa mtu ambaye hawezi kufanya makosa. Niliomba Mungu kimoyomoyo na kuanza kutubu makosa yangu.

"Mimi naitwa Joe Masanja. Na ni mwandishi wa habari juu ya 'Maonyesho ya Mavazi," Nimetoka Mwanza. Tanzania," nilisema.

"Pumbavu wee, unadhani unaweza kunidanganya mimi, mwandishi hawezi kuwa jasiri kama wewe hata kuweza kumshinda nguvu Kasha," alisema, kisha akanipiga kofi moja mpaka nikaona jua, ingawaje ilikuwa usiku. Fahamu zikaniruka kwa muda. Ziliporudi nilikuta bado ameshikilia bastola yake na kuniuliza tena mimi nilikuwa nani. Nilimjibu vile vile, "Oke, oke, mimi sitajali kama kesho nitakuona ukila chakula cha mchwa," alisema kwa kiburi sana.

Nilifumba macho maana niliona ndio mwisho wa maisha yangu. Hapo sikuwa na ujanja wowote . Kwani huyu kijana anavyoshikilia bastola, afadhali naye yule, mchezaji wa sinema wa kule Mexico, "Cowboy Cuchilo."

Wakati nilipoona anakaza mkono wake kuachia risasi, kufumba na kufumbua nilishtukia anaanguka chini. Alikuwa amepigwa risasi! Taratibu akakata roho! Niliruka mara moja kuchukua bastola yangu tayari kwa matata mengine yoyote. Mlango ulipofunguliwa nilikuta ni Sammy.

Kwa mara nyingine tena Sammy alikuwa ameponyesha maisha yangu, la sivyo dakika hii ningekuwa mfu.

"Willy - naona walikuwa wamekusakama sana. Sasa, tukimbie tutoke hapa ili ukanieleze jinsi mambo yalivyokuwa, alininong'oneza Sammy.

Kulikuwa na maiti tatu hapo chumbani sasa. Kabla sijatoka hapo chumbani nilienda kwenye mkoba na kuanza kukagua kagua. Nikaona hamna la kutusaidia. Tulipitia dirishani na kutelemkia kwenye ukuta na kutokea kwenye kijinjia.
Tulikimbia toka hapo mpaka River Road.

"Nilipiga simu baada ya dakika arobaini na tano kama ulivyosema," alisema Sammy," Simu ilionekana kuwa ilikuwa imekatwa, kwa hiyo tukaanza kuingiwa na wasiwasi. Ikabidi tungojee kwa muda wa dakika ishirini tena. Nilipotoka tu baada ya dakika kama tano hivi Lulu naye hakuonekana tena. Pia vijana fulani watatu waliokuwa wakienda lakini tukaona mambo yasingekuwa mazuri sana kwako. Maana usingalijua tumekwenda wapi. Baada ya kungoja kwa dakika ishirini tena, mimi na Robin tulianza kuwa na wasiwasi. Kwa hiyo mimi nikakata shauri nikufuate na kumwacha Robin humo Klabuni kuzidi kuchunguza.

Nilichukua taxi hapo nje mpaka nyuma ya Hilton Hoteli na kuanza kutembea kwa mguu mpaka hapa hotelini. Ndani ya bar watu walionekana kushughulika na ulevi. Kwa hiyo mimi nilienda kwenye kaunta na kuagiza 'bia' moja. Nilianza kumwangalia kila mtu kwa usiri sana. Mwishowe ndipo nikamwona mtu akipenya kwa haraka kati ya mlango mmoja unaotokea nje kwenda mwenye vyumba vya kulala. Huo mlango umeandikwa "HAKUNA KUPITA HAPA."

Nilipoona hivyo nilitoka kwenye 'kaunta' kwa siri na kuingia katika vyumba vya huko juu. Halafu nikangoja. Kwanza mtu huyo aliingia katika chumba cha mkono wa kulia. Baada ya kukaa kidogo alitoka na kuingia humu. Wakati wote huu miye nilikuwa nashindwa kutoka, kwani kulikuwa na wafanyakazi wa humu hotelini wakifanya kazi.

Alipotoka ndipo nikakimbia na kuingia katika chumba cha upande wa kulia. Baada ya kuchungua sana niliona hakikuwemo chochote humo. Ila ukutani katika pembe moja kuna matundu matatu. Haya matundu yanatosha kuingiza mdomo wa bastola. Na ninadhani ndimo huyu mtu wa pili alimomwulia mtu wa kwanza. Na kwa kutumia tundu hilo hilo ndimo mimi nimemwua huyo jamaa. Na nimetumia 'sailensa' hata mimi," alimaliza Sammy.

Na mimi nikamweleza mambo yote yalivyotokea.

Sasa tulijaribu kuunganisha mambo yote yalivyotokea.

Inaonekana hawa watu walijua John amekuja kufanya nini kwa hiyo walitumia kila njia wamwue. Pili wanajua kuwa kuna watu ambao watafanya kazi hii na John, hivyo walikuwa wanavizia mtu yeyote ambaye angekuja katika chumba cha John. Nilipokuwa nimepiga simu mara ya kwanza inawezekana hawa watu walikuwa chumba cha pili. Nilipokata simu, nadhani walionelea wakate waya wa simu, ndiyo sababu wewe uliponipigia haikuweza kulia kengele.

Nilipofika mimi walijua lazima ndiye mwenzake John, hivyo lililokuwepo ni kuniua hata mimi. Nilipoweza kumshinda Kasha. huyu mtu wa pili alikuwa chini ya hoteli akimngojea Kasha. Kasha alipokawia akaona aje aangalie. Alipofika humu hakuja moja kwa moja, akaona aingie mwenye chumba hicho cha pili sababu alijua kuwa wameshatayarisha hayo matundu. Alipochungulia aliona nimeshamshinda nguvu Kasha. Na Kasha alikuwa karibu atoe siri, kwa hiyo ikambidi amwue Kasha kabla hajasema.

"Angeniua na mimi papo hapo lakini alitaka kuwa na hakika mimi ni nani, kwa vile alivyodhani anaweza kunilazimisha kusema. Nilipokataa kumwambia uhakika aliona aniulie mbali, lakini wewe ukamuua kabla. Huyu mtu wa pili alionekana kuwa wa maana zaidi katika huu uhaini kuliko Kasha. Sasa lililopo ni kutaka kujua hawa ni akina nani." Nilinyamaza kumeza mate.

"Maswali ya kujiuliza sasa ni mawili au matatu. Je walimfahamuje John, mapema hivi? Je huyu mwenye hoteli ana uhusiano nao? Sammy alitaka kuzungumza.

"Willy mimi naona kuwa wewe uende tena huko Princess maana sasa ni saa sita kasoro robo. Miye nitarudi Starlight nikamwone Robin. Huenda akawa na jambo. Halafu wewe nenda kazungumze na wafanyakazi wa hapo upate kujua lini chumba hicho kimeacha kutumika. Nadhani vijana wa Robin wamemvia Lulu kwa hiyo huenda Robin anaweza kuwa na jambo juu ya Lulu na watu wake. Hizo maiti hazitatambuliwa huenda mpaka kesho asubuhi. Hii itatupa muda wa kutosha kufanya kazi zetu.

Ukitoka Princess njoo moja kwa moja mpaka Starlight Klabu kabla ya saa saba. Ukichelewa tutajua huenda umesakamwa na siye tutakimbia kuja hapo."

Mawazo ya Sammy niliyaona kuwa ya busara sana. Kwa hiyo tulifanya kama alivyosema. Nilikodisha gari toka River Road kupitia Compos Robeiro mpaka Princess. Sammy naye akakodisha gari kwenda zake Starlight.

Nilipofika Princess nilikuta watu wote bado wanashughulika na kunywa, na kila mtu alijali mambo yake. Wengi walikuwa wakimalizia vinywaji vyao kwani saa za kutoka zilikaribia. Katika pembe moja nilimwona msichana mmoja ambaye hakuonekana mwenye furaha hapo halipoketi. Nilipokuwa nikimfuata hakuonekana kupenda nimfuatie hivyo.

"Habari zako binti," nilimsalimu. Badala ya kunijibu alinitizama tu. Nilikaza roho kiume, nikaenda kukaa kwenye meza moja naye. Uso wake ulionyesha uhasama wa chuki, ingawa sura yake ilikuwa na haiba kiasi cha kutosha .

"Mbona nyiye wanaume hamwezi kujali mambo yenu wenyewe? Huko kuniona hapa unadhani mimi natafuta wanaume?" Alisema kwa dharau.

Si hivyo bibie. Miye mwenzio si mwenyeji sana hapa. Nimekujia ili unisaidie mambo mawili hivi. Na hakika nilistaajabu kuona kisura kama wewe kukaa peke yako hapa pembeni tena ukionekana mwenye kuwa na huzuni. Je, kuna jambo lmekuudhi? Ama ikiwa ni shemeji aliyekuudhi, nitumie nikamsihi," Nilinyamaza nikitabasamu.

"Sema basi unataka nikusaidie nini? Miye hapa napumzika na kawaida yangu huwa sipendelei sana kukaakaa na wanaume wanaokunywa pombe. Ndiyo sababu nimekaa hapa peke yangu. Wewe ni nani?" Aliuliza.

Mimi ni Joe Masanja, mwandishi wa habari juu ya maonyesho ya mavazi. Ninatoka Mwanza. Tanzania. Hii ni mara ya yangu ya kwanza kufika Nairobi. Nina haja ya kujua baa hapa Nairobi zinafungwa saa ngapi siku za jumapili?"

"Nenda uulize huko baa," alijibu kwa hasira.

"Ah binti! Mbona wasichana wa Nairobi wakali hivi? Msichana kama wewe hufai kuwa mkali kwa kijana kama mimi. Uzuri wako unakutaka uwe mkarimu na msikivu ili uweze kuziliwaza nyoyo za watu dhalili kama miye." Nikamjengea tabasamu pana la haiba.

Maneno hayo yalimlainisha kiasi. Ukitaka msichana afurahi, mwambie kuwa midomo yake ni mizuri na mitamu.

"Wanafunga saa saba, lakini unaweza unafungiwa ndani ukaendelea kunywa mpaka huenda hata saa tisa," alijibu.

"Jee unaitwa nani, na unakaa wapi?"

"Mimi naitwa Lina Samson. Kwetu Nakuru, lakini kwa sasa niko hapa kwa mapumziko kidogo ya mwezi mmoja. Ninaitambua vyema Nairobi sababu nilizaliwa nikakua na kusoma papa hapa mpaka baba alipohamia Nakuru, ambako ndiko masikani hasa," alijibu hali akimwemwesa.

"Sijui kama nitakuona tena Lina. Ningependa kukuona mara nyingi kama hutajali,"

"Ninaishi Guaden Hoteli chumba nambari kumi. Unaweza kupiga simu hapo hotelini, na watakuunganisha na chumba changu. Alamsiki," alimalizia hali akisimaa kujiandaa kuondoka hapo. Akaondoka.

Nilizunguka zunguka kidogo humo ndani kusudi niweze kuona kama naweza kumpata mfanyakazi anayeweza kuaminika kidogo. Nilimuona kijana mdogo hivi, apata umri wa miaka ishirini. Nilitoa noti ya shilingi mia na kumpa. Utafikiria kuwa huenda natumia pesa vibaya, lakini ukitaka cha uvunguni sharti uiname. Kijana kama huyo wakati wa mwambo kama huo ukimpa shilingi mia atakueleza hata yale aliyoyazungumza na mpenzi wake faraghani. Kijana huyo aligutuka sana hata akaniuliza, "He, unataka nini, pombe gani?".

"Hiyo fedha nimekupa, chukua ni yako. Sasa tafadhali naomba unielezee habari fulani fulani, Mbona chumba nambari hamsini hakina kitanda wala mtu?"

"Hicho chumba hakina mtu kwa sababu kinavuja kwa juu siku za mvua. Na siku hizi kuna manyunyu mengi".

"Kimeanza lini kuvuja?"

"Leo kiasi cha saa nne hivi kama unakumbuka kulikuwa na manyunyu,"

"Nambari hamsini na moja kulikuwa na mtu?"

"Ndiyo, mtu mmoja toka Uganda aitwae Fred, ndiye alikuwa amepanga humo kuanzia saa moja asubuhi."

"Kuna mtu yeyote aliyewahi kuingia chumba nambari hamsini kutoka nje wakati wa mchana?".

"Ndiyo, mtu mmoja aitwae Benny, alikuja na watu wengine watatu hivi. Waliingia kukitazama kama wanaweza kukiziba, lakini baada ya kukikagua sana walisema hawawezi, wakaenda zao. Sifahamu wanakaa wapi", alimaliza.

"Basi usimwambie mtu yeyote nilivyokuuliza."
 
Sura ya Nne

Nilipotazama saa yangu, ilikuwa saa tisa na nusu. Nilitoka hapo baa na kukodisha gari hadi Starlight. Niliwakuta Robin na Sammy wakitungojea.

Robin hakuonekana mwenye furaha. Nadhani Sammy alikuwa amemweleza mambo yalivyokuwa. Halafu niliamua kupiga simu polisi ili waweze kushughulika na hizi maiti.

"Hapo ni Polisi?".

"Ndiyo Bwana, unataka nini?".

"Naweza kuzungumza na Polisi Inspekta Tsumah?. Tafadhali".

"Ngoja kidogo" alijibu.

"Hallo, huyu ni Polisi Inspekta Tsumah. Nani mwenzangu, na nikusaidie nini?"

"Mimi ni rafiki yako, ambaye ninazo habari za kukugutusha kidogo. Ni kwamba ziko maiti tatu katika Princess Hoteli chumba nambari 51. Nenda ukajionee mwenyewe. Miye sina uhusiano nazo. Kwa heri." nilikata simu kabla hajaweza kusema neno lolote.

Nilipiga simu kwa Chifu saa hiyo hiyo, nikimweleza kuwa awashauri maafisa wa polisi wasishugulike sana na mauaji yoyote yatakayotokea hapa Nairobi mpaka tutakapokuwa tumemaliza kazi yetu. Pia nilimweleza kuuawa kwa John.

Robini alitoa taarifa aliyokuwa amepewa na vijana wake juu ya Lulu. Alisema, "Baada ya wewe kutoka, Lulu naye alitoka. Mmoja wa vijana wangu alimfuata, na ilionekana Lulu alikwenda moja kwa moja hadi International Cassino. Alivyofika huko alisimama nje kwanza. Kisha alitoka kijana mmoja katika International Cassino na kuja kuonana naye. Alinyamaza alipokuwa akimeza mate.

"Walikaa hapo nje kwa muda. Kisha huyo kijana alimpa busu Lulu. Ilionekana kuwa Lulu alikuwa akimtegemea huyo kijana huko Starlight, lakini kijana huyo hakuonekana. Ilionyesha kuwa Lulu alijua kwamba huyo kijana mara nyingi alikuwa akienda Cassino. Alipofika hapo nje kumbe huyo kijana naye alikuwa akitoka. Kijana wangu alifikilia kuwa lazima wawe marafiki. Kijana huyo alionekana nadhifu sana, lakini macho yake yalionyesha uovu mwingi. Kijana wangu hakuweza kusikia waliyokuwa wakisema, ila alibuni kuwa walikuwa wakizungumzia juu ya kitu fulani kuhusiana na Starlight Klabu.

"Kijana wangu alingoja hapo mpaka walipokuwa wakiondoka. Walipoondoka, Kama alivyoripoti kijana wangu, waliingia katika gari moja Zephyr 6 nambari KKK 117. Walivyoanza safari ya kurudi mjini na Uhuru High Way naye aliwafuata. Walienda na kusimama nje ya Hoteli Intercontinental. Na Lulu alitoka nje. Alipokuwa akiingia hotelini, kijana wangu alimsikia Lulu akimuaga huyo kijana kwa sauti, "Kwa heri Benny."

Kusikia jina la Benny, nywele zangu zilisimama kidogo, kwani yule kijana wa Princess alikuwa pia ameniambia kama unakumbuka. Benny alikuwa amekuja kuchunguza kile chumba nambari 50. Katikati yangu na wewe nadhani Benny ana jambo hapo.

Nami nilimweleza mambo ambayo niliyapata kutoka kwa yule kijana wa hotelini. Nao walianza kumshuku Benny na Lulu pia. Maana kama nilivyosema awali. Kwamba wasichana waliovipande wote ni sumu mbaya sana.

Wote tulifikiria kwa tulikuwa tukianza kuona mwanga kidogo. Lakini hee, makubwa yalikuwa bado yanakuja. kwani kama huyo Benny na Lulu ndiyo wanacheza haya mambo lazima kuna kitu!

Tuliondoka hapo nje ya Klabu na kila mtu akakodisha gari kwenda kulala. Tulikuwa tumepanga, kupigiana simu kesho yake asubuhi mnamo saa mbili. Robin alikuwa akilala New Avanue Hoteli.

Gari niliyokodisha ilinipeleka hadi hoteli Fransae. Kisha niliingia vichocholoni mpaka Embassy Hoteli. Kama mtu alikuwa akinifuata, angeweza kufikili kwamba nilikuwa nikilala hoteli Fransae. Niliingia chumbani kwangu ili nilale. Mawazo yangu yote yalikuwa juu ya mauaji ya John. Niliwaza kumuua huyo aliyemuua John iwapo muuaji huyo hatatangulia kiniua. Kitandani hapo chumbani, niliweka bastola yangu chini ya mto, kwani sikuweza kujua lini watu hao wangenifuata, maana wanaonekana kuwa wajuvi sana.

Asubuhi niliamshwa na mfagiaji, ambaye alikuwa anafagia nje ya mlango wangu. Kwa bahati mbaya akagonga mlango huo. Nilipotazama saa ilionyesha kuwa ilikuwa yapata saa mbili kasorobo. Nilikwenda kuoga, na kujiweka tayari kwa kazi ya mchana huo. Saa mbili kamili nilikuwa nimekwisha piga simu kwa Sammy na Robin.

Kabla sijapiga simu, Sammy alianza yeye kunipigia akisema, "hallo Willy, vipi? Umelala salama leo? Miye mwenzio nilikuwa na ndoto za ajabu na za kutisha. Nadhani kifo cha John bado kinanitisha. Sasa unasemaje, tuanzeje?"

"Sammy, nadhani haya tusiyazungumze kwenye simu, ila mpigie Robin simu umweleze mje hapa hoteli kwangu. Umeshapata kifungua kinywa ama vipi?"

"Bado sijapata, ila nategemea kupata sasa hivi."

"Vema, tutaonana saa tatu."

"Nililetewa kahawa na kuanza kunywa. Baridi ilikuwa kali sana... Ukungu ulikuwa umejaa kote. Siku ilianza kunitisha sana, hata kabla sijaanza kufanya lolote. Nilionekana mtu mwenye wasiwasi mwingi sana. Ungaliniangalia asubuhi hiyo hata wewe ungalinihurumia, ingawaje mimi si mtu wa kuhurumiwa. Ilipofika saa tatu. Sammy na Robin walifika. Mimi naona twende 'City Hall' maana maonyesho yanaanza leo saa tano. Na kama hamjui, leo ni sikukuu ya kufungua maonyesho. Kwa hiyo watu kote nchini wanapumzika hawaendi kazini. Na kwa sababu Lulu anasema ni mwonyeshaji mavazi, basi lazima atakuwepo. Na kama kweli Benny ni rafiki yake, hata yeye atakuwepo hapo 'City Hall' na kutokana na msongamano huenda tukafahamu lolote," alisema Robin.

'Gazeti la Daily National' lilikuja, na baada ya kuliangalia ilionekana mengi hayakuandikwa juu ya hivyo vifo. Maana waliandika tu ya kuwa "Watu watatu walikutwa wamekufa katika chumba kimoja Princess Hoteli. Polisi bado wanafanya uchunguzi," basi. Tulifikiria mkurugenzi wa usalama Kenya alifanya kama tulivyokuwa tumeomba.

Saa nne na nusu tuliondoka kuelekea City Hall. Sammy alibeba kamera na kuonekana kuwa mpiga picha hasa. Miye nilionekana kama mwandishi wa habari. Tulikuwa tumechukua vitambulisho vyetu. Tulipofika City Hall, baada ya kuonyesha vitambulisho vyetu, tulikuta siye tumepewa viti huko mbele karibu na jukwaa kusudi tuweze kuangalia na kuchukua picha vizuri. Mimi na Sammy tulikaa karibu karibu na Robin alikaa mbali kidogo nasi.

Robin alikuwa ameishafanya mpango na vijana wake kuwa karibu karibu katika huo ukumbi, kusudi ikiwa wataweza kuona lolote waweze kusaidia.

Kitu kilichokuwa kinaniuma ni kutaka kujua zilipokuwa hizo karatasi za siri. Pia wakati gani wamepanga kuzibadilisha. Na tatu wapi ambako haya mabadilishano yangefanyika. Mpaka hapo tulikuwa tumekwisha hakikisha kuwa Chifu alivyobuni itakuwa sawa. Maana mpaka hapo ilionekana ni watu wa Afrika Mashariki waliotuandama. Kule kujua kwao kwamba siye tumefika Nairobi na kuanza kuwasaka, kungefanya waharakishe kuzibadilisha hizo karatasi, kitu ambacho hatutaki kitokee. unaweza kuona mwenyewe jinsi muda ulivyokuwa mbaya. Akili zetu zilivurugika kama nini sijui.

"Hujambo mwananchi?" Nilisikia sauti kwa nyuma yangu ilinishtua sana kwa maana nilikuwa katika mawazo mengi. Nilipogeuka nikakuta ni mtu ninayemfahamu ambaye alikuwa muda mrefu sana Dar es Salaam. Huyu alikuwa Peter ambaye naye alikuwa mpigania uhuru na sasa akiwa ameletwa Nairobi kufanya kazi.

"Hallo Peter,habari? Mimi ni Joe Masanja nimekuja hapa kama mwandishi wa habari juu ya maonyesho ya mavazi. Na huyu ni Athumani Hassan, Mpiga picha".

Peter alijua nilikuwa na maana gani sababu ananijua, na anajua kazi yangu ni nini.

"Mmefika lini hapa. Lazima liwepo jambo alininong'oneza.

Kisha aliandika habari kwenye karatasi na kunipa. Humo aliandika maneno haya," Jee mmekuja kuchunguza kuhusu tukio la jana? Nimeambiwa na ofisi ya Dar es Salaam nisaidie. Kama ndivyo niko tayari kuwasaidia."

"Tulifika jana. Na hasa," nilijibu.

Peter alielewa, kisha alihama akaja kukaa na sisi. Alikaa upande wangu wa kulia na Sammy upande wa kushoto.

Baadaye nilimuona Lulu anaingia akiwa na Benny. Nilimuuliza Peter, "ati unawajua hawa?"

"Siwajui, ila tu nimewahi kumuona yule Benny katika mabaa fulani fulani tangu nifike hapa Nairobi. Kama ukipenda kujua jambo lolote juu yake hiyo ni kazi rahisi. Ninaweza kukupatia habari kabla ya usiku wa manane leo."

"Nitafurahi sana ukifanya hivyo na watu wako."

Peter alioneka mwenye kuhudhunishwa sana na jambo hili akiwa kama mpigania uhuru. Baadaye Lina naye aliingia. Alikuwa peke yake kama kawaida. "Ulitaka kumuona yule? Nilimuuliza Peter.

Ndiyo. Yeye ni Lina Samson."

Lina alikuwa msichana tofauti sana na wasichana wengine. Sura yake ilikuwa ya kupendeza vya kutosha, kama nilivyosema awali. Lakini licha ya Lina kuwa mzuri wa sifa hivyo, hakufua dafu kwa Lulu, kwani Lulu alikuwa 'Lulu' kweli. Pia Peter alisema utamkuta Lina siku zote peke yake mwenye mabaa akinywa soda akichanganya na 'Babycham'. Hivi ndivyo hata mimi nilimkuta usiku uliopita. Lina alituona akaja moja kwa moja kutusalimia. Kisha akanipigia kope akaenda kukaa mbali nasi kidogo.

Wakati Benny alipoingia na Lulu kila mtu aligeuka kuwaangalia. Lulu alitembea kwa maringo sana na Benny alionekana akifurahia kuona kila mtu akimwangalia wakati wakifuatana na mrembo huyo wa kushtua. Hata mimi nilimuonea wivu. Maana nilitamani niwe mimi badala yake nitembee na mrembo huyo. Lina alimwangalia sana Lulu. Nikaona huenda alikuwa pia akimuonea haya Lulu.

Nilitambua kuwa Lina anamfahamu Benny, kwani Benny alipokuwa anapita na Lulu, alipomuona Lina amekaa karibu na mahali walipokuwa wakipita, alitazama chini. Kwa hiyo niliona itakuwa vizuri kama nitafanya urafiki na Lina maana naweza kupata msingi mdogo wa kutusaidia. Pia niliona Lina angeweza kusikilizana na mimi, kwani kama nilivyosema alinipigia kope kuonyesha dalili ya urafiki.

Maonyesho yalipoanza wanawake walianza kutoka mmoja mmoja wakionyesha mitindo ya kila aina. Kulikuwa na wanawake kutoka karibu kote Ulimwenguni wakitoa mitindo mbali mbali. Niliandika kikaratasi na kumpa Sammy akiangushe katika mapaja ya Lina, wakati akijifanya kama kwamba anatafuta mahali pazuri kwa kupiga picha. Niliandika, "Tafadhali tuonane nje, kwenye mlango mkubwa, kama dakika kumi kabla ya watu wote kutoka. angalia watu wasifahamu unaningoja mimi************".

Sammy alikiangusha kama nilivyomueleza. Baada ya kusoma bila mtu kujua aliniangalia na kutikisa kichwa, akionyesha kuwa amekubali. naye alianza kuandika kwenye hicho kikaratasi. Akakitupa mbele ya Sammy. Alipokuwa anarudi. Sammy alijifanya ameangusha kasha la 'Film', akainama na kukiokota hicho kikaratasi pamoja na kasha la 'film' yake. Niliposoma nikakuta maneno haya. *************"Ndani ya gari langu jeusi namba No. KKT 581 - Mazda Delux - kulia mwa mlango mkubwa," basi niliona mambo yote yamekuwa kama nilivyopanga. Lakini ukavu wa macho ya Lina ulinitisha kiasi cha kwamba woga uliniingia kidogo. Lakini kwa sababu sikuwa mwoga kama wewe, sikujali lolote litalotokea baadae.

Lulu alijitokeza. Alipotokea kwenye jukwaa kila mtu alipiga kelele, kwa vifijo na ushangiliaji wa ajabu. Lulu aling'aa kama nyota. Alionyesha mtindo wake unaoitwa 'Popcom'. Wachukuaji wa picha walichua picha kwa fujo sana.

Alipokuwa anarudi kwenye chumba wanachotokea. Robin alipita karibu yangu na kudondosha kikarasi. Nikakisoma kilikuwa kimeandikwa "Mjiangalie sana, maana yametokea mauaji mawili tayari humu ndani", wakati Lulu alipotoka na watu walipokuwa wakipiga kelele na kushangilia vibaya sana, vijana wetu tuliokuwa tumewaweka kuviziavizia, wawili wao wameuawa. Inaonekana waliona jambo fulani ambalo limewaponza. Mueleze na Athumani, laa zivyo na siye tutakufa".

Lo wasiwasi ulinizidi sana. Sammy alipokuja karibu yangu nilimueleza mambo yalivyokuwa. Zilikuwa zimebaki kama dakika kumi na tano hivi maonyesho ya asubuhi yaishe. Hivyo tukafungashafungasha vijitabu vyetu tuondoke. Tulimuaga Peter baada ya kumweleza ninapokaa. Tulitazama huku na huku kwa mashaka makubwa sana. Nadhani hata wewe unaweza kufikiria mawazo tuliyokuwa nayo.

Tulipofika mlangoni, nilibahatisha kumuona Benny amesimama na kijana fulani akimueleza mambo fulani fulani na huku akitutizama kwa usiri mno. Nilijua alikuwa akimuambia huyo kijana atufuate. Hivyo nilimueleza Sammy abaki nyuma kidogo ili niweze kuwapoteza wasije wakajua ninaondoka na Lina.

Peter alikuwa kwenye dirisha moja la 'Hall" na akaniona nilipokuwa nikiingia katika gari la Lina. Akanipungia mkono. Nadhani aliweza kupata nafasi ya kukisoma kikaratasi cha Lina. Sikujali Peter kufahamu hayo, kwani na yeye ni mtu wetu.

"Mtu yoyote amekuona?"

"Hapana, uenda wamekuona wewe" alijibu.

"Sidhani kama wameniona"

Lina alitia moto tukaondoka. "Tupitie njia ipi?" aliuliza.

"Twende moja kwa moja, mpaka Embassy Hoteli."

Lina alivuta gari mpaka tukaingia Kenyatta Avenue. Nilipotazama nyuma, niliona gari moja kama kwamba linatufuata. Kutaka kuhakikisha nilimueleza Lina badala ya kuingia Koinange akate kona na kuingia uhuru High Way. Halafu aingie Haile Selassie Road. Gavament Road ndipo turudi Kenyatta Avenue. Kisha tuendelee na safari yetu. Kusema hili gari lilikuwa linatufuata maana kuzunguka kote huku nalo lilikuwa bado linazunguka kutufuata tu. Tulipofika kwenye kona ya Kenyatta Avenue nilimwambia Lina asimame, aliposimama hilo gari nalo likasimama karibu sana nasi. Nilitoka nje nikamfuata dereva wa gari hilo.
"Sikiliza bwana mdogo, Miye sitaki kufuatwafuatwa. Sikuzoea mambo hayo. Na kama hutaki meno yako zidi kunifuata. Kamwambie huyo mume wako aliyekutuma kuwa kama anataka kunitafuta aje yeye mwenyewe ajionee. Kama unataka usalama tia gari lako moto uende zako."

Kijana huyo hakuwa na la kufanya ila kufanya kama nilivyomwambia. akaenda zake. Nilirudi katika gari la Lina akaendesha mpaka Embassy Hoteli.

"Sikiliza Lina, nenda ukasimamishe gari hili mbali na Embassy Hoteli kusudi hawa wahaini wasijue tuko hapa wakatufuata"

Baada ya kuweka gari Lina alikuja tukapanda mpaka kwenye chumba changu. "Sijui kwa nini naonekana kukupenda, maana tangu jana mle Princess Hoteli, baada ya kutoka na kukuacha humo, usiku mzima sikulala ila kukufikiria wewe tu." Alisema Lina hali akijilaza.

"Oh Joe, mpenzi nakupenda sana ingawaje unaweza kuniona kuwa miye malaya kwa kukufuata baada ya kuonana siku moja tu. Lakini lazima ujue kuwa mtu unaweza kuwa hujapenda, lakini akaja mtu mgeni ukampenda kufa. Hapa Nairobi nimeishawahi kufanya mapenzi na mtu mmoja tu, ambaye anaitwa Benny Makunda. Lakini hata siku moja sikuweza kukosa usingizi juu yake, kama nilivyokosa juu yako jana. Ningejua unakaa hapa basi tu ningekufuata."

"Waaa, unasema kweli ama tu kunidhihaki? Hata mimi nimekupenda Lina. Tangu jana tabia yako ya utulivu na kiburiburi niliipenda sana. Maana mimi napenda watu kama hao hasa wakiwa wasichana"

Loo! Hapa niliona mambo yanakorogana sana Benny aliwahi kuwa mpenzi wa Lina. Na Benny ndiye tuliyekuwa tunamashaka naye. Huyu kijana anaonekana ni 'Champion' kwa wanawake, kwani sasa anatembea na Lulu. "Huyu msichana Lina ananitania ama vipi." ndiyo sasa yalikuwa mawazo yangu. "Lakini yote hayo nitafahamu muda si mrefu kwani naweza kumusoma msichana kama Lina Vizuri sana."

"Kumbe unamfahamu Benny, hata amewahi kuwa mpenzi wako?" Nilimuuliza.

"Ndiyo," alijibu.

"Mmeachana tangu lini?"

"Kuna huyu msichana wanayemwita Lulu. Msichana huyu anatoka Uganda na huwa yuko huku mara nyingi sana. Sura yake kama ulivyomuona inavutia wavulana wengi sana. Alipokuja huku mwezi wa jana Benny alimuona, na wakaanza mapenzi. Mwishowe Benny hakunijali tena. Nami kwa tabia yangu nikaona siwezi kupenda mtu ambaye hapendeki.

"Kwanza nilimuonya Benny asitembee na Lulu kwani Lulu ingawaje ni mzuri kiasi cha kutisha namna ile, lakini ni hatari sana kwa mambo ya ukahaba. Lakini baada ya muda mfupi Lulu alirejea Uganda. Benny akarudi sasa. Lakini miye sikumtaka tena.

"Benny ana fedha na ana fedha nyingi. anazitoa wapi sijui, lakini ana fedha. Kazi yake ni dereva wa taksi tu. Anaendesha taksi yake moja 'Mercedes Benz'. Nilipokataa Benny alinibembeleza sana lakini nikakataa tu bado. Aliniahidi kuwa angelininunulia gari moja aina ya 'Citron' mwezi huu, maana atakuwa 'Giriki' mwezi huu. Miye nilizidi kukataa tu. Na nilikuwa nimeapa hata siku moja sitafanya mapenzi na mvulana tena. Nilikuwa nafikiria kwenda kuwa mtawa. Bahati nzuri au mbaya ndipo akaja huyu kijana ambaye amenifanya hata sikuweza kulala. Oh, kweli mama aliniambia usimpende mgeni, lakini mimi hata, nitakupenda tu."alimalizia Lina.

Bado mimi sikumwamini hata punje.

"Benny alikwambia hiyo pesa angetoa wapi?" Nilimuuliza.

Alisema ati ana rafiki zake huko ng'ambo ambao wangemletea fedha hiyo. Benny anafahamiana na wazungu wengi sana," alisema kwa mashaka kidogo.

Ubaya wa huyu msichana ni kuwa huwezi kumwelewa hata kidogo kwani anaposema, husema kwa utulivu mno hivyo kwamba huwezi kumtambua yupo upande upi.

"Unaweza kuwatambua wazungu hawa ukiwaona?"

"La, wengi wao wamerudi kwao. Ndiyo sababu nakueleza kuwa, watamtumia pesa kutoka ng'ambo waliko," alijibu.

"Unafikiria ni Wazungu kutoka upande gani?"

"Sijui maana mimi nilikuwa sihusiani nao sana."

"Ni wanaume au wanawake?" Nilimwuliza huku nikijifanya siyajali sana mazungumzo yake haya.

"Lo, Joe, mimi sikuja hapa kujibu maswali juu ya Benny. Mimi nimekuja kwa sababu napenda kuzungumza juu ya maisha yangu na wewe na kufanya mapenzi. Kama unatafuta wanawake wa Kizungu, ambao Benny hutembea nao, ni rahisi sana kuwapata hapa Nairobi. Na kwa vile wengi wamekuja kwenye maonyesho, nenda tu ujipige utapata," alijibu kwa uchungu sana na hasira.

"Si hivyo Lina. Sina haja na wanawake wa kizungu, ila tu nilitaka kufahamu mengi juu ya Benny, kwani anaonekana anawakosha sana wasichana. Mtu wa kuweza kumuacha msichana wa haiba kama wewe, lazima awe mwamba hasa."

"Lakini unanipenda kweli Joe?" Alisema huku machozi yakimtoka.

"Ninakupenda sana Lina. Na sasa ninaanza kukuelewa na kukupenda zaidi. Je. Benny anakaa wapi?"

"Benny anakaa huko Westlands, karibu na maduka ya Westlands. Nyumba "plot No. 3" pembeni mwa Nakuru Road, baada ya kuvuka Motel Agip. Au kwa urahisi karibu na Sclaters Hostel."

"Mpenzi Lina, nataka kukuambia ukweli sasa. Mimi si Joe Masanja, mimi ni Willy, Willy Gamba." Lina alikuwa amelala kwenye kitanda lakini nilipotaja hilo jina, aliruka na kusimama mbele yangu huku anaonyesha hali ya kushangaa sana.

"Mimi ni mpelelezi wa Idara ya Uchunguzi ya Tanzania." Nilitoa kitambulisho changu cha upelelezi. "Usishtuke Lina, Kaa chini na huenda toka sasa tutaelewana vizuri zaidi. Na huenda toka sasa ukanisaidia." Nilienda kukaa karibu naye hapo kitandani.

Alinivuta akaanza kufungua tai yangu, kisha shati langu, halafu suruali yangu... tukajilaza.
 
Sura ya Tano

"Wuuuuu. Willy, Willy Gamba, umesema ndiye wewe! Loo! Siamini masikio yangu ni wewe kweli, kweli! Nimesikia jina lako mara nyingi. Nimesikia sifa zako. Nilikuwa nikidhani ni hadithi tu kama tunazosoma katika vitabu. Sikufikiria ama kuota kama nitakuona. Nimesoma habari zako katika magazeti, lakini nilikuwa sijaota ya kuwa siku moja nitalala kitandani na Willy Gamba." alisema Lina huku akitetemeka na kunibusu, "Nini kimekuleta sasa hapa, Willy?" aliuliza.

Nilifikiria sana kama naweza kumwambia. Mwishowe nikakata shauri nimwambie kwani siye nyakati zingine huwa tunaropoka kusudi tuone nini kitatokea. Mara nyingi huwa tunajitega wenyewe halafu tunatafuta njia ya kujinasua tena. Hivyo nilimweleza mambo yote tangu mwanzo mpaka mwisho. Pia nilimweleza jinsi tunavyomfikiria Benny. Na jinsi ambavyo tumenusurikanusurika usiku wa jana.

"Jana usiku nilipokuwa nikitoka nilimuona Benny hapo nje ya Princess katika gari moja ya Kimarekani 'Pontiac' yeye hakuniona" aliniambia Lina.

Kama Lina anasema kweli basi Benny ndiye alipanga mauaji ya John na kama nilivyokwambia ahadi chuki na uchungu viliniingia juu ya Benny.

"Je unamjua rafiki yake yeyote wa Kireno au wa Afrika ya Kusini?"

"Hapana lakini naweza kukusaidia ukitaka," alijibu.

"Kukuambia ukweli Benny si mchezo. Anatembea na bastola tatu, na kila nilipokuwa nikimuuliza ni za nini aliniambia kuwa ni za kujikinga kutokana na maharamia. Maana akiwa na taksi, wanaweza kuikodisha halafu kufika njiani wakakunyang'anya, hasa mtu mwenye 'Benzi' kama yeye. Tena akipiga risasi zake hazikosi. Maana siku moja tulikwenda msituni kuwinda katika bonde la ufa, ndipo nilimtambua.

"Tulikuwa na mdogo wake ambaye alibeba chupa za fanta ndogo. Basi alikuwa anaweka hizo chupa kwenye kichwa cha mdogo wake na kuanza kupima shabaha kwa bastola. Ajabu ni kwamba hakuweza kumjeruhi mdogo wake hata kidogo. Na aliniambia kuwa huwa anafanya haya mazoezi mara mbili kwa juma. Hivyo nakusihi Willy usimuendee ovyo.

"Asante sana kwa kunionya Lina maana kama ningalikurupuka huenda hata mimi ningeyala marisasi kama rafiki yangu John."

Mara simu ililia. "Huyu ni Peter nazungumza, ni Joe huyo?"

"Ndiyo Peter unataka nikupe hadithi gani?"

"Sikiliza Joe, nina habari. Nimepata habari kamili juu ya maisha ya Benny, Benny anakaa Westland 'plot No. 3' karibu na Sclatirs Hostel. Yeye ni dereva wa taksi. Anaendesha taksi moja aina ya 'Mercedes benzi 280 SE'. Nambari KKZ 601. Rangi ya kijani. Benny anafahamika kuwa kijana tajiri sana, maana hilo gari lake linapendwa na watu wengi hasa watalii. Hivyo anafahamiana na watalii wengi sana. Amesoma mpaka darasa la kumi na nne. Kisha akaenda nchi za ulaya, ambako inasemekana hakufanya vizuri katika mtihani wake ikapasa arejee. Amewahi kukaa ureno kwa muda fulani fulani huko. Ni kijana fundi sana katika kutumia bastola. Ana shabaha za ajabu. Walimuomba aende jeshini akakataa. Polisi huwa wana mashaka naye kuwa uenda akawa naye ndiye mmoja wa magaidi wa hapa Nairobi wanaonyang'anya mali katika maduka makubwa makubwa na benki. Lakini hawajawahi kumshika ila wanamfikiria tu. hajapelekwa kontini hata siku moja. Tabia yake ni ya utulivu sana, lakini ni shupavu sana na mvumilivu wakati wa shida. Wasichana wengi sana wanakufa kwake kwa sababu ana sura nzuri. Kama onavyomuona. kwa kifupi ndivyo mambo yalivyo."

"Asante Peter, endelea kufanya uchunguzi uwao wote ambao unaweza kutusaidia."

"Miye nitajaribu kila njia ya kuwasaidia. Na kama una shida nyingine yeyote unaweza kunieleza tu. Kwa kheri mpaka wakati mwingine."

Nadhani hata kama huwa unatumia makamasi badala ya ubongo, unaweza kuona mambo yanavyokuja yenyewe. Benny anafahamu kutumia bastola vizuri sana. Kwa hiyo Benny analo kundi la watu ambao amewafundisha namna ya kutumia bastola nao wamekuwa stadi kama yeye. Benny amekaa ureno kwa muda, na alipokuwa huko alifanya urafiki na watu wa huko na hata akaweza kutumia bastola vizuri sana. Ni wazi kuwa hao wareno wamejua habari za hizo karatasi za siri. Wakakata shauri waziibe.

Wamejaribu wao wenyewe na kushindwa. Waliposhindwa na kuona wao hawawezi kuziiba wakatafuta majambazi wa hapa hapa Afrika ya Mashariki. Kwa sababu wanamjua Benny na amewahi kuwa rafiki yao wakamwendea. Walipomwendea Benny akaona hawezi maana hana fedha ya kutosha. Lakini Benny anajua kundi fulani la majambazi, kwa hiyo akaenda kumwambia 'bosi' wa hayo majambazi juu ya wizi wa karatasi hizo. Na, pia kuahidiwa kupata fedha nyingi sana. Huyo 'bosi' akakubali.

"Kisha akamfanya Benny mkubwa wa genge hilo akapewa pesa, gari na kila kitu. Sasa shida ikawa watazipataje, kwa hivyo wakatafuta mtu mwenye kujua habari nyingi juu ya hizo karatasi na kuwapa mambo yote.

"Umeona basi mambo yalivyo? Kufika hapa sasa naanza kuona mwanga. Ila kuna maswali ya kujiuliza. Je huyu bosi ni nani? Je nani aliye na karatasi sasa? Tutawashikaje maana wameisha tufahamu. Huyu aliyetoa habari ni nani? Na wakati gani hivi vitabadilishwa? Na nani aliyekuja kuzichukua hizo karatasi toka Ureno?.

Ukinijibu maswali haya, nadhani tutakuwa tumemaliza kazi yetu. Lakini rafiki yangu, inaonekana kabla hatujajibu maswali haya tunaweza kuwa wote tumeisha kufa, maana kuyajibu, kuna maana ya ua au uuawe. Ureno, hii ni kazi ya Ureno. Kwa hiyo lazima mwenye kuzichukua kuzipeleka Ureno ni mwenye asili ya Kirenoreno. Na kama kubashiri kwangu ni sawa naona tunaweza kufanya kitu , lakini kama ndiyo nimekosea, basi tumekwisha kazi kabisa."

"Lina," nilimwita hatimaye, "tafadhali jaribu kuchunguza lini Benny alianza kuwa dereva wa teksi. Pili lini amenza kukaa huko Westlands, maana najua ni watu wenye fedha sana tu wanaoweza kukaa huko. Tatu, kama unaweza, jaribu kupata habari za Wazungu anaotembea nao Benny siku hizi. Ukiwa kama msichana wake wa zamani, ukijifanya bado unampenda, kwa hiyo unajaribu mrudiane, nadhani unaweza kupata majibu ya maswali yangu. Pia jaribu kuchunguza ni Wazungu wa kutoka wapi hao rafiki zake."

Niliagana na Lina akaenda zake. Nilijilazimisha kumwamini. Na kama nilikuwa nacheza na moto, Mungu ndiye anayejua. Kwani Chifu alisema, "Mara hii usiamini mwanamke yeyote."

Mnamo saa nane Sammy alikuja chumbani kwangu. Akanieleza, "Unajua Willy, huyu msichana Lulu pia ni hatari. Maana kila alipokuwa akitoka kuonyesha mavazi anafanya maringo kiasi cha ajabu hata watu wote kushangilia. Na wakati wanaposhangilia ndipo watu wanauawa.

Kwa hiyo inaonekana kuwa kila Lulu akitoka hawa watu huwa wameona hatari kwa upande wao hivyo hupeana ishara. Lulu anatoka, watu wanashangilia, wao wanaua!"

"Sasa wewe unafikiria tutaendelea vipi?" Nilimuuliza baada ya kumweleza yote niliyokuwa nimeambiwa na Lina pamoja na Peter.

"Mimi naona kuwa twende kwenye maonyesho ya saa kumi. Na twende tukitahadhali sana. Kitu tutakachotafuta ni mtu anayeruhusu hao wanawake kutoka. Tukimfahamu huyo basi tunaweza kujua mengi. Na pia lazima tumpate Lulu tuweze kujua anajua kiasi gani cha habari hii".

Nilikubaliana na mawazo ya Sammy, kwa hiyo tulimpigia Robin Simu kumweleza jinsi tulivyokwishakata shauri la kwenda maonyesho ya saa kumi. Naye alituambia kuwa angekuja kutupitia hapo chumbani kwangu. Mpaka sasa tulikuwa tumejua kuwa wameishatufahamu, la sivyo wasingelinifuata wakati nilipokuwa nikija nyumbani na Lina.

Robin akaja saa tisa na nusu, tukaanza safari kwenda zetu 'City Hall'. Kila mtu alikuwa amechukua bastola kwapani kama ingekuwa lazima itumike.

Tulienda tukakaa kwenye viti vyetu vil evile vya asubuhi. Peter naye alikuja akakaa karibu yetu tena. Lina hakuonekana mchana huo, watu wengi walikuwa wamekuja huo mchana na ukumbi wote ulijaa.

Kama kawaida ya Benny na Lulu walikuja wamechelewa kidogo. Kila mtu alipiga makofi walipokuwa wakipita. Lulu alivaa 'mini' moja inayoonyesha mapaja yake kwa uwazi mno kabla hajaenda kwenye chumba cha maonyesho, Lulu alimvuta Benny wakaja moja kwa moja mpaka tulipokuwa tumekaa mimi, Sammy na Peter. Benny hakuwa na furaha alipotuona. alionyesha kicheko, lakini kicheko chake kilikuwa cha chukichuki.

"Nadhani hamtajali kama nitawafahamisha kwa rafiki yangu huyu,"alisema Lulu.

"Hatutajali," alijibu Sammy.

"Huyu anaitwa Benny Makunda, dereva wa Teksi na ni rafiki yangu." Kisha aligeuka kwa Benny akasema, "Na huyu ni Joe Masanja, yule ni Athumani Hassani, wote waswahili kutoka Mwanza wamekuja kwenye maonyesho ya mavazi hapa petu, maana wao ni waandishi wa habari."

"Nimefurahi kuonana nanyi. Bila shaka mnaipenda hali ya hapa petu Nairobi," alisema Benny, huku tukishikana mikono.

"Nasi pia tumefurahi sana kukutana nawe. Na hali ya hapa inaonekana kuwa baridi, lakini tunaipenda, "nilijibu kwa niaba ya wenzangu.

"Mtakaa hapa muda gani?" aliuliza Benny akinikazia macho.

"Mpaka mwishoni mwa wiki," nilimjibu.

"Na mkitoka hapa mtarudi Mwanza, ama mtaenda mahali pengine?" aliuliza Lulu.

"Tutaenda Kampala," nilimjibu huku nikitabasamu kidogo.

Nakwambia tabasamu la Lulu, ni hatari, maana alipotabasamu nikasisimkwa na damu vibaya sana. Lulu na Benny walitupiana macho kisha wakatuaga, wakaenda zao.

Maonyesho yaliendelea kama kawaida. Nilitoka hapo nilipokuwa nimekaa nikaenda pande za ukutani, ukutani ambako ningeweza kuona vizuri Benny anafanya nini.

Nilimuona Benny akizungumza na Lulu katika chumba kimoja cha kubadilishia mavazi, maana mlango ulikuwa umefunguliwa. Kisha alimwendea kijana mmoja ambaye alikuwa amevaa vizuri sana huku akivuta mtemba. Huyo kijana, kule kumwona tu, utafikiri kuwa ni mwunguna sana.

Walizungumza kwa muda mfupi kidogo, lakini huyo kijana alionekana hapendelei hayo mazungumzo kwani alikuwa na wasiwasi sana. Baadaye nilikuja kutambua kuwa ndiye mruhusuiji wa wanawake kutoka katika chumba cha kubadilishia mavazi kwenda kwenye jukwaa. Wanawake walikuwa mara kwa mara wakitoka na kuingia.

Mwishowe nilimwona Benny akiirekebisha tai yake kwa kuivuta vuta, baada ya kijana furani kupita karibu naye na kumpa kijitabu. wakati huo wote huyo kijana alikuwa akiendesha mpango wa jukwaani alikuwa akimwangalia Benny kila baada ya nusu dakika. Hatimaye kijana huyo alikimbia moja kwa moja hadi kwenye chumba cha kubadilishia mavazi na kuzungumza na Lulu. Ilionekana ilikuwa zamu ya msichana mwingine kutoka lakini huyo kijana alibadilisha mpango na kumfanya Lulu atoke muda huo.

Moyoni nilijua kuna jambo, kutokana na tulivyoelewa asubuhi. Nilijiweka tayari, maana ilionekana huenda mimi ndiye nimetiliwa mashaka. Kwani wanaweza kuwa wameniona nikichunguza mienendo ya Benny, alipokuwa akizungumza na kijana wa kwenye jukwaa pamoja na Lulu.

Lulu alipotoka alikuwa amevalia Mufti. Mara hii alikuwa ameonyesha mtindo mwingine unaoitwa 'love at night' yaani 'mapenzi wakati wa usiku'. Kweli ulitisha kwani mwili wa ndani wa Lulu ulikuwa ukionekana kabisa. Kitambaa cha vazi hilo kilikuwa kama kioo. Ungeweza kuona ndani bila taabu hata kidogo. Umati mzima ulipiga kelele, na watu hawakuweza kuinua macho yao, maana kama unataka kujipatia taabu wewe mwangalie huyo mtoto kwenye jukwaa.

Kwa sababu mimi nilikuwa na mashaka sikuwa kipofu. Niliangaza huko na huko. Ghafla nikasikia mtu anaanguka nyuma yangu huku ameshikilia bastola karibu kufyatua. Watu hawakutambua maana kila mtu macho yake yalikuwa kwenye jukwaa. Nilipoangalia nyuma niliona mtu huyo amekufa kwa kupigwa risasi. Kabla sijakimbia toka hapo, na bado Lulu anavutia watu kwenye jukwaa. Sammy alipita na kuniangushia kijikaratasi. Niliangaza nione Benny alipo sikumwona. Kwa hiyo niliharakisha kutoka kwenye maiti hiyo na kukimbia hadi nilipoketi awali kabla ya mtu yeyote kunitambua.

Lulu alichukua muda mrefu kwenye jukwaa, hivyo alinipa muda wa kuweza kurudi na kukaa bila mtu kutambua. Kwani wakati huo Lulu bado anawapa watu wote moto kiasi cha kutojitambua.

Nilikaa na kusoma kikaratasi hicho. Utashangaa nikikueleza. Mtu huyo aliyepigwa risasi nyuma yangu nilidhani ni mmoja wa vijana wa Robin kumbe hapana. Huyo mtu alikuwa anakuja kuniua mimi. Maana walikuwa tayari wametambua kwamba nitakuwa nikichunguza mienendo ya Benny. Kwa hivyo walimkonyeza Benny. Naye Benny akapanga namna ya kuweza kunitupilia mbali. Mtindo wao waliotumia ni ule ule. Benny anampa ishara yule kijana wa kwenye jukwaa alafu kijana huyo anamtoa Lulu nje. Kisha Lulu anapofika kwenye jukwaa, anatia watu wote moto kiasi cha kutojitambua. Ndipo watu wa Benny wanapopata muda wa kuua mtu wao wanayemtaka bila kutambuliwa wakitumia bastola iliyo na kiwambo cha kuzima mlio.

Mpango huo huo ndiyo uliotumika kwa kutaka kuniua. Lakini bahati nzuri Sammy alishikwa na mashaka. Wakati Lulu alipotokeza aliniona mimi nimekaa mahali wanapoweza kunidhulu vizuri sana. Kwa hiyo yeye aliweka macho yake yote kwangu. Kumbe alikuwa sawa. Jamaa mmoja alitokea kwenye mlango mmoja unaotokea chooni ili aje animalizie mbali. Basi alikuja taratibu. Alipofika karibu alitoa bastola ili kufyatua. Kumbe Sammy naye alikuwa ameishamtilia mashaka akamuwahi kabla ajafyatua. Alikufa papo hapo bila mtu yeyote kutambua na Sammy akapita mahala pangu na kunitupia hicho kikaratasi bila kutambulikana. Kisha tukaenda mahali petu bila kutambuliwa.

Benny aliingia kutoka nje wakati Lulu alipokuwa akitoka kwenye jukwaa akirudi kwenye chumba cha kubadilishia mavazi. Benny aliponiona alishtuka sana. Rangi yake ikambadilika. Nywele zikasimama na jasho likamtoka. Akaenda moja kwa moja upande wa chooni. Nilimwangalia kwa usili sana alipoiona hiyo maiti ya mtu wake, akajiuma vidole na kwenda zake kwenye kundi, ndipo watu wakaigundua maiti hiyo.

Polisi waliitwa mara moja kila mtu akaanza kuulizwa ulizwa. Mapolisi walianza kukagua waone iwapo alikuwapo mtu mwenye bastola. Siye tulifahamu kuwa jambo linaweza kutokea hivyo bastola zetu tulikuwa tumeshampa mmoja wa vijana wa Robin na alikuwa ametoroka nazo tayari.

Huyo kijana wa kwenye jukwaa alipoulizwa na polisi kama alimuona mtu upande huo, mara moja alinitaja mimi. Polisi walinijia kuniuliza.

"Wewe ni nani?"

"Mimi ni Joe Masanja, mwandishi wa habari za maonyesho ya mavazi toka Mwanza,"nilijibu.

"Kwa nini ulikuwa umesimama upande ule wakati maonyesho ya mavazi yakiendelea, na hali watu wengine wote walikuwa upande huu?"

"Mimi kama mwandishi wa habari, niko huru kusimama mahali popote ninapoona ni pazuri kuwezesha kutazama mambo yote na kuandika kwa ufasaha." Nilimwambia huku nikionyesha hasira kidogo.

"Je ulimuona mtu yeyote akipigwa risasi karibu na wewe?"

"Hapana."

"Je, maiti hiyo ilikuwepo wakati ulipoenda kusimama pale?"

"Hapana."

Walianza kunikagua na wakanikuta bila ya silaha yoyote. Yule kijana wa kwenye jukwaa alikuja akaulizwa kama aliniona nikiwa na mtu yeyote hapo pembeni, akasema hakuona.

"Je, ulirudi wakati gani mahali pako, yaani hapa ulipo sasa?" waliendelea kuuliza.

"Nilirudi baada ya kuandika mambo yangu ambayo nilikuwa nahitaji."

"Kama dakika ngapi hivi zilizopita?"

"Sikutazama saa lakini ni wakati huyo msichana aliyeonyesha mtindo 'Love at night' alipokuwa akiingia tu kwenye jukwaa."

Waliniacha wakaendelea na kuhoji watu wengine. Sammy alikuwa ameniponyesha tena, la sivyo ningalienda kumsalimia babu yangu huko ndani ya udongo.

Maonyesho yalifungwa mpaka kesho yake saa kumi. Hii niliona itatupa muda wa kufanya kazi kama wakichaa. Na niliapa lazima nimpate Benny na vikalagosi vyake kabla hajafaulu kunitupilia mbali. Maana mara mbili sasa ninaponea chupuchupu.

Watu walipokuwa wakitoka mimi nilikuwa nikimvizia huyo kijana wa kwenye jukwaa. Alipotoka tu nikamfuata. Huku nikimuacha Sammy na Robin waendelee na uchunguzi mwingine. Huyo kijana aliingia kwenye gari na kuanza kuondoka. Alikuwa peke yake humo garini. Mimi nilichukua gari moja niliyokuwa nimefanya mipango na idara ya uchunguzi waniletee. Nilipotoka tu nikakuta kijana mmoja tayari ameileta hiyo gari. Gari hiyo ilikuwa ya aina ya 'Zephyr 6' ambayo hukimbia sana. Niliweka gari moto nikamfuata huyo kijana. Nilihakikisha kuwa sifuatwi, ila tu Peter ndiye alipita karibu yangu nikampungia mkono.

Huyo kijana aliendesha gari yake kuelekea pande za Pangani, kwa hiyo nami nilielekeza gari langu huko huko. Niliacha magari matatu hivi mbele yangu kusudi asije akawa na mashaka akiona gari linamfuata katika kila kona aliyokuwa amepita. Lakini nilihakikisha kuwa sitampoteza.

Tulipofika kwenye nyumba za ghorofa za Pangani, huyo kijana alikwenda mpaka kwenye nyumba moja ya ghorofa na kusimamisha gari lake na kutoka nje. Mimi nilihisi kwamba hapo ndipo alipokuwa akikaa. Saa hizo giza lilikuwa limeishaingia hivyo nami nikasimamisha gari langu katika sehemu moja, halafu nikaenda kumvizia huyo kijana. Alipanda mpaka ghorofa ya tatu. Akafungua mlango wa chumba kimoja na kuingia ndani. Wakati huo mimi nilikuwa nimesimama hapo chini nikimwangalia. Kisha na mimi nikapanda mpaka ghorofa ya tatu.

Ghorofa hiyo ilikuwa na vyumba vitatu, yaani jamii tatu zilikuwa zikiishi kwa kila mmoja. Nilipochunguza, niliona kuwa watu katika vyumba vingine hawakuwemo. Watakuja wakati gani, hiyo haikuwa shida yangu wakati huo. Nilichungulia kwenye chumba cha huyo kijana nikamuona akiwa amekaa kwenye sofa hali akivuta sigara. Alionekana bayana kwamba hakuwa na furaha hata kidogo.

Nilibisha kwenye mlango, na nilipokuwa nikifanya hivyo, nilikuwa nikimchungulia kwa dirishani. Kabla hajaja mlangoni akaonekana kubabaika sana hata sigara kumdondoka toka mdomoni. Alijiachia huku na huku kisha akafungua kabati lake la nguo. Akapapasa katika mfuko wa koti moja na kutoa bastola! Ndipo akaja mlangoni kunifungulia huku ameshika bastola hiyo mkononi. Naona hata yeye alikuwa akihisi kuwa lazima lilikuwepo jambo.
 
Sura ya Sita

Alipofungua mlango tu nikaupiga teke mkono wake uliokuwa umeshikilia bastola. Bastola hiyo ikaanguka kama hatua tatu hivi upande mwingine wa chumba. Nilikuwa nimeishatoa bastola yangu na kuiweka tayari mkononi. Alitaka kupiga kelele, lakini nikamuonyesha bastola, kwa hiyo akafunga akanyamaza.

"Funga hilo domo lako, la sivyo ukilipanua tu, risasi zote zitamalizikia ndani yako."

"Jina lako nani?" Wakati huo nikimuuliza tumeishaingia ndani na huku nimefunga mlango. Nilipomuuliza hakujibu. Kufumba na kufumbua wakati nikigeuza kidogo macho yangu upande mwingine akaipiga teke bastola yangu. Nayo ikaanguka mahala pengine. Hapo hapo akanitia ngumi moja mpaka nikaanguka chini.

Nilipokuwa nikiribu kusimama, akanitia nyingine, mpaka chini. Kweli huyu kijana, anajua kuzipiga, maana ngumi zake zinatoka mfululizo kama nini. Alipogeuka kuchukua bastola nilijikunja na kumpiga 'Farasi teke' mgongoni mpaka akaanguka chini. Nilisimama upesi upesi, na kabla yeye hajasimama nilimtia teke moja la usoni mpaka akaona nyota na kuzirai.

Nilimwendea hapo chini na kumsukumasukuma. Kisha nikaiendea bastola yangu na kumsogelea. Alipoanza kupata fahamu nilianza kumuuliza tena. "Jina lako ni nani?"

"Naitwa James, na wapenzi wangu huniita Jim, lakini wewe sitaki uniite Jim maana ni adui yangu. Tangu nizaliwe sijapigwa na mtu namna ulivyonipiga wewe kwa hivyo niite James, koroboi we."

"Unamfahamu Benny?"

"Ndiyo"

"Tangu lini"

"Kwa muda wa mwezi hivi."

"Kwani umekaa hapa Nairobi kwa muda gani?"

"Yapata miaka kumi sasa."

"Na kama Benny pia anakaa humu humu mjini mbona mlikuwa muda wote hamjafahamiana?"

"Kwani wewe unajua watu wote wa Mwanza?" alinijibu kwa jeuri sana.

"Nani amekuambia natoka Mwanza?"

"Lulu na Benny"

"Kwa nini ulimbadilisha Lulu kutoka kwenye jukwaa kabla ya zamu yake?"

"Hiyo ni kazi yangu si yako. Unataka nini?" alisema kwa wasiwasi hali akitazama dirishani."

"Nilipotupa macho nyuma kuangalia mlango ulifunguliwa na kijana mwingine akaingia ndani huku ameshikilia bastola mkononi. Nilijipindua mara moja na kumweka James juu yangu. Kisha nikasimama naye huku nimemfanya ngao yangu.

"Eh, kumbe una akili za kutosha." alisema huku sauti yake ikigundagunda.

"Jaribu, na kabla ujaniua mimi utakuwa umemuua James kwanza. Si ajabu hiyo?"

"James hana thamani sana akifa zaidi ya kifo chako. Kilivyo na thamani!" alijibu huku uso wake umekunjamana.

Ghafla nilimsukuma James na kumwangukia mwenzake na hapo wote wakaanguka chini. Kabla hawajasimama nilipiga teke mkono ulioshikilia bastola. Kisha nikaanza kuwapa kazi. Kijana huyo aliposimama nilimpiga kichwa mpaka chini. James akatupa ngumi lakini nikaepa. Nilimtia kichwa mpaka akatabawali. Maana alikuwa bado na maumivu ya magigano ya kwanza. Huyo kijana akabeba kiti na kunitupia lakini nikawahi kukidaka. Nilimtwanga kwa kiti hicho kichwani na kumfanya apepeseke mpaka ukutani. James alikuwa hawezi kusimama sasa ila kubaki akikoroma tu. Kijana huyo mwingine akaniwahi kwa ngumi moja kwenye shavu. Loo! mikono yake ni kama chuma, jino langu moja likanitoka. Hasira zilivyonipanda Mungu ndiye ajuaye. Maana sijawahi kupingwa ngumi mpaka jino likatoka. Kutokana na hiyo hasira nikamtia ngumi tatu mfululizo. naye akawa kama James.

Kwa bahati nikaiona kamba hapo ndani. Kabla hawajapata fahamu, niliwafunga pamoja kwa ustadi sana kisha nikafuata maji ya barafu na kuwamwagia. Walipopata fahamu nilivuta kiti nikakaa huku nimeshikilia bastola yangu mkononi.

Tuue basi unangoja nini?" alisema huyo kijana mwingine.

"Nitauaje watu waliokwisha kufa wenyewe?" nilijibu.

"Maana ya kutufunga hivi kama magunia ya kauzu ni nini?" aliuliza James.

"Maana nimeona nyinyi ni watu hatari sana."

"Sasa nadhani utajibu maswali yangu James maana utani sasa umekwisha. Jina langu ni Willy, Willy Gamba, wa Idara ya upelelezi ya Tanzania lakini ambayo inafanya kazi bega kwa bega na Idara za namna hii katika Afrika nzima." niliposema jina langu, kila mtu alitoa macho ya woga.

"Kama ni Willy Gamba, nitajibu maswali yako yote, sina njia nyingine. Lo! Kunaonekana kuna makubwa hapa mjini mpaka wakakuleta wewe. Maana nimeishasoma habari nyingi juu yako na vituko vyako vyote. Sina njia, uliza tu. Niko chini ya miguu yako," alijibu James.

"Mimi sikujua kama ni Willy na kama ningalijua nisingethubutu kukufuata." alisema huyo kijana mwingine.

"Nani alikutuma kunifuata?" nilimuuliza.

"Benny, ndiye alinituma."

"Kwa nini alikutuma kunivizia?"

"Alisema kuwa wewe unaonekana mwenye kuingilia mipango yake na hivyo lazima uuwawe mapema, kusudi mipange iweze kufanyika kesho usiku."

"Mipango gani hiyo?"

"Sijui, na hakunieleza zaidi."

"Wewe ni nani wake mpaka akutume kuniua.?"

"Mimi nimeanza kumfanyia kazi tangu juma lililopita, sababu najua kutumia bastola. Nimewahi kuwa jeshini kwa muda."

"Alikwambia kwa nini anataka mtu kama wewe?"

"Ati kwa sababu yeye ana pesa nyingi."

"Unamfahamu Lulu?"

"Ndiyo."

"Ni nani?"

"Ni mpenzi wa Benny."

"Tangu lini?"

"Sijui"

"Benny alipokuwa akikutuma Lulu alikuwepo?"

"Ndiyo"

"Lulu alisema nini juu yangu?"

"Naye alisema kama Benny tu, ila aliongezea kuwa lazima nikuendee vizuri maana unaonekana kuwa mtu mbaya sana."

Kisha nilimgeukia James, "Jim mpenzi, jibu swali langu ambalo nilikuuliza kabla kikaragosi cha Benny akijatuingilia."

"Hebu uliza tena"

"Kwa nini ulibadilisha wakati wa Lulu kuja kwenye jukwaa?"

"Kwa sababu niliona ishara toka kwa Benny."

"Ishara gani uliona?"

"Alishika na kurekebisha tai yake."

"Ulijuaje kuwa hiyo ni ishara ya kukuambia ubadilishe wakati wa Lulu kutoka?"

"Benny alikuwa ameniambia kuwa kuna watu wanaomtafuta, na yeye ni lazima awafutilie mbali kabla wao hawajafanya hivyo, na tena alisema kwamba anashughuli zake ambazo anataka ziishe kabla ya kesho kutwa asubuhi. Hivyo akanipa pesa ili nimfanyie kama alivyokuwa akitaka. Ati kwa sababu Lulu alikuwa akichukua mawazo ya watu, aliona kuwa akitaka wauwawe wangeweza kuuawa bila watu kujua nani amewaua."

"Kwa nini hukukataa?"

"Kwa sababu angeweza kuniua hata mimi, ndiyo alinitisha."

"Ulimuona mtu aliyemuua yule mtu aliyekufa pale ukumbini."

"Hapana sikumuona, lakini nilifikiria wewe unajua."

"Kwa nini ulichukua bastola nilipogonga mlangoni."

"Kwa sababu nilikuwa na wasiwasi juu ya mambo niliyokuwa nimeambiwa na Benny."

"Huwa unakaa na bastola hapa kwako, ama umepewa leo tu kuitumia.?"

"Nilipewa na Benny niitumie iwapo nitafuatwa na mtu yeyote."

"Kuna mtu mwingine yeyote anayeshirikiana na Benny?"

"Sijui hajaniambia lakini nafikilia huenda yupo, maana baada ya Lulu kuingia kwenye jukwaa leo, Benny alienda kupiga simu."

"Kuna watu wangapi waliotumia hiyo simu leo tulipokuwa kwenye maonyesho?"

"Ni Benny tu niliyemuona"

"Nambari ya simu aliyotumia Benny ni ngapi?"

"Una maana alikokuwa akipiga ama ile aliyokuwa anatumia?"

"Nina maana zote."

"Alikokuwa akipiga sijui, lakini ya mle mwenye 'hall' ni 21899."

Niliwambia wafunge midomo yao, mpaka baada ya siku mbili hivi. Nilionelea niwaache hivyo ningemwambia Robin aje awachukue awaweke ndani kwa siku mbili hivi."

"Haya wajomba, kama mnataka usalama fanyeni kama nilivyowaambia, na ujanja wowote, mnaweza kujikuta mko ndani zaidi. Na ndipo mtalia na kusaga meno." Niliondoka nikawapigia Sammy na Robin simu. Nilimweleza Robin juu ya hawa watu na jinsi ya kuwafanya. Akasema angefanya kama nilivyomwambia. Na pia akanieleza anahisi kupata fununu ya jambo fulani kwa hiyo lazima nimwone asubuhi hotelini kwake mnamo saa tatu hivi. Pia nilimweleza kuwa sasa naenda kumwona Lulu na nikamwambia Sammy apige huko hotelini kwa Lulu simu itimiapo saa nne hivi. Na kwamba ikifika saa nne na nusu bila ya kuniona aje huko hotelini kwa Lulu, huenda nitakuwa nimo msambweni.

Nilipiga simu kwenye Idara ya Uchunguzi nikawaeleza wanitafutie nambari za simu ambako simu ilipigwa kutoka kwenye simu nambari 21899 mnamo saa kumi na mbili na nusu. Na wakasema hiyo ni kazi rahisi. Pia niliwaambia wanipe jina la mtu mwenye simu hiyo, wakasema pia kuwa hilo lisinitie shida ni kazi ndogo.

Basi hatimaye niliondoka kwenda Hoteli Intercontinental. Nilipokuwa naingia nilimkuta Peter na Wazungu fulani fulani pamoja na wapigania uhuru wengine wakinywa kahawa katika chumba cha kahawa. Aliponipungia mkono nikaenda kuwasalimu. Nilikuta Wazungu wote hao walikuwa Marekani na walikuwa wanatoka katika Baraza la Umoja wa Mataifa, kwenye sehemu inayoshughulika na Afrika Kusini. Ilionekana walikuwa wamekuja kwa mazungumzo na wapigania uhuru.

Walininunulia kahawa, baadaye Peter na hao wageni wake iliwabidi waondoke wakalale maana walikuwa wamechoka. Nilimwuliza Peter kama amemwona Lulu, akasema alimwona akiingia ndani, lakini hajatoka nje. Pia nilimwuliza kama kuna mtu mwingine yeyote aliyekuwa ameingia na Lulu, akasema hakumwona yeyote. Basi tuliagana wao wakaenda zao miye Willy, nikakaza roho kupanda chumbani kwa Lulu.

Vijana wa Robin walikuwa wameishapata hata nambari za chumba cha Lulu. Nilienda moja kwa moja mpaka kwenye kile chumba. Lakini kwanza nilihakikisha hakuna mtu aliyeniona huko juu.

Hoteli Intercontinental ni nzuri sana na ghali. Na kama wee ni 'giriki' nusunusu huwezi, na msichana Lulu anatisha maana mtu wa kukaa katika hoteli hiyo lazima awe 'giriki'hasa. Hiyo ninaweza kusema kwamba Lulu ni 'giriki' hasa, ila sivyo asingeweza. Maana wanawake wengine wote wa kwenye maonyesho hata waliotoka ng'ambo ni yeye tu anayekaa hapa. Na kama kuna mtu aliyempangishia, lazima huyo mtu awe na pesa si mchezo. Na hii nadhani ndiyo ilikuwa kweli hasa, maana Lulu alikuwa msichana mrembo hasa. Mtu yeyote mwenye fedha angemfanyia lolote analotaka. Ninaamini kwamba, Lulu akikuambia wende ukamwibie fedha ili awe wako, Wallah utakubali ufungwe ikiwa utashikwa, lakini ukaibe.

Nilipofika kwenye kile chumba niligonga mlango. Ulifunguliwa na Lulu huku akitabasamu "Karibu ndani, mbona unakuja kunitazama usiku hivi? Nadhani mchana lingelikuwa jambo zuri zaidi." Alikuwa akisema maneno yote haya huku amenishikilia mkono mpaka kwenye sofa.

"Uh, naweza kukusaidia?"

"Maonyesho yako yamenipendeza sana mpaka imenibidi nije nikupe heko usiku huu," nilijibu. "Asante sana Joe nimefurahi kuwa umeweza kupendezwa na maonyesho yangu ukiwa kama mwandishi wa habari."

"Loo! Unakaa kwenye hoteli ghali sana Lulu, lazima baba yako awe tajiri sana."

"Hata, baba yangu ameisha kufa, na mama yangu pia."

"Huenda hata baba yako alikuwa tajiri sana, kuwa amekuachia mali nyingi sana. Na huenda kaka zako matajiri sana."

"Kaka yangu alikuwa mmoja tu, lakini alikufa huko Kampala kwa bahati mbaya baada ya kupigwa risasi wakati wa msukosuko kati ya Serikali na Kabaka. Halikuwa kosa la askari maana yeye mwenyewe ndiye alikuwa akizagaa mjini. Sasa niko peke yangu, na baba yangu hakuwa tajiri ila alikuwa anakijishamba kidogo cha kahawa tu, karibu na Kampala.

Tuseme maonyesho ya mavazi ndiyo yanayokuhifadhi kiasi hiki, eti?"

Aah Joe, unataka kuingilia katika maisha yangu? Nadhani ulikuwa ukija kunipa heko kama ulivyosema, lakini inaonekana sivyo. Nadhani utanibusu ukinipongeza!" Alisema kwa sauti ya mshangao sana.

Alisogea karibu yangu akanivuta. Akafungua tai yangu akaingiza mkono wake ndani ya shati langu na kisha akanibusu.

"Nimekupenda sana Joe, tangu nilipokuona siku ya kwanza katika Starlight Klabu. Oh! Sijui kwa nini sikuweza kukuona mapema."

"Kwani sasa unaye mpenzi wa kukuzuia usinipende?"

"Ndiyo nimeisha mpata, na naona siwezi kumwacha," alijibu huku akionyesha huzuni.

"Ni nani huyo?"

"Benny, yule niliyemfahamisha kwenye maonyesho."

"Tangu lini mmeanza mapenzi?"

"Tangu jana."

"Jana! Usinieleze, jana tu mmeisha ahidiana kuoana?"

"Kwani ni ajabu?"

"Mlikuwa mnafahamiana zamani?"

"Ndiyo, nilipokuwa nikija huku mara kwa mara alikuwa akinichukua katika gari lake."

"Ndiye amekupangisha katika hoteli hii naona."

"Ndiyo, Benny ana fedha si mchezo."

Kwa muda sote tukawa kimya. Kisha nikafumbua midomo,
"Samahani Lulu, ninasikitika kuwa nina jambo la kukuuliza," nilisema taratibu huku moyo wangu ukipiga upesi, maana hata mimi sikupenda kumchukiza msichana Lulu.

"Uliza tu Joe."

"Kwa nini katika maonyesho ukiwa kwenye jukwaa kunatokea mauaji wakati huo huo?"

Aligeuka rangi, nywele zikamsimama. Alikuwa anafunguwa vifungo vya shati langu, akaacha. Alikuwa akinibusu, akaacha! Na hapo hapo midomo yake yenye joto ikiwa baridi. Kisha akajibu " Mimi sijui, maana huwa niko kwenye jukwaa."

Mbona leo wamekubadilisha zamu yako na kutoka mapema? Na ulipotoka tu yakatokea mauaji, hasa wakati watu wakikushangilia?"

"Wewe ni nani mpaka uulize mambo kama hayo? Wewe si Polisi, waachie Polisi, waje wauulize. Sitaki maswali kama hayo. Na kama ndiyo yaliyokuleta humu toka kabla hujajisikitikia kwa nini unauliza maswali kama hayo."

"Sisi waandishi wa habari ni wazungumzaji wa mambo mengi kwa hiyo usijali. Kama hupendi hilo swali sasa nikueleze jambo jingine."

"Jambo gani," alisema huku macho yake yakionyesha hofu tupu.

"Kabla ya maonyesho hayajaanza Benny alikuwa akizungumza na wewe. Na akakueleza kuwa wanataka kuwaua watu fulani fulani. Kwa hiyo wewe utaambiwa uende kwenye jukwaa baada ya zamu kubadilishwa na James, Kijana wa kwenye jukwaa ambaye angepata ishara toka kwake. Kisha wewe utatoka kwenye jukwaa na kuwatia watu moto kwa mikogo yako ya ajabu. Halafu wao watapata muda kwa kuua bila kutambuliwa."

Alianza kutetemeka baada ya kusikia mambo hayo,"Mbwa wa Kishenzi we, nani alikuambia mambo hayo yote? Na kwa nini, unaingilia mambo yasiyokuhusu. Toka humu kabla hujawa maiti." Aliposimama alikuwa ameisha toa bastola iliyofichwa katika gauni lake kifuani, chini ya matiti.

"Toka, toka nje ya chumba changu la sivyo utakufa. Pilipili usiyokula inakuwashia nini?"

Nilimjibu huku nikicheka, "Wasichana wazuri kama wewe, hawafai kuwa na bastola, hebu iweke bibie, huenda tutazungumza vizuri kidogo."

"Unadhani natania, nakuua sasa." Kabla hajafyatua bastola yake, nilikuwa nimeishashika mkono wake. Nikaupinduapindua vizuri sana. Nikaichukua bastola yake na kuiweka ndani ya mfuko wangu wa koti.

"Mama Joe aliniambia usiwadhuru wasichana wazuri bure. Sasa nieleze uhusiano wako na mauaji haya. Na kama hutasema, miye nina ushaidi kamili wa kuweza kukupeleka mahakamani na ukahukumiwa kutiwa kitanzi."

Mlango ulifunguliwa na Benny akaingia pamoja na vijana wengine wanne, wote walikuwa wameshikilia bastola mkononi. Lulu alikimbia mpaka kifuani kwa Benny.

"Aha, mpenzi naona umeniletea zawadi nzuri sana, maana nilikuwa nimejaribu kuipata nimeshindwa." "Ahsante sana Lulu mpenzi."

"Wananchi waheshimiwa wenzangu, nadhani hamtastaajabu nikiwafahamisha kwa Willy Gamba, Mpelelezi maarufu sana katika Afrika hii. Anafanya kazi katika Idara ya Uchunguzi Tanzania. Naamini kila mtu anamjua kufuatana na usomaji wa habari zake katika magazeti ingawaje si kwa sura. Leo tunafurahi kuwa ndani ya mikono yetu na tunaweza kumfanyia lolote lile."

Alipokuwa akitoa hii hotuba yake fupi, niliona rangi za wengine wote zimebadilika sana hasa ya Lulu, na walionyesha mshangao mkubwa sana.

"Willy, ulikuwa mjinga sana ulipodhani umetufunika kwa kutumia jina la Joe Masanja kwamba ungeweza kutupumbaza! Lakini ujue kuwa kundi letu ni kubwa. Na lina watu wa aina nyingi na hata watu wenye vyeo vikubwa sana serikalini . Kwa vile kupata habari za aina yoyote ni rahisi sana. Hata John alipokuja hapa alijifunika kwa jina la Fred, tulijua mapema zaidi ya tulivyokufahamu wewe."

"Kwa nini ulimwua John?" Nilimwuliza.

"Kwa sababu alikuja kuingilia mipango yetu, jambo hata wewe hilo hilo muda si mrefu."

"Nilicheka hapo kidogo halafu nikamweleza, "Unadhani unaweza kusalimika na tendo hilo? Unajidanganya sana Benny. Ninakusikitikia kijana kama wewe kufa katika umri mdogo kama huu."

"Si mara yangu ya kwanza kufanya jambo kama hili, na nina akili zaidi yako na fedha zaidi ya kila mtu hapa Afrika ya Mashariki hasa itakapofika kesho kutwa nitakuwa na maelfu ya fedha. Na unajua kila siku fedha zinaweza kuponyesha mtu, kwa hivyo sitadhurika hata chembe. Najua nikiisha kukuua wewe sasa hakutakuwa na kizuizi katika mipango yangu," alisema kwa dharau sana.

"Hizo karatasi ziko wapi Benny?" Niliuliza.

"Hilo siwezi kukuambia, maana hata hawa wengine hawajui zilipo ila mimi tu."

"Lakini jua kuwa ukiniua mimi hapa, Lulu atashikwa sasa hivi maana watu wote wanajua niko hapa kwake," nilimwambia nilipotazama saa yangu na kuona karibu saa nne u nusu Sammy anipigie simu.

"Eh, unadhani miye ni mtoto katika kazi hii! Huwezi kunidanganya kwa jambo hili hata kidogo, maana hata mimi nimewahi kutishia watu na uongo wa namna hiyo !"

Alipotaka kuendelea kusema simu ililia, Lulu alienda kuijibu. Kisha aligeuka na kusema kuwa ilikuwa simu yangu. Benny alionyesha kuchukia kabla ya kusema, "Haya kaijibu tusikie utaongopa nini, mbwa we."

"Hallo, huyu ni Willy," nilijibu. "Oh, fanya hivi, kama usiponiona kwenye dakika tano hivi hapo basi, piga simu polisi uwajulishe habari yangu, na kwamba waje mpaka katika hiki chumba," niliendelea kusema.

"Ndiyo ndiyo, kumbe wengine wapo hapo chini, haya waambie hivyo. Asante sana kwa heri mpaka tutakapoonana kwenye dakika tano hivi," nilimaliza.

Wakati nikijibu simu, Benny, Lulu na wenziwe walionekana wamechukia sana. Tangu walipoingia wale vijana wanne walikuwa wameshikilia bastola zao tayari kufyatua baada ya kuamriwa tu na Benny. "Unasemaje mpenzi Benny, utaniua ama unaniachia huru niende zangu? Maana ukiniua tu utashikwa mara moja, kumbe hata polisi wengine wako nje ya hii hoteli," nilisema huku nikisimama taratibu kabisa.

"Oh, tutaonana siku nyingine Benny, na siku hiyo tutakapoonana si kama ambavyo tumeonana kirafiki hivi," Ilionekana hawakuwa na njia ila kuniachilia huru tu.

"Na wewe Lulu, siku nitakapokupata nitakupa siafu kwenye hayo mapaja yako wayaumeume, kusudi uweze kujikuna ovyo hata mbele ya baba mkwe wako,"

"Huwezi kuudhi mwanamke namna hiyo, na nitahakikisha kuwa unakufa kabla ya kesho jioni," alisema Lulu huku chuki imemjaa.

Alamsiki nyiye wote, niliondoka na kufunga mlango nyuma yangu.
 
Sura ya Saba

Nilitelemka taratibu kabisa mpaka chini. Hapo chini sikumkuta mtu yeyote, licha ya Sammy niliyetegemea kumuona. Niliingia katika gari yangu mpaka hotelini kwa Sammy. Nilimkuta Sammy akisoma gazeti liitwalo. 'The Detective' nilimweleza mambo yote niliyoyapata kutoka kwa Lulu

Sasa tulianza kuelewa mambo yote yalivyo, "Inaonekana Lulu ameingizwa katika mpango huu kusudi amsaidie Benny katika mambo fulani fulani. Mojawapo likiwa kama yale aliyokuwa akiyafanya maonyeshoni. Laiti isingekuwa sababu kama hiyo basi Benny asingefanya mapenzi na kupoteza fedha nyingi kwa Lulu. Pia tulianza kutambua kuwa Benny siye 'Bosi' ila 'Bosi' mwenyewe yupo', na Benny ndiye msaidizi wake.

Hivyo zile karatasi anazo 'Boss'. Na anayemjua huyo 'bosi' ni Benny peke yake wengine wanadhani 'Bosi' ni Benny.

Kwa hiyo kazi kubwa sasa ni kutafuta kwa kila njia tumjue huyo 'bosi' ni nani. Na kwa kufuatana na habari nilizozipata kwa James, hizo karatasi zitabadilishwa kesho usiku.

Jambo jingine ambalo lazima tuchunguze ni mahali ambapo mabadilishano ya karatasi hizo yangefanyika. Kwa kuwa wamekwishajua kuwa tunafanya kazi juu ya jambo hili, wanaweza wakaharakisha mambo zaidi na wakazibadilisha hizo karatasi haraka iwezekanavyo. Kwa hiyo nasi inatubidi tufanye kazi haraka kusudi tuweze kuzipata hizo karatasi kabla ya wao kuwapa hao watu, na kabla hawajalipwa.

Haya ndiyo mawzo yangu niliyokuwa nayo. Sammy pia alionekana kuwa na mawazo kama hayo. Tulimpigia Robin simu, tulimweleza juu ya mambo yote tuliyokuwa tunafikiri. Robin alisema, "Ninaona mawazo yenu ni sawa. Walakini inafaa mnipe wasaa maana mimi na vijana wangu tunaanza kupata fununu ya jambo fulani."

Sammy alitoa wazo kuwa yeye ataenda kuchunguza katika ile nyumba ya Benny kama anaweza kupata habari yeyote, kusudi mimi anipe nafasi nilale. Lakini mimi sikukubaliana naye niliona miye ndiye niende, na yeye akiona sirudi, anaweza kuja kunitazama huko. Maana kila siku tunapokuwa tukifanya kazi na Sammy, miye huenda kwanza tukijua ni mahala penye hatari na yeye huja nyuma. Na mara nyingi hii imefanya kuokoa maisha yetu.

Sammy alisisitiza kuwa, kwenda kule peke yangu kunaweza kuwa na maana ya kifo, kwa hiyo ni afadhali twende sote pamoja. Lakini bado niliona hili si sahihi. Mwishowe alikubaliana nami kuwa mimi niende kwanza halafu yeye aje baadaye,baada ya muda kama wa saa moja hivi.

Nilirudi hotelini kwangu nikabadilisha nguo. Mara hii nilichukua bastola mbili, moja ile yangu ya kawaida, '45 automatic' na ya pili ndogo kiasi cha kalamu ya wino. Hii ya pili niliisukuma kwenye mkunjo wa chupi niliyovaa.

Halafu nikanywa bilauli moja ya maji na whisky. Kisha nikaandika kijikaratasi cha kumwachia Lina, maana nilikuwa namtegemea usiku ule saa sita. Alikuwa amenipigia simu kuwa huenda angalikuwa na jambo kamili ambalo lingeliweza kunisaidia, wakati huo. Ghafla nikajiwa na wazo nimpigie Lina simu, nimweleze kuwa sintokuwepo ila nitaenda kufanya uchunguzi kwenye nyumba ya Benny.

Hii ingenisaidia mambo fulani fulani. Kwanza kama nikimpigia simu Lina, na kama Lina ananicheza yuko upande wa Benyy nitakuta Benny yuko tayari ananingojea maana Lina atamweleza hizi habari. Pili Lina amewahi kuwa mpenzi wa Benny kwa hiyo anafahamu kila kona ya kile chumba. Kwa hiyo anaweza kunipa muhtasari wa jinsi nyumba ilivyojengwa na jinsi vyumba vilivyokaa na hakuna uwezekano wa kufichwa vitu vya siri. Mwanamke..... japo siku moja tu ukikaa naye atakuwa amejua wapi hutaki aende na wapi unataka aende. Basi nilimpigia simu Lina.

"Hallo huyu ni Willy, habari Lina?"

"Salama tu Willy, mbona unanipigia simu na hali nimekwambia nitakuja? maana mpaka sasa nangojea simu toka mahali fulani ambayo inaweza kukusaidia sana."

"Oh. unafanya kazi vizuri kabisa Lina. Sababu ya kukupigia simu ni kwamba ninatoka. Naenda kufanya uchunguzi kwenye nyumba ya Benny, kwa hivyo nilitaka unipe muhtasari wa nyumba ilivyokaa, na jinsi ninavyoweza kuingia ndani kwa usalama bila kuzuiliwa."

"Lakini Willy, maahala hapo ni pa hatari sana. Mimi nilipopita karibu na mahali hapo niliona baada ya kuchunguza sana kuwa pamejaa walinzi. Na wote wako tayari kuua mtu yeyote atakayeenda hapo. Miye nilifanya uchunguzi huo nilikuwa huko 'Sclaters hosteli' na niliambiwa hivyo na msichana fulani ambaye ni shemeji ya Benny. Aliniambia kuwa Benny alikuwa amemwambia asiende pale leo maana pana hatari. Na kuwa ingekuwa salama kwake kama angebaki hostelini. Kwa hivyo mimi naona usiende, utahatarisha maisha yako bure tu, tafadhali."

"Hapana Lina, lazima niende. Na wewe njoo kwenye chumba changu ifikapo saa sita hivi. Nadhani bado una ufunguo niliokupa. Wakati huo nina uhakika kuwa nitakuwa nimerudi. Na kama nitakuwa sijarudi jua basi kumetendeka jambo. Sasa nipe huo muhtasari basi."

"Sikiliza Willy, nyumba yenyewe ina vyumba vitano sebule ya sita; choo, bafu na jiko. Vyumba vya kulala vine. Kile cha sita ni namna ya maktaba, maana huwa mna vitabu vingi sana na wageni hawaruhusiwi kuingia humo maana ndipo anatunzia bastola zake na hata za rafiki zake. Nyumba hiyo ina milango mitatu ya nje. Mmoja nyuma kutokea kwa 'Nakuru road'. Upande usio na mlango ni ule wa kulia, ambao unapakana na 'Scrates hosteli,' ila una dirisha moja kubwa la kutosha mtu kuingia kwa dirishani.

Unapoingia utaangukia ndani, utakuwa katika chumba kimoja cha kulala lakini hakina mtu sasa, maana yule shemeji yake ndiye alikuwa akilala humo. Vyumba vyote vya nyuma ni vya kulala. Benny analala kwenye chumba kinachofuata hicho chenye dirisha, mkono wa kushoto wa hicho. Chumba kinachotazamana na mlango wa mbele ukiwa sebuleni, ndicho hicho nilichokueleza, kinachotumiwa kama maktaba. Unataka nikueleze nini tena mpenzi!"

"Hayo yanatosha Lina, asante sana. Kama nikirudi salama ndipo nitaweza kutoa shukrani kwa udhati mbele yako. Hapana shaka tutaonana. Kwa heri mpaka hapo." nilijitengeneza sawasawa, mara hii nilionekana kama mpelelezi haswa mwenye cheti cha kuua.

Nilitoka nje nikaingia ndani ya gari yangu, nikaelekea Westlands. Nilipokuwa ninaenda niliona gari kama mbili zinanifuata kila ninapopita. Nilipofika karibu na 'Klabu 1900' nilisimama. Hizo gari mbili zilikuja zikanipita. Nilipoangalia nikagundua kuwa katika gari la mbele mlikuwa na vijana wawili ambao niliwaacha chumbani kwa Lulu na Benny. Katika gari la nyuma mlikuwa na yule kijana niliyemrudisha wakati akitufuata nilipokuwa na Lina katika gari lake. Nao walienda wakasimama mbele yangu.

Niliwasha gari langu moto nikaenda kulisimamisha na magari mengine hapo klabu 1900. Halafu nikangoja, wale jamaa nao wakaja wakasimamisha magari yao hapo nje kisha wote wakatoka na kuingia klabu 1900. Walidhani mimi nimetoka na kuingia humo, maana nilipokuwa nikizimisha gari langu kijana mmoja naye ndiyo kwanza anawasili hapo, alitoka katika gari lake na kuingia ndani. Alikuwa amevaa koti kama langu, na ni mrefu kama mimi, kwa hiyo walidhani ni mimi. Kisha nilitoka katika gari langu, nikaenda kwenye magari yao, nikapiga risasi magurudumu yote manne ya kila gari, yakawa hayana kazi alafu nikaenda katika hiyo klabu ambamo niliwakuta wote watatu wamekaa huku wakiangaza macho huku na huku. Nilienda nikakaa kwenye meza moja nao alafu nikawaambia,"Tafadhalini wazee, mimi sitaki kufuatwa fuatwa, na kama mkizidi mtaona cha mtema kuni. Mimi nilikuwa nikija hapa kunywa na nyie mnanifuata tu. Sasa nitawaacha hapa, na ninarudi kunywa mjini, na yeyote atakayenifuata nitamwadhiri vibaya sana." kabla hawajajibu niliondoka na kurudi kwenye gari langu. Nililitia moto na kuondoka halafu nikaenda kusimama hatua chache nione kama watatoka.

Kitambo walitoka, na kuingia katika gari zao. Walipowasha wakakuta magurudumu hayana upepo yote. Walitoka na kuanza kuzungumza. Miye Willy nikaweka gari langu moto, kuendelea na safari yangu.

Niliondoka hapo kwa mwendo mkali mno. Nilipofika kwenye ile nyumba nikapunguza mwendo. Nikasimamisha gari mbele ya Sclaters hosteli karibu na miti. Hlafu nilianza kurudi kwa miguu, taratibu. Nilikuwa nimeacha koti langu katika gari, halafu nikavaa kijambakoti, ambacho kinanifanya mwepesi zaidi.

Nilienda nikavuka Sclaters hosteli kisha nikaangaza macho yangu mbele ya nyumba hiyo nikaona watu wawili wakizungukazunguka hapo mbele. nikaenda kuchungulia upande wa nyuma pia nikaona kuna walinzi, kama Lina alivyosema. Nyumba yote ilikuwa giza maana hamkuwa na mwangaza hata sebleni. Basi nilikata shauri nifanye kama Lina alivyosema Hapo nikaanza kumsifia Lina kwamba yu mwenye akili hasa. Na kwamba angefaa sana kufanywa mpelelezi.

Nilienda nikaruka seng'enge, nikawa nimeisha anguka ndani ya seng'enge. Lakini mmoja wao alisikia namna ya kishindo kwa hiyo akaja upande ule wangu. Nilijibanza kwenye ukuta. Aliposogea karibu nikamtupia kisu shingoni. Hatimaye mtu huyo alikufa bila mtu kujua.

Nilipanda mara moja kwenye ukuta, nikakwea taratibu bila kufanya kelele yeyote, mpaka nikashika kwenye dirisha. Hlafu nikatoa tochi yangu na kumulika ndani ya chumba. Nikaona kulikuwa kumelala mtu kwenye kitanda huku ameshikilia bastola mkononi alikuwa amesinzia. Alionekana kana kwamba anataka kuamka lakini kabla ajaamka nilimtia kisu shingoni pia. Akawa hoi bila kutoa sauti. nikaanguka kwenye kitanda bila sauti kutoka kwenye dirisha.

Mlango wa hicho chumba ulikuwa umefunguliwa, kwa hiyo nilitoka nje ya chumba hicho bila kufanya kelele hata kidogo. Nilijaribu mlango wa pili yake ambao Lina alisema ndimo Benny alikuwa akilala, nikakuta umefungwa. Nilichukua funguo yangu malaya nikafungua, nilipopiga tochi mle ndani nikakuta hakuwemo mtu. nilienda kwenye kimeza cha karibu na kitanda, nikaanza kutafutatafuta vijikaratasi vyovyote vya maana lakini sikuona. Ila nilipata karatasi moja ya simu imeandikwa kwa kimombo. 'TELL THE BOSS TO MAKE SURE IT WON'T BE LATER THAN TUESDAY AT 10:00 P.M BECAUSE WE ARE EXPECTING THEM TO LEAVE THAT NIGHT AND BE HERE THE NEXT MORNING.' Fasili yake kwa kiswahili 'umwambie 'BosI' kuhakikisha kuwa Haitazidi jumanne saa nne usiku, maana tunawategemea kuondoka usiku huo na wawe hapa asubuhi ifuatayo"

Nilitoka kwenye hicho chumba na kufungua mlango nyuma yangu kisha nikaharakisha kwenda sebleni, kutafuta mlango wa maktaba. Maana nilikuwa nafikiRi kama Lina alikuwa anasema kweli, basi huenda humo ndimo mngepatikana mengi.

Niliingia sebuleni, bahati mbaya nikajigonga kwenye kiti: Yule kijana aliyekuwa mbele ya nyumba alishtuka. Niliweza kumuona sababu mlango ulikuwa wa vioo. Alikaa kidogo huku anaangaza macho ndani, nadhani kwamba alifikiri alikuwa yule mwenzake aliyekuwa amelala mle chumbani, lakini mwishowe alikata shauri ahakikishe, kwa hiyo alifungua mlango.

Mimi nilijibanza kwenye ukuta, alipoingia na kutaka kuwasha taa, nilimmulika na tochi machoni na hapo hapo nikatupa kisu, kikapambana naye kifuani. Kumbe na yeye alikuwa amefyatua bastola yake, na wakati alipoanguka tu, bastola yake ikafyatuka na kutoa sauti.

Wale walinzi wawili wa nyuma, walikimbia kwenye mlango wa mbele. Miye nilikuwa tayari nimekwishajibanza na bastola yangu nikiwangoja. Nilisimama kwenye 'swichi' ya taa kusudi wasije wakawahi kuwasha taa. Walipoangalia nje bila kuona lolote, walifungua mlango na kuingia ndani. Mmoja aliyekuwa mbele alitaka kuwasha taa hapo hapo nikaziachia risasi. Bastola yangu ilikuwa na kiwambo kwa hiyo haikutoa sauti. Yule wa nyuma akiwa bado anashangaa pia alizipata risasi.

Mara hii sikuwa na mchezo, madhihaka yote yalikuwa yamekwisha. Nilikuwa nimeishawachukia hawa watu kama kufa, hasa kwa sababu ya mauaji ya John. Kwa hiyo hata mimi sikuwa na huruma hata kidogo. Inaonekana kulikuwa na walinzi kama watano hivi na wote nilikuwa nimewafyeka kabisa.

Nilipiga tochi yangu sebleni, alafu nikakimbia kwenye mlango wa maktaba nikafungua na funguo zangu malaya. Nikaingia ndani halafu nikajifungia na kuanza kupekuapekua. Mlikuwa na vitabu vingi sana. Mlikuwa na masanduku ya vyuma yote yakiwa yamejaa vitabu. Nilifungua kabati moja la chuma, nikaona mlikuwa na bastola kadhaa pamoja na risasi. Pia niliona bahasha moja ambayo ndani yake mlikuwa na barua. Juu yake ilikuwa imeandikwa Dr. Dickisoni Njoroge.

Nikiwa bado naendelea na upekuzi wangu bila kufanikiwa kupata chochote nilichokuwa nikikitaka, nilisikia mlango wa maktana unafunguliwa. Zilikuwa zimepita dakika kumi. Na nilikuwa nimeweka dakika kumi na tano tu kuwa kwenye nyumba hiyo, kwa hivi zilikuwa zimebaki dakika tano. Na Benny alikuwa ameisha niwahi kabla sijaondoka.

Nilijificha nyuma ya kabati hilo la chuma. Alipofungua aliwasha taa, hakuwa Benny ila kijana mwingine. Aliangaza huku na huko bila kuniona. Lakini mwishowe niliona akija upande wangu. Nilitoa kisu changu, kabla hajageuka, nikampata mgongoni, akaanguka bila hata yowe! Nilikimbia mlangoni. Nikaangaza sebuleni ambamo sasa taa zilikuwa. Sikuona mtu, nikakimbia mpaka kwenye mlango wa mbele, kabla sijatoka nje, nilipigwa kichwani mpaka chini.

Nilipozinduka nilijikuta nimefungwa kitini! Karibu yangu alikuwa Sammy pia amefungiwa kitini huku bado amezimia! Benny na Lulu walikuwa wamesimama karibu nami huku wakionekana na furaha sana.

"Naamini muda huu huna ujanja Willy, ninakuhurumia sana, maana kifo chako pamoja na rafiki yako kitakuwa kibaya na cha maumivu sana. Nami nitahakikisha kuwa mmekufa kwa taabu maana nyie mnaonekana watu wa ajabu sana, kumbe mambo yote waliyoandika juu yako ni kweli".

"Wewe umeniingiza hasara sana ya watu wangu, maana umeua sita, na huyu rafiki yako ameua watano wakati akijaribu kuja kukuokoa lakini na yeye ameangukia kwenye mkasa huo huo." Alisema kwa kujivuna sana.

"Sasa unadhani utafaulu kwenye mipango yako eti?"

"Kwanini nisifaulu, mpaka sasa yote yamekwisha kamilika, ila wewe tu na huyu rafiki yako ndiyo mlikuwa mnanipa taabu, lakini sasa hamtanipa taabu tena. Na sasa watu wangu wote watafanya sikukuu wakisikia wewe, John, na huyu anayeitwa Sammy amekufa".

"Umefahamje kuwa huyu ni Sammy?"

"Lo! Wewe ndiye umechelewa kweli, nimekwambia saa zile kuwa kikundi chetu hata polisi wenyewe wamo. Nitashindwaje kujua basi. Nyie kila siku mnadhani ndiye wenye kujua habari nyingi, lakini mimi nina habari nyingi zaidi yenu, na ninatumia akili zangu zaidi yenu nyie. Na pia nahakikisha kuwa sifanyi kosa hata moja".

"Hii mipango mmeianza lini, na nani aliwasaidia katika jambo hili maana nyinyi msingelijua wapi pa uhakika ziliwekwa hizo karatasi?"

"Bosi' aliniambia kwamba nisiwaeleze jambo lolote mpaka amri itakapotoka kwake, lakini kwa sababu miye sitaki kuwaona mnaishi tena, nimeleta madebe mawili ya 'Petrol' na vijana wangu watawamwagia na kuwawasha moto mpaka mtakapokuwa mmeungua na kubaki majivu."

"Unafurahi, kuchoma watu eh Benny, lakini kabla sijamalizika kabisa wakati nikiungua na wewe utakuwa umekufa." Nilijibu kwa dhihaka.

"Uh, unadhani natania, Amani. Lete hayo madebe ya 'Petrol' pamoja na kiberiti," aliita kwa hasira.


Wakati huo Sammy alikuwa ameisha zinduka akasema, "Wewe shetani mwanamke, siku moja nitakata kipande cha nyama katika mwili wako na kukifanyia sikukuu."

"Nyamaza mwehu we, utaikataja nyama yangu na hali utakuwa umeisha kufa?" Alisema huku akitabasamu.

"Naona hapa tutakufa kama wanawake Willy, lakini hata hivyo huyu mwehu atashikwa na kutiwa ndani, nitafurahi sana kumpokea huko chini, na lazima nitahakikisha kuwa atapata taabu mpaka kupata makao," alisema Sammy huku akionekana hajali lolote. Benny alitoa kicheko. Halafu akamwambia Aman atumwagie petrol.

Kabla hajamwaga Lulu alitoa oni, "Nadhani 'Bosi' atapenda kuwaona hawa washenzi wakiungua, kwa hiyo afadhali tumfuate aje ajionee hawa watu mashuhuri wa Serikali wakifa kitoto, na kifo cha aibu. Unaonaje Benny?"

"Lakini lazima tuache ulinzi wa kutosha hasa. Mlango wa nyuma weka walinzi watatu. Huu wa mbele watatu. Na wengine kuzunguka nyumba, halafu kwenye mlango wa chumba hiki watatu pia. Naamini hata kama angekuwa malaika hawezi kutoroka kwenye ulinzi wa namna hii."

Wazo wako ni zuri sana Lulu. Nadhani 'Bosi' atafurahi ajabu na atatufanyia sikukuu. Lakini nyie wote angalieni kuwa hamfanyi kosa hata kidogo. Kosa lolote mshahara wake ni kifo cha namna hii hii.

Nilimuuliza mlinzi mmoja aliyekuwa akifunga mlango wa chumba tulichokuwa, "Itawachukua muda gani kwenda kwa 'Bosi' na kurudi?"

"Kama dakika kumi hivi". alijibu na kisha akatufungia ndani. Halafu wakasimama pale mlangoni hali walinzi watatu wakiwa tayari na silaha zao.

Tulikuwa tumefungwa sana, hivyo kwamba hatukuweza hata kujitingisha. Walikuwa wametuvua nguo zetu zote isipokuwa chupi tu ajabu ni kwamba niliweza kusikia bado bastola yangu ndogo imo kwenye mikunjo ya chupi yangu. Jinsi ya kuitumia ilikuwa haifahamiki hata kidogo. Kuwa nayo na kutokuwa nayo yote yalikuwa mamoja. Na pia tulijua tungefanya upuuzi wowote kabla Benbny, Lulu na 'Bosi' hawajarudi tungeliteswa na hawa walinzi.

"Mara hii hatuna ujanja kweli Sammy."

"Hata mimi naona, maana sidhani kwamba kunaweza kuja mtu wa kutuokoa, na kama pia atakuja atakufa kabla hajafika humu ndani!"

"Mie nilikuwa siku zote natabiri kufa kwa risasi, maana pia nimeisha ua wengi kwa risasi".

"Hakuna njia Willy, ila huenda mizimu ya mama Sammy ifanye kazi yake. Unakumbuka tulivyopona safari ile kule Lusaka?"

"Ndiyo, nakumbuka, lakini ulinzi pale haukuwa mkali kama huu wa hapa".

Mawazo yangu yalirudi Dar es Salaam. Nilimfikiria mpenzi Della, moyo ukaniuma namna ya ajabu. Nilijua Della angeweza kujiua kama angesikia nimekufa. Nilimpenda naye alinipenda. Alikuwa msichana wa peke yake aliyechukua moyo wangu na ambaye nilichukua moyo wake. Kisha nikamfikiria mama Willy. Lo! Mimi nilikuwa mtoto wake wa pekee. Hakuwa na mtoto mwingine hata mmoja. Mama Willy nilijua atakapoambiwa tu, ataanguka chini na kufa. Nilijua jinsi mama alivyokuwa akinipenda.

Nilionekana kama mawazo yangu si sawa. Nilikuwa katibu nipate kichaa kwa kufikiri mambo kama haya. Kisha nilimsikia Sammy akisema, "Nimesikia kitu kama mlio wa bastola yenye kiwambo!.

"Unaota nini Sammy".

"Hapana, kweli nimesikia." Kisha nami nilisikia kishindo kwenye mlango kana kwamba watu wanaanguka.

Mwishowe nilimwambia Sammy kuwa huenda ni 'Bosi' anafika kwa hiyo watu wanamtolea njia.

Tulisikia mlango wa chumba ukifunguliwa. Moyo wangu uliruka kwani nilijua sasa mwisho wetu umefika. Maana "Bosi" amafika. Nilipomtaza Sammy niliona nywele zake zikisimama na rangi ilibadilika. "Wameisharudi! Alisema.

Mlango ulipofunguliwa tulishtuka kuona ni Lina ndiye anafungua mlango. Alikuwa ameshika bastola mbili mkononi. Akazitupa chini akaja kunifungua. "Harakisheni tutoke hapa mapema kabla hawajarudi, maana nasikia watarudi mnamo dakika mbili au moja unusu hivi."
 
Haya yalikuwamambo yetu mwaka 1984.

Aristablus Elvis Musiba. R.I.P

Asante sana.
 
Ikifika mwisho nitag, maana nyinyi waandishi wa riwaya munazingua.kuna yule alietupia riwaya ya mtutu wa bunduki,kala kona hadi leo unaingia mwaka wa pili hajaweka muendekezo.hayo ni matangazo ya vijarida vyenu
Ishafika mwisho mkuu
 
Back
Top Bottom