SIMULIZI; BALAA.
Mwandishi; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010
SEHEMU YA MWISHO
Paaaaaaaaaaa!
Ulisikika mlio mkali wa bastola hewani. Kila mtu alipigwa na butwaa bila kujua nani kapigwa risasi ile, wote walijua kwamba Don Genge ndiye kafyatua risasi ile.
Haikuwa hivyo!
Ilikuwa ni bastola ya askari makini wa kike, inspekta Jasmine iliyopigwa hewani. Ndio iliyofanya kazi ile ya kuokoa uhai wa Mwanasheria mlevi. Kabla hata akili za watu pale hazijatulia, ghafla eneo lote lilizungukwa na askari Polisi. Ama hakika, kundi la Six killers walikuwa wamewezwa kisawasawa. Don Genge akiwa na bastola yake mkononi alitulia tuli, kidole chake cha shahada cha mkono wa kulia kikiwa bado kimeigusa triga ya bastola yake, ilikuwa afyatue ili afyatuliwe! Don Genge aliwaangalia askari wale lukuki kwa zamu. Akajua mwisho wake umefika, mwisho wa mchezo wao mchafu umefika. Sasa alitafuta namna ya kujiokoa. Hakuwa tayari kuingia katika mikono ya Polisi.
Tokea palepale mlangoni aliposimama aliruka sarakasi za kinyumenyume kurudi ndani ya nyumba ya bluu!
Askari wote walibaki mdomo wazi, hawakutegemea kabisa kutokea kitendo kile. Bila kujiuliza mpelelezi Daniel Mwaseba alitoka kasi kukimbilia mle ndani, huku akifuatwa kwa nyuma na Songelael Ntenga au Mwanasheria mlevi.
Pale nje Moja, Tatu na Nne waliwekwa chini ya ulinzi imara wa askari Polisi, wakafungwa pingu. Wakawekwa chini ya ulinzi wa askari kumi kuwalinda, huku askari wengine wakiizunguka ile nyumba ya bluu aliyoingia Don Genge. Wakihakikisha Don Genge hana pakutokea. Askari walichanga karata zao vizuri sana.
Kule ndani Daniel Mwaseba na Songelael Ntenga walifanya msako wa nguvu. Walitafuta kila chumba, walitafuta kila mahali, Daniel Mwaseba alipanda hadi darini lakini Don Genge hawakumuona! Ilikuwa kama hakuingia mle ndani. Daniel Mwaseba hakukubaliana na ukweli kuwa Don Genge alikuwa ameyeyuka! Atayeyuka vipi?
Askari thelathini waliingia ndani ya nyumba ile, walipekua sana, lakini majibu yalikuwa yaleyale. Hakukuwa na Don Genge mle ndani. Walianza kuwatesa mateka wao ili wawaambie mahali atakapokuwa amejificha Don Genge. Hakuna aliyethubutu kusema. Wote walijibu kijeuri, wote walikuwa sugu!
Hawakuwa na namna nyingine, wale kina Moja walipelekwa kituo cha polisi. Walionesha mahali walipowaficha watu waliowateka lakini hawakuonesha mahali alipo Bosi wao, Don Genge. Walikubali kuwataja wale madaktari wote waliohusika katika mpango huu wa BALAA lakini sio Don Genge, hawakumtaja kabisa. Manesi na madaktari wote walikamatwa kama vifaranga vya kuku. Ilikuwa rahisi sana. Hawakuwa na mbinu zozote za kuwazidi kina Daniel Mwaseba.
Baada ya mwezi mmoja wale wahalifu wa Six killers na madaktari wote walihukumiwa kifungo cha maisha katika mahakama kuu kanda ya Kusini iliyopo huko Mtwara. Haikuwa kesi ngumu sana, wahalifu wote walikubali makosa yao. Ilimshangaza kila mtu.
Suala la kupotea kwa Don Genge likabaki kitendawili kisicho na majibu. Wapo walioamini kuwa yule mtu katili kabisa alikuwa mchawi. Aliingia mle ndani na kuyeyuka! Lakini mawazo hayo hayakupata nafasi katika kichwa cha Daniel Mwaseba, hayakupata nafasi katika kichwa cha Songelael Ntenga, hayakupata nafasi katika kichwa cha Dokta Yusha, wote walikula yamini lazima wahakikishe wanamtia mikononi Don Genge, bila ya kujua watampata kwa namna ipi?
HUU NI MWISHO WA HADITHI YA BALAA SEHEMU YA KWANZA.