SIMULIZI: BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010
SEHEMU YA SABINI NA NANE
Tano wa Six Killers alikwenda mzima mzima kumvaa Daniel Mwaseba. Daniel Mwaseba alimuona vizuri sana, alikuwa ameshajipanga vizuri kimapambano, Daniel alisogea pembeni kidogo, Tano alipita moja kwa moja kwa kasi kubwa sana na kwenda kuuvaa ukuta.
Ebwana ee!
Alijigonga vibaya sana usoni. Dakika hiyohiyo uso wa Tano ulivimba na kutoa kitu kiitwacho nundu katikati ya paji lake la uso! Tano alipata maumivu yasiyo na kifani, alitumia nguvu nyingi sana kwenda kumvaa Daniel Mwaseba.
Tano wa six killers hakuweza kustahamili maumivu aliyokuwa anayapata, alianguka chini mzimamzima.
Danielle Mwaseba hakumuonea huruma kabisa. Sasa angalau kidogo alishayajua madhara ya Tano. Hakutaka kumpa mwanya wa kufanya chochote. Alimfata kwa teke la nguvu palepale chini alikokuwa amelala. Teke la kiume lililotua barabara katika kifua cha Tano, Tano alitoa mguno hafifu wa maumivu na kuanza kutoa madonge mazito ya damu mdomoni.
"Nakufaa"
Tano alisema kwa sauti dhaifu, ama hakika alikuwa amepatikana hasa.
Daniel Mwaseba alimjibu, alimjibu kwa teke kali sana la uso. Daniel alikuwa na huruma sana kwa raia wema. Lakini kwa bahati mbaya hakuwa na huruma kabisa kwa wahalifu kama Tano.
Uso mzima wa Tano ulitapakaa damu. Tano alijikusanya pale chini, akijitahidi kuvuta pumzi zake za mwisho. Daniel Mwaseba aliinama pale chini alipokuwa amejipweteka Tano, alimshika koromea kwa mkono wake wa kulia. Tano macho yalimtoka pima!, Daniel Mwaseba alimkaba kiasi kwamba alishindwa hata kumeza mate, ama kumeza damu ambazo ndizo zilikuwepo mdomoni mwake.
"Six killers ni nini?" Daniel Mwaseba aliuliza kwa nguvu akiwa anaangaliana na Tano.
"Hata nisi-po-kwambia uta-ni-fanya n-ini, mi-mi ni mfu ta-ya-ri, nifa-nye utakacho si-kwa-mbii ki-tu"
Daniel Mwaseba akajua yule jamaa amegoma kusema. Alimwacha pale, akasogea kwenye kabati lililokuwa ukutani, akafungua na kutoa mkoba wake. Alitoa kamba za katani, kamba alizotumia kumfunga vizuri sana Tano miguuni na mikononi, hakutaka kumuua, alitaka kujua vitu kwanza toka kwa yule jamaa. Alimwacha kamfunga vizuri tano na kutoka nje ya kile chumba. Hakwenda mbali sana Daniel, alijibana sehemu akiangalia kitatokea nini pale mlangoni.
Kwa jinsi Tano alivyofungwa kamba zile na kwa hali aliyokuwa nayo, mimi na wewe tusingeweza kufungua zile kamba. Lakini Tano wa Six killers hakuwa mimi na wewe. Tano alikuwa nunda kweli. Tano alikuwa mjuaji, Tano alikuwa jambazi mahiri, Tano alikuwa mbabe, Tano alikuwa mtemi. Tano alikuwa sugu!
Daniel Mwaseba akiwa amejibanza katika mpenyo katika korido ya nyumba ile ya kulala wageni alishangaa kuuona mlango wa chumba chake ukifunguliwa na mtu kutokea ndani...
ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA