Uchunguzi wa timu maalum ya wanahabari iliyoundwa kuchunguza mazingira ya mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari mwakilishi wa kituo cha televisheni ya Channel Ten, mkoani Iringa, marehemu Daudi Mwangosi, umethibitisha kwamba, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, alisimamia moja kwa moja mauaji ya mwanahabari huyo.
Kadhalika, timu hiyo imebainisha kuwa polisi kwa makusudi waliwashughulikia waandishi wa habari wa mkoa huo wakati wakikusanya habari za shughuli za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani humo, Septemba 2, mwaka huu.
Timu hiyo iliyoundwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), pia imebaini katika uchunguzi wake kuwa marehemu Mwangosi aliuawa mikononi mwa polisi chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Kamanda Kamuhanda.
Ripoti ya timu hiyo iliwekwa hadharani na Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, katika mkutano kati ya MCT, TEF, baadhi ya wajumbe wa timu hiyo na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.
Timu hiyo iliongozwa na Meneja wa Utafiti na Machapisho wa MCT, John Mirenyi, huku wajumbe wengine wakiwa ni, Hawra Shamte, Mhariri wa masuala ya Siasa wa gazeti la Mwananchi na Simon Berege, Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Kitivo cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma.
Mukajanga alisema matokeo ya uchunguzi huo yanathibitishwa na maelezo pamoja na ushahidi uliokusanywa kwa kutumia picha za video, za mgando na ushahidi mwingine muhimu wa taarifa za vyombo vya habari.
source: Nipashe leo