Richmond yaibukia Uganda

Kimbembe

Senior Member
May 14, 2006
122
15
Richmond yaibukia Uganda

Waandishi Wetu Machi 5, 2008SAKATA ya kampuni hewa ya kufua umeme wa dharura, Richmond Development LLC, ya Marekani, limevuka mipaka na kujadiliwa nchini Uganda katika mkutano wa wataalamu wa hali ya hewa, ambao wanasema kwamba Serikali ya Tanzania haikuzingatia ushauri wa wataalamu kwa wakati.

Ofisa Mwandamizi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) amelieleza RAIA MWEMA kwamba, sakata hilo limeibuka baada ya kuwapo taarifa kwamba Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza Richmond, ilizingatia taarifa za wataalamu wa hali hewa.

“Wataalamu na wadau walioshiriki mkutano uliofanyika Entebbe, Uganda, waligusia suala la Richmond kwa kuwa ni wao waliotoa taarifa za mfululizo kuanzia mwaka 2002 wakitahadharisha kuwapo kwa ukame katika maeneo mbalimbali ikiwamo sehemu kubwa ya Tanzania lakini wakashangaa kusikia suala hilo kwa Tanzania lilionekana kuwa la dharura,” alisema ofisa huyo.

Katika ripoti yake bungeni, Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, iliweka bayana kwamba serikali inapaswa kuzingatia taarifa za wataalamu wakiwamo wa hali ya hewa ili kuepuka kufanya mambo kwa mtindo wa dharura kama ilivyokua kwa suala la Richmond.

Kamati hiyo katika uchunguzi wake, Desemba 5, 2007 ilimhoji Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Mohamed Mhita, ambaye alibainisha wazi kwamba kamati yake imekuwa ikiwasilisha serikalini taarifa zote na baadhi ya taarifa hizo zimekuwa zikinukuliwa vizuri katika vyombo vya habari.

Alipoulizwa wanakopeleka taarifa zao, Dk. Mhita alieleza kamati hiyo kwamba wanapeleka katika idara zote serikalini ikiwa ni pamoja na Ikulu (kupitia Idara ya Usalama wa Taifa), Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Kilimo na pia kupeleka moja kwa moja kwa watumiaji wengine na wananchi kupitia vyombo vya habari.

Dk. Mhita alibainisha pia kwamba mbali ya kuwasilisha taarifa hiyo, wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja katika hatua zote na wataalamu kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Idara ya Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu ambao imefahamika kwamba wamekuwa wadau wakubwa wa TMA wakati wote.

Maelezo hayo ndiyo yaliyozingatiwa pia na washiriki wa mkutano wa kutoa mwelekeo wa hali ya hewa kwa kipindi cha Machi hadi Mei mwaka huuu, wakisikitishwa na jinsi Serikali ya Tanzania ilivyopatwa na mtikisiko katika jambo ambalo halikupaswa kuwa la dharura.

Ofisa mmoja wa TMA aliliambia RAIA MWEMA jana Jumanne kwamba taarifa iliyotolewa na wataalamu Machi 2005 na ile ya Septemba mwaka huo, iliikuta Serikali nzima ikiwa katika joto la Uchaguzi Mkuu huku baadhi ya wataalamu nao wakiwa washiriki wakuu wa harakati hizo kwa namna moja au nyingine ambao walikuwa wametelekeza ofisi zao.

“Taarifa tulizozitoa Machi 2005 na ile ya Septemba 2005 zilizoelezea bayana kuwapo kwa upungufu wa mvua katika maeneo mengi ya nchi, ziliwakuta viongozi na watendaji wetu wakiwa busy (katika harakati) za uchaguzi na walipokuja kuzinduka ilikua Februari 2006 wakati mambo yamekwisha kuharibika na hakuna mtu aliyekumbuka taarifa,” alisema.

Ofisa huyo ambaye amewahi kushiriki mikutano mingi ya hali ya hewa, aliliambia RAIA MWEMA kwamba pamoja na udhaifu wao mwingi wa kiutendaji na kimaadili, rais mstaafu, Benjamin Mkapa na Waziri Mkuu wake, Frederick Sumaye, walizingatia taarifa za utaribiri za mwaka 2003 na 2004 kwa kutenga fedha na mikakati ya kukabiliana na ukame ulioikumba nchi mwaka 2004.

“Mwaka 2004 hata Bwawa la Mtera lilifungwa kwa muda lakini hakukua na mgawo wa umeme na wananchi hawakupata shida ya chakula baada ya Serikali kuwasilisha bungeni maombi ya fedha za ziada ambazo zilitumika kuisaidia Tanesco na Hifadhi ya Taifa ya Chakula (SGR) kwa hiyo Serikali mpya ilijikuta haijajipanga ilipoingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2005 na mwanzoni mwa 2006. Nadhani hili ni fundisho kubwa kwetu,” anasema.

Katika Mkutano wa Entebbe, pamoja na kutabiriwa kuwapo mvua za wastani katika maeneo mengi ya nchi, bado kuna hatari ya kuwapo uhaba mkubwa wa mvua kutokana na kuwapo kwa mabadiliko makubwa ya joto katika Bahari ya Pacific inayoashiria kuwapo kwa hali ya La Niña, ambayo husababisha upungufu mkubwa wa mvua katika maeneo mengi ya Pembe ya Afrika, Tanzania ikiwamo.

Sakata la Richmond lilisababisha kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na mawaziri wengine wawili, waliowahi kuongoza Wizara ya Nishati na Madini iliyoshiriki katika mchakato wa zabuni ya mradi wa Richmond. Mawaziri hao, Dk. Ibrahim Msabaha, ambaye alikwisha kuhamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki na aliyechukua nafasi yake, Nazir Karamagi.

Katika utetezi wao, wote watatu walielezea hali ya udharura kama sababu ya msingi ya kuharakisha bila umakini kuingia mkataba wenye utata na kampuni ya Richmond Development LLC, ambayo haikuwa na uhalali wa kisheria kuwapo nchini, na ambayo ilibainika kutoa taarifa za uongo kwa Serikali na umma kupitia nyaraka na tovuti.

Pamoja na kujiuzulu kwa wanasiasa hao, Serikali imekuwa katika shinikizo kubwa la kutakiwa kuwachukulia hatua watendaji wake walioshiriki kuibeba Richmond na mrithi wake Dowans ya Falme za Kiarabu na hatimaye kuwachukulia hatua za kisheria wote waliohusika wakiwamo wanasiasa waliojiuzulu.
 
Ina maana tangu 2002 watu walijua kuna kuja ukame? Kwa hiyo ile dharura kimsingi haikuwa dharura maana dharura ni kitu usichotarajia, usichojua ujio wake, na kisichokupa taarifa ya kujiandaa; kama ulikuwa na miaka miwili ya kujiandaa na dharura, kweli itakapokuja utaiita tena dharura?

Maana yake, mtu akiuona ufa kwenye ukuta wa nyumba yako na kukuonesha ufa ule na kukuambia usipouziba ukuta utadondoka; na wewe ukasuasua kuuziba na miaka miwili ukuta wa nyumba yako ukadondoka kutokana na ufa ambao ungeweza kuuziba mapema hata kwa makusudi kuvunja ukuta na kujenga mpya; je bado unaweza kuita kuvunjika kwa kuta ya nyumba yako ni tendo la dharura; ni udharura wa bahati mbaya huo au wa kujitakia?

Kama ni ule wa kujitakia unaotokana na ku"tosikiliza" au uzembe, je una haki ya kuita dharura!?
 
Mheshimiwa nkapa alikuwa hajui umuhimu wa wataalam akazembea kimbembe kikamkuta JK.
 
Mheshimiwa nkapa alikuwa hajui umuhimu wa wataalam akazembea kimbembe kikamkuta JK.


Halafu JK akaamua kutulangua Watanzania wote wakishirikiana na swaiba wake Lowassa.

Ambaye hakuelewa umuhimu wa wataalam na aliyetumia matatizo yaliyoikumba nchi kuanzisha wizi kwa staili ya Mafia wote wako kwenye kapu moja la ununda.

Au wewe unadhani J M Kikwete ni nunda nusu na Mkapa ni nunda kamili??
 
Back
Top Bottom