Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi leo asubuhi Alhamisi Januari 14, 2021 amewasili Chato kwa ziara ya siku mbili.
Akiwa Chato Dk Mwinyi na ujumbe wake watakuwa na mazungumzo na mwenyeji wao, Rais John Magufuli.
Baada ya mazungumzo hayo Dk Mwinyi atatembelea soko la kimataifa la dagaa la Kasenda na kuzungumza na wananchi na wafanyabiashara wa soko hilo.
Dk Mwinyi ametua katika uwanja wa ndege wa Geita-Chato na kupokelewa na waziri wa Nishati, Dk Merdad Kalemani na Waziri wa Uvuvi, Mashimba Ndaki.
Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad akiwa njiani kuelekea Chato ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa daraja la Kigongo -Busisi mkoani Mwanza, ambalo limepewa jina la JPM na kuwataka wananchi kulinda miundombinu yake.