Rais Jukumu lako la Msingi ni Kulinda Umoja wa Kitaifa

Msambichaka Mkinga

JF-Expert Member
Oct 22, 2015
1,649
2,911
Sikumbuki tarehe wala kikao gani cha chama lakini nakumbuka wakati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere akisisitiza dhana ya kukosoana ndani ya chama, aliwahi kutamka, 'Kukubali upungufu huu siyo kujidhalilisha bali ni kujiimarisha'.

Mheshimiwa Rais ukitaka kuwa kiongozi mzuri, imarisha na kuikubali dhana ya kukosolewa na kukosoa.

Kuwa na msimamo usiobadilika katika mambo yanayowatenganisha watu, siyo hekima, siyo uongozi na wala hakuna tija kwa kiongozi wala kwa anaowaongoza. Ukikubali kuwa kiongozi wa watu ni lazima uwasikilize unaowaongoza na kuna wakati utalazimika kufuata yale wapendayo unaowaongoza hata kama hutaki au pengine siyo sahihi. Kama kiongozi ukiona huliwezi hilo, achana na uongozi, ufanye kazi nyingine. Mzee Mandela wakati wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, hakutaka watumie nguvu katika harakati za kupinga ubaguzi lakini wajumbe walio wengi waliamua kuanzisha Umkondowesizwe (mapambano ya silaha). Kama kiongozi alilazimika kukubali na kuusimamie uamuzi huo, siyo kwa sababu alitaka bali kwa sababu wengi ndivyo walivyoamua.

Dahana ya Umoja Katika Ujenzi wa Taifa

Waafrika Kusini weusi, waliishi katika siasa za kibaguzi kwa miaka mingi. Walionewa, waliteswa, walifungwa na wengine kuuawa. Tuna watu maarufu kama akina Mandela, Sisulu, Mbeki, n.k. walionja shubiri ya utawala wa makaburu. Pia wapo waliouawa, waliotiwa vilema na ambao walipoteza ndugu zao. Lakini ilipofika wakati wa kutaka kuijenga Afrika Kusini, licha ya Waafrika weusi wale kujua kabisa kuwa walidhurumika sana wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi, walilazimika kukubali kukaa na watesi na wauaji wao, Makaburu. Wakaunda Tume ya Maridhiano, chini ya mpigania haki, kiongozi wa dini, Askofu Mkuu Desmond Tutu (kioja cha hapa kwetu eti tunaambiwa viongozi wa dini hawastahili na hawana haki ya kuzungumzia siasa, kuzungumzia uhuru wa watu, demokrasia au haki za watu). Waafrika wale hawakukubali kukaa na makaburu kwa sababu walikuwa wanyonge (tena walikuwa tayari wameshika dola), siyo kwa sababu walichokuwa wanakipigania miaka yote kilikuwa batili bali kwa sababu walijua huwezi kujenga Taifa kwa kustawisha utengano.

Hapo Kenya baada ya uchaguzi mkuu 2013, watu zaidi ya 2000 waliuawa. Wakenya waligawanyika sana. Uhuru akawa Rais wa Kenya. Alikuwa na nguvu zote maana alikuwa tayari na dola. Lakini alikubali kuwakaribisha au kuwaomba watu wengine wawasaidie kama wasuluhishi ili Wakenya waweze kusafiri pamoja katika safari yao ya maendeleo. Na uchaguzi wa mwakajana, uliwagawa Wakenya tena. Licha ya kuwa Uhuru alikuwa tayari Rais, bado aliona haja ya kuhakikisha anaungwa mkono na mpinzani wake mkuu Raila ili kusaidia kuwaunganisha Wakenya. Siyo kwa sababu alikuwa amezidiwa na Raila bali ni hekima ya kiuongozi. Unaongoza watu, wenye uwezo tofauti tofauti, fikra tofauti, matarajio tofauti, itikadi tofauti, makuzi tofauti, kuwaunganisha kunahitaji utulivu na hekima.

Uganda, licha ya ukweli kuwa Joseph Kony kiongozi wa Lord's Resistance Army, aliua watu wengi, kuteka na kuwatesa, bado kuna wakati Mseveni alilazimika kumwita Joseph Kony kwenye meza ya mazungumzo. LRA kilikuwa kikundi kidogo tu na Mseveni alikuwa na serikali, wananchi na jeshi.

Kuna mifano mingi ya namna hiyo ndani ya Afrika na nje ya Afrika. Ujumbe ulio muhimu ni kwamba jukumu kubwa na la kwanza, na ni kipimo kizuri kwa kiongozi mwenye hekima ni uwezo wake wa kuwaunganisha watu tofauti, walio na mitazamo na fikra tofauti lakini wakabakia wamoja kama Taifa. A leader must have ability to show a way and mobilize mass to rally behind him.

Mara nyingi Rais wetu umekuwa ukitamka kuwa maendeleo hayana chama, tushikamane kwenye mambo ya msingi, mambo yanayohusu utaifa wetu. Maneno hayo ni sahihi kabisa lakini jambo la msingi, wewe kama Rais unafanya nini ili Watanzania wote washikamane katika mambo ya msingi? Wakati wote kauli na matendo yako yanaonesha kiu ya kuwataka Watanzania wawe wamoja? Watu wanatakiwa waoanishe unachotamka, jitihada zako za kuutaka umoja, na matendo yako wakati wote wa utendaji kazi wako.

Kiongozi unastahili kuishi kiuongozi. Kuwa kiongozi ni kutangulia katika usahihi, kuonesha njia iliyo sahihi. Ukiwa kiongozi, akatokea mtu akakuambia kuwa, 'mpumbavu wewe', wewe kiongozi huwezi kujibu kwa kusema, 'mpumbavu mwenyewe'. Ukifanya hivyo waliokuchagua watatilia mashaka kama kiongozi wetu ana hekima au hana. Unaongoza watu wengi, wenye busara na wasio na busara, walio na subira na wale wa kukurupuka, wenye akili na wasio na akili LAKINI tunatarajia kiongozi wetu atakuwa ni mtu aliyetoka miongoni mwetu aliye na hekima, busara, subira, upeo wa kuona na kupima mambo, na kuwaonesha watu wake njia iliyo sahihi. Maandiko ya biblia yanasema kiongozi anastahili kuwa kama kijito cha maji katika ardhi kame na jiwe lenye kivuli katika jangwa. Kiongozi hustahili kuwa kama makaa ya moto kwenye mchanga wa moto.

Kuna mambo mazuri Rais ameyafanya, na hayo si lazima kuyasema maana ndiyo tunayoyatarajia kutoka kwa kiongozi. Ulichaguliwa ufanye yaliyo mema. Lakini kuna yale uliyoyafanya vibaya:

1) Kutodhibiti kauli kama kiongozi

Kwa mfano kauli ulizowahi kuzitoa juu ya wawekezaji wa nje waliowekeza Tanzania kuwa ni majizi, unaweza kufunga biashara zao, n.k. ndani ya wiki moja ziliyatia hasara makampuni mbalimbali ya nje kati ya 30-60% kwenye masoko ya fedha Duniani. Ni ngumu sana kwa kampuni iliyofiliskia Tanzania kwa kauli tu za kiongozi bila ya uthibitisho wowote kurudi kuwekeza Tanzania. Lakini hiyo imefukuza wawekezaju wengi wa maana waliokuwepo na kuwazuia wapya kuja. lakini pia ilijenga hofu hata kwa wawekezaji wetu wa ndani.

2) Kuna Tatizo la Sera za Kiuchumi

Mara nyingi unasema kuwa watu wanaolalamika kuwa vyuma vimekaza, walikuwa mafisadi. Hivi mama nitile aliyekuwa anapata mapato yake kwa kupika vyakula kwenye site za ujenzi, na sasa hana watu wa kuwapikia, alikuwa anamfisadi nani? Mwenye duka aliyekuwa akilipa kodi zote lakini leo mapato yake yameanguka kwa sababu wateja hakuna, ufisadi wake ni upi? Wenye mahoteli ambao leo hawana wateja, walikuwa mafisadi kwa namna gani? Waliokuwa mafisadi hasa, mpaka sasa si wanaopiga kelele wala siyo wanaumia hasa, japo yawezekana mapato yao yameanguka. Wanaohangaika na kukosa hela ya kula ni watu wa hali ya chini kabisa kama vile Mama nitilie na wanafamilia zao, mafundi ujenzi na familia zao, wenye maduka na familia zao, waliokuwa wafanyakazi wa mahoteli na wategemezi wao, wakulima ambao wameshindwa kuuza mazao yao kutokana na serikali kuingilia biashara ya mazao, n.k. Tukubali kuwa kuna mahali sera zetu za uchumi kwa sasa hazipo sawa. Mh. Rais usikimbilie kutoa majibu mepesi, tena ya kejeli kwenye tatizo halisia.

3) Kudharau Makundi ya Kijamii

La karibuni kabisa ni la jana ambapo ulisema maaskofu wanalalamika kwa sababu wamekosa sadaka na zaka. Lakini pia kuna kauli za ajabu dhidi ya washindani wako wa kisiasa na asasi za kirai. Kuna wengine ndani ya serikali yako, labda kwa ulevi tu wa madaraka, wamedirika hata kusema kuwa maaskofu hawaruhusiwi kuongelea siasa! Hapo juu nimemtaja Tutu, kiongozi wa kiroho aliyeshiriki kikamilifu katika vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na baadaye kuwa kiongozi wa Tume ya maridhiano. Tutu ameendelea kuikosoa serikali ya Zuma mpaka hivi karibuni kabla ya Zuma kuondolewa, tena kwa maneno makali ambayo hakuna kiongozi wa kidini hapa kwetu amewahi kutamka dhidi ya serikali au Rais. Jambo la kujiuliza, hao wanaosema viongozi wa kidini hawastahili kuongelea masuala ya haki, demokrasia na uhuru wa watu, wanasema eti wazungumzie masuala ya kiroho, hivi hizo roho zipo wapi? Roho tunaziona? Ni nini kinachoifikisha roho mbinguni/aheri au jehanamu? Nijuavyo mimi ni kwamba matendo dhidi ya mwili ndiyo huamua kama roho ya mtu itaurithi ufalme wa mbingu au itaenda jehanamu. Matendo dhidi ya mwili yanaweza kuwa ya uonevu au upendo, haki au dhuluma, kulinda uhai au kuondoa uhai, mateso au faraja, amani au chuki, umoja au utengano, n.k. Chochote kinachouhusu mwili huangukia kwenye HAKI VS DHURUMA, UTII VS UKAIDI, UGANDAMIZAJI VS DEMOKRASIA, UHURU VS UTUMWA, USIKIVU VS KIBURI. Unapomtendea mtu haki, ukampa uhuru, demokrasia na kutimiza yale mliyokubaliana kama jamii umefanya tendo takatifu. Unapomdhurumu, unapomgandamiza, unapomfanya mtumwa, n.k. unatenda kazi ya shetani. Kiongozi wa dini ni na muumini yeyote anatakiwa kupinga matendo na viashiria vyote vya ufuasi wa shetani. Kristo alikuja Duniani kuwatangazia watu uhuru na kukombolewa kwao kutoka kwenye utumwa wa shetani. Kwa kiongozi wa dini, hasa ya kikristo ambayo mimi naijua, kuukubali tena utumwa wa shetani baada ya kukombolewa ni kuifanya kazi ya Kristo kutokuwa na maana. Mungu mwenyewe mara kadhaa alisimama na wana wa Israel katika vita vya kujikomboa. Walipigana na Mungu aliwabariki katika hilo, yaani vita vya kuitafuta haki, kuutafuta uhuru. Pale walipopigana dhidi ya yasiyo haki, Mungu alijitenga nao.

Katika hoja ya nyaraka za maaskofu, badala ya kauli ya jumla ya kejeli, kama kiongozi mkuu ulistahili kujibu hoja zilizoainishwa, na pengine kwa kuzungumza nao ana kwa ana.

4) Maendeleo ya Watu

Mambo ambayo binadamu huyaangalia kwa haraka ni maendeleo ya watu na siyo maendeleo ya vitu. Tunahitaji barabara, tunahitaji reli, usafiri wa anga na majini, umeme, hospitali na maji, n.k. Hata ukiyafanya hayo yote lakini kama hutagusa mambo yaletayo unafuu wa moja kwa moja kwa maisha ya jamii, watu hawatayaona mazuri yote katika miradi hiyo mikubwa. Kama unajenga barabara, basi pia uangalie sera za biashara ili barabara hizo ziweze kuyabeba mazao na bidhaa nyingine na kuzifanya ziuzike na kuwapa wazalishaji kipato. Kama sera za uzalishaji hazimwezeshi mtu kuzalisha, hata faida ya barabara inakuwa ni ndogo. Nimeenda maeneo ya mkoa wa Njombe, vijijini debe moja la mahindi linauzwa shilingi 1,500. Mtu ametumia sh 5,000 kuzalisha, anauza kwa shilingi 1,500. Hivi mwakani atakuwa na uwezo wa kuzalisha tena? Hata kama utakuwa umemtengenezea barabara, hiyo barabara inakuwa na msaada mdogo sana kwake. Ni lazima kuwepo na uwiano mzuri wa kati ya economic development na human development.

5) Kufuata Katiba

Watanzania tumeamua kuwa nchi hii ni ya vyama vingi. Kwenye mfumo huo kuna haki na uhuru wa vyama vya siasa lakini pia kuna miiko yake. Wewe kama kiongozi yawezekana hupendi vyama viwe na haki hizo lakini Watanzania katika uwingi wao ndivyo walivyoamua. Huna mamlaka kama kiongozi kuyabadilisha hayo ili yaendane na matakwa yako. Unachotakiwa ni wewe kujibadilisha ili uikubali katiba maana umeapa kuilinda. Ndani ya katiba kuna haki za raia, unalazimika kuzikubali, kuzisimamia, na kuwa mfano katika kuzifuata maana wewe ni kiongozi. Ni jambo la kusikitisha sana unaposhindwa kufuata katiba maana ndiyo mkataba kati ya wananchi na wewe kama kiongozi wao.

6) Kupuuza Kelele za Unaowaongoza

Ukumbuke kuwa wakati wa awamu iliyopita kulikuwa na kelele nyingi dhidi ya rushwa na katiba. Kwenye rushwa, naamini kuna jitihada japo kwa upande mwingine kuna maswali mengi kama tunapiga vita rushwa au rushwa ya watu fulani tu? Rushwa ya dola imeonekana kumea kipindi hiki. Hili ni jambo baya sana. Kelele za katiba hazijakoma, haya ni matakwa ya watu toka awamu iliyopita. Kiongozi mwenye busara hawezi kupuuza.

7) Umadhubuti wa Kiongozi

Mara nyingi umesikika ukisema kuwa wewe ni Rais hasa, na mara nyingine umesema wewe ni Rais jiwe. Jambo la muhimu ni kuwa umadhubuti wa kiongozi haupimwi katika ubabe au matumizi ya vyombo vya dola bali hupimwa katika uwezo wake wa kuufanya umma mkubwa wakati wote kuwa nyuma yake. Hiyo ndiyo sababu ya viongozi wengi wenye busara katika jamii zilizostaarabika, wakihisi watu wanawapinga, wanaitisha kura za maoni ili wajue nyuma yao wana umma mkubwa kiasi gani. Mh. Rais nguvu na uimara wako uutafute kwenye umma na siyo toka kwa polisi au jeshi.

Yanaweza kusemwa mengi lakini la muhimu, ni kwamba Rais unatakiwa kuhakikisha Watanzania wanakuwa wamoja. Watu wanatakiwa kuwa na ownership ya nchi yao, wilaya zao, mikoa yao, na vijiji vyao. Kuna baadhi ya viongozi wako inaonekana hawana hata ile misingi ya uongozi. Kiongozi hastahili kutamka kuwa, 'mkoa wangu', mkoa ni wetu, nchi ni yetu, wilaya yetu, vijiji vyetu. Kiongozi hastahili kupandikiza kwa watu fikra za wao kuona mkoa, nchi au kijiji ni cha mtu fulani. Ukiwaondolea watu ownership, unawaondolea uzalendo.

Mwenye busara hujifunza kutoka kwenye makosa ya wengine.
Hivi na sisi tunataka tufikie walipokuwa wamefikia Wakenya au Waafrika kusini ndiyo tuunde tume ya maridhiano? Kwa nini hatujifunzi kutokana na makosa ya wengine. Tunashindwa kuwa proactive badala yake tunataka tuwe reactive?

Rais fanya kazi ya kuwaunganisha watu. Hivi ukiwaalika maaskofu, viongozi wa vyama vya siasa, taasisi za kiraia, wawakilishi wa bunge, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, watu mashuhuri kama marasi wastaafu, mkazungumzia uimarishaji wa umoja wetu, utapungukiwa na nini? Hivi kuna kiongozi yeyote anaweza kuukataa mwaliko wako?
 
Mleta hoja uko vizuri sana!! Lakini vijana wa uvccm watakupinga tu!! Kwa sasa wamepandikizwa kushabikia u dictator wa aina yoyote duniani !!. Wao wanataka tusifu na kuabudu

Utawala huu umeingia madarakani kwa kukamia kutetemekewa, na hapo ndipo penye shida.
Kwao kukaa pamoja na watu wenye mtazamo tofauti ni unyonge!! Bahati mbaya na wasomi wa nchi hii nao wameisaliti nchi kwa kukalia kimya utaratibu wa utawala na uongozi unaponajisiwa!!! Sijui ni uoga, umaskini, au ni unafki ambayo ni asili ya mswahili
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom