Rais haya ya sasa yatapita, utafika wakati wataizoea hali halisi mpya

Phillipo Bukililo

JF-Expert Member
Dec 29, 2015
18,488
13,608
Kuna wanaosema Mheshimiwa Rais angalau angesubiri mpaka apewe uenyekiti wa Chama ndio aongee kwa mamlaka na kuwakaripia wote wanajaribu kumfanyia fitina za chini kwa chini.

Wanaona kama vile maamuzi yake ya kulihutubia bunge yameongozwa na jazba zaidi kutaka kuwaonyesha mamlaka aliyonayo hao wenye kuongozwa na kumbukumbu za aliyemtangulia.

Wapo wenye kuona kuwa maamuzi ya kulihutubia Taifa muda huu ni sahihi, akilazimika kujitambulisha anasimamia nini na anatarajia ushirikiano upi kutoka kwa wasaidizi wake wa kila sekta.

Wazungu wanalo neno Nostalgia likimaanisha zile kumbukumbu anazokuwa nazo mtu kuhusiana na miaka ya nyuma. Yote aliyoyafanya Hayati JPM yameingia katika hadhi ya kumbukumbu, zinaweza kuwa ni nzuri kwa baadhi ya watu na zinaweza kuwa ni mbaya kwa baadhi ya watu.

Naamini wanaomsema mitandaoni Rais Samia bado wanaishi ndani ya kumbukumbu, lakini sekunde hazigandi, hakuna kinachobakia na hali ile ile maishani kuanzia miti mpaka binadamu mwenyewe aliyepewa mamlaka ya kuvitawala vyote vilivyo katika upeo wa macho yake. JPM ameshalala hawezi tena kurudi na aliyoyafanya yataongea kwa niaba yake siku zote.

Miradi mikubwa itaongea kwa niaba yake miaka mingi ijayo, madaraja, ndege, barabara, upunguzaji wa bei za kuunganisha umeme na masuala mengi chanya. Yapo mengi mabaya pia yataongea kwa niaba yake, ameshapita kama walivyopita kina Julius Nyerere, Edward Sokoine, Benjamin Mkapa na wengine wengi.

Wale wote ambao walipata nafasi za uongozi kwa kuteuliwa nae, wote waliomkubali na kuweka hadharani mapenzi yao kwake watambue tu kuwa muda hauna urafiki na mtu, Huu ni wakati wa kuangalia namna gani urathi (legacy) wake unaweza kuwa hai kwa miongo mingi ijayo.

Pia watambue kuwa Rais wa sasa hana sababu ya kufanana na Hayati kwa kila kitu akifanyacho. Anao upeo wake wa kutazama yote yanayofanyika chini ya uangalizi wake. Anavyo vionjo vyake kuhusiana na aina ya wasaidizi anaowataka ili waende sambamba na maono yake kama Rais.

Sio uungwana kumkwaza kwa kujaribu kumjengea zile dhana kwamba hawezi kufanya kitu au hataweza kumfikia Hayati. Tuwe na mtazamo chanya tunapoujadili mustakabali wa nchi yetu. Kwani la muhimu ni Taifa letu kustawi kadri iwezekanavyo.

Hatutaweza kustawi kama Nostalgia za Hayati JPM ndizo kila kitu kwa baadhi ya watu kiasi cha kumkwaza Rais wa sasa. Nitumie nafasi hii kumshauri Mheshimiwa Rais kwamba kitafika kipindi haya majungu, fitina na maneno ya baadhi ya watu wasiotaka kukubaliana na ukweli wenyewe, vitakuwa ni sehemu ya historia.

Cha muhimu ni kufanya kazi kwa uwezo wako wote, kuwa mwema kwa maana ya kutanguliza busara kwenye maamuzi. Kujizungushia wigo wa marafiki wabunifu wasio na chembe chembe za kutaka kuonekana wema kwako. Siku zote hulka ya Mama huwa ni ie ya kutaka kuwaridhisha wote akiongozwa na upendo wa asili.

Lakini uzoefu wako wa siasa za hadhi ya juu utaweza kukusaidia katika mazingira yenye mitihani ya kimaamuzi.

Hawa wanaosababisha uwe mara kwa mara unakumbusha kuwa wewe ni wa jinsia ya kike, ipo siku watanyamaza, kwa sasa bado wanasumbuliwa na ukweli kwamba JPM ameshalala usingizi wa milele.

Na siamini kuwa mawazo au mitazamo ya wote wenye hizi Nostalgia ni tatizo kubwa kulinganisha na aina ya matatizo ambayo Taifa hili imeshakumbana nayo na mwisho tukadumu tukiwa na utulivu pamoja na ustaarabu unaotutambusha kidunia.
 
Back
Top Bottom