DSN
JF-Expert Member
- Feb 2, 2011
- 2,837
- 1,688
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kiko kwenye matatizo; matatizo ambayo kwa kweli hakijui kifanye nini kujitoa kwenye matatizo hayo na hasa linapokuja suala la Edward Lowassa kugombea nafasi ya urais kupitia chama hicho. Lowassa amekuwa ni alama ya kutatiza (enigma) kwa Chama cha Mapinduzi, wanachama na mashabiki wake. Kwa kila kipimo yeye ndiye mgombea ambaye wagombea wengine wote (waliotangaza nia na watakaotangaza nia baadaye) wanatakiwa kumshinda ili kupata nafasi ya kugombea. Ni vizuri kidogo kuelewa kwa nini Lowassa ni tatizo ambalo si rahisi kulitatua bila kukutana na matokeo mengine mengi yasiyotarajiwa.
Uchungu wa kujiuzulu kwa Lowassa
Uamuzi wa Lowassa kujiuzulu Uwaziri Mkuu kutokana na kuhusishwa kwake na kuingilia mchakato wa kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond kinyume cha sheria kumeacha ladha chungu kwenye ndimi za wapenzi na mashabiki wake ndani ya CCM (bungeni na nje ya Bunge). Lowassa – kwa maoni ya baadhi ya watu – hakupaswa kujiuzulu Uwaziri Mkuu kwani angeweza kutumia nafasi aliyopewa na Spika Samuel Sitta kujibu hoja kwa hoja madai yaliyotolewa na Kamati Teule ya Bunge. Hakufanya hivyo. Badala yake aliamua kuuzira Uwaziri Mkuu katika ile hotuba yake ya "Tatizo ni Uwaziri Mkuu".
Lowassa alifanya mojawapo ya makosa ambayo naamini atakuwa anayajutia hadi leo hii na labda kwa maisha yake yote. Ulikuwa ni uamuzi wa woga na hasira – kitu ambacho baadhi yetu kinatufanya tusiwe mashabiki wa aina ya uongozi wake. Badala ya kujibu hoja na kuonesha uongozi kwa kufafanua ni kwa namna gani kina Harrison Mwakyembe na kamati yake teule walifanya makosa Lowassa aliamua kujiuzulu. Alisema kuna jambo (kina Mwakyembe) wanalitaka na atakuwa tayari kuwapatia.
Marafiki na wapenzi wake wengi walisikitishwa sana na uamuzi wake ule kwani waliona kuwa ulichukuliwa kwa pupa bila tafakari ya kina au kushauriwa na watu wenye vichwa vilivyotulia. Hili limeacha uchungu kwa wapenzi na mashabiki wake ambao wengi wanaona namna pekee ya kujifariji na kuponya maumivu yale ni kuhakikisha Lowassa anaingia Ikulu. Asipoingia litakuwa ni pigo mara mbili.
Ukimya wa Lowassa
Baada ya kujiuzulu Uwaziri Mkuu katika ile hali ya kususa Lowassa alionekana kususa na kuzira hata kuchangia bungeni. Inawezekana ulikuwa ni uamuzi wa kukaa pembeni au ni kuwa hakutaka kuchangia tu (labda alikuwa anachangia kwa maandishi) lakini kwa muda alikuwa kimya bungeni. Na hata alipoanza kuzungumza – miaka zaidi ya mitatu tangu ajiuzulu – Lowassa wazi kabisa alikuwa ameamua kurusha ngumi ya kwanza kujibu mashambulizi dhidi yake.
Alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu Lowassa alitoa hotuba yake maarufu ya "Ugonjwa wa Kuogopa Kufanya Maamuzi". Katika Hotuba yake ile Lowassa baada ya kuisifia serikali yake alidai kuwa kulikuwa na huo ugonjwa wa viongozi kutofanya maamuzi. Alisema hivi "Kuna ugonjwa unaoingia wa kuogopa kutoa maamuzi, tutoe maamuzi. Heri ukosee kwenye kutoa maamuzi kuliko kutotoa maamuzi. Toeni maamuzi, acheni kuogopa, tumepewa nchi fanyeni maamuzi. Heri uhukumiwe kwa kutoa uamuzi kuliko kwa kutotoa uamuzi, toeni maamuzi!"Sijui kama katika kauli yake alikuwa anafikiria maamuzi aliyoyatoa yeye kuingilia mchakato wa Richmond au vipi. Vyovyote vile ukimya wa Lowassa bungeni ulifikia kikomo.
Lowassa na Haki ya Kuwa Rais 2015
Kama kuna mtu ambaye urais wa 2015 ni kama "haki" yake ni Lowassa. Kwa wanaokumbuka Lowassa na Kikwete ndio waliunda ushirikiano wao katika kutafuta urais baada ya kuwekwa pembeni 1995 ambapo Benjamin Mkapa alipewa nafasi hiyo. Imani kubwa (na ushahidi wa kauli zao mbalimbali) unaonesha kuwa wao wawili walikuwa wamekubaliana kutengenezeana njia; mmoja akishinda 2005 basi mwingine atakuwa Waziri Mkuu na ikifika 2015 itakuwa zamu yake.
Kujiuzulu kwa Lowassa 2008 kuliharibu sana mapatano haya na kwa wanaokumbuka kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwa wazee wa Dar es Salaam kuelezea kilichotokea Dodoma alijaribu kuelezea kuwa kama ni "ajali ya kisiasa" na kuwa bila ya shaka Lowassa anaweza kuinuka tena. Tukirejea matukio mbalimbali tangu kujiuzulu kwake hadi leo hii hakuna shaka kabisa kuwa Lowassa amekuwa kama Hillary Clinton yule mke wa aliyewahi kuwa Rais wa Marekani na Seneta kutoka New York.
Mwaka 2008 ulikuwa ni mwaka wa Hillary kuingia Ikulu. Watu wengi walikuwa wamempa nafasi kubwa ya kushinda tangu 2006 wakati kampeni za urais zilipoanza. Hillary alionekana ndiye mgombea mwenye fedha nyingi zaidi na mtandao mkubwa wa watu wenye kumuunga mkono hasa kutokana na uhusiano wake na Rais maarufu Bill Clinton. Hata hivyo hakuna mtu aliyeterajia kuwa Seneta kutoka Illinois na mtu ambaye hakuwa na jina kubwa angeweza kumbwaga Hillary Clinton. Lakini kama inavyosemwa Mungu siyo Athumani, Barack Obama akija na mvuto wa ushawishi wake kuliko uwezo wa fedha zake aligeuza kampeni nzima na kumnyang'anya tonge Hillary mdomoni. Hillary akaambulia kupewa Uwaziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kama pole yake.
Mwaka huu Hillary anaonekana tena kuwa ndiye atakuwa mgombea wa Demokrati mwakani; sasa hivi hata hivyo ana kazi ngumu zaidi kwani anahusishwa na kashfa mbalimbali ambazo kwa kweli zinamuweka katika wakati mgumu zaidi kushinda dhidi ya chama cha Wahafidhina wa Marekani (Republikani).Lowassa naye ni hivyo hivyo.
Ninaamini ingekuwa rahisi sana Lowassa kuelekea 2015 bila kuhusishwa na kashfa na hata kujiuzulu kuliko ilivyo sasa. Na njia ambazo imeonekana ametumia kuliuza jina lake (misaada ya fedha, kuombwa na makundi mbalimbali na kujionesha kuwa yupo fiti) vyote inaonekana vinamuweka yeye pagumu zaidi kuliko kitu kingine chochote na hasa mbele ya moto ambao unatishia CCM (na Kikwete ameutabiria kwa usahihi kuliko anavyoweza kufikiria) wa upinzani.
Na hapa ndipo kazi ngumu iko kwa CCM. Je, Lowassa apitishwe kwa vile inaonekana ni haki yake zaidi hata kama kwa kufanya hivyo watakuwa wamepitisha hukumu kali dhidi ya CCM kutoka kwa wananchi?
Je, Lowassa apitishwe kwa matumaini ya mazuri atakayokuja kuyafanya baada na hasa maamuzi ambayo yanaweza kuwa mabaya lakini atafanya tu (ukirejea hotuba yake bungeni)?
Je, Lowassa apitishwe kwa sababu anaonekana kupendwa na watu wengi ndani ya chama na labda wachache nje ya chama? Lakini upande mwingine je, jina lake likatwe kwa sababu tu ya kuhusishwa na kashfa ambazo inadaiwa yeye hakunufaika chochote kifedha?
Je, akatwe kwa sababu tayari jina lake linaleta mgongano ndani ya CCM na kusababisha kambi ambazo hazijasameheana tangu siku ile alipobwaga manyanga chini bungeni kususia Uwaziri Mkuu?
CCM ikilikata jina lake si itaonekana inamuonea kwa mtu ambaye amelipia gharama kubwa? Lakini ikimpitisha si CCM itaonekana imepiga magoti mbele ya altare ya mtu mmoja?
Tunaposubiri uamuzi wa Mkutano Mkuu wa CCM kumpitisha mgombea wake naweza kutabiri mawili. Kutatokea "mizengwe" ambayo inaonekana Kikwete ameidhamiria –tukirejea hotuba yake ya juzi kuhusu mgombea wa aina gani CCM impeleke kwa wananchi.
La pili ni kuwa CCM ili kushinda urais ni lazima itoke katika fikra zake za zamani na kumtafuta mgombea ambaye labda hata jina lake halijatajwa sana na ambaye uzoefu wake wa kiutawala na kiuongozi ndani ya chama na serikali haujafikiwa na mtu yeyote anayetajwa sasa; siyo Lowassa au mtu mwingine. Binafsi sitoshangaa CCM kuja na jina la mtu huyo.
Wakifanya hivyo naamini utakuwa ni mwisho wa Lowassa ndani ya CCM.
Swali ni je, ana uwezo wa kucheza karata yake nje ya CCM na hivyo kuendelea kuisumbua CCM kwenye Uchaguzi Mkuu?
Au itabidi kwa mara nyingine abwage manyanga chini na kuamua kuzira siasa hizi kama alivyofanya Rostam Aziz na kuamua kuachana na siasa jumla ili aendelee kula mafao yake ya Uwaziri Mkuu taratibu?