Chadema Mwanza yampiga stop Zitto
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Ziwa
kimesema hakitaki kumuona Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kwa
kuwa ni msaliti.
Pia kimewatahadharisha viongozi wa Chadema Kanda ya Ziwa
kwamba yeyote atakayeonekana kuwa karibu na Zitto katika shughuli za
chama au kutoa siri, atashughulikia haraka na kuwekwa kwenye kundi la
wasaliti.
Akizungumza jijini hapa jana, Kiongozi wa Operesheni Kanda
ya Ziwa Magharibi, Tungaraza Njugu, alisema kuwa wanaunga mkono kwa
asilimia 100 uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema wa kuwavua uanachama Dk.
Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, huku Zitto akipachikwa jina la Mbunge
wa Mahakama.
Njugu alisema uamuzi huo ni sahihi kwani watu hao watatu waliaminiwa na
chama, lakini wakakigeuka na kukisaliti kwa manufaa yao.
Kwa kitendo alichokifanya, kukisaliti chama na kukipeleka Mahakamani,
tunasema hatumtaki kabisa, ingawa ana haki ya kwenda sahemu yoyote na
kufanya mkutano lakini tunatoa tahadhari mapema.
Ikiwa atakuja Mwanza na kujihusisha au kutumia nembo ya chama katika
shughuli zake za kisiasa, hapo atakuwa amechokoza nyuki. Hivyo hivyo kwa
kiongozi atakayeonekana kuwa karibu au kumpa ushirikiano,
atashughulikiwa haraka.
Zitto hawezi kuwa kikwazo kwa Chadema kufikia malengo yake, tunasema
chama hiki hakijabomoka wala kugawanyika makundi yenye mitazamo tofauti,
hii ni kama hali ya baba kumwadhibi mtoto wake.
Tunajua hizi vurugu zinazotokea zinaratibiwa na Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Usalama wa Taifa na vyama vingine vya siasa ambavyo vinatishwa na
nguvu za Chadema. Lakini tunasema tutafika Ikulu salama, alisema.
Njugu alisema kitendo cha Zitto kutoa tuhuma kwa viongozi wa Chadema ni
dalili ya kuanza kutapatapa kutafuta huruma ya wananchi na Mahakama.
Alisema kama alikuwa anajua viongozi hao wana tuhuma za aina hiyo,
angezitoa mapema kabla ya kuibuka yaliyompata.
Unajua kuna wabunge ambao waliandaliwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe,
tangu wakiwa vyuoni akiwamo Zitto. Amefika hapo kwa sababu ya Mwenyekiti
sasa anakosa fadhila.
Wengine ambao Mbowe alikuwa akiwaandaa wakiwa vyuoni ni John Mnyika,
Halima Mdee, Ezekiel Wenje na John Mrema ambaye ni kiongozi mkubwa Makao
Makuu.
Mbowe alikuwa akiwafuata vyuoni na kukaa nao baada ya kuona ni vijana
wenye mwelekeo wa kuleta mabadiliko na chama kikawaamini na hata kuwapa
majimbo. Lakini naona Zito amejisahau.
Mimi nawaomba viongozi wa kitaifa kutofanya kosa la kumsamehe au
kumrejesha ndani ya chama pengine kutokana na uamuzi wa Mahakama.
Itakuwa ajabu kweli kweli na wanachama hawataelewa, alisema.
Wakati huo huo, makundi ya wanachama wa vyama mbalimbali walikusanyika
eneo la Kemondo maarufu kama Bunge la Mwanza kuzungumzia
kinachoendelea ndani ya Chadema.
Eneo hilo ambalo lipo katikati ya jiji likiwa na matawi ya Chadema na
CUF, wanachama wengi wa Chadema walipongeza hatua hiyo.
Wanachama hao walikuwa wakisoma magazeti mbalimbali kwa sauti kuhusu
Zitto, na kujadiliana ambapo asilimia kubwa walionekana kutoridhishwa na
mwenendo wa kada huyo wa Chadema.
Source: Rai