"Nimeshafanya uamuzi kuhusu suala la Urais katika uchaguzi ujao. Ninachosubiri ni chama kutangaza ratiba"
Profesa Muhongo
Juzi, umoja wa wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro nao umeibuka na kutangaza kumuunga mkono na kumshawishi aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuchukua fomu.
Siku moja baada ya wanafunzi kutangaza hatua hiyo, Profesa Muhongo aliyejizulu uwaziri kwa kushindwa kushughulikia vyema kashfa ya Tegeta Escrow, alijibu akisema amesikia na tayari amefikia uamuzi atakaoutangaza kipenga kikipulizwa.
kupitia kwa mwenyekiti wao, Charles Ngereza wanafunzi hao waliwaambia waandishi wa habari jijini Arusha kuwa watazunguka kwenye vyuo na taasisi zote za elimu ya juu nchini kuwashawishi wenzao kuungana nao.
"Sababu kuu ya kumuunga mkono ni rekodi ya utendaji wake. Kwa kipindi kifupi alichoongoza Wizara ya Nishati na Madini amefanya mapinduzi makubwa yaliyowashinda watangulizi wake ikiwamo kushusha bei ya kuunganisha umeme kufikia kati ya Sh27,000 hadi 177,000 vijijini," alisema Ngereza.
Alisema kasi ya utekelezaji wa mradi wa umeme vijijini, licha ya kuwapatia wananchi huduma ya nishati, pia imechangamsha uchumi vijijini kwa kuongeza shughuli za uzalishaji zinazotegemea nishati ya umeme.
Akizungumza mbele ya wawakilishi kutoka vyuo vikuu vya Tumaini Makumira, Semmco, Jomo Kenyatta, Mount Meru na Uhasibu Arusha (IAA), mwenyekiti huyo alitaja sifa nyingine ya Profesa Muhongo kuwa ni jasiri wa kusema na kutenda akitolea mfano alipozuia udalali katika sekta ya gesi na mafuta.
Wanafunzi waliohudhuria mkutano huo na vyuo vyao kwenye mabano ni Rahma Sengela (Jomo Kenyatta), Daudi Shayo (IAA), Sarah Aminarabi (Arusha), Nelson Machumu (Semmco) na Hobeshi Juvenary kutoka Makumira.
Kuhusu Profesa Muhongo kujiuzulu kwa kashfa ya Escrow, Ngereza alisema hatua hiyo ilitokana na uwajibikaji wa kubeba dhamana jambo lilipoharibika katika eneo analoongoza.
Alisema hiyo ni moja ya sifa za uongozi na kumtaja Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi aliyejiuzulu uwaziri wakati wa uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere na baadaye kuukwaa urais.
Msimamo wa Profesa Muhongo
Akizungumza kwa simu kuhusu kauli ya wanafunzi hao, Profesa Muhongo alithibitisha kuombwa na makundi kadhaa ya kijamii wakiwamo wazee wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na tayari ametafakari na kufikia uamuzi ambao alisema atautangaza mara baada ya chama chake, CCM, kupuliza kipenga cha uchaguzi.
"Nimeshafanya uamuzi kuhusu suala ya urais katika uchaguzi ujao. Ninachosubiri ni chama kutangaza ratiba ya uchaguzi ili niutangazie umma uamuzi wangu," alisema Profesa Muhongo.
Kuhusu kuunda timu au mtandao wa kampeni, Profesa Muhongo alisema: "Sina timu wala mtandao binafsi. Timu yangu na mtandao wangu ni Taifa la Tanzania na nachukua fursa hii kuwaomba Watanzania kukataa kugawanywa na makundi kwenye masuala yenye masilahi kwa Taifa kama kumchagua rais wa nchi."
Chanzo: Mwananchi jumatatu, Machi 2015