Serikali kushtakiwa Thursday, 13 January 2011 09:29 Na Waandishi Wetu, jijini Dar Leo
FAMILIA za ndugu waliouawa kishujaa kwenye maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wameazimia kuishtaki Serikali kutokana na Polisi kusababisha vifo vya makusudi vya ndugu zao.Wakizungumza na Waandishi wa Habari baada ya mazishi hayo, wamesema wamesikitishwa na vifo vya ndugu zao kwa kuwa waliuawa bila hatia.
Wamesema ndugu zao walipoteza maisha kutokana na polisi kutumia nguvu kubwa na kusababisha vifo vya watu hao na majeruhi kibao huku wengine wakikamatwa bila sababu za msingi.
Kutokana na hali hiyo wameazimia kufungua kesi mahakamani kuishtaki Serikali kudai fidia kwa kupoteza ndugu zao ambao walikuwa tegemezi kwa familia zao.
Familia za marehemu hao-Denis Shirima na Omary Ismail-zimeibuka na kuzungumzia azima hiyo kutokana na vifo hivyo vilivyotokea Januari 5, mwaka huu katika maandamano ya CHADEMA yaliyofanyika mkoani Arusha.
Akizungumzia adhima hiyo, mwanafamilia mmoja ambaye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini, amesema wamesikitishwa na vifo vya ndugu hao na hawapo tayari kuliachia suala hilo hewani hivyo ni lazima waiburuze Serikali mahakamani.