Pinda: Tuhukumuni sisi, kiacheni chama, Serikali
na mwandishi maalumu, iringa
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda,(pichani) amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali zake visilaumiwe moja kwa moja kutokana na upungufu wa mtu mmoja mmoja.
Amesema chama hicho, na Serikali zake, ni visafi, hivyo makosa au tuhuma za mtu mmoja mmoja, zisichukuliwe kuwa ni tuhuma au makosa kwa vyombo hivyo.
Pinda alikuwa akizungumza katika eneo la Kihesa mjini Iringa jana, wakati wa uzinduzi wa Tawi la CCM la Chuo Kikuu cha Tumaini. Alikabidhi kadi kwa wanachama wapya 700.
Alisema tuhuma kuhusu rushwa na wizi ni kwa mtu mmoja mmoja ambaye atakuwa na upungufu wake, lakini siyo kwamba ni sera ya chama na Serikali zake.
"Chonde chonde, nihukumuni mimi Pinda kwa yale ninayokosea
Muondoeni Pinda kama ni tatizo, lakini chama kiendelee na Serikali zake kwa vile ni utaratibu wa kujisafisha tu.
Chama hiki (CCM) ni kizuri na serikali zake ni nzuri, kama kuna upungufu, basi utashughulikiwa na hatua zitachukuliwa," alisema.
Akijibu hoja katika risala ya tawi hilo kuhusu ajira kwa wahitimu wapya na kupanua wigo wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo, Pinda alisema Serikali itajitahidi kuhakikisha wahitimu hao wanatumika vizuri.
Alisema pia kwamba utaratibu wa mikopo haujapangika vizuri kwa kuwa lazima kwanza kuwajua wote wasiokuwa na uwezo wanaohitaji hasa mikopo hiyo.
Hata hivyo, alipinga hoja kwamba Serikali imeharakisha kuanzisha vyuo vikuu kadhaa bila ya maandalizi ya kutosha ya uwezo wa kuviendesha.
Alisema nafasi za vyuo vikuu lazima ziongezeke kwa vile isipofanyika hivyo, kutakuwa na vijana wengi waliohitimu sekondari tu na hivyo hilo litakuwa tatizo kubwa zaidi.
Waziri Mkuu alizindua tawi la CCM la Chuo Kikuu cha Tumaini katika shughuli iliyopangwa kutekelezwa muda mfupi tu kabla ya kurejea Dar es Salaam.
Alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete kwenye sherehe za Mei Mosi kitaifa, juzi.
source:
http://www.newhabari.com/mtanzania/habari.php?id=4746§ion=kitaifa