Na Sammy Kisika, Sumbawanga
WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda amewaomba radhi viongozi wa dini hasa Kanisa Katoliki kutokana na kitendo cha baadhi ya wafuasi na wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutumia kauli zinazokinzana na imani zao wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita.
Bw. Pinda ambaye pia Mjumbe wa halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya CCM, aliomba radhi hiyo katika kikao baina yake na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini na baadhi ya wazee maarufu wa mjini hapa jana, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Libori mjini Sumbawanga.
"Najua tulimkwaza Mhashamu Baba Askofu (Damian Kyaruzi), tumekejeli imani ya dini yake, tunaomba radhi. Mimi naomba radhi kwa niaba ya CCM na serikali. Si hapa tu (Sumbawanga) lakini ni maeneo mengi nchini kama vile majimbo ya uchaguzi ya Hai na Same ambapo baadhi ya wagombea katika kuomba kura ya ndiyo, walilazimika kutumia baadhi ya maneno yanayotumika katika Injili.
"Uchaguzi mkuu uliopita haukuwa laini kama ilivyotarajiwa na kutazamiwa, lakini badala yake ulikuwa na changamoto nyingi ikiwemo tofauti za kimtizamo na kiimani, hivyo kwa yale yaliyojitokeza ya baadhi ya waliokuwa wagombea kugusa imani za dini za watu, halikuwa lengo lao kufanya hivyo na tunaomba mtusamehe kwa yote yaliyojitokeza na kukwaza imani za dini zenu," alisema Bw. Pinda.
Kauli hiyo ya Bw. Pinda imekuja wakati Kanisa Katoliki Jimbo la Sumbawanga likiwa limewasimamisha na kuwatenga baadhi ya waumini kwa kukashifu Utatu Mtakatifu kwa kuufananisha na kaulimbiu ya mafiga matatu, yaani rais, mbunge na diwani; wakifananishwa na Mungu, Yesu Kristo na Roho Mtakatifu wakati wa kampeni.
Vile vile waumini hao ambao ni wafuasi wa CCM wanadaiwa kukashifu alama ya kanisa, msalaba, kwa kuuzika wakati wa kushangilia ushindi wa mgombea wao.
Wakati Bw. Pinda akikiri makosa hayo na kuomba radhi, baadhi ya viongozi wa CCM mkoani humo wamekuwa wakissitiza kuwa waumini hao wametengwa kutokana na kushabikia chama hicho na mgombea wake wa Ubunge, na hivyo kutofautiana na mgombea wa CHADEMA wanayedai alikuwa anaungwa mkono na kanisa hilo.
Akitoa maoni ya jumla ya uchaguzi huo, Bw. Pinda alisema kuwa kutokana hali iliyojitokeza, CCM na Serikali yake imepata fundisho, na hivyo kuomba katika chaguzi zijazo viongozi wa dini, serikali na vyama vya siasa wakae pamoja na kuweka angalizo ili wagombea wajiepushe na kukejeli imani za dini za watu wengine.
Waziri Mkuu aliwasihi viongozi hao wa dini nchini nzima kuanza ukurasa mpya na kutumia muda mrefu kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo.
Akizungumzia suala la rushwa, alikiri kukithiri kwa vitendo hivyo katika uchaguzi mkuu uliopita na kuongeza kuwa ipo haja ya kuangali upya mfumo wa uchaguzi kuanzia ndani ya CCM ambayo inajiandaa kwa uchaguzi wa viongozi wake mapema mwakani, ili kuhakikisha hautatoa mianya ya rushwa.
Aliwaomba viongozi wa madhehebu ya dini na wazee kukemea kwa nguvu zote vitendo vya rushwa.
"rushwa ni rushwa tu, hakuna haja ya kusema kuna rushwa ndogo hata mtu anapotaka kutimiza haja zake fulani kwa kutoa kitu kidogo bado ni rushwa. Pia kwa mgombea anapotoa doti ya khanga ili apigiwe kura hilo ni tatizo, hivyo naiomba CCM ibadilike, najua ni jambo gumu lakini lazima tupigane nalo kikamilifu. Wagombea nao taabu tu, hasa kwenye chama, safari hii tujirekebishe," alisema Pinda.
Akitoa neno la shukrani, Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kikristo Tanzania mkoa wa Rukwa, Mchungaji Israel Moshi alisema kuwa madhehebu ya dini yamesamehe, na kuwataka viongozi kusameheana kwa kuwa wote ni binadamu.