SEHEMU YA 06...
Kila alipokuwa akipiga hatua kadhaa, alikuwa akijificha, hakutaka kuonekana kabisa. Safari iliendelea, baada ya mwendo wa dakika arobaini na tano, wakaanza kuingia katika sehemu kubwa iliyoonekana kuwa kama shamba kubwa, huko ndipo mzee Mwiku alipokutana na mzee Matumbo.
“Afadhali umekuja,” alisema mzee Matumbo.
“Kuna tatizo?”
“Ndiyo lipo. Unamfahamu huyu?” aliuliza mzee Matumbo,.
“Ndiyo namfahamu, ni kijana wangu.”
“Sawa. Ng’ombe wako walirudi tena shambani kwangu,” alisema mzee Matumbo, tayari kigiza kikaanza kuingia.
“Naomba umruhusu aondoke, sisi tubaki tukizungumza kama wazee,” alisema mzee Mwiku, hilo halikuwa tatizo, Sangiwa akaruhusiwa kuondoka.
Njiani hakutaka kutembea, mwendo wake ulikuwa ni kukimbia tu, alitaka kuwahi nyumbani kwani giza lile lililokuwa likikaribia kuingia, lilimuogopesha sana. Alikimbia mpaka alipotoka nje ya mashamba yale, hakutaka kuangalia nyuma, macho yake yalikuwa mbele tu.
Moyoni alimshukuru Mungu, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea, kitendo cha kuruhiswa kuondoka huku akijua kwamba kulikuwa na ugomvi mkubwa baina ya wakulima na wafugaji, kwake aliona kama muujiza.
“Sangiwaaaa.....” ilisikika sauti nyuma yake.
Kwanza akaogopa, tayari giza lilibakia dakika chache kukamilika, alipoisikia sauti hiyo, akaogopa, alijua kwamba alikuwa porini, sasa ni nani alikuwa akimuita, hofu ya kudhani kwamba sauti hiyo ilikuwa ni ya jini au mchawi ikamuingia, hivyo akaongeza kasi.
“Sangiwa nisubiri....Sangiwa nisubiri...” ilisikika sauti ile.
Masikioni mwake haikuwa ngeni, aliifahamu vilivyo, ilikuwa ni sauti ya msichana Frida, lakini pamoja na hayo, hakutaka kusimama.
Aliendelea kukimbia mpaka alipofika umbali fulani, sauti ile iliendelea kumuita, akaona bora asimame, kama ilikuwa ni ya jini kama alivyofikiria, hakuwa na jinsi, alikuwa tayari kufa.
Akageuka nyuma, kwa mbali akaanza kumuona mtu akija kwa kasi, mwili wake ukazidi kutetemeka, mapigo ya moyo yakaanza kumdunda kwa kasi kwa kuona kwamba kulikuwa na hatari ambayo ilikuwa ikimsogelea mbele yake.
Itaendelea.