Pengo la Upatikanaji huduma za kifedha na bidhaa lapungua 2023

G-Mdadisi

Senior Member
Feb 15, 2018
157
99


PENGO la kijinsia kati ya wanaume na wanawake katika kupata huduma rasmi za kifedha na bidhaa limepungua kwa kiasi kikubwa, kutoka asilimia 10 mwaka 2017 hadi asilimia 3.6 mwaka 2023.

Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Wanawake ya Ujumuisho wa Kifedha (WACFI), Bi. Beng’I Issa amesema hayo tarehe 25 Machi 2024 wakati akitoa taarifa ya WACFI kwenye mkutano wa Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za Kifedha makao makuu ya Benki Kuu, Dodoma.

Alisema asilimia 73.4 ya wanawake wanapata huduma za kifedha ikilinganishwa na asilimia 77 kwa wanaume.

"Matokeo haya yanaonyesha maendeleo makubwa katika kuziba pengo la kijinsia nchini Tanzania, mchango mkubwa ukiwa unatokana na ushirikiano mkubwa kati ya sekta ya umma na binafsi," amewaambia wajumbe zaidi ya 20 wa Baraza hilo chini ya uenyekiti wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Bw. Emmanuel Tutuba.

Licha ya mafanikio yaliyopatikana WACFI ilibainisha vikwazo vitatu vinavyochangia kuendelea kuwepo kwa pengo la kijinsia na kuwazuia wanawake kupata na kutumia huduma rasmi za kifedha.

Vikwazo hivyo ni; upatikanaji mdogo wa hati miliki na kukosekana kwa utaratibu wa kukubalika dhamana zinazohamishika, upatikanaji mdogo wa huduma na bidhaa za kifedha mahsusi kwa wanawake, na ukosefu wa elimu ya fedha.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, WACFI imependekeza kuharakishwa kwa utekelezaji wa mchakato wa sheria kuruhusu au kuwezesha mali zinazohamishika kutumika kama dhamana na kwamba utafiti kuhusu huduma za kifedha na bidhaa zinazowalenga wanawake ufanyike.

Kuhusu elimu duni ya masuala ya fedha, WACFI imependekeza "wadhibiti na wasimamizi wa sekta ya fedha, watoa huduma za kifedha, na jumuiya nyingine washirikiane katika programu za elimu ya kifedha."

Bi. Beng’i Issa pia ametoa wito wa kuendelea kutekelezwa kwa mpango wa elimu ya fedha ulioidhinishwa na Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za Kifedha unaozingatia mahitaji mahsusi ya wanawake.

Pamoja na kupokea taarifa hiyo ya WACFI, mkutano huo wa Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za Kifedha umejadili masuala mbalimbali yanayotokana na vikao vilivyopita.

Baadhi ya wajumbe wa Baraza hili ni makatibu wakuu wa Wizara za Fedha (Muungano) na Ofisi ya Rais Fedha na Mipango (Zanzibar), Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi za usimamizi na udhibiti wa sekta ya fedha, wadau wa sekta ya fedha zikiwemo jumuiya za mabenki, na kampuni za simu.
 
Back
Top Bottom