"Leo wameapisha Rais Mpya, Rais wao, Rais wa NEC, Rais ambaye anatokana na majina ya mfukoni ya mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi." Naweza nisiwe sahihi sana, lakini haya walau yanasadifu kwa kiasi fulani mawazo ya washabiki wa UKAWA na wenye mapenzi mema na umoja huo, ambao wanaonesha kutoridhika na uamuzi wa Watanzania waliomweka madarakani Rais John Magufuli.
Ukweli ni kuwa Chadema wameshiriki sehemu kubwa ya ukombozi wa kifikra wa taifa hili, ukombozi wa kisiasa wa baadhi ya majimbo na kata, lakini pia ukombozi wa Chama cha Mapinduzi hadi kikaona umuhimu wa kuwa na mgombea Urais muadilifu, mchapa kazi na mfuatiliaji.
Chadema hawahawa wakakubali bendera yao ipeperushwe na Edward Lowassa, mtu kutoka chama cha mapinduzi ambaye visa na visakale vyake vimeshasemwa sana tangu zamani, tangu zama za Mwalimu Nyerere, sina haja ya kuvirudia hapa, sote tunavijua.
Tukirejea kwenye upande mzuri, Lowassa ni alama ya mabadiliko, na ndiye aliyesababisha Watanzania wengi wazungushe mikono kwa bidii, wakitarajia kuikomboa nchi kutoka kwa Mkoloni mweusi, CCM, huku nae Bwana Mkubwa akipata nafasi ya kutimiza ndoto zake za kuwa Rais.
Kwa kipindi cha miezi kadhaa tangu jamaa ahamie Chadema, tumejua sifa zake zote, huku mashabiki, wanachama na wadau wa CCM nao wakijitahidi kumvua nguo, wakiwemo wale waliokuwa washabiki wake wa kutupwa.
Siko katika nafasi ya kusema kama wanaomshabikia wako sawa au wanakosea, lakini tuheshimu mawazo yao.
Lowassa wanampenda na wanamuamini, wampe uongozi ndani ya chama chao, na mimi nasema ni wakati sasa kwa wale wenye mapenzi mema na chama na wenye imani na Lowassa kushinikiza ndani ya chama Mzee apewe, au wampe uenyekiti wa chama.
Mwenyekiti anayemaliza muda wake, (kama wazo hili litapata mashiko) amekuwa msaada kwa chama na taifa, lakini haitapandeza kama tutakabidhi chama kwa mtu tunayemuamini, mwenye maamuzi magumu, alama ya mabadiliko, mwanasiasa anayependwa kuliko wote kwa sasa, mwenye nyota?
Najua fika kuwa Mzee alishasema ataenda kuchunga ng'ombe, lakini ni wakati muafaka wa kumbembeleza, kumuoshe tena gari, kumdekia barabara, awe mwenyekiti wa Chama chenu, awaonjeshe mabadiliko katika ngazi ya chama ili sote tuyashuhudie na mwaka 2020 tuseme kweli tulikosea kumchagua mpiga pushapu, kiongozi wa mfano si huyu?
Baada ya kuukosa Urais na kususa matokeo, Slaa aliendelea kujenga chama kwa moyo wake wote, nchi nzima, kwa nguvu zote, na matokeo yake walau nchi iwaponyoke nyamaume wa Chama cha Mapinduzi, Fisiem, kama mnavyowaita.
Nasubiri makamanda mpeane mwongozo, kwa maslahi mapana ya Taifa!
#KaziImeanza