Mahakama ya Kadhi yazidi kuwachanganya maaskofu
na Betty Kangonga
BARAZA la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania (PCT), limeitaka serikali kuacha suala la Mahakama ya Kadhi liendeshwe na kuratibiwa na Waislamu wenyewe badala ya kuingilia.
Wito huo waliutoa jana jijini Dar es Salaam kwenye makao makuu ya baraza hilo Kurasini walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu mchakato ambao wamesema unaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani.
Mwenyekiti baraza hilo, David Batenzi alisema serikali haipaswi kuhusika kwa kuwa katiba inaeleza wazi kuwa haina dini, lakini wanashangazwa na kujiingiza katika mambo ya dini.
Baraza la Maaskofu linakubaliana na uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, lakini tunashauri suala hili lisipelekwe bungeni kwa sababu ni uvunjaji wa katiba ya nchi kifungu cha 9 kanuni ndogo ya 6, alieleza Batenzi.
Aidha, alisema ingawa serikali iliamua kuwaachia Waislamu kufanya matengenezo ya kanuni, bado inatia shaka kwa kuwa suala hili lipo chini ya Kamati ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Wao wamewaachia Waislamu suala lao, lakini kwanini Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na kamati yake iamue kuwasaidia katika kutengeneza kanuni? alihoji Batenzi.
Alisema kujihusisha kwa Ofisi ya Waziri Mkuu katika matengenezo ya Katiba ya Waislamu, ni lazima kutakuwepo na matumizi ya fedha zinazotoka kwa walipa kodi ambao ni wafuasi wa dini mbalimbali.
Hata hivyo, Batenzi alishauri kuwa iwapo kuanzishwa kwa katiba hiyo ya Mahakama ya Kadhi kwa waislamu kutafika ukingoni, kuna dalili kuwa kanuni hiyo inaweza kutinga bungeni ili kufanyiwa majadiliano. Alisisitiza kwamba, kutokana na serikali isiyo na dini kulipeleka bungeni suala hili, linaweza kuwagawa wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi wenye itikadi za dini tofauti na hakuna mbunge atakayekubali kuona dini yake ikishindwa. Aidha, waliwataka viongozi wa serikali kufuata nyayo za hayati Mwalimu Julius Nyerere ambapo katika uongozi wake, aliongoza taifa kwa kutotaka ubaguzi katika dini au kuifanya dini moja kuwa bora kuliko nyingine.