Baada ya kusulubiwa kwa Yesu wa Nazareti mnamo mwaka 30.Ad harakati aliyoanzisha iliendelea ndani ya mfumo wa Uyahudi wa Hekalu la Pili. Wafuasi wake wa awali, ambao walikuwa Wayahudi, walimwona kama Masihi aliyesubiriwa kwa muda mrefu lakini bado walizingatia Torati na imani ya Mungu mmoja ya Kiyahudi. Katika muktadha huu, alijitokeza mtu mpya na wa utata: Paulo wa Tarso. Ingawa hakuwahi kukutana na Yesu wakati wa maisha yake, Paulo alikuja kuwa sauti yenye ushawishi mkubwa katika kubadilisha harakati ya Yesu kuwa dini tofauti iliyokuja kuitwa Ukristo.
🟥 Kuibuka kwa Ghafla kwa Paulo
Paulo (awali Sauli) anaonekana kwa mara ya kwanza katika rekodi za kihistoria kama mtesaji mwenye juhudi wa wafuasi wa Yesu. Kulingana na simulizi zake mwenyewe, uongofu wake wa kushangaza ulitokea kupitia uzoefu wa maono ambapo aliamini Yesu aliyefufuka alimtokea. Mnamo mwaka 48AD Paulo alianza safari zake za kimisionari na kuanza kuandika barua kwa jumuiya za waumini katika Asia Ndogo, Ugiriki, na Roma. Barua hizi zilitangulia Injili na ndizo nyaraka za kwanza zilizoandikwa katika Agano Jipya.
Muhimu zaidi, Paulo hajawahi kujieleza kama mwanafunzi wa Yesu au mwasilishaji wa mafundisho yake. Badala yake, alidai kupokea ujumbe wake moja kwa moja kupitia ufunuo.
Hakuzingatia mifano ya Yesu, mafundisho ya maadili, au ujumbe wake wa Ufalme wa Mungu. Badala yake, Paulo alisisitiza kifo na ufufuo wa Yesu kama njia ya wokovu wa ulimwengu mzima, inayopatikana kwa wote — hasa kwa watu wa Mataifa — kupitia imani pekee.
🟩 Uundaji wa Theolojia Mpya
Maandishi ya Paulo yalitambulisha dhana ambazo hazikuwepo katika mafundisho ya Yesu mwenyewe:
- Yesu kama Mwana wa Mungu wa milele.
- Wokovu kupitia imani, si kwa kufuata Torati.
- Kusulubiwa kama sadaka ya ulimwengu kwa ajili ya dhambi za binadamu.
- Kanisa kama jumuiya ya agano jipya, ikichukua nafasi ya Israeli.
Tafsiri ya Paulo iliifanya harakati ya Yesu kuwa ya ulimwengu mzima, ikiitenganisha na mizizi yake ya Kiyahudi. Alitangaza kwamba watu wa Mataifa wangeweza kuwa wanachama kamili wa watu wa Mungu bila tohara, sheria za chakula, au kuadhimisha Sabato.
Hii ilikuwa mapinduzi. Yesu alihubiri kwa "kondoo waliopotea wa Israeli," na ujumbe wake ulikuwa umejikita katika sheria na unabii wa Kiyahudi. Kwa upande mwingine, Paulo alijenga mfumo wa theolojia uliomgeuza Yesu kutoka kwa Masihi wa Kiyahudi hadi kuwa mwokozi wa ulimwengu mzima.
Kwa hivyo, Paulo wa Tarso alichukua jukumu muhimu katika kuunda Ukristo kama dini tofauti, akitofautiana na harakati ya awali ya Yesu ambayo ilikuwa imejikita katika Uyahudi.
Sikiliza kwa makini, maana haya siyo maneno ya wanadamu bali ni neno la Mungu linaloleta uzima. Kwanza kabisa, hata tarehe unazotumia sasa zinashuhudia Kristo. Leo hii unaposema mwaka 2025, unakiri pasipo kujua kwamba dunia nzima inahesabu miaka kwa jina la Yesu Kristo kabla ya Kristo (BC) na baada ya Kristo (AD). Hii ni alama ya wazi kwamba Yesu si mwanadamu wa kawaida, bali ni Mwana wa Mungu aliyeweka historia yote chini ya jina lake. Hakuna Nabii, hakuna mfalme, hakuna mwanadamu yeyote ambaye historia yote imepimwa juu ya jina lake isipokuwa Yesu Kristo pekee.
Sasa unasema Paulo ndiye aliyebuni Ukristo huo ni uongo unaotoka kwa adui wa roho zetu. Yesu mwenyewe kabla ya Paulo hajawahi kuandika barua yoyote, alisema kwa uthabiti: “Nitalijenga kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda.” (Mathayo 16:18). Kanisa ni kazi ya Kristo mwenyewe! Paulo hakuwa muanzilishi, bali alichaguliwa na Bwana kama chombo cha kubeba injili kwa Mataifa. Ni Kristo aliyemfunulia, na mitume waliokuwa Yerusalemu walimkubali na kumpa mkono wa ushirika. Hivyo siyo Paulo aliyebuni, bali ni Yesu aliye hai aliyefanya kazi kupitia Paulo.
Kisha unasema Yesu hakufundisha juu ya kifo chake kwa ajili ya dhambi. Hilo pia ni upotoshaji. Yesu mwenyewe alisema: “Mwana wa Adamu hakuja kutumikiwa bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia kwa wengi.” (Mathayo 20:28). Tena usiku wa kukamatwa kwake akasema: “Hii ndiyo damu yangu ya agano jipya, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.” (Mathayo 26:28). Maneno haya yalitoka kwa kinywa cha Bwana mwenyewe, kabla hata Paulo hajaanza huduma. Kwa hiyo kifo chake si jambo la kisiasa, ni mpango wa Mungu wa wokovu.
Ni kweli Wayahudi walipeleka mashtaka ya kisiasa mbele ya Pilato kwa sababu hawakuwa na mamlaka ya kisheria kumsulubisha mtu. Lakini kiini cha chuki yao hakikuwa kodi ya Kaisari, bali dai la Yesu la uungu. Soma Yohana 10:33, walimwambia waziwazi: “Si kwa tendo jema tunakupiga mawe, bali kwa kukufuru; kwa kuwa wewe u mwanadamu, wajifanya Mungu.” Hii ndiyo sababu kuu iliyowasha moto wa chuki, na kupelekea kusulubiwa. Hivyo hoja kwamba hakusulubiwa kwa madai ya uungu ni ya uongo kabisa, kwa sababu maandiko yameandika wazi.
Yesu alikuja kama mwanadamu ili apate kuchukua nafasi yetu. Ndiyo maana aliweza kusema “Mimi mwanadamu” (Yohana 8:40). Lakini huyo mwanadamu ndiye Neno aliyekuwepo tangu mwanzo, na Neno alikuwa kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu (Yohana 1:1). Neno hilo lilifanyika mwili (Yohana 1:14). Hii ndiyo siri ya umwilisho Mungu akawa mwanadamu kwa ajili ya wokovu wetu. Hii ndiyo injili yenye nguvu, injili isiyopingika, injili iliyojaa upako wa Roho Mtakatifu.
Kwa hiyo sema nini useme, tafsiri vipi, pinda historia na nukuu maandiko kwa namna unavyotaka ukweli mmoja unabaki: Yesu Kristo ndiye Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, Mwana wa Mungu aliyejifunua kwa mwili, aliyekufa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu, akafufuka siku ya tatu, na yu hai milele! Hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu tupate kuokolewa kwalo ila jina lake (Matendo 4:12).
Na leo hii sauti ya Roho Mtakatifu inasema: “Usiitie moyo wako ugumu.” Kristo hakuja kuanzisha siasa, Kristo hakuja kubuni dini, Kristo hakuja kwa hila za Paulo, Kristo alikuja kwa damu yake mwenyewe. Na damu hiyo inamlilia kila mmoja: wokovu, msamaha, uzima wa milele.