Part X: uko wapi rafiki? kuna cha kujifunza hapa!

Slim5

JF-Expert Member
Jan 7, 2014
28,110
37,645
Habari za w.end wanaJAMII wenzangu?

Poleni kwa kusubiri!

Mzigo wetu huu hapa:

Nilihisi kuwa nimeipa akili kazi ya ziada leo. Akili inafanya kazi tofauti na uwezo wake. Chakula kimekuwa kichungu. Uroho wa nyama kwisha. Simezi. Sitemi. Watu watatu wananipa wakati mgumu kwa mara nyingine. Kichwani taswira ya matukio yote yatuhusuyo mimi na wewe inanijia. Kila tukio linakuja na dakika zake, na kuondoka. Kuna maneno ulianza kuyaongea. Uliongea kwa pozi sana. Uliongea mithili ya mwanasheria anaemsihi mtuhumiwa akiri kutenda makosa, kwa ahadi kuwa atamsaidia kuimaliza kesi. Sijui cha kufanya.

Nikawaza. Kati kati ya kuwaza, nauona mlango wa kuingilia kwako unafunguliwa. Kuna mtu anaingia.


Mtu huyu anaingia kipindi hiki ambacho maneno ya mahaba yanakutoka kinywani mwako, si tu maneno bali ni kipindi hiki hiki ambacho kiliruhusu mkono wako mmoja uwe unasisitiza kila unachokisema kwa kupiga piga sehemu mbali mbali za mwili wangu. Nilikuwa nafurahia kuona mkono wako ukiwa busy kuliko hata kusikiliza maneno uliokuwa unayasema, nilipenda sana hali hii, nilitamani niione mwisho wake, nilitamani mwisho wa hii kitu ufike haraka sana, kwangu mimi hata kama ungekuwa unanipiga piga kimya kimya bila kutoa neno, mimi nilikuwa nimeridhika kwa kiwango tosha sana, kwa kila kile kinachotokea pale ktk kochi. Sikutaka kuskiliza unachosema, nilitaka kuskiliza unachonifanyia katika kochi!


Leo sifa zilibadilika. Zile sifa ulizokuwa ukinipa siku za nyuma, sio, leo unanipa sifa mpya kabisa. Wakati ukinisifia kwa sifa mpya ndipo akaingia mgeni. Mgeni wetu ni Yule mama msamariamwema, Yule alietukubalia kupokea na kuhifadhi amana zako, huyu ni Yule mama muuza duka la dawa, jirani na bara bara ya Mandela, mahali karibu kabisa na pale kisanga kilipokukuta. Ni mama mtu mzima. Vijana wangesema ni bi mkubwa. Hakubahatika kuja kukujulia hali kule Muhimbili, lakini amejitahidi ktk masiku haya ambayo umeshatoka hospitali, amekuja kukujulia hali.

Alikuwa na sababu ya kuja kukuona ili amjue mtu aliemhifadhia vitu vyake, lakini kubwa ni kudumisha ujirani mwema.
Nilikuona. Hukumfurahia wala hukumpenda. Hukupenda uwepo wake pale. Ni kama ulikuwa katika hali Fulani ya kutamani kumuaga kabla yeye hajaaga. Nilikuona ukimkaribisha chakula kwa sauti japo moyoni mwako ulikuwa unamuhoji "si umeshanijulia hali, nenda basi na hamsini zako na utuache na sisi na hamsini zetu." Mama wa watu hakuwa anaelewa lugha hii. Aliendelea kuwepo pale.

Ni alikuudhi zaidi na zaidi. Alikuudhi hasa pale alipoanza kunihoji namna tukio lilivokuwa, na hasa pale alipoomba nisimulie tukio lile la usiku ule. Nilisimulia huku ikiniuma kuwa kuna kitu nimekikosa leo. Tukio lako la ajali, kwa mara ya kwanza nakuwa mgumu kulisimulia ama niseme kufurahia ushujaa wangu nilioufanya.

Nilimsimulia bi mkubwa Yule kwa shingo upande. Na yeye sijui ni kusudi ama laaah, hakuonyesha kujali, hakuonyesha kuwa amekukwaza, na hakujua kuwa amenikwaza. Tulimvumilia.

Mambo yakazidi kuharibika. Wageni zaidi wanaingia. "Dada" na "mtu wako" wanaingia. Kwa aibu kuwepo ktk chumba kidogo cha master, bi mkubwa Yule akaaga. Hukufurahia kuaga kwake, nahisi uliamini Yule bi mkubwa amechelewa sana kuaga. Kwa mtazamo wako, bi mkubwa Yule ilibidi aaage kabla hata wageni hawa wawili hawajaingia. Lakini haikuwa hivo. Alichelewa kuaga. Aliaga na akaenda zake. Hukufurahia hata kidogo.
Maajabu hayaishi chini ya jua.
Katika watu wote wanne ndani pale, dada ako ndiye mtu aliekuwa anaongoza kwa kuwa na furaha mle ndani. Wewe na mtu wako hamna hata mmoja, si tu alieonyesha furaha, bali hata alie-pretend kuwa ana furaha. Kilichonchanganya ni kuwa hata ninyi kwa ninyi bado hamkuonyesha kuwa kila mmoja anafurahia uwepo wa mwenzie. Mimi ndiye pekee sikuwa naeleweka, sikuwa na cha kufurahia katika mazingira yale. Sikuwa na cha kuchukia pale. Ni kama useme nilikuwa kati kwa kati. Kwangu mimi, kumuona dada ilikuwa ni happy moment. Kumuona mtu wako ilikuwa ni sad moment. Sikuwa na uwezo wa kuchagua upande wa kukaa. Nilihiitaji msaada wa maamuzi hapa, msaada haukuwepo.


Kwa aliemuona dada yako usiku ule, angeweza kusema kama sio amevaa ili kuupania mtego wake uteguke katika njia chanya, basi alikuwa na special task – kazi maalum! Chochote katika haya mawili, kama ulikuwa mtego, baasi nilitegwa na nikategeka kiurahisi. Kama alikuwa na special task, basi hiyo kazi ni mimi. Dada alikuwa ameniingiza katika radar zake ama laah niseme nilishajiingiza katika radar za dada. Ni mara chache sana kukuta mtoto wa kike hajapendezwa na kivazi cha skin jeans, sikumbuki mara ya mwisho ni lini kumuona binti mrembo katupia kivazi hiki na hakupendeza, sikumbuki hata! "Dada" alikuwa ndani ya skin jeans!


Sasa kila mtu na eneo lake la kukaa. Tangu unyanyuke kujifanya kama unampakulia bi mkubwa Yule chakula, hukurudi tena ktk kochi langu. Dada nae kakaa kwake. Mtu wako nae kaka mbali kiasi na wewe, ila karibu na mimi. Ile picha ya mimi na wewe kuwa na vyakula ilikuwa ndio chanzo cha amani kupotea ndani mle. Ilikuwa chanzo cha Yule mtu wako kukosa amani. Hakufurahia hata. Hakunipenda. Hakuna alieanzisha stori hapa, kimya kimya, "dada" aliokoa jahazi kwa kuanzisha masihara na wewe, alikutania kuwa umepona, na sasa una uawezo wa kuwaandalia wageni misosi, mkacheka cheka kinafki! Nilihiisi mtafaruku kuibuka wakati wowote kuanzia sasa.

Kunguru muoga…………..! nilikuwa wa kwanza kuaga. Ukabaki kuniangalia tu, hukusema kitu, ungesema nini na sikuwa nimeomba ruhusa yenye kuitaji majibu, nilikuwa nimetoa taarifa tu.
Ukasimama kunisindikiza. Dada akakukalisha chini. Akakuambia pumzika uongee na ………., na huyu …… nitamsindikiza mimi. Ukajaribu kubishana na dadako kuwa utansindikiza kama sehemu ya mazoezi. Dada akakupinga, kwa kuwa umetoka kupika, basi ni wakati wako wa kupumzika. ile vita ya mabishano na dada ikakushinda, nikasindikizwa na dada mpaka nje, mpaka kituoni!

Ungetarajia mimi na dada tusimame eneo lenye mwanga wa kutosha usiku ule ili tuweze kuonekana na dala dala zinazokuja kwa kasi. Haikuwa hivo. Dada alichagua eneo la kusimama. Na wala sikujua dada alimaanisha nini. Na wala sikujishughulisha kujua, ya nini nihoji anachotaka wakati muda si mrefu, sio kuambiwa bali ntajionea mwenyewe? Dada alichagua sehemu yenye giza na kuniomba tusimame hapo. Sikukataa. Naanzaje kukataa.

Tulisimama sehemu ambayo hata ungepita hatua tano toka tuliposimama, ungeambulia kuamini kuwa wale ni binadamu na privacy zao, lakini usingejua kuwa wale ni X na Y wamejibanza pale.
Kule ndani moto ukawaka. Manusra wangu na "mtu wake" kimenuka. Ni vita ya kuharibiwa uhondo wake dhidi ya wivu! Ukatakiwa useme nilikuja pale kwako kama nani? Nilikuja kufanya nini? Ukahojiwa rafiki yangu useme, huu ni usamariamwema gani usio na ukomo? Uliombwa utoe maelezo kwa nini siku zote anazokuja yeye hukuwahi kuandaa msosi, kisha mkala wote, lakini leo, umeandaa msosi na kula na huyu jamaa! Ulitakiwa useme kwa nini naendelea kuwa karibu na wewe?

Hukuwa na majibu mazuri hata chembe. Ni kama volcano iliokuwa inasubiri kitundu kidogo hata cha ukubwa wa kitundu cha sindano ili ilipuke. Ulilipuka. Moto ukawaka kati ya mgonjwa na mpenzi wake. Kama alikuwa hakujui, basi alikujua siku hiii. Ulitoa la moyoni. Ulianzia tangu siku ile aliponkunja, ukamchana kuwa kitendo kile kimekuuma sana. Ukamueleza asivo muungwana. Ukamwambia kuwa amekosa subira, amekosa uwezo wa kufikiri, na kwamba amekutia aibu kwa tabia yake aliyoonyesha.


Ukamchana. Ukamlaumu namna alivonituhumu mimi na wewe kuwa tulikuwa tumetoka "guest" na kwamba kwa haraka haraka zetu, wewe ukagongwa na gari. Uliendelea. Ukamlaumu, kwa sauti kali sana, huku ukionyesha kuwa hujawahi kukasirika kama siku hii, kwa nini alijiweka nyuma wakati dada anajaribu kunishawishi niseme gharama ya pesa iliotumika kukuhudumia wewe usiku ule wa ajali! Kwamba kwa nini alikaa kimya na kumuachia dada mkubwa kazi hiyo! Ulimwambia kuwa imekuuma sana, imekuuma kwa sababu aliwaonyesha ndugu zako namna gani hakujali.


Kwa kawaida mimi nipo tofauti na vijana wengi. Wao wanapenda kukumbatiana. Mimi sipendi kukumbatiana. Mimi napenda kumkumbatia m-baby. Vijana wengi hupenda ku-hug na mabinti, hupenda kukumbatiana kwa style ya kifua kwa kifua, kutizamana. Mimi napenda ku-hug na –ke, lakini style yangu ya hugs ndio tofauti. Mimi napenda kumkumbatia m-baby tukiwa wote twatizama uelekeo mmoja, yeye mbele mimi nyuma. Katika style hii, huwa na-enjoy sana, sijawai kujua sababu ya mimi kuwa hivi. Basi. Sina makuu miye!

Tukiwa kituoni pale, kuna mistari nilipewa, siikumbuki ila kuna swali nilijaribu kujibu, nikajikuta tu tumekumbatiana. Nikabadili style ya kukumbatiana na "Dada." Nilimkumbatia "Dada" katika ile style yangu niipendayo.
Ndio nikipendacho hichi kitu.

Kutoka huko alikotoka mbaya wangu, moja kwa moja mpaka kituoni. Anatutafuta. Akatuona! Upande anakotoka yeye ndiko tunakoangalia sisi, nilimuona muda mrefu tu. Safari hii wala sikushtuka kama nilivofanya kule chumbani. Sina sababu. Sikuwa na uhakika kama huyu niliekuwa nae busy hapa na yeye alishamuona ama laah. Sikutaka kujishughulisha na kazi nyingine. Mkono wangu wa kulia nilishaupa kazi katika sehemu ya juu ya huyu nilienae hapa. Mkono wa kushoto ulikuwa na kazi yake, maeneo ya chini ya "dada", huu ni muda ambao akili niliipa majukum ya kufanya monitoring ya mikono na kile ambacho "dada" ananipa kama mrejesho wa kazi yangu. Kwa majukumu haya, sikuhitaji kushughulishwa na mtu mwingine yeyote Yule awaye. Na ndio maana sikutia akilini taswira ya mtu Yule, mbaya wangu!


Akanikuta nimemkumbatia "Dada", nimemkumbatia dada katika style yangu niipendayo! Nimemkumbatia ndiyo, nimeshikilia kiuno vizuri tu! Kuna maneno alianza kuyatoa. Hayakuniingia akilini hata moja, yangeniingiaje akilini wakati hata sikujua alikuwa akimsemesha nani kati ya sisi wawili pale. Dakika kadhaa zilipita mpaka "dada" alipokuja kushtuka na kuchomoka kutoka katika himaya yangu, katika style ambayo siikumbuki alichomokaje zaidi ya kuskia mfululizo wa maneno ya mtoto wa kike mwenye hasira, aliepandisha jazba zake ambazo ni kama ana muda mrefu hajapandisha jazba zile.

Sikupata hata chembe ya huruma kwa mtu Yule. Niliamini kuna kitu alikuwa anakitafuta, na ndio hichi anakumbana nacho hapa, ni stahili yake. Anakumbana nacho mbele ya macho yangu. Nilisimama pembeni kama refa anaependelea timu moja aipendayo. Sikuongeza. Sikupunguza. Kumbukumbu yangu ya mwisho kabisa, ni pale nilipotii amri ya kupanda dala dala. Amri ilitoka kwa "Dada". Amri iliambatana na shilingi elfu ishirini kutoka katika mfuko wa skin jeans. Nilipokea. Sikuhesabu ni ngapi. Nilikuja kujua ni elfu ishirini nikiwa nimeshakaa kwenye siti. Na ndio hapa nilipokuja kugundua kuwa "Dada" amenipandisha dala dala la Tabata na sio la buguruni. Sikujali sana. Mii nishaachana na kisanga, watajua namna ya kumalizana! Nafanya yangu tu.


Hiki ndio kipindi pekee sasa nilichopata fahamu kuwa, nimewaingiza watu watatu katika uadui. Nikaliona hili kuwa ni hatari. Nikajitetea. Kwa kuwa nimepoteza amani bila mimi kujua, kwa watu watatu wanaofahamiana, na hivyo sintaweza kuwa na akili ya kurudisha amani kwa watu wale.

Nilitumia siku kadhaa kutafuta majibu ya nini cha kuwafanya watu wale watatu. Nilitafuta namna ya kudeal na kila mmoja wao kivyake. Watu wa nyumbani walijua kuwa nina unyonge usio wa kawaida, wakahisi yamenikuta ya kunikuta. Sikuwa tayari kuwafahamisha kuwa Yule niliemsaidia katika ajali ameniingiza katika masahibu mazito. Nilipiga kimyaa. Moyoni niliamini kuwa, kama niliyakoroga mwenyewe, basi ntakunywa mwenyewe.


Kichwani zilikuja akili nyingi sana. Zipo zilizontaka nimtafune "sweet dada!" Akili nyingine ikasema nijipendelee manusra wangu, nijilipe machungu ya kukunjwa pale Muhimbili mbele ya macho ya kadamnasi na pili kumkomoa yule jamaa, tena huyu nimtafune mlemle chumbani kwake! Akili nyingine zikantuma nikawakusanye masela wangu wa kitaa, wengi wao mateja, niwape kazi ya kudeal na huyu jamaa. Hili nilikuwa nalimudu kwa kuwa ni muda nimekuwa mfadhili wa mateja hawa hapa mtaani, na hii imenifanya niwe huru kurudi muda wowote wa usiku, hasa ninaporudi kutoka club! Hili wazo la mwisho nililiogopa kwa hofu, sikujua kipimo halisi cha adhabu ya mateja wale kwa jamaa, kuwa isije huko mbele ikanirudia! Nikaachana na wazo hili!

Sijui utoto. Sikutaka ushauri wa mtu katika hii issue. Akili ya kukata mawasiliano na wale watu ikanijia. Akili ikakubali kuwa huu ni uamuzi sahihi zaidi. Nilikubali mawazo haya na nikaaanza utekelezaji wake haraka sana. Sitaki mawasiliano na mtu. Muda ukaanza kupita. Siendi tena kwa mgonjwa wangu, na wala sishuki tena Ubungo. "Dada alijaribu kunirudisha katika reli. Alikuja mpaka kibaruani kwangu. Nakumbuka kuna siku alinikuta mwili mzima nimetapakaa vumbi la chaki.

Alinitoa katikati ya pindi, alinikumbatia vile vile nlivo, cha ajabu aibu niliona mimi na si yeye. Darasa lilishona vya kutosha. Si wanafunzi, si walimu wenzangu, hata wapita njia na wazazi waliokuja kufuatilia habari za masomo pale, wote walipigwa na butwaa kuona namna bidada Yule, anavoongea na mimi huku nikionyesha sina interests na kinachozungumzwa pale. Wanafunzi kama kawaida yao, Walinong'ona, wakapeana umbea, wakacheka!


Ilipita miezi nadhani kama minane. Sina tena mawasiliano na watu wale. Sikujua tena hatima ya manusra wangu. Sikujua nini kilimpata "dada angu." Ni kwamba mawasiliano yalikufa kifo cha asili. Baada ya kitambo kirefu, picha likajirudia tena. Niliona tangazo katika gazeti, kuwa kidato cha sita walioomba kusoma UDSM mwaka ule, wanatakiwa wakafanye "matriculation exam" pale UDSM (sina uhakika na spelling) kama sehemu ya vigezo vya kuingia UDSM!


Siku ikafika. Mungu sijui katuumbaje watanzania, mamia ya waombaji tuliotakiwa kwenda kufanya mtihani ule, hatukwenda UDSM kabla kufuatilia kujua venues mbali mbali za mitihani ile. Wapo ambao tangu wazaliwe ndio mara yao ya kwanza kwenda UDSM, tulikuwepo ambao tushawai fika UDSM lakini hatujui ni nini tofauti kati ya classroom, lecture hall na lecture theatre, hatukujua ndio vitu gani, hawa wote leo asubuhi ndio wanahaha kutafuta wapi panawahusu kufanya mitihani yao.

UDSM walikuwa wastaarabu sana, walitupa zaidi ya siku tatu kujiandaa na kutembelea pale. Hatukujali waswahili sisi. Tayari muda wa kuanza mitihani ulishatimu. Wengi bado wapo nje kuliko walio ndani. Wengi wakataharuki. Wapo walionza kulia. Wapo walioingiwa na hofu ya kuukosa mtihani ule. Wapo waliochanganyikiwa na kutojua kama anaenda ama anarudi. Tupo tuliojikaza kisabuni.


Kati kati ya mvurugano huu na mnyukano huu, kuchanganyikiwa huku, purukushani zote zile, Elizabeth huyu hapa! Sikuamini. Yu ngali na uzuri wake, bado anavutia. Yaani hata sikuamini. Na wewe hakuamini. Ni kama hukumbuki nini kiliwahi kutokea, ulikuwa na zaidi ya furaha usoni mwako. Ushasahau kuwa unatafuta venue yako ya mtihani. Tukakumbatiana (safari hii kwa style yenu)! Tukacheka. Tukapeana namba za simu. Ulisisitiza tuonane baada ya mitihani na kwamba hata lunch tutakula sote pale pale UDSM, ukanambia "dada" ananiulizia sana. Bahati nzuri wewe ulishajua venue ya mtihani wako ni wapi, mimi nilikuwa bado sijajua kwangu wapi!


Nilimaliza kufanya mitihani ile. Niliondoka na hamsini zangu. Sikukutafuta wala sijui kama ulintafuta. Muda ulipita tena. Niliendelea na msimamo wangu wa kutotaka tena mawasiliano na ninyi viumbe. Ulijaribu sana kunipigia simu mara kwa mara. Hukupata mrejesho sahihi uutakao. Kuna wakati nikajaribu kuilazimisha nafsi irudishe hamu na wewe, nikakutembelea! Ulintambulisha kwa mashoga zako kuwa mimi ni nani, uliwaeleza kuwa mimi ni mtu muhimu sana kwako, uliwaambia kuwa kufahamiana na mimi ni bahati ya kipekee kwako.

Nilivimba kichwa mbele ya binti wale, ukanieleza mengi sana. Ukanieleza namna ambavyo una mgogoro mzito na "Yule mtu wako" na kwamba unaona wazi wazi kama uhusiano wenu unaelekea ukingoni. Ukasema penzi limeshachuja. Sikukusapoti katika hii mada. Unaona kuwa jahazi linazama, humuitaji tena kwa maelezo yako. Ulijielezea vizuri huku ukiamini kuwa mimi nakuelewa "unachoomanisha" kwa risala ile.

Ni kweli nilikuwa nakuelewa. Kwamba unafanya "open door policy!" hukujua kwamba tayari nafsi yangu ina kinyongo na watu nyinyi. Na leo kunieleza kuwa una mikakati ya kumwagana na jamaa yako, eti mimi naqualify kuchukua mikoba, nijitwishe mzigo, ndio ulizidi kujiaharibia kwangu. Uliyabomoa wakati ukiyajenga!


Uamuzi wa mimi kutoenda mbali sana na wewe ukapata nguvu mpya. UDSM wakatangaza majina ya waliochaguliwa kujiunga na masomo pale, wewe ulikuwa mmojawapo, mimi nilikosa. UDSM hawakunichagua. Hasira! Machungu! Nilijiona sina bahati. Nilijiona sikustahili kukosa nafasi UDSM. Nilikuwa na II ya points 10. Nawajua washikaji na maduu kibao ambao mwaka uliopita tu, waliingia UDSM wakiwa na II ya 11 na wengine II ya 10 kama mimi, iliniuma sana, niliamini the world is not fair, shida nilizokumbana nazo O level baada ya kufiwa na mtu wangu pekee, mama na bado nikafika A level kwa mbinde, ni kama nauona mwanga afu ghafla giza!

Kuniuma lilikuwa swala moja, lakini kwenda kusema nyumbani kuwa nimekosa nafasi UDSM, lilikuwa swala la pili gumu, gumu sana kuliko hili la kwanza. Ntaanzaje kusema nimekosa nafasi UDSM wakati ukoo mzima unantegemea mimi, ukoo mzima ulifanya dua maalum usiku mmoja kabla ya ule mtihani wa kuchujwa UDSM , maombi yalifanyika ili nipate nafasi, ukoo ulikuwa unajua tayari nikipata nafasi UDSM hali ya mambo pale nyumbani itabadilika, wapo kina dada ambao wangetamba mtaa mzima kuwa kaka anasoma UDSM! Vile viduu vilivokuwa vinaniringia, navyo vingeskia kuwa sasa nasoma UDSM, vingekuja kwa kupishana! Kibaya zaidi, naikosa nafasi ya kusoma UDSM huku nikiwa nimefanya application UDSM na Mzumbe tuu, na tayari nilishakosa Mzumbe mapema lakini sikujali!


Hili lilinipa chuki. Nilijenga chuki kwa watu wengi sana. Chuki hii ilisambaaa mpaka kwako. Nilikuchukia. Sababu sikujua. Sikutaka tena kukuona. Sikutaka tena kukuskia. Nilitaka uniache na yangu na wewe uendelee na yako pale UDSM! Ni kweli uliendelea na masomo UDSM, na mpaka leo sijajua uliishia wapi, kama utausoma huu uzi, mimi nipo, nipo DSM msamariamwema wako,nilihustle sana baada ya pale, karibu nipotee njia, namshukuru m. mungu niliweza kusimama, nikarudi katika njia sahihi, baadae nilienda iaa kufanya IT, nilikuja kurudi udsm kukamilisha ndoto zangu, nipo mtaani, nipo humu jukwaani, maisha yanasonga!


Kumradhi wanaJamii wote ambao wakati wa uwasilishaji wa sredi hii niliwakwaza kwa namna moja ama nyingine, sikuwa na nia ovu, nilipenda mpate burudani na mafunzo kutoka kisa hiki, pale nilipoahidi kurudi hewani afu sikurudi, mniwie radhi! Nashukuru kwa kuchukua muda wenu kunifuatilia! Nawashukuru kwa michango yenu!


Slim5

JF daima!

@1000gb kashesho miss neddy watu8 Blessed g click prospa michepuko naan ngik-kundie Foundation terasy Tarime one MJINI CHAI ZAMBI YANGU Mwana Lipa Kwanza Pritty wa joseph Freeland Mentor Munkari beb v Kanigini lin ram miss ngatara Kan'tangaze monanja Munkari Drama queen JEKI wisu tamuuuuu City hunter j 64gb The Boss muuza ubuyu mtvbase Honey Faith ICHANA Bulldog Denjo
Sauti imenikauka, naomba niitieni na muwapendao tuhitimishe sote!
 
Duu ngoja nimalize mishemishe wikend Leo afu ntasoma nistue sa mojamoja hivi!!!!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom