Padri 'mlawiti' atinga kizimbani
• Akana kosa, adhaminiwa kwa mil.20/-
na Charles Ndagulla, Moshi
PADRI Stanslaus Salla wa Parokia ya Mtakatifu, Theresa Lego Muro, jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za kumlawiti kijana wa miaka 16. Padri huyo alipandishwa kizimbani saa 8 mchana chini ya ulinzi mkali wa polisi ambapo alisomewa tuhuma zake na Wakili wa Serikali Abdallah Chagula, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Simon Kobero.
Katika kesi hiyo CC namba 743/2010 mtuhumiwa huyo alikabiliwa na makosa mawili; ilidaiwa kwamba Oktoba 30 mwaka huu usiku, maeneo ya Kilema Leso wilaya ya Moshi Vijijini, mtuhumiwa huyo alikula njama kwa nia ya kutenda kosa hilo.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mtuhumiwa alikana kutenda kosa na kesi hiyo iliahirishwa hadi Januari 10 mwakani itakapotajwa tena kwa kuwa upelelezi wake haujakamilika.
Hata hivyo, Mahakama hiyo ilimwachia kwa dhamana mtuhumiwa huyo baada ya kutimiza masharti ambayo ni wadhamini wawili waliosaini dhamana yenye thamani ya sh milioni 10 kila mmoja.
Kwa upande wake, wakili wa serikali alionyesha kutilia shaka uwezo wa wadhamini na kuitaka mahakama hiyo ijiridhishe juu ya uwezo wa kifedha wa wadhamini hao ili kuepusha uwezekano wa mshtakiwa kuruka dhamana aliyopewa.
Licha ya kuachiwa kwa dhamana, askari na ndugu wa padri huyo walishirikiana kumtoa kwa siri nje ya mahakama mtuhumiwa huyo huku maelfu ya wakazi wa mji wa Moshi na vitongoji vyake waliofurika kwenye viwanja vya mahakama kushindwa kumwona.
Aidha, kabla ya Padri huyo kupandishwa kizimbani, kulitokea vituko kadhaa kikiwemo cha polisi wanaodaiwa kupewa maagizo maalum kugoma kumuweka mshtakiwa kwenye chumba cha mahubusu cha mahakama hiyo kama ilivyo kwa washtakiwa wengine wa makosa ya jinai.
Kitendo hicho kilionekana kuwakera baadhi ya watu waliofika mahakamani hapo waliosema kuwa mtuhumiwa huyo hakupaswa kunyenyekewa na kulindwa kiasi hicho.