Kortini akituhumiwa kumuua mkewe

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
430
996
Mkazi wa kijiji cha Nyangomango Wilaya ya Geita, Baraka Shija (30) amefikishwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza akishtakiwa kwa kosa la mauaji ya kukusudia ya kumuua mkewe, Grace Daudi kwa kumpiga na kitu kizito kichwani.

Shauri hilo namba 75 la mwaka 2023 limesikilizwa leo Jumatatu Oktoba 30, 2023 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita chini ya Jaji Lilian Itemba.

Mshtakiwa huyo anashtakiwa kwa kumuua Grace chini ya kifungu cha sheria namba 196 na 197 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Wakili wa Serikali, Verena Mathias akishirikiana na Godfrey Odupay ameieleza Mahakama kuwa Juni 23, 2022 huko katika kijiji cha Nyangomango wilayani Geita mshtakiwa alimuua mkewe Grace Daudi.

Ameieleza Mahakama kuwa tukio hilo lilitokea wakati marehemu akiwa shambani ambapo mshtakiwa alimpiga na kitu kizito kichwani juu ya sikio la kushoto.

Mathias ameieleza Mahakama kuwa taarifa za kifo ziliripotiwa kituo cha Polisi Nyakagwe na mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi Juni 24, 2022 na chanzo cha kifo kubainika kuwa kilitokana na kuvuja damu nyingi.

Mshtakiwa amekana kutenda kosa hilo na upande wa Jamhuri utakuwa na mashahidi nane na vielelezo huku upande wa Mashtaka unao ongozwa na wakili wa kujitegemea, Erick Lutehanga ukitarajiwa kuwa na mashahidi watatu akiwemo mshtakiwa mwenyewe.

Shauri hilo limeahirishwa na mshtakiwa amerudishwa mahabusu mpaka litakapopangwa tena na Msajili wa Mahakama.

Wakati huo huo, Mkazi wa kijiji cha Bufunda Wilaya na Mkoa wa Geita, Pascal Batholomeo aliyekuwa akishtakiwa kwa kosa la kumuua Emanuel Constantine ameachiwa huru na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza baada ya kukaa mahabusu kwa miaka minne.

Katika shauri hilo namba 25 la mwaka 2022 limesikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita chini ya Jaji Lilian Itemba mshtakiwa huyo alikuwa akishtakiwa kwa kosa la kumuua Emanuel Constantine tukio lililotokea Oktoba 27, 2029.

Wakili wa Jamhuri, Godfrey Odupoy ameieleza Mahakama kuwa Jamhuri haina haja ya kuendelea na kesi hiyo na kuomba kuiondoa chini ya kifungu namba 91(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022 .

Kufuatia ombi hilo Jaji Itemba ametangaza kuondoa shauri hilo nakusema kuondolewa kwake hakuzuii mshatakiwa kukamatwa tena kama kutokuwa na ushahidi.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom