Operesheni KuKu (kufa kupona). riwaya ya kijasusi

RIWAYA; OPERESHENI KUKU (KUFA KUPONA)

NA; BAHATI MWAMBA

SIMU; 0758573660


VITABU VILIVYOTANGULIA
• KIKOSI CHA PILI
• MPANGO WA CONGO
• URITHI WA GAIDI
• SAUTI YA MTUTU
• DAKIKA ZA MWISHO
• OPERESHENI JICHO LA PAKA
• BAHARIA
• CHUMBA CHA SABA.


Soma

----Beni; Kivu kaskazini Congo.-


Vikosi vya kulinda amani vya umoja wa mataifa (UN) vilikuwa vinatoka kijiji cha Kubuhe na kuelekea mjini Beni ikiwa ni kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia wa maeneo hayo. Vikosi hivi vilikuwa kwenye mizunguko yake ya kawaida na kila siku.
Vikosi hivi vilikuwa na wanajeshi zaidi ya kumi na mbili huku magari ya kijeshi yenye nembo za UN yakiwa mawili na gari moja la kawaida ila nalo likiwa na chapa ya UN lakini pia kulikuwa kuna gari moja la msalaba mwekundu na magari haya yalikuwa yametanguliwa na vifaru viwili huku kimoja kikiwa nyuma na kingine mbele kuhakikisha usalama wa msafara ule.

Katika gari lile la kawaida aina ya Ford; kulikuwa kuna mwanajeshi mmoja na watu wengine wawili ambao walikuwa ni mwanamke na mwanaume huku vifuani mwao kukining’inia vitambulisho vyao ambavyo viliwatambulisha wao ni waandishi wa habari kutoka shirika la habari la umoja wa mataifa ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kuhabarisha ulimwengu yale yaliokuwa yakiendelea katika uwanja wa kulinda amani katika jimbo la Beni ndani ya Kivu ya kaskazini.

Na katika yale magari mawili ya kijeshi pia kulikuwa kuna wanajeshi ambao walikuwa wamebeba silaha zao vyema kabisa huku macho yao yakiwa makini kuhakikisha wanavuka salama katika msitu ule uliokuwa unatenganisha kijiji cha Butuhe na Kabasha kilomita kumi kutoka mjini Beni Kivu ya kaskazini.

Mara nyingi katika misafara hii ya patrol mawasiliano makubwa huwa yanatokana na simu za upepo baina ya msafara na wakuu wa kamandi ya ulinzi na usalama.
Na ndivyo ilivyokuwa hata wakati msafara huu ulipokuwa njiani mawasiliano yalikuwa yanafanyika ili kuhakikisha usalama unazingatiwa kwa wanajeshi wote na matabibu waliokuwa katika msafara ule.

Kwenye gari lile la ford wale waandishi wa habari walikuwa kimya kwa muda mrefu huku kila mmoja akitafakari lake.
Mara mwanaume akawa kama kazinduka kutoka usingizini na akamtazama mwenzake wa kike ambae alikuwa amegemea kiti na dhahiri akiwa mbali kifikira.

Mwandishi wa kiume akajipapasa hapa na pale, kisha akachukua mkoba wake uliokuwa na kamera na kompyuta mpakato.
Alitoa kamera yake na kuitazama kisha akatoa betri zake na kwenye kiunga betri alinyofoa kadi ndogo ya kuhifadhi kumbukumbu.
Kadi ile akaipachika kwenye diski mweko kisha akapichika kwenye kipakatarishi (kompyuta mpakato) na akaaza kuhamisha mafaili kadhaa ambayo ni yeye tu aliejua yana umuhimu gani kwake kisha alipomaliza akatoa na diski mweko na kutoa ile kadi na akarejea tena kwenye kipakatarishi na kufuta yale alioona yanafaa kufutwa.

Wakati akifanya hayo yote kwa kasi ya ajabu; muda wote mwandishi wa kike alikuwa akimtizama tu bila kusema neno.

Bwana yule hakujali macho ya mwenzake bali akajishika kwenye mkanda wake wa suruali na kutoka na kiwembe kikali ambacho mara nyingi hutumika kutahiri watoto.
Akavua shati lake.

“Unataka kufanya nini wewe!!” mwanamke alihoji huku akiwa ametumbua macho kama malaya alieona pochi ya mzungu.

“Tulia kidogo mama” mwanaume alijibu.

Bwana yule akajishika Kifua chake kilichonona minofu imara kwa mazoezi.

Akashika ziwa lake la upande wa kushoto, akagusagusa kidogo kisha akahamia upande kulia akagusa gusa kidogo na aliporidhika akashika kiwembe kwa mkono wa kushoto na kwa utaratibu sana akachana chini kidogo ya mtuno wa ziwa lake la kushoto na akarudia tena kwa kudidimiza zaidi kiwembe na aliporidhika akachukua ile kadi ndogo aliotoa kwenye diski mweko na kuididimiza pale kwenye lile jeraha alilochana.
Aliporidhika akachukua kitambaa laini na kukimwagia unga mweupe na kupaka jeraha lile ambalo lilikuwa linatoa damu na punde damu ikakatika; akachukua tena unga mwingine na kupaka kwenye hilo jeraha lake na kukakauka kabisa kama vile lilikuwa ni jeraha la siku nyingi.

Muda wote mwanamke alikuwa akimtizama bila kutia neno.

Mwanamke akapumua kwa nguvu baada ya jamaa kuvaa shati lake na kupachika kitambulisho chake kifuani.

“Sikwelewi kabisa ujue!!” mwanamke alisema.

“Hisia zangu zimeenda mbali sana kwenye msafara huu hivyo hii ni tahadhari tu” Jamaa alijibu.

“Zedi una….” Akataka kuropoka kitu yule mwanamke na jamaa akawahi kumzuia huku akimkata jicho kali sana.

“Sikia inabidi uzoee kabisa kutokuniita Zedi Wimba na badala yake uendelee kuniita jina hili la Sami Kinyozi na wewe sio Mina ni Kakere Masuti. Sawa bi Kakere?” Zedi akamwonya Mina na kisha hakutaka maelezo zaidi akajilaza kwenye kiti kama vile hakuwa ana maongezi na yule binti.

Msafara uliendelea kwa utulivu wa hali ya juu huku bado wakiwa wanacheza katikati ya msitu mnene wa Bwanga na kwa ubovu wa barabara basi iliwawia ugumu kuwa na kasi zaidi ya mwendo wa aste aste tu.

Zilikuwa zimebaki kilomita mbili kufika mji wa Kabasha ambao upo kilomita saba kutoka mjini Beni Kivu ya Kaskazini.

Kifaru kilichokuwa mbele kikasimama gafla na kufanya magari mengine nayo yasimame gafla huku vumbi likitimka kwa breki kali za gari zile.

Haraka haraka wanajeshi wakashuka na kujipanga kimakabiliano huku mtu wa mwisho kushuka akiwa ni patrol commander.
Wanajeshi wote walikuwa tayari kwa lolote hasa baada ya kuona mazingira yakiwa hayaeleweki na kilichosababisha msafara kusimama hakikuonekana kwa wakati huo.

Patrol commander akapiga hatua kusonga mbele kulikokuwa na kifaru na nyuma yake walifuata wanajeshi wengine wawili ili kumlinda na shambulizi lolote.

Hatimae kilichosimamisha msafara kikaonekaa.

Mbele hatua kama ishirini hivi kutoka kilipokuwa kifaru; kulikuwa kuna gari moja aina ya Land Rover ya wazi bila mambomba ikiwa imesimama huku bunduki kubwa ya msaada (Light machine gun) ikiwa imechungulia kwa mbele na nyuma yake kukiwa kuna mtu alievaa mavazi ambayo yalifanania na ya kijeshi huku suruali yake ikiwa ni ya kawaida tofauti na shati na kichwani alikuwa amefunga kitambaa na mikono yake ikiwa kwenye bunduki ile kubwa iliobeba mkanda wa risasi.
Mbali na mtu yule pia kulikuwa kuna dereva wa land Rover ile.

Patrol commander alinyoosha mkono wake wa kushoto na kuwapa ishara wanajeshi waliokuwa nyuma yake na ishara ile waliitambua mara moja ya kuwa mbele kulikuwa kuna kundi la waasi, hivyo kila mmoja alitakiwa kukaa sawia huku amri ya kushambulia ikiwa ni chaguo la mwisho endapo kutakuwa hakuna maelewano baina ya watu wale na wao.

Kwa kawaida vikosi vya kulinda amani huwa wanashauriwa kutokushambulia kiholela endapo kundi la waasi litakuwa limehitaji mazungumzo mana mazungumzo yanaeza kuwa na tija kwao.

Wakiwa bado wanatazama gari lile, mara watu wengine wenye silaha walijitokeza katikati ya nyasi ndefu huku wakiwa wanabunduki za kivita na vichwani mwao wakiwa wamevaa majani ili waweze kufanana na nyasi, hii ilikuwa ni mbinu moja wapo ya kujificha katika medani ya kivita (camouflage).

Walinda amani wakajikuta wakiwa wamezungukwa na kundi kubwa la waasi wa msituni huku hakuna ambae alikuwa anajua dhumuni la kuzungukwa kule.

Kiongozi wa doria ambae alikuwa ni raia wa Kenya hakuwa na namna zaidi ya kuwataka wanajeshi wake wawe makini kwa lolote.

Hakuna aliemsemesha mwenzake si walinda amani wala waasi na hakuna aliepiga hatua kumfuata mwenzie.

Ukimya ule ulidumu kwa dakika kama tano hivi huku kila jicho likiwa makini na jicho la mwenzake ili kuwahiana kwa hila yoyote ile.

Wakiwa wamedumu kwenye ukimya ule mara kuna gari jingine lililokuwa wazi likatokea porini huku likiwa na wapiganaji wanne wenye silaha na kila waliokuwa wamesimama nyuma ya gari ile na mtu mmoja akiwa amekaa mbele huku nae akiwa amepakata silaha yake.

Gari lile likanyoosha moja kwa moja hadi alipokuwa kiongozi wa msafara wa walinda amani.

Gari ilisimama kisha akashuka yule jamaa ambae alikuwa amekaa mbele, akamsogelea patrol Commander na kumpa mkono kuashiria wapo pale kwa heri na si shari.

“Sisi bwana tumetumwa tuwapelekeni kambini kwetu kistarabu tu” Jamaa alieshuka kwenye gari alisema huku akijitambulisha jina lake kuwa yeye anaitwa Sajini Lolo. Cheo alipokipata hakuna aliejua labda ni huko kambini kwao.

“Huko kwenu tukafuate nini wakati leo hatukuwa na ratiba ya kudoria hadi huko ?” Patrol Commander ambae kicheo alikuwa ni Luteni na jina aliitwa Njeremi; alimwambia Sajini Lolo.

“Ni mazungumzo ya amani tu wala si kwa ubaya ila ni endapo mkitii amri bila shuruti” Sajini Lolo alimwambia Luteni Njeremi.


“Ni itakuwaje tusipoandamana nanyi Sajini!” Luteni Njeremi alimwambia Sajini Lolo.

Sajini Lolo akacheka kwa sauti kisha akachukua sigara yake na kuwasha akapiga fumba kadhaa na kutoa moshi mwingi juu na kusema

“Hivi wewe ni Luteni gani ambae hujui kuwa hadi sasa umetekwa na kikosi chako? Au huoni umezingirwa?”

Luteni akageuza macho pande zote na kuona waasi wengi wakiwa wamewazunguka kila pande.

“Na kisheria mateka ndie anaefuata mashariti ya mtekaji Luteni au nalo hujui?” Sajini aliuliza kimzaha.

“anyway usiogope hakuna baya ni mazungumzo tu ya kawaida komredi” Sajini Lolo alizidi kusema.

Luteni akachumua simu yake ya upepo na kuwasiliana makao makuu na kuwapa taarifa jinsi ilivyo hali yao huko njiani na makao makuu wakamuomba ashushe silaha na awafuate waasi hao huku wao wakiwa njiani kuelekea huko kutoa msaada kama utahitajika.

Ilikuwa ni kitendo ambacho hakuna aliekitegemea hasa kutoka kwenye kundi la walinda amani, pale ambapo kiongozi wao aliwataka wawafuate waasi wale.

Kutoka kwenye gari la wale waadishi; Zedi p.a.k Sami kinyozi alimgusa begani mwandishi Mina p.a.k Kakere Masuti.

“Usihofu ni moja ya kazi iliotuleta huku” Sami alimwambia Kakere.

Lakini kamwe hawakujua usiku mnene aujua ni mlevi Komba. Wao hawakujua kabisa kitatokea nini huko na kama walihisi ni amani basi walikosea sana lakini hayo ni maisha ya mwanajeshi siku zote kifo ni ushujaa kwake.
Na hii ilikuwa ni mwanzo wa operesheni kufa kupona; operesheni KuKu.
Mwamba yupo vizuri
Uhariri Freelancer
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom