Operation Cold Chop-Ghana code G801009

Comred Mbwana Allyamtu

JF-Expert Member
Jun 28, 2016
348
847
"OPERATION COLD CHOP" ILIYO RATIBIWA NA CIA, ILITAMATISHA UTAWALA WA OSAGYEFO KWAME NKRUMAH NCHINI GHANA.

Na.Comred Mbwana Allyamtu
Saturday -5/1/2019

"Operation Cold Chop" ndio ilikuwa code name ya operation hiyo iliyopewa jina hilo na shirika la kijasusi la Marekani la CIA ili liratibu mapinduzi mazima ya kumuondoa madarakani Kwame Osagyefo Nkrumah (Coup that overthrew Dr Kwame Nkrumah) mipango yote ilipangwa Washington DC siku ya tarehe 21/3/1964 na kukamilika siku ya Alhamisi ya tarehe 24 Feb., 1966..

Mapinduzi ya Februari 24, 1966 yalioongozwa na askali wawili marafiki wa jeshi la Ghana ambao walikuwa ni Luteni Jenerali Emmanuel Kwasi Kotoka na Meja Akwasi Amankwa Afrifa kwa kushirikiana na Meja jenerali J.A. Ankra pamoja na mkuu wa jeshi la polisi la Ghana IGP J.W.K. Harlley, katika mapinduzi hayo yaliyo mwanga damu karibu raia 1600 walipoteza maisha, akitangaza mapinduzi hayo asubuhi ya siku hiyo ya alhamisi katika Redio ya Taifa mjini Accra, Luteni Jenerali Kotoka alisema:".....Nkrumah ameondoka na hatarudi tena Ghana. Ameondoka akiwa amechukua pauni milioni sita....."

Wakati hayo yakitokea Accra Ghana, Nkrumah na jopo lake la utawala walikuwa ziarani nchini China akiwa tayali amewasili mjini Peking (Beijing kwa sasa) akiwa hajui lolote linaloendelea nchini mwake, ghafra alifuatwa na Balozi wa Ghana nchini China na kumueleza: "Ndugu Rais ninazo habari mbaya, kumetokea mapinduzi nchini Ghana". Nkrumah akamuuliza "unasemaje?" Akarudia Balozi "kuwa kumetokea mapinduzi nchini Ghana". Akaendelea kumueleza kuwa "kwa kadri habari zilivyokuwa zikitufikia kutoka Accra ni kuwa wanajeshi waliasi na kulitokea mapigano makali sana".

Kwa simu ya maneno haraka Nkrumah akiongea kutoka Peking akatuma taarifa akisema:"Tulieni mkibaki makazini mwenu. Mimi ndiye Rais wa Ghana narejea Ghana haraka. Tumeni habari zenu kupitia ubalozi wa Ghana mjini Peking na si Accra".

Kufatia hali ya sintofahamu baadaye Nkurumah baada ya kushauliana na maafisa usalama wake akaamua kuondoka kuelekea Urusi. Ndege iliyomchukua ilitua Moscow alfajiri na pale kwa kadri muda ulivyokuwa unaenda akaona habari za kupinduliwa kwake ni za kweli na japo alitoa maagizo kwa balozi zote za Ghana kuwasiliana kupitia Peking, lakini kwa hali ilivyokuwa ni wazi hakuwa Mkuu wa nchi tena.

Sasa turejee Accra Ghana kwenye makazi ya raisi yafahamikayo kama Frag staff house ambako Nkrumah alitaalifiwa kupinduliwa kwake.... Huko Accra mapigano kama ilivyosemwa hapo awali yalikuwa makali sana lakini askari watiifu wa kikosi cha ulinzi wa Rais Ikulu walikuwa wagumu kusalimu amri. Walipigana hadi dakika ya mwisho na walipigana hadi ukuta wa Ikulu ya Nkrumah iliyokuwa ikijulikana kama Flagstaff House ukavunjwa. Mwishowe wakawa hawana jinsi bali kusalimu amri. Askari waliingia ikulu na kuchana picha za Nkrumah na kuharibu samani zingine huku wakimlazimisha mama yake Nkrumah aliyekuwa akijulikana kwa jina la Nyanibah amkane Nkrumah kuwa hakuwa mtoto wake wa kuzaa.Mama Nyanibah alikataa akasema Nkrumah ni mwanangu na nitaishi hadi atakaporejea Ghana.

Mama yake Nkrumah pamoja na mke wa Nkrumah ambaye alikuwa ni raia wa Misri wakalazimishwa kwenda kijiji alichozaliwa Nkrumah cha Nkroful kilichopo Magharibi mwa Ghana. Serikali ya Misri kupitia ubalozi wake jijini Accra ulituma gari na kuichukua familia ya Nkrumah yaani mama Fathia na watoto kisha ikatuma ndege iliyowapeleka Misri.

Wakati hayo yakitokea Ghana kule Moscow ndege iliyomchukua Nkrumah ilielekea Guinea ya Conakry mahali ambapo baada ya Nkrumah kuthibitisha kupinduliwa kwake aliamua kuomba hifadhi huko, kabla ya ndege ya Nkrumah kushuka Conakry ilpita kuongeza mafuta Bucharest Romania na Sofia Bulgaria ambapo kote alijaribu kufanya jitihada za kurejea Accra Ghana bila mafanikio.

Sasa turejeshe macho na uchambuzi wetu kwenye viunga vya jiji la Accra Ghana kuona namna mapinduzi yalivyo fanyika na kufanikiwa.... Ilikuwa ni saa 04:00 alfajiri siku ya alhamisi ya tarehe 24 February 1966, ambapo kulifanyika Mapinduzi ya kijeshi yaliyomng'oa madarakani aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Ghana Kwame Nkrumah. Mapinduzi hayo yalifanyika siku mbili tuu baada ya Rais Nkrumah kusafir kwenda Ziarani katika nchi za Vietnam na China.

Usiku huo wa kuamkia tarehe 24, Kanali E.K. Kotoka, Meja A.A. Afrifa, na luteni jenerali J.A. Ankra wakishirikiana na Mkuu wa jeshi la Polisi, IGP Harlley, wanaongoza vikosi vya wanajeshi 600 kuingia katika mji wa Accra na kisha kujigawa Katika mafungu na kwenda kuvamia majengo muhimu ya serikali, ikiwemo 'Ikulu. Kwa muda mfupi tuu majeshi yalifanikiwa kutwaa ikulu na sehemu zingine muhimu, ikiwemo kituo cha redio. Ndipo majira ya saa 12 asubuhi, sauti ya Kanali E.K Kotoka ilisikika nchini kote kupitia Redio ya taifa.

Sauti hiyo ilisikika ikisema hivi: "Fellow citizens of Ghana, I have come to inform you that the military, in cooperation with the Ghana Police, have taken over the government of Ghana today....The Convention People's Party is disbanded with effect from now. It will be illegal for any person to belong to it..." Yaani ..." wanaGhana wenzangu, nimekuja kuwataarifu kuwa Leo hii, jeshi kwa kushirikiana na polisi, tumepindua serikali ya Ghana..na kwanzia leo Chama cha CPP kimefungwa na itakuwa kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kujihusisha nacho."

Baada ya Mapinduzi hayo, Nchi ya Ghana ikawa inaongozwa na baraza la ukombozi wa Taifa, yaani National Liberation Council NLC, na luteni Jenerali Joseph Ankrah akateuliwa kuwa kiongozi wa baraza hilo na hivyo ilimaanisha kuwa yeye ndiye akawa Rais wa Ghana, baada ya Nkrumah. Kwame Nkrumah, akiwa hukohuko ziarani, alipokea kwa mstuko mkubwa kuhusu taarifa za kupinduliwa kwake. Na kitu cha kwanza alichokifanya ni kuwatumia taarifa viongozi wenzake, na kati ya Watu wa awali kabisa kuwajulisha alikua ni rafiki yake wa karibu sana, Sekou Toure, Rais wa Guinea wa wakati huo.

Kutokana na uhusiano mzuri waliokuwa nao maswahiba hawa, Rais wa Guinea akaamua kumpa hifadhi Kwame Nkrumah, na hivyo baada ya siku chache Kwame Nkrumah alitua katika Ardhi ya Guinea na kuanza maisha mapya ya uhamishoni. Na akiwa nchini hapo, tuliona Rais Sekou Toure anamtangaza rasmi Nkurumah kuwa Rais mwenza (Co-President) wa nchi ya Guinea. Hii ni heshima kubwa sana aliyopewa Kwame Nkrumah kwani ilikuwa ni kama vilè nchi inaongozwa na marais wawili kwa wakati mmoja.

Lakini ifahamike kwamba miaka ya nyuma kidogo, Nchi hizo mbili ziliwahi kuunda muungano wao, uliojulikanà 'Ghana- Guinea Union', hivyo kitendo cha Toure kumfanya Nkrumah kuwa Rais mwenza, ilikuwa ni ishara ya kudumisha muungano wao. Kitu ambacho atakumbukwa Kwame Nkrumah ilikuwa ni jitihada zake za kutaka kuunganisha mataifa yote ya Afrika, ikiambatana na falsafa ya "Pan-Africanism." Ndoto ya Nkrumah ilikuwa ni kuona bara la Afrika linaungana kuwa kitu kimoja kwa kudumisha umoja na mshikamano katika nyanja mbalimbali za maisha, ikiwa ni pamoja na kuepuka utegemezi wa nchi za magharibi. Na ndio maana unaona alianza kwa kuunganisha nchi ya Guinea na Ghana, na baadae Mali.

Hivyo basi , kutokana na kufanana kwa falsafa na mitazamo ya Nkrumah na Toure, ilikuwa ni rahisi kwa Nkrumah kukaa nchini Guinea na kuendeleza harakati za PanAfricanism. Alipokuwa Uhamishoni, Nkrumah aliweza kuandika vitabu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya mipango yenye nia ya kurejea Madarakani lakini jitihada zake ziligonga mwamba kwakuwa hakuwa na ushawishi tena nchini mwake. .

Huko nchini Ghana, serikali ya NLC iliendelea kuongoza nchi chini ya utawala wa Joseph Ankrah na tuliona kunafanyika mabadiliko ya katiba ambayo pamoja na vitu vingine yaliruhusu kurejeshwa tena kwa vyama vingi baada ya Nkrumah kuvifungia kwa Muda mrefu. Pia kulipangwa tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu Mwaka 1969. Ambapo Mwezi April 1969, Rais Ankrah ambaye pia ni Mwenyekiti wa NLC, alilazimika kujiuzuru kufuatia skendo ya Rushwa. na hivyo nafasi yake kuchukuliwa na Akwasi A. Afrifa, ambaye aliongoza kama Rais wa Tatu wa Ghana pia alikuwa moja ya askali walio ratibu na kuongoza mapinduzi ya mwaka 1966.

Katika katiba ile Mpya iliamuliwa kwamba Mamlaka au Nguvu ya Rais ipunguzwe, ili kumpa Nguvu waziri Mkuu. Hiyo ilimaanisha kwamba Waziri Mkuu ndiye atakayekuwa na nguvu ya utawala "executive Power" yani mamlaka Zaidi kuliko Rais. Kwahiyo, mnamo septemba mwaka 1969 kulifanyika uchaguzi na chama cha Progressive Party, (PP) kikashinda kwa kura nyingi na hivyo kuweza kuunda serikali inayoongozwa na Waziri Mkuu bwana Kofi Busia. Hivyo, kwa mujibu wa katiba, Kofi Busia, ndiye alikuwa kiongozi mwenye mamlaka zaidi kuliko Rais, ingawa marais walikuwepo. Katika kipindi cha utawala wa Kofi Busia walipita marais wawili, ambao ni Amaa Ollennu pamoja na Edward Akufo.

Katikati ya Mwaka 1970-71, hali ya kiafya ya Kwame Nkrumah ilidhoofika sana kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya kansa. Ndipo Rais Toure akatuma Ujumbe kwenda nchini Ghana kwa kuomba Nkrumah arudishwe nchini Ghana kwa ajili ya Matibabu. Lakini Kofi Busia alikataa ombi hilo. Kwa kifupi ni kwamba huyu Busia alikuwa na uhasama mkubwa na Kwame Nkrumah kwani kipindi cha utawala wa Nkrumah, Kofi Busia ndiye alikuwa kiongozi wa chama cha upinzani, na hata baada ya Uhuru Busia alikimbilia ulaya, na kukaa huko hadi siku Nkrumah amepinduliwa, ndipo akarejea nchini Ghana tena.

Baada ya Nkrumah kukataliwa kurejea Ghana, serikali ya Guinea ikaamua kumpeleka Nchini Romania kwa ajili ya matibabu. Utawala wa Kofi Busia uliendelea hadi mnamo Januari 1972 pale kulipofanyika Mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Jenerali Ignatius Kutu Acheampong. Huyu alikuwa ni mfuasi wa Nkrumah, na moja kati ya sababu zilizopelekea afanye Mapinduzi ni baada ya Busia kukataa Ombi la Nkrumah kurejea nchini. Hivyo yeye alijitahidi sana kuhimiza Nkrumah arudi Ghana kwa ajili ya kutibiwa, licha yakuwa jitihada hizo ziligonga mwamba kufuatia hali ya Nkrumah Kuwa mbaya.

Miezi Mitatu baada ya kuingia madarakani bwana Acheampong, yani tarehe 27 Aprili 1972
taarifa mbaya zikaenea ulimwenguni kote baada ya Kutangazwa kwamba Kwame Nkrumah Amefariki huko hospitalini mjini Bucharest, Romania. Ilikuwa ni majonzi kwa waafrika wengi hususani wale wenye itikadi za kijamaa na Pan-Africanism. Siku ya Jumamosi, Tarehe 29 April 1972, mwili wa Nkrumah ukasafirishwa kutoka Bucharest Romania, kuja mjini Conakry, Guinea. Wananchi walijipanga msururu kandokando mwa barabara, kutokea uwanja wa ndege hadi katikati ya mji , kuupokea mwili wa rais wao (Co-president). Msafara huo ulitumia muda wa masaa mawili na nusu hadi kufika eneo la 'Maison du Peuple' ambapo Rais sekou Toure alikuwa anasubiri kuupokea.

Kesho yake Jumapili, tulimuona Mke wa Nkrumah, Fathia Nkrumah anawasili nchini Guinea akiwa na wanawe watatu. Pale 'Air Port' alipokelewa na mke wa Rais Toure na kisha alipelekwa hadi ikulu kusalimiana na Rais Toure kisha baadae alifika 'Maison du Peuple' kuuona mwili wa Mumewe, ikiwa ni miaka sita tangu waonane kwa Mara ya mwisho walipo agana pamoja Accra Ghana kabla ya Nkrumah kuondoka kuelekea Vietnam kuanza ziara ya kikazi.

Watu mashuhuri na viomgozi wa mataifa mbalimbali waliendelea kumiminika mjini Conakry kwa ajili ya msiba wa Kwame Nkrumah. Baadae ilitangazwa kwamba kutakuwa na ugeni mzito sana kutoka nchini Cuba, ambapo mwanamapinduzi wa nchi hiyo Fidel Castro nae atahudhuria kwenye msiba. Siku ya Mei Mosi, Mwaka 1972, kulifanyika hafla ya kuuaga mwili wa marehemu Nkrumah ambapo historia yake ilisomwa. Viongozi waliohudhuria siku hiyo alikuwepo Fidel Castro, Rais wa Liberia William Tolbert, makamo wa Rais wa nchi za sierra Leone na Kongo Brazzaville. Pia alikuwepo Amilcar Cabral, huyu ni mpigania Uhuru wa Guinea Bissau na visiwa vya Cape verde. Huku Tanzania tuliwakilishwabna spika wa bunge. Lakini sambamba na hao, alikuweo pia mwanamuziki kutoka Afrika kusini, Miriam Makeba.

Wakati huohuo, serikali ya Ghana ilikuwa ikiomba mwili wa Nkrumah urudishwe nchini Ghana kwa ajili ya kuzikwa. Lakini Rais Sekou Toure naye akagoma. Mzozo ukaendelea baina ya pande zote!!..Rais wa Ghana Anataka mwili urudi Ghana, lakini Toure 'anaziba masikio'. Ndipo baada ya kuwepo kwa mvutano, Rais Toure akatoa masharti kwamba ili aweze kuusafirisha mwili, inabidi serikali ya Ghana ikubali yafuatayo, mosi kuwarudisha Kazini watumishi wote waliofanya kazi kipindi cha utawala wa Nkrumah, pia mwili uzikwe mbele ya jengo la Bunge, pia mazishi yafanyike kwa heshima. Majadiliano yalichukua miezi kadhaa hatimaye tarehe 7, July 1972 mwili ukasafirishwa hadi nchini Ghana, Mkewe mama Fathia raia wa Misri akiongozana na Maofisa kadhaa wa Guinea waliuchukua mwili wa Nkrumah na kwenda nao nchini Ghana.

Baada ya mwili kufikishwa nchini Ghana, Wakati mwili wa Nkrumah ukiteremshwa, bado kwenye uwanja wa ndege wa Accra ilikuwepo sanamu ya kiongozi wa mapinduzi ya mwaka 1966, Emmanuel Kotoka ambaye naye aliuawa tarehe 17 April 1967 katika jaribio la mapinduzi ambalo lilishindwa, jaribio hilo lilikuwa na mkono wa Nkrumah wakati akijaribu kutaka kurejea madarakani.

Jeneza la Nkrumah lilipoteremshwa Accra Ghana mama yake Nkrumah anaeitwa Nyanibah ambaye kwa wakati huo akiwa mzee wa miaka tisini na aliyepoteza nuru ya kuona alilipapasa na kuhakikisha mwili wa mwanaye na kusema kuwa sasa ninaweza kufa maana nimeuona mwili wa mwanangu na nimeishi hadi amerejea Ghana. Nkurumah alikuwa mtoto wa pekee kwa mama yake ingawa alichangia ndugu wengine kwa baba yake. Wakati wa utoto wake alikuwa akimsumbua sana Nyanibah kwa kumwambia kwa nini walau hakumpatia kaka au dada wa kucheza naye? Nyanibah akawa anajibu kwa upole na kumwambia: Unaiona miti ile kule mbali msituni? Nkrumah hujibu ndiyo. Kisha mama yake huendelea basi inajitegemea!

Mwili uliwekwa ikulu ambapo Watu waliuaga kwa kutoa heshima zao za mwisho na kisha kesho yake mwili ulisafirishwa kijijini kwao Nkrofu na kuzikwa huko.

KWANINI KWAME OSAGYEFO NKRUMAH ALIPINDULIWA?.

Kupinduliwa kwa Nkrumah kulitokana na siasa za Nkrumah kuegemea katika Ukominist na kuhimiza mapambano ya harakati za ukombozi pamoja na kuunganisha bara la Afrika huku siasa zake zikiegemea katika siasa za ukominist wenye mlengo wa USSR (Soviet) Jambo hili kimsingi ilimjengea uadui Nkrumah katika siasa za Ubepari na hasa Marekani kitu kilichopelekea kuanza kisukwa mipango ya kuondolewa kwake madarakani kwa serekali yake.

Mapinduzi hayo yalipangwa na Marekani kwa ushiriki wa karibu na askali wa Ghana ambao walihaidiwa ulinzi na madaraka na Marekani, kutokana na tishio la kuenea kwa Ukominist wenye mlengo wa Usoviet Afrika kuliipa hofu Marekani jambo lilopelekea kuratibiwa na kutekelezwa kwa mapinduzi hayo, toka kipindi hicho Marekani ilishindwa kukanusha wazi kuhusika na hivyo madai hayo kubaki kuwa ni ya kweli.

Hata hivyo uthibitisho wa Marekani kuhusika ulianza kupata ushahidi na mashiko mwaka 1978 pale John Stockwell, aliyekuwa Mkuu wa CIA nchini Angola katika Kikosi Kazi kipindi Kwame Nkrumah akipinduliwa, aliandika kwamba "Mawakala wa kutoka CIA waliokuwa katika ubarozi wa USA nchini Ghana mjini kipindi mapinduzi yakifanyika pale Accra katika kituo cha Ghana alisema alipokea ujumbe wa simu ya maneno uliosema "Ulinzi uiimarishwe kwa kuwa tayali kikosi cha mapinduzi kumewasiliana kwa ukaribu sana na plotters wa USA na kuwahakikishia kuwa mapinduzi yanafanyika na lazima wawalinde na taratibu zimeundwa tayali."

Baadaye John Stockwell alieleza kwamba alipokea ujumbe mwingine uliosema, "Ndani ya makao makuu ya CIA Kituo cha Accra wapokee taalifa kuwa sasa tayali rasmi fedha kwa ajili ya mapinduzi imetoka na kikosi cha Mapinduzi kiwekwe tayali .."

Wakati hayo yakielezwa na John Stockwell pia Uingereza ilaumiwa baadae juu ya taarifa za siri zilizo achiwa wazi (Declassified information) na baadae Bunge la Uingereza walifanya upelelezi wa nyaraka za MI5 zilizo onyesha kuwa Uingereza walifanya upelelezi wa walaka inayojulikana kama "Swift" ambayo ilionyesha kuwa M15 na M16 walikuwa wameweza kupenyeza duru zao za usalama katika serikali ya Nkrumah mapema mwaka 1964-65 katika mpango wa kuihujumu serikali ya Nkrumah.

CIA, M16 na vikosi vya mapinduzi nchini Ghana walishirikiana kwa karibu kumuondoa Nkrumah katika ikulu ya Flagstaff house, baada ya kupinduliwa bado walimuona Nkrumah kuwa tishio Afrika kwani pamoja na kuishi uhamishino bado njama za kumuua ziliendelea kupangwa na hata wakati moja kurilipotiwa kuwa mpishi wake aliandaa kumuua kwa kumwekea sumu katika chakula kitu kilichokuja kugunduliwa baada ya mpishi mwingine kula chakula kile kabla ya Nkrumah kukila chakula kile kitu kilichopelekea mtumishi yule kufa.

Na ikagundulika kuwa chakula kile kilikuwa na sumu, hivyo kupelekea Nkrumah kuanza kujipikia chakula katika chumba chake bila mfanyakazi wa kuandaa chakula chake. Yeye Nkrumah aliendelea kuwatuhumu mawakala wa kigeni hasa Marekani na Uingereza kuwa walikuwa wanapanga njama za kumuua na hata kuwalaumu kuwa ugonjwa wa kansa alio kuwa nao umetokana na kupewa sumu ya kuvuta harufu ambayo walimuwekea katika njia ya barua

Kifo cha Nkrumah kilidaiwa kusababishwa na ujasusi ulio husishwa na sumu, baada ya kifo chake alizikwa kijiji kwao Nkrofu lakini miaka 20 baadae, yaani 1 Julai 1992, mwili wa Nkrumah ulifukuliwa na kwenda kuzikwa upya tena mjini Accra kwenye jengo maalumu la makumbusho ya Nkrumah ijulikanalo kama "Nkrumah Mausoleum''. Huku Ghana ikimpa heshima kama baba wa taifa hilo huku mitaa kadhaa, majengo ya umma, vyuo vikuu kadhaa vikipewa jina lake kwa heshima yake.

Hii ndio "Operation Cold Chop" iliyo mfuta Kwame Nkrumah kwenye ramani ya siasa nchini Ghana.


Email- mbwanaallyamtu990@gmail.com
IMG_20190507_093652_467.jpeg
 
Back
Top Bottom