Ole wao | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ole wao

Discussion in 'Jukwaa la Lugha' started by X-PASTER, Nov 19, 2009.

 1. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #1
  Nov 19, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 106
  Trophy Points: 160
  Muumba Mwenye viapo kila aina,
  Anatuhakikishia kuwa ipo Siku itasimama,
  Wakati ukiwadia wa kuisagasaga milima,
  Mwezi na nyota zitakapokunjana,

  Ole wao siku hiyo hao wanaokana.

  Aliyetolewa tumboni atamkimbia wake mama,
  Aliyebeba mashaka tisa miezi atamuacha mwana,
  Rafiki na wapenzi walio karibu watafarikiana,
  Ndugu kwa ndugu watakaribia kupigana,

  Ole wao siku hiyo hao wanaokana.

  Sauti ya Mwingi wa Rehema Itakaponguruma,
  Makafiri na wanafiki nyoyo zao hazitatuwama,
  Waliokadhibisha kwao haipo katu salama,
  Vilio vyao havitawaweka sehemu njema,

  Ole wao siku hiyo hao wanaokana.

  Umri uliopotezwa hautarudi nyuma,
  Kwa nguvu watajaribu meno kuyabana,
  Wakijuta kujishughulisha zaidi na ngoma,
  Mipira na starehe zisizokuwa na maana,

  Ole wao siku hiyo hao wanaokana.

  Wale waliokadhibisha Zake nyingi neema,
  Wakafanya usengenyaji kuwa amali ya kuchuma,
  Wakati ukawapita Akhera hawakuitizama,
  Wataburuzwa ndani ya moto hutwama,

  Ole wao siku hiyo hao wanaokana.

  Waliokadhibisha neema watashuhudia Qiyaama,
  Wataingizwa katika moto ulio mrefu na mpana,
  Usio kuwa na kizuri chakula wala huruma,
  Adhabu zitapanda daraja kwa kufuatana,

  Ole wao siku hiyo hao wanaokana.

  Watiifu kwa Mola waliotumia vyema zama,
  Wataingizwa Peponi nyoyo zipate salama,
  Amani na utulivu utokao kwa Karima,
  Utawapatia faraja na furaha daima,

  Ole wao siku hiyo hao wanaokana.

  Waliomcha Mungu watalipwa mema,
  Watakula na kustarehe wapendavyo namna,
  Watakuwa na maisha yasiyo koma,
  Ni malipo yatokayo kwa mwingi wa Rehema,

  Ole wao siku hiyo hao wanaokana.

  Ewe Nduguyangu haujafika wakati bayana?
  Wa kujiweka mbali na sifa za anayekana?
  Ukatenda mazuri na yaliyo mema?
  Je unataka kulipwa mfano wa huyo anayekana?

  Ole wao siku hiyo hao wanaokana.
  A. Hikmany

   
 2. M

  Mbunge wa CCM JF-Expert Member

  #2
  Dec 23, 2009
  Joined: Nov 13, 2009
  Messages: 476
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  1.
  Kwa nini wasema ole, wewe uliye pasta,
  vipi walenga mishale, kwao walio marasta,
  bila kuacha wambele, wa nyuma pia fasta,
  Achana na zako ole, Mwenyezi si kama esta

  2.
  Mwenye enzi si kiumbe, hilo nataka ujue,
  Kuweka kwao viumbe, ole ule atishie,
  Eti awape uvimbe, viumbe wake walie,
  Achana na zako ole, Mwenyezi si kama esta

  3.
  Kaka umche Wenyezi, bila kumdhalilisha,
  Kejeli yake mapenzi, upendo wake kushusha,
  Kama mtia makwenzi, viumbe wake kutisha,
  Achana na zako ole, Mwenyezi si kama esta

  4.
  Kama angekuwa katili, maisha singefadhli,
  Wala asingekubali, viumbe tumsaili,
  Bali sasa tunasali, zetu sala akubali,
  Achana na zako ole, Mwenyezi si kama esta

  5.
  Wacha Mungu msihofu, waovu pata imani,
  Wetu yu mtakatifu, kwake limo tuaini,
  Wala hakumo kuhofu, ni mwema sio haini,
  Achana na zako ole, Mwenyezi si kama esta

  6.
  Eti mwisho wa dunia, hili pia li potovu,
  Yeye hawezi nuia, nchi kufanya majivu,
  Tangu zama liamua, dunia izae mbivu,
  Achana na zako ole, Mwenyezi si kama esta

  7.
  Mbingu ni zake Rabana, dunia ni yetu wana,
  Kukana kwenu laana, ishi kwingine utwana,
  Watoto nanyi vijana, dunia ndiyo yafana
  Achana na zako ole, Mwenyezi si kama esta

  8.
  Hakuna ole jamani, kwao wenye imani,
  Wafurahio nafsini, hapa hapa duniani,
  wakimwamini Manani, fuaha yao yakini,
  Achana na zako ole, Mwenyezi si kama esta
   
 3. Mentor

  Mentor JF-Expert Member

  #3
  Dec 29, 2009
  Joined: Oct 14, 2008
  Messages: 18,720
  Likes Received: 8,274
  Trophy Points: 280
  Mgombea sidakie, na kumkosoa pasta,
  manenoye yarudie, ndo utaelewa fasta,
  hakutuongelea sie, wala wale wenye rasta,
  Mwenyezi si kama Esta, jaribu tajionea!

  Ole wao wenye chuki, na kuonea wengine,
  wakaishi kwenye dhiki, wakizidisha unene,
  kuwakimbiza mikiki, wao wakila senene,
  Mwenyezi si kama Esta, jaribu tajionea!

  kahimizia imani, na mema kwa ndugu zetu
  yani tusile maini, na walale bila kitu,
  hiyo ndo nyepesi dini, itatuongezea utu,
  Mwenyezi si kama Esta, jaribu tajionea!
   
 4. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #4
  Dec 29, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 106
  Trophy Points: 160
  Ulimi ndio chanzo, Watu wengi wamefarikiana.
  Ndimi zimejaa uozo, hadi ndugu kukhasimiana.
  Simu zinaleta mzozo, uongo humo umejazana.

  Uchunge ulimi wako, Mungu Akupatie hifadhi.

  Badili yako mawazo, kumkumbuka wako Rabana.
  Mukhofu Mwenye uwezo, Akinena kun fayakuuna.
  Wewe sie mwanzo, utakufa shaka hapana.

  Uchunge ulimi wako, Mungu Akupatie hifadhi

  Ulimi waleta maangamizo, duniani zahma zimejazana.
  Yakamate yale mafunzo, waliyoacha Mutume al-amiyna.
  Hawakufanya uongo gumzo, uzushi hakupatapo kunena.

  Uchunge ulimi wako, Mungu Akupatie hifadhi
   
 5. Lukolo

  Lukolo JF-Expert Member

  #5
  Dec 30, 2009
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 5,137
  Likes Received: 76
  Trophy Points: 145
  X - Paster, Mgombea ubunge and ebbynature: Congraturalations. Nimeipenda sana kazi yenu, imenikumbusha enzi zileeee! Inaleta raha, manake kila ubeti nilikuwa nausoma kwa tuni fulani. So great guys
   
 6. M

  Mbunge wa CCM JF-Expert Member

  #6
  Dec 30, 2009
  Joined: Nov 13, 2009
  Messages: 476
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  1. Ebi tena umerudi, kabla sikukuu kwisha,
  wasema kama shahidi, kwao wanyonge wakesha,
  pasta wamwona jadidi, mie waona nabisha
  Achana na zako ole, Mwenyezi si kama esta
  2.
  katu sijaupuuza, usawa kwetu viumbe,
  watu sijawauza, ili nilipate sembe,
  hakika ninawajuza, wenye kuleta kimbembe,
  Achana na zako ole, Mwenyezi si kama esta
  3.
  siasa nayo dini, vyote vyapaswa kunena,
  mbunge naye kuhani, naye mtoa adhana
  si chuki bali imani, walama yatakikana,
  Achana na zako ole, Mwenyezi si kama esta
  4.
  Mungu mwenye upendo, apenda wenye kupenda,
  Yeye atupa uhondo hata tunapomponda,
  Pendole lafata mkondo, hatengi walomtenda.
  Achana na zako ole, Mwenyezi si kama esta
  5.
  Umerudi tena pasta, jongea nikupe siha,
  Umjue huyo esta, pia na yule masiha,
  Katu usimwite mista, yuko zaidi ya staha,
  Achana na zako ole, Mwenyezi si kama esta
  6.
  Mbona wajibu ulimi, badala ya wako ole,
  Naona waenda mikumi, sie tukiwa uyole,
  Ama hunacho kilimi, wapaswa kupewa pole,
  Achana na zako ole, Mwenyezi si kama esta
  7.
  Nimekupa elimu, yayo ya Mungu mapenzi,
  sio wako unajimu, pendo lake kutoenzi,
  bali wanadi hukumu, tena yenye makwenzi,
  Achana na zako ole, Mwenyezi si kama esta
  8.
  sitetei huo uovu, bali pendo la mola,
  hilo lapita upevu, wa hao wote ayala.
  sie hatuna ubavu, kwa yeye kutoa mkwala,
  Achana na zako ole, Mwenyezi si kama esta
   
 7. Abunwasi

  Abunwasi JF-Expert Member

  #7
  Dec 30, 2009
  Joined: Jun 25, 2009
  Messages: 3,166
  Likes Received: 1,064
  Trophy Points: 280
  huu ndiyo utamu wa lugha na mambo kama haya ndiyo tunayotaka ahsanteni saaaana kwani mnanikumbusha enzi zilee wakati kulipokuwa na rtd pekee kulikua na kipindi ambacho malenga wa enzi walikua wanachezea lugha yenye mtiririko mwanana
   
 8. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #8
  Dec 31, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 106
  Trophy Points: 160
  1
  Mgombea hiyo dhurma, Siha hutoa manani.
  Hii ni kubwa neema, kutoka kwa Rahmani.
  Na mtu mwenye hekima, hujua yake thamani.

  Soma na utafakari, Husipapie habari

  2
  Ulimi ndio sababu, balaa zote duniani.
  watu ukosa adabu, wakatukana adharani.
  Wakasahau hisabu, kawapata mitihani.

  Soma na utafakari, Husipapie habari

  3
  Kila jambo unabisha, sijuwi niseme nini.
  Wataka Kurekebisha, imetimia mizani.
  Sije kujihaibisha, kukumbushana ni shani

  Soma na utafakari, Husipapie habari

  4
  Wanipatia ilimu, sihitaji maishani
  ilimu ya unajimu, tanitia hasarani
  Wajitia uwazimu mbona hivi ikhwani

  Soma na utafakari, Husipapie habari

  5
  Watu wengi wanasoma, durusu mitandaoni.
  Wanasahau Hikima, Ndo furaha duniani
  Wanasoma wima wima, kujitia hatarini

  Soma na utafakari, Husipapie habari

  6
  Wahenga walisema, maneno mengi ya nini
  sita beti nasimama, kalamu naweka chini.
  Siku yako iwe njema, wewe na wako mwandani.

  Soma na utafakari, Husipapie habari
   
Loading...