Ole wako mwanadamu

Consigliere

JF-Expert Member
Sep 9, 2010
12,037
24,595
Kuna wakati Nimuangaliapo mwanadamu huwa ninasisimuka sana. Ninasisimuka nimuangaliapo mwanadamu katika umoja wake na zaidi pale wanapokuwa katika wingi wao.

Sisisimuki kwa sababu ya jinsia zao au maumbo yao… hapana, bali ninasisimuka kwa ajili ya kile nisichokijua na nikijuacho kuhusu yeye au wao, ninasisimka kwa yale nisiyoyajua kuhusu yeye kwasababu uzoefu unaonyesha kuwa japo una uhakika kuwa hamfahamiani na hamjawahi kuonana hapo kabla lakini cha ajabu ni kuwa tayari kwake yeye unaweza ukajikuta ni lengo lake, ninasisimka kwasababu kuna wakati najua mwanadam anajaribu kufanya jambo ambalo anaamini litamsaidia, wakati yeye mwenyewe hajitambui na wala hana takwimu za mahitaji yake ni kiasi gani. Maisha ya binaadam yametawaliwa na migogoro na maamuzi, migogoro ya ndani ya kichwa chake pia ile ya mtu na mtu na jamii na jamii, upande wa maamuzi ni juu ya nini kifanyike na kifanyike vipi.

Huwa ninatumia muda kila ninapoupata kumfikiria mwanadamu pamoja na mazingira anayoishi, mwanadamu huyu ambaye anajinadi kuwa na uelewa wa juu zaidi ya viumbe wengine, uelewa ambao ni matokeo ya utashi alionao, utashi ambao unamtofautisha na kumuweka juu ya viumbe wengine, kwa sababu unampa uwezo wa kupambanua mambo, utashi unaomfanya maisha yake yatawaliwe na migogoro, kwa sababu ni kupitia migogoro hii ndiyo hufikia maamuzi sahihi juu ya nini kifanyike na kwa wakati upi.

Nikiiangalia jamii tunayoishi ninajiuliza yuko wapi yule mwanadamu mjivuni mwenye akili na kitu cha ziada kiitwacho utashi. Utashi umezaa maarifa ambayo yamepelekea uvumbuzi wa mambo mbalimbali yenye lengo la kuyafanya maisha ya mwanadamu huyu yawe rahisi, mazuri na salama.

Je ni kweli maisha yamekuwa rahisi, mazuri na salama? Ili tuweze kukubaliana au kutokubaliana katika hili yatupasa kwanza tupate tafsiri ya maneno haya ( rahisi, mazuri na salama) kuanzia hapo tuanze mjadala, na mimi kwa makusudi kabisa naongeza mgogoro mwingine… kila mmoja atafsiri kwa namna yake maneno haya, halafu kuanzia hapo mimi nitaundeleza mjadala huu, kuona kama mwanadamu amefanikiwa au la….

Urahisi uko wapi wakati tunashuhudia watu wanashindwa kuyamudu maisha yao ya kila siku, wakifanikiwa ni pale tu wanapoweza kuyapoza makali ya tumbo, ni mazuri kwa kiasi gani wakati huduma za kijamii hususan zitolewazo na ofisi za umma ni kama hazipo kwa sababu wazifanyao ni kama vile wamelazimishwa au wapo kwenye mgomo fulani hivi, ni salama kwa kiwango kipi wakati uhalifu unazidi kuongezeka, na pengo kati ya aliyenacho na asiyenacho linaongezeka. Hapa usalama utatoka wapi.

Wazazi/walezi wamesahau wengine wamelazimika kuyaacha majukumu yao kiasili kwa familia, wote tunafikiria namna ya kuongeza kipato, na kuwasahau watoto na hivyo wakitumia muda mwingi chini ya uangalizi wa wasichana wa kazi (naweza nisilaumu sana katika hili kwa sababu ni matokeo ya mfumo wa kiuchumi wa dunia, ambao ni matokeo ya migogro), watoto hawa mara umri unapoongezeka wanaanza kujitafutia maadili na tabia kutoka kwa wenzao au kupitia mitandao ya internets, Video games na Televisions, hapo tutegemee matokeo yake yatakuwa ni nini? Ni lazima tutapata wanadam lakini wasio na utu ndani yake, ndiyo ninaa maanisha asiye na utu, ikumbukwe kuwa binaadamu ni maumbile na ule uwezo wake wa kibaiolojia, ila hali ya kuwa na utashi ndiyo inaumba utu ndani yake.

Hayo ndiyo yanayonifanya nisisimke sana kila nimuangaliapo mwanadam. Mwanadamu mwenye mipango mingi inayoonekana kuwa ni mizuri lakini inaleta mwisho mbaya.

Je ni kitu gani kinamfanya mwanadamu ajikute hapo alipo, na kila anapojaribu tena hali iishie kuwa hivyo? Wote tunakubaliana kuwa mpaka mwanadamu anapofikiria kuanzisha michakato ya kujikomboa ni kwa sababu anakuwa ameona tatizo na hivyo anajenga dhamira ya kuondokana nalo. Swali linakuja kwa nini kila akitatua tatizo moja yanaongezeka au kujitokeza mengine mengi?

Mimi nadhani hii ni kwa sababu kila tatizo ni sehemu ya tatizo kubwa na pia tatizo lenyewe limejengwa na mengine madogodogo mengi.

Lakini sababu nyingine ninayoipa nguvu mara tatu zaidi ya ile ya kwanza yaani asilimi sabini na tano (75%) ni kwamba:

JINSI TUNAVYOLIONA NA KULICHUKULIA TATIZO NDIYO TATIZO
Hapa nina maanisha kuwa tumekuwa tukikosa utulivu na umakini katika kuyatambua matatizo na kuyaainisha.
Inatubidi tutulie na ili mwisho tuweze kupata akili mpya ya kuweza kuyatatua matatizo yetu.

Pia ieleweke kuwa akili na nguvu iliyotumika katika katika kulibaini au kugundua tatizo si sahihi nguvu hiyo hiyo ikatumika katika kulitatua.

Ndiyo maana kuna kanuni zipo kwa ajili ya ugunduzi wa tatizo ufumbuzi hadi utekelezaji wake, kwa kifupi ni kuwa baada ya kuona tatizo unafuata utafiti na baada ya utafiti kinachofuata ni utekelezaji (Program)
 
Back
Top Bottom