Ole Sendeka adai mafisadi wamempania
Jackson Odoyo
MBUNGE wa Simanjiro kwa tiketi ya CCM, Christopher Ole Sendeka amesema matatizo anayokabiliana nayo kwa sasa na yaliyomsababisha amtandike ngumi mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM) mkoani Arusha, James Millya ni mkakati maalum wa mafisadi unaolenga kumfuta katika uwanja wa siasa na kuonya kuwa wakiachiwa, chama kitakwenda pabaya.
Ole Sendeka alimtwanga ngumi Millya wakati wa mapumziko ya chakula ya semina ya kimila iliyohusu matumizi ya ardhi wilayani Monduli mwishoni mwa wiki iliyopita akidai kiongozi huyo wa vijana wa CCM mkoani Arusha alikuwa akimshambulia wakati akiwasilisha mada yake kuhusu Matumizi na Sheria ya Ardhi.
Ole Sendeka alidai kuwa Millya alidai katika mada yake kuwa wanasiasa wanadhulumu wafugaji ardhi kwa kutumia sheria na kutoa mfano wa Simanjiro, kitu alichotafsiri kuwa alikuwa akinangwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, mbunge huyo aliyejizolea sifa kwa jitihada zake za kupiga vita ufisadi, alisema watu hao wameanza kumwandama ili kudhoofisha jitihada zake za kuendelea kupiga vita ufisadi ndani ya CCM.
Alisema mafisadi hao walianza kumwandama kipindi kirefu ndani ya chama hicho na hivi sasa wamefikia hatua ya kumuangamiza kisiasa ndiyo sababu wameanza kutafuta kila sababu za kumshitaki ili afikishwe mahakamani.
"Wameanza kutafuta kila sababu ya kunifikisha mahakamani ili nikose sifa ya kugombea jimbo langu mwaka 2010 na nitoweke katika siasa," alisema Ole Sendeka na kuongeza:
"Moja ya njama hizo za mafisadi zilianza kuonekana siku moja baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa UV-CCM baada ya mtu asiyejulikana kuniandikia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi kwa laini ya Tigo ukisema kwamba wameshaking'oa kisiki kimoja bado mimi na watafanikiwa kwa sababu hakuna haki hapa Tanzania na kwamba haki iko mbinguni."
Alisema Millya pia aliwahi kumuhakikishia kwamba amejitoa muhanga kwa ajili ya kumngoa katika siasa.
"Nia ya mafisadi hawa inafahamika na leo hii wameanzia kwangu kesho watahamia kwa (mbunge wa Same, Anne) Kilango na baadaye watakwenda kwa (mbunge wa Kyela, Harrison) Mwakyembe ili waweze kufanikiwa katika jitihada zao za kulimaliza kundi linalopiga vita ufisadi ndani ya CCM na kama hawatashughulikiwa kikamilifu na haraka, hali ya chama itazidi kuwa mbaya," alisema.
Alifafanua kwamba Mafisadi hao wasipodhibitiwa kikamilifu hali itazidi kuwa mbaya ndani ya CCM kwani lengo lao ni kutetea ufisadi ndiyo maana alipozungumzia suala la ufisadi katika semina hiyo, Millya alisimama na kuanza kumshambuliwa.
"Shambulio hilo lilikuwa la maneno na hatimaye likawa la mikono kwa kuwa alinirushia ngumi ambayo niliikwepa... alikuwa akinitaka niwataje hao mafisadi ninaowasema na baada ya tukio hilo niliwasiliana na Lowasa akiwa kama kiongozi wa semina hiyo ya kimila, lakini akasema kwamba hawezi kuzungumzia siasa za Simanjiro," alisema Ole Sendeka.
Hata hivyo, Ole Sendeka alifafanua kwamba hana wasiwasi wowote kuhusu taarifa kwamba Millya ana mpango wa kugombea ubunge katika jimbo lake kwa sababu ana haki ya kikatiba kufanya hivyo. Lakini alidai kuwa Millya hajaandaliwa kugombea ubunge wa jimbo hilo, bali kumchafua tu.
Aliongeza kuwa sakata lake na Millya ni ishara tosha kwamba safari hii mafisadi wameamua kumuangamiza.
Pia alidai haikuwa nia ya Millya kulifikisha suala lake mahakamani bali msukumo wa mafisadi, ambao bado hajawaweka hadharani.
Source:
Mwananchi Read News