Ole Sendeka kuburuzwa kizimbani keshokutwa
Mussa Juma Simanjiro
MBUNGE wa Simanjiro kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka, keshokutwa anatarajiwa kuburuzwa mahakamani.
Mbunge machachari, anatuhumiwa kumpiga na kutishia kumua Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wa Mkoa wa Arusha, James Ole Millya.
Akizungumza na Mwananchi jana jijini Arusha, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Basilio Matei, alisema vijana wake wanaendelea na upelelezi kuhusu tuhuma hizo kabla ya kumfikisha mahakamani Ole Sendeka.
"Maofisa wangu wanaendelea na upelelezi wa kesi hiyo na ninatarajia kwamba watakamilisha kazi yao, ili Januari 14 tumpeleke (Ole Sendeka) mahakamani,"alisema Matei.
Kamanda huyo alisema "Ole Sendeka anatuhumiwa kumpiga na kutishia kumuua mlalamikaji kwa kutumia bastola, ambayo imepatika baada ya mtuhumiwa kuidondosha wakati wa tukio".
Wakati huo huo, Ole Millya alipokelewa kwa shangwe katika Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, wakati wa ibaada ya shukrani ya kuombewa baada ya kushinda nafasi hiyo.
Ibada hiyo ilifanyika katika Kanisa la Usharika wa Olkesment na iliongozwa na Mchungaji Emanuel Kweka na kufuatiwa na sherehe kubwa ambayo watu wengi waliihusisha na uzinduzi wa kampeni ya Ubunge wa Simanjiro.
Sherehe hiyo iliyofanyika nyumbani kwa mwenyekiti huyo, ilihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo baadhi ya wanachama wa CCM na waumini wa kanisa hilo.
Wafuasi wa Ole Millya waliimba nyimbo mbalimbali za kumpongeza na kumtaja kama Mbunge Mtarajiwa.
Hata hivyo baadhi ya wafuasi wa Ole Sendeka walisusia ibaada hiyo ya shukrani kwa madai kuwa hizo ni kampeni za ubunge.
Vurugu za viongozi hao, zilitokea juzi katika semina ya viongozi wa mila iliyokuwa inafanyika katika Chuo cha Ualimu Monduli, na Ole Sendeka alikuwa miongoni mwa waalikwa.
Semina hiyo ambayo ilikuwa imeandaliwa na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na kuwashirikisha viongozi wa jadi wa Kimasai. Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chilligati
Habari za uhakika toka kwa viongozi wa CCM, zimeeleza kuwa vurugu hizo huenda zikajadiliwa katika vikao vya maadili vya chama hicho hivi karibuni.
Wakati huo huo mwandishi Hemed Kivuyo, anaripoti kutoka Simanjiro kuwa Ole Sendeka ameiomba CCM mkoani Arusha imuonye Ole Millya.
Sendeka alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mgogoro uliotokea wilayani Monduli muda mfupi baada ya mapumziko ya semina ya wazee wa jadi wa kimasai (Olaigwanani), waliokuwa wakijadili mada za ardhi na nafasi ya mtoto wa kike wa jamii ya wafugaji katika elimu.
Alisema kitendo cha Ole Millya kuandamana kwa magari, pikipiki, baiskeli na miguu kwenda Simanjiro kuwashukuru wajumbe aliomchagua na kutoa shukurani kanisani si cha kuungwa mkono.
Alisema pia inashangaza na kusikitisha kuona mwenyekiti wa UVCCM mkoani Arusha anakwenda Simanjiro kwa 'mbwembwe' kubwa na msafara mzito kwa lengo la kuwashukuru wajumbe na kutoa sadaka kanisani.
"Huyu ni Mwenyekiti wa UVCCM wa Mkoa wa Arusha alipaswa kufanya maandamano yake mkoani Arusha hata yangekuwa kwa mabasi na malori, lakini jimboni Simanjiro kwa maandamano ni ishara ya kutosha kuwa ana lake jambo na chama Mkoa wa Arusha, kinapaswa kumwonya vinginevyo anaweza kuleta balaa kwa wapiga kura," alisema.
Ole Sendeka alisema ingawa hakuna mwenye hati miliki ya ubunge katika jimbo lolote hapa nchini, lakini kwa yanayofanywa na Ole Millya ni ukiukwaji mkubwa wa maadili ndani ya chama na inaelekea anajiandaa kuwania ubunge katika jimbo hilo.
Akizungumzia ogomvi wao na Ole Millya uliofikia hatua ya kutwangana makonde, Mbunge huyo wa Simanjiro alidai kuwa aliuanza Millya kwa maneno na vitendo na kwamba yeye alichokifanya ni kujibu mashambulizi ya hali ya juu ikiwa ni njia pekee ya kujitetea.
Alisema semina ilikuwa ikizungumzia uporwaji wa ardhi na kumwendeleza kielimu mtoto wa kike wa kimasai, lakini yeye alifika hatua ya kumshambulia na kumkashifu wazi wazi hatua iliyomfanya hata mwenyekiti wa kikao hicho Vicenti Parseko Ole Kone Mkuu wa Mkoa wa Singida, kumkatiza kwa kumweleza juu ya kutoka nje ya mada zilizopo, lakini akikaidi hilo.
Alisema ulipofika wakati wa mapumziko alimwendea na kumuuliza lakini alijibiwa kashfa na kurushiwa "konde", jambo lililomsukuma kujibu mapigo.
"Mimi niko tayari kusuluhishwa na mtu yeyote awe wa kidini ama kiongozi wa chama, lakini kwanza lazima kijana huyo aelezwe kuwa anachokifanya nakijua na wanaomtumia kwa hilo nawajua kwa undani zaidi," alisema Sendeka.
Katibu wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Mohamed Mbonde, kuhusu madai kwamba Ole Millya ameanda Simanjiro kwa maandamano alisema hana taarifa hizo na kwamba hilo halihusiani na chama.
Source:
Mwananchi Read News