Salaam wanaJF,
Kama umesoma taarifa yenye kichea cha habari "Oil Com inahusika kuchakachua mafuta", tutaelewana vizuri katika taarifa hii ambayo ni muendelezo wake.
Dereva aliyejitambulisha kwa jina la Sulusi Alex Mkude amekiri kuendesha Scania la Oil Com lililopeleka lita 35,000 za dizeli zilizosadikiwa kuwa zilikuwa zimechakachuliwa, na amekiri kuziwasilisha kwa Gasper Msuya, aliyeajiriwa na kampuni inayotengeneza barabara Ushirombo wilayani Bukombe. Amekuwa dereva wa Oil Com kwa miaka 12 na miezi 6.
Amemtaja kwa jina moja askari polisi wa kituo cha Ushirombo, afande Luso, kuwa ndiye aliyekuwa mpelelezi wa shauri hilo. Anamtaja bosi wa Oil Com ofisi ya Kahama kwa jina moja la Ladwa kuwa ndiye aliita dereva ambaye yeye (Mkude) hamfahamu, akaondoa gari kwenye kituo cha polisi Ushirombo na kuipeleka wanakojua.
Alirejea Dar es Salaamaam Juni 5, mwaka huu. Akaugua kwa wiki moja na siku tatu kisha akajirejesha ofisini-yadi ya Oil Com iliyo Tabata relini ambapo alikutana uso kwa uso na Scania lililomwacha kituo cha polisi Ushirombo.
Anasema akamueleza Abdallah Bushilingi ambaye anawajibika kwake, kila kilichompata safarini. Abdallah akamwambia akazungumze na work shop manager anayetajwa kwa jina la Mbaraka. Naye akamwambia akazungumze na Islam ambaye ni meneja wa depot iliyo Kurasini. Hapo anasema hakuonana naye bali sekretari wake baada ya kumweleza uwepo wa Mkude kupitia simu, Islam alitoa maelekezo kwamba akaonane na Norshad ambaye ni msimamizi wa ofisi za Oil Com Tabata relini.
Akaambiwa, "hamna tatizo, rudi kazini lakini gari lako (scania alilosafirishia mafuta likamwacha kituoni Ushirombo) limerudi likiwa bovu, linatengenezwa hivyo lisimamie litengenezwa vizuri." anawataja mafundi waliyolitengeneza kuwa ni Omari na Rama. lilikuwa na ubovu mbalimbali ikiwemo kupasuka busta.
Akaambiwa kwa kuwa gari lake bovu, atakuwa anaendesha tiper linalofanya kazi za ndani ya kampuni hiyo kwa sababu dereva wa gari hilo alifiwa akaenda kwenye msiba Morogoro. aliendesha gari hilo kwa siku tatu. siku mbili alisomba kifusi kutoka kwenye eneo la kusaga mawe linalomilikiwa na kampuni hiyo lililopo Boko kukipeleka kwenye yadi mpya iliyopo Tabata relini jirani na AMI.
Siku ya tatu anasema alisomba udongo uliyochimbwa ndani ya yadi mpya-AMI kuupeleka kwenye yadi mpya nyingine iliyo Malawi cargo, kufukia mashimo. Dereva wa lori hilo aliporudi, akabaki na bila kazi, Juni 28 mwaka huu akapewa Scania T653 ABG aisimamie itengenezwe, ilipokamilika akaambiwa apakie matenki ayapeleke mkoani Mtwara.
Anasema alipoingia ofisini kwa Norshad kuomba nyaraka za kusafirisha mzigo huo, akaambiwa na Norshad, "Wewe sitaki kukuona ofisini kwangu wala ushike gari langu lolote, toka leo kazi basi, njoo kesho uchukue kiinua mgongo chako."
Anasema alipokwenda Ijumaa (juzi) akaambiwa aende kesho yake (leo) alipofika leo amepewa sh. 150,000/- kuwa ndicho kiinua mgongo chake kwa miaka 12 na nusu aliyofanyia kazi kampuni hiyo.
Anasema kwa muda wote huo hakuwahi kuwa na mkataba wa ajira wala kulipiwa mchango wowote katika mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii (NSSF) hivyo alichovuna pekee ni hiyo laki moja na nusu.
Zaidi anasema ameambiwa, asithubutu kushitaki mahala popote kwa sababu hana atakachopata bali atakuwa amejifungia milango ya ajira ya udereva kwa waarabu wote wanaomiliki magari ya kusafirisha mizigo ndani na nje ya nchi.
Pia anasema ameambiwa hivi, akae atulie, ikibidi atafute shughuli nyingine na kwamba ikipita muda kama mwaka mmoja hivi akihitaji kazi kwenye kampuni yao wanaweza kumchukua awafanyie kazi tena.
HAPA inaibuka hoja nyingine ya maslahi ya wafanyakazi katika mashirika ya usafirishaji wa mizigo masafa marefu kwa sababu kumbukumbu zinaonyesha kuwa mfanyakazi mwingine wa kampuni hii anayeitwa George amefungua shitaka kwenye Baraza la Usuluhishi na Upatanishi, kudai malimbikizo ya mapunjo ya mishahara yake na malipo ya kila siku alizokuwa akisafirisha mizigo ya Oil Com, nje ya Nchi.
Shauri hilo litatajwa tena kwenye baraza hilo la Taifa Julai 5, mwaka huu. Mkude anasema wapo madereva wengi, zaidi ya 300 wanaofanya kazi za kampuni hiyo hawana mikataba ya ajira wala hawalipiwi NSSF. Hoja ni kwamba, ina maana hata NSSF wamewekwa 'viganjani' na Oil Com?
Binafsi inanikera sana, nayaandika haya ili mnao husika najua mnayasoma. mtambue kuwa nchi ikiingia kwenye machafuko jeuri yenu haitasaidia na hao mnaodhani ni wenzenu hamtawaona bali mtashuhudia raia wasiyo na hatia wakiangamia.
Hata kama nyinyi mtafanikiwa kuepuka madhara lakini mtaweza kupoteza ndugu, wapendwa na au wana ukoo wenu na hizo mali mnazokumbatia hamtapata raha ya kuwa nazo kwa sababu zitawasuta kila mtakapoziangalia. Jamani, rudisheni moyo wa uzalendo kwa kuacha kukumbatia watu wenye uraia na asili ya Nchi zaidi ya moja ambao wamegeuza Tanzania kuwa sawa na Ubungo Terminal.
Yaani wapo Tanzania kama wasafiri vile, usafiri wao ukifika (vurugu), kila mmoja wao anachukua kilicho chake na kutokomea. siyo wajinga hawa watu wanajua wanalofanya. hawana hasara ya jina la Tanzania kuchafuka kwa sababu si lao, aibu kwenu vibaraka wao.
Kwa sasa niwaache, tukutane wakati mwingine nitakapowaletea yatakayozungumzwa na Haruna Masebu wa EWURA, Waziri/Naibu waziri au Katibu Mkuu Wizara ya Kazi, Ajira na maendeleo ya Vijana, uongozi wa NSSF - Taifa kuhusu suala zima la makato ya wafanyakazi hususani madereva wa Oil Com