Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, sekretarieti yake imesema Oburu yuko hai, salama na yuko katika hali nzuri, na kuwa Aananchi wanapaswa kupuuza taarifa hizo ambazo imezitaja kuwa propaganda na habari za uongo.
Kwa mujibu wa sekretarieti, wakati taarifa hizo zilipoanza kusambaa, Oburu alikuwa akiandaa hotuba yake rasmi kwa ajili ya hafla ya kukabidhiwa kwa Mausoleum ya kakake Hayati Raila Odinga huko Kang’o ka Jaramogi.
Hata hivyo, Ofisi yake imethibitisha kwamba Oburu anaendelea kufuata ushauri wa madaktari wa kupumzika na kupunguza shughuli nzito za hadharani, huku ikiendelea kusema kuwa yuko macho kiakili na anafuatilia masuala ya chama na taifa.
Taarifa hiyo imekuja baada ya Oburu kwenda Nairobi Hospital kwa uchunguzi wa kiafya. Mkurugenzi wa Mawasiliano wa ODM, Philip Etale, pia alisema Oburu yuko salama na kwamba ziara hiyo hospitalini ilikuwa kwa ajili ya routine check-up.
Aidha Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga pia amesema alimtembelea Oburu na kumkuta katika hali nzuri akiendelea kupata nafuu.