Nyota wa kikapu toka usa kuwasili dar leo 5/9/2011 kuendesha clinic 6-8/09/2011 don bosco

magesa

Member
Aug 19, 2009
10
2
NYOTA WA KIKAPU TOKA USA KUWASILI DAR LEO 5/9/2011 KUENDESHA CLINIC YA KIKAPU KWA VIJANA CHINI YA MIAKA 16, TAREHE 6-8/09/2011, DAR ES SALAAM

Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa Marekani nchini pomoja na wadau wetu wengine kama Coca-Cola kupitia kinywaji cha Sprite na Family Health International(FHI) tuna furaha kubwa leo kwa mara nyingine tena kufanikisha ziara ya kimichezo ya mafunzo ya wachezaji wa zamani wa ligi kubwa ya mpira wa kikapu duniani ya NBA na WNBA.

Wachezaji wanawasili leo jioni kwa ziara hii ni Tamika Raymond WNBA, Becky Bonner WNBA na Dee Brown NBA aliyechezea Dallas Mavericks, wote hawa ni wachezaji walioheshimika sana katika ligi hizo za Marekani. Msafara huo wa wageni toka Marekani utawasili Dar Es Salaam leo tarehe 5/9/2011 saa 6.50 jioni na wataanza mafunzo tarehe 6/9/2011 hadi tarehe 8/9/2011 katika viwanja vya Don Bosco Upanga na wataondoka Tanzania tarehe 9/9/2011.
Mafunzo haya yatafunguliwa na Balozi wa Marekani nchini Tanzania mheshimiwa Alfonso E. Lenhardt (Meja Jenerali Mstaafu) saa 2.30 asubuhi katika viwanja vya Don Bosco, Upanga.

Mwaka 2008 tulikuwa na ugeni kama huu wa wachezaji wa ligi hizo za Marekani - Matt Boner kutoka San Antonio Spurs na Jennifer Azzi mchezaji wa zamani wa WNBA, All Stars na mshindi wa medali ya dhahabu ambao waliendesha mafunzo kwa vijana chini ya miaka 17 katika viwanja wa Don Bosco Upanga kuanzia tarehe 8 hadi 11 Septemba 2008 ambapo jumla ya vijana 150 kutoka katika shule za Secondari 13 za Jiji la Dar es salaam pamoja na Zanzibar walifaidika.
Mwaka jana pia chini ya udhamini wa Coca-Cola kupitia kinywaji cha Sprite tulifanikiwa kuendesha mafunzo kama haya yaliyoendeshwa na mchezaji wa NBA Hasheem Thabeet ambapo vijana 350 walishiri na baadae Mchezaji nyota mwingine Steve Smith toka Marekani alikuja chini ya udhamini wa Sprite kuendesha mafunzo kama haya na vijana 30 walifaidika. Kati ya vijana hao 3 walichaguliwa na walienda katika ziara ya kimichezo Marekani, miongoni mwao mmoja wapo mwaka huu amepata Scholarship ya kwenda katika Chuo Kikuu cha Memorial cha Canada kwa masomo ya chuo kikuu na kucheza kikapu ngazi ya chuo. Pia baadhi ya vijana walitokana na clinic kama hizi sasa hivi wanachezea timu zetu za Taifa za vijana na timu ya watu wazima, na wengine bado tunaendelea kuwafuatilia ili nao wafikie malengo yao.
Hayo ni miongoni ya mafanikio ya mafunzo ya nyuma ya clinic hizi za vijana wadogo.

Baadhi ya vijana kutoka katika clinic hii watachaguliwa na kwenda ziara za mafunzo zaidi nje ya nchi na kuendelea na mipango mingine ambayo tutawatangazia baadae kwa kushirikina na wadhamini wetu.

Kwa upande wetu sisi TBF tayari tumeshamaliza maandalizi ya mafunzo haya tumepata vijana watakao shiriki katika mafunzo hayakutoka mikoa ya Dar-es-Salaam, Kagera, Mara, Tabora, Mtwara, Ruvuma, Singida, visiwa vya Zanzibar, Shinyanga, Kigoma ,Iringa, Rukwa, Lindi na Kilimanjaro ambapo kila mkoa utawakilishwa na vijana 3 walio chini ya miaka 16 na mwalimu 1 wa kikapu.
Tunatarajia kuwa zaidi ya vijana 100 wa kike na kiume watafaidika na mafunzo hayo.

Mbali na Kufanya Mafunzo kwa vijana pia wageni wetu hawa watapata nafasi ya kutembelea na kuongea na wanafunzi wa shule ya msingi mazoezi ya Chang’ombe na sekondari za Makongo na Jitegemee na pia watatemblea maeneo mengine ya Jiji la Dar es salaam kujionea baadhi ya vivutio na utamaduni wetu kama kijiji cha Makumbusho na maduka ya kuuza vinyago maeneo ya Mwenge.

Kwa kufanikisha program hii, sisi TBF na kwa niaba ya wapenzi na wadau wa mpira wa kikapu nchini, tunapenda kuwashukuru kwa dhati kabisa watu wa Marekani, wenzetu wa Ubalozi wa Marekani hususan Balozi Lenhardt pamoja na wafanyakazi wote wa Ubalozi katika kudumisha uhusiano wa kimichezo uliokuwepo baina yetu na watu wa Marekani.
Pia tunawashukuru Coca-Cola, FHI na wafadhili wengine wote waliotusaidia kufanikisa mpango huu.

Nachukua nafasi hii kuwakaribisha watanzania wote waje kwa wingi viwanja vya Don Bosco siku ya ufunguzi saa 2.30 asubuhi na siku zote za mafunzo ili wajionee mafunzo haya ya vijana wetu.

PHARES MAGESA
MAKAMU WA RAIS-TBF
 
Back
Top Bottom