Nyerere, Museveni na rafiki yangu Kabaka

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
BARAZANI KWA RAJAB

Nyerere, Museveni na rafiki yangu Kabaka

Na Ahmed Rajab

SIKU moja karibu na mwishoni mwa Julai 1993, nikiwa ofisini mwangu London kwenye jarida la Africa Analysis, nilipigiwa simu kutoka Kampala na mtu aliyeniuliza: “Vipi, huji kuhudhuria hichi kitu cha huyu kijana?”

Huyo kijana alikuwa ni yeye, Ronald Mutebi. Sisi rafikize humwita “Ronnie”. Kwa hicho “kitu” alikuwa na maana ya sherehe za kutawazwa awe kabaka, mfalme wa Wabaganda.

Nilimjibu kwamba sikualikwa. Akasema kwa tulivyo mimi naye sikuhitaji mwaliko. Hata hivyo, siku ya pili mjumbe wake aliniletea kadi ya mwaliko. Papo hapo nikatayarisha safari ya Uganda.

Wiki chache zilizopita aliniletea ujumbe kunitaka niweko Kampala jana, Julai 31, kwenye maadhimisho ya kutimu miaka 25 tangu awe kabaka. Bahati mbaya jana nilikuwa na udhuru ulionizuia nisihudhurie maadhimisho hayo.

Miaka 25 iliyopita nilipowasili uwanja wa ndege wa Entebbe, Jumamosi mpya ilikuwa inapambazuka. Ilikuwa saa chache kabla ya kuanza sherehe za kumtawaza katika uwanja wa Buddo, Kampala, siku hiyo ya Julai 31.

Nilipofika nyumba niliyoshukia nilimkuta mwenyeji wangu, Dkt. Tajudeen Abdul-Raheem, ameshaamka, amechutama akifua nguo. Siku hizo “Taju” alikuwa akiishi Kampala akiwa katibu mkuu wa Vuguvugu la Umajumui wa Kiafrika (Pan-African Movement), lenye makao yake makuu jijini humo.

Nilimhimiza afanye haraka kwani wakati ulikuwa unatupita. Akaniuliza: “Wakati unatupita kwenda wapi?” Nikamueleza kwamba alikuwa anifuate kushuhudia kabaka mpya akitawazwa. Akanambia kwamba yeye hendi popote. Mambo ya kifalme si yake.

Taju, ambaye hatunaye tena, alizaliwa Funtua, kaskazini mwa Nigeria, na akijua mengi kuhusu watawala wa kifalme wa nchini mwake. Alikuwa pia mwanahistoria aliyesomea sayansi ya siasa na aliyepata shahada yake ya uzamivu (PhD) katika chuo kikuu cha Oxford, Uingereza. Nikishikilia anifuate ili baadaye tuzitafakari na kuzichambua taasisi za kijadi, kama vile za uchifu au ufalme, tuone kama zina faida au madhara kwa mustakbali wa mataifa ya Kiafrika. Dola za Kiafrika zilizoundwa baada ya nchi zetu kupata uhuru kwa kiwango kikubwa ziliundwa kwa kuziiga tawala za wakoloni.

Hata kabla ya mataifa yetu kupata uhuru tumekuwa tukifanya kama nchi zetu zote zimekuwa na uzalendo namna moja ulio sawa. Tumekuwa tukifikiri kama uzalendo wa Zanzibar, kwa mfano, ni sawa na ule wa Tanganyika. Au wa Ghana ni sawa na wa Kenya. Nihisivyo ni kwamba kwa kufanya hivyo tulikosea na tunaendelea kukosea. Tulichotakiwa kufanya, na tunachohitaji kufanya, ni kuitia maanani historia ya kila uzalendo kwani kila uzalendo una historia yake. Na kila historia ya uzalendo wa nchi moja ni tofauti na historia ya uzalendo wa nchi nyingine.

Ingawa Taju alifanya ukaidi kukataa kunifuata, hatimaye aliniridhia nilipomueleza kwamba akinifuata atashuhudia tukio kubwa la kihistoria. Ataishuhudia historia ikinyosha mbawa zake na kupaa mbele ya macho yake. Fursa hiyo haitomjia tena ya kumshuhudia mfalme wa kijadi wa milki kubwa kama ya Buganda akirejeshewa kiti cha ufalme, kwa mbwembwe za utamaduni ulio na maana kwa Wabaganda wenyewe. Na ni Wabaganda wenyewe wenye kuzifahamu mila, desturi na mapokeo yalioufuma utamaduni wao.

Nilimkumbusha kwamba tukio hilo la kutawazwa kabaka lilikuwa na umuhimu mkubwa zaidi kwa sababu lilikuwa linatokea katika nchi ambayo kwa miaka mingi ilikuwa imezipiga marufuku tawala zake zote za kifalme za Ankole, Buganda na Bunyoro pamoja na utawala wa kichifu wa Busoga.

Tawala hizo za kifalme ziliharamishwa na waziri mkuu Milton Obote Septemba 17, 1967 na hivyo kuifanya Uganda iwe jamhuri yeye akiwa rais. Kabla ya hapo, rais alikuwa Kabaka. Tangu Obote aziue tawala za kijadi hakuna rais aliyethubutu kuzifufua isipokuwa Yoweri Museveni, ambaye ungedhani angeendelea kuutengua mfumo huo wa kimwinyi, kwa vile alikuwa na siasa za kimaendeleo.

Baada ya kumueleza na kuzielemeza hoja zangu juu ya historia, Taju alikubali twende pamoja historia ilikokuwa inaandikwa kwa wino wa kijadi, kwa kaida na matambiko.

Mwendo wa kama nusu saa kwa gari kutoka kitovu cha Kampala mtu hufika kwenye kilima cha Naggalabi-Buddo. Ni mahala penye mandhari ya kuvutia. Tangu karne ya 14 wafalme wa Buganda wamekuwa wakitawazwa hapo. Miaka 800 iliyopita wana wawili wa mfalme, Bemba na Kintu waliupigania ufalme mahala hapo.

Kintu alimuua Bemba kwa kumchoma kwa mkuki. Ukenda huko hii leo utaoneshwa mahala hasa alipomuulia Bemba. Baada ya kumuua, Kintu akatangaza kwamba wafalme wote wa Buganda wawe wanatawazwa hapo. Karibu na hapo kuna ile iitwayo Nyumba ya Buganda ambamo mfalme akishatawazwa tu anatakiwa awe anakaa kwa muda wa siku tisa.

Katika siku hizo tisa mwanamume yeyote aliye katika eneo hilo haruhusiwi kumgusa mwanamke. Kipindi hicho cha siku tisa kinaitwa “Enaku Ezobwerinde”, yaani siku za wahka. Katika siku hizo, kabaka huchagua mawaziri wake, akianza na waziri wake mkuu, “katikkiro”, na hupanga mikakati ya kuendesha milki yake.

Pia kuna ule mti mkongwe “Mbonelede” ambao katika enzi ya Kintu ulikuwa ukitumiwa kwa miaka kadhaa kama mahakama ya kijadi ya Buganda kabla ya ukoloni.

Uganda ilipopata uhuru 1962, ufalme wa Buganda ukijiendesha wenyewe ndani ya shirikisho la Uganda. Kulikuwa na serikali ya ubia ya chama cha Uganda Peoples Congress cha Obote na kile cha Kabaka Yekka, cha rais wa nchi, Kabaka Mutesa, baba yake Ronnie.

Hiyo serikali ya mseto ilianguka 1964 kwa sababu ya mvutano baina ya Obote na Kabaka. Obote alipanga kura ya maoni kuyauliza majimbo mawili ya Buganda iwapo yabaki ndani ya ufalme wa Buganda au yarejeshwe kwenye ufalme wa Bunyoro. Kabaka aliipinga kura ya maoni. Obote alishikilia ifanywe. Ilipofanywa, yale majimbo mawili yaliamua yarejeshwe Bunyoro.

Kufikia 1966, Obote alikabiliwa na mgogoro mwingine. Kulizuka mvutano ndani ya chama chake na mvutano huo ungeweza kumuondoa kwenye madaraka. Akaamrisha viongozi wane wa chama chake wakamatwe na kuwekwa kizuizini. Halafu akaisimamisha katiba ya shirikisho, akamuuzulu Kabaka na akajitangaza kuwa rais.

Hayo yalitokea Februari 1966. Kufika Mei 1966 bunge la Buganda lilipitisha azimio lililosema kwamba kwa kusimamishwa katiba ya shirikisho, Buganda haikuwa tena sehemu ya Uganda na bunge hilo likaitaka serikali ya shirikisho ijiondoe kutoka Kampala, mji mkuu, uliokuwa katika ufalme wa Buganda. Obote alijibu kwa kumpeleka Idi Amin kwenda kuishambulia kasri ya Mfalme, Kasri ya Mengo, akitumia silaha nzitonzito.

Kabaka Mutesa alikimbilia Burundi na halafu Uingereza. Mwaka 1967 Obote alitunga katiba mpya iliyozitengua tawala zote nne za kifalme nchini humo. Mutesa aliyekuwa akiishi uhamishoni London alifariki Novemba 1969.

Mwanawe, Ronnie, alipelekwa Uingereza kwa masomo akiwa na miaka 11 mnamo 1966. Baada ya masomo ya sekondari katika shule moja ya watoto wa kibwanyenye Ronnie aliingia Chuo Kikuu cha Cambridge alikosomea anthropolojia na sheria lakini hakumaliza masomo. Alifukuzwa kwa sababu alikuwa mcheza akijishughulisha zaidi na anasa. Mwenyewe anasema alionewa. Akiwajua wanafunzi waliokuwa watundu zaidi yake lakini hawakufukuzwa.

Ronnie alibahatika kuongozwa na binamu yake, ambaye ni kama mlinzi wa mila zao, Mwana wa Mfalme Badru Kakungulu, aliyekuwa mwanachuoni wa Kiislamu. Naye Badru ndiye pia aliyekuwa akimuelekeza namna ya kutekeleza majukumu yake ya ukabaka.

Mimi nilianza kujuana naye katika miaka ya 1970 nilipokuwa msimamizi wa kipindi cha Idhaa ya BBC World Service kilichokuwa kikiitwa “Africa Book of the Day”. Kilikuwa kipindi cha uhakiki wa vitabu na Ronnie alikuwa mmoja wa wahakiki wetu. Alikuwa kijana mahiri aliyekuwa akitafakari mambo kwa makini na alikuwa msomi. Wakati huo alikuwa akiyaandika magazeti ya Uingereza kama lile la kila wiki la “Spectator”, “The Guardian” na gazeti la “African Concord” lililokuwa likiandika kuhusu mambo ya Afrika.

Usuhuba wetu umezidi kukua miaka ikizidi kiasi cha kunifanya niwe miongoni mwa wasiri wake. Sasa naweza kuandika kwamba nilikuwa mmoja wa watu aliowashauri iwapo ende msituni Uganda kukutana na Museveni alipokuwa akiongoza mapambano yaliyompa madaraka.

Alipokwenda huko ndipo alipokubali ya kuwa atamuunga mkono Museveni. Naye Museveni aliahidi kuzifufua falme zote za Uganda zilizokuwa zimefutwa na Obote. Museveni alikuwa na uelewa mzuri wa jinsi nguvu za kijadi zinavyoweza kutumika kuleta umoja wa kitaifa. Yeye na kabaka wamekuwa wakivumiliana wakiendeleza mahusiano yao juu ya msingi wa “nipe, nikupe”.

Ronnie hasahau, na wala mimi sisahau, hafla iliyofanywa katika Royal African Society, London, Mwalimu Julius Nyerere alipokuwa anaaga kabla hajastaafu. Tulikuwa pamoja na Yusuf Hassan, ambaye sasa ni mbunge wa Kamukunji, Nairobi, Kenya. Ronnie alinitafadhalisha nimjulishe kwa Nyerere. Nilimwambia: “Mwalimu, huyu ni Ronnie Mutebi”. Mwalimu alimuangalia kidogo. Halafu nikaongeza: “Ni mtoto wa Kabaka Mutesa.” Mwalimu ghafla aligeuza uso akenda zake. Hakumpa mkono; hakumwambia kheri wala shari. Ronnie aliurejesha mkono aliokuwa ameunyosha, huku akifoka: “Ahmed umeona, umeona?”
 
Jamii yoyote ambayo haihenzi utamaduni wao ni kama "boti bila dira"....namlaumu nyerere kwa kudhoifisha utamaduni wetu....kwakisingizio cha umoja wakitaifa, wakati nchi kama uingereza uholozi ubiligiji nk. wana ufalume wao na umoja wakitaifa wanao...in short waganda wanajisikia raha sana wakiongelea ufalume wao na wanapenda tamaduni zao. Ila tu sisi viongozi wetu walikua wabinafsi hawakutaka watu wengine watukuzwe zaidi yao.
 
Back
Top Bottom