IMEKUWA kama bahati vile kukuta kwenye mtandao huuhuu mahojiano kati ya Mwalimu na Muulizaji maswali hodari huko Akhera kwa jina la Sirafili.
Bila ya kupoteza wakati 'interview' yenyewe tamu na inayofungua macho na masikio kwelikweli (Audio itawekwa baadaye na Mwnakijiji-kama DHL haijafilisika na wakimfikishia mzigo haraka) ilikuwa kama ifuatavyo:
SIRAFIL: Unaonaje maisha yako hapa Mwelimu Sr.?
MWALIMU: Hakika sina cha kulalamika maana nilifuata takriban amri zote kumi nilizotakiwa kama Nasara kuzifuata. Ila niliyumbishwa na ile njia ya Msalaba tu. Hata hivyo kwa kuwa nilikuwa nikisema mara kwa mara mimi binafsi yangu kuwa Mungu kwetu sote Waislamu na Wakiristo ni mmoja hayo nimeyaacha nyuma. Ila naomba wasiniharibie huko duniani kwa kunitakia utukufu jambo ambalo pamoja na cheo nilichopewa astaghafirulillahi hata siku moja sikuomba.
SIRAFIL: Umesikitika kuiacha dunia?
MWALIMU: Hata kidogo!
Nasikitika tu kuwa walioko huko hawajui kilichoko huku na hasa watakaokuwa viongozi kama mimi ambao hawatawatendea watu wao haki!
SIRAFIL: Bado unadhani Ujamaa ni kitu kinachowezekana huko duniani?
MWALIMU: Jibu ni ndio na hapana. Ndio kwa sababu lazima wasio nacho wabebwe na wenye nacho. Hapana kwa maana kwamba usawa sio sera ya huku kwa hiyo haiwezi kuwa ya huko duniani pia. Si unaona hapa tunazidiana sana Sirafil. Unaona wale walioko kwenye maghorofa ambayo mfano wake duniani hakuna. Na wale kule ambao sithubutu hata kuangalia. Wale waliokuwa wanyonge na walioonewa au kuteswa au kuuawa kwa kudai haki zao huko duniani ndio matajiri wa huku. Na wale matajiri na viongozi wakubwa wakubwa huku hawafikii hata daraja la ufakiri hapa akhera. Inatisha!
SIRAFIL: Unasemaje kuhusu Azimio la Arusha?
MWALIMU: Yapo mengi ya kutupwa, lakini kuna mengi pia ya kuyafanyia kazi. Azimio la Zanzibar halikuwa na nia nyengine isipokuwa kuhalalisha viongozi kuwinda na mbwamwitu na kukimbia na sungura. Hilo haliwezekani katu! Kiongozi awe kiongozi. Fulstopu. Akijiingiza kwenye mengine atavuruga mambo tu. Namshukuru sana Mo Ibrahim wa Sudan kwa kuona hili na ninamtakia mafanikio makubwa baada ya kupanda mbegu inayoruhusu wasio waroho, wasio walafi, wasio na uchu wa madaraka kuwa viongozi bora na bado wakatajirika kwa sifa hiyo ya uongozi bora na sio kwa kupora haki na mali za wananchi wao.
SIRAFIL: Ulimuonaje mwanao wa kufikia, yaani, kaka BM katika uongozi wake?
MWALIMU: Kaniangusha sana. Yote niliyomfundisha alisahau. Kaniigiza vibaya, kenda upogo.
Niltaka aprojusi kwanza majeolojisti wetu wenyewe na kisha ashirikiane na Wachina kuchimba dhahabu yetu lakini inaelekea kina Barrick bado wapo duniani na ujanja wao uleule wa kula asilimia 99 na kumuachia mwenye mali asili asilimia moja tu! Au aliridhika na kilo ya dhahabu aliyozawadiwa?
Nilifanya kosa la kutokifanya KISWAHILI lugha ya kufundishia toka nasari hadi Chuo Kikuu sanjari na kuleta walimu toka nje kufundisha lugha za kigeni na hivyo kuwa na Watanzania walioelimika kwa lugha mama yao na wakati huo wanaozivinjari lugha za nje kama mchezo tu. Huku ninaulizwa maswali mengi sanana hakika nina deni ambalo nimeshindwa kulilipa ukizingatia lugha hiyo ilivyonisaidia kuwaunganisha wananchi wangu na kuleta amani na mshikamano nchini. Kama huyu bwana angetupa turufu na kukienzi Kiswahili hivi leo mapungufu yake yote yangekuwa kwenye kaburi la sahau duniani na akhera. Lakini atakufa na kihoro cha kushindwa kufanya mengi ambayo alikuwa na nafasi ya kuyafanya kirahisi tu.
SIRAFIL: Yapo maendeleo makubwa katika mawasiliano nchini mwako hivi leo. Hakuna anayeitegemea tena TTCL. Kuna Televisheni 33 hivi sasa, redio karibu 70 nchi nzima na magazeti 14 ya kila siku na wavuti na blogi kabakaba nchini mwako, unasemaje?
MWALIMU: Je, zinatumika kama vyombo na vifaa vya kuelta maendeleo au vyombo vya kuongeza umasikini, maradhi na ujinga (ikiwa ni pamoja na wizi wa mitihani)?
TEKNOHAMA ni kitu muhimu sana (namsifu yule Mhariri wa magazeti huru ya kwanza kwa kutogoa jina hili) inachukua mahala pa yale niliyosema kama masharti ya maendeleo, yaani, watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.
Ambayo kama ningeliandika upya kitabu changu ningelisema ili tuendelee leo tunahitjai huduma zinazotumia TEKNOHAMA; biashara inayotumia TEKNOHAMA; watu wenye ubunifu na wajasiramali , wasio na ubinafsi wala ulafi, ambao wanaojali usafi, taratibu nzuri na wanaojenga mahusiano mazuri katika jamii; ardhi inayolimwa kisasa na kitaalamu; ardhi inayochimbwa madini yanayosaidia kuondoa umasikini wa Mtanzania; ardhi yenye wanyama wanaochangia biashara kubwa ya UTALII isiyo haribu maadili, utamaduni na utu wetu; siasa zinazoruhusu watu kutajirika lakini wakati huohuo masikini kutoachiwa kufa njaa au kukosa paa au kukosa huduma za afya au kukosa elimu au kukosa mahitaji yote ya msingi; na uongozi unaotambua kwamba una kazi moja tu nayo ni kuongoza na sio kujilimbikizia mali na kwamba familia na watoto wao ni Watanzania wote na sio wale waliowaoa au walioolewa nao au waliowazaa.
SIRAFIL: Unasemaje kuhusu migodi ya DHAHABU waliyopewa watani zako kwa bei sawa na bure!
MWALIMU: Wizi wa mchana! Angalia na laana niliyoiacha, je, huoni mfumo mzima wa Ubepari uko mashakani. Ubepari sio siasa itakayohimili vishindo duniani. Kwa sababu unalea sana ubinafsi na ulafi. Mimi sikukataa watu wasitajirike nilikataa ubinafsi na ulafi. Na huku nimejifunza tatizo kubwa huko duniani ni hili na wala sio jingine.
Ninatamani wangelijua kwamba kwa kuongeza royalty kidgo tu pasingekuwa na haja ya bodi za mikopo kwa wanafunzi wala bima za afya ambako wajanja wanaiba zaidi kuliko wanaohitaji huduma hizo wanavyofaidi.
Bado Tanzania ina madini na rasilimali mali asili za kutosha watoto wake wote kusoma bure; kutibiwa bure; na kupatiwa nyenzo za kuanza maisha kwa gharama sawa na bure.
Mnafuata ushauri wa IMF? World Bank? Hivi mbona hawakuwashauri wakina Gordon Brown na George Bush? Na wenzao wa Euro O-zone?
SIRAFIL: Chama chako kiliwaahidi Waislamu kuabudu kwa mujibu wa dini yao. Na ilani ya chama si uliiona kabla hujaja huku? Si iliahidi kuwarudisha Kadhi wao uliyewapokonya bila sababu za msingi? Vipi bado wanapiga danadana na wewe ulishawaambia kwamba kadhi ni haki yao uliyowadhulumu ?
MWALIMU: Ninashangaa hata mimi. Ahadi ni deni! Niliusimamisha Ukadhi ili tujenge umoja kama nilivyosimamisha kuwepo vyama vingi wakati ule au ushirika uliotishia nguvu za serikali. Sababu ya kuvunja umoja sasa hamna. Watakaovunja umoja ni mafisadi, viongozi wasiokuwa na uwezo wa kuongoza, madikteta uchwara, na wale wanaopayuka payuka ovyo bila kuwa 'sensitive' kwa tofauti zetu za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Aidha kwa chama kukosa sera na viongozi bora, wakweli na safi kama ilivyo huko Afrika Kusini, Zimbabwe na Kenya leo.
Kadhi ni haki ya Waislamu. Na fikira za kipumbavu za baadhi ya watu fulani fulani -kuwa hawa jamaa watapiga watu mawe (kwani yule Mchungaji aliyekampenia DP kule Tarime alipigwa mawe na Waislamu?) , watawachinja watu, watafanya ubaya huu na ule-huu ni unafiki mtupu.
Tatizo ni viongozi wa dini ambazo zina viongozi wanaojilimbikizia mali kutoka kwa waumini wao kuona wivu kwamba na viongozi wa Waislamu nao wanaweza kuneemeka na kuondokana na umasikini na hivyo kuifanya kazi yao pengine vizuri kulikowao wanavyofanya za kwao sasa. Kashfa za ngono, wizi na uporaji makanisani vinawafanya viongozi hao wa dini nyingine pia kutumia 'ukadhi' ili kuficha vitendo viovu vinavyoendelea katika makanisa kadhaa humu nchini bila waumini kujua hili wala lile!
Hivi hawa maaskofu wanaotaka kumfundisha Rais jinsi ya kufanya kazi zake kweli wao watakubali Rais aanze kuwafundisha jinsi ya kufanya kazi zao.
Hawa maaskofu vijana vipi hawa. Wanafanya inductive au deductive reasoning kweli? Mbona naona kama wanaishia kwenye 'fallacies' na kukontradikti hata 'basic tenets' za dini achilia mbali kugombanisha watu na katiba ya nchi ambayo waziwazi inaruhusu watu kupraktisi dini yao kwa mujibu wa sheria na kanuni zao na sio vinginevyo, ikiwemo, Waislamu kuwa na haki ya kufuata sheria zilizoko kwenye kitabu chao kitakatifu!
Kwanini Askofu akosee kwa kusema Mahakama ya Kazi inataka kuanzishwa na sio kurejeshwa? Haoni tofauti ya hili?
Je, maendeleo ya Waislamu sio maendeleo ya Watanzania. Hayo mambo muhimu wanayozungumzia wao ni yapi wakati imeandikwa: ' Pata ufalme wa Mungu kwanza, na mengine yatafuatia!' Au hapo mabwana hawa walisinzia?
Katika dhambi Mwenyezi Mungu anazozichukia zaidi ni dhambi ya UNAFIKI. Viongozi wa dini kwa kweli kama wanataka umoja na amani ya Tanzania iendelee kuwepo ni lazima wawe mbali kabisa na laana hii ya UNAFIKI-yaani kusema uongo ukijua fika unasema uongo; au kuwa na tadi na inda na kumhini anayestahili kupata kitu fulani, kitu ambacho wewe ukipewa pia hutakataa! Na ukijua fika hicho kitamfaa, na hakina balaa kwa wengine!
Aidha, huu ni wakati muafaka wa kunufaika na fedha za IOC kwani nchi za magharibi zimechacha ile mbaya na Vatican au Wajerumani hawawezi kusaidia wananchi wote wa Afrika.
SIRAFIL: Kada wako mmoja kawa swahiba sana wa Marekani na kiongozi wao wa sasa Bwana Kichaka. Unaonaje hili?
MWALIMU: Kapotea! Kapotea sana. Nilimwachia wasia BM-akae mbali na watu hawa kama ukoma. Ni wanafiki wakubwa. Wakikuahidi hutakaa ukipate. Utakufa hujakiona ulichoahidiwa. Hivi hana habari kuwa ni China ndio inayoununua makampuni ya Kimarekani na 'treasury bonds' karibu asilimia 50 za Federal Bank yao. Lakini hili ndio tatizo la vijana virongozi wetu wa Kiafrika. Wanatarajia watu wao wawe wajasiriamali na wagunduzi wa mambo na njia mpya za kutajirika na kutajirisha nchi lakini wao wenyewe hawana chembe ya 'entrepreneurhsip' wala ' intrapreneurship'! Kisha mtu anafanya makosa ya kuzungukwa na watu ambao ni hovyo kuliko hata yeye mwenyewe. Wao sikuzote ni watu wa KUTUMIA lakini hawavuti hatua nyuma hata siku moja kuwaza na kuwazua jinsi ya kuongeza uzalishaji mali na pato la taifa.Bila shaka kazungukwa na watu ambao hawana ushauri wowote wa maana wa kumpa. Angalia hii hotuba yake ya leo Oktoba 14, 2008. Hotuba yote ni kulalamika tu hana la kuwatia watu matumaini. Ni kama vile Watanzania na ninasikia, anasimamia piaAfrika siku hizi hawana wanachoweza kufanya wao wenyewe. Mimi wakati wangu Bwana nisingewaachia BOT peke yao wafanye upembuzi yakinifu na kuja na mikakati juu ya majibu sahihi kwa hili. Ningeleta jopo la watu toka kila kona ya nchi na dunia nzima ili nitoke na kitabu juu ya: ' Mikakati ya Kuhimili Tufani la Fedha na Uchumi katika Dunia ya Utandawazi' ! Na yote haya ningekuwa nimeyasikia wakati wa mazungumzo na waalikwa mbalimbali. Kijana ajaribu hili. Mimi ninadhani vijana wamekuwa sasa. Wasiwategemee sana wazungu. Wana mengi ya kujifunza toka kwa Wajapani, Wachina, Wahindi,Waarabu, Ulaya Mashariki, Wabrazili, Warussi na Wakorea ambao wameshaonja makali ya 'Credit crunsh sometime back' !
SIRAFIL: Umesikia sakata la EPA ?
MWALIMU: Kuna kazi unaweza ukawaachia watu wengine wafanye mwanzo hadi mwisho. Lakini kuna zingine lazima uzifanye mwenyewe au uziidhinishe peke yako. Kisha lazima mtu kutenganisha kati ya undugu na urafiki kwa upande mmoja na kazi kwa upande mwingine. Urafiki huharibu sana kazi! Heri mweke rafiki pembeni umlipe mshahara kila mwezi lakini mambo yako yawe safi. Hili naona kwa hakika mwenzetu linamshinda mshinda vile! Kwa mengine anajitahidi kwa kweli. Lakini ili uwe safi lazima uzungukwe na watu safi-kuanzia nyumbani, katani, jimboni, chamani, Ikulu hadi barazani.
Tatizo kama ni Chama mimi sikuibia serikali kukipa chama. Labda kwa kuwa wakati ule tulikuwa hatuna vyama vingi.
Ukishawafundishia watu tabia ya kudokoa dokoa vya wengine ujue lazima watakudokolea na wewe mwenyewe. Sasa hivi kuna vijana wenye BCom, BBA, MBA -kwanini chama kisijizatiti na kuanzisha upya miradi yake ili iache kupokea asilimia 10 toka kwa wanaoiibia serikali?
Badala ya kumiliki moja kwa moja waanzishe mifuko ya pamoja ya kuwawezesha makada wenye uwezo wa kibiashara aidha mmoja mmoja au katika vikundi katika ubia wa asilimia 60:40 hivi ili chama kiweze kuvuna kinapowekeza na sio kuiba toka hazina!
SIRAFIL: Mradi wako wa NYUMBU hukumuachia mtu urithi?
MWALIMU: Amiri Jeshi Mkuu! Labda kasahau hili. Awaulize rafiki zake Wamarekani jinsi jeshi lilivyogundua na kuanzisha mambo mengi ambayo ni biashara kubwa sana duniani leo. Mrahaba au mrabaha? uongezwe ili jeshi liwe na kitengo cha 'Research and Development ' ili sasa vitu vyote vya msingi vinavyohitajika kutengeneza barabara, reli, mabomba,pampu za maji, majenereta makubwa kwa madogo, mitambo ya hiki na kile ikiwemo ya redio zinazochipua kama uyoga nchini, madaraja na kadhalika viwe vinatengenezwa nchini.
Nilitaka sana kulizungumza hili kabla ya kuja huku lakini ndio tena Ziraili akaniharakisha mno!
SIRAFIL: Unasemaje kuhusu Madaraka Mikoani?
MWALIMU: Ah, nilidhani mwanangu! Kwa hayo, msimamo wangu ni pale pale. Hata Rais akiwa na dege lake mwenyewe na anaweza akaruka toka Mbeya hadi Tanga kwa dakika tano. Bado. Wapeni watu uhuru wa kuamua juu ya masuala yao ya maendeleo ya kiuchumi na jamii.
Mtu wa aja leo, aondoka kesho atakusaidianiii bwanaee! Angalia Tanga, kama mkoa ulivyodumaa, lakini fursa kadhaa zipo za mkoa kuonesha maajabu! Mwataka jenga bandari Bagamoyo, mbona ya Tanga hamjaipanua? Waishia kuiba magari toka Zanzibar kwa majahazi na kuwatajirisha askari walioamia kando ya bahari za Tanga sikuzhizi enhe!!! Au ndio mitihani mnayowapa watu wangu sasa?
Vinginevyo tofauti inavyozidi kati ya mkoa na mkoa itazua mitafaruku itakayowasambaratisha kama Urusi. Na mwishowe kwani wameishia wapi. Hawaoni hawa jamaa kweli?
SIRAFIL: Mwanahalisi, hizi ni habari za karibuni limefungiwa miezi mitatu. Unasemaje?
MWALIMU: Hivi ule ujinga wa serikali kuwa mshtaki, wazee wa baraza, mwendesha mashtaka na jaji bado upo nchini kwetu?
Na wizara ambayo kazi yake ni kufungia tu magazeti ipo? Na waziri wake anajihesabu ni waziri? Au wananchi wameshindwa kuwafundisha viongozi wao ni wizara zipi zinazohitajika. Na fedha yao ya kodi itumike vipi? Shauri yao kama hawajui kuna nchi zina tawaliwa na mijambazi, zinaitwa Kleptocracy. Isije fikia na nchi yetu inatawaliwa na mawaziri na wabunge wanaolipwa mishahara lakini hawana wanachokifanya au hawana kazi unayoweza kuwauliza leo wamfanyani eti? Hatari sana watu wangu wakielekea huko.
Katika miaka hii ni muhimu nchi iwe na MAADILI kwa watu wote. Na kiongozi awe yule anayeishi kwa kufuata na pengine kupiku maadili yote hayo. Kiongozi asiwe juu ya sheria. Tutajuaje kama sio tapeli, kama ndugu zake hawatudhulumu, kama mke au wake zake hawana biashara zisizoelweka, kama watoto wake hawapendelewi na yeye mwenyewe au na watu wanaomzunguka? Kwamba hakuna uovu na dhambi za kutisha zinazofichwa? Na jamaa kasoma hiyo ' FOIA' baada ya kukabidhiwa au kwa uvivu wa viongozi wangu kama nilivyowajua ndio kaenda kubwaga mahala ambako hata hapakumbuki. Angelisoma, hivi angelikuwa na pupa ya namna hii. Au anataka kujipendekeza zaidi ya hapo kweli ....? Si ndio uwezo wake wa juu kabisa? Na hata kauli zake zaonesha hili. Ni vyema viongozi Tanzania wakajua kuwa kuna Watanzania wenye akili, utajiri na takwa mara mia zaidi yao lakini wanaishi kwa kumhofu muumba wao na hawajioneshi katu hadi wanapolazimishwa saaaana! Ukimuona Waziri, Mkuu wa Mkoa, Katibu Mkuu, Mkuu wa wilaya au Mbunge anajisikia na kujiona mkubwa. Keshafika.Hamna kitu hapo. Bomu hilo. Lingoje tu kuteguliwa na kutupwa jalalani uchaguzi ujao! Kiongozi kama nilivyojifunza mimi ni unyenyekevu na kuwatumikia watu. Mtu mwenye ujibari na kutaka kutumikiwa huyo ni mfalme au sultani. Na sijui kama tunawahitaji kwa kweli katika miaka hii? Na hawa ndio pia wenye ile dhambi ya kutaka kujilimbikizia na kujilimbikizia mpaka kama yuel bwana aliyeona pilau kwa mara ya kwanza, anakula na kuzidisha mno na kisha tumbo kupasuka....
Si mmeona walafi wakupindikua na yaliyowakuta au?
Mliona nilivyowalea kina Mag, Roz, Mada na wale wa kufikia sio? Mimi huku silaumiwi kwa kuwapa wanangu haki kuliko haki niliyowapa watoto wote wa Tanzania. Yaani watoto wa Tanzania walifaidi kuliko wangu binafsi walivyofaidi. Uongo?
Hili Sirafil ni tatizo la kumpa mtu Uwaziri kwa sababu za fadhila badala ya uwezo wake. Anaishia kukuabudu badala ya kuwatumikia wananchi. Ni msiba mkubwa sana katika nchi yoyote ile duniani. Nimejenga misingi mizuri. Ningelipenda viongozi wote baada yangu wasikubali kuogopwa au kuabudiwa au kutetemekewa. Maana waoga, wanaoabudu na wanaotetemeka wakikuona au kukusikia tu-aghalabu ni wababaishaji wa kutupwa!
Huyu bwana hajui kwamba kuna Baraza la Habari -ina maana kalidharau? Sikuacha Tanzania Editors Forum (TEF) -kwanini wasiachiwe kumuonya Mhariri mwenzao? Na wao sio kukurupuka tu bali baada ya kuangalia ukweli na haki iko wapi? Mwanzo wa kumuogopa mkuu wa nchi ndio mwanzo wa kukaribisha udikteta wa kishenzi kama ule wa Zimbabwe eti! Watanzania nimewalea uzuri sana wanajua kwanini nilikuwa na kaudikteta wakati ule; lakini siamini kama watamvulia yeyote yule anayetaka kuwa dikteta kwa dakika hata moja- awe katibu kata, mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa, waziri au hata rais wa muungano au wa Visiwani!
SIRAFIL: (Baada ya kusikiliza simu ya mkononi). Alikuwa Jibrili. Ananiambia CHADEMA imeshinda ubunge na udiwani Tarime.
MWALIMU: Sishangai. Hiki si kile chama cha Waziri wangu wa zamani wa Fedha, Edwin? Na kimechukuliwa na mtoto wa rafiki yangu mpenzi, yule Mzee kwenye bustani njema ya ghorofa ile pale.....Ndio chama pekee kinachoweza kuongoza Tanzania ukitoa CCM-A na CCM -B.
Chama changu hakina tena mtu kama Nnauye, Kingunge-walinisaidia sana kuandika andika sera hawa. Sasa ukiweka mtoto wa mjini kuwa Katibu Mkuu wa chama unatarajia nini.
Ninashangaa kwamba chama kimeshindwa kuwapata vijana wazuri kushika nafasi nyeti za chama na badala yake wanalazimika kukimbilia kwenye upinzani au kwenye biashara zisizo na kichwa wala miguu huku tunaachia makapi k uongoza chama. Na chama sasa kimejenga tabia ya kuwakatisha tamaa na kuwafukuza watu wazuri na badala yake ndio hivyo wana pumba tu, kufikia tunaitwa CHAMA CHA MAFISADI na hakuna anayeweza kutoa jibu la kuua na kumaliza kabisa tuhuma kama hii!
Ningelikuwepo duniani ningeliwaandikia CHADEMA kitabu juu ya : 'MIKAKATI ya kupambana na CHAMA TAWALA na kujenga demokrasia ya kweli !'
........na wakati huo huo ningelimuomba yule mwandishi wa BLOGI ya DEMOKRASIA ambayo sijui hata kam CCM wameisoma kuandika kitabu cha kukishauri chama changu jinsi ya: ' CHAMA: MIKAKATI YA KUZALIWA UPYA: Katiba Mpya na Demokrasia Kamili kwa uhai wa CCM!'
Washauri wao wanawadanganya eti kuendelea na Katiba viraka ndio CCM itaendelea kuwepo. La hasha. Katiba ya sasa na tabia zote mbaya za kuutafuta na kuuwekea mikwara upinzani ndio unaochimba haraka kaburi la chama changu. Laiti wangelijua?
Hivi vyama vingine vya njaa kali haviwafai kabisa Watanzania. Hawa ni matapeli kama matapeli wa aina nyingine tu. Ukiwa na padri anayeacha kazi yake ya uchungaji na anakwenda kueneza siasa inayopingana na amri kumi za Muumba unategemea nini? Anakejeliwa hadi na TV ya taifa na haoni wala hasikii? Hakuna laana mbaya kwa mchungaji kama ile ya kuwa mnafiki na nusu hayawani!Unapokuwa na chama cha kina nanihino unategemea kuna baraka za Muumba hapo kweli?
SIRAFIL: TBC imerudi. Unaonaje hili?
MWALIMU: Kweli. Kwanini haikuwa AFRICAN BROADCASTING CORPORATION. Afrika inahitaji Kiswahili sasa kuliko wakati wowote mwingine huko nyumba. Mkinirihusu nitawaambia hili. Ya nyumbani sawa iwe TBC lakini ile ya nje, yaani, redio, TV na internet ziwe ni ABC!
SIRAFIL: Una habari madaraja ya Rufiji na Msumbiji yameshajengwa?
MWALIMU: Daa! Kwa hiyo sina deni tena duniani? Allahamdulillahi. Basi kawaambie Wachagga haraka waende Lindi na Mtwara... ... wakifika hapo tutajenga kusini bila wasiwasi! Aikaeli unasemaje?
SIRAFIL: Unamshauri nini Rais wa sasa kuhusu Kabila na Kongo?
MWALIMU: Unajua ukiacha shamba la mwenzako linavamiwa tu na magugu na wewe unakaa kimya huku jirani zako wengine wakimhinikiza muacha magugu ang'oee magugu japo hawana sauti na uwezo kama wewe unajipalia mkaa hata kabla jua halijatoka.
Askari waliopelekwa na UN huko Kongo ni wakora na watu wanaotafuta maisha na maslahi binafsi tu kwa kujitajirisha na utajiri wa masikini wa Kongo.
Hivi hauoni kuna upofu hapa. Eti Mugabe atume jeshi Tanzania isitume na ni Tanzania inayotishiwa na magugu ya Mashariki ya Kongo?
Vikosi vya magharibi vinatosha kabisa kuleta amani ya kudumu Kongo Mashariki na hivyo kuhakikisha amani Tanzania kwa miaka mingi ijayo. Vinginevyo, vita Tanzania vitaanzia magharibi ya nchi hiyo na vitaletwa na wageni na wala sio wazawa!
SIRAFIL: Hesabu zinaonesha sio tu Watanzania wanalipwa mishahara isiyokidhi mahitaji yao ya msingi bali pia malipo yao yancheleweshwa, yanakatwa ndivyo sivyo na mashirika ya hifadhi na bima yanawadhulumu ziada katika mapato yao yanayowekezwa kwenye mambo mbalimbali. Unasemaje kuhusu hili?
MWALIMU: Ni kweli. Hii ni miaka ya utandawazi na kama tunataka kuumuka haraka na sio kujiweka kwenye mafungu ya umasikini sikuzote lazima tukubali kuwa na wafanyakazi kutoka popote pale duniani wanaolipwa vizuri lakini sio vizuri kuliko wazawa au wenyeji wenyewe. Waende nchi za Uarabuni zilizoendelea wakajifunze hili!
[ Nina hakika nikiipitisha hii kwa Mwalimu Jr. basi itasambaa dunia nzima. Na ingawa haya yamo kama kejeli lakini vionozi wan chi hii wakiyachambua ndani nje watainusuru nchi hii wakati huu wa mashaka na giza Tanzania!-Ideas.Unlimited}