*Njia nyembamba --- 22*
*Mtunzi: SteveMollel*
Kwa kutazama tu uso wa Al Saed ungelifahamu ni kwa namna gani habari hizo zilimgusa. Macho yalimtoka na uso ukawa mweusi kwa haraka mno. Kwa muda alichanganyikiwa akiwa hajui la kufanya. Alisaga meno akikunja ngumi.
"Sawa, tutacheza kwa mujibu wa ngoma!" Alijikuta akisema.
Mara aliamuru naibu mwenyekiti wa kamati ya ulinzi pamoja na mjumbe mtuhumiwa wauawe, tena kwa kunyongwa, punde tu baada ya kuwafanyia mahojiano. Hakutaka hata kuwatia machoni.
"James!" Aliita. "Hamna muda wa kujiandaa tena. Kakusanye watu wako na muanze oparasheni mara moja!"
Aliwatazama Rambo na Johnson, nao akawaambia:
"Unganeni na James. Malizeni wale wasaliti kisha mkakate vichwa vya hao magaidi na kuniletea hapa!"
Haraka James na wenzake wakatoka kwenda kutekeleza amri. Al Saed alirudi ndani akajiandaa na kutoka kwenda kufanya ziara maeneo yaliyorudhika na milipuko.
Loh! Ilikuwa inatisha kuona. Jiji la Monrovia lilikuwa linateketea kama moto wa kifuu. Moto mkali mkubwa ulikuwa umetawala mitaani ukitafuna majengo. Zimamoto wachache waliokuwepo hawakuweza kabisa kuumudu.
Al Saed alistaajabu sana kuona moto huo. Alihisi mwili unaishiwa nguvu. Jasho jepesi lilimteremka. Macho yake yaliweka ukungu wa machozi. Moyo ulimuenda mbio sana akipaliwa na ghadhabu kuu.
Kila eneo lilikuwa limeshikwa na vilio. Kama siyo rafiki, basi ni ndugu ama jamaa alikuwa amekwapuliwa uhai na milipuko hiyo. Wengine walilia kwa hofu juu ya kesho yao iliyoonekena ni ya kubahatisha, wakati wengine wakizirai kwa kushindwa kuhimili.
Ilikuwa ni ndani ya muda mfupi tu maisha yalikuwa yamegeuzwa juu chini, chini juu, mikono ikashika vichwa. Simanzi ilizizima.
"Ni maeneo gani haswa yalilengwa?" Aliuliza Al Saed. Alikuwa amesimama kando na afisa wa kikosi cha zimamoto na uokoaji: mwanaume mnene mweusi aliyevalia nguo za kazi.
"Jengo kuu la makutano ya biashara," alijibu afisa zimamoto. "Soko kuu na makutano ya maduka, mkuu."
Al Saed akasonya kwa masikitiko. Maeneo hayo tajwa yalikuwa ni maeneo yanayokuwa na idadi kubwa ya watu kutokana na mizunguko yake ya kibiashara. Ni maeneo ambayo ni vitega uchumi vizuri vya taifa.
Alishusha pumzi ndefu, akakamata kiuno chake akitazama anga la Liberia. Alijaribu, akilini, kukokotoa idadi ya watu watakaokuwa wamekufa na kujeruhiwa. Hakutaka hata kuuliza maana alihisi angeutoboa moyo wake.
Alishuhudia namna watu wanavyowahishwa hospitalini wakiangua kilio, ama wengine wakiwa hawajiwezi abadani.
Akiwa anaongozana na walinzi wake watatu, alitembea akikatiza mitaa. Akifariji na kutia watu matumaini. Matumaini ambayo yalikuwa kama vumbi jepesi kwenye pepo ya bahari. Macho ya wahanga yalikuwa yamebeba maumivu, na hasira.
"Sitaki kuongea chochote!" Alisema Al Saed akiwatazama waandishi wa habari waliokuwa na kiu ya kusikia neno toka kwake. Waandishi hao walijazana punde tu walipojua uwepo wa kiongozi huyo mkuu maeneo hayo.
"Kiongozi, naomba utuambie msimamo wa serikali yako kuhusiana na hili?" Ilisikika sauti moja ya mwandishi wa habari.
Al Saed alishindwa kupuuzia swali hili. Aligeuza shingo yake akamtazama mwandishi aliyeuliza.
"Msimamo wangu ni kuwaua wote waliohusika na haya mauaji," alijibu na kuongezea, "hakuna yeyote atakayetoka salama. Na wote nitawanyonga chaneli ya taifa ikionyesha mubashara."
Baada ya kusema hivyo basi kazi ikawa kwa walinzi kuwazuia waandishi kwa kuwasukumizia kando wasimbughudhi mkuu kwani hawakukaukiwa maswali, bado waliendelea kuyatiririsha.
Al Saed akipuuzia maswali hayo, alitoa simu yake mfukoni akapiga. Alikuwa anataka kuulizia oparesheni aliyoiagiza. Upande wa pili, bwana James alipokea simu hiyo mara moja!
"Tayari tumewashawatia wote nguvuni, mkuu. Tupo nao tunawahoji muda huu!" James alinguruma hewani.
"Safi sana," akasema Al Saed akitikisa kichwa. "Wabane wawatajie hao wauaji wenzao. Baada ya hapo malizeni kabisa!"
"Sawa, mkuu!"
"James, nataka mrejesho wa maana."
"Bila shaka, kiongozi. Tutafanya kila liwezekanalo."
Simu ilipokatwa, James aliwatazama walengwa wake waliokuwa wamefungwa kwenye viti: naibu mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na mjumbe wake. Watu hawa walikuwa wamelowana damu, sura zao zikitepeta kichapo.
Mkononi mwa James kulikuwa kuna spana kubwa ya chuma. Spana hiyo ilikuwa imechafuka damu. Hata mikono ya James pia ilikuwa mekundu kuashiria imeshika majeraha.
"Sasa tunaingia kwenye awamu ya pili," alisema James. Uso wake haukuwa na masikhara. Mdomo wake aliubinua katika namna ya kuonyesha kebehi.
"Unataka nini tena na nimeshakuambia?" Alilalama mjumbe kwa tabu. Macho yake yalikuwa yamevimba. Mdomo wake ulikuwa unachuruza damu, huku ngao za mashavu yake zikiwa zimejazwa majeraha.
"Hujaniambia ni wapi naweza nikawapata hawa walipuaji!" Alisema James akitikisa kichwa.
"Kwasababu sijui wapi utawapata," akajibu mjumbe. "Hawana makazi ya kudumu kwa sasa tangu makazi yao ya kule kijijini yalivyoharibiwa. Wanakaa popote pale!"
James alikuna kidevu chake. Alimtazama Naibu mwenyekiti wa kamati ya ulinzi, akamuuliza;
"Nani anafadhili hicho kikundi?"
"Sijawahi kuambiwa. Si kila kitu nafahamu kuwahusu," alisema Naibu. Uso wake ulikuwa umevujishwa damu za kutosha kukufanya upate shida kumtambua.
"Kama nilivyokuambia hapo awali, walikuwa wananitumia kwasababu ya kuhofia usalama wangu. Kama ningeliwageuka basi wangelinimaliza."
"Muongo!" Sauti ya Mjumbe ilidakia. James aliyarusha macho yake upesi kwa Mjumbe huyo.
"Wote tulifanya hii kazi kwasababu ya ahadi!"
"Ahadi gani?" Aliuliza James upesi.
"Tuliahidiwa maisha mazuri, na vyeo vinono serikalini," alijibu Mjumbe. Alikuwa anapata wasaa mgumu sana kuongea.
James alitikisa kichwa chake akisema:
"Sawa, sasa tunakaribia kumaliza zoezi letu." Alimgeukia Naibu akamwambia:
Ningependa kukupa nafasi yako ya mwisho ya uhai kwa kusema ukweli. Ni maeneo gani ninapoweza kwenda kuwatafuta hawa watu mbali na kule kijijini?"
Naibu alimtazama James kwanza. Aliona namna gani uso wa James ulivyokuwa mkavu. Alishusha macho yake chini akiyaambatanisha na pumzi ndefu. Akataja maeneo matatu anayohisi yanaweza yakawa yanakaliwa na wanamgambo wa AMAA.
Alipotoa taarifa hizo, James aligeuka malaika Israel akanyofoa roho zao akiwanyonga kwa mikono yake mwenyewe. Kisha akapiga simu kuwataarifu wenzake.
***
Ndani ya sebule ndogo yenye samani zilizopangiliwa vema. Picha kubwa ya farasi wawili; mweusi na wa kahawia ilikuwa inaning'inia ukutani. Mezani kulikuwa kuna bakuli kubwa la kioo likibebelea matunda mbalimbali.
Pembeni ya meza hiyo kulikuwa kuna makochi mawili tu ya ngozi rangi kahawia. Kila kochi likiwa limeegemea dirisha kubwa la chuma.
Sebule hiyo ilikuwa pweke, na kulikuwa kimya. Ila baada ya muda mfupi, sauti zilisikika nje ya sebule. Ilikuwa ni ya mwanaume na mwanamke. Sauti hizo zilisogea karibu na sebule na mara mlango ukafunguliwa.
Alikuwa ni Kone na Rose. Kone alikuwa amevalia kaunda suti rangi ya udongo, Rose alikuwa amejisitiri kwa kuvalia bukta ya kitenge na tisheti jeupe.
"Karibu!" Alisema Rose akitabasamu.
"Ahsante sana, Rose. Nimeshaingia sasa."
Kone aliketi, Rose akamletea kinywaji; juisi ya embe ndani ya glasi kubwa. Kone hakutaka chakula.
"Kazana kula, Rose. Umekonda sana," Kone aliteta. Rose akatabasamu.
"Kwani nimekuwa mbaya?" Aliuliza.
"Hapana, sema sijazoea kukuona hivyo. Naona kama unaumwa."
Kwa mtu ambaye hakuwa anamfahamu Rose hapo kabla, asingegundua tofauti yoyote ile kwa mwanamke huyo. Bado alikuwa mzuri na mwenye kuvutia. Hakuwa ametia kikorombwezo chochote usoni mwake, lakini aliita.
"Itabidi uzoee, Kone. Nataka kubakia hivi hivi niweze kufanya kazi yangu vizuri."
"Kazi ipi?"
"Ya kummaliza Talib! Siwezi nikamuacha hata kidogo kwa namna alivyon'tendea. Lazima nimmalize kwa mikono yangu mwenyewe!"
"Si rahisi kihivyo, Rose."
"Najua. Nitaenda na ugumu wake hivyo hivyo. Lazima nimuue, mara hii niende jela kwa kustahili!" Rose alipiga ngumi paja lake kwa msisitizo.
"Nisingependa kukupoteza, Rose," Kone alisema akimtazama mwanamke huyo machoni. "Kuna mambo makubwa na muhimu sana tunapaswa kuyatekeleza. Na mambo haya si tu kwa faida yetu bali kwa taifa zima."
Rose alimtazama Kone kwa umakini. Alikitikilia maanani kila litokalo kinywani mwa mwanaume huyo.
"Hapa tunavyoongea, Guinea ipo kwenye hali mbaya. Vita yaweza kutukia siku yoyote. Natilia mashaka sana juu ya uchaguzi huu unaokaribia, hauwezi kuisha kwa amani ... sasa nataka tukaokoe jahazi nyumbani, Rose."
"Umejuaje kuhusu haya, Kone?" Rose aliuliza, na kuongezea: "Ni kwa muda mrefu sina habari juu ya kinachoendelea huko."
"Ni habari ndefu kidogo nitakayojaribu kuifupisha ..."
Maongezi hayo hayakudumu, mara yakakatishwa na mlio wa ujumbe kwenye simu ya Kone. Mwanaume huyo alitoa simu yake mfukoni akaitazama. Alikuwa Amadu.
"Kama una muda, naomba tuonane nje ya makazi yako sasa hivi." Ujumbe ulisomeka hivyo.
"Sawa, nakuja." Kone akajibu upesi.
Rose aligundua mabadiliko kwenye uso wa mwanaume huyo. Alipata hamu ya kujua, akauliza:
"Vipi Kone kuna nini?"
Kone akamueleza juu ya Amadu.
"Tunaweza kwenda wote?" Rose aliuliza. Macho yake yalijawa na ashki. Alikuwa tayari ameshasimama.
"Ngoja kwanza," Kone akamtuliza, kisha akamtumia ujumbe Amadu juu ya ujio wake na Rose.
"Unamuamini?" Ujumbe wa Amadu uliuliza.
"Ndio, namuamini sana," Kone akajibu.
"Sawa, unaweza kuja naye." Akapewa ithibati.
Rose alijiandaa upesi kwa kuoga na kujivika suruali, kisha wakatimka na Kone kwenda mahali walipoelekezwa na Amadu wakutane. Walifika eneoni wakakuta patupu.
Amadu alikuwa ameketi kando akiwatazama. Zilipopita dakika tatu akihisi shwari, ndipo akajongea kuwafuata. Alikuwa amebebelea begi kubwa jeusi mgongoni. Alivalia tisheti jekundu, suruali nyeusi ya jeans na viatu vya wazi.
Alisalimu kisha akapendekeza wakafanyie maongezi yao ndani ya gari alilokuja nalo; Suzuki Vitara. Pendekezo hilo likaungwa mkono na wote.
"Kuna jambo nimeona ni vema nikakushirikisha Kone," alisema Amadu. Alikuwa amekaa viti vya mbele yeye na Kone wakati Rose akiketi nyuma. "Si tu kwamba kwasababu linakuhusu, bali unaweza ukatoa mchango wako mkubwa sana.
Kwa muda mrefu sasa, mimi na wenzangu tulikuwa tumetenga muda wa kuchambua mambo kwa kina kuhusu siasa za huu ukanda wetu. Na yote hiyo ni kwasababu tuliona hatuwezi tukatibu nchi moja wakati zingine zikiendelea kuumwa, kwa maana nchi hizi huambukizana, huathiriana kwa namna kubwa mno. Kwa Liberia kuwa na amani, basi Sierra na Guinea zinapaswa kuwa tulivu. Vilevile kwa Sierra na Guinea. Hakuna anayebaki salama wakati mwenzake akiwa vitani.
Tulikuja kugundua kwamba, unaweza ukawa unaipigania nchi yako ndani ya nchi jirani. Ukahangaika kusuluhisha na kumaliza migogoro yao kwa ajili ya kwako kuwe hai, kwasababu mbegu ya chuki, uhasama na ukabila huzaa mti mpana wenye matawi marefu yanayoziba mwanga wa jua. Siyo tu kwa aliyepanda, hata pia kwa majirani. Nyoka watakaokaa hapo, hawatamng'ata tu mwenye nyumba, bali pia na jirani.
Hivyo basi kuukata mti huo si kazi ya mwenyenyumba pekee, yumo pia na jirani.
Kulitambua hilo kukatupa nguvu na haja ya kusambaza watu wetu kila kona ya nchi hizi. Watu hawa kazi yao ilikuwa kuwa macho na masikio. Waone kila liendalo, wasikie kila lisemwalo. Kazi yao ilikuwa kukusanya taarifa za kutosha, za kina, ili tujue nani chanzo, nani mtekelezaji, nani funiko.
Katika hilo tukafanikiwa, kilichobakia sasa ni utekelezaji. Hapa tuongeavyo, kikundi cha THE GHOST kipo tayari muda wowote kuanza kuisaka shwari. Katika hili, ningependa tuwe pamoja.
Ila pia ningependa kukupa wasaa wa kufikiria."
Amadu alifungua begi akatoa mafaili matatu na kumkabidhi Kone. Kila faili lilikuwa lina rangi yake, na juu ya kila faili kulikuwa kuna jina la nchi moja miongoni mwa Sierra Leone, Liberia na Guinea.
"Kwenye kila faili, kuna picha na maelezo ya kila mmoja tunayetakiwa kummaliza, pia sababu na njia za kufanya hivyo. Chukua muda wako kapitie, alafu utanipa mrejesho karibuni.
Muda si mpenzi wa kweli," Amadu alihitimisha.
****
☆Steve
Sent using
Jamii Forums mobile app