Njia nyembamba (Simulizi mpya by SteveMollel)

*Njia nyembamba -- 19*




Mtunzi: SteveMollel





Ni furaha kubwa kwa Al Saed. Fursa ya kuhema ilikuwa imepatikana sasa baada ya kunyanyaswa kwa muda. Alikutana na kikundi chake cha oparesheni huko ikulu kwa ajili ya kuwapongeza. Aliwaalika pia na viongozi wake wa usalama ambao kwa muda wote huo alikuwa amewaficha aliyokuwa anafanya.

Kwa idadi walionekana watu ishirini na tano ndani ya uwanja wa tafrija wa ikulu. Mikononi walikuwa wamebebelea glasi za vinywaji vilivyokuwa vinapitishwa kila pale vilipokauka vyomboni. Hakukuwa na viti, watu wote walikuwa wamesimama. Taratibu muziki laini ukiwa unasindikiza shughuli.

“Leo ni siku ya furaha sana kwangu, na kwa taifa kwa ujumla!” alipaza sauti Al Saed akinyanyua juu mkono wake uliobebelea glasi ya kinywaji. “Sina haja ya kusema sana, nimepaliwa na furaha. Kazi ambayo imewashinda simba, fisi wakaitekeleza.”

Maneno hayo yaliwafanya viongozi wa usalama watazamane kwa macho ya tai. Midomo yao haikutema kitu ila kwa namna waliguswa. Walitabasamu kwa aibu.

“Najua kuna wanafki miongoni mwetu,” aliendelea kumwaga Al Saed. “Hapa wamevaa ngozi ya kondoo ila ndani ni fisi. Ni kitendo tu cha muda, nitawagundua. Na punde nitakapowagundua, watafia mikononi mwangu.” Alisema Al Saed akionyeshea ngumi yake nzito.

Kulikuwa tulivu muziki ukiwa unavuma kwa mbali. Sauti ya Al Saed ilikuwa inanguruma kama simba mwituni. Kila mtu alikuwa amenyamaza akimtazama kwa kuguswa. Sura yake ilikuwa imejifuma katika namna ya umakini akimaanisha ayasemayo.

“Ni aibu sana!” alipaza. “Ni aibu kuona kazi zinaenda pale tunapoifanyia vichochoroni. Kisa tu watu wachache! Watu ambao hawataki kuiona Liberia inatamalaki kwa amani.”

Alisafisha koo lake, akanywa fundo moja la kinywaji. Ni kana kwamba maigizo jukwaani namna watu walivyokuwa wanamtazama.

“Hii ni nafasi yao ya pili; nafasi ya kujitazama, kujikosoa, kujitathmini. Na ni kwasababu naamini kwenye nafasi ya pili. Nafasi ya pili, nafasi ya mwisho. Tufurahi!”

Alinyanyua tena mkono wake juu, watu wakagongesha glasi na kuendelea kunywa. Tafrija ilidumu kwa masaa mawili mbele kabla haijakoma na watu kundoka zao.


Punde gizani …

“Haikuwa rahisi, mzee. Kazi ilisukwa kwa usiri sana. Tusingewezeza kutambua hata punje,” sauti ilisema. Kulikuwa giza chumbani.

"Unajua uzembe wako umenigharimu kiasi gani?" Sauti ilifoka. "Wapambanaji wangu lukuki wameuawa. Makazi yao yameharibiwa. Unataka nianzie A na nipo Che? Unajua itanihitaji rasilimali ngapi kujenga ngome hiyo tena?"
"Nisamehe mkuu."
"Samahani yako itarepea majeraha yangu?"


Kulikuwa kimya kwa muda. Ni kana kwamba hakukuwa na mtu hapo. Ndani ya giza hili ungejiuliza wanaonanaje.


"Najua wanadhani nimekufa," ilisema sauti. "Hii ndiyo nafasi yetu kubwa kupanga mashambulizi mazito; mashambulizi ya kushtukiza! Na tutakapoanza, haitakoma kamwe."
"Ndio mkuu. Kipi naweza kufanya kusadia?"
"Nataka uanze kufanya kwa kufanya kazi moja kwanza. Nataka hao watu wote waliohusika na mauaji na uvamizi, nipate kuwafahamu. Nahitaji picha na maelezo juu yao. Wapi wanaishi, kikosi gani wanafanya kazi. Nataka taarifa hizo kesho!"
"Sawa mkuu."
"Nitawachinja kama kuku. Na video zao zitasambaa dunia nzima!"


Baada ya tisho hilo, simu ikakata na kukaendelea kuwa kimya.

***
***

Talib alizima sigara yake kubwa kwenye uso wa kisosi kisha akaufunika mdomo wake kwa kiganja. Macho yake yalizama fikirani. Hakuonekana mwenye furaha. Alitikisa miguu yake juu ya meza akigonganisha visigino.


Alikuwa mwenyewe kwenye chumba kikubwa cha makutano. Viti vilikuwa vitupu. Ndani kulikuwa kuna kajoto chepesi cha kiyoyozi kuzimwa karibuni.
Runinga kubwa ukutani ilikuwa inaonyesha taarifa ya habari. Mtangazaji alikuwa amevaa suti nyeusi kama ngozi yake. Miwani yake ya macho ndiyo kidogo ilimfanya aonekane vema. Sauti yake kavu ilisikika vizuri ingawa msikilizaji hakuwepo.


Kwa muda mchache mtangazaji aliongea. Kadiri alivyokuwa anatema habari, taratibu akaanza kukamata mishipa ya fahamu ya Talib. Hatimaye mwanaume huyo alitupia macho kideoni apate ona na kuskiza vema. Aidha angeweza kupata jambo.


Baada ya muda mfupi tu aliona habari mbaya, mtangazaji akiwa ni yuleyule kiooni. Sauti kavu ya mtangazaji huyo ilimuumiza masikio ikifikisha ripoti juu ya namna kundi la waandamanaji nchini Sierra Leone lilivyogeuka kuwa kundi la waasi. Kundi tishio.


Nani anayelifadhili kundi hili? Ndiyo hoja iliyokuwepo mezani. Swali hilo lilikuwa limeandikwa kwa rangi nyeupe juu ya ubao mwekundu chini ya runinga. Kwa namna chanya lilimfanya Talib alizingatie.


"Kumekuwa kuna ushawishi na nguvu kubwa nyuma ya kundi hili la waandamaanaji. Wana silaha nzito na hata mfumo wao wa mawasiliano si haba. Wanapanga mikakati ya kuwaua viongozi na familia zao katika namna ya ustadi. Hapa lazima kutakuwa na namna,"alisema mchambuzi wa mambo ya siasa za Afrika magharibi, bwana Rigorbet Ayatoye.


Kana kwamba anatazama tamthilia sisimuzi, Talib alitega sikio.


"Pasipo shaka tukio hili sio la mwisho. Yataendelea zaidi na zaidi. Kwa serikali ya kidikteta kushindwa kuhimili kitu hiki, kinaashiria tatizo si dogo. Kinaashiria mizizi mikubwa ambayo imeijenga kikundi hiki, na hili linaweza likaleta athari kubwa kwa siasa za Afrika ya magharibi. Wengine wanaweza kuliiga." Alinguruma mchambuzi.
"Sawa sawa," akadakia mtangazaji. "Na unaongeleaje juhudi za Al Saed, wa Liberia, kwenye kutokomeza uhasi. Kwa muda huu anaonekana kama mshindi. Ameibuka na kukamata anga la habari kwa sasa."
"Alichofanya Al Saed ni jambo la kishujaa. Al Saed ni mhasi mstaafu, ametumia namna nzuri sana ya kupambana nao kwa kupanga mipango madhubuti. Ila mpaka sasa haijulikani kama kiongozi wa kundi la waasi ameuawa ama lah! Ndio, inasemekana amekufa ila hamna ushahidi wowote, na mimi nitakuwa mtu wa mwisho kuamini kama alikuwamo na kufia ndani ya kile kijiji."
"Unadhani ni kwanini vita ya uasi inakuwa ngumu sana kukoma, haswa katika maeneo haya?"
"Tatizo kubwa ni madaraka, ndugu mtangazaji. Kila mtu ana haja na madaraka. Uchu. Kila mmoja anataka kiti cha dhahabu. Na shida kubwa inakuja kwamba mataifa haya ni mahasimu. Hakuna anayemsaidia mwengine, na wengine wanashutumiwa kuhusika na kuwafadhili waasi wa nchi jirani."
"Unadhani nini sasa kifanyike, mchambuzi, ili kurudisha shwari?" Aliuliza mtangazaji. Mchambuzi akasafisha koo lake kwanza kabla hajajibu;
"Nadhani ni wakati sasa wa mataifa makubwa na mashirika ya kimataifa kurushia macho yao kwenye haya mambo kabla hayajawa mabaya zaidi. Hali ya Sierra Leone itasisimua uhasi Liberia, na hata Guinea vilevile. Tunaweza tukajikuta tunarudi kwenye jinamizi la mauaji makubwa kama miaka ya nyuma. Hakuna anayejua, ila yanaweza kutabirika."


Baada ya maneno hayo kipengele cha mchambuzi kilikoma vikaendelea vingine ambavyo havikumgusa Talib. Mwanaume huyo alizama fikirani akipembua mambo kadhaa. Baada ya dakika kama mbili tatu hivi alinyanyua mkonge wa simu na kuita.

"Njoo mara moja," aliagiza. Punde akaja mwanaume mmoja, mwanajeshi, aliyekuwapo kwenye kikao cha kuwatokomeza waandamanaji. Alikuwa ni miongoni mwa wale waliokuwa wanaunga mkono mikakati ya Freeman, marehemu: Oparesheni mwanzo, kati na mwisho. Kwa jina alifahamika kama Rauli, ama mbweha kwa jina la utani.


"Freeman ameshaenda. Hali naona inakuwa mbaya zaidi," alinena Talib kwa utulivu. Hakuwa na hasira bali umakini, kama alikuwa nayo basi alifanikiwa kuifichama.
"Tunahitaji mrithi wake, tena haraka, ambaye atafanikisha kazi hii pasipo na makosa kabisa. Na nimetazama upana wa jaruba hili, nikaona wewe unastahili kufanya hii kazi."
"Mimi?" Rauli alijinyooshea kidole.
"Ndio, wewe. Vipi, huwezi?"
"Hapana, naweza mkuu!"
"Nakupa siku moja tu, utanianishia mipango yako yote ya kumaliza hao wapumbavu. Kaa na wenzako muone mnafanyaje alafu mtanishirikisha."
"Sawa."
Ila kabla Rauli hajaondoka, anasema:
"Mkuu, kuna jambo."
Talib anampatia macho ya kuguswa.
"Ni kuhusu kifo cha Freeman."


Uso wa Talib unaungana mkono na macho yake. Alionekana ana hamu ya kujua zaidi kuhusu hiyo mada.
"Kifo cha Freeman kilitupatia maswali mengi sana. Na kwa namna moja, tulijikuta tunaamini kwamba kina mkono wa mmoja wetu."
"Unamaanisha nini?"
"Namaanisha kwamba kuna mmoja wetu alimuua ama kupanga mauaji ya Freeman."
"Nani huyo na mmemjuaje?"
"Ni Richard. Tukiwa kwenye kikao alipinga kabisa mipango ya Freeman na aliapa kabisa mpango huo hautafanikiwa kwa vyovyote vile. Siku hiyo hiyo muda mchache mbele, Freeman anauawa. Inakuaje Richard alikuwa anajiamini kiasi kile? - Na alichobashiri kitimie?"


Talib alivuta pumzi ndefu. Alilaza mgongo wake kwenye kiti akitafakari kwa dakika mbili kabla hajasema:
"Unajua kweli inawezekana kukawa kuna mtu ndani ya mfumo wetu akawa anashirikiana na hawa wapuuzi!"
"Ndio, mkuu. Inawezekana." Alisema Rauli kabla hata ya kufikiria.
"Hao waandamanaji walijuaje kama Freeman alikuwa anaelekea kuwatokomeza? Itakuwa kuna mtu amewapasha habari!"
"Ndio, mkuu. Na si mwingine bali Richard. Ni yeye tu!"
Talib alivaa uso wa chui. Aling'ata meno yake kwanguvu. Akiwa ameyabana meno vivyo hivyo kana kwamba anataka kuyang'oa, alibamiza meza kwa ngumi yake nzito akisema ;
"Nataka kichwa cha huyo hanisi hapa!"


Hiyo ilikuwa amri. Rauli alisimama akatoa salamu na kuondoka kwenda kuitimiza.

***
***

"Naona leo umetingwa," sauti ya Bi Fatma iliita nyuma ya mgongo wa Kone. Mwanaume aligeuka na kumtazama mkewe kwa macho ya karibu.
"Kiasi tu mpenzi. Si nimekaa hapa muda si mrefu tu."
"Muda si mrefu? Aah aah ... mi nakuhitaji kitandani bwanaa," alisema Bi Fatma kwa sauti ya puani. Alimsogelea Kone akampapasa mabega kwa viganja vyake vilaini.
"Twende baaasi."
"Embu kaa hapa." Kone alimvuta mkono mkewe na kumketisha kando.


Bi Fatma alikuwa amevaa gauni jepesi pekee. Kone alikuwa amevalia bukta rangi ya bluu iliyokoza kifua chake kikiwa wazi. Mbele yao kulikuwa na tarakilishi mpakato Kone akihangaika nayo kwa muda wote ule.


"Unajua kuna mambo hayajakaa vizuri huko nyumbani,"alisema Kone kwa uso tashtiti. "Hali ya kisiasa si shwari kabisa. Inasemekana kuna vuguvugu la mapinduzi ya jeshi. Ndani ya chama tawala mpaka sasa hakuna maridhiano juu ya nani atakayekaimu nafasi hiyo, ni hovyo. Watu wamegawika kimakabila; wa Fula na wa Malinke. Kila mmoja anataka kushika hatamu. Kuna uwezekano mkubwa viita ikajiri."


Bi Fatma alimshika mumewe shavu akimtazama kana kwamba mtoto mdogo.


"Mpenzi, unaweza ukasahau kuhusu Guinea hata mara moja?" Aliuliza kwa sauti karimu. "Lini utapata amani ya moyo wako? Jaribu kupumzika, na kufanya mengineyo. Siasa za Afrika ni mapacha wa mama mmoja."
"Mama," Kone akaita. "Kumbuka Guinea ni kwetu, ni nyumbani. Wazazi, ndugu jamaa na marafiki zetu wote wapo huko. Nitaipuuziaje? Watoto wetu wataishi katika ardhi ngeni mpaka lini? Daima?"
"Hapana mume wangu. Ila hauna chochote cha kufanya kubadili hali hiyo, sasa ya nini kukonda na mawazo?"
Kone alitikisa kichwa.
"Cha kufanywa hakikosekani mpenzi, ila tu namna ya kukifanya. Na namna itapatikana tu. Siwezi nikakaa nikishuhudia mambo yaenda kombo chomboni. Hata nafsi yangu itanisuta."


Bi Fatma alibadilisha sura. Hakupendezwa na mwenendo wa mumewe. Alijinasua karibu akaenda zake.


"Mpenzi!" Kone aliita. Alinyanyuka akamfuata mke wake. Alimdaka kiuno akamgeuza.
"Nini mpenzi wangu?"
"Unaniudhi sana!" Alijibaraguza Bi Fatma. Aliufuma uso wake kwa maudhi. Alideka.
"Tuachane na hayo basi mke wangu," alisema Kone. Alimbeba mkewe akampeleka kitandani alipombwagia.
"Niahidi kwanza, hautafikiria tena hayo mambo ya siasa," alisema Bi Fatma. Alimtazama Kone machoni kana kwamba kachero anambana jasusi wa kigeni.
"Nakuahidi mpenzi, sitafikiria tena," alisema Kone. Ila sauti yake ilimsaliti.
"Najua unanidanganya, Kone. Naju ..."
"Sshhh ... yameshapita hayo mpenzi," alinong'oneza Kone akiweka kidole chake kwenye lips za mkewe. Alimbusu shingoni na kumkumbatia vizuri ...


Masaa yalipoenda, jua liliamka kukawa na mwanga, ila dhoofu. Siku ilikuwa na kaubaridi cha upepo na anga lake liliahidi kuleta mvua muda si mrefu ujao.


Fatma alikuwa amejikunja akijifunika shuka gubigubi. Kitandani alikuwa peke yake. Joto alilolipata toka shukani lilimpa hamasa zaidi ya kutaka kuendelea kuchapa usingizi. Ila alipokuja kugundua yu peke yake, baada ya kunyoosha mkono, alikurupuka akaangaza.


Alitoka kitandani akatazama kila eneo isipokuwa tu vyumba vya watoto, hakumuona Kone. Alijaribu kupiga simu lakini nayo haikupatikana. Alifura.
"Kone, unataka nini zaidi ya maisha yako?"


Mara aliona kikaratasi kidogo mezani. Alikisogelea akakikwapua. Kilikuwa kimeandikwa ujumbe kwa maneno madogo ya mwandiko wa kiume:
"Nimetoka kwenda kumtoa Rose. Niwie radhi sijakuaga."


Fatma alichana hicho kikaratasi katika vipande milioni. Alirudi kitandani akaketi na kudaka kichwa chake kana kwamba kilikuwa kimemzidi uzito. Alitibua nywele akiukunja uso.


Alighafirika. Alishiriki kwenye kidonda cha wivu na sasa alikuwa anaumia.


**
**


Ndio, kwa mujibu wa ratiba alikuwa yu sahihi. Saa yake ya mkononi ilimwambia ni saa tano asubuhi na sasa ilikuwa imebakia nusu saa tu ya yeye kuwa njiani kabla hajafika eneo analotakiwa kuwepo kwa ajili ya misheni.


Akiwa ndani ya gari, alikuwa anatafakari. Ingawa mipango yake yote ilienda sawa, bado alikuwa na shauku la hofu. Hakutaka kufeli hata kidogo. Kwa namna yoyote ile aliadhimia kufanikisha aliyoyapanga, tena kwa muda.


Ni siku moja tu nyuma, alimpata askari magereza, anayehusika na gereza linalomhifadhi Rose, na kumpatia pesa nyingi kwa ajili ya kumsaidia kwenye haja yake ya kumtorosha mwanamke huyo. Kwa donge hilo nono la pesa, askari alishindwa na tamaa, akaweka bayana taarifa nyeti.


Hivyo basi Kone alikuwa anajua fika, wafungwa kadhaa watakuwa njiani wakipelekwa kufanya kazi za jamii mahala fulani. Na ndani ya gari hilo, atakuwapo Rose. Askari alimhakikishia hilo. Lazima atakuwepo, na kwa data zaidi atakuwepo kiti cha mwisho upande wa dirisha la mkono wa kulia.


Kone akiwa ndani ya muda, alifika ndani ya msitu mwepesi barabara ikatizapo. Alifungua buti ya gari akatoa mtungi wa gesi alioulaza chini kana kwamba umetupwa. Alijiingiza kwenye gari lake na kujitokomeza mitini usijue kama yupo maeneo hayo.


Iliwahi kusemwa; hakuna haraka Afrika: no hurry in Africa, msemo huu ulikuwa na kweli ndani yake. Kone alionekana kuusahau ama kutoujua kabisa. Alizingatia muda pasipo kujua kama anaowangoja watakuwa watiifu wa muda kama aenendavyo. Alingojea kwa masaa, kiasi kwamba akahisi ameachwa kwenye mataa. Ila moyo wake ulimpatia subira akaendelea kungoja.


Ikiwa ni majira ya saa nane mchana, gari kubwa aina ya Fiat, kuukuu rangi ya bluu inayofanana na nyeusi, linachipuka na kushika barabara. Ubavuni lilikuwa kimeandikwa MAGEREZA kwa rangi nyeupe isiyo na nakshi. Madirisha yake yalikuwa ya wavu wa chuma. Vioo vyake vya mbele ya dereva vilikuwa vichafu huku kifuta maji na uchafu, ama waipa, kikiwa kimoja tu.


Ndani ya gari hilo kulikuwa kuna wafungwa wanawake. Walionekana hovyo haswa. Walikuwa wamevalia nguo nyeusi zenye mistari meupe ambayo ilikuwa imefifia kwa uhaba wa matunzo.


Askari walikuwa watatu ndani ya gari hilo mbali na dereva, wawili walikuwa na bunduki. Ajabu askari mwanamke alikuwa mmoja tu, tena mikono tupu. Alikuwa ameketi karibu na dereva akitazama mbele kana kwamba anasafiri kwenda kumsalimu mjomba kijijini.


Gari lilisonga. Lilipokatiza mtungi wa gesi, askari mmoja alipaza sauti kuamuru lisimame. Askari huyu alikuwa amevalia sare chakavu, suruali yake ilikuwa ina kiraka pajani. Viatu vyake vilijaa kama mtumbwi. Alishuka akaufuata mtungi ule wa gesi na kuupakiza ndani.


"Mali hii!" Alisema askari huyo akitabasamu. Wenzake hawakuhangaika naye, wakaendelea na kazi na safari yao.


Walitembea kwa muda mfupi, mara gari likapoteza mwelekeo. Lilivamia miti ya kando na kukomea hapo. Uso wote wa gari wa mbele uliharibika vibaya, dereva akiwa mahututi. Paji lake la uso lilichanika na kuchuruza damu pomoni.


Hakuna mtu yeyote aliyekuwa anajielewa ndani ya gari. Ni punde, Kone anaingia ndani ya chombo hicho na kuangaza. Alikuwa amevalia kinyago cheusi usoni. Mkono wake wa kuume ulikuwa umebebelea bunduki ndogo.


Alimuona Rose kule kule alipopewa maelekezo, haraka akamfuata na kumbeba. Alimhamishia kwenye gari lake kisha akatimka toka eneo hilo upesi. Kasi yake ilikuwa inatisha.



***
 
Tusichokonoane umesikia wewe fala! Kama wewe ni mgeni na mimi funga bakuli na sio unaanza kuleta usenge wako hapa. nilishasema hapa toka awali sitakuja kuuza simulizi yangu hata moja! Na nilishasema nitaiandika na kuituma hapa yote.


Infact, simulizi zipo nyingi humu si lazima ukaisoma ya mzushi, sawa bob?

Sent from my SM-J110F using JamiiForums mobile app
Pole chalii yang msamehe bure
 
Back
Top Bottom