NJIA NYEMBAMBA --- 17
Mtunzi: SteveMollel
Taswira ya jiji la Freetown ilikuwa imefifia, halikuwa linatamanika tena. Magari yalikuwa machache na hata watu pia. Ungeweza kusema ni jangwa, ama mji wenye watu wachache kabisa juu ya uso wa dunia. Hii yote ilitokana na upungufu maradufu wa usalama nje ya milango. Bado maandamano, tena yanayoambatana na vurugu kali, yalikuwa yanaendelea kuzizima ndani ya jijii. Hakukuwa salama.
Watu kadhaa waliripotiwa kuuawa wengine wakijeruhiwa vibaya. Makundi ya watu walioongozwa na hamu kali ya kuuondoa utawala wa Talib walirandaranda huku na kule kuutafuta ushawishi. Kila mwananchi alitakiwa kuwaunga mkono la sivyo angelionjeshwa joto. Haikuwa ombi sasa kumpinga Talib, bali ni amri! Kwa yule aliyekaidi angeachwa anatiririka mito ya damu.
Ikiwa ni majira ya mchana sasa wa saa nane, ndani ya nyumba kubwa mno nyeupe inayovutia machoni, chumbani, anaonekana naibu kiongozi wa ulinzi wa taifa: Meja jenerali Edward Simon akiwa amevalia nguo za kutafutia joto. Ingawa kiyoyozi kilikuwa kinapuliza kwa wingi, bado alionekana kutotosheka.
Chumba kilikuwa kikubwa kama uwanja wa mchezo wa tenesi. Kitanda kilitapakaa kikiwa kimefunikwa na sufi laini nzito. Madirisha, mawili, yalikuwa mapana mno kiasi cha kutengenezea milango. Viti na meza, pamoja na maua feki yaliyokuwa chumbani humo, kwa macho tu, yalieleza bei yake ya kikubwa. Palikuwa pazuri mno usitamani kutoka ukiingia.
Ni siku ya tatu sasa meja jenerali huyu hajaenda ofisini kwa sababu ya usalama. Amekuwa akibakia ndani kwake tena akiwa amezungukwa na wanajeshi kadhaa waliobebelea silaha za kisasa. Mke na watoto wake wawili pia walibakia nyumbani, shule na shughuli zao zikisitishwa kwa muda usiojulikana.
Mitaani hakukuwa shwari. Wanajeshi si wengi kama wananchi. Hata kwa wingi wao silaha bado hakufui dafu. Wananchi hawana sare hivyo basi haujui yupi aliye mawindoni na yupi aliye mafichoni, yupi anataka tabasamu lako ama damu yako!
Mwanamke mnene aliyevalia taulo pekee kifuani anaingia chumbani akitokea kwenye bafu. Mwili wake umejazwa na matone matone ya maji. Kichwani amejifunika na taulo dogo jeupe kama pamba. Mwili wake rangi ya maji ya kunde wenye umbo zuri la chupa. Ila uso wake ulikuwa wa mwanamke mchanga. Alionekana mdogo asiye hata na miaka ishirini na tatu.
“Mpenzi,” mwanamke huyo aliita akijifuta kichwa na taulo. Meja akamtazama mwanamke huyo pasipo kusema jambo.
“Nahitaji kutoka mara moja leo.” Alisema mwanamke.
“Kwenda wapi?” Akawahi kuuliza Meja.
“Kwa rafiki yangu – Diana.”
“Una matatizo gani Sarah? Utaacha utoto lini wewe? Hivi niwe nakuimbia kila siku kwamba huko nje si salama?”
“Sasa mpenzi, tutakaa humu ndani mpaka lini? Si nitaongozana na walinzi? Shughuli zangu nyingi zinakwama.”
“Shughuli zipi hizo?”
Mwanamke akaguna, “basi yaishe.”
“Au unataka kwenda kwa hivyo vijana – vijana vyako huko?”
“Sasa hayo yanaingiaje hapa?”
“Nakwambia hivi, nikija kugundua unaendelea na huo ujinga wako. Nitakuua!”
Mwanamke akaguna kwa kubinua mdomowe.
Si bure kwa Meja kuhofia. Umri wake ni kama mara tatu ya binti huyu mchanga mrembo, ni wazi mwanamke huyu anaweza akawa anatafuta injini zingine huko nje zenye moto zaidi, pengine.
Mwaname alifuata kabati lake la nguo akalifungua. Lilikuwa limesheheni nguo. Akiwa anatazama ni nguo ipi inayoweza kusitiri mwili wake, mara sauti kali ya mlio wa risasi inasikika. Anashtuka! Anageuka upesi kumtazama mumewe akitumbua macho.
Meja alikuwa tayari ameshasogea dirishani kuchungulia.
“Kuna nini?” Sauti ya hofu ya mwanamke iliuliza.
Meja hakujibu, aliendelea kukazana kutazama. Ila baada ya sekunde chache aligeuka akamtazama mkewe kwa sura yenye mushkeli wa mashaka.
“Watoto wapo wapi?” Aliuliza.
“Kuna nini?” Mwanamke akajibu kwa swali. Alikuwa ameshapata woga, mikono yake ikitetemeka.
Milio ya risasi iliita tena, mara hii mara tatu kwa fujo kuu! Mwanamke alichanganyikiwa akakimbilia kufungua mlango.
“Watoto wanguu!” alipiga yowe. Alitoka chumbani haraka akakimbilia sebuleni alipoangaza na kisha haraka akaenda vyumbani, akatoka na watoto wawili wa kike. Walishika korido, wakakutana na Meja, mkononi alikuwa amebebelea bunduki ndogo.
“Nendeni chumbani mjifungie!” Aliagiza Meja, mwanamke akiongozana na watotowe wakazama chumbani na kuupiga mlango kufuli.
Meja alisogelea sebuleni. Kulikuwa kuna kelele za watu huko nje. Aliangaza macho yake upesi akaona simu ya mezani, aliikimbilia apate kupiga. Aliinyakua simu hiyo haraka akaiweka sikioni na kubofya namba kadhaa. Simu ikaita.
Makelele ya watu, yakiwa ni ya kufoka, yalizidi kuongezeka. Yalisikika yakikaribia mlango, na bado simu haikuwa imepokelewa.
Macho ya Meja yalitazama mlangoni kwa mashaka. Mkono wake uliobebelea bunduki ulielekea pia huko. Alilaani kwanini simu haipokelewi, alichanganyikiwa. Punde mlango unagongwa na mara unavunjwa!
Haikudumu muda mrefu, mwanamke aliyekuwepo chumbani, anasikia sauti ya risasi inayojibiwa na risasi nne huko sebuleni. Walikuwa ndani ya kabati yeye pamoja na wanawe wakiwa wamejikunyata kama wanaosikia baridi kali.
Sauti za kufoka na kuropoka zinaendelea. Kwa mujibu wa sauti hizo waweza sema kulikuwa kuna idadi toshelezi ya watu. Sauti hizo zinaruruma, zinasogea karibu chumbani, baada ya muda mlango unavunjwa. Hapo kabla ilisikika milango miwili ikitendwa vivyo hivyo.
“Wako wapi?” Sauti moja inauliza. Kwa kupitia ka-mwanya ka mlango wa kabati, wanaonekana wanaume kama nane hivi, watatu wakiwa wamebebelea bunduki kubwa ndefu na wengineo wakiwa wamebebelea mapanga.
“Tafuteni! Tafuteni kila sehemu!” Inatoka amri kwa mmoja wao. Wanaume hao wanagawanyika kutazama huku na huko. Punde kabati linafunguliwa, mwanamke na watoto wake wanatolewa kwa nguvu. Wanarushiwa sakafuni kama mizigo.
Taulo liliacha mwili wa mwanamke, akabakiwa mtupu: mbele ya watoto na wageni wake wa lazima.
“Naam! Wewe si miongoni mwa wale wanaokula jasho letu, sasa leo utaliwa wewe!” alisema mwanaume mtoa amri. Macho yake yalikuwa yameshatepeta uchu.
Pasipo kujali kama kuna watoto, alivua suruali. Mwanamke alilia, pamoja na watoto pia wakiomba mama yao aachwe, hawakusikilizwa. Mbele ya macho ya watoto, mama akabakwa kwa zamu mpaka alipopoteza fahamu.
Wanaume walimaliza haja zao, wakammaliza mwanamke huyo na watoto wake kwa kuwakatakata mapanga. Palitapakaa damu kana kwamba machinjioni. Viungo vilitenganishwa mwili ukipasuliwa kama kuni.
Watu hawa hawakuwa hata na lepe la huruma. Waliwakata binadamu wenzao kana kwamba wanamkata mnyama. Walipomaliza wakatokomea.
***
NDANI YA KUNDI LA WHATSAPP …
“Tukutane wote kwenye mazishi ya Bernard pasipo kukosa.”
“Tutafika kumpumzisha mpambanaji mwenzetu.”
“Nani anayefuata kwa sasa baada ya yule mbwa tuliyempeleka jehanamu?”
“Tutalitazamia hilo siku za usoni.”
“Unajua haya mambo yanahitaji utulivu na mipango.”
“Ni kweli.”
“Kweli, tusije tukaingia mkenge.”
“Unachokisema ni sahihi.”
“Ila tutampata mwingine mwenye mwanamke mtamu kama yule malaya?”
Viwanasesere vya kufurahi vinatumwa kwa wingi kundini.
“Aisee yule mwanamke ni mzuri bwana. Hata tukimkuta mwingine ni bibi, tuwafanye tu! tena sasa hivi wakiwa wanaona tunavyowashughulikia wake zao kama wao walivyotushughulikia kwa muda wote huo.”
“Wazo zuri!”
“Tunaweza tukanogewa tukakamatwa.”
“Ni muda wa hawa watu kuumia. Hawastahili kufa hivihivi.”
“Hey, tukutane kwenye mazishi ya Bernard. Tutaongea na kupanga mengi huko.”
“Mustafa anasisitizia tusikose kufika.”
Jumbe zinaendelea kutiririka na kutiririka, mamia.
***
Mwanga wa simu ulifukuza kagiza kalichoanza kujirundika chumbani. Ilikuwa ni majira ya jioni sasa lakini chumba hakikuwa kimewashwa taa. Mwanga huu wa simu ndani ya kiza unadumu kwa sekunde kadhaa kabla ya mlio wa soketi kuita, na mara chumba kinakuwa cheupe.
Anaonekana Kone akiwa amevalia bukta fupi nyeusi ya drafti drafti. Mkononi mwake alikuwa amebebelea simu, ile iliyokuwa inatoa mwanga. Anaitazama tena simu hiyo kabla hajayarusha macho yake kwa bi Fatma aliyekuwa amejilaza kitandani.
Mwanamke huyo alikuwa amejifunika kwa nguo nyepesi iliyosadifu mwili wake vema. Alionekana amechoka, mdomo wake ulikuwa wazi akikoroma kwa mbali.
Kone aliweka namba fulani kwenye simu yake alafu akapiga, namba haipatikani. Alijaribu tena, bado majibu yalikuwa hayo hayo. Alisonya akamuamsha mkewe kwa sauti chovu.
“Bado hapatikani,” alisema. “Inabidi niende kwake sasa.” akaongezea.
“Kuwa makini sana, Kone,” alisema Fatma mwenye mang’amung’amu ya usingizi. “Inawezekana kuna kitu kikawa kimemtokea kikakuweka nawe hatarini.”
“Najua hilo, usijali. Lazima Rose atakuwa yupo shidani, hii si kawaida. Alikuwepo wakati nikimuhitaji, na sasa ni wakati wa mimi kuonyesha kujali kwangu.”
“Lakini … huoni kama unaweza kuharibu kote kote, Kone. Tutakimbilia wapi?”
Kone aliweka mkono wake begani mwa Fatma. Akamtazama katika namna ya kumuondoa hofu.
“Niachie mimi, najua cha kufanya.”
Alinyanyuka akatumia dakika kumi tu kujiandaa. Alivalia suruali nyeusi ya kadeti pamoja na tisheti nyeupe iliyofunikwa na koti kubwa refu rangi ya kaki lenye vifungo vinene. Aliaga akaondoka.
Akiwa yu njiani, ndani ya gari lake, kuelekea kwa mwanamke Rose, mawazo yanakula kichwa chake. Mwanzoni alikuwa anafikiria usalama wa Rose kwenye mikono ya mshenzi Talib, ila baadae, katika kasi ya ajabu, mawazo juu ya mkewe yalimparamia.
Usiku wa kuamkia siku hiyo haukuwa mwepesi kwake hata kidogo. Ulikuwa ni usiku wa mzozano na malumbano baina yake na mkewe. Ulikuwa ni usiku wa kukata mzizi wa fitna, kudadavuliana kwanini na sababu za mambo mbalimbali, haswa mahusiano ya Fatma na marehemu Raisi wa Guinea.
Ukweli una gharama kubwa, waliwahi sema wahenga. Japokuwa Kone aliuhitaji ukweli, ulimuumiza. Alipata kujua mambo kadhaa ambayo yaliutoboa moyo wake na kuufanya chujio. Akili yake ilitibukwa na nyongo ikapasuka.
Ni baada tu ya miaka miwili ya yeye kuwa kazini kama mhusika muhimu kwenye usalama wa taifa, alijikuta anateuliwa kuwa mtu muhimu kwa usalama wa Raisi. Maisha yalienda kasi sana. Aliaminiwa sana na Raisi akapewa kazi ambazo hakustahili, bali wale walio juuye.
Kwa muda wote huo alikuwa akiamini kazi, vyeo na mshahara wake mnono ni majibu ya kazi yake aliyoifanya kwa utashi mkubwa. Kumbe lah! Jasho na damu aliyoimwaga kwenye uwanja wa vita, huku na kule, havikuwa vishawishi hata kidogo, bali mkewe, bi Fatma.
Mkono wa Raisi uliokuwa unampapasa mkewe pindi anaposafiri, ndio huo huo uliokuwa unatia saini kwenye izimisho za mishahara na cheo chake. Hili lilikuwa chungu.
Ilikuwa ngumu kwake kuamini. Hapana. Hapana. Hapana. Alisema na moyowe. Ila Bi Fatma hakutaka kumficha, alimweka wazi. Hakuna yeyote aliyekuwa anajua mchezo huo isipokuwa mke wa Raisi aliyewahi kuwafumania siku moja wakiwa Ikulu. Na hiyo ndiyo sababu mke huyo, wa Raisi, akajiondokea.
Moyo wa Kone ukawa mgumu mno kama jiwe, aliuhisi kifuani ukiguruguta kama wataka kuchomoka. Alijizuia sana kutoa machozi siku hiyo. Alijikaza kisabuni mwanamke andelee kumwaga mboga.
"Sio kwamba nilifanya hayo kwasababu ya kazi yako tu, bali pia na usalama. Kuna kipindi alinitishia endapo nisipofanya anayoyataka, basi atateketeza familia yangu. Nilishindwa kumkwepa kila ulipokuwa unaondoka kwani alikuwa anajua ratiba zako. Ndio maana nilikuwa nakusisitizia sana ubaki nyumbani japokuwa sikuweza kukwambia haswa kwanini."
Maneno hayo yalitafuna mtima wa Kone. Aliambiwa usiku wa kuamkia siku hiyo lakini ni kana kwamba aliambiwa dakika moja tu nyuma. Aliyasikia yakiimba vizuri masikioni mwake. Yalimuumiza.
Alijitahidi kujikomboa toka kwenye mawazo hayo, ikawa ngumu. Ni mpaka pale kafoleni kepesi kalichokuwa kamemzinga kalipoanza kutembea, basi ndipo akili yake ikahamia barabarani. Alitembea mpaka karibu na jengo la Rose, ilikuwa majira ya saa tatu usiku, akarusha macho yake getini. Aliwaona wanaume watatu ndani ya jezi za jeshi wakiwa wamebebelea bunduki.
Alisogeza gari lake mbali alafu akalizima na kutoka ndani akiwa amebebelea bunduki ndogo.
Tusijue kwa namna gani, Kone anaingia ndani ya jengo pasipo walinzi kushtuka hata kope. Anazama mpaka ndani, mfanyakazi, aliyekuwa jikoni, anashtuka akiitwa kwa kunong'oneza.
"Ssshhhhh! ... ni mimi, Kone. Unanikumbuka?"
Mfanyakazi anatikisa kichwa chake kwa uoga. Haraka mwili wake ulianza kutetemeka.
"Mimi rafiki yake Rose. Hukumbuki nilishawahi kuja hapa?"
Hofu iliziba kumbukumbu ya dada wa kazi. Alifanya jitihada za ziada kumkumbuka Kone. Bahati nzuri haikuchukua muda mrefu.
"Ndio, nimekukumbuka!"
"Rose yupo wapi?" Kone aliwahi kuuliza.
Dada wa kazi alibanwa kigugumizi. Ilimbidi ashushe pumzi kwanza kabla hajateta:
"Dada amechukuliwa na wanajeshi, walisema wanampeleka jela!"
Alieleza tukio zima lilivyokuwa, Kone akaishiwa nguvu kwa upungufu wa matumaini. Ni jela gani atakayokuwa amepelekwa Rose? Hakuweza hata kubashiri. Kichwa chake kiliingia kazini upesi, punde akapata jibu, ila jibu hili lilikuwa na ukakasi: njia yake ya mafanikio ilikuwa nyembamba.
Yuko radhi kuipita?
Hakukuwa na namna sasa, ilimlazimu Kone awarudie wale walinzi getini. Kwa namna moja ama nyingine watakuwa na majibu ya maswali yake kadhaa. Alijaribu sana kulikwepa hili, ila halikuwezekana. Hiki kikombe kilikuwa chake.
***
Post sent using JamiiForums mobile app