Njia nyembamba -- 12
Mtunzi: StevwMollel
“Haraka batilisha mpango wako kabla sijakutoa roho!” Sauti nzito ilinguruma ndani ya kinyago.
Macho ya Samweli yalitoka kana kwamba vipande vya matango. Moyo wake ulilipuka na pumzi ilianza kukimbia. Ni kwa namna gani mwanaume huyo alizama ndani pasipo yeye kujua? Hakupata majibu. Ama ni jini! Anataka nini kwangu?
Hofu ilikamata uso wa Samweli na mwili wake ukaanza kujibu mapigo kwa kutetemeka mithili ya kifaranga aliyenyewa na mvua.
“Wewe nani?”
“Huna haja ya kujua. Nimesema batilisha mpango wako haraka!” mvamizi aliongea akinyooshea mdomo wa bunduki kwenye simu ya mezani.
Haraka Samweli akanyanyua simu na kuiweka sikioni.
“Ukifanya jambo lolote la kipumbavu nitatoboa kichwa chako!” Alitisha mvamizi. Bwana Samweli aliita namba ya mkuu wa jeshi, ilipopokelewa akatoa amri ya kusitisha oparesheni ya uvamizi wa kijiji makazi cha AMAA haraka iwezekanavyo.
“Mkuu, unasitishaje mpango huu ghafla hivyo?” Aliuliza mkuu wa jeshi.
“Nimesema rudisha hivyo vikosi haraka!” Samweli akafoka kabla ya kurejesha simu mezani akiilaza kando ya kitako chake hivyo kupelekea simu hiyo kuendelea kuwa hewani.
“Tayari,” alisema Samweli akimtazama mvamizi kwa macho ya huruma. Mvamizi yule alikuwa mwerevu, alitambua janja ya Samweli. Pasipo kusema jambo, alinyooshea bunduki yake kwenye simu akampa Samweli ishara ya kuikobeka simu ile kwenye kitako chake.
Samweli alitii, akaweka simu kitakoni. Hapo ndiyo mvamizi akaongea:
“Unajifanya mjanja siyo?”
Kabla Samweli hajajibu, risasi ilitoka kwenye mdomo wa bunduki ya mvamizi ikazama ndani ya fuvu lake la kichwa. Tundu kubwa lililozuka kichwani hapo likaanza kuvuja damu pomoni, wakati huo mvamizi akitazama.
“Kapumzike jehanam!” alisema mvamizi.
Masaa manne baadae, gari nyeusi, Harrier, muundo mpya iliingia ndani ya nyumba ya bwana Samweli. Ndani yake ilikuwa imembebelea mwanamke mnene mweusi na mtoto mdogo wa kike mwenye umri wa miaka kumi kwa makadirio mepesi.
Mwanamke huyo alikuwa ni mke wa Samweli na mtoto huyo akiwa ndiye mtoto pekee wa mheshimiwa huyo.
Walistaajabu kukuta hamna mlinzi hata mmoja getini hali iliyowalazimu wafungue geti wenyewe. Waliingia ndani na hawakuwakuta walinzi vilevile. Mke alipata mashaka, akakamata mkono wa mwanaye.
Kitu cha kwanza walichokiona baada ya kuingia ndani ya sebule, kilikuwa ni kichwa cha bwana Samweli juu ya meza. Kichwa hiko kilikuwa kimetapakaa damu na kimepatapakaza damu mezani. Kiwiliwili chake kilikuwa kimelala kwenye kochi, nacho kikiwa kimechafuza damu.
Sebule ilikuwa inanuka damu!
Mke wa Samweli alipiga kelele kali wakati mwanaye akiachama mdomo kwa bumbuwazi. Alidondoka chini akizirai, mtoto pekee akibakia hajui cha kufanya bali tu kulia na kuchanganyikiwa.
***
Hilo la Samweli kuuawa na kisha kuchinjwa halikuwa siri. Baada ya takribani nusu saa habari iliwasili kwenye masikio ya kiiongozi mkuu bwana Al Saed.
Wakati huo alikuwa yu ikulu akiwa anangojea kwa hamu mrejesho wa oparesheni ya kutokomeza kijiji kinachowatunza wanamgambo wa AMAA. Ndani ya mkono wake wa kushoto alikuwa amebebelea sigara aliyokuwa anaivuta kwa zamu.
Bwana Al Saed si mvutaji wa sigara mara kwa mara isipokuwa tu pale anapokuwa ametingwa na mawazo. Tabia hii inajulikana kwa watu wake wote wa karibu. Pindi anapovuta sigara basi anakuwa katika hali tulivu na ahitaji usumbufu wowote.
Hii aliyokuwa anaivuta sasa ilikuwa ni sigara yake ya tatu tangu aanze kusubiria taarifa za oparesheni ya uvamizi wa kijiji. Alishapigiwa simu mara moja tu na bwana Samweli, na sasa ulikuwa umepita muda mrefu kabla ya kuhabarishwa nini kilichokuwa kinaendelea, ila aliamua kuvuta subira.
Simu yake ilipoita, aliwahi kuitazama, alidhani ni bwana Samweli. Alikuta ni kamishna wake wa jeshi, akapokea, akapewa taarifa ya kifo cha bwana Samweli.
Mwili wa Al Saed ulipigwa ganzi kwa muda. Sigara yake ilidondoka chini akiendelea kusikiliza. Simu ilipokata, akanyanyuka upesi na kwenda ndani ya ikulu moja kwa moja mpaka kwenye chumba chake cha mawasiliano. Alifungua tarakilishi yake mpakato akatazama barua pepe. Huko akakuta ujumbe.
Ujumbe huo ulitumwa mapema sana. Laiti kama angelitazama mapema basi asingelikuwa na haja ya kupewa taarifa ya mauaji ya Samweli na kamishna wake wa jeshi.
Picha kubwa ya kichwa cha Samweli kikiwa kimekatwa ilijaa kwenye uso wa tarakilishi. Picha hiyo ilikuwa inatisha lakini Al Saed aliitazama. Alipomaliza akasoma na ujumbe uliombatana na picha hiyo:
“Nilikwambia usithubutu kufanya jambo lolote la kijinga, ulidhani natania.” Ujumbe huo ulitoka kwa Mr. X.
“Hiyo ni rasharasha tu, Al Saed. Kadiri utakavyoendelea kufanya ujinga ndivyo utakavyoadhibiwa. Tii amri sasa!”
Al Saed alifunga tarakilishi yake kwa nguvu. Alirejea kule alipokuwa awali akawasha sigara nyingine na kuendelea kuvuta. Alivuta sigara hii kwa hisia sana. Kichwa chake kilikuwa mbali mno kwa mawazo. Aliwaza mambo mengi ambayo aliyakosea majibu. Ila mwishowe kuna mambo akakubaliana nayo na baraza lake la kichwa.
Kuna watu ndani ya serikali yake, wanaungana na kundi hili la AMAA kwani hao ndio watakuwa wamevujisha mpango huo wa siri. Alijitahidi kuchambua jambo hilo, labda linaweza likawa limeonekana huko nje, akili yake ikagoma kabisa. Aliamini kazi hiyo imesukwa na msaliti.
Hakutaka kupaparakia hiyo oparasheni, akampigia mkuu wa jeshi na kumtaka mpango huo usitishwe mpaka pale atakapotoa taarifa zaidi.
“Sawa, mkuu,” aliitikia mkuu wa jeshi. “Tayari wapo njiani kurudi.”
Magari mawili yaliyowabebelea wanajeshi yalikuwa yanarudi kwa mwendo mkali baada ya mpango wa uvamizi kusitishwa. Yalikuwa ndani ya eneo kame lenye udongo mwekundu na vichakachaka vya hapa na pale. Eneo hilo lilikuwa tajiri kwa vumbi jekundu.
Baada ya matembezi ya kilomita kadhaa ndani ya eneo hilo jekundu, madereva waliona magari matano mbele yao umbali wa kilomita kama sita. Magari hayo yalikuwa ni makuukuu ila imara yakiwa yamewabebelea watu lukuki kwa nyuma.
Baada ya kusogeleana zaidi, ndipo wanajeshi wale ndani ya magari yao mawili wakapata kutambua magari yale yalikuwa yamewabebelea wanaume wenye silaha, na tena walikuwa njiani kuwashambulia! Midomo ya bunduki zao ilikuwa imeelekezwa kwao.
Kabla wanajeshi hawajaanza kujihami kwa kushambulia, walijikuta katika matata mazito baada ya kuanza kupokea mashambulizi mazito tokea nyuma! Hawakufahamu ya kwamba nyuma yao kulikuwa kuna magari matatu yalikuwa yanawafuata. Maadui hao waliweza kutumia vizuri vumbi lililokuwa linatimuliwa na magari ya wanajeshi hao kwa kujificha dhidi ya vioo vya pembeni. Walijipanga katika mstari mmoja wakicheza na vumbi zito. Haikujulikana walijikobeka humo muda gani.
Risasi zilirushwa kwa fujo kufuata magari ymawili ya jeshi. Risasi hizo zilitokea mbele na nyuma. Wanajeshi hawakuweza kumudu mashambulizi hayo, madereva walishindwa kumudu vyombo, vikakengeuka!
Kwa uhakiki zaidi, wanaume wale waliokuwa ndani ya magari yale nane kwa idadi, waliendelea kushambulia magari ya wanajeshi wa Liberia mpaka pale yaliposhika moto na kulipuka, ndipo wakatokomea eneo hilo.
***
Ni jioni tulivu ndani ya kipande kidogo cha ardhi ya Guinea.
Ndani ya jengo kubwa jeupe lililozingwa na wanajeshi watatu getini, sebuleni, alikuwa ameketi bi Fatma; mke wa Kone. Mkononi alikuwa amebebelea glasi maridadi yenye mvinyo mwepesi rangi ya kahawia. Hali yake ya mwili ilikuwa imetengemaa sasa, majeraha usoni yalikuwa kwa mbali, labda kwasababu ya vipodozi.
Nywele zake zilikuwa zimesukwa na kufumwa vema. Mwili wake ulikuwa umefunikwa na gauni ghali la heshima. Alikuwa ananukia kama bustani. Kila kitu kilikuwa mahala pake; hakika mwanamke alipendeza. Usingeweza kudhani kama ana watoto kadhaa.
Macho yake yalikuwa yanatazama filamu ya kilatini akiwa amezama haswa. Filamu hiyo alikuwa anaishushia na kinywaji chake maridadi kabisa mkononi. Kwa muda kidogo alikuwa kwenye ulimwengu wa peke yake.
Wakati filamu hiyo ikiendelea kunguruma, mlango wa sebule ulifunguliwa akaingia mwanaume aliyevalia kanzu ndefu nyeupe na kofia nyekundu. Mwanaume huyo alikuwa mweusi na aliyejaza nyama, uso wake haukuonekana mpaka pale alipogeuza uso kuuacha mlango na kumtazama bi Fatma kwa tabasamu.
Alikuwa Raisi!
Bi Fatma alinyanyuka akamkimbilia na kumkumbatia kwa furaha. Walipeana mabusu kabla hawajaachana na kuketi. Walijuliana hali kisha wakawa wanateta hoja za ziada. Wakati huo filamu iliisha na sasa macho na akili ya bi Fatma ikawa kwa Raisi.
“Nina habari njema kwako,” alisema Raisi.
Kiu kikaonekana kwenye macho ya bi Fatma.
“Habari gani hiyo?” aliuliza bi Fatma akijilaza kwenye mapaja ya Raisi. Raisi alichezea nywele za bi Fatma akiongea:
“Kwanzia sasa hutohitaji tena kuwa na wasiwasi wala mashaka,” alidokeza Raisi. “Hivi tunavyoongea hapa, Kone yupo ndani, na hatotoka kamwe!”
Bi Fatma akakurupuka toka kwenye mapaja ya Raisi. Alitazama kwa bumbuwazi uso akiwa ameukunja.
“Unasemaje?”
“Kone yupo ndani mpenzi,” Raisi alisema kwa tabasamu. “Hatimaye sasa amenipa sababu nzuri sana ya kumweka ndani; kutotii maagizo ya mkuu wa nchi.”
Akaangua kicheko.
“Sasa tunaweza tukajivinjari tutakavyo … vipi hujafurahi?”
Macho ya bi Fatma yalikuwa mekundu. Alimtazama Raisi kwa uso wa kughafirika akisaga meno.
“Tafadhali, naomba ukamtoe,” alisema kwa sauti ya kutetemeka.
“Wewe mzima kweli?” Raisi aliuliza. “Nikamtoe nimpeleke wapi? Ina mana bado unataka kuwa naye pamoja na kukutenda yote hayo?”
“Tafadhali tafadhali, naomba ukamtoe. Akiwepo ndani watoto watapata shida mno. Nakuomba sana.”
“Siwezi kumtoa,” alisema Raisi. “Unadhani nikimtoa alafu akagundua itakuaje?”
Si bure Raisi alitilia shaka. Kone hakuwa mtu wa kumpuuza hata kidogo. Kwanza ni mtu anayejulikana kama mmoja wa maafisa weledi serikalini, watu wengi wanamtambua, huo ni mtandao. Pili, ni mwanaume aliyeumbwa kwa mafunzo ya kutumia viungo vyake kujilinda na hata kuutoa uhai wa mtu.
Rekodi yake ya jeshi si ya kubeza. Si mzuri sana kwenye habari za upelelezi ila ni mwanaume ambaye ana uwezo mkubwa sana wa kumfanya binadamu mwenzake amuogofye. Jambo hili halikuwa linajulikana sana kwasababu Kone si mtu wa maonyesho wala majigambo.
Sifa zake hizo ndizo zilimvutia Raisi na kumweka mwanaume huyo karibu akimtuma kwenye kazi zake nyeti. Kone ni mtu wa kutunza siri lakini pia mwenye kuzimudu asiyewahi kukata tamaa. Hakuna kazi aliyowahi kushindwa, labda tu kukawia.
“Nipo chini ya miguu yako. Kone hajakutenda lolote baya, astahili haya kabisa! Amejitolea sana kukufanyia kazi leo unakuja kumlipa kwa kumfunga?”
Raisi hakutaka kusikiliza, alinyanyuka akaondoka zake kuelekea chumbani.
Bi Fatma alilia na kusaga meno. Alijiona msaliti asiye na huruma. Kwa muda aliwafikiria wanae na mumewe aliyeko lupango, kifua kikajaa uchungu na hasira. Alikumbuka namna familia yake ilivyokuwa hapo awali, tabasamu na cheko. Akashindwa kuvumilia.
Ilimlazimu sasa atoroke ndani ya jengo hilo akaikute familia yake. Ndivyo roho yake ilimwambia.
Ila anatorokaje?
Alifikiria namna ya kutoroka katika jengo lenye walinzi getini, mawazo yake hayakujipa kabisa. Alikaa hapo sebuleni akiendelea kuwaza na kuwazua mpaka mishale ya saa saba usiku. Hata lepe la usingizi hakuwa nalo.
Alinyanyuka akafuata dirisha akatazama nje. Aliona wanajeshi wawili wakiwa wanateta na bunduki zao mabegani. Kwa namna walivyokuwa wamesimama hapo usingeweza kudhani kama Raisi yupo ndani. Bila shaka yale yalikuwa ni makazi ya siri ya Raisi. Hata vyombo vya usafiri vilivyokuwemo ndani havikuonyesha kama ni vya mtu mkubwa kiasi hicho.
Bi Fatma alienda mlangoni mwa chumba alimoingia Raisi, akaita kwa sauti ya chini. Hakukuwa na majibu. Aliporidhia kwamba Raisi hasikii, alitoka ndani ya nyumba kwa kutembea taratibu. Alifungua mlango akatazama usalama, akaona unaridhisha.
Alizunguka nyuma ya nyumba kwenda ukutani akidhamiria kuruka. Ila kabla hajafanya hivyo, alihisi kuna mtu anamsogelea. Bila kutazama, haraka akapandisha gauni lake juu na kushusha kufuli yake chini.
Mapaja yake yote yalikuwa wazi. Gauni lake alilolinyanyua lilikomea chini kidogo mwa makalio.
Sauti ya mwanaume akisafisha koo ilisikika, bi Fatma akaigiza kujifunika kwa aibu. Alikuwa ni mwanajeshi mlinzi aliyebebelea bunduki akisogea kwa tahadhari, lakini tayari picha ya mapaja ya bi Fatma ikiwa kichwani.
“Kuna tatizo lolote mama?” aliuliza.
“Hapana,” akajibu Fatma kwa sauti ya puani. “Kwani kuna tatizo afande?” akauliza kichokozi.
Akili yake yote ilikuwa inaifikiria bunduki ya mwanajeshi ni kwa namna gani ataitia mkononi.
****
Kuna nini kwenye mahusiano ya Raisi na bi Fatma?
Nini hatma ya Kone lupango?
☆Steve