Njia nyembamba --- 09
Mtunzi; SteveMollel
Si punde nyingi taarifa inamfikia Al Saed kwa njia ya barua pepe. Kwa muda huo hakuwa na habari yoyote na aidha alikuwa anangojea habari njema ya kuteketezwa kwa ‘kijikundi’ cha AMAA, wapumbavu waliokuwa wameanza kumchezea sharubu.
Alikuwa amekaa kwenye uwanda wa nyumba yake, ikulu, macho yake ndani ya miwani yakiwa yanatembelea baadhi ya mikataba iliyokuwa mbele yake, mikataba iliyokuwa inahusisha nyanja mbalimbali za kimaendeleo mathalani uvuvi, ukulima na madini. Macho yake yalikuwa yamezama ndani ya makaratasini akiwa amebeba tahadhari kubwa. Lakini ghafla anashikwa begani na kutibuliwa utulivu huo.
“Kuna ujumbe wako, mkuu.” Alikuwa ni mtumishi wake aliyevalia suti nyeusi akitamka.
“Kutoka kwa nani?” aliuliza Al Saed akiendelea na kazi yake ya kupekua mikataba.
“Mr X,” akajibu mtumishi.
Moyo wa Al Saed ukapasuka. Alivua miwani yake akamtazama mtumishiwe.
“Una uhakika?”
Uso wake ulitambaliwa na puzo la shaka. Hata kabla hajajibiwa alionekana kupata jibu la swali alilouliza.
“Ndio, mkuu. Umeingia sasa hivi!”
Al Saed alipandisha kichwa chake juu kabla hajamruhusu mtumishi wake aende zake. Alibakia kitini kwa muda kidogo akitafakari na kubashiri nini ambalo Mr. X atakuwa amelituma. Kwa namna moja kubwa aliona si alama njema kupokea ujumbe toka kwa Mr. X kwanza kabla ya ujumbe toka kwa Samweli.
Alishusha pumzi ndefu akaenda ndani. Alimkuta mtumishi wake yupo karibu na tarakilishi yake mpakato, akaivuta na kutazama. Loh! Hakukuta maneno yoyote bali picha; picha za kutisha na kusisimua; picha za vichwa vitatu visivyo na viwiliwili!
Kama vile aliyemtumia picha hizo alijua ya kwamba Al Saed yupo hewani, mara ujumbe mfupi unaingia. Al Saed bado alikuwa kwenye pumbazo la kujiuliza zile picha azitazamazo ni za nani na kwanini ametumiwa. Alishtushwa na ujumbe huo, haraka akarusha macho yake kuusoma:
“Hiyo ni salamu kwako kafiri, usithubutu kufanya jambo lolote la kipumbavu.”
Al Saed alidadavua ujumbe huo kwa dakika moja, haraka akampigia simu Samweli na kumjuza. Habari hiyo ikapokelewa kwa mshangao; Samweli hakutegemea kama ingalikuwa rahisi kwa makachero wake anaowaamini kumalizwa namna hiyo. Ilimlazimu sasa kuchukulia jambo hilo kwa namna tofauti; kwa namna nzito na kwa umakini zaidi.
Hawakuongea sana, simu ikakatwa. Al Saed aliendelea kutazama picha alizotumiwa kwa takribani dakika tatu. Kila alipojaribu kutuma ujumbe wa kumjibu Mr. X, ujumbe haukwenda. Uligoma na kumtaka aweke kwanza anwani ndipo apate kutuma. Al Saed akaishia kughafirika na kutoka ndani.
Miwani sasa ilibidi ibadilishwe, pasi na shaka. Jambo lilikuwa kubwa kuliko walivyodhania, lakini pengine bado lilikuwa kubwa kuliko ambavyo bado wanadhania.
Wafuasi wa AMAA, si kwamba walikuwepo ndani ya kile kijiji kidogo tu, walikuwa wametapakaa maeneo yote ya karibu na eneo hilo wakiwa wamejihami kwa silaha nzito lakini pia wakiwa wamejiweka katika mazingira ya kujificha vya kutosha kiasi cha kutoonekana kwa wepesi.
Kijiji kizima kilikuwa kina mahesabu kamili ya wanamgambo hao wa kikundi cha AMAA. Hiyo ndiyo ilikuwa ngome yao na hivyo basi kila namna iendeleayo humo walikuwa wanaifahamu. Kila mwanakijiji alikuwa ni mhusika wa kikundi hicho aidha kwa njia moto ama vuguvugu. Kila mgeni aliyeingia humo alitazamwa kwa ukaribu akifuatiliwa nyendo haswa.
Shaka kwa makachero wawili wa Samweli lilikuwa ni la kawaida hapo awali. Hata wenyeji wao hawakuwa wameng’amua lolote la kugutusha. Ila pale gari la Samweli lilipotua maeneo hayo, ndipo mambo yakaanza kuwa uchi.
Walifwata nini ndani ya lile gari? Kwanini gari halikuja ndani ya kijiji? Nani yupo ndani ya gari? Hapo ukakasi ukaanza. Japokuwa makachero hao na mkuu wao, bwana Samweli, walidhani wapo wenyewe baada ya kukiacha kijiji kilomita kadhaa, ukweli ni kwamba kulikuwa kuna watu watatu ambao walikuwa wanatazama gari hilo na darubini kali.
Lakini kama kuna kosa kubwa ambalo makachero hao walilifanya basi ni kwenda msikitini siku hiyo hiyo baada ya kuonana na mkuu wao. Mbona siku zote hawakwenda na ingali walikuwemo ndani ya kijiji? Mosi. Pili, walitolea wapi kanzu mpya wakati hali yao ya kimaisha ilionekana ni duni? Walijichimbia kaburi. Jicho la karibu lililokuwa linawatazama likageuka kuwa upanga uliokula vichwa vyao.
***
Agizo la Raisi ni amri. Japokuwa kishingo upande, Kone alijiandaa kwenda Sierra Leone kutimiza alichotumwa. Yeye ni nani abishane na Raisi?
Macho yake yalikuwa yamevimba. Uso wake ulikuwa na uchovu. Ulikuwa ni muda wa jioni akiwa tayari ameshakata tiketi ya ndege ya kumtwaa masaa manne mbele. Alioga kisha akachukua mashati mawili aliyoyatupia kwenye gari. Alijiveka viatu vyeusi vya ngozi vilivyokuwa vinang’aa, akamwita mlinzi na kutoka naye garini.
Hawakuongea neno lolote mpaka pale walipokaribia uwanja wa ndege. Kone alikuwa mwingi wa mawazo. Alisonya kwanza kabla hajasema kwa uchovu:
“Nadhani unakumbuka niliyokwambia.”
Mlinzi akatikisa kichwa chake kukubali.
“Ndio, kiongozi. Nakumbuka.”
Kukawa kimya tena mpaka wanaingia eneo la uwanja wa ndege.
“Nakuamini,” alisema Kone. “Natumai hautoniangusha.”
“Sitakuangusha kiongozi wangu.” Mlinzi akasema kwa kujiamini.
Kone alivuta begi fulani dogo toka viti vya nyuma, akalipakia mashati yale mawili kisha akashuka akienda ndani ya uwanja. Mlinzi alijisogeza kwenye kiti cha dereva, akatia moto gari apate kutimka. Alirudisha nyuma gari, ila kabla hajaondoka alisikia gari likipigwa kwa nyuma. Alitazama kwa kutumia vioo vya pembeni, akamwona Kone!
“Hakuna safari!” Kone aliwaka akiwa dirishani mwa gari. “Safari zote za kwenda Sierra Leone zimesitishwa mpaka pale taarifa itakapotolewa.”
Mlinzi akaachama kwa mshangao.
“Kumbe taarifa ilitolewa masaa kadhaa hapo nyuma, sikutazama simu!”
Kone alitabasamu. Mlinzi alikuwa anamtazama mwanaume huyo kwa macho ya duwazo, na kwa namna fulani alihisi Kone anaweza akawa amechanganyikiwa.
“Kwanini safari zimesitishwa?” Mlinzi aliuliza.
“Ni kwasababu za kidiplomasia. Hakuna mahusiano mazuri kati ya Sierra Leone na Guinea kwa sasa. Hawatutaki nchini mwao!”
Gari lilitoka uwanja wa ndege mlinzi akiendesha. Kone alimpigia simu Raisi akamjulisha kuhusu jambo la Sierra Leone. Raisi kwa utulivu akaagiza kwa sauti yake nzito:
“Ni lazima leo uende Sierra Leone kwa namna yoyote ile, Kone.”
Uso wa Kone ukawa mweusi.
Raisi alikata simu. Baada ya robo saa akapiga tena kumpa maagizo Kone. Alimtaka aelekee mashariki kusini kuukuta mpaka uwatenganishao na Sierra Leone. Huko atakuta usafiri utakaomwingiza ndani ya nchi hiyo kimagendo.
Haikujalisha Kone alikuwa amekwazika namna gani, gari liligeuza mwelekeo kutii amri ya Raisi. Baada ya masaa matano wakawa wamefika panapotakiwa. Kone alikuta gari aina ya van rangi ya bluu iliyokoza. Lilikuwa limechoka mno na lilikuwa linakaribia kujaza watu, hohehahe kwa hali, lipate kutimka.
Ndani ya gari kulikuwa kuna wanyama mathalani kuku, mbuzi na ndama. Lakini pia lilikuwa limejaa joto na uvundo. Sura za watu waliomo humo zilikuwa zinarandana kwa ukata na kuchakaa.
Kabla ya Kone kupanda humo, alimuuliza kondakta:
“Kuna usalama wa kufika Sierra Leone?”
Kondakta alimtazama kwa mshangao.
“Ndio mara yako ya kwanza kwenda Sierra?”
“Hapana,” akajibu Kone. “Ila ndiyo mara ya kwanza kutumia usafiri huu.”
Kondakta akatabasamu.
“Usijali, usalama upo. Ila bila shaka utatusaidia endapo tukikamatwa na wanajeshi.” Alisema akimtazama Kone. Bila shaka alimwona ni wa tofauti.
“Kivipi?”
“Usijali, ni kuwahonga tu. Ukiwapatia kitu kidogo basi wanaturuhusu. Huwa tunafanya hivyo mara kwa mara endapo wakishikwa na njaa.”
Kone alitikisa kichwa chake kwa masikitiko. Alitazama lile gari analoeleka kupanda, akajikuta akitokwa jasho. Aliagana na Mlinzi wake kisha akajitweka ndani ya gari hilo mbanano, na punde safari ikaanza.
Ni umbali mfupi tu tokea pale safari ilipoanzia mpaka ndani ya Sierra Leone, ila kwa mujibu wa gari lile ambalo lilikuwa linasimama na kubustiwa, ama kutiwa maji ndio lipate kwenda, wakatumia masaa manne kuingia.
Ilikuwa ni usiku sasa. Kone alilazimika kutafuta mahali pa kulala. Alikosa kabisa sehemu nzuri akaishia kulala kwenye nyumba fulani iliyochoka mno, akipewa hifadhi na mzee mmoja mkarimu. Alipata chakula hapo na kukabidhiwa mkeka autumie kama kitanda. Mazingira hayo yalimwia vigumu lakini hakuwa na namna zaidi ya kukabiliana nayo.
Mwenyeji wake alimwambia mahali hapo huwa panatembelewa mara kwa mara na wanajeshi kwasababu ya kukaa karibu na mpaka, hivyo basi asiwe mtembezi. Akatii.
Alimpigia simu Rose, akawa hapatikani. Wakati akiendelea bado kumtafuta mwanamke huyo alijikuta akipitiwa na usingizi mzito kutokana na uchovu mkali. Alikuja kuamka saa kumi na mbili asubuhi ambapo aliaga na kufanya mpango wa kuitafuta Freetown.
Akiwa njiani alimpigia simu Mlinzi, simu ikaita mara tatu pasipo kupokelewa. Aliachana na hilo zoezi lakini haikupita muda mrefu, simu ya Rose ikaingia. Alipokea na kumtaka mwanamke huyo waonane ndani ya jiji la Freetown baada ya masaa kadhaa, Rose akaridhia.
Mwanamke huyo alikuwa ndani ya hoteli kubwa wakila raha na Talib. Ilimpasa aende chooni kuwasiliana na Kone kwasababu za usalama. Alimwomba Talib muda wa kwenda kupumzika nyumbani kwake, Talib pasipo na kinyongo akamruhusu. Alijiweka kwenye gari lake, akiendesha yeye mwenyewe, akaenda mpaka nyumbani kwake.
Alioga na kujivesha nguo maridadi kabla tena hajatoka nyumbani kwake, na mazingira yasiyomjuza, akaelekea mahali fulani ufukweni mwa bahari. Miwani yake kubwa ya macho na nywele nyingi za bandia zilimfanya asijulikane kama ni katibu mkuu wa nchi, bali mwanamke fulani aliye kwenye starehe zake.
Ilikuwa imebakia kama nusu saa tu, Kone atinge ndani ya Freetown. Alikuwa amesinzia kwenye kiti cha basi akiwa ameegemea kioo cha dirisha. Alikuwa amechoka, ungeweza kumwona kwa macho tu. Mdomo wake ulikuwa umeachama akikoroma kwa mbali.
Simu yake iliita mara nne, hakusikia. Alikuja kugundua hilo aliposhuka toka kwenye basi baada ya kushtuliwa na kondakta kuwa basi limefika mwisho. Kioo cha simu yake kilimjuza Mlinzi alimtafuta mara zote hizo. Pasipo kujivunga, akaamua kumpigia.
“Amekuja leo kumjulia hali,” Alisema Mlinzi.
“Lile lile gari?”
“Ndio, amekuja leo asubuhi na mapema, sijui amejuaje kama shemeji yupo hapa.”
“Umemfuatilia?”
“Ndio! Nimemfuatilia mpaka nyumba aliyoingia.”
“Safi sana. Umefanya kazi nzuri!”
“Lakini kiongozi kuna jambo kidogo.”
“Niambie.”
“Kwenye nyumba ambayo gari hilo limeingia, kuna ulinzi mkali mno. Ni ngumu hata kusogea karibu; inaonekana huyu jamaa ni mtu mzito serikalini.”
Kone akanyamaza kwa muda. Alijaribu kuvuta picha ya huyo mtu kichwani kumbukumbu zake zikagoma kabisa kuunga mkono hoja kwamba anamjua. Ni mtu gani mzito kwenye serikali hii ya Guinea asipate kumjua? Aliwaza.
***
Liberia: ndani ya chumba chenye mwanga hafifu.
Walikuwemo watu watatu ndani ya chumba kimoja msikitini. Nyuso zao hazikuwa zinaonekana vema kutokana na uhafifu wa mwanga. Wawili walikuwa wamevalia kanzu nyeusi na mmoja pekee ndiye alivalia kanzu nyeupe. Walikuwa wameketi chini wakitengeneza umbo la pembe tatu.
Kulikuwa ni kimya usidhani kama kuna watu.
“Nadhani maelezo yote umeshayapata,” alisema mwanaume mmoja ndani ya kanzu nyeusi. Sauti yake ilikuwa nzito na ya kukwaruza. “Wewe ndiye umeteuliwa kufanya sadaka hii, utasaidiana na mwenzako hapo. Ni muda sasa wa dunia kujua uwepo wetu rasmi.”
Baada ya kusema hayo, mwanaume huyo alipeleka mkono wake wa kuume upande wa kushoto nyuma kwake, akavuta begi fulani kubwa. Alilisogeza karibu na yule pekee aliyevaa kanzu nyeupe akisema:
“Kila kitu mnachohitaji kipo humo. Kila kitu mnachohitaji kwenye kufanya kazi yako hii takatifu.”
Pasipo kuhakikisha kama yasemwayo ni kweli, yule mwanaume aliyevaa kanzu nyeupe alilitwaa begi akatikisa kichwa chake.
“Tutafanikiwa kama vile Mungu apendavyo.”
Wenzake wakatikisa kichwa na kumwekea viganja kwenye bega lake la kulia.
Asubuhi na mapema, gari dogo jekundu Toyota Starlet linatoka kijijini hapo likiwa limebebelea wanaume wawili. Wote wamevalia kiraia. Macho yao makubwa yanaangaza na nyuso zao zimejawa tahadhari.
Kwa mwendokasi wa wastani gari hilo lilitembea. Mpaka kufikia karibu na jioni, walikuwa tayari wameingia ndani ya jiji la Monrovia. Walikodisha chumba cha malipo nafuu wapate kumpuzikia hapo. Walikula chakula cha kawaida na kuswali kabla ya kulala.
Asubuhi ya mapema, waliamka wakaswali. Mmoja, mweusi kuliko mwenzake, alivua nguo zake akibakiwa na nguo ya ndani pekee, mwenzake akaanza kumfunga ‘kikoti’ cheusi alichokitoa ndani ya begi, kisha akamfunga na mkanda mnene mweusi kiunoni. Baada ya hapo akahakikisha kama vitu hivyo vimekaa vema. Aliporidhika, alimvesha mwenzake kanzu yake na kumkabidhi rimoti ndogo.
Walitazamana wakawekeana viganja kwenye mabega yao ya kulia na kutikisa vichwa vyao. Kisha wakatoka ndani kuendea gari.
***
☆Steve