Njia nyembamba (Simulizi mpya by SteveMollel)

Njia nyembamba (Simulizi mpya by SteveMollel)

*Njia nyembamba -- 13*



*Mtunzi: SteveMollel









“Hapana,” akajibu Fatma kwa sauti ya puani. “Kwani kuna tatizo afande?” aliuliza kichokozi. Alilegeza macho na lips zake alizibinua katika namna ya pekee. Kwa muda mchache sana alifanikiwa kuufanya uso wake kuwa mithili ya mtoto – asiye na makosa na anayevutia, kwa pamoja.

“Hamna tatizo mama. Nipo tu lindo,” alisema Mwanajeshi kwa sura nyepesi. Bi Fatma alinyanyua miguu yake akamfuata mwanaume huyo akimtazama machoni. Uso wake ulitosha kabisa kumpumbaza mwanaume wa watu aliyekuwa hajui cha kufanya kwa muda huo zaidi tu ya kumtazama.

“Kuna kitu nataka kukwambia,” alinong’oneza Fatma. Alikuwa sasa anatia huruma na macho yake yalidai kusikizwa. “Ila sidhani kama una kifua.”
“Niinacho,” alidakia mwanajeshi. “Unaweza tu ukanambia.”
“Kweli?”
“Ndio, mama.”

Fatma alisogea zaidi. Alishika vifungo vya shati la mwanajeshi akimtazama kwa macho ya ashki. Huwezi amini mwanajeshi yule alikuwa tayari ameshaikomaza dhakari yake. Akili yake ilishakimbilia kwenye mapenzi wakati ya Fatma ikiwaza namna ya kutoka eneo hilo haraka kabla kitumbua hakijaingia mchanga.

Siku zote silaha ya kwanza ya mwanamke kwenye uwanja wa mapambano, ni nguvu ya ushawishi wake kimapenzi. Mungu hakuwapatia nguvu ya misuli, ila pia hakuwanyima namna nyingine ya kusogeza milima, tena katika njia nyepesi kama vile kumuua mbu.

Damu ya mwanaume ilikuwa inazunguka upesi. Fatma alijikusanya akafyatua goti lake kukita kende za mwanajeshi aliyekunja sura na kulalama kwa maumivu makali kisha akaikwapua bunduki ya mwanajeshi huyo na kumzaba nayo kichwani, akazirai.

Fatma alitazama kushoto na kulia, hakukuwa na mtu. Mkononi akiwa na bunduki, alikimbia kuufuata ukuta. Aliukwea upesi na kujitupia nje. Alidondoka mithili ya kiroba lakini hakubakia kuugulia maumivu, alinyanyuka na kuondoka kwa kukimbia.

Akiwa ameacha jengo hilo kwa umbali wa robo kilomita, alisikia filimbi kali iliyomshtua. Aligeuza uso wake kutazama, punde akaona wanaume wawili wanatoka ndani ya uzio. Walikuwa wamebebelea bunduki mikononi mwao wakiteta kupeana maelekezo. Ilikuwa ni wazi wanamtafuta yeye.

Haraka Fatma alikimbia akielekea upande wa kaskazini. Kwenye kona ya kwanza, aliitupa bunduki, kona yake ya pili akakutana na pikipiki aliyoisimamisha na kukwea.

“Twende upesi!” aliamrisha.
“Hii siyo pikipiki ya biashara dada.”
“We twende! Twende!” Fatma alisema akimpiga dereva makofi ya mgongo.
“Unaelekea wapi sasa?”
“We twende tu bwana! – ila siyo huku!” alinyooshea kidole alipotokea.

Dereva akaondoa chombo chake kwa kasi. Baada ya kuendesha kwa muda kidogo, Fatma akampa maelekezo wapi anataka kwenda. Alielekezea nyumbani kwake.

“Kuna mtu anakukimbiza dada?” Dereva aliuliza. Fatma alikuwa yu bize kutazama nyuma kama anafuatwa. Uso wake ulikuwa umetwaliwa na hofu. Moyo wake ulikuwa unapiga kwa kasi. Dereva alirudia swali lake mara mbili ndipo akamsikia.

“Ni wezi tu walikuwa wanataka kuniibia.”
“Pole sana.”

Fatma alifika nyumbani akaonana na mlinzi. Alimuuliza kituo alipopelekwa mume wake, akamwambia. Alimkabidhi dereva fedha, akazikataa akidai ni msaada tu. Fatma alikwea tena pikipiki hiyo mpaka kituoni kukutana na mumewe. Baada ya kujitambulisha, aliruhusiwa kuonana na mlengwa wake, ila kwa kishingo upande sana, na tena akipewa muda mchache mno. Laiti kama Kone angelikuwa ni mwananchi wa kawaida, Fatma asingelipata fursa hiyo.

Alienenda mpaka kwenye chuma za lupango aliyoelekezwa, akazishika na kuita jina la mumewe mara moja kwa sauti ya chini. Kulikuwa ni giza na hakuwa anaonekana yeyote ndani. Mbu walikuwa wamejaa wakisikika wanaimba kwaya.

Baada ya muda mfupi, vishindo vya miguu vilivuma, na mara Kone akatokeza. Macho yake yalikuwa mekundu, uso wake ulikuwa mzito. Hakudumu ndani ya lupango hata kwa siku mbili ila alikuwa tayari amejaa vipele. Hakula muda wote aliokuwemo humo ndani, hakutaka kabisa. Kichwa chake hakikupata mapumziko dhidi ya mawazo.

“Nisamehe mume wangu,” yalikuwa maneno ya kwanza Fatma kuyasema baada tu ya kumuona Kone.

“Najua nimekukosea sana. Hata haya unayoyapitia ni mimi nimesababisha, ila natamani nipate muda wa kurekebisha makosa yangu. Naomba unipe muda wa kunisikiliza, nina mengi ya kusema.”

Kone hakusema jambo. Kwa kutazama tu uso wake ingetosha kukupa jibu ni namna gani alivyokuwa ameghafirika, amekwazika. Macho yake hayakuweza kuvumilia zaidi, yakaanza kudondosha machozi. Meno yake yaliumana nusura yavunjike.

“Nisamehe mume wangu. Haikuwa lengo langu, wala haikuwahi kuwa dhamira yangu,” aliendelea kudai Fatma.

“Watoto wapo wapi?” Kone akauliza.
“Kwa bibi yao.”
“Mara yako ya mwisho kuwaona ni lini?”
Fatma alijiuma kujibu.
“Nenda kawatazame na ukae na watoto. Sitaki kukuona hapa kamwe!”
“Siwezi kwenda kuwaona. Na sijui kama nitapata hiyo nafasi, Kone. Inawezekana hata hii ikawa ndiyo nafasi yangu ya pekee kukuona.”

Fatma alitazama pande zote, kisha akasema kwa sauti ya chini zaidi.

“Raisi ananiwinda kwa sasa. Hapa nimetoroka toka kwenye makazi yake. Najua ataniadhibu punde tu atakaponikamata. Kwa muda wote huo nilikuwa kwake, nikiishi kama mtumwa …”

Hakuendelea zaidi, kiganja kikubwa kikamgusa begani.

“Muda wako umeisha.” Sauti kavu nzito ilinguruma. Alikuwa ni polisi, mwanaume mrefu mweusi. Macho yake yalikuwa yanang’aa kama ya paka. Alimtazama Kone kwa jicho kali kabla hajamsukuma Fatma kuelekea upande wa kutoka.

Kone hakusema jambo, alibakia pale vyumani akitazama mkewe akiyoyoma. Muda mfupi mbele, masikio yake yakamtaarifu kuna ujio mpya pale kituoni. Walikuwa ni wanaume wawili ambao walijitambulisha kwa sauti za kujiamini, Kone hakusikia vema, ila mwishowe sauti ya polisi, yule aliyekuja kumtwaa Fatma, ilifika vizuri masikioni mwake ikisema:

“Mnaweza mkamchukua!”

Fatma alipaza sauti ya kukataa, ila mara sauti ya kofi ikavuma kisha kimya. Mara sauti ya gari nayo inasikika na kisha kutulia. Ni dhahiri shayiri, Kone akawa amejua nini kilichotukia. Aliminya vyuma vya lupango kwanguvu mno. Alisaga meno yake akiwa bado hana cha kusema. Alisimama hapo kwa muda wa kama nusu saa, kichwa chake ndicho kikihangaika huku na kule.

Mwishowe alihitimisha kwa kusema:
“Hii ni vita: Aliyelikoroga atalinywa.”
Aliacha vyuma vya lupango akarudi kule alipokuwa. Gizani.



***



Wakati wa mchana mchanga; Sierra Leone.

Rose yupo ndani ya nyumba yake kubwa akiwa karibu na dirisha kubwa la kioo. Macho yake yalikuwa yanatazama nje, barabarani, ambapo hakukuwa shwari. Kuna muda watu walikuwa wanaonekana wakipita kimakundimakundi mikononi mwao wakibebelea silaha za jadi.

Mitaa haikuwa salama kabisa kwa watu kufanya shughuli zao. Tokea maandamano ya wafanyakazi yalipotukia, idadi ya watu waliouawa na kujeruhiwa ilikuwa inaongezeka maradufu. Si wananchi wala wanajeshi na polisi waliokoma kupambana. Huku na kule vurugu zilikuwa zinaripotiwa.

Tangu asubuhi alipoamka, Rose alikuwa ameketi karibu na dirisha akitazama. Alijaribu kumpigia simu Kone apate kumweleza, ila alikuwa hapatikani. Aliwaza nini itakuwa shida. Kwa namna moja akili yake ikamtaarifu Kone yupo matatizoni. Lakini atamsaidiaje ilhali kutoka tu ndani ya nyumba si salama?

“Dada!” Sauti ya mfanyakazi wa ndani ilimshtua Rose.
“Unahitaji chochote?”
“Hapana, ahsante.”
Rose aligeuza shingo yake akaendelea kutazama nje, ila mfanyakazi wake hakuondoka.
“Simu inaendelea kuita, dada,” alisema mfanyakazi kwa sauti ya unyenyekevu. Uso wake ulikuwa mpole akionekana si mjuvi sana wa jiji, ila ndani ya sare alipendeza.
“Nani anapiga?”
“Yule yule!”
Rose alisonya kisha akanyoosha mkono wake, mfanyakazi akampatia simu. Alikuwa ni Talib anapiga. Aliitazama simu akifikiria, mwishowe akapokea.

“We mwanamke kwanini napiga simu muda wote hupokei!” Sauti ya Talib ilifoka saizi ya kuumiza masikio.

“Simu ilikuwa mbali,” Rose akajibu kiwepesi.
“Simu ilikuwa mbali tokea juzi?” Talib aliuliza. Rose akakata simu na kuizima kisha akaendelea kuangaza macho yake nje ya nyumba, huko barabarani.

Haikupita muda mrefu msafara mzito wa Talib ukafika mbele ya nyumba ya Rose. Wanajeshi kibao wakiwa wamebebelea bunduki walitapakaa huko nje kuhakikisha usalama.

Talib, kwa kasi kubwa, aliingia ndani ya nyumba ya Rose akipaza sauti kumuita mwanamke huyo. Uso wake ulibebelea hasira nzito, hata hatua zake zilisema hivyo. Alimtafuta Rose sebuleni pasipo mafanikio. Akaenda chumbani. Huko akamkuta Rose ameketi kitandani.

Kwa namna Talib alivyokuwa amevaa, nguo za jeshi, msako wake ulikuwa ni kama vile anamsaka hayawani, ama msaliti wa taifa.

“Hivi we mwanamke, nini kinakupa jeuri kiasi hiki?” Talib alifoka.

Rose alimtazama mwanaume huyo kwa uso wa utulivu. Akili yake ilimtahadharisha mapema kwamba ujio ule haukuwa wa amani, hivyo upesi akaanza kufanya jitihada za kujihami. Jitihada hizi Talib hakuwa na taarifa nazo.

“Si nakuuliza wewe!” Talib aliendelea kufoka. Aliufunga mlango kwa kuubamiza kisha akaanza kumfuata Rose akikunja vema mikono ya shati lake.

“Naona huna adabu, unataka kunipanda kichwani. Sasa leo nitakuonyesha upande wangu wa pili.”

Kabla hajamgusa mwanamke huyo, alijikuta yupo chini baada ya kubamizwa kichwani kwanguvu na taa ya mezani. Alidondoka chini kama kiroba. Macho yake yalikosa nguvu, akawa haoni kabisa. Kichwa kiligonga kwa maumivu makali mno. Upande wa kushoto wa uso wake alipasuka, damu ikawa inavuja.

Ilimchukua kama dakika kumi kurejea katika hali ya ahueni. Alinyanyuka akiwa ameshikilia kichwa chake, na uso ameukunja. Alitazama huku na kule, hakumuona Rose! Alitazama dirisha akaliona li wazi. Haraka alitoka chumbani akawapasha habari walinzi wake wamtafute Rose popote pale alipo. Aidha akiwa hai au amekufa, anataka amwone.

Upesi wanajeshi kadhaa walisambaa mtaani kumtafuta Rose. Talib alirejea ndani ya nyumba akaketi sebuleni. Bado alikuwa ameshikilia kichwa chake katika namna ya kuugulia maumivu.

Baada ya muda alimuona mfanyakazi, akamuita na kumuuliza wapi alipo Rose. Kwa hofu, mfanyakazi alijibu hajui wapi alipo mtu huyo kwani hakumuona tangu alipoingia chumbani kwake.

“Ebu niletee kinywaji haraka!” Talib akaagiza. Basi upesi mfanyakazi akapanda ngazi za juu kufuata jokofu kubwa la kuhifadhia vinywaji. Alifungua jokofu akatwaa kinywaji mmoja kilichofadhiwa kwenye chupa yenye chapa ya Jack Daniels. Alitwaa na glasi ndefu akaziweka kwenye sahani ndefu ya aluminiam tayari kwa ajili ya kumpelekea Talib.

Ila kabla hajashika ngazi ya kushuka chini, alisikia akiitwa kwa sauti ya chini. Aligeuka akaangaza, hakumuona mtu! Aliogopa.

“Tazama nyuma ya ua kubwa hapa,” sauti ilisema. Mfanyakazi akatazama. Loh! Akamuona Rose. Kwa namna alivyokuwa amejibana kwenye ua hilo kubwa, ni labda tu malaika akuambie kuna mtu hapo, la sivyo huwezi ukagundua.

Mfanyakazi alisogea kwenye ua hilo, Rose akamnong’oneza.

“Mtilie sumu!”
Macho ya dada wa kazi yakatumbuka.
“Siwezi!”

Rose alichukua glasi akatia kitu kama mchanga wenye rangi nyeusi. Ni kama vile alijiandaa na lile tukio, haikujulikana wapi alitolea kile kitu alichokitia glasini. Alirejesha glasi kwenye sahani kisha akamtaka mfanyakazi aende kumpatia Talib kinywaji.

“Hakikisha anakunywa,” alisisitizia. “Nenda!”

Dada wa kazi aliondoka akiwa anatazama nyuma. Ni kama vile hakuamini macho yake. Alijawa na shaka, mikono yake ilikuwa inatetemeka.

“Mbona umechukua muda hivyo?” Aliuliza Talib.
“Nil – nilikuwa nakuchagulia …”
“Nini?”
“Kinywaji mhesh-imiwa.”
“Ndio muda wote huo?”
“Samahani mheshimiwa.”

Dada wa kazi alifungua kinywaji, akamiminia kwenye glasi. Sasa alikuwa anatetemeka mno kiasi kwamba alishindwa kabisa kutulizia mdomo wa chupa glasini. Talib alimtazama, akamuuliza:

“We mwanamke una shida gani?”



***



☆Steve
 
Back
Top Bottom