Njia nyembamba (Simulizi mpya by SteveMollel)

Njia nyembamba (Simulizi mpya by SteveMollel)

Njia nyembamba --- 07



Mtunzi: SteveMollel





Tabasamu la Rose lilikuwa zuri mno, hata macho yake pia. Lakini roho yake, hakuna binadamu anayeiweza zaidi tu ya yule aliyemuumba. Ni mwanamke hatari kuwa naye karibu kwani akili yake inafikiria mara mbili ya wewe unapoishia.
Baada ya dakika kama kumi na tano barabarani hatimaye waliwasili mbele ya nyumba kubwa yenye uzio mrefu na wanajeshi kadhaa mlangoni wakiwa wamebebelea bunduki. Geti lilifunguka lenyewe, gari likazama ndani na kuwatema Talib na Rose walioingia ndani ya jumba na kuketi sebuleni.
Ndani ya muda mfupi, mhudumu alikuja kuwasikiliza wanahitaji chakula na vinywaji gani. Alikuwa ni mwanamke mrefu mweupe aliyevalia sare rangi nyeusi na nyeupe. Alikuwa amependeza ndani ya sare yake na pasipo shaka alionekana anajua kazi yake na namna ya kuitenda. Alitabasamu akiwa anapewa oda alizokuwa anaziandika kando. Aliomba radhi na kuondoka akiahidi ndani ya muda mfupi atakuwa amerejea.
Ni kama vile hotelini, kumbe ni ndani ya nyumba ya mtu! Maisha yanataka nini zaidi ya hapo?
Vililetwa vyakula vya maana kabla hata ya waliokuwa wanangoja hawajameza mate. Vinywaji navyo visiwe nyuma vikajazwa kwenye meza, tena vile vya ghali. Yani ni kana kwamba kulikuwa kuna tafrija, kumbe vyote ni vya watu wawili tu! Hawakutumia vijiko bali visu na uma.
Wakiwa wanakula hapo kwa kunyoosha mikono huku na kule kutwaa nyama, matunda ama vinywaji basi wakawa wanateta yanayosibu kwa muda huo. Rose alikuwa wa kwanza kuyateta kuhusu hali ya afya ya Kessy. Mwanamke huyo alikuwa ana kiu ya kutaka kufahamu.
“Bado hajapata fahamu zake. Hali yake si ya kuridhisha kwakweli,” alisema Talib akiwa anatafuna kisha akashushia na kinywaji. Rose alimsikiliza kwa hamu lakini jibu hilo halikukata kiu yake hivyo akaendelea kudadisi.
“Kwani daktari anasemaje?”
“Anasema inawezekana kurudi kwenye fahamu zake lakini kuna madhara makubwa atayapata. Sijui yule dhalimu alitumia sumu gani kwakweli!”
“Ila una uhakika ni yeye, Al Saed.”
“Hakuna mwengine zaidi yake. Yeye ndiye alikuwa wa mwisho kula na Kessy, na tena alimletea mvinyo toka Liberia.”
Talib akajikuta anaguna.
“Cha ajabu ni kwamba kwenye ule mvinyo hakujaonekana ishara yoyote ya sumu. Yani daktari anasema haijulikani aliitumia lini hiyo sumu, lakini wanaamini haitakuwa muda mrefu kutokana na madhara yake makubwa, na ndio hapo ninapoamini bado tu atakuwa ni Al Saed. Bado tu sijafahamu alitendaje na ni kwa nia gani.”
Wakala kwa muda pasipo kunena. Mara Rose akazuka tena na swali:
“Kessy akigundua tulikuwa wote itakuwa shida,” Rose alichokoza. Bado alikuwa anamchimba Talib pasipo mwanaume huyo aidha kujua ama kutokujua.
“Hawezi akagundua,” Talib alisema kwa kujiamini.
“Unajuaje?”
“Kwa hali yake ile si wa leo wala wa kesho.” Talib akajibu pasio kumtazama Rose. Alikuwa anakula lakini uso wake ukionyesha hana kabisa wasi na aongealo, basi kwa namna moja ama nyingine, Rose akatabasamu. Alipendezwa na jibu hilo. Lakini kumbuka adhma yake ilikuwa ni Kessy afe na sio kulazwa kitandani, sio? Kwahiyo bado kulikuwa na haja kwa yeye kuendelea kuchanga karata zake.
“Hivi ikitokea akafa, ikitokea lakini, itakuaje?”
“Nitakuchukua wewe!” Talib akaropoka kisha akaangua kicheko. Rose aliishia kutabasamu kisha akanyamaza. Alijua kabisa sasa mahali alipopagusa palikuwa ni penyewe, na Talib lazima azame.
“Au hutaki?” Talib aliuliza kwa kukejeli, lakini bado adhma yake ilikuwa nzito ndani ya kejeli hiyo.
“Naogopa,” Rose alijibedeuza.
“Unaogopa na nini na hatokuwepo duniani? Au hunipendi?” Talib aliuliza akimtazama mwanamke huyo kwenye paji la uso.
Rose aliona hiyo ndiyo fursa ya kuua mbweha. Aliyaminya macho yake kana kwamba amepaliwa na aibu, akatazama chini akitabasamu tabasamu pana. Basi Talib akajikuta anahisi kifua chake kimekuwa cha baridi. Mambo si ndo’ haya? Nafsi yake iliteta.
“Rose, unaweza ukawa na mimi?”
Rose kimya. Aliacha kula sasa akawa anatazama vidole vyake alivyokuwa anaviminya. Ushawahi kumtongoza mwanafunzi? Basi ndivyo Rose alivyokuwa: fisi dhalimu ndani ya ngozi ya kondoo!
“Eti mama, unaweza ukawa na mimi? Au mie so’ kama Kessy?”
“Talib, siwezi kukujibu swali lako kwa sasa,” Rose alifunguka. Alikuwa mjawa wa aibu nzito ambayo ilimfanya Talib azidi kuwehuka.
“Sawa, mpenzi, ila natumai nina nafasi yangu kwako. Lakini sitakulazimisha uimulike upesi hivyo n’takupa muda zaidi.”
Rose hakujibu, alitabasamu tu. Uso wake ukawa mweupe zaidi.
“Usihofie kitu chochote, Rose. Kila kitu kipo chini yangu kwa sasa. Hauna haja ya kumhofia yeyote yule.”
“Kweli?” Rose aliuliza akimtazama Talib kwa macho ambayo yanaweza msimisha kunguru kula mzoga.
“Kweli nakuambia,” Talib akaapia. Utaanzaje kukataa mbele ya macho yale tekaji?

***

Ni mida ya jioni, Al Saed anakaa mbele ya ikulu, makazi yake mapya. Hakuna mtu yeyote aliyeketi naye isipokuwa bakuli kubwa lililosheheni matunda ya kila aina likiwa limejaa kwenye meza ya ukubwa wa kawaida ikisheheni kwa urembo.
Mwanaume huyo alikuwa amevalia gauni kubwa jeupe la kitamaduni, pamoja na kofia yake. Mkono wake wa kulia ulikuwa umekamatia fimbo ndefu ya mbao ikiwa inameremeta. Kweli alionekana ni mkubwa wa nchi, haikujalisha aliingiaje madarakani, alikuwa ana muonekano wa kuvutia na wa kimadaraka.
Alikuna kidevu chake chenye ndevu za kumwaga akitazama ukutani kitafakuri. Kichwa chake kilikuwa kimebanwa na mawazo na kwa muda huo hakuwa anataka mtu yeyote amghasi. Akiwa anatafakari, alikuwa anakuna ndevu zake, muda mwingine akipindua mdomo wake mweusi, ama kuupeleka kando na kando.
Ndani ya kichwa chake ni ajenda mbili zilimnyima raha. Mosi, ilikuwa ni kuhusu muelekeo wa utawala wake baada ya kukutana na vikwazo toka nchi kubwa za nje. Pili, ilikuwa ni kumhusu Kessy na afya yake. Ni siku kadhaa sasa, Kessy hajaamka toka kitandani. Alikuwa anamhitaji ampatie ushauri haswa kwa muda huu anaokumbana na taabu za ‘wazungu’ kwani yeye pekee ndiye mtu aliyekuwa anarandana naye, ama tuseme marafiki.
Akiwa hapo anajinyima kwa ajili ya mawazo, mwanaume mrefu mweusi aliyevalia nguo za kijeshi alitokea nyuma yake akasimama umbali wa kama hatua tatu kabla hajamuita Al Saed kwa taadhima.
“Unasemaje, Man?” Aliuliza Al Saed pasipo kumtazama anayemuita.
“Kuna ujumbe wako,” alisema mwanaume yule, kwa jina Man. Uso wake ulikuwa umejawa na makovu. Mwili wake ulikuwa kakamavu na ulioshiba mazoezi ya viungo.
“Kutoka kwa nani?”
“Sijajua ni nani. Amejitambulisha kwa jina la Mr. X.”
“Mr X?”
“Ndio.”
“Ni ujumbe wa aina gani?”
“Barua pepe.”
Al Saed alitulia kwanza, kisha akajibu:
“Sawa, nakuja.”
Yote hayo aliyasema akiwa hamtazami Man. Alichukua kama dakika dakika tano ndio akanyanyuka kwenda kuukuta ujumbe wake. Haukuwa umefunguliwa, ilikuwa ni barua pepe ila haikuonyesha umetoka kwa nani, yani haikujulikana mtumaji ni akaunti gani!
Al Saed alibofya ujumbe huo uliokuwa umejaa kwenye kioo cha tarakilishi yake mpakato ya kisasa kabisa. Ndani yake akakuta maneno machache, kama mistari mitatu tu:
“Kwa usalama wako na wa wananchi wasio na hatia, tangaza taifa kuwa la kiislamu.”
Moyo wa Al Saed ukalipuka. Alijitahidi kujibu ujumbe huo kwa kuuliza ni nani mtumaji lakini ujumbe haukufanikiwa kwenda. Kila alipotuma uligoma akapewa taarifa ya kuweka akaunti ya mtumaji kwanza. Man naye alijaribu kama atang’amua tatizo, akashindwa.
Al Saed alirudi zake alipokuwepo mwanzoni akaketi na kuendelea kutweta kwa mawazo, sasa yakiwa yameongezwa maradufu. Aliwaza Mr X ni nani, amepataje akaunti yake ya barua pepe? Anataka nini?
Mwishowe kichwa chake kikawa chepesi kuamua inawezekana akawa ni Odong; mwanaume mnaijeria aliyekuwa kwenye kikundi chao cha uasi, Le tueurs, mpaka pale alipokuja kujinasua toka kwenye kikundi hicho yeye pamoja na wenzake kumi na tatu baada ya kukinzana kwenye namna ya kutenga misingi ya kikundi. Odong na wenzake walitaka kikundi kiwe na mrengo na itikiadi yenye Imani kali ya kiislamu kitu ambacho Al Saed na wenzake walipinga kwakuwa taifa lao lina watu wa dini zote, na si tu huko bali hata kundini pia.
Tangu pale walipojing’amua toka kwenye kikundi hicho cha Le tueurs, haikujulikana Odong na wenzake walielekea na wapo wapi. Al Saed alishawasahau watu hao, ila baada ya barua pepe ile sasa anawakumbuka kwa haraka mno. Lakini pia anahofia.
Baadae usiku wa saa nne, Al Saed anaketi kikao na wanaume watatu ndai ya kajieneo kadogo ndani ya ikulu. Kikao hicho hakikuwepo ndani ya ratiba yake bali kilikuwa ni dharura, tena ikiwa imeitishwa na msimamizi wa ulinzi, Samweli, akiwa na makachero wake wawili: Bui na Tariq.
Ilikuwa ni ajenda nyeti ya usalama. Hata kabla Samwel hajafungua mdomo, tayari Al Saed alilijua hilo. Alitulia tuli kusikiliza.
“Mkuu, kuna jambo linalotishia amani,” Samweli alitambulisha, kisha akaongezea: “Upande wa kusini mwa nchi tumepata taarifa kuna kikundi kinachojiita AMAA – Alwaqt min ajil alttaharrur. Hatujajua makazi yake ni yapi na kinaongozwa na nani, ila watu wanakiongelea. Ni cha siri mno kiasi kwama ni ngumu sana kupata taarifa zake kwa kina.”
Haraka kichwa cha Al Saed kikarejesha mawazo kwenye ile barua pepe. Mr X ni mhusika wa hicho kikundi? Alijiuliza. Hakutaka kusema kwa wale watumishi wake juu ya ile barua pepe. Aliwaagiza wakalifanyie kazi hilo swala kwa umakini zaidi kabla halijakuwa kubwa na hatarishi zaidi.
Alienda akanywa mvinyo wa kutosha maana ndiyo pekee iliweza kumpumzisha toka kwenye mkanda wa mawazo uliokuwa umembana.

Masaa nane baadae, Guinea:

Ni saa moja asubuhi na inamkuta Kone akiwa macho kwa kukosa usingizi. Anafungua pazia la dirisha lake kutazama nje, jua limesha amka. Haamini kwani anaona usiku umeenda haraka mno akiwa mpweke.
Macho yake ni mekundu mno. Amevalia suruali ya kitambaa na mkanda wake. Chumba kipo hovyo; si viatu wala soksi kilikuwa mahala pake.
Alinyoosha mkono wake kuupeleka kaskazini mwa kitanda akatafuta tafuta kitu, hakufanikiwa. Aliupeleka kusini akaikumba simu yake aliyoipeleka usoni na kutafuta jina la Rose. Alimpigia mwanamke huyo kisha akaiweka simu sikioni. Simu iliita mara tatu, ikapokelewa.
Alimuuliza juu ya hali ya Kessy, Rose akamtaarifu na kumpasha yote mpaka ya Talib.
“Raisi haniamini tena. Hataki kuniona na amesema ataendelea na vile yeye alivyopanga,” alilalama Kone. “Sijui cha kufanya kwa sasa, Rose. Nimechanganyikiwa kwakweli.”
“Usijali,” Rose alimpa moyo. “Nakuhakikishia Kessy atakufa si zaidi ya siku mbili.”
“Nimeshazoea ahadi, Rose. Raisi hataki tena ahadi!”
“Hii siyo tena ahadi bali ni uhalisia,” sauti ya Rose ilitamba, kisha: “Ngoja ntakupigia baadae, kuna kazi nafanya.”
Alisema hivyo na simu ikakata.
Kone alishusha pumzi ndefu, akalaza kichwa chake juu ya kitanda. Alitazama dari kwa muda kidogo, mara ghafla akasikia honi ya gari huko nje. Alinyanyuka upesi akakimbilia huko mithili ya mwehu. Alijua ni Fatma anarejea, na sasa alikuwa anataka kumuona huyo mwanaume anayemleta kila siku.
Alifikia geti akalikuta limefungwa. Alimkurupusha mlinzi ndani ya kibanda chake na kumtaka afungue geti upesi. Mlinzi alifanya hivyo, Kone akatoka nje. Huko alikutana na Fatma uso kwa uso na gari lililomleta likiwa bado halijaondoka. Lilikuwa ni lile lile, Prado, alilowahi kuambiwa na mlinzi.
Alilikimbilia apate kumwona mwanaume anayemharibia mkewe. Alipofika kwenye vioo vya mbele vya gari akamwona mwanaume rangi ya kahawia akiwa amevalia shati la bluu na tai nyeusi. Alikuwa ameshikilia usukani na punde tu alipomuona Kone alikanyagia mafuta akatimka.
Mwanaume huyo alikuwa mgeni kwa Kone, hakuweza kumtambua kabisa. Alivuta kumbukumbu yake ikagoma. Alichoweza kukifanya ni kunakili namba ya usajili ya gari na kisha akageuka kumtazama mkewe, hakumuona. Alikuwa tayari ameshazama ndani.
Haraka alifuata geti akajaribu kufungua, akashindwa. Lilikuwa limefungwa kwa ndani. Alimwita mlinzi na kumwamuru amfungulie, mlinzi akamtaarifu ya kwamba mkewe, Bi Fatma, ameondoka na funguo kwenda nazo ndani. Kone akapandwa na hasira maradufu. Ulikuwa ni muda wake sasa wa kutumia ujuzi wake aliojifunza jeshini miaka kumi na tano iiyopita; alikwea uzio kama nyani akajitupia ndani.
“Sasa twatiana vidole puani!” Alifoka na nafsi.
Alitembea haraka kwenda ndani na baada ya muda mfupi sauti ya kuvunjwa mlango iliita, na mara ikafuatiwa na ya kilio cha mwanamke. Sauti hiyo ilidumu kwa dakika tano tu na mara ikawa kimya, tena kwa ghafla.
Bi Fatma alikuwa amepoteza fahamu!

Masaa kumi baadae, Sierra Leone:

Bado giza halikuwa limeingia japokuwa mwanga wa jua tayari ulishakuwa hafifu. Kwa muda ilikuwa ni saa kumi na moja jioni iendayo kwenye kumi na mbili wakati gari lililombebelea Talib likifika kwenye uwanja wa hospitali likiongozwa na msafara wa magari manne.
Talib, aliyekuwa amevalia shati na suruali nyeusi, alitoka garini akatembea kuingia ndani ya hospitali akisindikizwa na mlinzi mmoja mwenye mwili mpana ndani ya suti. Safari yake hiyo ilikomea mbele ya mlango wa chumba alicholazwa Kessy ambapo aliwakuta wanajeshi wawili waliobebelea mitutu ya bunduki.
Wanajeshi walimsalimu mkuu wao kisha wakamruhusu kuingia ndani. Talib aliketi pembeni ya kitanda alicholazwa Kessy, akamtazama mgonjwa huyo kwa uso wa masikitiko. Sura ya Kessy ilikuwa nyeusi kana kwamba imevujia damu. Alikuwa amevimba kama kitumbua kiasi kwamba unaweza usimtambue. Kwa kumuona ungeweza kumsamehe yale yote aliyoyatenda huko nyuma.
Talib hakusema kitu kwa muda wa kama dakika mbili. Alikuwa anamtazama tu Kessy. Ila mwishowe alivuja chozi pale alipotwaa mto uliokuwepo kitandani. Alimvua Kessy kinyago cha kuhemea kisha akamfunika na mto aliombania nao kwanguvu mpaka pale Kessy alipotulia tuli kuashiria amekufa.
Talib alishusha pumzi ndefu, akasema:
“Samahani Kessy. Ni wakati wangu sasa.”



***




☆Steve
 
Muosha huoshwa sasa wajinga wanauana kama marobot
 
Wenyewe kwa wenyewe wameuana kweli uraisi mzuri

tivu sante
 
Njia nyembamba --- 08



Mtunzi: SteveMollel







Talib alishusha pumzi ndefu, akasema:
“Samahani Kessy. Ni wakati wangu sasa.”
Baada ya muda mfupi akiwa anamtazama Kessy ambaye sasa alikuwa marehemu, alijikuta anatabasamu. Alijihisi sasa amekuwa kipepeo toka kwenye muundo wa dudu washa. Alijihisi amekuwa mwepesi kama unyoya lakini kwa wakati huo akiwa mwenye kujawa nguvu na madaraka.
Alah! Ati Talib alikuwa amekufa. Kifua chake kilichobebelea chuki kilikua kimetuama. Ndio alikuwa amekufa. Hilo halikuwa na pingamizi tena, alienda na ngebe zake.

***

Kinyume na yalivyokuwa matarajio ya wengi, msiba wa Kessy ulidumu kwa siku mbili tu. Viongozi wachache sana waliudhuria tena toka mbali, wengi wao waliishia kutoa salamu za rambirambi ama kunyamaza kabisa ikiwemo Guinea. Lakini kilichoshangaza zaidi ni kwamba hata basi Al Saed wa Liberia naye? Hakufika! Ni wazi kulikuwa kuna jambo, hili lilitatiza raia ingawa hawakuwa wanampenda kabisa Kessy. Na kwa namna moja ama nyingine, Talib akatumia hii fursa kutimiza haja.
“Habari zenu wananachi wa taifa kubwa la Sierra Leone,” ilikuwa sauti ya Talib ikitokea kwenye spika za redio, na kwa wale wenye televisheni wakapata kumuona kabisa kiongozi huyo kwenye chaneli ya taifa akiwa amevalia sare za jeshi zilizopambwa na ‘vidudedude’ vingi vinavyong’aa. Alikuwa na uso wa tanzia lakini mkakamavu.
Watu walivutika kumwona na hata kumtazama. Kila mmoja alikuwa anataka kujua hatma ya nchi, lakini zaidi juu ya kifo cha Kessy ambacho kiligubikwa na utata na wingi wa siri. Walitumai watapata majibu ya maswali yao yaliyotuama kichwani hivyo wakaandaa macho pamoja na masikio.
Talib alijua kiu hiyo, na basi tokea alipoanza kuhororoja akawa anakuna pale panapowasha. Lakini si kwa kucha kama vile ambavyo wasikilizaji na watazamaji walidhani, bali kwa chuma! Alijaza uongo na pumba za kulaghai akiwa anajimiminia sifa kedekede. Ila zaidi alijenga uhasama baina ya nchi yake na mataifa mengine, haswa jirani.
“Inasikitisha sana kusema ya kwamba, kiongozi wetu mkuu aliuawa na rafiki yake kabisa, bwana Al Saed, ambaye alimtilia sumu walipoonana mara ya mwisho katika jiji la Freetown kwa ajili ya kujadili mambo kadha wa kadha ya maendeleo. Na kwa matokeo yake, jirani yetu huyo ameona aibu hata kufika kwenye msiba, amebakia kujificha nyumbani kwake. Inashangaza sana hili maana hamna taarifa rejeshi yoyote inayoonyesha kama walikuwa na mtofautiano wa mawazo.”
Hapa kwa wale waliokuwa mbali na vyombo vya taarifa ya habari wakajisogeza karibu zaidi. Lilikuwa linasisimua hili.
“Inasononesha kuona pia hata jirani yetu, Guinea, nao wameamua kuonyesha unafki wao hadharani kwa kutojihusisha kwa namna yoyote kwenye msiba wa kiongozi wetu. Ni vema, na tunampongeza kwa kuweka wazi ngozi yake ya chui. Lakini aishi akifahamu ya kwamba atakapobanwa na kiu, ni sisi wa karibu ndio tutakaomhudumia.”
Hakukomea hapo, akajinadi mbele ya wananchi.
“Wale waliodhani ya kwamba Sierra Leone itatetereka baada ya kumuua kiongozi wetu, basi wamejidanganya, tena sana. Nataka kuwahakikishia wananchi wote wa Sierra Leone usalama wa kuaminika kabisa, nchi yetu haitotetereka kwa namna yoyote ile, wala hakuna yeyote atakayehatarisha usalama wetu. Tumejipanga kwenye mipaka yetu yote na tupo tayari kwa wakati wowote kumwaga damu kwa ajili ya nchi yetu.”
Hapo uso wake ulionekana kusahau tanzia, ukachanua tabasamu kwa mbali. Ni kwa mtazamaji makini ndiye angeligundua hilo.
“Kwanzia sasa nchi itakuwa chini ya wizara ya ulinzi, na ningechukua hii fursa kutangaza safu mpya ya uongozi. Naamini kabisa kwa kushirikiana na hawa watu tutahakikisha ufanisi kwenye kuendesha nchi yetu.”
Sasa hapo akashindwa kuzuia kabisa tambazo la furaha kwenye paji lake la uso. Aliwataja watu kumi na mbili akiwagawia nyadhifa mbalimbali, watu hao wote wakitokea kwenye jeshi la Sierra Leone. Lakini kaba hajafunga mjadala huo wa madaraka, akamtaja na bibie Rose. Haikuwashangaza wanachi kwani hawakuwa wanamjua Rose, ila lilimshangaza Rose mwenyewe. Karibia litoe moyo wake nje ya kifua!
Katibu mkuu wa nchi! Si cheo kidogo. Rose alijihisi kichwa chake ni chepesi kulinganisha na majukumu aliyotwikwa. Lakini bado tabasamu lilimjaa usoni, pia na hofu ndaniye.
Alitaka kumshirikisha mtu furaha yake hiyo, na hakuwepo yeyote isipokuwa Kone. Alimtafuta mwanaume huyo simuni lakini hakumpata, mpaka pale alipojaribu mara tatu. Kiu chake kilikuwa kikubwa na hakuweza kutunza furaha yake kifuani.
“Unasema kweli?” Aliuliza Kone. Sauti yake ilikuwa ya kukoroma usipate shida kujua ametoka usingizini.
Rose alijinasibu juu ya bahati yake hiyo, lakini hakuchukua muda mrefu akagundua Kone hakuwa sawa. Mwanaume huyo alikuwa anajitahidi kuficha hali yake, ila haikutosha kumfanya Rose asing’amue kuwa mwanaume huyo yu matatizoni.
“Mke wangu yupo hospitali. Sijisikii vizuri kabisa, maisha yangu yapo mrama,” alieleza Kone. Macho yake yalikuwa mekundu. Hakuwa nadhifu kabisa.
Rose alimpatia pole. Alikata simu baada ya kuona Talib anampigia, lakini aliahidi kumtafuta tena Kone baada ya kumaliza kuongea.
Hivyo akatimiza ahadi baada ya dakika tatu.
“Amesema tutaapishwa keshokutwa. Nadhani kesho nitakuja kukuona huko Guinea lakini itakuwa siri sana. sitaki afahamu kabisa kama nina mahusiano na Guinea,” Rose alisema. Kone aliafiki mpango huo.
“Najua una mawazo fulanifulani kichwani. Si salama kuongelea kwenye simu bali uso kwa uso,” aliendelea kueleza Rose. Napo Kone akaafiki na simu ikakatwa.
Alirudisha simu mfukoni mwake akashika tama. Alikuwa kwenye hospitali kubwa kwa ajili ya kumjulia hali mkewe. Nafsi yake ilikuwa inajuta kwanini alimshushia kipondo bi Fatma kiasi kile. Alijuta kwanini hakuweza kumudu hasira zake. Alijiona mpumbavu, na baba asiyestahili. Lakini alikuwa na maswali mengi kichwani juu ya Fatma. Alikuwa anataka majibu, bahati mbaya hakuwepo pale kumjibu.
Aliwaza na kuwazua. Aliona ana haja ya kwenda kwa Raisi kumpa taarifa juu ya kifo cha Kessy. Ndio, aliona hilo ni sahihi kwa muda huo. Alifikicha macho yake akasimama.
Usiku mzima hakuwa amelala vema kutokana na mbu wa hospitali. Muda pekee aliopata wa kulala ilikuwa ni pale alipoegemea kiganja chake cha mkono wa kuume ama kushoto. Hakuweza pia kufanya hivyo kwa muda mrefu, zaidi dakika tano.
Alipopiga hatua tatu tu, simu yake iliita; alikuwa ni Raisi. Aliipokea simu hiyo haraka akaiweka sikioni.
“Ndio nilikuwa nina mpango wa kuja huko, mheshimiwa.” Aliikarimu simu kwa maneno hayo. Raisi alisafisha koo lake, akasema:
“Nahitaji uende Sierra Leone haraka iwezekanavyo.” Sauti ilikuwa kavu na usingehitaji kuelezewa kujua ya kwamba ilimaanisha kile kilichotamkwa.
“Huu ndio muda wa wewe kutazama fursa ya kutimiza kile tulichokiazimia kabla serikali hii haijatengemaa,” aliendelea kusema Raisi.
Kone alitabasamu, kisha naye akasema:
“Hakuna shida mkuu. Ila hatuna haja ya haraka kwa sasa kwani Rose, yule mdada niliyekuwa naye pamoja, ni mmoja wa watu walioteuliwa, tena kuwa katibu mkuu wa nchi! Hivyo hatuna tena haja ya papara.”
“Rose anihusu, Kone. Wewe ndiye mwenye hii kazi na si mwinginewe,” alisema Raisi. Kone tabasamu likajiminya.
“Nimesema haraka iwezekanavyo. Nadhani tumeelewana,” Raisi alisema kisha simu ikakata.
Kone alikosa cha kufanya kwa muda wa dakika mbili; alikuwa amesimama kama mnara. Alishika kiuno akitazama chini. Mwishowe alirudi kwenye viti vya hospitali akaketi na kushika tama.
Mwanaume ameumbwa mateso, lakini aliona sasa yamezidi. Aliona sasa ulimwengu unamuonea. Awali alikuwa anatamani Kessy afe basi amalize kazi, tayari amekufa, bado tena yaja kazi nyingine! Kufa kwa Kessy kwake kulikuwa kuna maana sana, si kwamba Raisi wake atapata anachokitaka, la hasha! Bali atapata muda wa kuketi na familia yake.
Sasa nayo ndoto yake ilikuwa inayoyoma. Alihisi moyo wake unasagwa kuwa chapati. Kama isingelikuwa jicho la mwanaume ni gumu kupokea chozi, basi angelikuwa tayari ameshabubujika. Alimfikiria mkewe na hali yake ile. Aliwafikiria wanawe na hivi hawana mzazi wa kuwatazama. Alikumbuka sauti ya mkewe ikimuonya dhidi ya mpango huo awali kabisa. Akajikuta anasaga meno.
Alibadilisha kila aina ya tama akachoka. Alizinduliwa na mtetemo wa ujumbe mfupi kwenye simu yake. Alitoa simu yake akatazama. Ulikuwa ni ujumbe toka kwa Raisi. Kone alitikisa kichwa akiufungua apate kuusoma.
“Pesa tayari imeshaingizwa kwenye akaunti yako. Fanya ulichoagizwa.”
Ujumbe ulisomeka hivyo.
Kwa hasira, Kone alibamiza simu sakafuni.

***

Ndani ya Toyota Prado nyeusi yenye vioo visivyoonyesha ndani.

Samweli, msimamizi mkuu wa ulinzi Liberia, alikuwa pamoja na wanaume wawili waliovalia kiraia. Wanaume hao walikuwa wanamtazama Samweli kwa umakini akiwapa maelezo juu ya nini cha kufanya. Walikuwa ndani ya eneo lijulikanalo kama Pleebo, ndani ya kata kubwa ya Maryland, kusini mwa nchi ya Liberia. Eneo ambalo kwa mujibu wa msimamizi wa ulinzi, bwana Samweli, lilikuwa linahisiwa kuwafadhili kundi changa la AMAA – Alwaqt min ajil alttaharrur.
Walitakiwa kuwa waangalifu sana kwenye eneo hilo lenye udongo mwekundu ndio maana wakachukua hatua kadhaa kuficha uhalisia wao. Usingeweza kudhani kama ndani ya gari hilo lililokuwa limechafuka matope kuna mtu mkubwa kama Samweli, lakini pia usingeweza kudhani kama wale wanaume wawili waliokuwa wanamtazama na kumsikiliza Samweli, walikuwa ni makachero. Sio tu kwamba walivalia kiraia, hapana. Walikuwa pia wachafu kama wengi waishio maeneo hayo.
Kuna mahali wamepahisi panaweza pakawa kitovu cha kikundi hicho. Wanaume hao wawili baada ya kuketi kwa siri eneo hilo huku wakiwa wanapeleleza kwa macho ya upande, waligundua mahali hapo pa siri. Ni mahali ambapo si watu wote huingia, isipokuwa ijumaa tu kwa ajili ya sala; ni mahali palipojitenga mbali kidogo na makazi ya watu; ni mahali ambapo nje yake kuna wanaume wawili wanaopalinda, na wanaume hao hubadilishwa kila baada ya siku moja na kuja wapya.
Hakuna mwenye taarifa kamili kuna nini ndani ya eneo hilo, na kabla ya kuchukua hatua yoyote dhidi ya eneo hilo ndipo makachero hao waliamua kuonana na mkuu wao awapatie amri.
“Ni lazima kwanza tuwe na uhakika kabla ya kuchukua hatua,” alisema Samweli kwa msisitizo. “Leo ni ijumaa na muda si mrefu …” akatazama saa yake mkononi, “muda si mrefu wataanza sala. Kwahiyo basi mtumie hiyo fursa kusali humo na mpekenyue kuna nini.”
Hiyo ikawa imeeleweka. Wanaume hao wawili walishuka toka kwenye gari, Samweli akaondoka. Walikuwa mbali na mji kwa sababu za usalama, kwahiyo kurudi kwenye makazi walilazimika kutembea kama lisaa limoja.
Walimaliza lisaa hilo wakaingia ndani ya mji, lakini kila mtu kwa upande wake. Walifikia kwenye makazi yao ya kuzugia, kila mmoja akiwa na yake, kisha wakajiandaa kwa ajili ya kwenda msikitini. Walivalia kanzu, mmoja yake ikiwa nyeusi na mwingine ikiwa nyeupe.
Adhana ililia ikawakuta wakiwa njiani kwenda msikitini. Walifika mlangoni wakakaguliwa kama wana silaha, ilipothibitika wapo safi, wakaruhusiwa kuzama ndani kama wengineo. Waliswali ndani ya msikiti huo lakini akili yao ikiwa haipo ibadani. Walikuwa wanaperuzi kutazamataza mazingira katika namna ya siri.
Kulikuwa kuna holi kubwa la kuswalia walipokuwa wamejazana watu kama hamsini na kitu hivi, wote walikuwa wanaume. Wanawake walikuwa kwa upande wa pili huko, nyuma ya mwongoza ibada aliyekuwa upande wa kaskazini mwa holi. Upande wa kusini mwa holi kulikuwa kuna milango miwili iliyokuwa imefungwa. Zaidi ya hapo hakukuwa na lolote la kukufanya uwaze kuna nini mule ndani.
Sasa kwanini kulikuwa kunalindwa? Tena na watu wabadilishwao kila baada ya muda fulani?
Maswali hayo yaliwafanya makachero wale wawili waendeleze macho yao ya upekuzi. Baadae wakati ibada yaelekea ukingoni, kachero mmoja akagundua kitu pale alipokuwa amekanyaga. Palikuwa pamefunikwa na zulia jekundu na hivyo basi ukadhania ni sakafu, ila kachero huyo alipopakanyaga mara mbili na kisigino chake aligundua chini ya hapo apakanyagapo pana uwazi. Huweza ikawa ni handaki!
Alijivunga na hakufanya kitu mpaka ibada yakwisha. Akiongozana na mwenzake, walijipanga katika mstari wa wanaotoka ndani, lakini walipofika mlangoni wakasimamishwa na wanaume wanne waliokuwepo mlangoni. Walikuwa na nyuso za kughafirika. Macho yao yalikuwa makali ambayo yangekufanya uhofie. Mmoja alikuwa ana asili ya kiarabu, wenzake watatu wakiwa weusi kama mie na wewe.
Kwa ishara yule mwarabu akaonyesha uelekeo wa kusini. Mkono wake wa kuume ulikuwa umeshikilia bunduki kubwa iliyokuwa ndani ya kanzu. Kwa kuhofia usalama wao, makachero wale wawili wakatii amri. Walisindikizwa na wanaume hao wanne mpaka ndani ya chumba kimoja upande wa kusini mwa holi.
Mlango ulifungwa tusijue nini kilichoendelea humo ndani. Ila baada ya kama robo saa, damu nzito ilichuruzika ikitokea chini ya mlango.


***




☆Steve

Sent from my SM-J110F using JamiiForums mobile app
 
Duuuuh, wamesha rest in peace!! Maskini kone!! Basi sawa mkuu, tuko pamoja!!!
 
Back
Top Bottom