*Njia nyembamba -- 06
*Mtunzi: SteveMollel
Baada ya kukaa hapo kwa muda wa lisaa limoja tu, daktari alikuja kuwapa taarifa ya mgonjwa. Alimtazama Talib kisha Al Saed, akameza mate. Ni kana kwamba alikuwa anahofia kuongea. Na ni kweli kwa namna alivyokuwa anatazamwa, alikuwa ana haki ya kuogopa. Talib alikuwa ametoa macho kama nyanya mbichi wakati Al Saed akiwa amekunja uso mithili ya tambara la kikongwe.
“Nasikitika kuwaambi …”
“Amekufa?” Talib aliwahi.
“Hapana, hajafa.” Daktari akajibu kwa sauti ya upole. Talib alishusha pumzi akadaka kiuno chake.
“Raisi ni aidha amekula ama amepewa sumu kali sana. Ni bahati kwake kuwa hai mpaka muda huu. Tunaweza tukauita muujiza.”
Jambo hilo likawachanganya Talib na Al Saed kwa mawazo. Kessy amekula sumu muda gani, na hivyo basi nani kampa? Japokuwa waliteta na kuulizana sana kuhusu hilo swala hawakupata jibu wakaishia kutegemea labda Kessy atakapopata uwezo wa kufungua kinywa basi utajulikana upi ni mchele na upi ni pumba.
Lakini zaidi ya hapo hilo swala pia likaonekana gumu baada ya muda kidogo daktari kuja na kuwapa taarifa ya kwamba hana uhakika ni kwa muda gani Kessy atakuwa kitandani mpaka aje kupata fahamu zake kwani sumu aliyotumia bado haijajulikana ni ipi ili basi wafahamu namna ya kuikabili.
“Kwahiyo daktari unataka kusemaje?” Talib alikunja sura.
“Mi – mie sina usemi mheshimiwa. Laki …”
“Lakini kitu gani? … kwani wewe kazi yako ni nini? Unavyotuambia haujajua ni sumu gani sisi ndio tutajua?”
“Tutajitahidi mheshimiwa kwa kadiri ya uwezo wetu. Tunaomba tu utupatie muda.”
“Daktari, kaa ukijua ya kwamba; akifa nawe utazikwa naye.”
Hilo tisho likafunga maongezi kati ya Talib na daktari aliyeondoka upesi kuelekea ndnai ya chumba maalum alipolazwa kiongozi mkuu wa nchi.
Baada ya muda mchache mbele, Al Saed akaaga anaondoka kurudi Liberia, lakini akiahidi kuendelea kumjulia hali rafiki yake huyo aliye taabani. Talib alimsindikiza kiongozi huyo mpaka uwanja wa ndege, akaondoka zake.
Wakati Talib akirejea kurudi hospitalini, bado kichwa chake kilikuwa kinachakata swala la Kessy. Mambo yalikuwa magumu lisilionyeshe dalili ya kung’amulika. Ila kwa namna moja ama nyingine akili ya Talib ikaanza kuelekea kwa Al Saed ya kwamba yeye ndiye anaweza kuwa mtuhumiwa wa tukio hilo. Alijitahidi kukataa lakini bado akili yake ilitokea kuamini hivyo.
Al Saed ndiye mtu wa mwisho kuwa na Kessy, kwa siku zote hizo za nyuma Kessy alikuwa mzima. Al Saed alikuwa ndiye mtu wa mwisho kula na Kessy, na pia kwa mujibu wa maelezo yake, Al Saed alimletea Kessy mvinyo kama zawadi.
Ila afanye hivyo kwasababu gani ingali hawakuwa na ugomvi wowote? Kama wangekuwa na tofauti yoyote basi Talib aliamini angekuwa anaifahamu.
Alijitahidi kuitafuta sababu ya Al Saed kutenda hilo tendo, akakosa kabisa. Sasa basi akili yake ikawa inaamini yule ndiye mtenda lakini pia kwa wakati huohuo tena akiwa anajikosoa.
Kufa kufaana lakini, waswahili walinena. Japokuwa Talib alikuwa kwenye rundo la mawazo, alijikuta anapata tabasamu katikati yake baada ya kujigundua ya kwamba ni yeye peke yake sasa ndiye atakaimu kiti cha uongozi wa Sierra Leone mpaka pale Kessy atakapopona. Na kama je asipopona?
Kabla hajapata jibu alikuwa ameingia ndani ya hospitali pamoja na msafara wake. Aliendea karibu na chumba alicholazwa Kessy akaketi karibu.
***
Zilipita siku tatu.
Siku inayofuata, yaani ya nne, ilikuwa ni mahususi kwa THE GHOSTS kutoka ndani ya jiji la Freetown waende kutafuta mahali tulivu na papekee kwa ajili ya kujiandaa kama kikundi na hata pia kuongeza idadi ya watu baada ya kuona kuna haja hiyo.
Hilo halikuwa shida, bali watatokaje nje ya jiji hilo ukizingatia wanajeshi wameambaa huko kwenye barabara, njia za maji na hata uwanja wa ndege? Mipango ilihitajika, tena mipango thabiti ya kukwepa vikwazo. Mipango itakayowawezesha kuwakwepa wanajeshi lakini kwa wakati huohuo wasafirishe silaha na wajisafirishe na wao pia.
Hivyo basi kwa usiku mzima walipanga namna ya kutenda ili kukwepa. Asubuhi ilipodamka, gari kubwa, canter nyeupe iliyofunikwa na shuka kubwa la ngozi, lilitoka ndani ya nyumba hiyo na kushika barabara ya lami. Mwendo wake ulikuwa wa wastani na vioo vyake vilikuwa vimejiveka rangi nyeusi usiwaone waliomo ndani.
Gari hilo lilielekea upande wa kusini wa jengo lilimotokea. Baada ya muda mfupi likaingia kwenye barabara kuu na kuanza safari ya kuelekea upande wa mashariki. Halikudumu sana katika barabara hiyo kuu, likachepuka na kwenda upande wake wa kushoto. Huko lilikaa kwa muda wa masaa matatu likafika mahala kulipokuwa na msururu wa magari yakingojea zamu ya kukaguliwa.
Kulikuwa kuna wanajeshi sita kwa macho ya haraka. Wote walikuwa wamebebelea bunduki ndefu mikononi mwao na kwa kugawana walikuwa wanakagua magari, huyu akishika hili basi yule lile.
Taratibu magari yalienda, na mpaka ukafikia muda ambapo Canter lilikuwa la pili kwenye msururu. Basi kutokana na ukubwa wa gari hilo na kufanya ukaguzi uwe wa kiufanisi zaidi, wanajeshi watatu walilidaka ambapo mmoja alisimama upande wa dereva wakati wengine wakiwa wanalitazama kiubavu.
“Shukeni chini,” ilitoka amri. Alikuwa ni yule mwanaume rasta, mwanaume aliyekubali kuungana na Amadu pasipo shuruti.
Alishuka akatia mikono yake mfukoni. Rasta zake zilikuwa zinamtekenya mabega, na uso wake haukuonyesha hofu yoyote.
“Umebeba nini humu?” Aliuliza mwanajeshi kwa uso kakamavu.
“Nimebeba nyama. Nawapelekea wazazi wangu kijijini,” akajibu Rasta.
Aliamriwa aonyeshe nyama hiyo, akaenda nyuma ya gari na kufungua shuka lililofunika gari. Humo ndani kulikuwa kuna ‘dude’ kubwa rangi nyeusi lenye pembe nne. Rasta aliamriwa alifungue hilo dude kionekane kilichomo ndani. Akasita.
“Samahani, nina aleji na nyama. Nitapata matatizo endapo nitanusa harufu hiyo.”
Basi mwanajeshi mmoja akajitolea kwenda kutazama. Alifungua dude hilo na kukuta mfuko mweupe ukiwa umefunika nyama iliyokuwa inanukia vilivyo. Alipekua nyama hiyo asikute kitu. Waliporidhika hamna jambo, walieleka na kwa dereva wakapekua, napo hawakukuta kitu hivyo wakamruhusu Rasta aende zake. Gari likaenda.
Ilipita kama dakika kumi na tano, mwanajeshi yule aliyepekua nyama, pamoja na yule mwenzake, wakaanza kuwashwa miili. Walijikuna kama hawana akili nzuri. Mwasho ulizidi kuongezeka sambamba na muda, sasa wakawa kama vichaa. Walipiga kelele kali na kuzua tafrani, walitokwa na vidonda kwa kujikuna wakawa wanavuja damu. Wenzao walisitisha zoezi la ukaguzi wakawajongea kuwatazama kwa bumbuwazi.
Walitaka kufanya utaratibu wa kuwawaisha hospitali ya karibu kwa kutumia usafiri wao, lakini kabla hawajatenda hivyo wakaliona gari la wagonjwa. Na kwenye ubavu wa gari hilo kulikuwa kumeandikwa jina la hospitali iliyo karibu. Basi kwa haraka wanajeshi wakawasaidia wenzao kuingia kwenye gari la wagonjwa wapate kwenda kupata tiba. Na kwa msaada zaidi, mwanajeshi mmoja mzima, sajenti, akaongozana na wenzake.
Hakukuwa na muda wa kukagua gari hilo la wagonjwa, wanajeshi wagonjwa walipakiwa na chombo kikaondoshwa kwa kasi kuelekea hospitali. Dereva alikuwa ni Chui akiwa sambamba na Ulsher. Walikuwa wamevalia kofia nyeupe za nailoni na miwani ya macho. Walifika mbele Ulsher akachomoa bunduki na kumtwanga yule mwanajeshi mzima kisha akatoa simu ndani ya mfuko wake na kupiga.
“Muda ndio huu.”
Kisha akakata alafu akampisha Ulsher ashike usukani kabla hajaenda kutwaa ‘redio koo’ na kuitumia kuwasiliana na wanajeshi waliobakia kule kwenye kitengo cha upekuzi. Aliwapa taarifa ya kwamba kuna ujio wa gari kubwa hapo, canter ya kijivu, akalitaja na namba zake za usajili. Taarifa ni kwamba gari hilo linatakiwa kupita upesi.
Isipite muda mrefu, wanajeshi watatu waliobaki kwenye ukaguzi wakaliona gari hilo. Baada ya kujiridhisha ndilo lenyewe, gari hilo likapita wasijue ndaniye yapo mabaki ya wana THE GHOSTS.
Canter hilo lilitembea kwenda kukutana na ambulance pamoja pia na canter nyeupe ya mwanzoni. Tayari wanajeshi wale wawili, waliokuwa wanawashwa, walishakufa kwenda kukutana na mwenzao aliyeuwawa kwa risasi. Wote walivuliwa nguo zikapuliziwa dawa kabla ya kuvaliwa na Fredy na rafiki yake Rasta, Thomas, sasa wakaonekana ni wanajeshi.
Walijipaki wote kwenye canter ya kijivu huku sehemu ya dereva na mwenza wakiwepo wanaume hao ndani ya sare. Sehemu ya nyuma palipokuwa pamezibwa, pakawa pamehifadhi silaha na wengineo wana THE GHOSTS.
Canter hiyo ilisonga kwa muda wa masaa matatu mbele kabla ya kukutana na kizuizi cha mwisho watoke ndani ya Freetown. Kwa muda wote huo Chui alikuwa anaisikiliza redio koo kwa umakini ili wapate kujua kama kuna namna yoyote mpango wao upo hatarini. Lakini mpaka wanafika kwenye kizuizi cha mwisho, walikuwa salama.
Kwenye kizuizi hiki hakikuwawia vigumu, wanaume wale waliokuwa wameketi mahali pa dereva walitumia nguo za za jeshi vema kuwalaghai wapekuzi na kisha kwenda zao sasa nje ya Freetown. Kwenda huko msituni wapate kujikoboa kwa mafunzo, lakini pia kujiongeza.
Kukaa ndani ya Freetown kungewanyima fursa hiyo ya ‘kujiachia’ wapendavyo. Kwa namna iliyopendeza machoni, kutumia mfumo wa MDR kwa kuketi mbali na mkono wa serikali, lakini pia karibu na raia, ulikuwa ni mpango mtamu zaidi kufikisha malengo.
***
Japokuwa ilikuwa ni mchana kamili, Kone alikuwa amechoka na yu kitandani akiwa hajafanya lolote tangu asubuhi, hata kunawa uso.
Alikuwa amejifunika shuka mpaka kiunoni. Mara moja moja bado alikuwa anafunga macho yake kwa usingizi na kisha akiyafungua tena. Ni dhahiri shairi alichelewa kulala, alafu hakuwa anatakata kulala tena.
Alitafuta simu yake ya mkononi, akaikuta kitandani. Aliitazama kama kuna habari yoyote kwenye kioo, hakukuta. Alisonya kisha akatafuta jina la Rose aliloliita akiiweka simu sikioni. Baada ya muda mfupi simu ikapokelewa, na sauti ya kike ikanena upande wa pili.
“Vipi umepata taarifa zozote za Kessy?” Kone aliuliza.
“Hapana,” sauti ikamjibu.
“Inakaribia juma sasa, Rose. Kweli ulimpatia sumu?”
“Bila shaka.”
“Mbona hamna majibu?”
“Sijajua kwanini. Nitajitahidi kufuatilia.”
Kone alikata simu akairushia mbali. Kwa namna moja aliona ulimwengu umeamua kumfanya asiwe na amani. Ni siku kadhaa sasa anawinda habari njema na hazipati, si kwa mkewe wala huko Sierra Leone. Alijiona yupo kwenye jehanamu ndogo. Aliona kana kwamba watu wa ulimwengu wamekaa kando wakifurahia anavyotaabika.
Alijinyanyua toka kitandani alipatie tumbo lake chochote kitu. Alijiiandalia chakula cha upesi: cornflakes na maziwa, kisha akaketi mahala pa kulia chakula. Alijitahidi kula lakini alishindwa, hakuwa na hamu kabisa japokuwa alihisi njaa. Alijikuta anasogeza bakuli la chakula kando na kushika tama.
Mke wake, bi Fatma, alitawala kichwa chake. Na hata pale alipompa ahueni, basi Kessy akachukua zamu. ‘shift’ hiyo ilimnyima raha. Alihama kila kona ya nyumba mpaka jioni ikawasili. Wakati sasa akiitafuta usiku, alikuwa sebuleni akitazama taarifa ya habari. Alitamani aone habari ya msiba wa Kessy lakini kadiri muda ulivyokuwa unazidi kusonga, matumaini yakawa yanafifia.
Akiwa hapo bado anakodoa, alisikia mlango wa mlango wa sebuleni unafungwa. Upesi aligeuka kutazama akamwona mke wake, bi Fatma, akiwa amevalia dera na anatembea kwa kuyumba. Alikuwa amelewa!
Kone alisimama akamfuata mkewe akimwita jina. Fatma alimpuuza mumewe na hakutaka kuzozana juu ya hali yake. Hakusema wapi ametokea wala wapi alipokuwa siku zote hizo. Mdomo wake ulikuwa unanuka mvinyo wa bei ghali. Alikuwa mkali kama mbogo akisisitiza asiguswe.
Hatimaye, alijifungia ndani ya chumba akimwacha mume wake mlangoni na mabumbuwazi.
“Fatma fungua!” Kone alibamiza mlango. Macho yake yalikuwa mekundu. Uso wake ulikuwa mweusi.
Alikaa hapo kama lisaa asifunguliwe mlango. Alimwendea mlinzi na kumuuliza juu ya ujio wa mke wake, mlinzi akamtaarifu ya kwamba aliletwa na gari kubwa, Toyota Prado nyeusi. Kone akachanganyikiwa kwa fundo la wivu.
Alirudi ndani akaenda kubwatukia maswali yake mlangoni mwa chumba alimo Fatma, lakini hakupewa jibu lolote. Fatma alikuwa amelala na inawezekana alikuwa hata hasikii linaloendelea.
Kone alikata tamaa akaenda zake kulala kwa matumaini ya kwamba kesho yake, pombe zikiwa zimemtoka Fatma, basi atapata majibu anayoyataka. Alijitahidi kupunguza jazba.
Ilimchukua kama masaa matatu kitandani kuupata usingizi. Alikuja kuamka muda wa saa mbili asubuhi, kesho yake, akaendea kile chumba kilichomficha mkewe.
Mlango ulikuwa wazi. Aliingia ndani akakuta kitanda cheupe, hakuna mtu! Alitafuta nyumba nzima asimuone mke. Alimwendea mlinzi akamuuliza, mlinzi akamhabarisha ya kwamba mwanamke huyo aliondoka kwenye majira ya saa kumi na mbili, na gari lililomleta jana ndilo limekuja kumtwaa.
Kone alirudi ndani aking’ata kidole chake kana kwamba anataka kukitemea chini. Alimpigia simu mkwe wake kumuuliza kama mkewe yupo huko, akakanusha. Aliwapigia na rafiki wa mke wake anaowajua, nao wote wakakanusha. Hakuna aliyempatia majibu zaidi ya kusema “sifahamu”.
***
Zinapita siku tano.
Talib akiwa nyumbani kwake anamkumbuka mwanamke yule aliyekutana naye klabu ya usiku ya Aces. Anakumbuka namna alivyoshika maungo yake na namna alivyomkonyeza akiwa na Kessy, basi akajikuta anatabasamu mwenyewe kama mwehu.
Alijikuta anatamani kumuona tena mwanamke huyo. Alijikuta ana kiu ya kutaka kumtia mikononi. Kessy alikuwa yu hoi kitandani, hivyo basi hakuna wa kuukata mkono wake mrefu unaotaka kumdaka mwanamke huyo.
Lakini kumbuka Talib hakuwa na namba ya simu wala hawakuwa anajua makazi ya mwanamke huyo, hivyo basi ilimlazimu kufanya namna ya ziada kumpata mwanamke huyo basi amfaidi kabla Kessy hajarudi fahamuni.
Alimtafuta dereva aliyemleta Rose ikulu siku ya mwisho kumuona mwanamke huyo, akampata. Zoezi hilo lilikuwa rahisi kwake kwasababu alikumbuka ni gari lipi lilitumika baada ya kuliona limepaki nje alipokuwa njiani kutoka ikulu siku ile. Lakini pia alikumbuka ilikuwa ni majira gani na gari lilifanya tukio gani.
Dereva alimweleza mahali alipomtoa mwanamke yule, basi Talib akaanza kuchukua hatua. Alijiweka kwenye gari akiwa na ‘kamsafara’ ka magari matatu mpaka eneo anapoishi Rose. Alimkuta mwanamke huyo akiwa amevaa sketi fupi nyeusi na blauzi rangi ya udhurungi ikiishia juu ya kitovu. Hakika alipendeza japokuwa haikuwa dhamira.
Talib alimsalimu na kumtaka waende mahali bora zaidi ya pale wapate kuteta. Rose alitaka kubadili nguo lakini Talib hakuweza kuvumilia, alimtaka waende vivyo hivyo kwani bado alikuwa anavutia sana.
Walijipaki kwenye gari wakaondoka. Rose alitabasamu akimtazama Talib, Talib akajiona yu peponi kwa wasaa.
Lakini kama angelijua ni nini Rose alikuwa anakiwaza kichwani, basi angemshusha mwanamke huyo aende zake ili apate kujinasua toka mtegoni.
Tabasamu la Rose lilikuwa zuri mno, hata macho yake pia. Lakini roho yake, hakuna binadamu anayeiweza zaidi tu ya yule aliyemuumba.
***
☆Steve